Maisha magumu ya changamoto ya mke na mme

Nilianza kujisikia vibaya hata kabla ya kufunga ndoa. Nakumbuka miezi mitatu kabla wakati tukiwa katika maandalizi maandalizi ya Bashiri kuja nyumbani kuleta mahari miguu ilianza kuuma kiasi cha kushindwa hata kutembea. Mama ainikanda mara kwa mara na ilikuwa ikivimba na kutoa maji kama vile jasho lakini la baridi.

Nilienda hospitali zote lakini sikugundulika na kitu chochote, nilipewa dawa tu za maumivu ambazo kusema kweli hazikusaidia chochote. Ndiyo nilikuwa nimemaliza chuo hivyo hata mchakato wa kuzunguka kutafuta kazi ilibidi niusimamishe, Bashiri alinipa moyo na kuniambia kuwa kazi nitapata tu nishughulikie afya yangu kwanza.

Nilifuata ushauri wake na mipango iliendelea huku nikipata nafuu na kuzidiwa, napata nafuu nazidiwa hivyo yani. Kutokana na hali yangu tuliamua kuchanganya sherehe zote kwamaana ya Send off na Reception, Kitchen Party ilifanyika kwa watu wachache na muda wote nilikuwa nimekaa. Siku ya sherehe niliingia ukumbini vizuri, sherehe ikaanza tukakata keki, tukala chakula lakini zawadi kule kusimama kupokea zawadi nilishindwa kabisa.

Miguu ilikuwa inawaka moto huku ikitoa jasho la baridi, sijui nini kilikuwa kikiendelea huko chini kwani viatu nilivyokuwa nimevaa vilijaa maji, niliwekewa kiti na MC akasema maharusi wakae na alipoona nimezidiwa alisema watu wacheze mziki na maharusi tuachwe wakapumzike. Watu hawakuelewa chochote kwani ingawa nilishindwa hata kunyanyuka lakini MC alikuwa mjanja.

Aliongea kua Bwana Bashiri sasa hembu mbebe mke wako kuonyesha upendo kuwa utamlinda na kubeba katika maisha yako yote. Mume wangu alininyanyua na kunibeba kunitoa nnje, nililazimisha tabasmu mpaka nilipoingia kwenye gari ambapo moja kwa moja tulielekea Muhimbili ambapo nilikaa kwa wiki mbili bila kupata nafuu yoyote. Walishindwa kwani walikuwa hawajui ni kitu gani kilikuwa kikisababisha hali ile.

Miguu ilikuwa inauma kwenye mifupa, mwanzoni ilikuwa ni mpaka magotini lakini kadri siku zilivyokuwa zikienda maumiivu yalipanda mpaka kiunoni. Mbali na maumivu nilikua nikitokwa na jasho la baridi kama maji, yaani nikilalia shuka au nikivaa nguo baada ya masaa mawili nakuwa kama nimemwagiwa maji. Mwili unachemka lakini natoa jasho la baridi.

Kutokana na maumivu sikuweza kufanya chochote, hata kunyanyuka kwenda kujisaidia ilikuwa shida hivyo mume wangu alikuwa na kazi ya kunibeba kila siku mpaka chooni na kunisafisha. Anapokuwa kazini tulikuwa na mfanyakazi ambaye alikuwa akinisaidia kama kunikausha maji lakini alikuwa hawezi kuninyanyua hivyo kazi zote za kunibadilisha na kunisafisha ilikuwa juu ya mume wangu.

Mwaka uliisha nikiwa katika hali ile, mume wangu alijitahidi sana akauza na viwanja vyake alivyo nunua kipindi cha ujana na kunipeleka mpaka India lakini haikusaidia, nilipewa dawa tu kwaajili ya kukausha jasho ambazo zilisaidia kidogo lakini maumivu yalikuwa hayakomi, sanasana mwili ulikuwa unakakamaa tu.

*

Yale hayakuwa aina ya maisha ambayo nilipanga kuishi katika ndoa, kila nilichokuwa nikikiwaza kilikuwa kinyume chake, nilimuonea sana mume wangu huruma kwani badala ya kuwa mume alibadilika na kuwa nesi. Muda ulikuwa unaenda na kama mtoto wa kwanza nyumbani kwao wazazi walishakata tamaa, walihitaji mjukuu na kila siku walimsumbua kutafuta mke mwingine.

Hata mimi nilitamani aoe mke mwingina au hata atafute kimada wa kumtuliza hisia zake kwani tangu kuoana tulikuwa hatuja kutana kimwili, kamba mwaka uliisha bila mimi na mume wangu kufanya mapenzi. Siku moja uvumilivu ulinishinda na nikiwa katika maumivu makali nilimshauri kuwasikiliza ndugu zake na kutafuta hata mwanamke wa kuzaa naye tu kwani mimi sikuwa na dalili za kupona.

Aliniangalia kwa huzuni kisha akaniuliza. “Unataka kuniambia kama ni mimi ningekuwa kwenye hali hiyo na wewe ungeniacha ukatafuta mwanaume mwingine?’ Jibu lake lilikua rahisi “Hapana, wewe ni mume wangu nakupenda sana…” Niliongea kwa suti ya unyonge lakini ya kumaanisha. “Sasa kama ni hivyo mbona mimi unataka nikusaliti…”

Nilitulia kidogo na kumuambia “Lakini wewe ni mwanaume, unahisia, sisi wanawake tunaweza kuvumilia, lakini wewe ni mwanaume, wazazi wako wanataka wajukuu, mimi siwezi kupona leo wala kesho oa mwanamke mwingine hata kama hutaniacha nitafurahi kukuona unafuraha…” Nilijitahidi kujibu kwa sauti ya kutetemeka na ya kukata tamaa. Bashiri aliniangalia machoni kwa muda mrefu kisha akaniuliza.

“Hivi kuna fomu ambazo ulijaza kufanya maombi ya huu ugonjwa kwa Mungu?” Aliniuliza swali ambalo sikupata jibu… “Mimi ndiyo napaswa kukuonea huruma kutokana na maumivu uliyonayo sio wewe kunionea huruma eti nahitaji mwanamke wakutuliza hisia zangu au mtoto ili na mimi nionekane mwanaume!Kama siwezi kuvumilia hisia za mwili wangu kw asababu ya ugonjw abasi sipaswi hata kuitwa mwanaume achilia mbali mume wako!” Aliongea maneno ambayo yalinipa faraja na kunifanya niandelee kupigana bila kukata tamaa.

Miaka miwili ilipita hali yangu ikiwa bado haijatengamaa, nilitamani kukata tamaa lakini kila siku mume wangu alinipa nguvu ya kuendelea kupambana. Tulienda kwennye maombi na kutumia dawa mbalimbali za hospitalini na za kienyeji lakini haikusaidia. Watu wengi waliamini nimelogwa lakini kutokana na imani tulimkabidhi Mungu awe muamuzi wa yote.

Siku moja mume wangu alikuja na Mzee mmoja pale nyumbani, wakati huo sikua najua alimpatia wapi lakini yule mzee alikaa nyumbani pale kwa miezi sita akiondoka mara moja moja na kukaa kama siku nne tano na kurejea. Alikuwa akija na dawa za kienyeji za kunikanda, kunichemshia na kunywa, dawa zilikuwa chungu na kusema keli ilikuwa kama adhabu kwani ilikuwa kutwa mara tatu na kukandwa tena dawa za moto.

Ukichanganya na maumivu basi ilikuwa kazi sana lakini sikua na namna nilivumilia. Kweli miezi sita ile nilianza kupata nafuu, maumivu yaliisha kabisa ingawa bado nilikuwa siwezi kunyanyuka, miguu haikuwa ikitoa maji tena wala kukakamaa niliweza kukunja lakini sikuwa na nguvu ya kusimama. Baada ya kupata nafuu ile yule mzee alituambia kuwa ameshafanya yake yaliyo ndani ya uwezo wake sasa kilichobaki ni kumuachia Mungu, alinipa dawa za kunywa na kumpa mume wangu jukumu la kunifanyisha mazoezi.

Hali yangu ilianza kutengamaa, kila siku asubuhi na jioni mume wangu alikuwa akinifanyisha mazoezi. Kwa mara yakwanza tangu kuingia kwenye ndoa, niliweza kumuangalia mume wangu na kuanza kumuona kama alivyo bila maumivu. Siku moja wakati akinifanyisha mazoezi, nilimkodolea macho, alikuwa amekonda kupita kiasi, kusema kweli kila siku nilikuwa naye lakini siku ile ndiyo niliona tofauti.

Yaani alikuwa amepungua na kuwa kama mtoto, uso wake ulionekana hauna nuru ingawa kila mara alikuwa akilazimishia tabasamu lakini alionekana kweli na mawazo. Nilijipa moyo nikiamini labda ni sababu ya ugonjwa wangu ndiyo ulikuwa unammaliza kutokana na mawazo, siku nilimuomba kuangalia picha zetu za harusi kweli alikuwa amekonda sana kuliko hata nilivyowaza awali.

Nilishindwa kuvumilia na kumuuliza nini kilikuwa kinamsumbua tofauti na hali yangu, aliishia kutabsamu na kusema hakuna kitu ni maisha tu nikipona na yeye atakuwa sawa. Lakini ukweli mume wangu hakuja kuwa sawa tena. Sikumoja mume wangu aliingia chumbani, nilishaanza kupata nafuu ingawa bado nilikuwa siwezi kunyanyuka wala kufanya chochote.

Alionekana kuwa na huzuni kuliko kawaida yake, ingawa alijaribu kutabasmau lakini nilimuona kabisa akilengwa lengwa na machozi. Aliongea na kunikalisha kitandani kisha nayeye akakaa pembeni yangu na kuniambia. “Mke wangu kuna kitu naomba unisaidie, yaani uniahidi kukifanya, nakuomba sana unahidi kitu hicho na hata iweje usijekubadilisha mawazo, naomba sana…”

Aliongea huku akilengwa lengwa kwa machozi, nilimuambia hakuna hata haja ya kuuliza nilikuwa tayari kufanya kitu chochote. Alisisitiza niahidi kufanya na mimi niliahidi huku nikinyanyua mikono yangu kumkumbatia. “Mke wangu naomba nikifa uolewe tena na kama Mungu akikujalia mtoto basi kama ni wakiume umpe jina langu na kama ni wakike basi jina la kati liwe la kwangu…”

Aliongea machozi yakimtoka, sikutaka kumsikiliza kwanini anaongelea kufa nilijaribu kumtuliza lakini aliniomba ni muahidi hicho kitu. Alirudia zaidi ya mara kumi ndipo nilipomuahidi kua nitafanya hivyo. Baada ya kumuahidi aliniambia kuwa yeye hawezi ishi mdua mrefu, aliamua kunificha lakini anajua hana muda hivyo kuamua kuniambia. Mwaka mmoja uliopita aligundulika kuwa ana kansa na ilikuwa katika hatua mbaya.

Hakutaka kuniambia kutokana na ugonjwa wangu lakini Daktari aliyekuwa anamhudumia alimuambia kuwa hana zaidi ya mwaka ila mpaka wakati ananiambia ilikua ni karibu miaka mwili kitu ambacho ilikuwa ni kama miujiza. Aliniambia hajisikii vizuri na kaamua kuniambia kwani hata nguvu ya kunihudumia hana tena. Kweli mume wangu alikuwa amechoka na hali yake ilikuwa mbaya.

Sijui nilipata wapi nguvu lakini nilijikuta nasimama, ingawa sikusimama kwa muda mrefu lakini sikutaka kulia, nilijitahidi kuzuia machozi na kumkumbatia mume wangu. Ilikuwa ni karibu miaka mitatu tangu tuoane na katika muda wote huo tulikuwa hata hatujakutana kimwili, alivumilia ugonjwa wangu tangu siku ya kwanza ya ndoa yetu na mimi nilimuomba Mungu anipe nguvu hata niwezie kumhudumia lanini haikutokea. Sikuweza kusimama tena mpaka sasa wakati naaandika hapa.

Ingawa nimeweza kupona lakini magoti yangu hayana nguvu kuubeba mwili wangu hivyo nalazimika kutumia kiti cha magurudumu. Mume wangu alifariki mwezi mmoja baada tu ya kunipa zile taarifa na kila siku katika mwezi huo alisisitiza niolewe ili niwe na furaha. Ni mwaka wa pili sasa, sijaolewa na sidhani kama nitakuja kuwa na furaha, naweza kufanya kazi zangu lakini sijui kama nitaweza kuufungua moyo wangu tena.

**

Kila siku maneno ya mume wangu hunijia, najua alitaka niwe na furaha na kila siku na muomba anipe mwanaume wa kunipa furaha. Natamani sana nimzalie mtoto ili tu abebe jina lake, nadhani hicho ndiyo kitu ambacho kinanipa nguvu mpaka sasa. Mungu alinipa Mume akanipa na Nesi. Alijitoa kwaajili yangu akiwa mzima na hata baada ya kugundua kuwa ni mgonjwa aliweka ugonjwa wangu mbele na kunihudumia mimi kwanza.

Natamani kuandika mengi ila leo niishie hapa. Lengo la kuandika kisa changu hiki nikuwaasa tu nyie mlioko katika ndoa kuwa msipoteze muda wenu katika kunyanyasana na kuudhiana, katika kugombana, kuna muda mchache sana wa kupendana na kila siku utakua ukijuta kama hukumpenda mwenza wako ipasavyo. Mapenzi ni furaha, ingawa ndoa yangu yote ilikuwa ya mateso lakini yalikuwa ni mateso ya ugonjwa, ilikua ni ndoa ya amani na mume wangu kila siku alihakikisha natabasmau.

Alifanya kila kitu ili kuhakikisha kuwa nina furaha hakuchoka kunifanya nitabasamu hata nikiwa katikati ya maumivu makali. Nakumbuka alijua napenda sana kuvaa viatu virefu hivyo karibu kila mwezi aliniletea zawadi ya viatu na kila viatu vipya vilipotoka alikuwa akiniletea. Alivipanga ndani na kuniambia hakutaka fasheni inipite hivyo nikipona nita vaavvyote. Mpaka sasa sijaweza kuvvaa kwani bado sijaweza kutembea ila naamini ipo siku Mungu atanisimamisha na nitaweza kutembea na nitavivaa vyote kwaajili yake.

Naomba nimalizie hapa, samahanini kwa stori ndefu nitafurahi sana kama utatumia sekunde chache kushea stori yangu. Lengo langu ni kwa yule anayesoma awe mwanamke au mwanaume kumpenda sana mtu aliyenaye na kumuonyesha mapenzi ya kweli kwani siku akiondoka utatafuta mtu wa kumuonyesha mapenzi itashindikana. Mimi nina mambo mengi ya kumkumbuka Mume wangu, hembu jiulize wewe ukiondoka leo mume au mke wako atakukumbuka kwa nini? Atakukumbuka kwa mazuri au mateso uliyompa?

Ahsante sana kaka, huwa natumia muda wangu mwingi kwenye ukurasa wako nikisoma unachoandika kuhusu mapenzi. Watu wengi wanachezea upendo wanaoonyeshwa leo kwakuwa wanadhani labda hautakoma, siku ukikoma ndipo watajuta. Mungu awabariki wote na awasaidie msije kujuta kwa mnayowafanyia wapenzi wenu bali muwatengenezee kumbukumbu nzuri na kuwapa faraja kila siku.

Kumbuka kuna siku utatamani kumuambia mko au mumeo unampenda lakini hatakuwepo kukusikia, kuna siku utatamani kumnunulia zawadi na kumpa tabasamu, kuna siku utatamani kutoka na familia nzima kufurahia maisha lakini mwenza wako hatakuwepo. Kwanini unatumia muda wko mwingi kutengeneza ugomvi, chuki na manyanyaso kwa mwenza wako. Ahsante sana kaka Iddi kwa kukubali kukiandika kisa changu na kunisikiliza, Mungu awabariki wote mliosoma kis ahiki na kitumieni kusambaza upendo.

Shopping Cart