Mbinu za Kilimo na Ufugaji Kukuongezea Mapato

Jinsi ya kutumia mashonanguo kama dawa ya kuzuia wadudu kwenye mimea

Mashonanguo kwa kiingereza ni Blackjack au kwa kisayansi yanajulikana kama (Bidens
pilosa)
Mashona nguo yanazuia wadudukama vile Vidukari, Siafu, bungo, katapila, chenene (crickets), nyenyere, siafu na inzi weupe.

Jinsi ya Kutayarisha na kutumia mashonanguo

  1. Jaza kikombe kilichojaa mbegu ambazo zimekomaa na maji;
  2. Chemsha kwa dakika kumi au loweka kwenye maji kwa saa ishirini na nne, kisha upooze.
  3. Ongeza lita moja ya maji na kijiko kimoja kidogo cha sabuni;
  4. Kisha unyunyizie mimea.

Matumizi mengine

  1. Mbegu zinaweza kutawanyishwa karibu na vichaka kuvutia mchwa.
  2. Mmea waweza kupondwa au kufikichwa kisha maji yake yatumike kunyunyizia mimea.

Angalizo: Kiasi kingi cha dawa hii chaweza kudhuru baadhi ya maua ya mimea.

Kilimo bora cha matikiti maji

Ili kulima tikiti maji, inakubidi uwe na sehemu ya kutosha, yenye jua la kutosha, maji mengi na ardhi yenye rutuba ya kutosha, matikiti maji hukua haraka kama mimea mingine ya jamii yake itambaayo mfano matango, maboga na makwash.

Hali ya Hewa

Matikiti yanahitaji hali ya hewa yenye joto na mwangaza wa jua wa kutosha.Yanahitaji kiwango kidogo cha unyevu kwa sababu unyevu mwingi unasababisha maradhi. Unyevunyevu mwingi unaadhiri ubora na utamu wa tunda.Pia kiwango cha joto kiwe baina ya sentigredi 18 hadi 38

Udongo unao hitajika

Matikiti yanastawi vizuri katika aina mbalimbali za udongo. Matikiti yanahitaji ardhi yenye rotuba ya kutosha na wenye kupitisha maji vizuri. Uzalishaji wa matikiti unaweza kuathiriwa na maradhi ya vimelea ya
Fusari (Fusarium). Wakulima wanahitajika kupanda mbegu zinazohimili
magonjwa ama kuwa na mfumo wa mzunguko wa mimea kwa zamu katika
kipindi cha miaka saba. Kiwango cha uchachu (pH) kiwe baina ya of 5.0-6.8 ilikuiwezesha mimea kufyonza madini.

Utumizi wa mbolea

Nitrojeni ina nyunyizwa mara mbili; wakati mmea una matawi kati ya 2 na 4 na pia sehemu inayobeba matunda inapoanza kutambaa.

Nafasi katikati ya mimea

Ukubwa wa tunda unaohitajika ndio utakao eleza nafasi inayopaswa kuachwa katitati ya mimea. Nafasi kati ya sentimita 100 kwa 150 ndio bora zaidi. Ekari moja inahitaji mbegu 5,000. Mimea zaidi inaweza kupandwa ikiwa unyunyizia maji ni kwa mifereji na dripu (drip irrigation).

Maua na uchavushaji

Uchavushaji ni muhimu. Weka mzinga wa nyuki ili kuhakikisha kuwa uchavushaji unafanyika. Njia zinazotumika kuzuia wadudu zitekelezwe kwa njia itakayo wahifadhi nyuki Inastahili kuwe na unyevu kiasi wakati wa maua na matunda

Jinsi ya kuzuia wadudu na magonjwa

Wadudu wanao vamia matikiti, melon fly na aphids ndio tishio kubwa katika kuvuna matikiti.Unatakiwa kutumia madawa yaliyo sajiliwa kupigana na wadudu hawa.
Maradhi ya fangasi kama Alternaria, Fusarium, Antrachnose na ubwiri poda (Powdery Mildews) ni makali lakini yanaweza kukabiliwa kwa kutumia madawa ya Fungicide na kupanda mbegu yenye kuhimili maradhi.
Magugu yaendelee kungo’lewa, angalia usiharibu mizizi ya
mimea.

Uvunaji

Matikiti maji huvunwa yakiwa karibu sana na kuiva. Huu ni wakati ambapo sehemu ya juu ya tunda inayo gusa mchanga ina rangi ya samli/njano au sehemu inayo beba tunda inapoanza kusinyaa.
Sehemu inayobeba ua inakatwa kuizuia kukwaruza ngozi ya tunda ambayo inaweza kusababi sha maradhi mengine. Matikiti yana hatari ya kupasuka wakati au baada ya kuvuna ikiwa mkulima atakosa kuzimudu vizuri Matikiti hayafai kurushwa wakati wa kuvunwa, wala kukanyagwa au kurundikwa zaidi.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Faida ya kupanda maharagwe katikati ya kabichi

Maharagwe yanapandwa kwenye kabichi yanafanya kazi zifuatazo;

Kudhibiti wadudu (mtego).

Maharage yanaweza kupandwa kati ya mistari ya kabichi yakiwa kama mitego kwani yanasaidia kulinda kabichi dhidi ya buibui wekundu.

Kuboresha udongo.

Maharagwe yanaongeza nitrojeni kwenye udongo

Chakula cha mifugo.

Maharagwe yanaweza kutumika kulishia mifugo kama ng’ombe mbuzi na kondoo.

Matandazo.

Maharage yanaweza yakatumika kama matandazo kwenye shamba kusaidia kulinda unyevu.

Kutengenezea mbolea.

Maharagwe yakioza yanaweza kuwa mbolea nzuri ya shamba lako

Namna ya kukabiliana na Magonjwa ya kuku

Hakikisha unamuona mtaalamu wa mifugo mara uonapo dalili zozote za kuumwa kwa mifugo wako.

Tenga na wapatie tiba au kuwaua na kuteketeza kabisa kuku wagonjwa kuepuka kuenea kwa magonjwa.

Ondoa ndege waliokufa mara moja, uwafukie au kuchoma moto. Usile kuku aliekufa. Baadhi ya magonjwa ya ndege yanaweza kuambukizwa kwa binadamu.

Endapo kuna mlipuko wa ugonjwa katika eneo lako, usiruhusu watu kutembelea banda lako. Watu wanaweza kuleta maambukizi kwa miguu yao katika mabuti, nguo na mikono.

Pia magari yanaweza kuleta madhara kwa mabanda yako kupitia matairi na upakuaji wa mizigo.

Jinsi wigo wa mimea kwenye shamba unavyoweza kukinga mazao yako na wadudu waharibifu

Jinsi wigo wa mimea kwenye shamba unavyoweza kukinga mazao yako na wadudu waharibifu

Wigo wa mimea ni kinga nzuri ya mazao shambani. Mimea ya wigo inaweza kutumika kama kizuizi cha wadudu kuhama hama.

Wigo hutatiza vidukari kuhama na kuingia bustanini. Kwa mfano, mimea kama tithonia ni kizuizi kwa aina nyingi sana za wadudu.

Safu za mbaazi zimekuwa zikitumika kulinda nyanya, viazi, kabichi dhidi ya buibui wekundu.

Maharage yanaweza kupandwa kati ya mistari ya kabichi yakiwa kama mitego kwani yanasaidia kulinda kabichi dhidi ya buibui wekundu.

Maharagwe yanapandwa kama mtego kwenye kabichi lakini yanafanya kazi ya kudhibiti wadudu (mtego), kuboresha udongo, chakula cha mifugo, matandazo au kutengenezea mbolea.

Vile vile wigo wa mimea ni makazi ya wanyama/wadudu wanaowinda.

Mambo makubwa yanayosababisha kulazimika kulima au kutifua udongo

Kutifua udongo ni jambo la muhimu sana ili kuufanya udongo kuwa bora.

Umuhimu wa kutifua udongo ni kama ifuatavyo
1. Hulainisha udongo ili kuruhusu mizizi ya mimea kupenya kwa urahisi.
2. Kutifua kunaboresha uwezekano wa kupenya kwa nitrogen na oxygen kutoka kwenye hewa.
3. Kunawawezesha viumbe hai waliopo kwenye udongo kufanya kazi zao ipasavyo.
4. Kunasaidia Kuandaa sehemu ya kuwekea mbegu.
5. Kutifua kunauongeza uwezekano wa maji kupenya kwenye udongo na kupunguza uyeyukaji wa maji.
6. Kuchanganya mabaki ya mimea na samadi kwenye udongo

Jinsi ya kutunza nyumba ya kuku ili kuzuia magonjwa

1. Nyumba ya kuku iwe safi na kavu muda wote kuzuia ueneaji na kuzaliana kwa vijidudu vya magonjwa

2. Nyumba ya kuku iwe na nafasi za kupitisha hewa ya kutosha ili kuepuka joto na unyevunyevu ambao unachangia uwepo wa magonjwa kwa kuku

3. Hakikisha unaondoa matandazo na takataka zote kwenye banda wakati wote hasa yenye unyevu.

4. Fagia banda na kuhakikisha ni safi wakati wote. Weka matandazo mapya mara kwa mara.
5. Weka sehemu za kutosha kuku kupumzikia.
6. Weka viota vya kutosha.
7. Weka maji sehemu ambayo ni rahisi kusafisha.
8. Hakikisha unaondoa wanyama kama panya na wadudu nyemelezi kwenye sehemu ya malisho ya kuku kwani wao hubeba vimelea vya magonjwa.

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya mboji kitaalamu na kwa urahisi

Mbolea ya mboji hutokana na mabaki ya majani na miti. Majani na miti yanapooza hugeuka na kutengeneza virutubisho ambavyo husaidia kurutubisha udongo na kupunguza gharama.

Mboji ikichanganywa kwenye udongo huifanya mimea kustawi na kuwa na afya ya kujikinga na magonjwa yanayoshambulia mimea. Kwa kawaida wadudu waharibifu hutafuta mimea ambayo ni dhaifu. Udongo ambao umeimarishwa kwa mboji huwa na mimea michache dhaifu. Kwa hivyo, siyo rahisi kushambuliwa na wadudu.

Mbolea ya mboji ina madini yanayosaidia kuyeyusha madini mengine yaliyo kwenye udongo na kufanya yapatikane zaidi kwa ajili ya mimea kwa muda mrefu. Vijidudu ambavyo hujilisha kwa njia ya mbolea ya mboji kwa muda mfupi hushikilia udongo pamoja, na kuufanya udongo uwe bora na wenye afya.

Faida nyingine ya mbolea ya mboji ni kwamba mbolea hii hupunguza ama huondoa kabisa utumiaji wa mbolea za chumvichumvi na dawa za kuua wadudu ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa afya za watu na udongo, ambazo pia ni gharama sana kununua.

Mahitaji ya kutengenezea mboji

Wakati wa kutengeneza mboji unahitajika kuwa na malighafi za kijani na kahawia.

Malighafi za kijani
Mimea yenye kijani kibichi na ambayo haijachanua inafaa zaidi katika kutengezeza mboji, na iwe imekatwa karibuni. Mabaki ya chakula na matunda pia yanajumuishwa katika kundi la malighafi za kijani.

Malighafi za Kahawia
Kundi la malighafi za kahawia ni pamoja na mimea ambayo imekauka baada ya kukatwa muda mrefu, pamoja na kinyesi cha wanyama wafugwao. Udongo na maji ni sehemu muhimu ya mahitaji kwa ajili ya kutengeneza mboji.

Vitu visivyotakiwa kwenye mboji

  • Mabaki ya mimea ambayo imeambukizwa magonjwa au imeshambuliwa na wadudu haitumiwi kwani inaweza kuwa na mayai ya wadudu na inaweza kuendelea kuzaliana.
  • Mimea yenye tindi kali kama vile migunga na Eucalyptus haifai, ijapokuwa kuna wakati inaweza kutumika kutengeneza mboji maalum kwa ajili ya kuongeza kiwango cha tindi kali kwenye udongo inapohitajika.
  • Magugu sugu kama sangare, mashona nguo na ukoka mgumu hayafai kwa kuwa yatasambaza mbegu za magugu katika shamba lako.
  • Usitumie kinyesi cha wanyama kama mbwa na paka.

Kutengeza mboji

Ili uweze kutengeneza mboji nzuri, unatakiwa kurundika rundo kwa matabaka. Kiwango cha wastani kinachofaa kutengeneza mboji ni chenye urefu wa mita moja, na mita moja upana. Rundo ambalo ni dogo kuliko hili haliwezi kuhifadhi joto la kutosha kuozesha malighafi. Hakuna kikomo cha ukubwa wa biwi la mboji, inategemea na ukubwa wa eneo ulilonalo na unataka mboji kiasi gani. Chakuzingatia ni kuwa lisiwe dogo.

Hatua za kufuata kutengeneza mboji

Hatua ya 1
Ondoa majani yote pamoja na vitu vingine vinavyoweza kuharibu mboji yako, kisha lainisha udongo kiasi cha inchi sita kwa kutumia rato au jembe. Hatua hii inasaidia maji kupenya chini
ya rundo la mkusanyiko wa kutengenezea mboji.

Hatua ya 2
Weka tabaka la kwanza kubwa kuliko matabaka mengine. Unaweza kutumia majani makavu, mabuwa ya mahindi na matawi madogo madogo ya miti. Vitu hivi pia ni vizuri kwa rundo la mboji na hurahisisha umwagiliaji maji. Weka rundo la tabaka la kwanza la mabuwa ya mahindi vijiti na matawi madogomadogo ili liwe tabaka lenye inchi sita kwa mita moja kila upande.

Hatua ya 3

Tengeneza tabaka la pili lenye ukubwa wa inchi mbili na malighafi za kijani. Kumbuka kwamba: Tabaka liwe jemjembamba kuliko tabaka la kwanza. Kama una mabaki ya chakula ongeza kwenye tabaka hili.

Hatua ya 4

Weka Tabaka la tatu la udongo lililochanganywa na mbolea au majivu. Tabaka hili liwe jembamba, kama unene wa robo inchi. Unahitaji kutumia kiasi kidogo tu cha mbolea kufunika sehemu ndogo tu katikati ya rundo la mboji kama vile futi moja kwa futi moja. Ni muhimu kutotumia mbolea nyingi kwenye rundo la katikati. Kama unatumia majivu, kiasi kidogo tu kitumiwe katikati ya rundo la mboji. Ukishaweka mbolea katikati, unaweza kuizungushia udongo kufunika tabaka la kwanza.

Hatua ya 5

Ongeza maji ya kutosha kila wakati kwenye rundo la mboji ili liwe na unyevunyevu, lakini yasiwe mengi kiasi cha kutota. Kumbuka, rundo la mboji liwe na unyevunyevu mfano wa sponji iliyowekwa kwenye maji na kukamuliwa.

Hatua ya 6

Kwa kufuata hatua zilizotangulia, kama unataka kuongeza matabaka, rudia kama ulivyofanya mwanzo. Tabaka la majani makavu, ya rangi ya kahawia lenye inchi mbili, likifuatiwa na tabaka la kijani la inchi mbili, likifuatiwa na tabaka jembamba la udongo uliochanganywa na mbolea au majivu au vyote. Endelea kuweka matabaka haya mpaka matabaka yako yawe na urefu wa futi tatu au nne kwenda juu.

Hatua ya mwisho

Weka tabaka la juu mwisho lenye majani makavu ya kikahawia lenye unene wa inchi tatu. Hii husaidia kuhifadhi harufu ambayo wakati mwingine hutokea wakati wa uozaji. Hii pia husaidia kufukuza wanyama ambao huvutiwa na kutaka kuona kuna nini kwenye rundo la mboji.

Baada ya muda Rundo la mboji litakapokuwa tayari, utabakiwa na mboji ambayo itaonekana kama udongo mweusi ulio na mbolea nzuri.

Matumizi ya mbolea ya Mboji

Chukua mboji ambayo ni tayari yani iliyo na udingo mweusi wenye mbolea nzuri na utandaza tabaka jembamba kwenye mazao yako na mimea itastawi, kunawiri vizuri na kutoa mazao bora.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Jinsi ya Kufuga vizuri kware Kwa Faida

Kware au Kwale au Kereng’ende ni jamii ya ndege ambao kwa sasa wanafugwa majumbani na wanaotaga mayai kama kuku ama bata na kwa wingi sana.

Ndege hawa ni wadogo 280gm – 300gm, rangi ya kwale ni kahawia au kijivu na wana michirizi au madoa. Mara nyingi miguu yao ni myekundu au rangi ya manjano na koo lao ni jekundu, jeupe, jeusi au rangi ya manjano.

Chakula

1. Kware anakula chakula chochote anachoweza kula kuku ikiwemo chakula cha broiler. Kama utaamua kuwapa chakula cha broiler unawapa “starter” kware wenye umri kuanzia siku moja hadi wiki ya tatu baada ya hapo unawapa Falcon au hill.

2. Ukiweza kuwatengenezea chakula chako mwenye kutumia pumba nk. Ni vizuri zaidi kwa mayai yenye lishe 100%

3. Kware 100 wenye umri wa mwezi hutumia kiroba cha kilo 20 kwa wiki 3.

4. Kware hawamalizi chakula kama kuku.

5. Pia kware hupewa majani kama mchicha nk.

Kutaga na kuatamia kwa Kware

Kware dume humpanda jike kwa muda kidogo, Hapo jike anakuwa tayari kutaga na hutaga mayai 290 hadi 310 kwa mwaka (hii hulingana na lishe nzuri atakayopatiwa).

Mayai ya Kware huatamiwa kwa siku 18 na huanza kuanguliwa vifaranga kwa muda wa siku 2, kuanzia siku ya 18 na hadi 20.

Njia bora ya kutotolesha mayai ya Kware ni kwa kutumia incubator ambapo mayai huatamiwa kwa wingi ndani ya siku 18.

Utunzaji wa vifaranga vya kware na chakula

Utunzaji wa vifaranga vya kware Siku 1 – 7

Vifaranga wapatiwe chakula “STARTER PELLET” na maji masafi ya kutosha. Siku ya 1 wawekee ‘GLUCOSE’ kwenye maji, Packet moja kwa lita 20 za maji, na siku ya pili hadi ya tano wawekee Amin Total kwenye maji, Wape maji pekee siku ya sita na siku ya saba wapatie chanjo ya Newcastle. Utawapatia joto kwa njia ya umeme kwa ‘BULB’ mbili (2) za 200watts kwa kila vifaranga 300, ama unaweza kuweka taa ya ‘Energy Server’ pamoja na jiko la mkaa uliofunikwa na majivu ambao utakidhi kuwapatia joto sawia kwa masaa 24 kwa siku 7. (Majivu yanasaidia moto kukaa kwa muda mrefu)

Banda/box lako liwe la ukubwa wa 1.5m x 1.5m (au eneo la ukubwa huo ndani mwa banda kubwa la kufugia kuku) lazima uzingatie usalama wa vifaranga dhidi ya panya, paka au vicheche. Unatakiwa kuweka magazeti au mabox chini kwenye sakafu yatakayosaidia usafi. Kwa week ya kwanza chakula kitawekwa chini na tunashauri utumie chakula cha pellet ili kusaidia vifaranga wasiteleze na kuathiri miguu. NOTE: Weka gololi au mawe kwenye drinkers zako ili kuzuia vifaranga wasizame ndani ya (drinkers) maji na kufa.

Utunzaji wa vifaranga vya kware Siku 8-14

Vifaranga wataendelea kupewa chakula “STARTER PELLET” na maji safi. Wataendelea kuhitaji ‘mwanga’ wa kutosha muda wote na joto la wastani bulb 2 za watts 100 au moja ya watts 200

Utunzaji wa vifaranga vya kware Siku 15-21

Uhitaji wa joto utapungua, ila ni kipindi ambacho wanakula chakula zaidi kwa ajili ya kukua. Ni vizuri waendelee kupata taa ili kupata mwangaza utakayowawezesha kula mchana na usiku.

Utunzaji wa vifaranga vya kware Siku 21 na Kuendelea

Kware wako hawatahitaji joto tena wawekee taa tu za energy server kipindi cha usiku, wape chakula na maji ya kutosha zaidi kwa ajili ya kukua.

UTAGAJI WA KWARE

WIKI YA SITA

Wiki ya sita kuelekea ya saba Kware wako wataanza kutaga mayai kila siku, kwa wastani Kware mmoja hutaga mayai 300 kwa mwaka.

Magonjwa ya Kware

Kware ni ndege wenye kinga kubwa na ni vigumu sana kushambuliwa na magonjwa kama kuku na mara wanapougua ni rahisi sana kutibika. Magonjwa yanayoweza kuwapata Kware ni typhoid, mafua na kuharisha .

Tiba za asili za kware

Waweza kuwatibu vifaranga au Kware wako kwa kutumia njia ya asili ambayo pia ni rahisi, gharama nafuu na bora zaidi kuliko kutumia madawa yaliyochanganywa na kemikali na yenye gharama.

Vifuatazo ni vitu vya asili vinavyotumika kutibu magonjwa mbali mbali kwa Kware na yanayopatikana kwa wingi katika maeneo ya mfugaji. Madawa haya hutumika kwa kiwango cha wastani na hayana kipimo maalum kwani hata ukiyazidisha hayana madhara.

Mwarobaini na Aloe Vera:

Madawa haya hutumika kutibu kuharisha damu pamoja na mafua kwa vifaranga vya Kware. Chukua kiasi kidogo cha mwarubaini kisha twanga vizuri kupata maji maji. Kamua maji yale, kisha weka katika maji uliyoandaa kuwanywesha vifaranga wako. Kata vipande vidogovidogo vya aloe vera (jani moja laweza kutosha) na tia katika maji yaliyochanganywa na mwarobaini, kisha wapatie vifaranga wanywe (Aloe Vera itaendelea kujikamua yenyewe ikiwa ndani ya maji huku vifaranga wakiendele kunywa).

Kitunguu swaumu:

Hii hutumika kukinga na kutibu vifaranga vya kware wanaosumbuliwa na kuharisha damu. Unachukua kitunguu swaumu na kuondoa maganda ya nje kisha kusafisha na kukata vipande vidogo sana, na kuwawekea kama chakula. Vifaranga wanapenda sana vitunguu hivyo na watakula kwa kasi kama chakula lakini ni tiba tayari. Unaweza kuwapatia kila siku hadi watakapo pona.

Maziwa:

Maziwa yanayotokana na ng’ombe pia hutumika kutibu ugonjwa wa kuhara pamoja na kuwapa nguvu Kware waliolegea. Mnyweshwe maziwa hayo Kware anayeumwa bila kuyachemsha na umnyweshe maziwa ya kutosha kiasi cha kushiba. Unamnywesha mara tatu kwa siku. Hakikisha maziwa unayotumia yanatoka kwa ng’ombe wanaotibiwa kila mara.

Angalizo

Siyo lazima Kware waugue ndipo uwapatie tiba hizi. Hakikisha unawapa tiba kabla hata hawajaugua hivyo utawakinga na magonjwa hayo. Waweza kuchanganya madawa hayo yote kwa wakati mmoja kwani hayana madhara.

Endapo madawa ya asili hayapatikani katika eneo la mfugaji basi waweza kuwatibu Kware kwa madawa yafuatayo ambapo vipimo huelezwa moja kwa moja kwa maandishi katika madawa hayo au kuelezwa na muuzaji pale utakaponunulia; Amprolium kwa ugonjwa wa kuharisha damu (Coccidiosis), Fluban,Coridix au Doxyco kutibu mafua (Coryza) na Esb3,Trisulmycine au Trimazine hutumika kwa homa ya matumbo (Typhoid).

ZINGATIA:

Wanapokosa madini ya kutosha kwenye chakula huweza kupata madhara yafuatayo:-
1. Kuharisha
2. Kunyonyoka manyoya
3. Kupunguza kasi ya kutaga mayai.

Chanjo Ya kware

Siku ya 7 lazima vifaranga wapatiwe chanjo ya “kideri/mdondo”
(respiratory & digestive diseases) kwa dawa inayoitwa ‘newcastle’. Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi na pia husababishwa na virusi kwa njia ya hewa.

Siku ya 14 lazima wapewe chanjo ya “gumboro”. Chanzo cha
maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi na pia husababishwa na virusi kwa njia ya hewa.

Siku ya 21 lazima warudie chanjo ya “Newcastle (aina ya IBDL)”. Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi na pia husababishwa na virusi kwa njia ya hewa.

Siku ya 35 lazima wapate chanjo ya “Ndui”.

Soko la kware

Mayai ya Kware ni bidhaa adimu sana hapa nchini kwa kuwa ni wafugaji wachache waliojikita katika ufugaji huu, Ufuatao ni muhtasari wa wastani wa bei ya bidhaa za Kware sokoni

1. Trei ya (mayai 30) ya KWALE inauzwa shilingi 30,000 .
2. Kifaranga wa Kware wa siku moja anauzwa shilingi 2500 – 3000
3. Kware wa week 4 (mwezi mmoja) anauzwa kwa shilingi 10,000– 12,000
4. Kware aliyeanza kutotoa (week 6) huuzwa shillingi 20,000 – 25,000
5. Kware kwa aliyekomaa kwa ajili ya kitoweo huuzwa kwa shilingi 25,000
6. DROPING za Kware huuzwa kwa shilingi 10,000 kwa 50kg kwa wafugaji wa samaki

Soko la KWALE liko juu sana kwa mayai na nyama. KWALE pia hutofautiana bei kwa jike na dume.

FAIDA ZA KUFUGA KWALE

Ufugaji wa kwale hua na faida ukilinganisha na ufugaji wa ndege wengine

· Chanzo cha kipato kwa wafugaji.
· Hawana gharama sana katika suala kufuga.
· Hawataji utaalam sana katika kuwafuga.
· Mayai yake ni tiba ya magonjwa mbalimbali.
· Mayai yake hayakosi soko.

Jinsi ya kufanya nyuki waingie kwenye mzinga mpya

Ukitaka kuwavutia na kuingiza nyiki kwenye mzinga unatakiwa kufanya yafuatayo;

  1. Tafuta mahali pazuri pa-kuning’iniza mzinga wako.
  2. Weka nta kwenye mizinga yako ili kuwavutia nyuki.
  3. Hakikisha unaweka mizinga yako katika hali ya usafi na kusiwe na wadudu. Nyuki hawapendi kukaa mzinga mchafu.
  4. Hakikisha hakuna siafu wala panya wanaoishi kwenye mzinga.
  5. Ning’iniza mzinga msimu ambao kuna makundi mengi ya nyuki yanayohama. Makundi ya nyuki huama wakati ambao nyuki wamezaliana kwa wingi na kuwepo malikia mwingine kwenye mzinga hivyo kusababisha kuhama ili kuunda kundi jingine. Msimu huo wa mgawanyiko ni rahisi nyuki kufanya makazi katika mzinga wako kwa haraka. Kama haujui msimu wa makundi ya nyuki kuhama waulize wakulima wenzio wanaofuga nyuki katika eneo lako.

Mambo 8 ya kuzingatia kabla ya kuleta mifugo (kuku, ng’ombe,mbuzi n.k) wapya bandani

Mambo hayo ni haya yafuatayo;
1. Hakikisha unaondoa matandazo yote ndani ya nyumba,
2. Ondoa vyombo vya kulishia na kunyweshea.

3. Ondoa uchafu wote unaoonekana bandani.
4. Safisha banda lote kwa kutumia maji na dawa.
5. Suuza na uache likauke.
6. Puliza dawa ya kuua wadudu.
7. Weka matandazo mapya,
8. Weka viombo vya kulishia na kunyweshea.

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya maji ya kunyunyiza kwenye majani

Mbolea ya kunyunyiza ni nzuri kwani inasaidia kuupa mmea virutubisho moja kwa moja kupitia kwenye majani au shina ambapo ndipo chakula kinahitajika.

Faida za mbolea ya maji ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha mavuno, uwezo wa mimea kukabiliana na wadudu pamoja na magonjwa, kuvumilia ukame, na kuongeza ubora wa mazao.

Jinsi ya kuandaa mbolea ya maji kwa kutumia samadi

Mbolea ya maji hutengenezwa kwa kuchukua kiroba kilichojazwa samadi, aina mbalimbali ya mimea yenye virutubisho na inayoaminika kuwa dawa ya mimea. Kiroba hicho kinafungwa kwenye kijiti, na kutumbukiza kwa kuning’inia kwenye pipa lililojazwa maji.

Kiroba hicho ni lazima kichukue kati ya kilo 30-50 za samadi pamoja na aina nyingine za mimea kwa maji lita 200 (tazama mchoro). Unaweza kushika upande mmoja wa mti na kunyanyua na kushusha kila baada ya siku tano ili kuchanganya na kuharakisha kutolewa kwa virutubisho zaidi.

Kwa kawaida mchanganyiko huo unakuwa na harufu kali sana maana Nitrojeni nyingi inayopatikana hugeuka kuwa Amonia. Ni vizuri kufunika pipa ili kuzuia kuyeyuka kwa nitrojeni. Harufu ikishaisha, ujue mbolea yako ipo tayari kwa matumizi.

Ongeza maji na utingishe vizuri kabla ya kutumia. Nyunyizia mimea yako kila wiki mpaka utakapoona mabadiliko.

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya maji kwa kutumia mimea peke yake (Majani fresh)

Mbolea hii hutengezwa kwa kuchukua majani mabichi na kuyakatakata na kisha kuyachanganya na maji kidogo.

Baada ya kuchanganya na maji unaacha kwa siku tatu au nne ambapo utatikisa mchanganyiko wako kila siku.

Baadae utatikisa na kuchanganya na maji na kunyunyiza shambani.

Vilevile Unaweza kutumia mbolea ya majani ambayo itakuwa kama dawa ya kuulia wadudu, kwa kutumia aina ya mimea kama vile mivule, mibangi mwitu, majani ya minyanya, mwarobaini, mashona nguo, pamoja na vitunguu saumu. Aina hii ya mimea inasaidia sana katika kuzuia magonjwa, wadudu na kutoa virutubisho muhimu kwa mimea vinavyosaidia mkulima kupata mazao bora bila gharama ya ziada ya kununua virutubisho.

Vigezo vya kunyunyiza mbolea ya maji

Ili upate matokeo mazuri wakati wa kunyunyiza mbolea ya maji unatakiwa kufuata vigezo vifuatavyo:
• Inashauriwa kutumia mbolea iliyochanganywa vizuri ili kuepukana na kuunguza mimea.
• Acha maji utakayotumia kuchanganyia mbolea yako nje katika pipa lililowazi usiku kucha, hii inasaidia kutoa madini hatarishi, na kufanya mchanganyiko wenye faida kwa mimea.
• Unatakiwa kutingisha vizuri mbolea yako ya maji kabla ya kunyunyiza. Chembechembe ndogo ambazo hazikuyeyuka zinaweza kuziba mdomo wa bomba la kunyunyizia.
• Matokeo mazuri yanaweza kupatikana endapo mbolea imechanganywa vizuri na kunyunyiziwa wakati hakuna upepo.
• Unatakiwa kunyunyizia mbolea wakati wa asubuhi au jioni wakati hakuna joto na upepo ukiwa umepungua.

Angalizo
Kabla ya kunyunyiza dawa au mbolea uliyoitengeneza mwenyewe shambani nyunyiza kwenye eneo dogo au mimea michache kwanza ili uone kama inaunguza au haiunguzi. Kumbuka kuwa mchanganyiko mwingine ukiwa cream au ukikolea sana unaweza kuchoma. Kwa hiyo kuepuka hili nyunyiza mahali padogo kwanza.

Jinsi vitunguu swaumu vinavyosaidia kuzuia wadudu shambani

Vitungu saumu vina manufaa sana katika kukabiliana na aina mbalimbali za wadudu waharibifu na baadhi ya magonjwa kutokana na kuwa na harufu kali inayosaidia kuwafukuza wadudu kama vidukari, bungo na hata panya.

Hatua za kufuata kutengeneza dawa ya kitunguu saumu

  1. Saga kitunguu saumu kimoja,
  2. Changanyakwenye lita moja ya maji
  3. Nyunyizia kwenye mazao.

Namna nyingine ya kutengeneza dawa

  1. Unaweza pia kusaga vitunguu saumu 3,
  2. kishachanganya na mafuta taa,
  3. acha ikae kwa siku tatu,
  4. kisha ongeza lita 10 za maji ya sabuni na unyunyizie.

Hii itaondoa aina nyingi sana ya wadudu wanaosababisha magonjwa.

Namna ya kulisha kuku ili wasipatwe na magonjwa

Safisha vyombo vya kulishia na kunyweshea kila siku. Osha, sugua vizuri, kisha suuza kuondoa utando unaobeba bakteria.

Kuku wanahitaji wapewe chakula cha kutosha na chenye virutubisho vyote. Unaweza kuwaongezea majani, makombo, nafaka, mchanga laini, au maganda ya mayai.

Wapatie kuku maji safi muda wote. Wafugaji wengi wameripoti kuwa na matokeo mazuri baada ya kuchanganya dawa ya kuua vimelea kwenye maji ya kunywa.

Nunua chakula kwa wauzaji wazuri na wanaoaminika ili kuepuka minyoo na sumu hatarishi. Usiwape kuku chakula chochote kinachoonekana kuoza au kunuka uvundo.

Hifadhi chakula cha kuku katika sehemu kavu isiyo na joto na isiwe kwa zaidi ya miezi mitatu ili kuepuka kuharibiwa na fangasi.

Jinsi ya kulima vizuri zao la kabichi

Kichwa cha kabichi kinapofunga vizuri, hutumika kama chakula na huvunwa baada ya kufunga na kukomaa vizuri. Kwa kawaida kabichi hupandwa kwa msimu mmoja, lakini iwapo itakuzwa kwa ajili ya kutoa mbegu hukuzwa zaidi ya msimu mmoja. Endapo inalimwa sehemu yenye maji ya kutosha, inaweza kulimwa msimu wote wa mwaka. Soko lake ni la uhakika katika kipindi chote na ni muhimu kwa afya. Pia, linaweza kutumika kama malisho ya mifugo
Mizizi: Mizizi ya kabichi hutawanyika ardhini vizuri. Kwa kawaida, huenda chini kiasi cha sentimita ishirini (20 sm), na hujitawanya kwa kiasi cha sentimita sabini na tano (75sm).
Shina: Shina la mmea wa kabichi huwa na rangi ya kijani au zambarau. Hii hutegemeana na aina ya kabichi, na kwa kawaida ni fupi.

Aina za kabichi

Kuna aina nyingi za kabichi na zifuatazo ni miongoni mwa aina hizo:
1. Prize drumhead

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5
2. F1-High Breed

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 2-4
3. Duncan

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3
4. Early Jersey wakefield

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5
5. Sugar loaf

Aina hii hukomaa mapema sana, kiasi cha miezi 2.5
6. Glory of enkhuizen

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5

Jinsi ya kulima kabichi

Hali ya hewa

Kabichi hustawi vyema katika sehemu yenye hali ya baridi, hali ya joto jingi haifai kwa kabichi kwa kuwa huathiri uotaji na ukuaji wake. Joto jingi pia husababisha kulegea kwa vichwa vilivyofunga. Zao hili hustawi vema katika maeneo yenye mwinuko wa zaidi ya mita 100 toka usawa wa bahari.

Udongo

Zao hili linaweza kustawishwa kwenye udongo wa aina yoyote mradi tu udongo huo usiwe na chumvichumvi nyingi na usiotuhamisha maji. Udongo wa kichanga na ule usio na rutuba ya kutosha husababisha kabichi kukomaa upesi na kuzaa kabichi hafifu zenye vichwa vidogo.

Kitalu cha kabichi

Kitalu ni muhimu katika uzalishji wa zao hili. Ni vema kutengeneza matuta yenye upana wa mita moja, na urefu wowote kulingana na matakwa ya mkulima. Mbolea za samadi na zenye asili ya chokaa zichanganywe vizuri kwenye udongo. Kiasi cha gramu 500 za mbegu huhitajika kwa hekta moja. Katika upandaji kwenye kitalu ni vizuri kutengeneza mistari katika tuta, umbali toka mstari hadi mstari uwe sentimita ishirini (20). Udongo kiasi kidogo utumike katika kufunika mbegu.
Baada ya mbegu kuota ni vizuri kupunguza baadhi ya miche na uwe katika kipimo cha sentimita 2-3 toka mche hadi mche. Hii itasaidia kuwa na miche mifupi na yenye nguvu. Inafaa kunyeshea kitalu mara moja au mbili kwa siku na katika sehemu za joto ni vizuri kuweka kivuli katika matuta. Katika wiki ya tatu, hadi wiki ya nne, ni vyema kuondoa kivuli kidogo kidogo huku ukipunguza unyeshaji. Hali hii itasaidia miche isipate mshtuko wa uhamishaji shambani.

Kuhamisha na kupanda

Hamisha na kupandikiza miche shambani ikiwa na umri wa wiki nne, wakati huo miche ikiwa na majani manne ya mwanzoni na urefu wa kiasi cha sentimita kumi na mbili (12). Wakati wa upandaji, ni vizuri udongo ukashindiliwa kwenye kila mche. Inafaa upandaji ufanyike mara moja, na ni vizuri ukafanyika nyakati za jioni au asubuhi sana, na udongo uwe na unyevu wakati wote.

Nafasi kati ya mmea

Katika mstari hadi mstari inatakiwa iwe sentimita 60-75. Kutoka mmea hadi mmea ni sentimita 30-60. Pia sentimita 75-90 inaweza kutumika kati ya mstari na mstari.

Mbolea

Ni vizuri kuweka kiasi cha viganja 2-3 vya mbolea ya samadi iliyooza vizuri katika kila shimo.

Palizi

Wakati wa palizi ni vizuri mkulima akawa mwangalifu ili asiharibu mizizi. Wakati kabichi inapoanza kufunga hufunika ardhi, hivyo, husaidia kuzuia magugu yasiote, kwa wakati huu hakuna haja ya kupalilia.

Kuvuna:

Kabichi hukomaa katika kipindi cha siku 60-100 tangu kupandwa. Kwa ajili ya kuuza ni vizuri kuvuna wakati vichwa vinapofunga vizuri na huwa na uzito wa kutosha kabichi iangaliwe na kutunzwa baada ya kuvunwa ili isikwaruzwe na kuoza kabla ya kutumiwa. Kwa kawaida hekta moja hutoa mavuno kiasi cha tani 50-80.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Mambo 6 muhimu ya kuzingatia kupata udongo bora mzuri shambani

1. Usiuchoshe sana udongo

Udongo ni kiungo muhimu sana katika uzalishaji wa mazao. Ni mfumo wa uhai kwa mimea. Kwa hiyo, mkulima ni lazima alenge katika kutunza uhai wa udongo na kuepuka usumbufu kwa uhai wa udongo.
Sababu muhimu za kulima/kutifua udongo ni:
• Hulainisha udongo ili kuruhusu mizizi ya mimea kupenya kwa urahisi.
• Kutifua kunaboresha uwezekano wa kupenya kwa nitrogen na oxygen kutoka kwenye hewa.

• Kunawawezesha viumbe hai waliopo kwenye udongo kufanya kazi zao ipasavyo.
• Kunasaidia Kuandaa sehemu ya kuwekea mbegu.
• Kutifua kunauongeza uwezekano wa maji kupenya kwenye udongo na kupunguza uyeyukaji wa maji.
• Kuchanganya mabaki ya mimea na samadi kwenye udongo

2. Acha udongo upumue

Kama ilivyo kwa binadamu, viumbe hai wanahitajika kwa udongo wenye rutuba, pia mimea inahitajika kwa ajili ya binadamu kupata hewa safi ya oxygen. Kuchanganya matandazo,na mboji kwenye udongo ni muhimu sana ili kuboresha mzunguko wa hewa. Viumbe hai wadogo wadogo, wadudu, minyoo, na wanyama wengineo wanapenyeza hewa kwenye udongo.

3. Weka Matandazo kwenye udongo

Huu ni utaratibu wa kufunika udongo kwa kutumia mabaki ya mimea, kwa mfano, matawi madogo madogo ya miti, majani, mabaki ya mimea ya mazao, magugu na kadhalika. Hata hivyo inahitajika nguvu kazi kwa ajili ya kutawanya matandazo.

Matandazo yanazuia mmomonyoko wa ardhi unaotokana na maji na upepo, yanasaidia ardhi kunyonya maji ya mvua, kutunza unyevu unyevu kwenye udongo kwa kuzuia myeyuko wa maji ardhini.

Matandazo yanapo oza hutoa virutubisho vinavyoboresha na kuongeza rutuba kwenye udongo, mbali na hilo pia hubadilika kuwa udongo mweusi wenye rutuba zaidi. Kama kuna uhitaji wa kuharakisha kuoza kwa matandazo ili kuongeza rutuba kwenye ardhi kwa haraka, kinyesi cha ng’ombe kinaweza kuwekwa na kutandazwa juu ya matandazo, hii husaidia kuongeza virutubisho vya nitrogen.

Matandazo yana faida nyingi sana kwenye ardhi, lakini pia yanaweza kusababisha madhara. Mabaki ya mboga za majani yasitumike kama matandazo kwani yanaweza kusababisha wadudu na magonjwa kwa mimea. Viumbe hatari kama bangu (stem borers) wa shina wanaweza kuishi kwenye mabaki ya mimea.

Mabaki ya mimea iliyokuwa imeathiriwa na magonjwa ya virusi au fangasi yasitumike kama matandazo kuepuka uwezekano wa magonjwa hayo kuambukizwa kwa mazao yatakayopandwa msimu utakaofuata. Kilimo cha mzunguko ni njia bora kuepuka athari hiyo.

4. Panda mazao kwa mzunguko

Kupanda mazao kwa mzunguko ina maana ya kuwa na aina mbalimbali ya mazao katika eneo moja kwa msimu.

Kwa mfano, kama shamba lako umepanda mahindi na maharagwe kwa kipindi cha mwaka mmoja, mkulima anaweza kubadili mzunguko kwa kupanda aina nyingine ya mazao katika eneo hilo kwa mwaka unaofuata.

Mimea iliyo mizuri zaidi katika kilimo cha mzunguko ni pamoja na jamii ya kunde, au malisho kama sesbania ambayo husaidia kuongeza rutuba kwenye udongo.

5. Lisha udongo

Udongo unatakiwa ulishwe ili uwe na virutubisho. Hii ni kazi muhimu sana kwa kila mkulima. Mkulima anaweza Kuulisha udongo kwa kutumia samadi na mboji. Kumbuka udongo uliotumika sana bila virutubisho, umekufa, hauwezi kuzalisha.

6. Kuwa makini na maji

Maji ni mazuri shambani, lakini maji yakizidi ni hatari. Maji yakizidi shambani yanaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo. Mmomonyoko wa udongo ni tishio na baa hatarishi kwa rutuba kwenye udongo. Mmomonyoko unaondoa tabaka la juu la udongo, sehemu ambayo ndiyo yenye rutuba zaidi.

Kupanda mimea kwa matuta (kontua) hupunguza kasi ya maji. Baada ya miaka kadhaa, nyasi zinazopandwa zinazopandwa kwenye matuta ya kontua husaidia kuunganisha na kusawazisha sehemu iliyotengwa, kwa kuwa udongo unaomomonyolewa hukusanyika katika sehemu iliyozuiwa na kuunganishwa kwa matuta.

Kwenye mwinuko mkali, kuta au mashimo, ndiyo njia pekee inayoweza kuzuia mmomonyoko wa udongo. Changanya na mimea kama matete, inasaidia kuzuia mmomonyoko na pia kutoa malisho kwa mifugo.

Mbali na matandazo (tazama hatua ya 3) mimea inayotambaa ni mbinu nyingine nzuri zaidi inayoweza kuzuia mmomonyoko wa ardhi. Matone ya maji hufikia ardhi yakiwa na nguvu kidogo sana hivyo kuepuka kumomonyoa ardhi, kwa kuwa yanakuwa tayari hayana nguvu ya kutiririka kwa kasi. Pia mimea inayotambaa hutumika kama kivuli kwa udongo. Mmea wowote unaofunika udongo na kuongeza rutuba unaweza kutumika.

Mfano maharage na mimea mingine ya jamii ya kunde, ambayo ina virutubisho vya nitrogen kwa wingi. Mimea inayopendekezwa ni ile ya jamii ya kunde. Inastahimili ukame, inatoa virutubisho vya naitrojeni, inatoa chakula, na pia inaweza kutumika kama chakula cha mifugo kilicho na protini nyingi. Kwa kuongezea inaweza pia kukabiliana na wadudu waharibifu.

Kilimo kizuri cha pilipili hoho

Pilipili hoho ni zao la jamii ya pilipili isiyo kali, tunda lake ni nene kiasi la duara pia linaweza kuwa lililochongoka. Pilipili hoho hutumika katika kutengeneza rangi za asili za vyakula ambazo kwa sasa hupendwa zaidi kuliko zile zinazotokana na kemikali na pia huongeza ladha na harufu katika vyakula. Hivyo hutumika katika viwanda vya kusindika vyakula, kwa mapishi ya nyumbani na hata katika viwanda vya vipodozi kama rangi ya mdomo, uso n.k. Ina virutubisho muhimu vinavyohitajika mwilini kama madini ya chuma, vitamin A na C.

Hali ya hewa

Hoho hustawi vema katika maeneo ya usawa wa bahari hadi mwinuko wa mita 2,000 yenye mvua ya wastani wa mm.600-1,250 na wastani wa joto la nyuzi za sentigredi 21 hadi 24.

Udongo

Udongo wa tifitifu wenye rutuba, usiotuamisha maji na wenye hali ya uchachu (pH) kati ya 5.0-6.5 hufaa zaidi. Umwagiliaji ni muhimu pale mvua inapokuwa chache.

Jinsi ya kulima hoho

Kitalu

Tayarisha kitalu kabla ya msimu wa mvua. Andaa vizuri matuta manne yenye urefu wa wastani wa mita 10 kila moja na upana wa mita moja (1) ili kustawisha miche inayotosha ekari moja. Chagua eneo katika ardhi isiyo na mtelemko mkali na yenye rutuba ya kutosha. Ardhi iwe imepumzishwa bila kuoteshwa mazao ya jamii ya pilipili, biringanya, nyanya, n.k. ili kuepukana na mashambulizi ya wadudu na magonjwa.

Upandaji wa mbegu

Mwagilia maji ya kutosha siku moja kabla ya kusia mbegu na endelea kunyweshea kulingana na hali ya hewa na hali ya udongo. Sia mbegu kwenye, mstari, nafasi kati ya mstari na mstari ni sm 10 na kina cha sm1. Kiasi cha mbegu cha nusu kilo kinatosha eneo la hekta moja. Weka matandazo kwenye kitalu au tumia nailoni nyeusi ili kuhifadhi unyevunyevu na kuzuia uotaji wa magugu.
Mbegu ambazo hutumika ni chotara ambazo huuzwa kwenye maduka ya pembejeo za kilimo nchi nzima. Haishauriwi kutumia mbegu kutoka zao la msimu uliopita kwani ubora wa paprika utaharibika na hivyo kuharibu soko unashauriwa kununua mbegu bora.

Utayarishaji wa shamba

Shamba lilimwe vizuri na kuweka matuta ili kuhifadhi unyevunyevu na kurahisisha umwagiliaji. Matuta yanaweza kuwa makubwa au madogo kulingana na matakwa ya mkulima. Matuta makubwa hupandwa mistari miwili na matuta madogo hupandwa mstari mmoja.

Upandaji wa miche

Mbegu huoteshwa na kukuzwa kitaluni kwa muda wa wiki 6-8 na miche hupandikizwa shambani ikiwa na urefu wa sm.6-10. Mwagilia maji kitaluni kabla ya kuhamisha miche. Panda shambani kwa nafasi ya sm.75-90 kati ya miche kwa sm.90-105 kati ya mistari, wastani wa miche 12,500 itapatikana kwa hekta. Weka samadi shambani tani 25-37 kwa hekta wiki 1-2 kabla ya kupandikiza miche, au kilo 560-670 za NPK (mbolea ya viwandani) kwa hekta kwa uwiano wa 4:7:7 katika udongo usio na rutuba ya kutosha.

Utunzaji wa shamba

Tumia mbolea kiasi cha kilo 140 za SA au CAN kwa hekta hasa wakati mmea inapotoa matunda ili kupata matunda makubwa na kuvuna kwa muda mrefu (hadi miezi 10). Palizi ifanyike mara magugu yanapotokea shambani. Umwagiliaji maji ufanyike kama ilivyo kwa mazao mengine kama nyanya.

Wadudu Waharibifu

  • Funza wa vitumba
  • Vidukari
  • Kidomozi (Leaf miner)

Kudhibiti: Tumia dawa aina ya permethrin

Magonjwa

  • Kuoza mizizi
  • Mnyauko wa majani
  • Batobato

Kudhibiti: Choma nyasi kwenye kitalu kabla ya kusia mbegu.
Badilisha mazao yasiyo ya jamii ya pilipili.

Uvunaji

Matunda ya kwanza huwa tayari kuvunwa kuanzia miezi 2-3 baada ya kupandikizwa; matunda yaliyokomaa vizuri na kuwa na rangi nyekundu ndiyo huvunwa. Matunda 30-80 hupatikana kwa mmea mmoja.
Ubora wa hoho huongezeka kutegemeana na kiwango cha rangi yake ikiwa ni nyekundu njano au kijani. Mazao kiasi cha tani 3.5 kwa hekta hupatikana. Baada ya kuvuna mwagilia maji, piga dawa (kama ni muhimu) na weka mbolea kuongeza uzalishaji unaofuata.

Usindikaji

Hoho huuzwa ikiwa bado fresh tofauti na jamii nyingine za pilipili ambazo zinaweza kukaushwa na kusindikwa kasha kuuzwa baadae.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

KILIMO BORA CHA ZAO LA MBAAZI

Utangulizi

Mbaazi ni zao la chakula ambalo pia linaweza kulimwa kama zao la biashara kutokana na kuwa na soko zuri la Mbaazi.Mbaazi ina kiasi kikubwa cha protini.Mbaazi inaweza kutoa mavuno ya tani 3.5 hadi 4 kwa hekta

HALI YA HEWA INAYOFAA KWA KILIMO CHA MBAAZI

Mbaazi zinafaa kulimwa katika maeneo ya ukanda wa chini kutoka usawa wa bahari na pia hata sehemu za nyanda za juu nazo zinafaa kulimwa zao hili. Ni zao linalostahimili ukame na hili linalifanya kulimwa hata katika maeneo yanayopata mvua za wastani na yale yanayopata mvua kwa kiasi kidogo.

UDONGO UNAOFAA KWA KILIMO CHA MBAAZI

Mbaazi zinastawi katika udongo wowote ambao hautuamishi maji.Hivyo zao hili linaweza kulimwa katika maeneo yoyote na pia linaweza kulimwa katika udongo wenye asili ya mfinyanzi katika maeneo yanayopata mvua kwa kiasi kidogo.

AINA KUU ZA MIMEA YA MBAAZI

Kuna aina kuu tatu za mimea ya mbaazi
1)Mbaazi za muda mrefu: Hii ni mbaazi ambazo zinawezwa kuvunwa katika misimu zaidi ya miwili.Huchukua muda mrefu kukua hadi kuvunwa kwa mbaazi zake.Baada ya mbaazi kuvunwa Mbaazi hukatwa nusu yake na kuruhusu Machipukizi yake kukua na kuvunwa tena msimu unaofuata na zoezi hili hufanyika ziadi ya msimu mmoja.Huchukua Siku 180 hadi 270 kupandwa hadi kuvunwa

2>Mbaazi za Muda wa kati; Hizi hulimwa kwa msimu mmoja ila huchukua mda wa kati katika kukomaa kwake.huchukua siku 140 hadi 180

3)Mbaazi za muda Mfupi:Hizi hulimwa kwa msimu mmoja na baada ya kuvunwa mimea yake hukatwa na kung’olewa na kupandwa mbegu mpya msimu unaofuata.mbegu hizi huchukua siku 120 hadi 140.

MAANDALIZI YA SHAMBA

Andaa shamba lako mapema kadri utakavyoweza kulima kulinga na aina ya kilimo unachotumia, hakikisha umeondoa magugu shambani na uchafu mwingine ambao unaweza kuinyima mimea ya mibaazi kukua vizuri.

UPANDAJI

1> Mbaazi za Muda Mirefu; Panda kwa mistari kwa umbali/ nafasi ya sentimeta 150 kwa 100.
(Sentimeta 150 Mstari na mstari na sentimeta 100 Shina hadi shina katika mstari)
2>Mbaazi za Muda wa Kati; Mbaazi.Panda kwa mstari nafasi ya sentimeta 100 kwa 60

3>Mbaazi za Muda Mifupi;Panda kwa mstari kwa umbali/ nafasi ya sentimeta 90 kwa sentimeta 60

ANGALIZO: Maaneo ya Pwani ambayo yanarutuba kwa wingi na joto la kutosha mimea inakuwa kwa kasi na ili upate mavuno bora lazima uhakikishe mimea yako unaipa nafasi ya kutosha,Hivyo uwe makini na nafasi za mimea yako uanapopanda shambani.

MBOLEA ZA VIWANDANI NA SAMADI

Mara nyingi zao la mbaazi halihitaji matumizi ya mbolea na samadi.Ijapokuwa Hustawi zaidi katika shamba lenye rutuba ya kutosha.

PALIZI

Mimea ya mibaazi huitaji kupaliliwa mapema ili kufanya ikue katika hali ya afya bora na kusaidia kuongeza mavuno yako.

WADUDU WANAOSHAMBULIA MIBAAZI NA MBAAZI

Mbaazi ni mojawapo ya mazao ambayo hayashambuliwi sana na wadudu japokuwa wapo wadudu ambao kuna maeneo mengine hushambulia kwa kiasi kikubwa mbaazi nao ni funza wa tumba na wadudu wapekechaji wa mbaazi. Zuia wadudu hawa kwa dawa za wadudu kama ATTAKAN-C,Karate au dawa nyingine za wadudu.

MAGONJWA YA MBAAZI

Ugonjwa mkuu unaoshambulia mbaazi ni mnyauko wa fusaria ( fusarium wilt).Ambao husababisha shina la mbaazi kuwa na rangi nyeusi,ugoro au kahawia.ugonjwa huu huzuia mfumo wa usafirishaji wa mmea.Zuia ugonjwa huu kwa kuzungusha mazao shambani kila baada ya msimu kuisha.usipande kila msimu mbaazi tuu.Kila msimu badilishaz zaa.

UVUNAJI WA MBAAZI

Mbaazi zikishakomaa na kuanza kukauka zivunwe mapema kwa kukatwa matawi yenye mbaazi na kukaushwa zaidi kisha Mbaazi zitenganishwe kwa mikono au kwa kupigwa hayo matawi taratibu baada ya kukaushwa sana.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About