Mafundisho ya Msingi ya Kanisa Katoliki: Makala za Katoliki

Nafasi ya Bikira Maria Katika Kanisa Katoliki

Kanisa katoliki linamthamini Bikira Maria kama Mama wa Mungu, Mama wa Kristu, Mama wa Mkombozi pia Mama wa uhai kuna maneno kadhaa hutumika pia kufafanua zaidi hiyo heshima mfano HYPERDULIA zaidi yaโ€ฆ. Bikira Maria tunamheshimu zaidi ya watakatifu, PROTODULIA ikiwa na maana ya heshima kwa Bikira Maria zaidi ya Mt. Yoseph na pia LATRIA likiwa na maana ya heshima kwa Mungu peke yake kwani ndani yake kuna kunakuabudu pia!!!
๐ŸŒปBikira Maria anatuelekeza kwa mwanae kama alivyo waelekeza waliokuwa harusini kana lolote atakalo waambieni fanyeni Yoh.2:5
๐ŸŒปBikira Maria ni Mama wa uhai, mlei, muuguzi wa kwanza/ muhudumu wa kwanza alienda kwa haraka kuanzisha kliniki ndogo nyumbani mwa Zakaria amhudumie Elizabeti Mama wa Yohane Mbatizaji aliyekuwa mjamzito
๐ŸŒปTunasema Bikira Maria ni mzazi bora wa kuiga kwani alitetea uhai, Mama huyo hakutoa mimba japo misuko suko ilikuwa mingi Mfano maneno ya pembeni ya watu kwa vile mimba haikuwa ya Yoseph mumewe, hali mbaya ya uchumi na ukiangalia hivyo Familia takatifu ya Maria na Yosefu haikuwa na hali nzuri kifedha Lk. 2:22-24 Bikira Maria alivumilia hali hiyo kwani angetoa angemuua Mkombozi wetu, na sababu hizo ndizo hata dunia ya leo zina wafanya watu watoe mimba Ikiwa kutoa ni kuua na hatimaye tunapoteza
-Mama wa watoto wa kesho
-Baba wa watoto wa kesho
-Padre wa kesho
-Mtawa wa kesho
-Raisi wa kesho n.k
๐ŸŒปBikira Maria alikombolewa kwaajili ya mastahili ya mwanae tena kwa namna ya pekee sana, aliangaliwa naโ€ฆ..
-Baba kama Binti yake Mpenzi
-Mwana, mama mheshimiwa
-Roho Mtakatifu, hekalu lake
SWALI: Sisi nasi kama tunaamini heshima anayopaswa kupewa Bikira Maria ni sawa na kwamba pia sisi tunaelewa kwamba tumekombolewa kupitia yeye?
Nafasi ya Bikira Maria Katika Biblia ya kanisa katoliki
๐ŸŒปSisi kama wanakatoliki tunasema Bikira Maria ni Mama wa Mungu kweli kwa kzingatia mambo makuu mawili ambayo ni kama ifuatavyo:
1. Kwanza lazima Bikira Maria awe mama halisi wa Yesu
2. Pili ni kuwa Yesu aliyemzaa Ni Mungu.
1. BIKIRA MARIA NI MAMA HALISI WA YESU
๐ŸŒปSote tunapaswa kufahamu kama kweli BiKira Maria ni Mama halisi wa Yesu kupitia vifungu vifuatavyo na hii ndio nguzo pekee ya kujinasua katika makundi yasiyo amini kama Bikira Maria anastahili heshima twende pamoja sasa:
-Lk. 1:30-31 neno linasema
Malaika akamwambia ‘ usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu, tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume na jina lake utamwita Yesu kwahiyo ni dhahiri kwamba huyu ni mama halisi wa Yesu ambae sisi tunamuimba kila leo.
-Mt. 1:18 neno linasema:
kuzaliwa kwake Yesu Kristu kulikuwa hivi: Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu huu ni ushahidi tosha kuwa Bikira Maria ni Mama halisi wa Yesu kwani ndiye aliye pewa hadhi zaidi ya wanawake wote kuzaa kitakatifu Mwana wa Mungu.
-Rom 1:3 neno linasema hivi
yaani habari za mwanawe, aliye zaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili ikikumbuka wakati tunasali nasadiki kama sehemu ya kuikiri imani yetu kuna maneno huwa tunatamka kwamba akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria, akawa mwanadamu hivyo ni connection nzurii sana kwetu kuendelea kumheshimu Mama yetu Maria kwa kutuunganisha na Mungu kwa ubinadamu wetu!
-Nabii Isaya 7: 14 anatabili:
kwahiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara, tazama , Bikira atachukua mimba , atazaa mtoto mwanamume naye atamwita jina lake Imanueli(yaani Mungu pamoja nasi tazama maneno haya yalitabiliwa na Nabii huyu juu ya mama huyu Mtakatifu atakavyo tuletea ukombozi kwann tusimheshimu na kumtetea mpaka tunapotoshwa?
– Mate 1:14 neno linasema
hawa wote walikuwa wakidumu kwa Moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake na mariamu mama yake Yesu na ndugu zake wanawake wengine walihesabiwa pamoja lakini mama Maria anasemwa kwa upeke yake ktokana na uzito wake kupita wanawake wengine kwani ndiye mama wa Yesu Kristu ni heshima kubwa!!!
2. Yesu ni Mungu na Bikira Maria ni Mama wa Mungu
๐ŸŒปkatika sehemu ya jambo letu la pili ni kwamba je alichozaa Mama Maria ni Mungu? Kama ni muhimu kujua hilo hebu tuone uthibitisho wa hili kupitia baadhi ya vifungo bdani ya Biblia zetu ambazo pia wenzetu wanaopinga Habari ya mama yetu Maria waone twende pamoja:
-Yoh. 1:1-2 neno linasema
hapo mwanzo kulikuwako Neno naye Neno alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu Huyo Mwanzo alikuwako kwa Mungu kwa maneno hayo na ukiendelea kusoma ukitafakari utaona anaezungumziwa na Yesu Kristu ambaye ndie nuru halisi ya ulimwengu ni ndie uzima wetu kwa Mungu na huyu Yesu basi alizaliwa na Bikira Maria hivyo alichozaa Maria ni Mungu kweli.
-Rom 9:6 neno linasema:
ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya Mwili, ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu mwenye kuhimidiwa milele. Amina hayo ni maneno yanayo tambulisha koo ya kibinadamu kwamba ndiko pamoja ubinadamu wetu amezaliwa Mungu soma injili ya mtakatifu Mathayo sura ya kwanza aya ya kwanza na kuendelea habari za ukoo wa Yesu naamini hapa Tmcs tunapasikia sana!!!
– Fil 1:6-7 neno linasema:
nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu nakuendeleaโ€ฆโ€ฆโ€ฆ.. maneno hayo yanaonyesha kuwa Kristo ndie mambo yote katika kuupata uzima wa milele na huyu anae onekana ni mwisho wa yote amaezaliwa na Mwanamke Maria.
-Mitume nao walikiri kuwa Yesu ni Mungu mtu Yoh. 20:28
Tomaso akajibu, akamwambia Bwana wangu na Mungu wangu kutokana na matendo na kazi ya Yesu Kristu iliwafanya mitume waone kuwa ufalme wake sio wa dunia hii tu bali ni wa milele na kazi yake ni Takatifu na sio hapo tu kumbuka pia wale wanafunzi walio kuwa wanasema yatufaa sasa tujenge vibanda vitatu kimoja cha Musa na kingine cha Eliya mara sauti ikasikika ikisema huyu ni mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye na mara akageuka sura maneno hayo ilikuwa ni uthibitisho juu ya umungu wa Yesu Kristu ambaye huyu alizaliwa na Bikira Maria.
– Lk. 1:35 neno linasema
Malaika akajibu akamwambia “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako , na nguvu zake aliyejuu zitakufunika kama kivuli, kwasababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu mwana wa Mungu” haya maneno ni dhahiri yanatufundisha kwamba Bikira Maria alimzaa Mungu katika ubinadamu wake.
-Gal. 4:4 neno linasema:
huyu ni mwana wa Mungu, ni mwana wa mwanamke, huyo mwana wa Mungu, pia ni mwana wa Maria tuseme nn sasa tusiyumbishwe yumbishwe na maneno yasiyo na tija juu ya mama Maria kwani kupitia yeye tunakuwa salama katika Roho na Mwili
Maneno ya Busara
-Mt. Germanus alishwahi kusema *Maria mahali pa kuishi pa Mungu*
-Mt. Jerome alisema Maria Hekalu la mwili wa Bwna
-Martine Luther, hata baada ya kujiengua kutoka kanisa katoliki alikiri kuwa Bikira maria ni Mama wa Mungu akisema:
hakuna jambo kubwa zaidi ya hili kuwa Bikira Maria alipata kuwa Mama wa Mungu ambalo kwalo zinatoka zawadi(heri) kubwa na Nyingi ambazo amepewa inakuaje leo tusione umhimu wa heshima kwa mama huyu?
-Mt. Bernado alisema Maria alimpendeza Mungu kwa ubikira wake, na alichukua mimba kwa unyenyekevu wake
MWISHO: FUNDISHO MAISHANI
– Sote ambao tupo chini ya utawala wa Yesu Kristo tunawajibu wa kutetea uhai kwa nguvu zote tukipiga marufuku utoaji mimba kwa visingizio mbalimbali
– Eva alishindwa kumtii Mungu akaleta mauti lakini Bikira Maria alitii kubaki mwamnifu na kumtunza Kristu na hatimaye ameleta uhai na neema zote , akina dada na mama zetu igeni mfano wa Maria na Elizabeti katika malezi bora!!
-Sisi sote tuliowabatizwa tunapapaswa kuwa wanyenyekevu kama Maria na familia yao yote kwani unyenyekevu umejengwa juu ya upendo pia ni mama wa fadhila nyingi utii, uchaji, ibada, uvumilivu, kiasi, upole na amani.

Je, Bikira Maria ni Bikira Daima au alizaa watoto wengine?

Jibu fupi ni kwamba Bikira Maria hakuzaa watoto wengine na hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu
Hapo zamani hakuna mkristu au dehebu lolote lililokuwa linapinga kuwa Bikira Maria sio Bikira Daima hata Waprotestanti/walokole waliamini Bikira Maria ni Bikira Hata Baada ya Kumzaa Yesu. Kwenye Miaka ya 1400-1600 Watu wote wakwanza waliopinga Kanisa Katoliki walikubali kuwa Bikira Maria ni Bikira daima wakiwemo Martin Lutha aliyeanzisha kanisa la Lutheran, John Calvin aliyeanzisha Ulokole/Protestanti, Mchungaji Ulrich Zwingli, Heinrich Bullinger, and Thomas Cranmer. Kwa miaka zaidi ya 350 Waprotestant/walokole waliendelea kuamini kuwa Bikira Maria ni Bikira Daima.
Lakini baadae wakristo wengi walianza kupinga kuwa Bikira Maria ni Bikira Daima.

Tunaweza kuthibitisha kuwa Bikira Maria hakuzaa watoto wengine kwa kunukuu Biblia Kama ifuatavyo;

1. Bikira Maria Alikuwa Bikira Kabla ya kumzaa Yesu

Biblia inatuambia wazi kwamba Bikira Maria alikuwa Bikira Kabla ya kumzaa Yesu Kama tunavyosoma katika Luka 1:26-35
26 Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27 kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28 Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe.” 29 Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30 Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31 Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33 Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” 34 Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?” 35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. (Luka 1:26-35)

2. Biblia Haiwataji ndugu wa Yesu wakati Yosefu na Maria walipokimbilia Misri kumficha Yesu na wakati waliporudi

19 Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, 20 akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumwua mtoto huyo wamekwisha kufa.” 21 Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea katika nchi ya Israeli. 22 Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao mwanawe Herode alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda katika mkoa wa Galilaya, 23 akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: “Ataitwa Mnazare.” Matayo 2:19-23
Kama wangekuwepo wadogo zake Yesu Biblia ingetuambia kwamba walikuwa wapi wakati huo na walikuwa na Yesu au la.

3. Biblia haituambii kuwa Yesu alikua na wadogo zake alipokuwa na miaka 12

Wakati wa Maria, Yoseph na Yesu walipoenda Yerusalemu Yesu akiwa na miaka 12 Biblia haituambii kuwa Yesu alikuwa na wadogo zake na walikuwa wapi. Kumbuka walikuwa na Desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka kwa ajili ya Pasaka familia nzima kama familia. Je hao watoto wengine walikuwa wapi. Kwa nini walikuwa na Yesu Mwenyewe? Maana yake ni kwamba Yesu hakuwa na Wadogo zake.
41 Wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. 42 Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43 Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. 44 Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. 45 Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta. 46 Siku ya tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. 48 Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, “Mwanangu, kwa nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni.” 49 Yeye akawajibu, “Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” 50 Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia. 51 Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. 52 Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu. (Luka 2:41-52).
Kwa hiyo Biblia haionyeshi kuwa Yesu alikuwa na kaka na dada wakati akiwa na miaka 12. Kama wangekuwepo wangetajwa hapa kuwa walikuwa pamoja na Wazazi wao kama Yesu au walikuwa na Yesu wakati anapotea. Biblia haituambii chochote kwa hiyo wakati huo hapakuwa na wadogo zake Yesu.

4. Kukosekana kwa neneo “Binamu” kwenye lugha ya Yesu

Wakristu wa kwanza pamoja na Yesu aliongea Kiaramaiki au Kiebrania. Katika lugha zote hizo hakuna neno “Binamu” kwa hiyo mabinamu walijulikana kama dada na kaka wa mtu. Kwenye Agano jipya Neno kaka na Dada lilitumika pia kuwakilisha binamu.
Biblia inapotuambia kuwa Kaka na dada zake Yesu haimaanishi kaka wa kuzaliwa bali ndugu au Binamu
55 Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?” (Mathayo 13:55-56)
Kwa hiyo wanaotajwa hapa ni ndugu wa Yesu kwa maana maneno kama; ndugu, kaka au dada lilitumika badala ya Binamu yaani mtoto wa shangazi au mjomba. Hapa juu Yosefu ametajwa kama kaka yake Yesu lakini tunajua kuwa Yosefu ni Baba yake Yesu. Baba na mwana hawawezi kuwa na jina sawa.

5. Biblia haitumii neno Ndugu, kaka au dada ikimaanisha ndugu wa kuzaliwa mama mmoja na baba mmoja

Sio mara zote Biblia imetumia neno Ndugu kumaanisha ndugu (Dada na Kaka) wa kuzaliwa yaani kaka na dada kwa mfano
Kwa kuangalia lugha ya Kiswahili na Kiingereza 1 Wakorintho 15:6 tunaona tafsiri tofauti.
KISWAHILI 6 Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa.
ENGLISH 6 After that, he appeared to more than five hundred of the brothers and sisters at the same time, most of whom are still living, though some have fallen asleep.
Kwa hiyo hapa neno kaka dada na ndugu linaonekana wazi halikumaanisha ndugu au kaka wa damu.

6. Undugu wa Yakobo, Simoni, Yosefu na Yuda kwa Yesu Sio wa mtu na kaka zake

Wasemao kuwa Bikira maria alikuwa na wana zaidi ya Yesu wananukuu kifungu hiki;
55 Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?” (Mathayo 13:55-56)
Kumbuka kulikuwa na Yakobo wawili wakati wa Yesu, Vifungu vifuatavyo yunaweza kuona kuwa kulikuwa na yakobo wawili ambao walikuwa ndugu za Yesu lakini sio kaka wa kuzaliwa kwa mama.
35 Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.” (Marko 10:35)
55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. 56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. (Matayo 27:55-56)
Tunaweza kuona Undugu huu na Yesu kwa kusoma;
19 Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. (Wagalatia 1:19)
Lakini Yuda anasema;
1 Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, nawaandikia ninyi mlioitwa na Mungu na ambao mnaishi katika upendo wa Mungu Baba, na katika ulinzi wa Yesu Kristo. (Yuda 1:1)
Kwa hiyo Yakobo na Yohane walikuwa watoto wa Mama mwingine ambao baba yao ni Zebedayo. Na Yakobo na Yosefu walikuwa watoto wa Maria Mwingine. Kwa hiyo ni Yakobo wa wili wa Mama wengine Tofauti na Maria. Yuda alikuwa ni ndugu yake Yakobo. Yakobo vilevile alikuwa ndugu yake Yesu.
Kuthibitisha kuwa Hawa kina Mama ndio waliokuwa Mama zao kina Yakobo wote hao wawili na wengine tunaweza kusoma;
25 Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene. (Yohana 19:25)
Kwa hiyo kwenye (Yohana 19:25) tunaona Kuwa ni kwenye Msalaba wa Yesu alikuwepo Mama yake Yesu (Bikira Maria), Dada yake Bikira Maria, Mke wa Cleopa na Maria Magdalena. Na kwenye (Matayo 27:55-56) wamwtajwa ni Mama za kina nani kama inavyoonekana kwenye kifungu kifuatachi;.
55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. 56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. (Matayo 27:55-56).
Kwa hiyo hii ina maanisha kulikua na wanawake watatu wenye majina sawa ya Maria waliokuwa chini ya Msalaba. Yakobo na Yuda walikuwa watoto wa Maria Mke wa Cleofasi, na sio Mama wa Yesu, na hivyo sio kaka za Yesu.

7. Yesu alimwacha Mama yake kwa Yohane kwa kuwa hakuwa na Kaka na dada wakumwachia mamaye

26 Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.” 27 Halafu akamwambia yule mwanafunzi: “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.
Ndiyo maana Bikira Maria tangu siku ile alihamia kwa Yohani kwa kuwa hakuwa na watoto wengine.

JE, WAKATOLIKI WANABUDU SANAMU?

Mpenzi msomaji, kumekuwa na tuhuma nyingi dhidi ya wakatoliki kwamba wanaabudu sanamu. Je, tuhuma hizo zina ukweli gani? Hilo ndilo swali tunalotaka kujibu leo.
Amri ya kukataza ibada kwa sanamu imewekwa wazi katika Biblia Takatifu, Kutoka 20:4-5, โ€œUsijifanyie sanamu ya miungu wa uongo, au kinyago chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini chini ya dunia. Usiisujudie wala kuitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.โ€
Sheria hiyo inapatikana pia katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:8-9: โ€œUsijifanyie sanamu za miungu za kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Isivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.โ€
Ni kutokana na vifungu hivyo vya Maandiko Matakatifu, Waamini wa Kikatoliki wamekuwa wakituhumiwa, kushtakiwa na kushambuliwa na baadhi ya waamini wa madhehebu mengine kwamba wanapingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu, yanayokataza ibada kwa sanamu. Tuhuma hizo zinakuwa nzito zaidi, hasa zinapohusishwa na Ibada inayofanywa na Waamini Wakatoliki siku ya Ijumaa Kuu kila mwaka.

KUNA TOFAUTI KATI YA KUABUDU NA KUHESHIMU

Mpenzi msomaji, kuna tofauti kubwa kati ya kuabudu na kuheshimu. Kamusi ya Kiswahili ya Maana na Matumizi, ya mwaka 1993, iliyoandikwa na SALIM K. BAKHRESSA, na kuchapishwa na OXFORD UNIVERSITY PRESS, DAR ES SALAAM, inaeleza kuwa neno โ€œkuabuduโ€ maana yake ni โ€œkuomba au kufanya ibadaโ€; na neno โ€œkuheshimuโ€ maana yake ni โ€œkutukuza, kustahi au kuogopa.โ€
Katika maana yake ya ndani, anayeabudiwa na mwenye haki ya kuabudiwa ni Mungu peke yake. Hakuna mtu, kiumbe wala kitu chochote kinachopaswa kuabuduiwa na chenye haki ya kuabudiwa. Mtu, kiumbe au kitu hupewa heshima tu, tena ya kiwango maalum. Kwa mfano, Bikira Maria, kwa sababu ya nafasi yake katika kazi ya ukombozi, anapewa heshima ya juu kuliko watakatifu wengine. Watakatifu hao wengine hupewa heshima ya kadiri tu, chini ya heshima ile anayopewa Bikira Maria.

KWA NINI MUNGU PEKE YAKE ANASTAHILI KUABUDIWA?

Tumesema ni Mungu pekee yake, ndiye anayestahili kuabudiwa, kwa sababu ndiye MUUMBA wa vitu vyote, vinavyoonekana na visivyoonekana; ndiye anayevitawala na kuviongoza vitu vyote; ndiye mwenye uwezo juu yetu sisi wanadamu na viumbe vingine vyote; ndiye anayejua yote; ndiye aliye pote kwa ajili yetu; ndiye mwanzo na mwisho wa kila kitu; ndiye mkuu na Bwana wa wote.
Aidha, tunapomwabudu Mungu, tunakiri kwamba ndiye aliyetuumba na โ€œndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu na tuko!โ€ (Mdo.17:28). Kwa kufahamu hilo, Wakatoliki hawawezi kumwabudu mtu, kiumbe au kitu chochote, isipokuwa Mungu tu.

MAMBO MAKUU NA MUHIMU KATIKA IBADA YA SANAMU

Ili kufahamu vema kinachofanywa na Wakatoliki ni vema kufuatilia na kutafakari yale wanayoyafundisha na kuyasadiki wao wenyewe, badala ya kuwahukumu kadiri watu wengine wanavyofikiri na kusema. Ukweli ni kwamba hakuna Ibada yoyote ya sanamu katika Kanisa Katoliki. Hilo ni dhahiri kwa sababu ili ibada ya sanamu iwe kweli kuabudu sanamu lazima yawepo mambo makuu na muhimu mawili: Kwanza, NIA KAMILI YA KUABUDU SANAMU INAYOHUSIKA;
Pili, KUWEPO NA IBADA YA DHATI YA KUABUDU SANAMU. Ikitazamwa kwa makini, hayo mambo mawili yanakosekana katika Kanisa Katoliki linapokuja suala la picha na sanamu. Kwa hiyo, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala picha. Kama ni hivyo, wakatoliki wanafanya nini na hizo sanamu au picha? Wanaziheshimu tu! Tukumbuke kuwa anayemwabudu mtu, kiumbe au kitu, ni sharti akihesabu na kukisadiki kuwa ndicho kinachomwezesha kuishi, kujimudu na kuwa na uhai wake (Rej. Mdo.17:28).

JE, BINADAMU TUNAHITAJI SANAMU AU PICHA?

NDIYO. Binadamu tunahitaji sananmu au picha, tena ni jadi yetu! Kwa sababu gani tunahitaji picha maishani mwetu? Kwa sababu katika udhaifu wetu, mara nyingi tunaweza kufikiri vema kwa kutumia vielelezo au vichokoo vyenye kuonekana na kugusika. Kwa njia ya vielelezo hivyo, binadamu tunaweza kuyafikia kwa urahisi mambo magumu na mafumbo yaliyo juu ya fikra zetu za kawaida. Ndiyo maana tukiona picha au sanamu ya Yesu au Mama Maria au Watakatifu wengine, akili zetu zinaweza kutafakari mambo matakatifu na kupata picha ya kina cha msamaha wa dhambi na mapendo ya Mungu kwetu wanadamu.

KWA NINI WAKATOLIKI HAWAABUDU SANAMU AU PICHA?

Wakatolikihawaabudu sanamu kwa sababu wanajua kwamba Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa. Kwa hiyo, hawaziabudu sanamu au picha kwa sababu wanajua kwamba hivyo siyo Mungu. Zaidi hayo, wanajua kwamba Mungu mwenyewe amekataza kuziabudu sanamu na picha kwani hazina daraja la Muumba. Mungu amepiga marufuku kuzigeukia na kuzisujudia (Law.19:4). Aidha, wameaswa kuziepuka sanamu na Ibada kwa sanamu โ€“ โ€œWatoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu!โ€ (1Yoh.5:21). Pia wakatoliki wanajua kuwa sanamu na picha hazina uwezo wowote wa kimungu. โ€œMungu wetu yuko mbinguni, hufanya yote anayotaka. Miungu yao ni fedha na dhahabu; imetengenezwa na mikono ya wanadamu. Ina vinywa lakini haisemi. Ina macho lakini haioni. Ina masikio lakini haisikii. Ina pua lakini hainusi. โ€ฆ Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo, kadhalika na wote wanaoitumainia. Enyi wa nyumba ya Israeli mtumainieni Mwenyezi Mungu, yeye ndiye msaada wenu na ngao yenuโ€ (Zab.115:3-9). Pia kuziabudu sanamu ni jambo la kidunia, ambalo haliwezi kumpeleka mtu peponi (Rej. Isa.45:16; Isa.45:20; Gal.5:20). Kwa hiyo, Wakatoliki wanajua kuwa kuabudu sananmu na picha ni jambo haramu kabisa mbele ya Mungu, Mwumba wao (1Pet.4:3-4).

IBADA YA KWELI YA SANAMU INAKUWAJE?

Ibada ya kweli ya sanamu siyo rahisi hivyo, kama baadhi ya watu wanavyodhani! Ibada ya kweli ya sanamu siyo kitu cha mchezomchezo, kama baadhi ya watu wanavyofikiri na kusema. Ibada ya Sanamu ni suala la kuabudu, na kuabudu siyo suala la kuwa na kitu au kikiheshimu tu, bali ni kwenda mbali zaidi ya hapo! Hivyo kumiliki sanamu au picha, mathalani majumbani au kanisani, hakusemi lolote juu ya uwepo wa ibada ya sanamu kwa wale wanaohusika nazo. Kwa hiyo, ikiwa watu hawazipi sanamu au picha hizo mahali pa Mungu wa kweli, basi hawana hatia yoyote.
Jambo muhimu hapa ni kwamba wamiliki wa sanamu au picha hizo wanaziheshimu tu huku wakijua kuwa wenyewe wanaowakilishwa na sanamu au picha hizo hawapo pale kwa hali halisi. Katika maana hiyo, inakuwa sahihi kabisa kuziheshimu picha za marais, ndugu na marafiki wetu tunaowapenda, ambao hawapo karibu nasi. Picha zao hatuzikejeli wala hatuzibwagi chini na kuzikanyaga au kuzitia vumbi. Hatufanyi hivyo, siyo kwa sababu tunawaabudu watu hao au vitu hivyo, bali kwa sababu tunawapenda na kuwathamini wenyewe katika hali zao halisi.
Kwa mfano ikiwa tuna kitabu cha picha (Album) chumbani, chenye picha 100 za ndugu, rafiki na jamaa zetu, hatusemi tuna miungu 100 tunaowaabudu nyumbani mwetu! Vinginevyo, mambo yangetisha sana majumbani mwetu! Wenye picha hizo hatuwaabudu kamwe, ila tunawapa heshima tu kwa sababu tunawajali na kuwapenda. Kwa nini tusiwape heshima hiyo, ambayo ni kitu cha bure! Ukweli huo pia unahusu Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa, nk.

JE, MUNGU ANACHUKIA KILA SANAMU NA PICHA?

Mungu hachukii kila sanamu au picha. Hapa inafaa ieleweke vema kwamba Mungu alipopiga marufuku sanamu katika Kitabu cha Kut. 20:3-5 na Kumb. 5:7-10, hakupiga marufuku kila sanamu. Yeye mwenyewe anaonesha kwamba anazichukia sanamu zinazotengenezwa kusudi zichukue nafasi yake tu. Kama sanamu au picha hazihatarishi nafasi yake, hana maneno nazo! Ndiyo maana, basi, baada ya kumwagiza MUSA awaambie watu wasizitengeneze sanamu na kuziabudu kama miungu (Kut.20:4-5), alimwagiza MUSA huyo huyo azitengeneze sanamu zisizokuwa hatari, ambazo hazikupewa daraja la Mungu. Mungu alimwagiza MUSA kutengeneza sanamu katika nafasi mbili:
(i) Musa anaagizwa atengeneze sanamu mbili za Makerubi azibandike kwenye Sanduku la Agano wakifunike kiti chake cha rehema. โ€œUtatengeneza pia mfano wa viumbe hai viwili kwa kufua dhahabu, uwaweke kwenye miisho miwili ya kiti hicho; kiumbe kimoja mwisho mmoja na kiumbe mwingine mwisho mwingine. Waweke viumbe hao kwenye miisho ya hicho kiti, lakini wawe kitu kimoja na hicho kiti. Viumbe hao wataelekeana, mabawa yao yamekunjuka kukifunika kiti cha rehema, nyuso zao zitakielekea kiti hichoโ€ (Kut.25:18-20; Rejea pia Ebr.9:5).
(ii) Mungu alimwagiza pia Musa atengeneze Nyoka wa Shaba kama dawa kwa wale ambao walingโ€™atwa na nyoka wa moto kule Jangwani. Musa alielezwa wazi kwamba wale ambao wangemtazama huyo nyoka wa shaba kwa imani kwa Mungu wa Israeli wangepona. โ€œNdipo naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: Tengeneza Nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona. Basi, Musa akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu aliyeumwa na nyoka alipomtazama huyo nyoka wa shaba, aliponaโ€ (Hes. 21:8-9; Rejea pia Yoh.3:14-15).
Basi, Musa alitekeleza maagizo hayo ya Mwenyezi Mungu, naye alifurahia. Kwa maagizo hayo mawili ni dhahiri kwamba Mungu hachukii kila sanamu au picha. Mungu anachukizwa na sanamu zile ambazo zimekusudiwa kuchukua daraja la umungu wake, maana ni yeye tu ndiye anayestahili kuabudiwa. Yule nyoka wa shaba alikuwa dawa kwa wale walioumwa na nyoka wa moto. Watu hao hawakumwabudu nyoka wa shaba, lakini walipona, siyo kwa sababu ya nguvu zake, ila kwa nguvu za mwokozi zilizokuwa nyuma yake. โ€œKama mtu akiitazama alama hiyo aliponywa, lakini kilichomponya siyo hicho kitu alichokiona, bali wewe uliye Mwokozi wa watu woteโ€ (Hek.16:7).
Hapa ni vifungu vingine vya Maandiko Matakarifu, vinavyoonesha kuwa Mungu hachukii kila sanamu au picha.
1Fal. 7:29 โ€œkulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe vyenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali zilikuwa, zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuriโ€.
2Nyak.3:10 โ€œAlitengeneza sanamu mbili za viumbe wenye mabawa kwa mbao, akazifunika kwa dhahabu na kuziweka mahali patakatifu sanaโ€
Ezek.41:17-18 โ€œโ€ฆ kwenye ukumbi palikuwepo na michoro iliyofanana na mitende na picha za viumbe vyenye mabawa. Kila baada ya mtende kulichorwa picha ya kiumbe chenye mabawa kukizunguka chumba choteโ€.
Yoh. 3:14-15 โ€œKama vile Musa alivyomwinua yule nyoka wa shaba kule Jangwani, naye Mwana wa mtu atainuiliwa juu vivyo hivyo, ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele.โ€
Ebr.9:5 โ€œJuu ya hilo sanduku kulikuwa na viumbe wenye mabawa, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewaโ€

UBAYA WA SANAMU AU PICHA UKO WAPI?

Ubaya wa sanamu au picha upo katika kuzipa sanamu au picha daraja la Mungu. Hatari na ubaya wa sanamu au picha vimo katika kitendo cha binadamu kuzipa sanamu au picha hizo daraja la Mwenyezi Mungu. Kama sanamu au picha hazipewi daraja la Mungu, haziwi hatari na wala hazina ubaya wowote mbele ya Mungu. Kwa sababu hiyo, basi, mtu anaweza kuwa na sanamu au picha ndani ya nyumba yake au kanisani, lakini bila kumkasirisha Mungu.
Zaidi ya hayo, Mungu mwenyewe anajua fika kuwa sanamu au picha fulani imepewa daraja lake au siyo. Kwa nini Mungu akasirike pale ambapo sanamu au picha haziingilii daraja na ukuu wake? Mungu mjinga wa aina hiyo hayupo! Mungu wa kweli hawezi kukasirikia picha na sanamu ambazo zinaheshimiwa tu, na wala haziabudiwi. Aidha, Mungu mwenye haki hawezi kumwadhibu na kumtupa Jehanamu mtu ambaye anamiliki picha au sanamu duniani lakini bila kuziabudu, yaani pasipo kuzipa daraja la Mungu.

BIBLIA INAWEZA KUTUSAIDIA KUIELEWA IBADA YA SANAMU?

Jibu ni ndiyo! Biblia inatoa maelezo ya kina na ufafanuzi mzuri juu ya ibada ya sanamu. Tumesema hapo juu kuwa ibada ya sanamu siyo jambo la mzaha au mchezo wa kitoto! Ni suala la kuabudu, na kuabudu siyo tu jambo la kuwa na sanamu au picha na kuiheshimu tu. Ni zaidi ya hapo! Kuna mambo muhimu ambayo lazima sanamu zitendewe, ndipo ihesabike kuwa ni ibada ya sanamu.
a) Tukitaka kujua kama kitendo fulani mbele ya sanamu ni kuabudu au sivyo, kwanza lazima iwepo nia thabiti ya mtu anayehusika katika kitendo hicho kinachofanyika. Ibada inakuwa ya kuabudu sanamu ikiwa mtu anayefanya kitendo hicho anaamini moyoni mwake kwamba hiyo sanamu au picha inayofanyiwa kitendo hicho inachukua daraja na nafasi ya Mwenyezi Mungu. Katika kitendo hicho, mtu anaamini kuwa sanamu au picha hiyo ndiyo inayomwezesha kwenda, kuishi, kujimudu na kuwa na uhai wake hapa duniani.
b) Jambo la pili ni kuangalia kama kitendo hicho kinachofanyika katika ibada hiyo ni Liturujia ya kueleweka/maalum. Baada ya kubaini nia thabiti ya mtendaji, tunaweza kuitambua ibada ya sanamu kwa kuangalia yale yanayofanyika mbele ya sanamu au picha kwa kufuatilia mambo ambayo waabudu sanamu huyafanya. Mambo hayo, ambayo waabudu sanamu wanayafanya tunaweza kuyakusanya kutoka katika Biblia yetu. Agano la Kale linaonesha kuwa Ibada ya Kuabudu Sanamu inajumuisha mambo makuu yafuatayo:
i. Kuzitolea sadaka: za kuteketezwa: Rej. Hos.4:13; nafaka na vyakula 2Fal.5:17.
ii. Kuzitolea ubani kwa heshima kamili: Rej. 1Fal.11:8; Isa. 57:6; Yer.7:18.
iii. Kuzimwagia matambiko: Rejea Isa. 57:6
iv. Kuzitolea zaka ya sehemu ya kumi ya mapato ya mwaka ya mazao ya mashambani: Rejea Hosea 2:8
v. Kuziandika meza mbele yao: Rejea Isa. 65:11
vi. Kuzibusu sanamu kwa kuzisujudia kama viumbe vyenye enzi.
Rejea 1Fal. 19:18; Hos.13:2; Ayu. 31:2.
vii. Kuziinulia sanamu mikono katika kuzisujudia: Rejea Isa.44:20
viii. Kuziangukia sanamu kifudifudi ama kuzipigia magoti kwa kuziabudu: Rejea 1Fal.18:26,28.
ix. Kuzichezea ngoma na wakati mwingine kujikatakata kwa visu kama kitendo cha ibada kwa sanamu: Rejea 1Fal.18:26,28.
Hayo yote yakichunguzwa kwa makini, tutaona wazi kuwa hakuna Ibada ya kuabudu sanamu katika Kanisa Katoliki. Kwa hiyo, shutuma kwamba Wakatoliki wanaabudu sanamu siyo za kweli, hazina msingi, na ni uchochezi wa bure wenye lengo la kuleta mafarakano na magomvi. Jambo hilo ni dhahiri kwa sababu Wakatoliki hawana nia thabiti ya kuabudu sanamu wanapotoa heshima kwa sanamu au picha mbalimbali. Pili, matendo ya kiliturujia yanayofanywa na wakatoliki katika kuheshimu sanamu hayalingani na matendo ya kiliturujia yanayofanywa na waabudu sanamu, kama ilivyoelezwa katika Biblia Takatifu, hususan Agano la Kale. Kifupi, wakatoliki hawana nia thabiti moyoni ya kuziabudu sanamu au picha, tena hawazifanyii liturujia yoyote sanamu au picha walizo nazo majumbani au makanisani.
Ni wapi ambapo Kanisa Katoliki linafanya au kuwafundisha rasmi na kuwahimiza wafuasi wake wafanye matendo hayo tisa ya kiliturujia kwa ajili ya kuabudu sanamu? Hakuna! Kwa hiyo, Wakatoliki hawana hatia yoyote ya kuabudu sanamu mbele ya Mungu. Kama mtu mmoja akifanya hivyo, hilo ni shauri lake binafsi, siyo shauri au utaratibu wa Kanisa lote. Aidha, afanyaye hivyo amepotoka peke yake, kwa sababu hajafundishwa na Kanisa Katoliki afanye hivyo. Hilo ni kweli kwa sababu mambo binafsi, siyo mambo rasmi ya Kanisa lote!
Kwa hiyo, tunaona wazi kwamba Wakatoliki hawaabudu sanamu kamwe, kama inavyodaiwa na baadhi ya waamini wa madhehebu mengine ya kikristo. Wanaotoa shutuma hizo inafaa wajiangalie kwanza wao wenyewe, maana imeandikwa: โ€œโ€ฆ mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisiโ€ (Rom.14:14).

JE, IJUMAA KUU WAKATOLIKI WANAABUDU NINI?

Je, ni kweli kwamba Siku ya IJUMAA KUU Wakatoliki wanaabudu Sanamu au Mti wa Msalaba? HAPANA! WANAMWABUDU WOKOVU-YESU! Kiini cha utata hapa ni โ€œNINI MAANA YA IBADA YA KUABUDU MSALABAโ€ inayoendeshwa siku ya Ijumaa Kuu? Madhehebu hayo yanayofanywa na Wakatoliki Siku ya IJUMAA KUU siyo Ibada ya Kuabudu Sanamu. Labda hapa ni tatizo la lugha au maneno yanayotumika, ndiyo yanayowachanganya watu! Hilo ni kweli kwa sababu jina la madhehebu yenyewe halisemi wazi kitu gani hasa kinanuiwa kufanywa katika ibada hiyo.
Wengi hawajui nini hasa kinanuiwa kufanyika siku ya Ijumaa Kuu katika โ€œIbada ya Kuabudu Msalabaโ€ โ€“ jina ambalo nimesema halitoi picha halisi ya jambo linalokusudiwa kufanyika. Mtu mwenye akili timamu akijua kitu halisi kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu, hawezi kusema madhehebu hayo ni Ibada ya Sanamu au kuabudu mti. Tatizo hapo ni lugha tu inayotumika katika kuieleza ibada hiyo. Labda jina hilo lichunguzwe upya na wataalamu wetu katika Kanisa na ikiwezekana kulirekebisha ili kuondoa utata kwa baadhi ya watu wenye uelewa mdogo, wenye wanaokwazwa nalo!

NINI HASA KINAFANYIKA SIKU YA IJUMAA KUU?

Wanachofanya Wakatoliki Siku ya Ijumaa Kuu ni KUUHESHIMU MTI WA MSALABA na KUMWABUDU WOKOVU. WOKOVU ni nani? WOKOVU NI YESU KRSITO BWANA WETU. Basi, kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu ni kumwabudu WOKOVU yaani YESU KRISTO, ambaye alitundikwa msalabani. Hivyo ndivyo anavyotangaza Kiongozi wa Ibada hiyo ya Ijumaa Kuu, pale anapotoa mwaliko kwa waamini mara tatu, ili kila muumini ausikie na kuelewa vema: โ€œHUU NDIO MTI WA MSALABA, AMBAO WOKOVU WA DUNIA UMETUNDIKWA JUU YAKE, NJOONI TUUABUDU.โ€ Waamini wanaalikwa kiimani kuuabudu WOKOVU, na hilo ndilo linalofanyika, yaani kuuabudu WOKOVU โ€“ YESU KRISTO. Waamini wote wanaalikwa kujongea mbele kwa imani kwenda kumwabudu YESU. Watu wanamwabudu YESU kwa sababu WOKOVU maana yake ni YESU.
Jina YESU ambalo linatokana na Kiebrabia โ€œYESHUAโ€, maana yake โ€œWOKOVUโ€ (Rej. Mt.1:21;1:25; Lk.1:31). Ikiwa wokovu ni YESU, basi Ijumaa Kuu Wakatoliki hawaabudu sanamu au mti, bali wanamwabudu YESU KRISTO. Kwa sababu hiyo, yote yanayofanyika Siku ya Ijumaa Kuu, yanafanyika kihalali na kwa haki kwa sababu YESU KRISTO, ambaye ni WOKOVU ni MUNGU, na MUNGU peke yake ndiye mwenye haki na anayepaswa kuabudiwa. Ikiwa mkristo hataki kumwabudu YESU KRISTO, aliye Mwana wa Mungu na Mungu kamili, na ambaye ameeleta wokovu, anafanya makosa makubwa!
Basi, nasisitiza kuwa Siku ya Ijumaa Kuu, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala mti. Wanamwabudu WOKOVU, yaani YESU KRISTO, Nafsi ya Pili ya MUNGU. Kutomwabudu YESU KRISTO ni sawa na kumkana Mungu, kukana wokovu ulioletwa naye. Basi, tujiepushe na ukanaji Mungu wa aina hiyo. Nawaalika wote Siku ya Ijumaa Kuu tufungue mioyo yetu kwa imani kubwa ili tumwone WOKOVU aliyetundikwa msalabani, apate kuukomboa ulimwengu. Kwa imani, wote tumsujudie YESU ili apate kutukumbuka katika Ufalme wake wa milele.
Hatimaye, niseme kwamba ingawa Mungu ametoa amri ya kukataza sanamu na picha (Kut. 20:4-5; Kumb. 5:6-10), lakini hachukizwi na kila sanamu au picha. Sanamu na picha ambazo hazipewi daraja la Mungu, Yeye hazichukii, kwa sababu hazichukui nafasi yake kama Muumba. Basi, Wakatoliki hawaendi kinyume na Biblia kwa kuziheshimu sanamu na picha zilizoko kwenye majumba yao na makanisani.
Shopping Cart
๐Ÿ  Home ๐Ÿ“– Reading ๐Ÿ–ผ๏ธ Gallery ๐Ÿ’ฌ AI Chat ๐Ÿ“˜ About