Mbinu za Kilimo na Ufugaji Kukuongezea Mapato

Ugonjwa wa tetanasi au pepopunda unaoathiri sana punda na binadamu

Huu ni ugonjwa hatari sana kwa maisha ya binadamu. Kinyesi cha punda kinabeba vimelea vijulikanavyo kama clostindium tetanii vinavyosababisha ugonjwa wa tetanasi.

Wadudu hawa wanaweza kuishi katika viumbe wote wenye damu moto maarufu kama mamalia na ndege, na wanapotoka ndani ya miili ya viumbe hao wadudu hao wanaweza kuishi kwenye udongo kwa miaka mingi. Bakteria hawa huingia mwilini kupitia kwenye vidonda vilivyo wazi. Kama mnyama au binadamu ana afya dhaifu basi huonesha dalili zote za tetanasi na kufa mara moja. Lakini endapo mnyama au binadamu ana afya nzuri basi hakuna tatizo kwani kinga ya mwili itapambana na vimelea hivyo.

Kumbuka kwamba tatizo hili halipo kwa punda peke yake, bali hata mbuzi, kondoo, mbwa na ndege wote wanaweza kuathirika. Lakini wanyama jamii ya punda na binadamu wanaathirika kwa haraka zaidi. Kinyesi cha punda mwenye vimelea vya tetanasi kikiingia kwenye mwili wa binadamu, vinaweza kusababisha tetanasi.

Na vile vili si kinyesi cha kila punda kimebeba vimelea vya tetanasi. Punda anaeishi katika mazingira machafu anaweza kuathirika, hasa wale wenye vidonda ambavyo havisafishwi. Ukiwa katika hali ya usafi na miguu yako iwe imefunikwa vizuri, huwezi kudhurika.

Jinsi ya kulima vizuri vitunguu twaumu (swaumu)

Vitunguu twaumu viungo vinavyopendwa na watu wengi hasa kwa harufu yake nzuri Kwenye chakula na uwezo wake wa kuondoa harufu mbaya Kwenye chakula (shombo). Vile vile vitunguu twaumu vinatumika kama tiba mbadala ya maradhi mbalimbali.

Jinsi ya kulima vitunguu twaumu

Aina nyingi za vitunguu twaumu vitakuwa kama vinatoa mbegu kwenye mmea ingawa kuna nadharia nyingi lakini inashauriwa kukata hizi mbegu chini kabisa kwa kisu kikali na kisafi, usikate mapema mara baada ya kutokeza bali subiri mpaka mmea unapoanza kama kujikunja ndipo ukate. Mbegu hizi kwa kawaida zikipandwa kwa msimu wa kwanza zitazaa kitunguu kimoja tu cha duara lakini chenyewe ukikipanda tena kwenye mzunguko wa pili kitazaa vitunguu vingi kama kawaida.

Mahitaji ya udongo

Vitunguu twaumu vinahimili aina nyingi za udongo, ila vinastawi zaidi katika udongo usiotuamisha maji kabisa na wenye mbolea asili, kama mbolea si ya kutosha kwenye udongo, tumia samadi iliyokwisha oza vizuri usitoe samadi bandani na kuipeleka shambani moja kwa moja kwenye shamba la vitunguu thwaumu, labda kama utaliacha shamba bila kulimwa kwa zaidi ya miezi 6, pia unaweza kutumia mbolea za viwandani kama ammonium nitrate, ammonium sulphate, urea n.k wakati wa kupanda na kila baada ya wiki 4 – 6 mara mbili zaidi

Kupanda

Kipindi kizuri kwa upandaji ni kipindi ambacho hakuna joto. Uotaji mzuri hutegemea pia namna vitunguu thwaumu vilivyo hifadhiwa kabla ya kupandwa, kama vilihifadhiwa sehemu zenye joto na hewa finyu uotaji wake utakuwa duni na dhaifu. Unachukua kitunguu twaumu na kutenganisha vitunguu kimoja kimoja (bulbs) na kuchagua vile vikubwa maana hivi ndivyo vitakavyo kupa mazao mengi na bora, nafasi kati ya kitunguu na kitunguu ni sentimeta 10 na kati ya mistari ni sentimeta 30. Baada ya kupanda pandishia udongo na uukandamize kuhakikisha kwamba kimekaa vizuri na hakiwezi kuathiriwa na mvua au maji wakati wa kumwagilia ili kisikae upande au kungolewa kabisa.

Palizi

Ungoleaji wa magugu na majani ni muhimu muda wote ili kuondoa kugombea rutuba, hewa na maji shambani, kwa wenye mashamba makubwa wanaweza kutumia dawa za kemikali kama ROUNDUP na nyinginezo ili kudhibiti magugu.

Umwagiliaji

Kwa kipindi chenye upungufu wa mvua au ni kipindi cha kiangazi ni vizuri ukamwagilia vitunguu twaumu ni asubuhi na sio jioni au mchana, hii inasaidia vitunguu twaumu kujijengea uwezo wa kupambana na magonjwa, baada ya mizi miwili unaweza kupunguza umwagiliajai huku ukiangalia kwa kuchimba kidogo kama vitunguu twaumu vimezaliana vya kutosha na kuanza kukomaa, ukiona vimekomaa acha kabisa kumwagilia ili visioze

Magonjwa

Magonjwa kama botrytis (kuoza shingo) blue mould na fusarium (kuoza kwa vitunguu) husababisha hasara kubwa kama hayatadhibitiwa kwa kutumia viuatilifu mara unapoona dalili, pia magonjwa kama white rot huchukua zaidi ya miaka 20 kuondoka kama yatavamia shamba lako, inashauriwa kufanya mabadiliko ya zao kila baada ya miaka mitano kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii moja kama vitunguu maji, unaweza kupanda maharage, mahindi, karoti na kabichi katika mzunguko huo. Pia magonjwa kama kutu ya majani husababisha na unyevu mwingi hasa kama mimea itakuwa kwenye udongo unaotuamisha maji au mimea kumwagiliwa jioni au usiku,

Kudhibiti magonjwa

Tumia viuatilifu vinavyotakiwa kwa ugonjwa husika na pia kumbuka kumwagilia asubuhi tu Ili kudhibiti ugonjwa huu wa kutu mimea ingolewe na ichomwe au utumie viuatilifu vya kuulia fangasi wa mimea.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Aina kuu ya mizinga bora ya nyuki kwa ajili ya kupata asali nyingi

Mizinga ya Kifuniko juu (Top bar)

Hii ni aina ya mizinga inayotumika sana na wengi. Gharama yake ni ndogo kiasi kulinganisha na mingine. Ni aina nzuri sana kwa mtu anaeanza ufugaji wa nyuki kwa kuwa ni wa gharama nafuu. Mfugaji wa nyuki anaweza kutengeneza mzinga Yya aina hii mwenyewe kama ana utaalamu wa useremala.

 

Mzinga wa Top bar

Faida ya Mizinga ya Kifuniko juu (Top bar)
• Ni rahisi kukagua asali iliyo tayari.
• Ni rahisi kuvuna asali kuliko kuvuna toka kwenye mzinga wa kienyeji.
• Ni rahisi kuwatunza nyuki wakati wa kiangazi na inapokuwa hakuna maua. Kwa mfano unaweza kuwapatia nyuki chakula ili kuongeza uzalishaji wa asali.
• Ni rahisi kurina asali ukilinganisha na mizinga ya magogo inayotundikwa juu ya mti, kwa kuwa haihitaji vifaa maalumu.
• Aina hii ya mizinga huwekwa kwa kuninginia jambo ambalo siyo rahisi kushambuliwa na wadudu/wanyama wanaokula asali kwa kuwa Inajaa haraka sana wakati ambao ni msimu wa asali kutengenezwa kwa wingi.

Hasara ya Mizinga ya Kifuniko juu (Top bar)
• Kichane kwenye mzinga wa boksi hakina kishikizo hivyo huvunjika kwa urahisi sana kama hakitashikwa kwa uangalifu.
• Masega huvunwa pamoja na asali, kwa hiyo nyuki wanalazimika kutengeneza tena masega mengine ambapo husababisha kupungua kwa uzalishaji wa asali.

Mzinga wa Langstroth

Mzinga wa Langstroth unaweza kukupatia asali zaidi kulinganishwa na mizinga mingine Hii ni aina nzuri na rahisa sana ya mzinga. Mizinga hii hufahamika kama mzinga wa fremu, kwa kuwa ina fremu ambazo vichane vya masega hujishikiza. Chumba kikubwa ambacho malkia hutagia mayai. Malkia anazuiliwa kuhama kwenda chumba kingine kwa kutumia waya. Kwenye chemba maalumu ya kutagia juu yake pana chemba ya kuhifadhia asali.

 
 

Mzinga wa Langstroth

Vichane vya masega vinatengezwa kwenye fremu na si kwenye nguzo kama ilivyo kwenye Top bar. Ili kuvuna asali, mfugaji akiwa na masega yaliyojaa asali, hutumia vifaa maalum kwa ajili ya urinaji na kuhifadhi asali bila kupata tabu.

Mzinga wa Langstroth ni gharama kiasi kulinganisha na mizinga mingine.Unaweza kuipata kutoka katika taasisi zinazojiusisha na uuzaji wa mizinga, taasisi na karakana binafsi, au wakala wa Serikali.

Mambo muhimu ya kuzingatia kwenye ufugaji wa nyuki wa asali

Mtaalamu wa nyuki

Unapohitaji unahitaji kufuga nyuki ni lazima uwe na uelewa wa mzunguko wa maisha ya nyuki. Unapoanza ni lazima uulize mtaalamu wa nyuki, wafugaji wenzako ambao wana uzoefu wa kutosha, au kujiunga katika kikundi cha ufugaji ili apate ufahamu zaidi juu ya ufugaji wa nyuki.

Sehemu salama kwa ajili ya mzinga

Unahitaji kutafuta mahali pazuri, salama, na penye sifa ya kufugia nyuki. Vifaa vyote vikishapatikana kinachofuata ni kuchagua mahali gani pa kuweka mzinga. Hakikisha sehemu hii ni mahali ambapo makundi ya nyuki hukusanyika mara kwa mara.

Uwekaji Bora wa Mizinga

Ukishatafuta ya sehemu ya kuweka mizinga, kinachofuata ni kuandaa mizinga kwa ajili ya kuweka panapotakiwa.

Mambo ya muhimu ya kuzingatia
• Kwanza Safisha mzinga kuondoa uchafu wote, utando wa buibui na aina nyingine za wadudu.
• Kisha Weka chambo kwenye mzinga (maranyingi nta hutumika kama chambo) kwa kuipaka katika kuta za mzinga kwa ndani.
• Halafu Mzinga unaweza kutundikwa kwenye mti, kwenye nguzo, kuweka kwenye jukwaa au kwenye miamba. Hii inategemea wewe mwenyewe anapendelea njia ipi.

Faida ya kupanda maharagwe katikati ya kabichi

Maharagwe yanapandwa kwenye kabichi yanafanya kazi zifuatazo;

Kudhibiti wadudu (mtego).

Maharage yanaweza kupandwa kati ya mistari ya kabichi yakiwa kama mitego kwani yanasaidia kulinda kabichi dhidi ya buibui wekundu.

Kuboresha udongo.

Maharagwe yanaongeza nitrojeni kwenye udongo

Chakula cha mifugo.

Maharagwe yanaweza kutumika kulishia mifugo kama ng’ombe mbuzi na kondoo.

Matandazo.

Maharage yanaweza yakatumika kama matandazo kwenye shamba kusaidia kulinda unyevu.

Kutengenezea mbolea.

Maharagwe yakioza yanaweza kuwa mbolea nzuri ya shamba lako

Jinsi ya kumlisha n’gombe anayekamuliwa atoe maziwa mengi

Ng’ombe wa maziwa wanahitaji virutubisho zaidi ili kuweza kuzalisha maziwa kwa wingi hasa katika kipindi cha miezi 3-4 ya mwanzo baada ya kuzaa, wakati ambao uzalishaji wa maziwa unakuwa juu.

Malisho ya ng’ombe wa maziwa ni lazima yawe na uwiano sahihi wa viungo. Mifugo inahitaji chakula kitakachowapa nguvu, protini, madini, na vitamin ili kujenga miili yao, kuzalisha maziwa, na kuzaliana.

Kulisha ng’ombe wa maziwa kwa kutumia aina yoyote ya malisho haitoshi kukuhakikishia ng’ombe anakuwa na afya nzuri na kutoa maziwa ya kutosha. Kama ilivyo kwa mifugo mingine kama kuku na hata binadamu, ng’ombe anahitaji
mlo bora yaani kamili.

Vyakula vinavyohitajika kwa ng’ombe wa maziwa

Malisho ya kijani (Majani)

Huu ni mlo mkuu kwa ng’ombe wa maziwa. Mlo ni muhimu na wenye virutubisho. Lakini malisho bora ya kijani ni yale yanayoweza kumpatia ng’ombe wa maziwa virutubisho muhimu vinavyohitajika.

Malisho ya kijani yanatakiwa yawe ya kijani kibichi na machanga, hii ina maana kuwa, majani ya malisho ni lazima yakatwe na kuhifadhiwa yakiwa bado machanga na kabla ya kuchanua. Hii ina maana kuwa mimea ambayo imepoteza rangi yake halisi ya kijani inaweza tu kuwasaidia mifugo kuishi lakini haina virutubisho muhimu vya kuwapa mifugo nguvu, madini, protini na haiwezi kusaidia katika uzalishaji wa maziwa.

Malisho yenye viwango vya chini vya virutubisho yanatakiwa yaongezewe kwa chakula cha ziada chenye virutubisho vya kutosha kitakachoziba pengo la virutubisho vilivyokosekana.

Vyakula vya kutia nguvu

Kwa kawaida aina zote za majani ni chanzo kizuri cha vyakula vya kutia nguvu kwa mifugo, kama tuu tu yatalishwa yakiwa bado machanga.

Mfano wa Majani yaliyo maarufu kwa malisho ni matete, ukoka, majani ya tembo, seteria na Guatemala. Majani ya mahindi au mtama ni chakula kizuri sana kwa kuwapa nguvu mifugo.

Vyakula vingine vinaweza kutokana na aina zote za nafaka, punje za ngano, au molasesi.

Vyakula hivi vya kutia nguvu vinatakiwa vilishwe kwa kiasi kidogo.

Vyakula vya Protini

Mimea michanga ina kiasi kikubwa cha protini kuliko mimea iliyokomaa. Mahindi machanga pamoja na majani ya viazi vitamu ni mahususi kwa protini.

Mikunde ina protini nyingi zaidi kuliko nyasi. Mfano, mabaki ya majani ya maharage, njegere, desmodium na lusina. Majani yanayotokana na mimea kama lusina, calliandra au sesbania ina kiwango kikubwa cha protini pia.

Aina nyingine ya vyakula vyenye protini ni mashudu ya pamba, mashudu yaalizeti na soya.

Ng’ombe wa maziwa wasilishwe kwa kutumia aina zote za jamii ya mikunde kwa zaidi ya asilimia 30 ya uwiano wa mchanganyiko wa malisho ili kuepuka matatizo ya kiafya.

Madini

Ng’ombe wa maziwa wanahitaji madini ya ziada. Madini Ni lazima yapatikane muda wote, mfano kama jiwe la chumvi au kama chumvi ya unga ya kuweka kwenye (chakula) pumba.

Wanyama wanaokuwa, wenye mimba, na ng’ombe anaenyonyesha wanahitaji kiasi kikubwa cha madini, mfano calcium na phosphorous kwa kuwa madini mengi yanatoka kwenye maziwa.

Madini yanaweza kupatikana katika Mimea ya jamii ya mikunde na mengineyo isipokuwa nyasi. Mimea hii inatoa kiasi kikubwa cha calcium na madini mengineyo.

Chakula cha ziada (mf. Pumba)

Ng’ombe wa maziwa anapewa cha kula cha ziada mfano pumba. Pumba inahitajika kwa ng’ombe lakini kwa kiasi kidogo. Pumba aina ya Dairy meal ina kiwango kikubwa sana cha madini. Lakini ina madhara kwa mifugo endapo wanyama watalishwa kwa kiwango kikubwa.

Malisho yanayotokana na majani au nyasi kavu ni lazima yabakie kuwa chakula kikuu kwa mifugo. Haishauriwi kulisha zaidi ya kilo 6 za pumba kwa siku kwa ng’ombe mwenye kilo 450.

Ni lazima wapewe kwa kiwango kidogo sana, ambacho si zaidi ya Kilo 2 kwa mara moja na kichanganywe na majani. Kuongeza kiwango cha pumba kabla na wakati wa kunyonyesha/kukamuliwa, kisizidi kiasi cha kilo 2 kwa wiki ili tumbo la mnyama lizoee.

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya maji ya kunyunyiza kwenye majani

Mbolea ya kunyunyiza ni nzuri kwani inasaidia kuupa mmea virutubisho moja kwa moja kupitia kwenye majani au shina ambapo ndipo chakula kinahitajika.

Faida za mbolea ya maji ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha mavuno, uwezo wa mimea kukabiliana na wadudu pamoja na magonjwa, kuvumilia ukame, na kuongeza ubora wa mazao.

Jinsi ya kuandaa mbolea ya maji kwa kutumia samadi

Mbolea ya maji hutengenezwa kwa kuchukua kiroba kilichojazwa samadi, aina mbalimbali ya mimea yenye virutubisho na inayoaminika kuwa dawa ya mimea. Kiroba hicho kinafungwa kwenye kijiti, na kutumbukiza kwa kuning’inia kwenye pipa lililojazwa maji.

Kiroba hicho ni lazima kichukue kati ya kilo 30-50 za samadi pamoja na aina nyingine za mimea kwa maji lita 200 (tazama mchoro). Unaweza kushika upande mmoja wa mti na kunyanyua na kushusha kila baada ya siku tano ili kuchanganya na kuharakisha kutolewa kwa virutubisho zaidi.

Kwa kawaida mchanganyiko huo unakuwa na harufu kali sana maana Nitrojeni nyingi inayopatikana hugeuka kuwa Amonia. Ni vizuri kufunika pipa ili kuzuia kuyeyuka kwa nitrojeni. Harufu ikishaisha, ujue mbolea yako ipo tayari kwa matumizi.

Ongeza maji na utingishe vizuri kabla ya kutumia. Nyunyizia mimea yako kila wiki mpaka utakapoona mabadiliko.

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya maji kwa kutumia mimea peke yake (Majani fresh)

Mbolea hii hutengezwa kwa kuchukua majani mabichi na kuyakatakata na kisha kuyachanganya na maji kidogo.

Baada ya kuchanganya na maji unaacha kwa siku tatu au nne ambapo utatikisa mchanganyiko wako kila siku.

Baadae utatikisa na kuchanganya na maji na kunyunyiza shambani.

Vilevile Unaweza kutumia mbolea ya majani ambayo itakuwa kama dawa ya kuulia wadudu, kwa kutumia aina ya mimea kama vile mivule, mibangi mwitu, majani ya minyanya, mwarobaini, mashona nguo, pamoja na vitunguu saumu. Aina hii ya mimea inasaidia sana katika kuzuia magonjwa, wadudu na kutoa virutubisho muhimu kwa mimea vinavyosaidia mkulima kupata mazao bora bila gharama ya ziada ya kununua virutubisho.

Vigezo vya kunyunyiza mbolea ya maji

Ili upate matokeo mazuri wakati wa kunyunyiza mbolea ya maji unatakiwa kufuata vigezo vifuatavyo:
• Inashauriwa kutumia mbolea iliyochanganywa vizuri ili kuepukana na kuunguza mimea.
• Acha maji utakayotumia kuchanganyia mbolea yako nje katika pipa lililowazi usiku kucha, hii inasaidia kutoa madini hatarishi, na kufanya mchanganyiko wenye faida kwa mimea.
• Unatakiwa kutingisha vizuri mbolea yako ya maji kabla ya kunyunyiza. Chembechembe ndogo ambazo hazikuyeyuka zinaweza kuziba mdomo wa bomba la kunyunyizia.
• Matokeo mazuri yanaweza kupatikana endapo mbolea imechanganywa vizuri na kunyunyiziwa wakati hakuna upepo.
• Unatakiwa kunyunyizia mbolea wakati wa asubuhi au jioni wakati hakuna joto na upepo ukiwa umepungua.

Angalizo
Kabla ya kunyunyiza dawa au mbolea uliyoitengeneza mwenyewe shambani nyunyiza kwenye eneo dogo au mimea michache kwanza ili uone kama inaunguza au haiunguzi. Kumbuka kuwa mchanganyiko mwingine ukiwa cream au ukikolea sana unaweza kuchoma. Kwa hiyo kuepuka hili nyunyiza mahali padogo kwanza.

Canibalism Kwa Kuku Au Tatizo La Kudonoana

“Cannibalism,”
Kudonoana kwa kuku ni tatizo linalo wa sumbua wengi, ni moja ya athari ya lishe duni. Ni kisema lishe duni na maanisha chakula wanacho kula kukosa vurutubisho muhimu vya madini au kuku kutokula chakula cha kutosha.

Hizi ni moja ya sababu zinazo pelekea kuku kudonoana.

1.Kuku kukaa wengi kwenye eneo dogo

2. Tabia yao

3.Ubaguzi wa rangi

Hii Mara nyingi hutokea kwa kuku weusi ukiwachanganya na kuku mweupe au rangi ingine tofauti, kuku weusi Mara nyingi huwa ni wakali sana Kwahiyo ukiona kuku bandani kwako kadonolewa chunguza kwa makini chanzo ninini! Kama ni ubaguzi wa rangi unaweza watenga hao weusi.

4. Kuku kutokupata chakula cha kutosha

5.Upungufu wa madini ( protini)

6. Kukosa kitu walicho kizoea au kuboreka

Kwa mfano kuku ukiwazoesha kuwa changanyia Damu kwenye chakula , siku utakapo punguza kipimo au kuacha kabisa kuwa changanyia damu ambayo umewazoesha kuwa changanyia lazima watadonoana.

Kuku ukiwa zoesha kuwa fungia mchicha hasa wale kuanzia mwezi mmoja hadi wa miezi 4 siku utakapo acha kuwafungia mchicha inaweza sababisha wakadonoana.

Kuku hupenda kuparuaparua na kuzunguka zunguka. Wakikosa nafasi na vitu vya kudonoa donoa huanza kudonoana wenyewe kwa wenyewe.

7. Mwanga mkali

8. Msongo

Banda lenye joto sana na lisilo pitisha hewa vizuri huwapatia msongo/stress kuku, na kuku huweza kuanza kudonoana.

9. Uhaba wa vyombo bandani👇

Hii hutokana na kuwa na kuku wengi halafu vyombo vichache vya chakula , Kwahiyo wakati wa kula lazima watagombania na kudonoana

Kuku wa umri tofauti kuwekwa kwenye banda moja

Tiba Kinga

Tiba

Tumia Protini (Amino Acid) stahiki kulingana na tatizo.

Mfano: (methionine , lysine nk)

Kinga

Changanya Proteni kiwango kizuri kwenye chakula cha kuku,chakula cha kuku kijumuishe virutubisho vyenye asili ya wanyama ambavyo ni chanzo kizuri cha Proteni

Hakikisha kuku wako wanakaa kwenye eneo la kutosha . hii inategemea aina ya kuku na umri wake.

KILIMO BORA CHA ZAO LA MBAAZI

Utangulizi

Mbaazi ni zao la chakula ambalo pia linaweza kulimwa kama zao la biashara kutokana na kuwa na soko zuri la Mbaazi.Mbaazi ina kiasi kikubwa cha protini.Mbaazi inaweza kutoa mavuno ya tani 3.5 hadi 4 kwa hekta

HALI YA HEWA INAYOFAA KWA KILIMO CHA MBAAZI

Mbaazi zinafaa kulimwa katika maeneo ya ukanda wa chini kutoka usawa wa bahari na pia hata sehemu za nyanda za juu nazo zinafaa kulimwa zao hili. Ni zao linalostahimili ukame na hili linalifanya kulimwa hata katika maeneo yanayopata mvua za wastani na yale yanayopata mvua kwa kiasi kidogo.

UDONGO UNAOFAA KWA KILIMO CHA MBAAZI

Mbaazi zinastawi katika udongo wowote ambao hautuamishi maji.Hivyo zao hili linaweza kulimwa katika maeneo yoyote na pia linaweza kulimwa katika udongo wenye asili ya mfinyanzi katika maeneo yanayopata mvua kwa kiasi kidogo.

AINA KUU ZA MIMEA YA MBAAZI

Kuna aina kuu tatu za mimea ya mbaazi
1)Mbaazi za muda mrefu: Hii ni mbaazi ambazo zinawezwa kuvunwa katika misimu zaidi ya miwili.Huchukua muda mrefu kukua hadi kuvunwa kwa mbaazi zake.Baada ya mbaazi kuvunwa Mbaazi hukatwa nusu yake na kuruhusu Machipukizi yake kukua na kuvunwa tena msimu unaofuata na zoezi hili hufanyika ziadi ya msimu mmoja.Huchukua Siku 180 hadi 270 kupandwa hadi kuvunwa

2>Mbaazi za Muda wa kati; Hizi hulimwa kwa msimu mmoja ila huchukua mda wa kati katika kukomaa kwake.huchukua siku 140 hadi 180

3)Mbaazi za muda Mfupi:Hizi hulimwa kwa msimu mmoja na baada ya kuvunwa mimea yake hukatwa na kung’olewa na kupandwa mbegu mpya msimu unaofuata.mbegu hizi huchukua siku 120 hadi 140.

MAANDALIZI YA SHAMBA

Andaa shamba lako mapema kadri utakavyoweza kulima kulinga na aina ya kilimo unachotumia, hakikisha umeondoa magugu shambani na uchafu mwingine ambao unaweza kuinyima mimea ya mibaazi kukua vizuri.

UPANDAJI

1> Mbaazi za Muda Mirefu; Panda kwa mistari kwa umbali/ nafasi ya sentimeta 150 kwa 100.
(Sentimeta 150 Mstari na mstari na sentimeta 100 Shina hadi shina katika mstari)
2>Mbaazi za Muda wa Kati; Mbaazi.Panda kwa mstari nafasi ya sentimeta 100 kwa 60

3>Mbaazi za Muda Mifupi;Panda kwa mstari kwa umbali/ nafasi ya sentimeta 90 kwa sentimeta 60

ANGALIZO: Maaneo ya Pwani ambayo yanarutuba kwa wingi na joto la kutosha mimea inakuwa kwa kasi na ili upate mavuno bora lazima uhakikishe mimea yako unaipa nafasi ya kutosha,Hivyo uwe makini na nafasi za mimea yako uanapopanda shambani.

MBOLEA ZA VIWANDANI NA SAMADI

Mara nyingi zao la mbaazi halihitaji matumizi ya mbolea na samadi.Ijapokuwa Hustawi zaidi katika shamba lenye rutuba ya kutosha.

PALIZI

Mimea ya mibaazi huitaji kupaliliwa mapema ili kufanya ikue katika hali ya afya bora na kusaidia kuongeza mavuno yako.

WADUDU WANAOSHAMBULIA MIBAAZI NA MBAAZI

Mbaazi ni mojawapo ya mazao ambayo hayashambuliwi sana na wadudu japokuwa wapo wadudu ambao kuna maeneo mengine hushambulia kwa kiasi kikubwa mbaazi nao ni funza wa tumba na wadudu wapekechaji wa mbaazi. Zuia wadudu hawa kwa dawa za wadudu kama ATTAKAN-C,Karate au dawa nyingine za wadudu.

MAGONJWA YA MBAAZI

Ugonjwa mkuu unaoshambulia mbaazi ni mnyauko wa fusaria ( fusarium wilt).Ambao husababisha shina la mbaazi kuwa na rangi nyeusi,ugoro au kahawia.ugonjwa huu huzuia mfumo wa usafirishaji wa mmea.Zuia ugonjwa huu kwa kuzungusha mazao shambani kila baada ya msimu kuisha.usipande kila msimu mbaazi tuu.Kila msimu badilishaz zaa.

UVUNAJI WA MBAAZI

Mbaazi zikishakomaa na kuanza kukauka zivunwe mapema kwa kukatwa matawi yenye mbaazi na kukaushwa zaidi kisha Mbaazi zitenganishwe kwa mikono au kwa kupigwa hayo matawi taratibu baada ya kukaushwa sana.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Namna ya kutunza kuku na kuwakinga na magonjwa

1. Zingatia chanjo muhimu kwa kuku ili kuzuia magonjwa kama utakavyoshauriwa na mtaalamu wa mifugo.
Chanjo huanza katika wiki ya kwanza (mfano chanjo ya kuzuia sotoka) na inaweza kurudiwa baadaye.

2. Epuka kuweka kuku wengi mahali pamoja.
Ni rahisi magonjwa kuenea kwa haraka kuku wanaporundikana.

3. Kumbuka kutenganisha vifaranga na kuku wakubwa (isipokuwa kutoka kwa mama) kwa sababu vifaranga ni rahisi na wepesi sana kushambuliwa na magonjwa.

4. Hakikisha unaweka mipaka na madaraja ya sehemu za kuku kuzunguka/kucheza.

Jinsi ya kulima vizuri zao la kabichi

Kichwa cha kabichi kinapofunga vizuri, hutumika kama chakula na huvunwa baada ya kufunga na kukomaa vizuri. Kwa kawaida kabichi hupandwa kwa msimu mmoja, lakini iwapo itakuzwa kwa ajili ya kutoa mbegu hukuzwa zaidi ya msimu mmoja. Endapo inalimwa sehemu yenye maji ya kutosha, inaweza kulimwa msimu wote wa mwaka. Soko lake ni la uhakika katika kipindi chote na ni muhimu kwa afya. Pia, linaweza kutumika kama malisho ya mifugo
Mizizi: Mizizi ya kabichi hutawanyika ardhini vizuri. Kwa kawaida, huenda chini kiasi cha sentimita ishirini (20 sm), na hujitawanya kwa kiasi cha sentimita sabini na tano (75sm).
Shina: Shina la mmea wa kabichi huwa na rangi ya kijani au zambarau. Hii hutegemeana na aina ya kabichi, na kwa kawaida ni fupi.

Aina za kabichi

Kuna aina nyingi za kabichi na zifuatazo ni miongoni mwa aina hizo:
1. Prize drumhead

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5
2. F1-High Breed

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 2-4
3. Duncan

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3
4. Early Jersey wakefield

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5
5. Sugar loaf

Aina hii hukomaa mapema sana, kiasi cha miezi 2.5
6. Glory of enkhuizen

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5

Jinsi ya kulima kabichi

Hali ya hewa

Kabichi hustawi vyema katika sehemu yenye hali ya baridi, hali ya joto jingi haifai kwa kabichi kwa kuwa huathiri uotaji na ukuaji wake. Joto jingi pia husababisha kulegea kwa vichwa vilivyofunga. Zao hili hustawi vema katika maeneo yenye mwinuko wa zaidi ya mita 100 toka usawa wa bahari.

Udongo

Zao hili linaweza kustawishwa kwenye udongo wa aina yoyote mradi tu udongo huo usiwe na chumvichumvi nyingi na usiotuhamisha maji. Udongo wa kichanga na ule usio na rutuba ya kutosha husababisha kabichi kukomaa upesi na kuzaa kabichi hafifu zenye vichwa vidogo.

Kitalu cha kabichi

Kitalu ni muhimu katika uzalishji wa zao hili. Ni vema kutengeneza matuta yenye upana wa mita moja, na urefu wowote kulingana na matakwa ya mkulima. Mbolea za samadi na zenye asili ya chokaa zichanganywe vizuri kwenye udongo. Kiasi cha gramu 500 za mbegu huhitajika kwa hekta moja. Katika upandaji kwenye kitalu ni vizuri kutengeneza mistari katika tuta, umbali toka mstari hadi mstari uwe sentimita ishirini (20). Udongo kiasi kidogo utumike katika kufunika mbegu.
Baada ya mbegu kuota ni vizuri kupunguza baadhi ya miche na uwe katika kipimo cha sentimita 2-3 toka mche hadi mche. Hii itasaidia kuwa na miche mifupi na yenye nguvu. Inafaa kunyeshea kitalu mara moja au mbili kwa siku na katika sehemu za joto ni vizuri kuweka kivuli katika matuta. Katika wiki ya tatu, hadi wiki ya nne, ni vyema kuondoa kivuli kidogo kidogo huku ukipunguza unyeshaji. Hali hii itasaidia miche isipate mshtuko wa uhamishaji shambani.

Kuhamisha na kupanda

Hamisha na kupandikiza miche shambani ikiwa na umri wa wiki nne, wakati huo miche ikiwa na majani manne ya mwanzoni na urefu wa kiasi cha sentimita kumi na mbili (12). Wakati wa upandaji, ni vizuri udongo ukashindiliwa kwenye kila mche. Inafaa upandaji ufanyike mara moja, na ni vizuri ukafanyika nyakati za jioni au asubuhi sana, na udongo uwe na unyevu wakati wote.

Nafasi kati ya mmea

Katika mstari hadi mstari inatakiwa iwe sentimita 60-75. Kutoka mmea hadi mmea ni sentimita 30-60. Pia sentimita 75-90 inaweza kutumika kati ya mstari na mstari.

Mbolea

Ni vizuri kuweka kiasi cha viganja 2-3 vya mbolea ya samadi iliyooza vizuri katika kila shimo.

Palizi

Wakati wa palizi ni vizuri mkulima akawa mwangalifu ili asiharibu mizizi. Wakati kabichi inapoanza kufunga hufunika ardhi, hivyo, husaidia kuzuia magugu yasiote, kwa wakati huu hakuna haja ya kupalilia.

Kuvuna:

Kabichi hukomaa katika kipindi cha siku 60-100 tangu kupandwa. Kwa ajili ya kuuza ni vizuri kuvuna wakati vichwa vinapofunga vizuri na huwa na uzito wa kutosha kabichi iangaliwe na kutunzwa baada ya kuvunwa ili isikwaruzwe na kuoza kabla ya kutumiwa. Kwa kawaida hekta moja hutoa mavuno kiasi cha tani 50-80.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Namna ya kukabiliana na Magonjwa ya kuku

Hakikisha unamuona mtaalamu wa mifugo mara uonapo dalili zozote za kuumwa kwa mifugo wako.

Tenga na wapatie tiba au kuwaua na kuteketeza kabisa kuku wagonjwa kuepuka kuenea kwa magonjwa.

Ondoa ndege waliokufa mara moja, uwafukie au kuchoma moto. Usile kuku aliekufa. Baadhi ya magonjwa ya ndege yanaweza kuambukizwa kwa binadamu.

Endapo kuna mlipuko wa ugonjwa katika eneo lako, usiruhusu watu kutembelea banda lako. Watu wanaweza kuleta maambukizi kwa miguu yao katika mabuti, nguo na mikono.

Pia magari yanaweza kuleta madhara kwa mabanda yako kupitia matairi na upakuaji wa mizigo.

Jinsi ya kutunza nyumba ya kuku ili kuzuia magonjwa

1. Nyumba ya kuku iwe safi na kavu muda wote kuzuia ueneaji na kuzaliana kwa vijidudu vya magonjwa

2. Nyumba ya kuku iwe na nafasi za kupitisha hewa ya kutosha ili kuepuka joto na unyevunyevu ambao unachangia uwepo wa magonjwa kwa kuku

3. Hakikisha unaondoa matandazo na takataka zote kwenye banda wakati wote hasa yenye unyevu.

4. Fagia banda na kuhakikisha ni safi wakati wote. Weka matandazo mapya mara kwa mara.
5. Weka sehemu za kutosha kuku kupumzikia.
6. Weka viota vya kutosha.
7. Weka maji sehemu ambayo ni rahisi kusafisha.
8. Hakikisha unaondoa wanyama kama panya na wadudu nyemelezi kwenye sehemu ya malisho ya kuku kwani wao hubeba vimelea vya magonjwa.

Namna ya kulisha kuku ili wasipatwe na magonjwa

Safisha vyombo vya kulishia na kunyweshea kila siku. Osha, sugua vizuri, kisha suuza kuondoa utando unaobeba bakteria.

Kuku wanahitaji wapewe chakula cha kutosha na chenye virutubisho vyote. Unaweza kuwaongezea majani, makombo, nafaka, mchanga laini, au maganda ya mayai.

Wapatie kuku maji safi muda wote. Wafugaji wengi wameripoti kuwa na matokeo mazuri baada ya kuchanganya dawa ya kuua vimelea kwenye maji ya kunywa.

Nunua chakula kwa wauzaji wazuri na wanaoaminika ili kuepuka minyoo na sumu hatarishi. Usiwape kuku chakula chochote kinachoonekana kuoza au kunuka uvundo.

Hifadhi chakula cha kuku katika sehemu kavu isiyo na joto na isiwe kwa zaidi ya miezi mitatu ili kuepuka kuharibiwa na fangasi.

Mambo makubwa yanayosababisha kulazimika kulima au kutifua udongo

Kutifua udongo ni jambo la muhimu sana ili kuufanya udongo kuwa bora.

Umuhimu wa kutifua udongo ni kama ifuatavyo
1. Hulainisha udongo ili kuruhusu mizizi ya mimea kupenya kwa urahisi.
2. Kutifua kunaboresha uwezekano wa kupenya kwa nitrogen na oxygen kutoka kwenye hewa.
3. Kunawawezesha viumbe hai waliopo kwenye udongo kufanya kazi zao ipasavyo.
4. Kunasaidia Kuandaa sehemu ya kuwekea mbegu.
5. Kutifua kunauongeza uwezekano wa maji kupenya kwenye udongo na kupunguza uyeyukaji wa maji.
6. Kuchanganya mabaki ya mimea na samadi kwenye udongo

Mambo 6 muhimu ya kuzingatia kupata udongo bora mzuri shambani

1. Usiuchoshe sana udongo

Udongo ni kiungo muhimu sana katika uzalishaji wa mazao. Ni mfumo wa uhai kwa mimea. Kwa hiyo, mkulima ni lazima alenge katika kutunza uhai wa udongo na kuepuka usumbufu kwa uhai wa udongo.
Sababu muhimu za kulima/kutifua udongo ni:
• Hulainisha udongo ili kuruhusu mizizi ya mimea kupenya kwa urahisi.
• Kutifua kunaboresha uwezekano wa kupenya kwa nitrogen na oxygen kutoka kwenye hewa.

• Kunawawezesha viumbe hai waliopo kwenye udongo kufanya kazi zao ipasavyo.
• Kunasaidia Kuandaa sehemu ya kuwekea mbegu.
• Kutifua kunauongeza uwezekano wa maji kupenya kwenye udongo na kupunguza uyeyukaji wa maji.
• Kuchanganya mabaki ya mimea na samadi kwenye udongo

2. Acha udongo upumue

Kama ilivyo kwa binadamu, viumbe hai wanahitajika kwa udongo wenye rutuba, pia mimea inahitajika kwa ajili ya binadamu kupata hewa safi ya oxygen. Kuchanganya matandazo,na mboji kwenye udongo ni muhimu sana ili kuboresha mzunguko wa hewa. Viumbe hai wadogo wadogo, wadudu, minyoo, na wanyama wengineo wanapenyeza hewa kwenye udongo.

3. Weka Matandazo kwenye udongo

Huu ni utaratibu wa kufunika udongo kwa kutumia mabaki ya mimea, kwa mfano, matawi madogo madogo ya miti, majani, mabaki ya mimea ya mazao, magugu na kadhalika. Hata hivyo inahitajika nguvu kazi kwa ajili ya kutawanya matandazo.

Matandazo yanazuia mmomonyoko wa ardhi unaotokana na maji na upepo, yanasaidia ardhi kunyonya maji ya mvua, kutunza unyevu unyevu kwenye udongo kwa kuzuia myeyuko wa maji ardhini.

Matandazo yanapo oza hutoa virutubisho vinavyoboresha na kuongeza rutuba kwenye udongo, mbali na hilo pia hubadilika kuwa udongo mweusi wenye rutuba zaidi. Kama kuna uhitaji wa kuharakisha kuoza kwa matandazo ili kuongeza rutuba kwenye ardhi kwa haraka, kinyesi cha ng’ombe kinaweza kuwekwa na kutandazwa juu ya matandazo, hii husaidia kuongeza virutubisho vya nitrogen.

Matandazo yana faida nyingi sana kwenye ardhi, lakini pia yanaweza kusababisha madhara. Mabaki ya mboga za majani yasitumike kama matandazo kwani yanaweza kusababisha wadudu na magonjwa kwa mimea. Viumbe hatari kama bangu (stem borers) wa shina wanaweza kuishi kwenye mabaki ya mimea.

Mabaki ya mimea iliyokuwa imeathiriwa na magonjwa ya virusi au fangasi yasitumike kama matandazo kuepuka uwezekano wa magonjwa hayo kuambukizwa kwa mazao yatakayopandwa msimu utakaofuata. Kilimo cha mzunguko ni njia bora kuepuka athari hiyo.

4. Panda mazao kwa mzunguko

Kupanda mazao kwa mzunguko ina maana ya kuwa na aina mbalimbali ya mazao katika eneo moja kwa msimu.

Kwa mfano, kama shamba lako umepanda mahindi na maharagwe kwa kipindi cha mwaka mmoja, mkulima anaweza kubadili mzunguko kwa kupanda aina nyingine ya mazao katika eneo hilo kwa mwaka unaofuata.

Mimea iliyo mizuri zaidi katika kilimo cha mzunguko ni pamoja na jamii ya kunde, au malisho kama sesbania ambayo husaidia kuongeza rutuba kwenye udongo.

5. Lisha udongo

Udongo unatakiwa ulishwe ili uwe na virutubisho. Hii ni kazi muhimu sana kwa kila mkulima. Mkulima anaweza Kuulisha udongo kwa kutumia samadi na mboji. Kumbuka udongo uliotumika sana bila virutubisho, umekufa, hauwezi kuzalisha.

6. Kuwa makini na maji

Maji ni mazuri shambani, lakini maji yakizidi ni hatari. Maji yakizidi shambani yanaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo. Mmomonyoko wa udongo ni tishio na baa hatarishi kwa rutuba kwenye udongo. Mmomonyoko unaondoa tabaka la juu la udongo, sehemu ambayo ndiyo yenye rutuba zaidi.

Kupanda mimea kwa matuta (kontua) hupunguza kasi ya maji. Baada ya miaka kadhaa, nyasi zinazopandwa zinazopandwa kwenye matuta ya kontua husaidia kuunganisha na kusawazisha sehemu iliyotengwa, kwa kuwa udongo unaomomonyolewa hukusanyika katika sehemu iliyozuiwa na kuunganishwa kwa matuta.

Kwenye mwinuko mkali, kuta au mashimo, ndiyo njia pekee inayoweza kuzuia mmomonyoko wa udongo. Changanya na mimea kama matete, inasaidia kuzuia mmomonyoko na pia kutoa malisho kwa mifugo.

Mbali na matandazo (tazama hatua ya 3) mimea inayotambaa ni mbinu nyingine nzuri zaidi inayoweza kuzuia mmomonyoko wa ardhi. Matone ya maji hufikia ardhi yakiwa na nguvu kidogo sana hivyo kuepuka kumomonyoa ardhi, kwa kuwa yanakuwa tayari hayana nguvu ya kutiririka kwa kasi. Pia mimea inayotambaa hutumika kama kivuli kwa udongo. Mmea wowote unaofunika udongo na kuongeza rutuba unaweza kutumika.

Mfano maharage na mimea mingine ya jamii ya kunde, ambayo ina virutubisho vya nitrogen kwa wingi. Mimea inayopendekezwa ni ile ya jamii ya kunde. Inastahimili ukame, inatoa virutubisho vya naitrojeni, inatoa chakula, na pia inaweza kutumika kama chakula cha mifugo kilicho na protini nyingi. Kwa kuongezea inaweza pia kukabiliana na wadudu waharibifu.

Jinsi ya kutumia mashonanguo kama dawa ya kuzuia wadudu kwenye mimea

Mashonanguo kwa kiingereza ni Blackjack au kwa kisayansi yanajulikana kama (Bidens
pilosa)
Mashona nguo yanazuia wadudukama vile Vidukari, Siafu, bungo, katapila, chenene (crickets), nyenyere, siafu na inzi weupe.

Jinsi ya Kutayarisha na kutumia mashonanguo

  1. Jaza kikombe kilichojaa mbegu ambazo zimekomaa na maji;
  2. Chemsha kwa dakika kumi au loweka kwenye maji kwa saa ishirini na nne, kisha upooze.
  3. Ongeza lita moja ya maji na kijiko kimoja kidogo cha sabuni;
  4. Kisha unyunyizie mimea.

Matumizi mengine

  1. Mbegu zinaweza kutawanyishwa karibu na vichaka kuvutia mchwa.
  2. Mmea waweza kupondwa au kufikichwa kisha maji yake yatumike kunyunyizia mimea.

Angalizo: Kiasi kingi cha dawa hii chaweza kudhuru baadhi ya maua ya mimea.

Jinsi ya kulima vitunguu (vitunguu maji) kwa mbinu za kilimo bora na kwa faida

Vitunguu ni zao la mbogamboga na hulimwa kwa ajili ya balbu zake ambazo hutumika kama kiungo cha chakula. Vitunguu vina matumizi mengi sana na vina madini joto, chuma, vitamin A, vitamin B, vitamin C na vitamin E.
Vitunguu hulimwa na hukubali zaidi nyanda za baridi. Nyanda zenye joto vitunguu hulimwa pia. Vitunguu vinaweza kulimwa mwaka mzima endapo maji yanapatikana.

Aina za vitunguu vinavyolimwa Tanzania

  • Red Creole
  • Bombay Red
  • Hybrid F1

Hali ya hewa

Joto linatakiwa sana kwa ajili ya ukuaji wa balbu ila joto likizidi vitunguu hukomaa mapema kabla balbu hazijafikia ukubwa unaostahili, hivyo mkulima anaweza kupata mazao kidogo.

Udongo

Vitunguu huweza kupandwa kwenye udongo wowote wenye rutuba, usiotuamisha maji na usionata sana. Hufanya vizuri kwenye udongo wenye asidi kidogo japo udongo wenye alkali kidogo sio mbaya sana. Kwenye udongo wenye mchanga mchanga umwagiliaji ni lazima. Udongo mzuri sana kwa ustawi wa vitunguu ni tifutifu-kichanga.

Mbolea

Epuka matumizi ya mbolea mbichi isioiva vizuri kwani husababisha vitunguu kuwa na shingo pana sana majani hukua sana badala ya balbu.

Umwagiliaji

Umwagiliaji ni muhimu sana hasa wakati wa kuanza kutengeneza balbu. Unyevu uliozidi ni hatari sana kipindi cha ukuaji.

Kitalu cha vitunguu

Ni muhimu kumwagilia maji ya kutosha siku kumi za mwanzo tangu kusia mbegu kitaluni. Vitunguu hukaa kitaluni kwa wiki 6-8 na miche ifikiapo upana wa penseli na urefu wa sm 15 ni tayari kwa kuhamishia shambani/bustanini.

Upandaji

Kabla ya kupanda udongo ni lazima utifuliwe vizuri na reki kuondoa mabaki ya mimea na mawe ama Vipande vikubwa vya udongo. Matuta yawe na upana wa mita moja. Vitunguu hupandwa kwa mstari mojakwamoja ama kutokea kitaluni. Pia huweza kupandwa kwa mstari pacha. Vitunguu hupandwa sm 10-15 kutoka mmea hadi mmea na sm 10-15 kutoka mstari hadi mstari, kama inavyoonekana kwenye mchoro hapa chini. Pia epuka kupanda vitunguu mahali palipopandwa mboga jamii ya vitunguu siku za nyuma. Mfano Vitunguu saumu na vitunguu majani.

Utunzaji wa shamba

Kutandazia shamba na majani yaliyooza vizuri ama mabua inashauriwa ili kuongeza ruba ya ardhi, zuia magonjwa yatokanayo na udongo na magugu. Kupanda vitunguu kwenye matuta yaliyoinuka ni muhimu sana kuzuiya utuamishaji wa maji na mlipuko wa magojwa ya miche. Kungoa magugu na uvunaji ufanywe kwa mkono.
Vitunguu hufanya vizuri kama shamba litawekewa mbolea ya samadi ama mboji ilioiva vizuri. Kiasi cha tani 25-40 kwa heka kinashauriwa. Hii ni sawa na kilo 7.5 -12 kwa tuta lenye urefu wa mita 3 na upana wa mita 1.

Uvunaji

Vitunguu huvunwa kuanzia siku 90-150 tangu kusia mbegu. Dalili za kukomaa ni kuanguka kwa majani. Vitunguu huvunwa kwa kuvuta kwa mkono na kuhifadhiwa siku kadhaa shambani vikiwa vimefunikwa na majani. Baada ya hapo majani hukatwa na balbu hupakiwa kwa ajili ya kuhifadhi kusubiria bei nzuri. Vitunguu huweza kuhifadhiwa hadi miezi 9 tangu vivunwe bila kuharibika. Vitunguu vihifadhiwe kwenye nyuzijoto chini ya 4.4 °C ama juu ya nyuzijoto 25°C ili visiharibike.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About