Maana kamili ya Kwaresma
Ni kipindi cha kutafakari maana na umuhimu wa dhabihu ya YESU kristo katika ukombozi wa dunia na kumrudia Mungu. Aidha ni kipindi ambacho wakristo wanakumbushwa kufanya toba na kumrudia Mungu kwa mujibu wa maandiko matakatifu.
Ingawa kipindi cha kwaresma ni kipindi cha mafungo kwa wakristo, watu wengi na hasa wa dini nyingine hushindwa kutambua funga inayofanywa na wakristo katika kipindi hiki na hasa kwa sababu wakristo wengi huonekana wakiendelea kula na kunywa wakati wa kwaresma. Wakristo walio wengi pamoja na kufuata kielelezo cha Yesu kristo ambae alifunga siku arobaini (usiku na mchana) huzingatia maagizo ya YESU mwenyewe na nabii Isaya ambao kwa kiasi kikubwa hufafanua aina ya funga ambayo wakristo wanapaswa kuizingatia.
“Walakini wanitafuta kila siku, hupenda kujua njia zangu ; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao. Hutaka kwangu sheria za haki, humkaribia Mungu. Husema, mbona tumefunga lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu lakini huangalii? Fahamuni siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je, kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je, ni siku ya mtu kujitabisha nafsi yake? je ni kuinamisha kichwa kama unyasi na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? je utasema ni siku ya kufunga na ya kukubaliwa na BWANA? Je, saumu niliyoichagua sio ya namna hii? Kufunguo vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaachia huru walio onewa, na kwamba mvunje kila nira? Je, sio kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? umwonapo mtu aliye uchi umvike nguo, wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapo pambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia, utukufu wa BWANA (Mungu) utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita na BWANA ataitika, utalia nae atasema mimi hapa…” (Isaya 58: 2-9).
Kwa vile Mwenyezi Mungu wetu ni wa upendo na huruma, alimtuma nabii isaya kuwaambia watu hao kuachana na funga hiyo isiyo na maana na badala yake kuelekeza nguvu zao katika mambo muhimu ambayo Mungu anaangalia katika kutathimini utu wa mtu. Mambo hayo ni upendo, huruma na kujitoa kama ilivyoelezwa hapo juu na kuachana uovu wa aina zote.. Kwa msingi huo, mtu mwenye upendo na anaejitoa kusaidia wengine ana thamani kubwa mbele za Mungu kuliko mtu anaeshinda njaa siku 300 za mwaka pasipo kuonesha upendo wa kweli kwa wengine.
Yesu kristo alipokuja ulimwenguni, alisisitiza maneno ya nabii Isaya kwa kutaka watu waache tabia ya funga za kujionesha kwa watu, na badala yake wajitahidi kumpendeza Mugu.
Recent Comments