Ufugaji wa Kuku wa Kienyeji

Mambo Ya Kuzingatia Kuongeza Utagaji Wa Kuku

Inafahamika kuku kutaga mayai mengi hutokana na aina ya mbegu ya kuku, ila jua kwamba hata aina ya mbegu ya kuku yenye sifa ya kutaga mayai mengi kama haitapewa matunzo mazuri  basi sifa yake ya utagaji itapotea.

Kwa kawaida Tetea anatumia muda wa masaa 24 – 27 (siku moja) kutengeneza yai. Hakuna njia ya kupunguza muda huu (yaani atengeneze mayai miwili katika siku moja). Hiyo ndio asili yake. Njia Nzuri ya kumfanya kuku atage muda mrefu ni kumfanya awe na furaha na afya.

Njia za kuwafanya kuku wawe na furaha na afya:

1. Wape chakula bora chenye virutubisho vya kutosha. Usichakachue chakula chao hawatataga.

2. Viota vyao viwe safi. Safisha viota vyao mara kwa mara ili watage sehemu safi.

3. Wawe na sehemu ya wazi ya kuzunguka zunguka na kuparua parua.

4. Wawekee calcium ya kutosha kwenye chakula chao ili mayai wanayotaga yawe na gamba gumu.

5. Wachunguze mara kwa mara
kama wana dalili za kuumwa, na endapo dalili zipo watibu mara moja.

6. Wapatie maji safi kila siku. Pia safisha vyombo vyao kwa sabuni kila siku.

7. Hakikisha banda lao ni safi muda wote ili kusiwe na wadudu kama viroboto, chawa na papasi. Wadudu hawa huwasumbua kuku na kuwafanya wapunguze kutaga.

8. Hakikisha kuku hawapati msongo/stress, mfano kusiwe na wanyama wa kuwatisha wanaopita au kuingia bandani kwao.

9. Chagua aina ya kuku wanaotaga mayai mengi.

10. Umri wa kuku. Kuku wenye umri wa miezi 6 – 18 wanataga sana. Wakiwa na miezi 19 – 24 wananyonyoka manyoya (Annual Molt), hivyo hupunguza kutaga, na wakianza kutaga tena, wanataga mayai makubwa na machache kuliko mwanzo.

11. Wasihamishwe hamishwe banda. Kuku hutaga vizuri zaidi wakiwa kwenye mazingira waliyoyazoea.

12. Walishe mboga za majani za kutosha.
Kumbuka: Kuku wenye furaha na afya ndio watakaotaga sana kwenye maisha yao.
Note: Wakati mwingine inadhaniwa kwamba Jogoo anaweza kumsaidia Tetea kutaga mayai mengi. Jogoo hawezi kuongeza utagwaji wa mayai, lakini anahitajika kuyarutubisha mayai (kuyafanya yawe na mbegu). Kama kuku wako anataga mayai machache, kuongeza Jogoo hakutamfanya Tetea atage mayai mengi.