Sala za Tafakari

Sala ya Usiku kabla ya kulala

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

SALA YA KUSHUKURU

Tunakushukuru, ee Mungu, kwa mapaji uliyotujalia leo. Amina.

Baba yetu …

Salamu Maria …

SALA YA IMANI

Mungu wangu, nasadiki maneno yote. Linayosadiki na linayofundisha Kanisa Katoliki la Roma. Kwani ndiwe uliyetufumbulia hayo. Wala hudanganyiki, wala hudanganyi. Amina.

SALA YA MATUMAINI

Mungu wangu, natumaini kwako, nitapewa kwa njia ya Yesu Kristo. Neema zako hapa duniani, na utukufu mbinguni. Kwani ndiwe uliye agana hayo nasi, nawe mwamini. Amina.

SALA YA MAPENDO

Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote. Kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu, kama nafsi yangu, kwa ajili yako. Amina.

KUTUBU DHAMBI

Tuwaze katika moyo wetu makosa ya leo tuliyomkosea Mungu kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu. (Husubiri kidogo ).

Nakuungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno, kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo, na kwa kutotimiza wajibu.
Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana nakuomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.
Mungu Mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele. Amina.

SALA YA KUWAOMBEA WATU

Ee Mungu, nawaombea watu wa nchi hii, wapate kusikia maneno yako na kukupenda wewe Bwana Mungu wetu.

SALA KWA MALAIKA MLINZI

Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote za roho na za mwili. Amina.

MALAIKA WA BWANA

(kipindi kisicho cha Pasaka)
Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria.
Naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Salamu, Maria,…..
Ndimi mtumishi wa Bwana.
Nitendewe ulivyonena.
Salamu, Maria….
Neno la Mungu akatwaa mwili.
Akakaa kwetu.
Salamu, Maria….
Utuombee, Mzazi mtakatifu wa Mungu.
Tujaliwe ahadi za Kristu.
Tuombe:
Tunakuomba, Ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba Mwanao amejifanya Mtu kwa mateso na msalaba wake tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. AMINA.

AU;

MALKIA WA MBINGU (kipindi cha Pasaka)

Malkia wa mbingu, furahi, aleluya.
Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.
Amefufuka alivyosema, Aleluya.
Utuombee kwa Mungu, Aleluya.
Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya.
Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.
Tuombe.
Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao, fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.

ATUKUZWE (mara tatu)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.

KUJIKABIDHI

Enyi Yesu, Maria na Yosefu nawatolea moyo na roho na uzima wangu!
Enyi Yesu, Maria na Yosefu mnijilie saa ya kufa kwangu!
Enyi Yesu, Maria na Yosefu mnijalie nife mikononi mwenu!

(Rehema ya siku 300).

WIMBO:

Kwa heri Yesu mpenzi mwema,
Naenda usiudhike mno.
Nakushukuru, nakupenda,
Kwa hizo nyimbo za mwisho.
Asubuhi nitarudi.
Yesu kwa heri.

Kwa heri Mama mtakatifu,
Sasa napita pumzika.
Asante kwa moyo na nguvu,
Leo umeniombea.
Asubuhi nitarudi.
Mama kwa heri.

Kwa heri Yosefu mnyenyekevu,
Kazi zatimilizika.
Kama mchana, leo usiku,
Nisimamie salama.
Asubuhi nitarudi.
Yosefu kwa heri.

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

KUOMBA ULINZI WA USIKU

Mungu wangu naenda kulala naomba malaika 14, waende nami, wawili juu, wawili chini, wawili upande wa kuume, wawili upande wa kushoto, wawili wanifunike, wawili waniamshe, wawili wanipeleke juu mbinguni. Mimi mtoto mdogo, roho yangu ni ndogo, haina nafasi kwa mtu yoyote ila kwa Yesu pekee. Amina.

AMRI ZA MUNGU

1. NDIMI BWANA MUNGU WAKO, USIABUDU MIUNGU WENGINE.
2. USILITAJE BURE JINA LA MUNGU WAKO.
3. SHIKA KITAKATIFU SIKU YA MUNGU.
4. WAHESHIMU BABA NA MAMA, UPATE MIAKA MINGI NA HERI DUNIANI.
5. USIUE
6. USIZINI
7. USIIBE
8. USISEME UONGO
9. USITAMANI MWANAMKE ASIYE MKE WAKO
10. USITAMANI MALI YA MTU MWINGINE

SALA MBELE YA SAKRAMENTI KUU II

Yesu, Mungu wangu mpenzi,/ upo hapa katika Altare mbele yangu;/ na mimi napiga magoti mbele yako.// Waniangalia sana,/ siyo kwa kunipeleleza,/ lakini kwa sababu wapenda kuniona hivi karibu na wewe,/ wafurahiwa nikija kukuabudu./ Wayasikiliza maneno yangu yote/ yenye kutoka mdomoni mwangu,/ na zaidi wapokea maneno yangu yanayotoka moyoni./ Nataka kuzungumza na wewe peke yako,/ na kusahau mambo mengine yote/ na watu wengine walioko kanisani pamoja nami./

Yesu wangu,/ nakushukuru/ kwa sababu umekubali kutupa Sakramenti hii kuu kabisa,/ ukitaka kukaa pamoja na sisi,/ na hata ukakubali kuwa chakula chetu/ chenye nguvu ya ajabu./ Mfalme wangu Yesu,/ Sultani wangu Mkuu,/ naamini kabisa kwamba upo katika Altare/ na kwamba umejificha chini ya umbo la mkate./ Ulipokuwapo bado hapa duniani mbele za watu,/ ulikuwa hujifichi kama sasa;/ lakini hata siku zile/ watu hawakuweza kukuona vile ulivyo./ Hawakuweza kuutambua Umungu wako,/ ikalazimu kukuamini tu sawa kama sisi./ Wakainama kichwa wakisema,/ “Bwana wangu na Mungu wangu”./ Na mimi kadhalika naungama/ U Bwana wangu na Mungu wangu/ na Mkombozi wangu/ na salama yangu yote./ U Yesu wangu tu,/ siwezi kusema zaidi./ Nakuabudu ee Yesu./ Najua sana, mimi ni mdogo kabisa,/ sina maana hata kidogo./ Mimi ni dhaifu na maskini mno./ Lakini Wewe katika hruuma yako kubwa/ waniita nije kwako./ Wewe huuangalii umaskini wangu,/ bali wanivuta katika mapendo yako./

Nasikia maneno yako usemayo:/ “Njooni kwangu ninyi nyote mnaoelemewa na mizigo/ nami nitawasaidia”./ Kwa ajili ya maneno hayo/ nakuja kwako bila hofu./ Najua kwamba wanipenda,/ najua wataka kunisaidia na kuniponya,/ najua kuwa wataka kunitakasa./

Nahitaji sana msaada wako, hakika./ Unaniona katika mwendo wangu wa kila siku,/ Jinsi ninavyohangaika na vishawishi mara nyingi;/ jinsi nilivyo na lazima ya kushindana kila siku/ nikitaka kukaa mwema na safi katika utumishi wako./ Naungama mbele yako Wewe Mkombozi wangu,/ kwamba sikukaa imara siku zote vile nilivyopaswa./ Naungama kwamba nimeshindwa mara nyingine/ na kwa hivi naomba toba./ Lakini kwa nini nimeshindwa mara nyingine?/ Kwa nini nikakosa?/ Ni kwa sababu nalikuwa nimekwenda mbali nawe;/ nalianza kujitegemea mwenyewe./ Katika majivuno yangu nikajisifu mwenyewe,/ nikajiona mwema,/ nikasahau udhaifu wangu./ Na kwa ajili hiyo nikajitia katika hatari bure,/ sikujilinda tena,/ nikampa shetani nafasi ya kunishambulia kwa hila zake zote./ Unihurumie ee Yesu wangu./

Sasa nafahamu jinsi nilivyokuwa mjinga kwelikweli./ Ndiyo maana nakuabudu kwa moyo wangu wote./ Najiweka mikononi mwako/ ufanye nami vile unavyotaka./ Wewe utanitunza;/ Wewe utanilinda vema;/ Wewe utaniongoza nijue namna ya kuepa hatari zote,/ na jinsi ya kufukuza kila kishawishi./ Chukua moyo wangu kabisa,/ kwa sababu ni mali yako kamili;/ Wewe ndiwe uliyeniumba,/ ndiwe uliyenipeleka katika Ukristo,/ nawe ndiwe utakayenihukumu siku ya mbele./ Ndivyo ninavyojitolea kwako./ Ndivyo ninavyokuabudu,/ wala sijui njia nyingine ya kukusifu zaidi./

Yesu wangu mpenzi,/ naomba upokee kwa uzuri heshima hiyo yangu./ Angalia: naitolea pamoja na heshima yote/ unayopewa daima na watakatifu wako/ na malaika wako./ Nikipiga magoti hapa mbele yako sasa,/ siko peke yangu,/ nakuabudu pamoja na Mama yako Bikira Maria,/ ambaye sala zake zinakupendeza kabisa./ Sala zangu naweka pamoja na sala zake yeye,/ uzipokee zote pamoja,/ zikupendeze zote sawa./ Ee Mama Maria!/ Nifundishe maneno ya kumsifu Mwanao Yesu vizuri./ Nipeleke kwa Yesu tumwabudu pamoja./ Nifunike na utakatifu wako/ kusudi Yesu asiangalie tena umaskini wangu/ na makosa yangu,/ aniponye katika huruma yake./

Sasa najisikia vizuri, Yesu wangu./ Sasa nina moyo wa kuweza kuendelea vema/ katika njia njema./ Sasa ninatumaini kwamba/ nitakaa mkristo mwema,/ nitakuwa mtumishi wako mwaminifu./ Nasikia amani kubwa sana moyoni mwangu,/ kwa kuwa nimo mikononi mwako./ Baada ya dakika chache/ nitaondoka tena kanisani,/ nitarudi nyumbani kwangu,/ lakini hatutaachana,/ hapana./ Mapendo yetu yatatuunganisha pamoja daima./ Wewe utanikumbuka nikiwa kazini,/ nikilala usingizi,/ nikienda njiani,/ kila mahali nilipo,/ Wewe utaniona,/ utafuatana na mimi./ Kadhalika nitakukumbuka tu./ Nitafanya bidii nisikuache kabisa./ Amina.

SALA YA KUMWABUDU BWANA YESU KATIKA SAKRAMENTI TAKATIFU

Ee Yesu Kristu,/ Bwana wangu na Mungu wangu/ ambaye ninasadiki kuwa upo hapa/ katika Sakramenti Takatifu ya Altare;/ pokea kitendo hiki cha kukuangukia kifudi fudi/ kama ishara ya tamaa niliyonayo ya kukuabudu Wewe/ bila kuchoka/ na kukushukuru kwa mapendo yako makubwa/ yasiyo na kipimo/ ambayo Moyo wako Mtakatifu sana/ unawaka katika Sakramenti Takatifu hii./ Siwezi kukushukuru vizuri zaidi/ kuliko kama ningetolea kwako/ matendo yangu yote ya kukuabudu/ unyenyekevu wangu/ uvumilivu na mapendo/ ambayo huu Moyo Mwabudiwa ulifanya,/ bado unafanya/ na utaendelea kufanya katika uzima wa milele mbinguni./ Ninaahidi kupitia Moyo huu,/ nitakupenda,/ nitakutukuza,/ na nitakuabudu kama nitakavyoweza./ Ninajiunganisha na hii Sadaka Takatifu/ ambayo unatoa kwa Baba Mungu/ na ninatolea kwako utu wangu./ Ninakuomba kuangamiza ndani yangu/ dhambi zote pamoja na majeraha yake/ na usikubali kunitenga nawe milele./ Amina.

(Na Mt. Margareta Maria Alakoki)

Shopping Cart