Ikiwa leo ni tarehe **1/12 huwezi amini kuwa hakuna tarehe 1 nyingine tutakayoiona ya mwaka huu hivyo sichelei kusema kuwa mwaka umeisha .Lakini mwaka unaishaje??? pengine hili ndilo swali gumu na la muhimu la kujiuliza .Je, Mwaka unaisha ukiwa umefanya nini cha kujipongeza??? .Je mwaka unakaribia kuisha maarifa yako yakiwa yameongozeka kwa kiasi gani???.Haya ni maswali muhimu sana unavyooanza kufikiria juu ya sherehe za mwisho wa mwaka.
Watu waliopiga hatua katika fikra (waliofanikiwa) huu ndio mwezi wao wa kurudi kwenye malengo waliyokuwa wameweka na kuona ni kwa njinsi gani wametembea na mambo waliyokuwa wameyapanga mwaka uliopita .
Leo nataka nikuekeze mambo muhimu ya kufanya mwezi huu pamoja na kuwa unawaza sikukuu na kusafiri kwenda kwenu .Mambo haya unaweza kuwa hujawahi kufanya lakini ni muhimu sana ukafanya mwaka huu ili mwakani tuone mabadiliko .Mambo hayo ni pamoja na ;
1.Fanya Tathimini (Evaluation)
Tathimini ni kipimo kinachoonesha kushindwa kwako na kufanikiwa kwako .Mwezi huu ni mwezi wa kukaa chini na kurejea kwenye malengo na mikakati uliyokuwa umejiwekea na kuona ni kwa jinsi gani umefanikiwa .Ainisha mambo uliyofanikiwa na ambayo hujafanikiwa .Kwa yale uliyofanikiwa jipongeze kwa kufanikiwa kwa yale ambayo hujafanikiwa jiulize kwanini hayajafanikiwa ili yakupe mbinu na hatua mpya mwaka ujao.
Andika kwa mtindo huu;
SEHEMU A:MAMBO NILIYOFANIKIWA HUU
-Mwaka huu nilifanikiwa kuwapata marafiki wazuri wanaounga mkono maono yangu
-Mwaka huu nilifanikiwa kuanzisha biashara ya genge
-Mwaka huu nilifanikiwa kusoma vitabu viwili
*Jitihidi sana kujipongeza kwa yale uliyofanikiwa na hii ni tabia ya watu waliofanikiwa .Usione umefanya madogo lahasha.*
SEHEMU B:MAMBO AMBAYO SIKUFANIKIWA mwaka huu
-Sikufanikiwa kuhudhuria semina hata moja ya ujasiriamali
-Sikufanikiwa kuboresha ofisi
Kwa yale ambayo hukufanikiwa jiulize kwanini hukufanikisha utagundua wewe ndiye sababu kubwa ya kutoyafanikisha .
2.Anza kuandaa malengo ya mwaka ujao (GOAL SETTING)
_Pasipo maono, watu huacha kujizuia_
~(Biblia)
Ndiyo bila malengo hutafika na utafanya kila kitu bila mpangilio .Huu ndio mwezi kwako ambao unapaswa kuandaa malengo ya mwaka ujao haijalishi hukuwahi kuweka malengo toka unazaliwa .Najua malengo yako yalikuwa yanakaa kichwani mwaka huu amua kuandika kwenye notebook Nzuri .Andika kwa ujasiri mkubwa sana .Malengo yako yafuate kanuni za malengo(yapimike,yawe na ukomo,yawe mahususi na yakufikika ).
Andika kwa mfano huu;
-Kufikia Mei nitakuwa nimefuga kuku watatu hata kama nyumba yangu ni ndogo .
-Kufikia Agosti nitakuwa nimehudhuria semina 2 za ujasiriamali
Ukiandika kwa mfumo huo itakusaidia kuyafikia malengo yako maana yamefuata kanuni za malengo.
3. Andaa Bajeti ya mwaka (Budgeting)
Hii ni sehemu ambayo inaleta shida sana .Na hii ni kwa sababu hata wazazi wetu wametulea bila kutufundisha bajeti.Masomo ya darasani wengi hatufundishwi kuishi kwa bajeti .Lakini Tusilaumu sana kutofundishwa maana lawama ni tabia ya kimaskini tuamue mwakani 2017 kuishi na kutembea na bajeti
Mara nyingi tukiulizwa hela zetu zinaenda wapi huwa hatuna majibu sahihi .Hii ni kwasababu hatuna bajeti .Kwanini bajeti??? .Bajeti hutusaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na yaliyo nje ya bajeti .Bila bajeti sehemu ya kutembea kwa mguu utapanda bodaboda .Bila bajeti utanunua simu ya laki saba wakati unasema huna mtaji wa laki sita.Bajeti itaamua uchangie harusi na kitchen party ngapi kwa mwaka.
Ndiyo lazima tubadilike hata mimi nimeamua hivyo mwaka ujao.Kama una familia kaa na mke wako tengeneza bajeti ya mwaka.Kuna vitu vinaweza kujitokeza njiani na hivyo kumbuka kuweka dharura .
Bajeti itatoa picha ya nini kinahitajika mwaka ujao na unahitaji kuwekeza nguvu kiasi gani za kwenda na bajeti hiyo.