Mapishi – Fish Finger

Leo tunaangalia mapishi ya fish finger ( sijui kama unaweza kusema kidole cha samaki)!, Ni mlo mzuri hasa kuliwa kama kitafunio au mboga ya pembeni.

Mahitaji

500g Fileti ya samaki
120g Chenga za mkate
100g Unga wa ngano
Mayai 2
Ndimu 1
Kitunguu saumu 1
Kotmiri
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Menya vitunguu saumu kisha visage

Katakata fileti kwa muundo wa mraba (kama vidole) kisha paka mchanganyiko wa vitunguu saumu

Kata ndimu na kamulia kwenye fillet yako

Weka chenga za mkate kwenye bakuli kisha uchanganye chumvi kiasi na kata kata kotmiri majani 3 na uchanganye pamoja.

Kwenye bakuli lingine weka mayai na uyapigepige yawe kama uji mzito

Weka unga kwenye bakuli jingine.

Chukua kipande cha fillet kiweke unga kidogo kisha kizamishe kwenye yai na baada ya hapo kizamishe kwenye mchanganyiko wa chenga za mkate. Fanya hivyo kwa vipande vyote.

Weka mafuta kwenye kikaago na subiri yachemke kisha weka fillet zako vizuri na zikaange pande zote hadi zimekuwa rangi ya brown ( hakikisha moto sio mkali sana).

Epua na weka pembeni mafuta yote yakauke

Weka kwenye sahani tayari kwa kula.

Mapishi – Mayai Mchanganyiko, Tosti na Soseji

Karibu tena jikoni, leo tunaandaa vitafunwa kwa ajili ya kifungua kinywa asubuhi.

Mahitaji

Mayai 3
Soseji 2
Mkate slesi 2
Mafuta ya kupikia vijiko 2
Chumvi

Matayarisho

Piga piga mayai vizuri kwenye bakuli na weka chumvi kidogo kisha weka kikaango kwenye moto na mafuta kidogo.

Kikisha pata moto miminia mchanganyiko wa mayai na uanze kukorogo pale tu unapomiminia, endelea kukoroga hadi uone yanakuwa magumu na kuanza kuiva. Pika kwa kiwango unachopendelea na kusha epua na weka kwenye sahani.

Weka mafuta kijiko kimoja kwenye kikaango na kisha weka soseji zako na uzipike kiasi pande zote kisha epua na weka pembeni.

Weka slesi za mikate kwenye toster na zikiwa tayari unaweza weka siagi ili kuongeza ladha na mvuto.
Andaa mlo wako pamoja na juice, maziwa au chai.

Jinsi ya Kuvaa hereni kwa Mpangilio kuongeza Mvuto wako

HERENI ni pambo linavoliwa masikioni na kwa kiasi kikubwa linachangia kuongeza mvuto na muonekano mzuri. Kuna aina nyingi za hereni katika tamaduni mbalimbali. Zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia vito vya thamani kama vile Dhahabu, Almasi, Shaba au Kopa.

Vilevile zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia malighafi za asili kama vile ubao, vifuu vya nazi, mfupa kioo na shanga ambazo zimekuwa zikivaliwa sana na wanawake wa kimasai. Hereni zilizotengenezwa kwa shanga zimekuwa zikiwavutia watu wengi kuvaa kutokana na nakshi zake za asili.

Mara nyingi uvaaji wa hereni unatakiwa kuzingatia aina ya nguo uliyovaa, hapo unatakiwa kucheza na rangi. Mpangilio wako wa nguo na hereni hata na viatu utakufanya uonekane maridadi muda wote.

Unapotoka kwenda katika shughuli zako, au uwapo nyumbani basi zingatia uvaaji wa hereni na nguo. Uvaaji usiozingatia mpangilio wa rangi na hereni zako huondoa ladha ya urembo na si rahisi kwa mtu mwingine kugundua umependeza.

Licha ya kuwa hapo awali hareni zilikuwa zikivaliwa na wanawake pekee lakini miaka ya hivi karibuni tunaona urembo huu unaanza kuwavutia baadhi ya wanaume hususan vijana wa mjini.

Kutokana na hilo kuna hereni ambazo zimetengenezwa maalum kwa kuvaliwa na wanaume, hizi huwa za kubana na huwa na umbo dogo ukilinganisha zile zinazopendwa kuvaliwa na wanawake.

Angalizo: Epuka kuvaa hereni zaidi ya moja katika tundu la sikio kwani kufanya hivyo kunaweza kupelekea ukubwa wa tundu kuongezeka na hatimaye nyama ya sikio kuchanika. Hereni nzito sana nazo huchangia kutokea kwa tatizo hili.

Mapishi – Saladi ya Matunda

Matunda ni mojawapo wa kundi la vyakula, ni muhimu sana kwa afya bora. Matunda yakitengenezwa vizuri yanavutia sana na yanakuwa ni chakula kizuri sana.

Mahitaji

Embe iliyoiva kiasi
Nanasi
Tango
Tikiti maji
Zabibu
Papai

Matayarisho

1. Ondoa maganda kwenye embe, nanasi, tango, papai na tikiti maji kisha kata kata vipande vidogo vidogo vya mraba

2. Changanya vipande vya matunda kwenye bakuli safikisha weka na zabibu zilizotolewa kwenye kikonyo chake.

3. Weka kwenye friji yapate ubaridi kidogo

4. Saladi yako tayari kwa kuliwa

Waweza kula saladi hii kama mlo wa kati au kama mlo kamili wa usiku.

Njia bora za kumfanya mtu aache kuvuta sigara

Ni kazi ngumu kidogo kuacha uvutaji wa sigara. Uvutaji ni tishio kwa maisha yetu. Yawezekana hufahamu kwamba nusu ya watu wanaovuta sigara watakufa, ikiwa ni matokeo ya athari kilevi hicho. Sigara inasababisha robo ya vifo vyote vya kansa nchini Uingereza kila mwaka.

Kuacha uvutaji sio jambo rahisi sana. Hii ndiyo sababu kwa nini hadi sasa bado kuna watu milioni 10 wanaovuta sigara nchini Uingereza. Huku watu kati ya milioni tatu hadi nne wanajaribu kuacha wakati wowote bila ya mafanikio.

Njia tofauti zinazowezesha kuacha matumizi ya kilevi hicho ni zifuatazo, kama zinavyotambuliwa kwa majina yafuatayo:

1. Cold turkey

Ni njia ya kujikatalia kuvuta sigara.

Mvutaji anatakiwa aishi na kanuni ya ‘angalau mvuto mmoja.’ Kwa mujibu wa wataalamu hao, hamu ya kawaida ya sigara inadumu kwa mtu walau kwa takribani dakika tano.

Hivyo, mvutaji anatakiwa kuwa na orodha ya mikakati ndani ya dakika tano hizo kuvuruga hisia, iwapo hamu ya kuvuta itakapomjia.

2. Tembe za kumung’unya(Patches, gum, lozenges)

Kutumia tembe za kumung’unya kwa wiki nane yaweza kuongezea mara mbili nafasi ya kuacha sigara. Itapunguzia tamaa ya kuvuta sigara, bila ya kuharibu afya binafsi. Inafanya kazi kwa kuchukua nafasi ya nikotini ipatikanayo kutoka kwenye sigara au tumbaku.
Ni lazima kufwata masharti utakayopewa na dakitari kabla na wakati wa kutumia dawa hizi

3. Sigara ya kielektroniki (Vape)

Watu wengi wamegeukia uamuzi wa kuacha sigara, kwa kuvuta sigara za kielektroniki ambazo kimsingi zimeumbwa mfano wa sigara haliso na zinazopatikana katika aina zote za miundo na ladha. Hivyo, ni rahisi kupata picha, kwa nini Waingereza wapatao milioni 2.9 wanaitumia.

Aina hiyo ya sigara, huifanya mikono ya mvutaji iwe na shughuli ya kufanya kwa kuvuta aina hiyo ya sigara isiyo na majivu na gesi chafu ya ya aina ya carbon monoxide au vingine vinavyopatikana katika sigara halisi.

Hata hivyo, tafiti kadhaa zinaonyesha hewa hiyo inaweza kusababisha mabadiliko ya chembehai zinazoweza kusababisha kansa.

Hayo ni matokeo ya tafiti mpya, ambayo yanaelezwa hayana ushahidi unaojitosheleza , jambo linaloleta hoja nyingine kwamba ‘vape’ inatakiwa kuvutwa kwa tahadhari.

4. Ushawishi kitaalamu (Hypnotism)

Utafiti uliofanywa kwa watu 6,000 wanaovuta sigara, inaonyesha kuwa njia hiyo ina mafanikio makubwa, kwa kuwashawishi wavutaji watambue madhara na faida za kuacha sigara

“Inachukua siku chache tu kwa nikotini kuondoka mwilini mwako. Kwa hiyo, kile unachoachwa nacho ni tamaa ya kisaikolojia,” anasema mtaalamu Brian Jacobs, anayesema kinachoshughulikiwa hapo ni tamaa, wakati mtu yupo mapumzikoni.

Baada sigara ya mwisho

Baada ya saa nane, oksijeni hurudi katika hali ya kawaida mwilini na tindikali ya nikotini na hewa ya carbon monoxide hupungua kwa kiwango cha nusu ya kilichokuwapo.

Baada ya saa 48, mwilini mwa binadamu hakuna nikotini inayobaki mwilini na uwezo wa kuonja na harufu unaboreshwa. Hatari ya kuwa na mashambulizi ya moyo, nayo inaanza kupungua.

Hatua inayofuata baada ya kati ya wiki mbili na 12, mzunguko wa damu, hewa, maji na mahitaji mengine mwilini yanaboreka.

Ni hali inayoendelea hata kufika baada ya miezi mitatu hadi tisa, mapafu yanakuwa yameboreka kwa asilimia 10 na kukohoa kunakuwa kumepungua.

Inapofika mwaka mmoja umepita, hatari ya ugonjwa wa moyo kwa mvutaji inakuwa katika kiwango cha nusu ilivyokuwa awali na ikiendelea katika miaka 10 baadaye, hatari ya saratani ya mapafu huwa nusu kwa mvutaji, kulinganisha na alivyokuwa awali.

Ikiendelea baada ya miaka 15, moyo unakuwa salama dhidi ya hatari ya mashambulizi ya sawa na kuwa sawa na asiyetumia sigara.

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Jinsi ya kutibu chunusi kwa kutumia kitunguu swaumu

Kitunguu swaumu hujulikana kama kitu cha kushangaza katika tiba huko mashariki ya mbali, Kitunguu swaumu ni maajabu ya Mungu mwenyewe.

Kina nguvu za kuua bakteria mbalimbali na kuzuia magonjwa ikiwemo kutibu chunusi. Kuna namna 2 za kutumia kitunguu swaumu kutibu chunusi; namna ya kwanza ni kukitumia kitunguu swaumu kwenye vyakula vyako unavyopika kila siku, namna ya pili ni kukitwangwa kitunguu swaumu na kukipaka moja kwa moja katika sehemu yenye chunusi.

Ukiacha harufu yake isiopendwa na wengi, kitunguu swaumu kinaweza kukupa afya na urembo unaouhitaji.

Kitunguu swaumu husaidia kupunguza ukubwa wa chunusi. Hata hivyo uwe makini kwani kitunguu swaumu kinaweza kuunguza ngozi yako usipokuwa makini na ili kuepuka hili jaribu kuchanganya kidogo na maji baada ya kukitwanga ili kupunguza makali yake.

Toba, msamaha na Baraka

Inashangaza kwa sasa watu wengi hawapendi kuambiwa kuhusu kutubu dhambi zao bali wanataka waambiwe watabarikiwa. Kama vile wewe huwezi kumvika mwanao nguo nzuri kabla ya kumuogesha vivyo hivyo na Mungu hawezi kukubariki kabla ya kukutakasa. Unapotubu unasamehewa na kutakaswa dhambi zako kisha unakua umefungua milango ya baraka. Huwezi kubarikiwa bila kutubu kweli.

Jinsi ya kupika Visheti Vya Kastadi Vya Shepu Ya Kombe

Viamba upishi

Unga wa ngano 1 Kilo

Siagi ¼ kilo

Mayai 2

Kastadi (custard) 3 vijiko vya supu

Baking powder 1 kijiko cha chai

Maziwa 1 ½ gilasi

Mafuta Ya kukaangia kiasi katika karai

Maandalizi na upikaji

Weka unga katika bakuli kubwa kisha changanya na unga wa kastadi na baking powder.
Tia siagi uchanganye vizuri.
Tia mayai, kisha maziwa ya baridi uchanganye vizuri usiukande sana.
Fanya madonge kisha kata vipande vidogovidogo kisha ubonyeze kwa kidole uvikwaruze kwenye chujio lenye tundu itokee shepu (design) yake.

5- Tia mafuta katika karai yakipata moto, kaanga visheti hadi viive. Usiache hadi vikageuka rangi sana.

6- Eupua, weka katika sufuria au chombo kikubwa kusubiri shira.

Vipimo Vya Shira

Sukari ½ kilo

Hiliki ilosagwa 1 kijiko cha chai

‘arki (rose flavor) 5 matone

Maji 1 gilasi

Namna Ya Kutyarisha

Changanya sukari na maji uipike hadi iwe nzito.
Ukiona mapovu yanatoka tia hilik na ‘arki .
Mwagia katika visheti uchanganye vizuri hadi vishike na sukari.

Jinsi ya kutibu chunusi kwa kutumia limau au limao

Dawa nyingine nzuri kwa ajili ya chunusi usoni na mwilini ni limau. Limau linajitokeza kwenye vyakula vingi tunavyokula kila siku mathalani limau halikosekani pakiwepo supu au mapishi yoyote ya samaki.

Limau lina kiasi kingi cha vitamini C ambayo inaweza kutumika kama antibiotiki inayozuia kuongezeka na kukua kwa bakteria wanaosababisha chunusi.

Limau pia ina tindikali maalumu inayohamasisha chunusi kutoka katika ngozi.

Unachotakiwa kufanya ni kukata limau pande mbili au nne na upake majimaji yake moja kwa moja kwenye chunusi pole pole kwa dakika 10 hivi kasha jisafishe na maji safi.

Tindikali katika limau inaweza kuzidhuru seli zilizopo juu ya ngozi yako hivyo tumia dawa hii mara 1 au 2 tu kwa wiki na siyo kila siku.

Vitamini C iliyomo kwenye limau husaidia kukinga mwili dhidi ya magonjwa mengi sababu ndiyo vitamini inayosaidia kuongeza kinga ya mwili.

Kinga ni bora kuliko tiba!

Hivyo tumia vitamini C mara kwa mara au kunywa juisi ya limau kila siku ili kuweka mwili wako katika afya bora zaidi muda wote.

Jinsi ya kupika Slesi Za Chokoleti Na Karameli

Viamba upishi

Unga 1 Magi (vikombe vya chai)

Sukari ya browni ½ Magi

Siagi iliyoyayushwa 125 g

Nazi iliyokunwa ½ Magi

Mjazo wa karameli (Caramel filling)

Syrup 1/3 kikombe cha chai

Siagi iliyoyayushwa 125 g

Maziwa matamu ya mgando 2 vikopo (condensed milk)

Mjazo wa chokoleti (Chocolate filling)

Chokoleti 185 g (dark chocolate)

Mafuta 3 Vijiko vya chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya unga, sukari, siagi na nazi iliyokunwa kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.

2. Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30 cm au (8 in kwa 12 in) unaweza kuweka karatasi ya kuchomea chini ukipenda.

3. Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa dakika 15 mpaka 18 au mpaka ibadilike kuwa rangi ya browni.

4. Kwenye sufuria ndogo tia syrup siagi na maziwa matamu ya mgando na changanya kwa moto mdogo mpaka uwe mzito kasha mimina juu ya keki uliyochoma na choma tena kwa muda wa dakika 20 mpaka karameli iwe rangi ya dhahabu.

5. Kwenye sufuria ndogo nyingine tia vipande vya chokoleti na mafuta na ukoroge kwa moto mdogo mpaka iyayuke kisha wacha ipoe kidogo mimina juu ya mjazo wa karameli kisha weka kwenye friji mpaka ishikamane.

6. Kata vipande weka kwenye sahani tiyari kwa kuliwa

Jinsi ya kutibu chunusi kwa kutumia aloe vera

Mshubiri au Aloe Vera kama ilivyozoeleka na namna nzuri kwa wale wote wanaotaka kubaki na ngozi nyoro na ya kupendeza kila siku.

Chukua kipande cha mshubiri freshi na ukikate kasha chukua maji maji yake (jeli) na upake moja kwa moja kwenye uso wako na ujisuguwesuguwe kwa dakika 15 hadi 20 hivi pole pole kasha jisafishe na maji safi.

Tumia dawa hii mara 2 au 3 kwa wiki. Hii ndiyo njia rahisi ya kutibu chunusi bila kukuacha na madhara mengine mabaya.

Jinsi ya kupika Biskuti Ya Keki Kavu kwa kizungu Shortcake

Viamba upishi

Unga 2 Magi (vikombe vya chai)

Sukari iliyosagwa 2/3 Magi (kikombe cha chai)

Siagi   220 g

Unga wa mchele ½ Magi

Yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya vitu vyote hivyo kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.

2. Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30 cm au (8 in kwa 12 in)

3. Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa saa nzima au mpaka ibadilike kuwa rangi ya dhahabu.

4. Epua acha ipoe kisha kata vipande kama mstatili, weak kwenye sahani tayari kunywewa na chai.

Jinsi ya kupika Labania Za Maziwa

Viamba upishi

Maziwa ya unga 2 vikombe

Sukari 3 vikombe

Maji 3 vikombe

Unga wa ngano ½ kikombe

Mafuta ½ kikombe

Iliki kiasi

Jinsi ya kuandaa na kupika

Paka sinia mafuta kabla ya kupika labania
Katika sufuria chemsha maji na sukari pamoja na iliki mpaka inate vizuri
Kisha mimina mafuta koroga
Halafu mimina unga wa ngano na ukoroge haraka haraka
Kisha tia unga wa maziwa, endelea kukoroga usiwe na madonge mpaka uwe rangi ya browni isiokoleza.
Kisha mimina mchanganyiko kweye sinia uliyoipaka mafuta, iwache ipoe na kata kata upendavo na itakuwa tayari.

Maana ya kubarikiwa

Kubarikiwa ni Kutokutindikiwa na kuwa na matumaini ya siku zijazo. Kubarikiwa ni kuwa na amani, furaha, na matumaini katika maisha ya sasa na yajayo. Kubarikiwa sio kuwa na mali nyingi. Yesu hajawahi kumwambia mtu kuwa utakua tajiri sana kwa kuwa umebarikiwa wala hajawahi kumuahidi kumpa mtu utajiri. Unaweza ukawa na mali nyingi lakini zikakufanya ukakosa Amani, furaha na matumaini ya siku zijazo. Ndiyo maana Mungu anatupa kulingana na vile tunavyohitaji ili visiwe mtego kwetu.

Jinsi ya kutunza kucha kujiepusha na maradhi shambulizi ya Kucha

Mikono, viganja na vidole ni kati ya sehemu muhimu katika mwili wa msichana. Mikono hutumika kufanya shughuli nyingi za nyumbani, shuleni na sehemu mbalimbali katika maisha kuanzia kutandika kitanda, kupika, kufanya usafi, kuandika, kujiremba pamoja na majukumu mengine mengi.

Mikono isipotunzwa vizuri ni rahisi sana kuharibika, kupoteza mvuto wake wa asili na kuharibu afya ya kucha. Hitaji la urembo wakati mwingine humsukuma msichana katika matumizi ya vipodozi vya kupaka kwenye kucha zake ili kukamilisha urembo wake.

Urembo wa vidole na kucha sio lazima ufanyike katika saluni au kwa wataalamu wa kupamba kucha, msichana anaweza kushughulikia afya na urembo wa vidole na kucha zake kwa gharama nafuu na kwa muda ambao mwenyewe anaona unafaa kufanya hivyo hata akiwa nyumbani.

Hii pia itamsaidia Msichana kuchagua vipodozi salama kwa afya ya kucha zake na mwili kwa ujumla. Ni jambo la muhimu kufahamu kuwa baadhi ya vipodozi vinavyotumika katika urembo wa kucha, vina rangi na sumu zisizofaa kwa afya. Sumu kama vile ‘Formaldehyde na Toluene’ zinazopatikana katika baadhi ya rangi za kucha zina madhara kwa afya ya msichana.

Ni kweli kuwa kucha nzuri huongeza urembo, mvuto na furaha ya msichana lakini pia ni busara kukumbuka kuwa afya ni muhimu kuliko urembo na uzuri. Afya ya mwili na kucha za msichana kwa ujumla hutegemea chakula bora chenye protein, madini na vitamini na siyo rangi na vipodozi.

Upungufu wa vitamini A, B Complex, proteni, madini ya chuma na chokaa (kalishiamu) mwilini husababisha kucha zipoteze afya yake ya asili. Kucha ambazo hazina afya zinaweza kuoza, kukauka, kupinda, kupasuka au kuwa na umbo kama kijiko. Magonjwa ya kuvu (fungus), na baadhi ya dawa za kupunguza makali ya virusi pia huharibu afya ya kucha. Mojawapo ya athari za dawa za kupunguza makali ya VVU aina ya Zidovudine (ZDV) ni kucha kuwa na rangi nyeusi.

Kwa ajili ya afya bora ya kucha msichana anashauriwa kula mboga za majani, maharage, korosho, asali na matunda kwa wingi kila siku. Usafi wa kucha kila siku kwa kuziosha kwa maji ya uvuguvugu na sabuni laini pamoja na brashi ndogo ya mikono huimarisha afya ya kucha. Kucha pia zinaweza kusafishwa kwa maji ya mmea wa mshubiri (Aloevera), kitunguu saumu kilichopondwa pondwa au kitunguu maji kisha viganja na vidole vikaushwe vizuri na kupaka losheni.

Kucha za msichana zinatakiwa zisiwe ndefu ili kuepuka utunzaji wa vimelea vinavyosababisha magonjwa na kurahisisha utunzaji na usafi wa kucha. Kucha ndefu zinaweza kuwa chanzo cha hatari kwa afya ya msichana na familia yake hasa pale msichana anapohusika na uandaaji wa chakula cha familia. Katika familia nyingi, hasa familia za kiafrika wasichana ndio wanaobeba wajibu na majukumu ya kuandaa chakula cha familia.

Kwa afya nzuri ya kucha, msichana anashauriwa kukata kucha zake ili ziwe fupi kadri anavyotaka kwa kutumia ‘nail cutter’ au mkasi mdogo au wembe mpya ambao haujatumiwa na mtu mwingine. Kuchangia nyembe za kukatia kucha si salama kwani kunaweza kuwa njia mojawapo ya kusambaza vimelea vya magonjwa hatari ya kuambukiza kama vile virusi vinavyosababisha UKIMWI na ugonjwa wa homa ya ini.

Ni vizuri kulainisha ncha za kucha baada ya kuzikata kwa kutumia tupa ya kucha (nail file) na kuzisugua kuelekea upande mmoja ili kuepuka kucha zisivunjike au zisisababishe michubuko ya ngozi wakati wa kujikuna. Kusugua kucha kwa kwenda mbele na nyuma kunaweza kusababisha kucha zivunjike kwa urahisi na haraka.

Kwa afya njema ya kucha, msichana pia anashauriwa asifungue pini za barua au kukwangua vocha za simu kwa kutumia kucha. Kucha zisikatwe kwa kutumia meno na zisilowekwe kwenye maji kwa muda mrefu hasa pale maji hayo yanapokuwa na kemikali au sabuni.

Kwa ajili ya afya njema ya kucha za miguuni, ni muhimu kuhakikisha kuwa, viatu kabla ya kuvaliwa vinakuwa vikavu na safi kabisa. Viatu visipotumiwa pia vihifadhiwe sehemu kavu isiyo na vumbi, maji au unyevunyevu ili kuepusha visiwe makazi ya kuvu (fungus)

Shopping Cart
2
    2
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About