Baba Yetu uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe;
ufalme wako ufike,
utakalo lifanyike
duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku,
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.
Usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni.
Amina
Ufafanuzi wake uliotumiwa na Fransisko wa Asizi
BABA YETU mtakatifu kabisa: muumba, mkombozi, mfariji na mwokozi wetu.
ULIYE MBINGUNI: katika malaika na katika watakatifu, ukiwaangazia wawe na ufahamu, kwa sababu wewe Bwana ni mwanga; ukiwawasha wawe na upendo, kwa sababu wewe Bwana ni upendo; ukikaa ndani mwao na kuwajaza furaha, kwa sababu wewe Bwana ni wema mkuu kabisa, wema wa milele, ambaye kwako hutoka mema yote, na bila yako hakuna jema.
JINA LAKO LITUKUZWE: ujuzi wetu juu yako uwe wazi zaidi na zaidi, tuweze kujua upana wa baraka zako, urefu wa ahadi zako, kimo cha ukuu wako, kina cha hukumu zako.
UFALME WAKO UFIKE: utawale ndani yetu kwa njia ya neema yako na kutuwezesha kuingia katika ufalme wako ambapo unaonekana kama ulivyo, unapendwa kikamilifu, unatia heri ya kukaa nawe, unatia raha ya kukufurahia milele.
UTAKALO LIFANYIKE DUNIANI KAMA MBINGUNI: tuweze kukupenda kwa moyo wetu wote, kwa kukuwaza wewe daima; kwa roho yetu yote, kwa kukutamani wewe daima; kwa akili yetu yote, kwa kuelekeza nia zetu zote kwako na kwa kutafuta utukufu wako katika yote; kwa nguvu zetu zote pia, kwa kutumia uwezo na hisia zote za roho na mwili katika kuhudumia upendo wako na si chochote kingine; na tuweze kuwapenda majirani wetu kama tunavyojipenda, kwa kuwavuta wote kwa nguvu zetu zote kwenye upendo wako, tukifurahia mema ya wengine kama tunavyofurahia ya kwetu, na tukihuzunika pamoja na wengine kwa mabaya yanayowafikia, bila ya kumuudhi yeyote.
MKATE WETU WA KILA SIKU: Mwanao mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo.
UTUPE LEO: kwa ukumbusho, ufahamu na heshima ya upendo ule aliokuwanao kwetu sisi na ya mambo yale ambayo alisema na kutenda na kuteseka kwa ajili yetu.
UTUSAMEHE MAKOSA YETU: kwa huruma yako isiyosemeka, kwa nguvu ya mateso ya Mwanao mpendwa, pamoja na stahili na maombezi ya Bikira mbarikiwa daima na ya wateule wako wote.
KAMA TUNAVYOWASAMEHE NA SISI WALIOTUKOSEA: na lolote tusilosamehe kikamilifu, wewe Bwana utuwezeshe kulisamehe kabisa, tuwapende kweli maadui wetu kwa ajili yako, na tuwaombee kwa bidii mbele zako, bila ya kumlipa yeyote ovu kwa ovu, bali tukijitahidi kumsaidia kila mmoja katika wewe.
NA USITUTIE KATIKA VISHAWISHI: kilichofichika au cha wazi, cha ghafla au cha muda mrefu.
LAKINI UTUOPOE MAOVUNI: yaliyopita, ya sasa na yajayo.
ATUKUZWE BABA NA MWANA NA ROHO MTAKATIFU KAMA MWANZO, NA SASA NA MILELE. AMINA.
Read and Write Comments