Daraja na ndoa ni tofauti na sakramenti nyingine kwa sababu gani?
Daraja na ndoa ni tofauti na sakramenti nyingine kwa sababu hazilengi hasa faida ya mtu anayezipokea, bali huduma zake kwa ajili ya Kanisa na jamii. Daraja inatia uwezo wa Kristo kwa ustawi wa Kanisa, Bibi arusi wake. Ndoa inatia upendo wake mwaminifu kwa ustawi wa familia, kanisa dogo la nyumbani.
“Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe” (Mdo 20:28).
“Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa” (Ef 5:29-32).
Je, daraja takatifu zinahitajiwa kabisa na Kanisa?
Ndiyo, daraja takatifu zinahitajiwa kabisa na Kanisa kwa sababu kazi ya wokovu haimtegemei binadamu, bali Mungu.
“Hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni. Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu” (Eb 5:4-5),
Yesu alisisitiza alivyopewa na Baba uwezo wa kutuokoa. “Baba ampenda Mwana, naye amempa vyote mkononi mwake” (Yoh 3:35).
“Kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele” (Yoh 17:2)
.
Kisha kufufuka alitumia mamlaka hiyo kuwatuma wanafunzi kumi na mmoja waliobaki:
“Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi. Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari” (Math 28:18-20).
Mpaka mwisho wa dunia uwezo huo wa Kimungu utatolewa tu kwa sakramenti ya daraja, inayounganisha mtu na Mitume kupitia mlolongo usiokatika wa kuwekewa mikono ili kushirikishwa mamlaka. Bila yake, kuna upungufu katika ufundishaji, utoaji wa sakramenti na uongozi.
Je, wenye daraja wanastahili heshima?
Ndiyo, wenye daraja wanastahili heshima kwa sababu ya mamlaka ya Kiroho waliyonayo kutoka kwa Kristo.
“Amin, amin, nawaambieni: Yeye ampokeaye mtu yeyote nimpelekaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenipeleka” (Yoh 13:20).
“Jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu” (Gal 4:14).
“Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii” (Tito 3:1).
Wenye daraja wanaotimiza kazi zao vizuri wanastahili heshima kwa uaminifu wao pia.
“Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu, hasa hao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha” (1Tim 5:17).
Je, wenye daraja wanaweza wakatenda dhambi?
Ndiyo, wenye daraja wanaweza wakatenda dhambi kwa sababu ni binadamu kama sisi sote. Yesu alionja ukosefu wa Mitume hasa wakati wa mateso.
“Je, mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani?” (Yoh 6:70).
“Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao, na kuniacha mimi peke yangu” (Yoh 16:32).
Paulo alionya mapadri, “Katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao” (Mdo 20:30).
Ili tuwe na wachungaji wengi waaminifu tunapaswa kufanya nini?
Ili tuwe na wachungaji wengi waaminifu tunapaswa hasa kusali.
“Mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake” (Math 9:38).
Halafu yanahitajika maandalizi ya muda mrefu, juhudi na ushirikiano wa kidugu.
“Asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi… Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia… Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine” (1Tim 3:6; 4:16; 5:22).
Je, wanawake wanaweza kupewa daraja?, Mwanamke anaweza kuwa padri?
Hapana, wanawake hawawezi kupewa daraja, kwa sababu kwa karibu miaka elfu mbili mfululizo Kanisa limejiona halina mamlaka ya kufanya tofauti na Yesu. Yeye alichagua wanaume tu kuwa Mitume wake, ingawa walikuwepo wanawake waaminifu kuliko wengi wao, hasa Maria, mtakatifu kuliko wote.
“Petro, na Yohane, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake… Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya… kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja” (Mdo 1:13-14,23,26).
“Walimchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao” (Mdo 6:5-6).
Je, kutoa daraja kwa wanaume tu ni kuwakosea haki wanawake?
Hapana, kutoa daraja kwa wanaume tu si kuwakosea haki wanawake, kwa kuwa hizo ni huduma zinazofaidisha wote.
“Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye” (Lk 22:27).
Mwenye daraja anahudumia Kanisa kwa kumwakilisha Yesu; hivyo anatakiwa kuwa mwanamume kama yeye mbele ya Bibiarusi wake. Kukubali mgawanyo wa majukumu maishani ni kusifu hekima ya Mungu aliyetuumba watu wa jinsia mbili tofauti ili kustawisha familia, jamii na Kanisa.
“Walakini si mwanamke pasipo mwanamume, wala mwanamume pasipo mwanamke, katika Bwana… Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake” (1Kor 11:11; 12:27).
Je, mwenye daraja anaweza kuwa na ndoa?
Ndiyo, mwenye daraja anaweza kuwa na ndoa.
“Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu, kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa?” (1Kor 9:5).
Paulo, akiwa mseja, hakudai kila mmojawao aoe, ila asiwe ameoa mara mbili, bali “mume wa mke mmoja” (1Tim 3:2; Tit 1:6), kama alivyoagiza mjane aandikishwe akiwa tu “mke wa mume mmoja” (1Tim 5:9).
Polepole mang’amuzi yakaelekeza Kanisa kubana nafasi hiyo kwa Maaskofu, na katika majimbo mengi kwa mapadri pia. Useja mtakatifu unawalinganisha zaidi na Yesu na kuwaachia uhuru wa moyo na wa muda kwa ajili ya huduma.
“Wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee” (Math 19:12).
Ni zipi Sakramenti za Huduma ya ushirika na utume?
Ni Sakramenti mbili ambazo ni Sakramenti ya Daraja na Sakramenti ya Ndoa
Sakramenti ya Daraja ndiyo nini?
Sakramenti ya Daraja ndiyo Sakramenti ambayo mwanamme mkatoliki aliyeitwa na Mungu hupata mamlaka na neema ya kuendeleza ndani ya Kanisa Utume Kristo aliowakabidhi Mitume wake
Ni kwa nini inaitwa Sakramenti ya Daraja?
Inaitwa Sakramenti ya Daraja kwa sababu mtu anapata Sakramenti hii kwa kuweka wakfu kwa ibada ya pekee inayomwezesha kwa nguvu ya Roho Mtakatifu atumie uwezo Mtakatifu kwa niaba na mamlaka ya Yesu Kristo ili kuhudumia Taifa la Mungu
Sakramenti ya Daraja ina ngazi ngapi?
Sakramenti ya Daraja inazo ngazi tatu, nazo ni Ushemasi, Upadre, Uaskofu
Ibada ya kutolea Daraja ya uaskofu ina matokeo gani?
Ibada ya kutolea Daraja ya uaskofu ina matokeo yafuatayo;
1. Inampa utimilifu wa SSakramenti ya Daraja Takatifu
2. Askofu anakuwa Mwandamizi rasmi wa Mitume
3. Inampa Askofu ushirika na Papa na maaskofu wengine wa kuwajibikia Makanisa yote
4. Inampa uwezo wa kufundisha, kutakasa na kuongoza
Askofu ni nani?
Askofu ndiye mchungaji mkuu wa kanisa Mahalia au Jimbo lake
Askofu ana kazi gani katika Jimbo lake?
Askofu katika Jimbo lake anamwakilisha Kristo akitimiza kazi ya kichungaji akisaidiwa na mapadri na mashemasi wake.
Askofu ni kiongozi wa kiroho katika jimbo mahalia. Na sio mambo ya kiroho tu ila hata ya kijamii lakini watu/mtu akiitaji ufafanuzi na msaada toka kwake.
Kazi zake ni:-
1. Kuliongoza taifa la Mungu alilopewa yaani wakristo/wengineo pia
2. Kusimamia na kuongoza Litrujia katika eneo husika.
3. Kueneza amani kwa kupitia karama na wadhifa aliopewa na Mungu.
4. Kueneza upendo katika eneo/jimbo mahalia.
5. Mtoa kauli ya mwisho kwa mambo ya kikanisa katika jimbo.
6. Kusimamia miito ya kanisa na kuchochea bila kukata tamaa
7. Kusimamia baraza la walei na kulishauri kwa kutolea kauli ya Mwisho kabla ya kwenda kwingine
8. Kuwashauri watu waliokata tamaa au kushindikana katika ngazi za chini
NB. Hivyo ndani ya kanisa kuna miogozo ili kupata nafasi zisizokinzana
Ni nani ampaye padri Daraja la Uaskofu?
Ni Baba Mtakatifu pekee au humteua Askofu mmoja akisaidiwa na maaskofu wengine wawili humweka wakfu Padri huyo kuwa Askofu (Mt 13:2-3)
Baba Mtakatifu ni nani?
1. Ndiye Askofu Mkuu wa Maaskofu wote
2. Ndiye mchungaji mkuu wa Wakatoliki wote hapa duniani
3. Ni Wakili wa Yesu Kristo hapa duniani. (Mt 16:18-19; Yoh 21:15-17).
Ibada ya Daraja inachapa alama gani nafsini mwa aliyepewa?
1. Ibada ya Daraja inatia rohoni alama isiyofutika
2. Inamlinganisha mpokeaji na Kristo Kuhani
3. Inamwezesha mwenye Daraja kutenda kwa Jina la Yesu aliye Kichwa cha Kanisa
Kwa Sakramenti ya Daraja Padri anapata mamlaka gani?
Kwa Sakramenti ya Daraja Padri anapata mamlaka ya
1. Kuadhimisha sadaka ya Misa Takatifu na kutakasa watu kwa njia ya Sakramenti.
2. Kuhubiri neno la Mungu
3. Kuwaongoza watu (Ebr 5:1-4)
Ni nani wenye uwezo wa kutoa Sakramenti ya Daraja?
Wanaotoa Sakramenti ya Daraja Katika ngazi tatu Uaskofu, Upadre, Ushemasi ni Maaskofu waliopewa Daraja halisi kama waandamizi wa Mitume.
Ni nani aweza kupewa kihalali Sakramenti ya Daraja Takatifu?
Mwenye kupewa kihalali Sakramenti ya Daraja Takatifu ni Mwanaume peke yake aliyebatizwa, akiwa na wito nasifa zinazotakiwa na kukubaliwa na Mamlaka ya Kanisa. Ndivyo Yesu Kristu alivyotaka mwenyewe
Alama wazi ya Sakramenti ya Daraja Takatifu ni nini?
Alama wazi ya Sakramenti ya Daraja Takatifu ni kuweka mikono juu ya yule anayepewa Daraja na kutamka maneneo ya sala ya wakfu.
Anayetaka kuwa padri yampasa nini?
Yampasa;
1. Awe na tabia njema, akili za kutosha na afya nzuri.
2. Apende sana wokovu wa watu na kujitolea kwa huduma ya Mungu
3. Awe tayari kuishi hali ya useja maisha yake yote
Kwa sababu gani cheo cha Padri ni kikubwa sana?
Kwa sababu Padri anashiriki Upadri wa Yesu Kristo na ni mjumbe kati ya Mungu na Mwanadamu
Yatupasa nini kwa wenye Daraja Takatifu?
Yatupasa
1. Kuwaheshimu
2. Kuwasikiliza na kufuata mafundisho yao
4. Kuwasaidia katika utumishi wao kwa Sala na sadaka zetu
Matokeo ya Sakramenti ya Daraja ni yapi?
1. Inaleta mmiminiko wa kipekee wa Roho Mtakatifuambao unamlinganisha mhusika na Kristo
2. Inatia alama ya kiroho isiyofutika. kwa hiyo haiwezi kurudiwa au kutolewa kwa muda tuu.
Read and Write CommentsReferences:
Google ScholarResearchGateSemantic ScholarAckySHINE