Usiwe Bahili wa kutumia Mali ulizojaliwa na Mungu. Mungu amekupa Mali hizo ili ufurahie maisha uliyonayo ambayo siku moja yana mwisho.
Biblia inatufundisha hivi katika Kitabu cha Hekima ya Yoshua Bin Sira;
3Si sawa kwa mtu mchoyo kuwa tajiri.
Utajiri una maana gani kwa mtu bahili?
4Mtu anayekusanya mali kwa kujinyima mwenyewe,
anawakusanyia watu wengine.
Hao wataiponda mali yake katika anasa.
5Aliye bahili kwake mwenyewe atakuwa mkarimu kwa nani,
kama hafurahii utajiri wake mwenyewe?
6Hakuna mtu bahili kuliko anayejichukia mwenyewe;
ndivyo ubaya wake unavyomlipa yeye mwenyewe.
7Hata kama akitenda wema, hutenda kwa ajali,
na mwishowe hujulisha hali yake duni.
8Mtu mwenye kijicho ni mwovu;
huangalia pembeni na kuwadharau watu.
9Jicho la mchoyo haliridhiki na kile alicho nacho,
na uchoyo huidhoofisha roho.
10Mtu mchoyo ni bahili wa chakula,
haweki chakula mezani pake.
11Mwanangu, tumia vitu vyako kukufurahisha uwezavyo,
na mtolee Bwana tambiko zitakiwazo.
12Kumbuka kwamba kifo hakitakawia,
na kwamba hujatangaziwa kauli ya kuzimu.
13Mtendee rafiki yako mema kabla hujafa;
uwe mkarimu na kumpa kadiri ya uwezo wako.
14Usijinyime siku moja ya furaha,
usiache sehemu yako ya furaha halali ikuponyoke.
15Siku moja utawaachia wengine matunda ya jasho lako;
yote uliyochuma kwa kazi ngumu yatagawanywa kwa kura.
16Wape wengine na kupokea kwao ujifurahishe moyo,
maana mtu hatazamii starehe huko kuzimu.
17Viumbe vyote hai huchakaa kama vazi,
maana kauli ya tangu zama ni: “Lazima mtakufa!”
18Kama vile majani katika mti uliotanda matawi:
Hupukutika yakaanguka na mengine huota,
ndivyo ilivyo kwa binadamu wenye mwili na damu:
Mmoja hufa na mwingine huzaliwa.
19Kila kilichotengenezwa huchakaa na kutoweka,
naye mtengenezaji hutoweka na kazi yake. (Sira 14:3-19)
Unaweza ukajikuta unatafuta Mali katika Maisha yako yote kwa kujinyima na kujikatalia lakini mwisho wa siku Mali ulizotafuta hutozifaidi wewe. Tena hata wale watakaozifaidi wanaweza wakasahau kwamba wewe ndio uliyezitafuta. Na tena wanaweza wakazitumia vibaya.
Inawezekana unajibana masha yako yote kutafuta hela bila hata kula chakula kizuri na kunywa vizuri pamoja na kuishi maisha ya furaha, lakini maisha yako yatakapokuwa yameisha wale utakaowaachia mali hizo wakaziponda na kuzitumia vibaya.
Kwa ubahili na ugumu wa kutumia Mali unaweza ukashindwa kuonyesha upendo wako kwa watoto wako, ndugu na marafiki zako. Ukiwa bahili wa kutumia mali huna nafasi ya kufurahi na wanao, ndugu na marafiki. Wakati maisha yako yatakapokuwa yameisha hao uliowabania kutumia mali zako wataishia kukuona kuwa hukuwapenda japokuwa ulitafuta mali kwa ajili yao na umewaachia mali hizo. Utakaowaachia mali hawatakukumbuka kwa sababu hukuwahi kuishi nao kwa furaha kwa kuwa ulikuwa unabania matumizi ya mali zako.
Kwa sababu ya ubahili unashindwa kutimiza wajibu wako kwa Mungu wako wa kutoa zaka na sadaka pamoja na kusaidia masikini na wahitaji.
Matokeo ya ubahili wa matumizi ya mali ni kukosa yote na kupoteza yote.
ANGALIZO: Sikwambii kwamba utumie mali vibaya bila kujalli Maisha yako ya baadae na maisha ya wale wanaokutegemea. Nakwambia kwamba tumia mali zako kwa staha na kwa kujinufaisha mwenyewe na wale ulionao wakati ungali hai. Usijibane sana kwa kujinyima nafasi ya kufurahia maisha yako na ya wale unaoishi nao.
Ni vizuri kujiwekea akiba ya Maisha ya baadae lakini ni vizuri zaidi kuweka wazi kwamba ni nani atakayemiliki mali zako wakati utakapokuwa haupo. Ukishaamua ni nani atakayemiliki mali zako wakati ukiwa haupo, ni wajibu wako pia kumuandaa na kumlea kwa namna ambayo ungependa aendeleze yale uliyoyaanza ili juhudi zako zisiishie tuu pale unapokua haupo, bali ziendelee hata utakapokuwa haupo.
Maisha ya binadamu ni kama majani ya mti; yanachipua, yanakomaa, yananyauka na mwishowe yanaanguka. Wakati jani linakauka na kuanguka, yapo mengine yanayo anza kujichipua na kukomaa. Jani likianguka, linaachia nafasi yale yanayochomoza na kukomaa.
Tutumie Maisha yetu vizuri, kwa furaha, amani na upendo huku tukiwatengenezea wale watakaokuja baada yetu mahali pema pa kuishi.
Zaidi sana, Tumuombe Mungu atupe hekima na Busara ya kutumia Mali anazotujalia kwa manufaa yetu na manufaa ya wenzetu huku tukimtukuza Mungu.
Read and Write Comments