Dondoo za Urembo na Mitindo

Mavazi ya Ofisini kwa Wadada

Wengi wetu tunashindwa kutofautisha mavazi ya sehemu husika mfano Ofisini, michezoni, na yale ya usiku na sehemu nyinginezo leo nitagusia vazi la ofisini kwa akina dada.

Unapotaka kuvaa vazi ,lazima uangalie vazi unalolivaa mda gani na mahala unapokwenda,siyo vazi la kutokea usiku au la kimichezo unalivaa ofisini,utakuwa kichekesho mbele za watu hata kwa wafanyakazi wenzio.

Mavazi ya kiofisi yanaeleweka lakini hasa kwa mwanamke basi vaa sketi fupi au ndefu na blauzi ya heshima iliyofunika kitovu chako, au suti ya heshima na koti na hata suruali ambayo haijakubana sana inafaa sana kwa ofisi.

Kama utapendelea kuvaa gauni basi angalia mkao wa hilo gauni ukoje maana mara nyingi gauni huwa halipendezi kuwa vazi la ofisini bali vazi la jioni.

Jinsi ya Kutumia Bamia kuondoa chunusi Usoni

Wiki hii kwenye urembo tutaongelea mboga aina ya bamia jinsi inavyotibu chunusi na kuziondoa moja kwa moja. Mbali na chunusi, pia husababisha ngozi kuteleza na kuwa nyororo.

JINSI YA KUFANYA

Chukua bamia zikatekate vipande, ziweke kwenye brenda kisha chukua limao kipande na maji kidogo, weka kwenye brenda kisha saga. Baada ya kupata mchanganyiko wako upake usoni mpaka kwenye shingo, acha kwa muda likauke kisha bandua kama unavyoondoa maski nyingine usoni.

FANYA HIVI SIKU TATU KWA WIKI ITAKUSAIDIA KUONDOA CHUNUSI.

Jinsi ya Kujaza nywele kwa njia za Asili

Zingatia mambo haya yafuatayo;

  1. Chukua parachichi kubwa moja, asali vijiko vitatu na kiini cha yai.
  2. Osha nywele zako kwa shampoo na uzikaushe.
  3. Ponda ponda parachichi mpaka lilainike kabisa. Chukua vijiko vitatu vya asali na kiini cha yai kisha changanya yote kwa pamoja.
  4. Paka mchanganyiko huo kaa nao kwa muda wa dakika 15 kisha osha.
  5. Fanya hivyo kwa muda wa wiki moja hadi mbili na utaweza kuona matokeo mazuri katika nywele yako

Mambo ya kuzingatia kama una ngozi yenye Mafuta

Ngozi yenye mafuta kwa kawaida huwa inang’ara, nene na yenye rangi iliyotitia. Mara nyingi ngozi yenye mafuta mengi sana huwa na chunusi nyingi na vipelepele na mara nyingine huwa na chunusi zenye vichwa vyeusi. Katika aina hizi za ngozi mafuta hutokana na tezi za sebaceous na kuzalisha mafuta zaidi ya kiwango kinachotakiwa. Mafuta hayo husambaa katika ngozi na kuifanya iwe na mafuta mafuta.

Mafuta katika mwili yanatengenezwa na ‘sebaceous glands’,kwa hiyo kuna baadhi ya watu wana sebaceous glands ambazo zinatengeneza mafuta kwa wingi sana na hivyo kufanya ngozi zao kung’aa kwa sababu ya hayo mafuta mengi.

Sebaceous gland zipo kwa wingi usoni(face) shingoni(neck), kifuani, kichwani na mgongoni, ndiyo maana hayo maeneo yanakuwa na mafuta kwa wingi.

Sababu zinazosababisha ngozi kuwa na mafuta:

  1. Kurithi.
  2. Lishe.
  3. Kiwango cha homoni mbalimbali mwilini.
  4. Ujauzito.
  5. Vidonge vya kuzuia mimba.
  6. Baadhi ya vipodozi.
  7. Hali ya hewa ya joto.

Namna ya kutunza ngozi zenye mafuta

Faida kubwa ya kuwa na ngozi yenye mafuta ni kuwa haizeeki kwa haraka ikilinganishwa na aina nyinginezo za ngozi. Miongoni mwa mambo yanayosaidia ili kuitunza ngozi yenye mafuta na kuiepusha na chunusi na hali isiyopendeza ni:-

Ngozi yenye mafuta inahitajia kusafishwa vyema kwa maji ya moto na sabuni ili kuzuia vinyweleo visizibwe na mafuta.

Epusha vifaa vigumu visikwaruze uso wako na kupelekea ngozi kubanduka, kwani suala hilo husababisha tezi za mafuta kufanya kazi zaidi ili kujaza sehemu iliyopotea ya mafuta.

Epuka kutumia vipodozi ambavyo huifanya ngozi yako ipoteze maji au kukauka. Kwani husababisha sehemu ya juu ya ngozi inyauke, na hivyo kusababisha mafuta kuziba vinyweleo na kupelekea kutokea vichwa vyeusi.

Jitahidi kuitunza vyema ngozi yako na kuisafisha vizuri. Jaribu kuosha uso mara mbili au tatu kwa siku. Usioshe mara nyingi kwani kufanya hivyo huufanya uso kutoa mafuta zaidi.

Chagua kile unachosafishia kwa makini, jiepushe kutumia cream nzito nzito au vifaa vugumu wakati wa kuosha uso wako. Ni bora utumie sabuni za kawaida zisizokuwa na madawa. Unaweza kutumia lotion ya kuua bacteria au sabuni zisizo na dawa nyingi (lightly medicated), au sabuni zenye madini mbalimbali. Ni bora usioshe au kutumia lotion au michanganyiko yenye alkoholi.

Tumia maji ya moto au ya vuguvugu wakati unaosha uso wako.

Wakati unapoosha uso wako, ukande kwa kutumia ncha za vidole, jiepushe kupaka sabuni moja kwa moja usoni, inaweza kuganda na kuzuia vinyweleo kuziba.

Kutumia mask za udongo (clay) na tope (mud) husaidia katika ngozi za aina hii. Ni bora utumie mask mara moja au mbili kwa wiki.

Jitahidi kutumia vipodozi vya uso ambavyo vimetengenezwa kwa ajili ya ngozi yenye mafuta.

Jinsi ya Kujiremba Macho

Kuna urembo mbalimbali wa macho kulingana na taste ya mtu na mapendeleo yake . Leo nitazungumzia “smoky eyes” au macho yaliyapambwa kwa eye liner, mascara na eye shadows zenye rangi nyeusi, grey au za mng’aro.

Jinsi ya kuremba jicho:

Hakikisha uso na ngozi inayozunguka jicho ni safi kabla ya kuanza urembo wowote usishawishike kupaka vipodozi juu ya ngozi chafu haitakaa vizuri make up yako. Safisha kwa kutumia face towel iliyochovywa kwenye maji ya moto(huwa naona ni rahisi kwangu hasa kama kitambaa nitumiacho ni cheupe ni rahisi kujua kuwa u msafi au la kwa kuangalia kitambaa) kamwe usioshe uso wako kwa sabuni au maji ya moto. Ngozi ya uso iko rahisi kudhulika ikipata msukosuko kidogo. Sabuni huwa na kemikali nyingi na maji ya moto yanapausha uso. kama utalazimika kutumia sabuni osha uso kwa maji ya baridi kwa muda kiasi ili kuondoa kemikali zitakazokuwa zimeachwa.

Tayarisha kope/eye lids zako kwa kupaka wanja mweusi kwa uangalifu au eyeliner ya dark colour kama ni mtu anayejiamini unaweza tumia rangi yoyote ile sababu si wote wanaweza paka rangi ya njano au kijani na wakawa confident na muonekano wao.

Kwa matokeo mazuri uwe na eye shadow za aina mbili moja ya rangi iliyokolea na nyingine iliyo light. Anza na rangi iliyo light paka kwa uangalifu kuelekea kona ya nyusi kama picha hapo chini.

Endelea kama unapenda ming’ao machoni(hususani kwa sherehe) unaweza kupaka juu ya kope zako ila hakikisha hufiki mbali sana karibu na nyusi . Kisha malizia na darker colour kama picha ya kulia inavyoonyesha anzia kona ya kushoto ya jicho kwenda kulia kwa kiasi upendacho.

-Linganisha macho yako yote kama yana muonekano sawa kisha unaweza kuongezea mascara kwa juu ya nyusi ikiwa ni mpenzi.

Mambo ya msingi kwa mwanamke kuyajua unapojiremba

Kope nazo humpendezesha mwanamke kuna aina ya rangi za kupaka kwenye kope, lakini zinatofautiana. Ni vyema ukawasiliana na wataalamu wa mambo ya urembo kwa ushauri na siyo kukurupuka. Siyo umemuona fulani kapendeza na aina fulani ya rangi ya kwenye kope halafu na wewe ukakimbilia kupaka, utachekesha.

Rangi ya mdomo nayo ni eneo lingine linalompendezesha mwanamke. Ukweli ni kwamba tunatofautiana sana midomo wazungu wanaita ‘Lips’ Kila mwanamke ana tofautiana midomo na mwingine kwa hiyo hata rangi ya midomo nayo inakwenda sambambana aina ya lips na rangi ya ngozi ya mwili aliyo nayo mwanamke, siyo unajisiriba rangi ya mdomo halafu unaonekana kituko. Wasiliana na wataalamu wa urembo kwa ushauri zaidi.

Kucha kwa wanawake ni eneo lingine linolatakiwa kuwekwa katika unadhifu. Kuna baadhi ya wanawake unaweza kukutana nao kucha zao zimelika aidha kwa kung’atwa au kwa kuliwa na fangasi.

Ni vyema wanawake wenye tatizo hilo kumuona mtaalamu wa ngozi kwa msaada wa tiba. Unaweza kukutana na mwanamke kucha zake zimelika na zina sharp edges kiasi kwamba akikugusa utadhani umeguswa na msasa.

Au akishika Glasi ya Kinywaji ukiangalia kucha utadhani mkono ni wa mwanaume maana kwa jinsi kucha zake zilivyo hata hafanani nazo. Kuna kucha za bandia kama mwanamke ana matatizo ya kucha basi akazinunue kusitiri aibu.

Marashi, manukato au unyunyu kama wanavyoita vijana wa mjini ni muhimu kwa wanawake lakini ni vyema nikaweka angalizo. Haipendezi kwa mwanamke anayepulizia manukato yanayonukia sana mpaka yakawakera wengine ni vyema wanawake wakajipulizia marashi yenye staha na yasiyokera.

Ngozi ya mwanamke ni bora ‘sensitive’ sana na inaakiwa ipakwe aina ya mafuta au lotion yenye virutubisho kulingana na aina ya Ngozi. Kuna wanawake wenye Ngozi ya mafuta ‘Oil Skin’ kuna wenye Ngozi mchanganyiko na kuna wale wenye ngozi kavu (Dry Skin).

Ni vyema mwanamke kujua aina ya ngozi yake ili ajie aina ya product ya ngozi anayopaswa kutumia na siyo kwa sababu umemuona mwenzio anapaka aina fulani ya losheni na wewe unakimbilia kununua. Omba ushauri kwa wataalamu wa ngozi watakusaidia. Kuna baadhi ya maduka yanyouza vipodozi wanatoa msaada huo bure kabisa.

Jinsi ya Kuondoa Makovu Mwilini

Makovu sio kidonda naomba hili uelewe, ila makovu ni alama ya majeraha ambayo yamebaki kwenye ngozi baada ya kupona majeraha.
Kuna baadhi ya watu husumbuliwa na shida ya kuwa na makovu sehemu mbalimbali ya mwili.
Hivyo kama wewe ni miongoni mwao maandishi haya yanakuhusu sana.

Zifuatazo ndizo mbinu za kuondoa makovu mwilini.

1. Tango

Unachotakiwa kufanya ni; Pondaponda tango na kisha kutumia mchanganyiko wake kwa kupaka juu ya kovu. Hii husaidia sana kulainisha makovu na ikiwa utatumia kwa muda mrefu huondoa makovu pia.

2. Aloe vera.

Unachotakiwa kufanya ni; kata majani hayo na utumie utomvu wake kupaka katika makovu kisha mara baada ya muda Fulani utaona mabadiliko na itapunguza na kuondoa makovu.

3. Asali

Unachotakiwa kufanya; Paka asali juu ya kovu na kuiacha usiku kucha. Rudia mara kwa mara kupaka asali hadi pale kovu litakapotoweka.

Jinsi ya kusafisha na Kutunza Kucha zako

Inashauriwa kwamba kabla ya kuchukuwa uamuzi wa kwenda kununua vifaa husika ambavyo utavitumia unapaswa kufahamu aina ya kucha ili uweze kununua vifaa vinavyoendana na kucha zako kwa lengo la kuzilinda badala ya kuvamia na kuziharibu.

Kwa kawaida kucha za mikononi na miguuni zinakabiliwa na mazingira magumu kutokana na majukumu ya kazi za kila siku hali inayochangia kuziweka katika mazingira magumu kiafya.

Mbali na kucha kukosa afya, pia kuharibu shepu yake ya awali kutokana na shughuli za kila siku katika maisha ya binadamu yeyote, hivyo ni vyema kuzikinga kucha zako na maradhi kwa kuzifanyia usafi kila siku au mara kadhaa kwa wiki ili kuzilinda zaidi.

Ili kuweza kugundua aina ya kucha zako katika kuzipangilia wakati wa kuzifanyia usafi, unapaswa kuwa makini wakati unachagua rangi ya kupaka, kuangalia muonekano wa kucha zako zilivyo ili uweze kupangalia rangi ziweze kuwa na mvuto zaidi.

Ni vyema kwa mtu anayejali afya ya kucha zake kuchukua muda mwingi kufuatilia kucha zake na kuelekeza nguvu zake katika kuhakikisha zinakuwa katika matunzo mazuri na kujitahidi kubuni mtindo ambao unaweza kuwa tofauti na wengine ambao wanapenda kuzifanya kawaida.

Hata hivyo katika kutunza kucha ziwe nzuri, vyakula ambavyo ni mlo kamili ni muhimu sana, vinginevyo utajikuta ukishauriwa na wataalamu kutumia vitamini mbalimbali kama vile vitamini A, vitamini C, Culcium, Folic Asidi, Protini na Vitamini B12.

JINSI YA KUSAFISHA KUCHA.

Wekeza vifaa vizuri vya kisasa vya kutunzia kucha.
Tumia brush ya kucha kwa kusugua chini ya kucha na kuutoa uchafu na kufikia sehemu ngumu ambapo uchafu unajilundika. Unaweza tumia mswaki ukiwa huna vifaa vya kisasa.
Tumia maji moto na sabuni ya kunawia mikono.
Anza kwa kusugua chini kabisa kwa kushikilia brush chini na sugua kuanzia nyuma kuja mbele pole pole, kisha juu ya kucha fanya hivyo kwa kuzunguka.

Toa rangi kwa kuloweka pamba kwenye polish remover na usugue kwa vidole vyenye hinna huna haja ya kuitoa. kwa vidole vya afya na nguvu vipumzishe kwa kutumia polish kila baada ya wiki kadhaa.

Loweka kucha na maji kwenye bakuli,au sinki,au kifaa cha uwezo wako hata dishi poa,kwa maji ya moto ya uvuguvugu na pitisha sabuni ya kunawia mikono.Na ni kucha tu usiloweke mkono mzima,kwa dakika tatu,sabuni kwenye maji hufanya mikono kuwa mikavu .

Suuza kwa maji ya bomba ya uvuguvugu,au yalokua kwenye chombo yaani jimwagie,kisha zifute na taulo laini.

Kisha tumia kikatio kucha kukata maana zitakua laini,au kifaa cha kuzipunguza kuweka sawa kama hauzikati.

Jinsi ya kuondoa weusi kwenye magoti na viwiko vya mikono

Ngozi nyeusi katika magoti na nyuma ya mikono hutokana na mkusanyiko wa cells zilizokufa, na hata unavyoweka pressure kwenye magoti na vipepsi vya mikono yako. Kama ukiwa unaweka mikono kwenye meza ukiwa kazini, ule msuguano unafanya ngozi iwe nyeusi.

Kama una magoti myeusi na nyuma ya mikono pia ni peiusi, tumia hizi njia asili kuweza kuondoa weusi huo:

Tumia Aloe Vera Juice.

Juice ya Aloe Vera inasaidia kuondoa weusi, all you have to do ni kupaka juice hiyo kwenye sehemu yenye weusi na uache kwa nusu saa kisha nawa na upake moisturizer. Rudia kufanya hivi mara mbili kila siku.

Tumia Binzari Manjano, Asali na Maziwa.

Changanya vyote hivi utapata mchanganiko mzito, paka kwenye magoti na kwenye mikono yako palipo na weusi. Kaa nayo kwa dakika 30, nawa na paka moisturizer. Rudia hii kila siku kwa wiki 3-4, utapata matokeo mazuri.

Tumia Ndimu.

Chukua pamba na uitumie kupaka juice ya ndimu katika sehemu zenye weusi. Au unaweza kuikata tu ndimu na kuipaka directly kwenye sehemu zenye weusi. Kaa nayo kwa lisaa 1 kisha nawa. Rudia hivi kila siku hadi weusi utakapopotea.

Tumia Olive Oil na Sukari.

Changanya vizuri, hii itakuwa kama exfoliation/scrub kwa ajili ya magoti na mikono. Paka katika hizo sehemu zenye weusi kisha kuwa kama una-massage polepole. nawa kwa maji ya uvuguvugu kisha paka moisturizer.

Faida za kutumia mafuta ya Nazi

Mafuta ya nazi hung’arisha ngozi:

Siyo sehemu za ndani tu ya mwili zinazofaidika na mafuta haya ya nazi kama yanavyofanya mafuta mengine ya asili, kama unataka kuwa na ngozi nzuri yenye mng’aro na yenye afya na yenye muonekano wa asili basi paka mafuta ya nazi kila siku kwenye ngozi yako, mafuta ya nazi yana uwezo mkubwa katika kuua bakteria, virusi, na vijidudu vya aina yeyote vinavyoweza kuidhuru ngozi, haya ni mafuta kwa mwili mzima yaani pakaa kwenye ngozi yote usoni, mwilini, kwenye nywele na kwenye kucha. Pia unaruhusiwa kuyatumia mafuta haya wakati wa masaji.

Huongeza nguvu mwilini:

Mafuta ya nazi ni chanzo kizuri cha nguvu ya mwili kwani yana sifa ya kuelea kwa kiasi kidogo kwenye damu ‘medium chain triglycerides – MCT’ ambapo sifa hii huyafanya kusafirishwa moja kwa moja hadi kwenye ini ambako hutumika kama chanzo cha haraka cha nguvu au hubadililishwa kuwa ‘ketones’ ambacho ni chakula cha ubongo. Kwahiyo ikiwa unatafuta lift ya kuinua nguvu yako basi chukua kijiko kimoja cha chai cha mafuta ya nazi weka kwenye kikombe chako cha juisi au uji na utaona maajabu.

Hutumika kulainisha uke mkavu:

Mafuta ya nazi yana matumizi mengi sana mwilini zaidi ya 100, kuna wanawake wana tatizo la kuwa na uke mkavu muda wote hata wakisisimuliwa vipi bado huwa wakavu, kuondokana na tatizo hilo pakaa mafuta ya nazi katika uke wako na utaona faida yake tena bila madhara yeyote hasi.

Husaidia katika ugonjwa wa mzio/aleji:

Tukisema tuelezee faida zote za mafuta ya nazi kwa hakika hatutaweza, moja ya faida zake zinazoshangaza wengi ni uwezo wa kudhibiti dalili za ugonjwa wa aleji, kila siku pakaa mafuta ya nazi ndani ya pua zako na uone kama utapiga chafya unapokuwa karibu na kile kinachokuletea aleji/mzio.

Ni mafuta mubadala ya kupikia yenye afya:

Tofauti na mafuta ya alizeti au hata mafuta ya zeituni, kupika chakula kwa mafuta ya nazi ni zaidi ya afya. Mafuta haya yana uwezo mkubwa wa kuungua na bado yakabaki na viinilishe vyake kama kawaida hata baada ya kuunguzwa au kuchomwa katika moto, hii ni kwamba mafuta kama ya zeituni ambayo huweza kuliwa hata yakiwa mabichi lakini yanapochomwa katika moto basi ubora wake hupungua au kwa maneno mengine huzalisha taka sumu kama ilivyo kwa vitu vingi vinapounguzwa lakini hili halitokei kwa mafuta ya nazi!

Ni mafuta mazuri kwa wasiopenda kutumia mafuta yatokanayo na wanyama:

Siyo kupika tu na mafuta ya nazi ndiko huleta afya, bali pia ni mafuta mazuri kwa wasiopenda kutumia mafuta yatokanayo na wanyama kama mubadala kwa siagi au vitu vingine mnavyopaka juu ya mikate mnapokula. Hii nikwa sababu mafuta ya nazi hubaki kuwa magumu hata katika joto la kawaida la chumba tofauti na mafuta mengine.

Huzuia maradhi mengi hatari mwilini:

Kama ilivyo katika kuipunguza kolesteroli, mafuta ya nazi yanao uwezo mkubwa katika kuzuia na kutibu magonjwa mengine sababu ya kuwa na kiasi kingi cha asidi iitwayo lauric acid. Utafiti mwingi umeendelea kuthibitisha kuwa hii lauric asidi hubadilishwa kuwa asidi mafuta nyingine ijulikanayo kwa kitaalamu kama ‘monolaurin’ ambayo inayo sifa ya kudhibit na kuvizuia baadhi ya virusi ikiwemo vile vya ukimwi kuziingia na kuzidhuru seli za mwili na kusababisha maradhi mwilini. Ili kutibu virusi vya ukimwi inashauriwa kunywa glasi 4 za tui la nazi kila siku kwa muda wa miezi mitatu mine na utaona maajabu.

Hutibu tatizo la kupoteza kumbukumbu:

Hii inaweza ikakushangaza kidogo unapoisikia kwa mara ya kwanza lakini tafiti nyingi zimeonyesha kuwa mafuta ya nazi yanao uwezo kuziamusha seli na shughuli za ubongo na katika kufanya hivyo kutasaidia kuzuia matatizo ya uwendawazimu au ukichaa (dementia) na kupoteza kumbukumbu (Alzheimer).

Mafuta ya nazi kwa afya ya Moyo:

Mafuta ya nazi yana asidi mhimu sana kwa afya ya moyo iitwayo ‘lauric acid’ ambayo ina uwezo mkubwa kuuweka moyo wako katika hali ya afya na furaha kwa kuidhibiti kolesteroli/lehemu mbaya katika moyo na mwili kwa ujumla. Lauric acid huongeza uwepo wa kolesteroli nzuri mwilini ijulikanayo kwa kitaalamu kama High Density Lipoprotein (HDL) huku ikiishusha ile kolesteroli mbaya ijulikanayo pia kwa kitaalamu kama Low Density Lipoprotein (LDL) jambo ambalo ni mhimu kwa afya ya moyo kama anavyosema Lovisa Nilsson, mtaalamu wa lishe wa Lifesum.

Mafuta ya nazi huuongezea nguvu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula:

Hii ndiyo moja ya faida ya mafuta ya nazi niipendayo zaidi. Ndiyo mafuta ya nazi yanayo uwezo kusaidia kudhibiti uzito uliozidi kwa sababu mafuta haya ni mepesi kumeng’enywa na hayagandi kama yalivyo mafuta mengine mazito (fatty acids) jambo linalosaidia kuuondoa uzito uliozidi mwilini. Kutokana na kitendo hiki cha kuongeza uwezo wa mwili kukimeng’enya chakula, watu wanaoyatumia mafuta haya kupikia vyakula vyao kila siku kwa kawaida huwa na uzito wa kawaida. Anasema Geeta Sidhu Robb, mtaalamu wa lishe na mwanzilishi wa Nosh Detox.

MHIMU: Hakikisha unapata mafuta ya nazi ambayo ni ya asili kwa asilimia 100, ikiwa utanunua dukani kuna uwezekano mkubwa yakawa yamechanganywa na kemikali zingine au haidrogeni kitu kinachoyapunguzia thamani ile ya asili. Kama unapikia kwenye chakula najuwa wengi mnapenda wali wa nazi au hata tui lake likiwekwa kwenye samaki au hata mboga yoyote lazima utajing’ata ulimi, basi nakushauri usichanganye na mafuta mengine kwenye hicho chakula.

Jinsi ya kufanya nywele zako ziwe na mvuto na kuvutia zaidi

Mwanamke unywele hasa ukiwa nao, hii ni kauli upya ambayo Muungwana blog inakupa siku ya leo. Miongoni mwa maswali ambavyo huwa tunaulizwa na wasamoaji wetu ni pamoja ni kwa jinsi gani naweza kutengeneza nywele zangu ili ziwe za kuvutia?

Basi nasi bila ya haiana yeyote ile tunakuletea somo hili maalum kwa ajili ya watu wote ambao wanatamani kujua namna ya kuzifanya nywele zako zivutie. Kwanza kabisa kuna vitu vingi vinavyoweza kufanya nywele zako zikakosa afya na mvuto, vitu kama vumbi, upepo, mvua, jua, maji na madawa tunayoweka kwenye nywele zetu pamoja na vyakula tunavyokula ni chanzo kikuu cha nywele zetu kuharibika na kukosa afya na mvuto

Hivyo zifuatazo ndizo njia ya kufanya nywele zako zivutie:

Tumia shampoo inayoendana na nywele zako

Tumia shampoo inayoendana na nywele zako, kuna nywele za aina tofauti. kuna nywele kavu, zenye mafuta, mchanganyiko, na pia kuna nywele nyepesi, laini, ngumu na nzito. zipo aina tofauti za shampoo zinazoendana na aina ya nywele zilizopo . hivyo basi ni vyema unapotaka kuosha nywele ukajua ni aina gani ya shampoo utumie, pia kwenye condition napo unatakiwa kufanya hivyo hivyo.

Usichane nywele kwa nguvu zikiwa mbichi.

Jaribu kuzichana nywele kwa kichanuo kikubwa, au jaribu kuziacha mpaka zikauke ndo uzichane. unapochana nywele mbichi tumia kitana kikubwa na chana taratibub ukianzia nyuma kuja mbele. kuchan nywele zikiwa mbichi bila kufuata utaratibu kutafanya nywele zako zikatike na ziharibike.

Kula vyakula venye protin na matunda

kula vyakula venye protin na matunda kutasaidia kuimalisha afya ya nywele zako na kuzifanya ziwe nzuri na za kuvutia.

Kata ncha za nywele zako

kukata ncha za nywele zako kunasaidia kufanya nywele zako kujizaa upya, mara nyingi seli katika ncha za nywele hufa. seli zinapokufa huzui nywele zinazozaliwa kushindwa kustawi vyema na hivyo kuzifanya nywele zako kukosa afya. japo wanawake wengi huwa hawapendi kukata ncha za nywele zao wakihofia nywele zao kuonekana fupi. lakini ukweli ni kwamba unapokata ncha za nywele zako unasaidia nywele zako kupata nafasi ya kukua vizuri na kuwa zenye afya nzuri na kuvutia.

Osha nywele zako angalau mara moja kwa wiki

kuosha nywele zako angalau mara moja kwa wiki kutasaidia kuzifanya nywele zako ziwe na afya. Hata kama uko busy sana basi jitahidi isipite wiki mbili bila kuonsha nywele zako.

Zifunge nywele zako kabla ya kulala

Unapotaka kulala hakikisha unazifunga nywele zako, unaweza kuzisuka mabutu au kuzifuna vizuri na kuzibana. kulala huki ukiwa umeziachia nywele zako hufanya nywele zikatike na kuharibika

Tumia mafuta asili

Badala ya kutumia mafuta yenye kemikali nyingi kutoka viwandani, jaribu kutumia mafuta ya asili katika kutunza nywele zako. tumia mafuta kama ya nazi au parachichi kupaka nywele zako.

Zilinde nywele zako na jua

W akati utakapokuwa unaelekea kwenye sehemu yenye jua kali, vumbi au upepo. zilinde nywele zako kwa kuzifunika na kofia, scarf au mtandio. Pia unaweza kuzipaka sunscreen.

Mambo ya Kuzingatia ili uwe na ngozi laini

Takribani kila mtu angependa kuwa na ngozi laini, au hata laini zaidi. Watu wengi wamekuwa wakiitafuta ngozi nzuri au kujitahidi kuitunza ili isiharibike. Lakini je, wamefanikiwa?
Wachache hufanikiwa na wengi hushindwa. Na hata hao waliofanikiwa wengi wao hutumia vipodozi vikali ambavyo vingi huchubua na kuharibu ngozi zao na kuwaletea madhara makubwa sana baadae.

Vipi wewe, ungependa kuwa na ngozi nzuri bila kuidhuru afya yako? Karibu somo la leo ili uweze kuwa na ngozi nzuri bila kuidhuru afya yako.

Ngozi laini ni nzuri na inaongeza mvuto wa mwili. Ulaini wa ngozi hupotezwa na mambo mbalimbali kama vile seli za ngozi kupungukiwa na maji na kuanza kusinyaa na kunyauka, seli za ngozi kujeruhiwa, na seli za ngozi kufa. Matokeo yake ni michirizi, makunyanzi, makovu, chunusi, madoa, ngozi kufubaa na kuzeeka.

Kuifanya ngozi kuwa laini unahitaji kuupatia mwili virutubisho vyote vya kujenga mwili vizuri na kunywa maji ya kutosha ili seli zisikauke, kusinyaa wala kunyauka. Kula mlo kamili, matunda mengi na kunywa maji ya kutosha.

Pia unahitaji kuepuka jua kali ambalo litaunguza ngozi, kuikausha na kuifanya iwe na makunyanzi na vitu vingine vinavyoota kwenye ngozi kutokana na jua.

Tumia vipodozi vizuri vinavyosaidia ngozi kuwa laini bila kuidhuru. Hapa kuna vipodozi vya aina mbali mbali na vinavyofanya kazi kwa njia mbali mbali. Vipodozi vya muhimu ni

  1. Vipodozi vya kuongeza unyevu au maji kwenye (seli za) ngozi
  2. Kwa kiingereza vinaitwa “Moisturizers”. Hivi hufanya kazi ya kufunika ngozi na kuzuia maji yasipotee kutoka kwenye ngozi, na pia husaidia kuongea maji kuingia kwenye seli za ngozi. Vipo katika mtindo wa sabuni, mafuta na losheni.
  3. Vipodozi vya kusaidia kuongeza kasi ya kuzalishwa kwa seli mpya za ngozi
  4. Hivi husaidia kuzalisha seli mpya za ngozi ambazo zitaleta ngozi mpya na nzuri na kuondoa ile ya zamani iliyochoka na kuzeeka. Mifano ni losheni na krimu zenye Vitamini A na Vitamini E.
  5. Vipodozi vya kusaidia kuondoa uchafu na seli (ngozi) zilizozeeka au kufa

Tumia sabuni zenye uwezo mkubwa wa kuondoa uchafu kutoka kwenye ngozi, na ukiweza tumia “face wash” au “facial cleansers”. Hivi husaidia kusafisha kabisa ngozi na kuondoa uchafu.

Kwa upande wa seli zilizokufa na kubaki juu ya ngozi tumia “scrub”. Scrub hufanya kazi kwa kuondoa seli zilizoharibika na zilizokufa na kuacha seli changa na ngozi nzuri.

USHAURI:

  1. Pata ushauri wa kulainisha na kupendezesha ngozi yako kutoka kwa wataalam wanaojua vizuri afya, urembo na vipodozi. Utashauriwa vizuri jinsi ya kufanya, vipodozi vya kutumia na jinsi ya kuvitumia vizuri kwa matokeo mazuri zaidi. Epuka wauza vipodozi wasio waaminifu au wasiovijua vizuri vipodozi, maana wanaweza kukupa vipodozi vya tofauti na mahitaji yako au vipodozi vinavyodhuru afya yako.
  2. Safisha ngozi yako vizuri, kila siku. Hakikisha unaondoa uchafu na vijidudu vyote vinavyotua na kukaa juu ya ngozi yako. Ondoa vumbi, seli zilizokufa, mafuta ya ziada, jasho nk Lala na pumzisha ngozi yako kiasi cha kutosha ili iweze kujitengeneza na kuwa nzuri. Ipumzishe kila siku kwa matokeo mazuri zaidi. Pata usingizi wa kutosha na ulio bora
  3. Tumia vipodozi vizuri vyenye uwezo wa kukupa matokeo mazuri unayoyataka na visivyodhuru afya yako. Pata ushauri mzuri kutoka kwa wataalam ili uweze kufanikisha hili vizuri. Tumia vipodozi vinavyoendana na ngozi yako. Kama ngozi yako ni kavu tumia vipodozi ambavyo ni maalum kwa ajili ya ngozi kavu, na kama ngozi yako ni ya mafuta basi tumia vipodozi ambavyo ni mahususi kwa ajili ya ngozi ya mafuta.
  4. Usitumie vipodozi vinavyoharibu ngozi na kuihatarisha ngozi yako. Epuka vipodozi vyote visivyo salama na vile visivyoendana na ngozi yako.
  5. Jihadhari na michubuko au majeraha mengine yoyote yatakayoweza kuharibu ngozi yako. Hii ni kwa sababu michubuko na majeraha hayo yatakuharibia uzuri wa ngozi yako na pia yatakuachia makovu baada ya kupona
  6. Kuwa na furaha, amani na tabasamu itakusaidia pia kuwa na ngozi nzuri, hususan ngozi ya usoni.

Dawa za nywele zinazosababisha uvimbe kwenye Kizazi kwa wanawake

Dawa za kulainisha nywele (relaxer) zimekuwa zinapendwa na wanawake wengi wa Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele na kumfanya apendeze na awe wa kuvutia.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo zinasababisha uvimbe kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa hizo ambazo huingia mwilini kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupaka.

Daktari wa Manispaa ya Ilala, Laurent Chipata alifanya utafiti na kubaini kuwa dawa za nywele na vipodozi zina kemikali ambazo husababisha uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi kikubwa na kusababisha uvimbe kwenye kizazi uitwao fibroids au leimyoma.

“Kemikali hizi hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine hata kwa harufu tu, husababisha kuzalishwa kwa wingi wa vichocheo aina ya estrogen ambavyo huchangia kuota kwa uvimbe wa fibroids,” anasema.

Dk Chipata anasema kukua kwa uvimbe kwenye kizazi hutokea katika kipindi ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma hedhi.

Utafiti wa Dk Chipata ulifanywa nchini na kujumuisha wanawake wa kada tofauti tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia na ukubwa wa tatizo hili ulibainika.

“Zipo kemikali tofauti tofauti zinazosababisha uvinbe kwenye kizazi, zipo za kwenye dawa za kilimo kama DDT na za kwenye mafuta ya ngozi kama vile mercury na hydroquionone,” anasema.

Dk Chipata anasema madhara yanayopatikana katika kemikali za vipodozi ni makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha saratani au kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya zebaki (mercury).

“Dawa za nywele zina madhara si lazima zipenye kwenye ngozi baada ya mtu kupata jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya zenyewe kwenye ngozi kutokana na mfumo wa ngozi,” anasema.

Anashauri kuwa ni vyema watu wakasoma kipodozi kimetengenezwa kwa nini kabla ya kukitumia na kuongeza kuwa ni salama zaidi kubaki na ngozi au nywele halisi badala ya kujibadilisha.

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza vipodozi vyenye kemikali kama biothionol, hexachlorophene, mercury, vinyl chloride, zirconium na bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform.

Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dk Lauren Wise na wenzake nchini Marekani na kuchapishwa kwenye jarida la afya la nchini Marekani ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya estrogen ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au vivimbe hivi hujulikana kama fibroids au myoma.

Dk Wise anasema aliwafanyia uchunguzi wanawake wanaotumia dawa za kulainisha nywele na kuangali umri walioanza kutumia dawa hizo, mara ngapi, waliungua kiasi gani na walikaa na dawa hizo kichwani kwa kipindi gani.

Aliwafuatilia wanawake 23,580 wanaotumia dawa za kulainisha nywele na baada ya kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146 waligundulika kuwa na uvimbe kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi na wengine kufanyiwa upasuaji.

Kwa nini relaxer ni hatari kwa wanawake?
Dk Wise anasema mchanganyiko ulio kenye dawa za nywele hasa zilizoandikwa “Lye Relaxer” ni sodium hydroxide wakati makopo ya dawa yaliyoandikwa “No Lye Relaxer” yana calcium hydroxide na guanidine carbonate.

Bidhaa za kulainishwa nywele zilizoandikwa ‘no lye relaxer’ zinadaiwa kusababisha majeraha kwa kiasi kidogo ukilinganisha na zile zilizoandikwa “Lye Relaxer”.

Namna nzuri ya kutunza Hips na Makalio

KUNA kitu ambacho wengi wetu huwa hawakifikirii nacho ni makalio. Makalio yetu ndiyo yanatoa shepu fulani kwa mwanamke katika vivazi na ukiyaachia ovyo yanaweza kukuletea mushkeli na kama ukiyatengeneza kama yale makalio yanayosifiwa sana na watu wa Televisheni ya Jeniffer Lopez hayawezi kufua dafu.

Wanawake wengi kwa sasa wanakwenda kuboresha makalio yao ili kuyapatia ukubwa unaostahili kwa jinsi wao wanavyopenda.

Tatizo hili halipo hapa nchini lakini wapo walionituipia swali sasa inabidi nikiri kuwa lipo sana marekani na mpasuaji wa masuala ya urembo wa Miani Dk Costantino Mendieta amethibitisha.
Katika fasihi yake mtaalam huyo amezungumzia sana utunzaji wa makalio kwa kuyagawa katika madaraja manne.

Anasema makalio daraja la kwanza ndiyo yanayotakiwa sana > Ni kama vile umechukua moyo halafu ukaugeuza chini juu haya ndiyo dizaini ambayo Marekani wanalilia sana. Watu wa huko wanajimwaga katika majumba ya upasuaji kupata shepu hiyo adimu.

Hatua hizo ni kama ifuatavyo.

1.fanya masaji na losheni zinazoimarisha na kutengeneza ngozi mwororo katika mapaja yako ukianzia chini ya makalio mara mbili kwa siku.

2.Ondoa miinuko midogo midogo isiyotakiwa ni yako kwa kuskrabu mara mbili au tatu kwa wiki ukitumia salt scrub.

3.Pamoja na matatizo ya michuchumio, ivae ili kukupa nafasi ya kutembea kwa miondoko ya twiga inayotoa nafasi nzuri kwa makalio kuwa na mvuto.

4.tafuta namna nzuri ya kuficha michirizi ya kunyooka kwa misuli ya mwili.

5.Mazoezi yatakufanya uwe mtu tofauti zaidi pandisha ngazi kwa dakika kumi au zaidi na chukua mazoezi ya kubana makalio yako na sehemu za kiuno kwa kusukuma kwa ndani na kutulia hivyo kwa sekunde tano na kujiachia na unaweza kufanya hivyo unavyotaka.

Pia unaweza kuongeza uzuri wa makalio yako kwa kuhakikisha unakula vyema na unakula inavyostahili

Jinsi ya kuchagua rangi sahihi wakati wa Kujipodoa

YAPO mambo mabalimbali katika tasnia ya urembo hasa katika vipodozi yanayopaswa kuzingatiwa katika kuboresha muonekano wa mtu.
Moja ya mambo hayo ni ujuzi na uelewa wa kutumia rangi katika kujipodoa kwani ni wanawake wachache wenye ujuzi huu.
Katika makala hii, nitakuelezea namna ya kuchanganya na kutofautisha rangi za vipodozi, lengo likiwa ni kuboresha muonekano wako.

Uchanganyaji wa rangi za vipodozi ni muhimu sana kwani katika kujipodoa, rangi zote za vipodozi unavyopaka zinatakiwa zioane ili kuleta muonekano ulio sawa na wa kueleweka.

Kwanza kabisa unatakiwa uwe makini katika kuoanisha rangi za vipodozi pamoja na rangi ya ngozi yako, hivyo katika hili unatakiwa kuwa na ujuzi maalumu ili usije ukafanya makosa na kuharibu muonekano wako.

Pia inabidi ufahamu hatua za upakaji vipodozi ili usije ukafanya vipodozi vingine visionekane katika uso wako.

Namna ya kuoanisha na kutofautisha rangi

Siku zote vipodozi vyako lazima viendane na mavazi yako ili kuleta maana zaidi kwa mfano, mara nyingi rangi ya mdomo ‘lipstick’ huendana na vazi lako wakati shedo ‘eye shadow’ zinatofautiana.

Kwa nguo za pinki

Katika mavazi haya, unatakiwa kupaka rangi ya mdomo yenye rangi ya pinki ambayo itaendana sawasawa na mavazi yako huku ukichanganya na shedo ‘eyeshadow’, inaweza kuwa ya rangi ya bluu ili kuitofautisha na mavazi yako, hapo utakuwa sawa katika kanuni za urembo.

Vazi la kijani

katika vazi hili unatakiwa kupaka rangi ya mdomo yenye rangi ya kahawia huku ukichanganya na shedo ya rangi ya kijani au kahawia iliyoingiliana na pinki au rangi ya machungwa.

Kwa vazi la njano au kahawia

Katika vazi hili unatakiwa kupaka ‘lipstick’ ya rangi ya kahawia iliyokolea, kwa upande wa shedo waweza kupaka ya rangi ya dhahabu.

Kwa vazi la bluu

Katika vazi hili unatakiwa kupaka ‘lipstick’ yenye rangi ya pinki huku ukipaka shedo ya rangi ya bluu kwa mtindo huu utakuwa mwenye kuvutia siku zote.

Madhara ya Kuvaa/ Kuweka Kope Za Bandia

Mapokeo ya urembo wa kisasa katika nchi zinazoendelea ni sehemu ya mchango wa urembo na mvuto tunaouona kwa baadhi ya wasichana na wanawake ambao kwa hakika unaleta hamasa ya kuangalia.
Hata hivyo, urembo huu huja na hatari zake ambazo wengi wanaweza kuzichukulia poa kwa kuwa hazitokei kwa haraka ama katika muda unaoweza kutolewa ushahidi kwa sasa.

Moja kati ya urembo unaofanywa na wanawake wengi wa kisasa ni kuweka kope za bandia juu ya kope halisi, kweli wengi wanakuwa na mvuto wa aina yake wakikuangalia hasa mtoto wa kiume. Lakini hatari inayotokana na urembo huo ni kubwa zaidi ya matokeo ya muda mfupi.

Wataalam wanaeleza kuwa kope za bandia ambazo hugundishwa kwa kutumia gundi ya nywele inayotumika kugundisha nywele bandia kwa wenye vipara inaweza kuwa chanzo cha upofu wa mtumiaji.

Gundi hiyo hupukutika taratibu sana kiasi cha kutoshtukiwa na kuelekea kwenye mboni ya jicho ambayo ndio moyo wa ‘kuona’. Endapo mtumiaji ataendelea kwa muda mrefu kutumia kope hizi bandia anaweza kujikuta anakuwa na tatizo la kuona ama hata upofu wa haraka katika maisha yake ya baadae.

Hata hivyo, hatari kubwa imeelekezwa kwa maduka ama vibanda vinatumia vifaa vya bei nafuu ikiwemo gundi inayotumika. Ukwepaji wa gharama ama kutokuwa na uwezo wa kutumia gharama kubwa kunamuingiza mrembo kwenye hatari zaidi.

Kuwa mwangalifu, urembo usiwe chanzo cha kuhatarisha afya yako. Kumbuka Afya ni uhai wa mwili wako.

Uvaaji wa Tai kulingana na Umbo lako

Kuna mambo mengi ya kufanya ili tuwe watu wa kuvutia kila wakati.Mpangilio wa mavazi hufanya mtu kuonekana maridadi. Kama wewe ni mvaaji wa tai unapovaa unazingatia mambo yapi? Na je unafunga tai yako kwa namna inayokubalika?

Wengine huwa hawafahamu jinsi ya kufunga tai na hivyo kuleta mushkeri wakati wa kuvaa tai na kusababisha tai kukaa upande. Unapoamua kuvaa tai na shati ambalo halijanyooshwa ambalo linakuwa kwenye mikunjo au kuvaa tai na ndala unakuwa umeua maananzima na kulivunjia heshima vazi hili.

Tai ni vazi lawatu walio maridadi kama huwezi kuwa maridadi basi vazi hili halikufai kabisa.
Unapovaa taa unatakiwa kuzingatia aina ya umbo lako kama wewe ni mnene vaa tai inayoendana na mtu mnene na kama wewe ni mwembamba basi vaa tai inayoendana na mtu mwembamba.

Kuna wengine huvaa tai zinazofika magotini na kuwa kichekesho anapopita mtaani
Tai ni vazi ambalo huongeza heshima na hadhi ya mvaaji cha muhimu ni jinsi gani unavaa tai yako na ikiwezekana jaribu kumechisha tai na suruali kwa vile ili tai upendeze ni laima iendane na nguo unayovaa.

Ni vyema ukahakikisha kuwa unakuwa na tai zenye rangi tofauti ambazo zitaendana na nguo unazovaa.

Namna nzuri ya kuhudumia nywele zako za asili kirahisi

Kwa wale ambao tuna nywele asilia (natural hair), tayari tunafahamu changamoto kadhaa tunazokumbana nazo. Kwa wale mnaofikiria kuanza kuwa na nywele asilia, karibuni sana tuendelee kujuzana namna ya kutunza nywele zetu kama tulivyopewa na Mungu.

Katika mada ya leo, nitakwenda kuzungumzia vitu vya kuzingatia ili kuikuza nywele yako asilia kwa haraka zaidi. Je,unazifahamu nywele zako vizuri?Una nywele za aina gani? Zina tabia gani? Zinataka nini?

Zifuatazo ndizo njia ya kuzihudumia nywele zako;

1. Kuzikubali kama zilivyo na kuzipenda.

Utasikia ..hiki kipilipili changu ni steelwire ya kimataifa, ..hakitikisiki hata upepo wa dunia yote ungevumia pande hizi. Mwingine oh..nywele zangu kama miti ya mibuyu kichwani…hazishikiki.T atizo ni kwamba hamjafahamiana vizuri yani wewe na nywele zako. Hata mimi niligombana nazo sana huko nyuma kabla ya kuzielewa vizuri. Jenga mahusiano mazuri tu na nywele zako,zielewe,ukifikia hapo utaanza kuzipatia hata hazitakusumbua.

2. Usafi wa ngozi ya nywele na nywele zenyewe.

Nywele zenye afya huanzia kwenye ngozi safi ya nywele.Nafahamu unataka nywele zako zisidumae kwa hiyo zioshe vizuri.Wakati uliopita nilizungumzia kuziosha kwa product zilizo rafiki( ‘friendly’) .Ngozi safi ya nywele itasababisha nywele kupata njia ya kujitokeza nje kwa urahisi.Unapoziacha chafu,ule uchafu unaziba matundu ya nywele zako na kuzuia njia,kama ambavyo matundu ya uso yakiziba unapata machunusi maana uchafu unajaa basi kwa nywele hazitakua vizuri.

3. Linda unyevu wa nywele zako

Kila mtu akisikia kiu hunywa maji.Nywele zako zinahitaji kulindwa zisisikie kiu.Unapoziosha,yale mafuta asilia ya kuzilinda huondoka na uchafu.Nywele inabaki ikiwa na udhaifu fulani maana haiwezi hata kushikilia hayo maji yaliyopo vizuri,na zikikauka zinakua kavu sana.Ni vizuri kabla hazijakauka vizuri,ukazi-’condition’.Kwa nywele ambazo ni nyepesi na chache,pia kuna product za kuzisaidia ziweze kutunza vizuri unyevu na hivyo kuwa na afya nzuri.

4. Zifahamu nywele zako

Yani hapa ndo shule ilipolalia kabisaa maana ukizijua tu basi utazihudumia kwa usahihi. Unatakiwa kuangalia namna gani nywele zako zinanyonya unyevu .Unajuaje?

Chukua kikombe,kijaze maji safi.Ukipata glass itakuwa vizuri zaidi.

Chomoa unywele mmoja kichwani,hakikisha unatoka na kale kamzizi kake keupe keupe hivi.

Tumbukiza unywele wako kwenye glass yako ya maji hakikisha imeingia yote.Kama ikizama hapo hapo na hainyanyuki tena,basi nywele zako zinanyonya unyevu kwa haraka kabisa.Kama inachukua muda kuzama,au haizami kabisa,nywele zako zinanyonya unyevu taratibu au zinanyonya kwa shida.

(Wala usihofu,zipo namna ya kuzifanya zinyonye unyevu kwa haraka,tutajuzana.)Ni kwamba ‘cuticle’ zake zimefunga haswa,ndio maana unyevu au maji haviingii kwa haraka.

Kwa hiyo ukifanya ‘deep conditioner’ kwa kutumia joto kama la drier lakini uwe moto mdogo sana au ufanye ‘hot oil treatment’ itakusaidia ‘cuticle’kufunguka na unyevu kupita.

Mbadala,unaweza baada ya kuosha suuza na maji ya vuguvugu halafu weka mafuta ya kimiminika.Inasaidia sana.

Mimi nina aina gani?..Nina nywele zinazonyonya unyevu haraka.

5. Mafuta ya Kupaka kichwani.

Ni ya muhimu mnoo!.Nimefanya utafiti wa kina nimeona mafuta ya nazi yanaweka afya nzuri kwa nywele aina nyingi hivyo na mimi nikaanza kuyatumia. Kwangu mimi,mafuta ya nazi ya kutengeneza mwenyewe yamenikubali sana. Japo huwa nanunua pia mafuta kama ya olive(extra virgin) na ya tea tree.

6. Kuzichambua vizuri kabla ya kuchana.

Uwe mkarimu na mwenye subira kwa nywele zako. Mimi zikijifunga huwa nazichambua kwa mikono taratibu wakati mwingine nazilowesha na maji kwa mbali halafu nachana kwa chanuo lenye mapana sio ambalo reli zake zimebanana. sio kitana. Chanuo kubwa(wide toothed comb).

7. Usizisumbue mara kwa mara na usuke mitindo ya kuzitunza zikue.

Kama unataka zikue haraka, usizisumbue sana. Unaweza ukasuka mitindo mizuri tu ukakaa nazo wiki nzima au kadri zitakavyodumu. Au upunguze kuzichana mara kwa mara lakini utafute siku kama wikiendi ukae uzichambue taratibu na vidole kuondoa mafundo. Kuchana mara kwa mara zinapukutika,zinaanguka. Zitakua lakini sio kwa kasi ya kama ukizisuka ukaziacha kwa muda.

8. Punguza matumizi ya vitu vya moto kwenye nywele zako kama pasi ya nywele na vingine vya hivyo.

Mimi dryer la nywele situmii zaidi ya mara mbili kwa mwezi. Mara nyingi naziacha zikauke na hewa hata kama nimezifunga rollers natoa kesho baada ya masaa 24

Jinsi ya Kuvaa hereni kwa Mpangilio kuongeza Mvuto wako

HERENI ni pambo linavoliwa masikioni na kwa kiasi kikubwa linachangia kuongeza mvuto na muonekano mzuri. Kuna aina nyingi za hereni katika tamaduni mbalimbali. Zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia vito vya thamani kama vile Dhahabu, Almasi, Shaba au Kopa.

Vilevile zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia malighafi za asili kama vile ubao, vifuu vya nazi, mfupa kioo na shanga ambazo zimekuwa zikivaliwa sana na wanawake wa kimasai. Hereni zilizotengenezwa kwa shanga zimekuwa zikiwavutia watu wengi kuvaa kutokana na nakshi zake za asili.

Mara nyingi uvaaji wa hereni unatakiwa kuzingatia aina ya nguo uliyovaa, hapo unatakiwa kucheza na rangi. Mpangilio wako wa nguo na hereni hata na viatu utakufanya uonekane maridadi muda wote.

Unapotoka kwenda katika shughuli zako, au uwapo nyumbani basi zingatia uvaaji wa hereni na nguo. Uvaaji usiozingatia mpangilio wa rangi na hereni zako huondoa ladha ya urembo na si rahisi kwa mtu mwingine kugundua umependeza.

Licha ya kuwa hapo awali hareni zilikuwa zikivaliwa na wanawake pekee lakini miaka ya hivi karibuni tunaona urembo huu unaanza kuwavutia baadhi ya wanaume hususan vijana wa mjini.

Kutokana na hilo kuna hereni ambazo zimetengenezwa maalum kwa kuvaliwa na wanaume, hizi huwa za kubana na huwa na umbo dogo ukilinganisha zile zinazopendwa kuvaliwa na wanawake.

Angalizo: Epuka kuvaa hereni zaidi ya moja katika tundu la sikio kwani kufanya hivyo kunaweza kupelekea ukubwa wa tundu kuongezeka na hatimaye nyama ya sikio kuchanika. Hereni nzito sana nazo huchangia kutokea kwa tatizo hili.

Faida za kuoga maji ya Baridi

Watu wengi hupenda kuogea maji ya moto, hii ni kutokana na kuogopa baridi au sababu za kimazoea tu. Ingawa mara nyingi umekuwa ukisisitiziwa kuwa maji moto yana manufaa mengi, lakini hata maji ya baridi nayo yana manufaa yake.

Je uko tayari kuongeza maarifa au hata kubadili mtazamo wako? Karibu nikushirikishe faida za kuogea maji ya baridi.

Huongeza utayari katika mwili.

Maji ya baridi hukufanya uchangamke, hili ni tofauti na maji ya moto. Mara nyingi mtu anapoogea maji ya baridi hasa baada ya kuamka humfanya awe katika hali nzuri ya kuwa tayari kuendelea na majukumu yake.

Kumbuka hata wakati wa kuogea maji baridi kasi ya upumuaji hubadilika na kukufanya kuongeza kiasi cha oksijeni kinachoingia mwilini.

Hulainisha ngozi na nywele

Maji moto huchubua ngozi na nywele, hasa kwa kuondoa mafuta laini yanayolinda ngozi na nywele na kuvifanya viwe vikavu sana.

Kwa kuogea maji ya baridi, ngozi na nywele zako havitapaushwa bali vitasafiwa na kuachwa katika hali nzuri ya kupendeza.

Huboresha kinga mwili

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Thrombosis Research Institute, ulibainisha kuwa watu wanaoogea maji ya baridi wanaongeza uzalishaji wa seli nyeupe za damu.

Utafiti huu unaeleza kuwa kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha metaboli mwili unapojaribu kujipasha moto, ndipo seli hizi nyeupe ambazo hupambana na maradhi zinapozalishwa.

Huhamasisha kupunguza uzito

Kupunguza uzito? Ndiyo kupunguza uzito. Baada ya binadamu kula vyakula, kiasi fulani huhifadhiwa mwilini kama mafuta. Baadhi ya mafuta haya huyeyushwa na kutumiwa kuupasha mwili joto.

Hivyo kuogea maji ya baridi kutawezesha aina fulani ya mafuta kuyeyushwa ili kuzalisha joto mwilini, jambo ambalo litapelekea kupungua kwa uzito.

Huchangia katika afya ya misuli

Wanamichezo wanafahamu kuwa kuogea maji baridi baada ya michezo au mazoezi huwafanya wajisikie vizuri mapema. Hili ni kutokana na maji baridi kuhamasisha mzunguko wa damu ambao huiwezesha misuli kujijenga tena upya vyema.

Huondoa msongo wa mawazo

Utafiti uliofanyika kwenye chuo cha tiba Virginia, ulibaini kuwa kuogea maji baridi huzalisha kemikali ya noradrenaline ambayo husaidia kukabili msongo wa mawazo.

Hukusaidia kulala vyema

Je umeshawahi kuogea maji baridi ukiwa umechoka sana au umefanya kazi ngumu? Kama umeshawahi kuogea maji baridi ni wazi kuwa ulijisikia vizuri na ukalala vizuri pia.

Hili ni tofauti na maji ya moto kwani badala ya kukupooza na kukufanya ulale vyema yatakufanya uchemke na kuchoka zaidi.

Naamini umepata maarifa juu ya faida za kuogea maji baridi. Naamini sasa hakuna haja ya kuongeza foleni za maji jikoni wakati unaweza kuogea maji ya baridi na ukapata manufaa yaliyoelezwa hapa.

Shopping Cart
2
    2
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About