Sala za Ibada

SALA MUHIMU ZA MKRISTO ZA KILA SIKU ASUBUHI

SALA YA ASUBUHI

Tuusifu Utatu Mtakatifu wa Mungu Mwenyezi, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, milele na milele, Amina.

Ee Utatu Mtakatifu wa Mwenyezi Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, nasadiki kuwa upo hapa na mahali pote. Ee Mungu wangu, umeniumba, umenikomboa, umenifanya mkristo, umenizidishia neema zako hapa duniani, umenitayarishia makao yangu mbinguni, umenijalia na siku hii nikutumikie. Ee Mungu wangu! Nakuabudu, nakushukuru, nakuomba toba, nakupenda! Ee Mungu wangu, nakutolea roho yangu, na mawazo, na maneno, na kazi, na furaha, na mateso yangu: uyapokee unipe neema yako nisikutende leo dhambi!

Majitoleo ya Asubuhi

Ee Baba yetu Mungu Mkuu, Umenilinda usiku huu, Ninakushukuru kwa moyo, Ee Baba, Mwana na Roho, Nilinde tena siku hii, Niache dhambi nikutii, Naomba sana Baba wee, Baraka yako nipokee, Bikira safi ee Maria, Nisipotee unisimamie, Mlinzi Mkuu Malaika wee, Kwa Mungu wetu niombee, Nitake nitende mema tu, Na mwisho nije kwake juu, Amina.

Kuweka nia njema

Kumheshimu Mungu wangu, Namtolea roho yangu, Nifanye kazi nipumzike, Amri zake tu nishike, Wazo neno tendo lote, Namtolea Mungu pote, Roho, mwili chote changu, pendo na uzima wangu, Mungu wangu nitampenda, Wala dhambi sitatenda, Jina lako nasifia, Utakalo hutimia, Kwa utii navumilia, Teso na matata pia, Nipe Bwana neema zako, Niongezee sifa yako, Amina.

Majitoleo

Ee Yesu, kupitia mikono safi ya Bikira Maria, na kwa maungano na sadaka yako kuu, ninakutolea sala, matendo, kazi, masumbuko, na furaha zangu zote za siku hii ya leo, kwa ajili ya nia za Moyo wako Mtakatifu, Ee Yesu ufalme wako utufikie!

Baba Yetu….
Salamu Maria, …..
Nasadiki …….
Amri za Mungu ……
Amri za Kanisa ……

Sala ya Malaika wa Bwana

Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria, naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Salamu Maria,….

Ndimi Mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena. Salamu Maria, ……
Neno wa Bwana akatwaa Mwili, akakaa kwetu. Salamu Maria, …..

Utuombee, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, tujaliwe ahadi za Kristo.

Tuombe:

Tunakuomba ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika, kwamba, Kristo Mwanao amejifanya mtu: kwa mateso na Msalaba wake, utufikishe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu, Amina.

Sala kwa Malaika Mlinzi

Ee Malaika wangu, uliyewekwa na Mungu mwema unilinde, naomba uniongoze leo, unitunze, unisimamie, unishauri. Amina.

Sala kwa wenye kuzimia

Ee Yesu mwenye huruma, mpenda roho za watu, nakuomba kwa ajili ya kuzimia kwa Moyo wako Mtakatifu, na kwa ajili ya Mama Yako asiye na doa, uwatakase kwa damu yako, watu wote wenye dhambi wanaokufa sasa, na watakaokufa leo.
Moyo wa Yesu uliozomia, uwahurumie watu wanaokufa X3.

Sala kwa Mtakatifu Yosef

Ee Yosef mwenye heri, tunakimbilia kwako, katika masumbuko yetu, na kishaomba shime ya Mchumba wako Mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda nayo Bikira Mtakatifu, Mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya tunza ya Baba, uliyomtunza nayo Mtoto Yesu, tunakuomba sana, utuangalie kwa wema, sisi tuliokuwa fungu lake Yesu Kristo, tuliokombolewa kwa damu yake, utusimamie katika masumbuko yetu, kwa enzi na shime yako.
Ee Mlinzi amini wa Jamaa Takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristo, ee Baba uliyetupenda mno, utuepusha na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji,utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwokoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi, ulikinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote, mtunze daima kila mmoja wetu, tupate mfano wako, tusaidie kwa msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupokelewa mbinguni makao ya raha milele. Amina

Sala kwa Mtakatifu Yuda Thadei

(Sala hii inaweza kusaliwa kila siku au kama Novena ya siku tisa mfululizo kuomba kitu kilekile)
Mtakatifu Yuda Tadei,/ Mtume Mtakatifu,/ Mtumishi mwaminifu na rafiki wa Yesu./ Jina la yule msaliti aliyemwuza Yesu/ limewafanya wengi wakusahau./ Walakini Kanisa zima linakuheshimu/ na kukuomba kama Msaidizi katika mashaka makubwa,/ na katika mambo yasiyo na matumaini tena./
Uniombee mimi mnyonge./ Ninaomba utumie uwezo ule uliojaliwa/ wa kuleta upesi msaada kwa watu walioukosa./ Unisaidie sasa katika mahitaji yangu,/ ili nipate kitulizo na msaada wa mbinguni/ katika lazima zangu,/ masumbuko na mateso,/ hasa/ (taja shida yako)./ Pia ili niweze kumsifu Mungu nawe na wateule wote milele./
Mtakatifu Yuda Tadei,/ utuombee,/ na uwaombee watu wote wanaokuheshimu na kukuomba msaada./
Baba yetu……. Salamu Maria ……… Atukuzwe ……….

Sala ya Medali ya Mwujiza

Ee Bikira Maria uliyekingiwa dhambi ya asili, utuombee sisi wenye kukimbilia kwako, uwaombee na wale wasioukimbilia kwako, hasa maadui wa Kanisa Takatifu, na wale waliokabidhiwa kwako. Amina.

Majitoleo kwa Bikira Maria

(Sala iliyotungwa na Mtk. Aloisi)
Bibi yangu mtukufu Maria, nakuwekea amana ya roho yangu na mwili wangu, nikikuomba uipokee amana yangu, kuitunzia ulinzi mwema ulinzi bora, ninakuaminia na kila neno langu, matumaini na kitulizo na kisongo chote, na masumbuko na uzima na ukomo wa uzima wangu: nitakayo ndiyo unifanyizie kwa maombezi na stahili zako, ili mambo yangu yote yapate kuongoka, yakiwa na kufuata mapenzi yako, pamoja na mapenzi ya Mwanao. Amina.

ROZARI YA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Tumia tasbihi ya kawaida yenye chembe ndogo 53.

Kwenye Msalaba Sali:

“Ee Yesu tupe moyo wako kama amana ya upendo wako na kimbilio letu, ili tupate pumziko salama wakati wa maisha yetu na faraja tamu saa ya kufa kwetu”.
Baba Yetu ……..
Salamu Maria ……. (mara tatu)
Nasadiki ………..

Kwenye chembe kubwa Sali (Badala ya ‘Baba Yetu’):

“Ninakuabudu, ninakutukuza na ninakupenda, Ee Moyo wa Yesu wangu mpenzi, uliopenywa na huzuni nyingi kwa ajili ya dhambi, ambazo zimekuwa zikitendwa hata leo, dhidi ya Sakramenti Takatifu sana ya Altare. Ninakutolea hapo kwa kuridhika, moyo wa Mama yako mpendevu, na mastahili ya watakatifu. Amina”.

Kwenye chembe ndogo sali (Badala ya ‘Salamu Maria’):

“Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, uwakao mapendo kwetu, washa nyoyo zetu kwa mapendo yako”

Novena ya Noeli

Novena ya Noeli (maarufu kama novena ya Mt. Andrea)

Husaliwa kuanzia tar 30 Nov hadi usiku wa Noeli, tar 24 Disemba. Inajulikana kama novena ya Mt. Andrea kwa sababu novena hii huanza kusaliwa katika siku ya kumbukumbu ya Mt. Andrea Mtume.

“IHESHIMIWE, NA IBARIKIWE, SAA ILE NA WAKATI ULE, AMBAO MWANA WA MUNGU, ALIZALIWA NA BIKIRA MBARIKIWA SANA, USIKU WA MANANE, KULE BETHLEHEM, WAKATI WA BARIDI KALI.
WAKATI HUO, UPENDE E MUNGU WANGU, KUSIKIA MAOMBI YANGU, NA KUNIJALIA YALE NINAYOYAOMBA KWAKO, KWA NJIA YA MASTAHILI YA MWOKOZI WETU YESU KRISTO, NA YA MAMA YAKE MBARIKIWA. AMINA. (Sali mara 15 kwa siku).

Inasadikika kuwa chochote uombacho kwa imani kwa sala hii utakipata mradi kipatane na mapenzi ya Mungu. Sali na watoto/ familia kuwatafakarisha na kuwaongezea matazamio juu ya sikukuu ya Noeli.

Isambaze sala hii kwa wengine.

LITANIA YA KUWAOMBEA MAPADRE WOTE 1

Kwa ajili ya Baba Mtakatifu wetu ..(N); Bwana, umpe moyo wako wa uchungaji mwema
Kwa ajili ya warithi wa Mitume; Bwana, uwape wawe na uangalifu uliojaa upendo kwa mapadre wao
Kwa ajili ya Maaskofu wako waliochaguliwa na Roho Mtakatifu; Bwana, uwabakishe karibu na kondoo wako
Kwa ajili ya wachungaji wako; Bwana, uwafundishe kutumikia kuliko kutafuta kutumikiwa
Kwa ajili ya waungamishi na washauri wa kiroho; Bwana, uwafanye kuwa vyombo visikivu kwa Roho wako Mtakatifu
Kwa ajili ya mapadre wanaotangaza neno lako; Bwana, uwawezeshe kushirikisha Roho wako na Uzima wako
Kwa ajili ya mapadre wanaosaidia utume wa walei; Bwana, uwatie moyo wa kuwa mifano bora
Kwa ajili ya mapadre wanaofanya kazi na vijana; Bwana, uwajalie wawakabidhi vijana kwako
Kwa ajili ya mapadre wanaofanya kazi kati ya watu fukara; Bwana, uwajalie wakuone na wakutumikie kupitia hao
Kwa ajili ya mapadre wanaoangalia wagonjwa; Bwana, uwajalie wawafundishe thamani ya mateso
Kwa ajili ya mapadre fukara; – Uwasaidie ee Bwana
Kwa ajili ya mapade wagonjwa; – Uwaponye ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wazee; – Uwapatie tumaini la raha ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye huzuni na walioumizwa; -Uwafariji ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wanaohangaishwa na wale wanaosumbuliwa; – Uwape amani yako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wanaodharauliwa na wanaonyanyaswa; – Uwatetee ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre waliokata tamaa; – Uwatie moyo ee Bwana
Kwa ajili ya wale wanaosomea upadre; – Uwape udumifu ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; – Uwape uaminifu kwako na kwa Kanisa lako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; – Uwajalie utii na upendo kwa Baba Mtakatifu na kwa maaskofu wao ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; – Uwajalie waishi katika umoja na maaskofu wao ee Bwana
Tunawaombea mapadre wote; – Wawe wamoja kama Wewe na Baba mlivyo wamoja ee Bwana
Tunawaombea mapadre wote; – Waishi na kuendeleza haki yako ee Bwana
Tunawaombea mapadre wote; – Washirikiane katika umoja wa ukuhani wako ee Bwana
Tunawaombea mapadre wote, wakiwa wamejawa na uwepo wako; – Waishi maisha yao ya useja kwa furaha ee Bwana
Tunawaombea mapadre wote; – Wajalie ukamilifu wa Roho wako na uwageuze wafanane nawe ee Bwana
Kwa namna ya pekee, ninawaombea mapadre wale ambao kwa njia yao nimepokea neema zako. Ninamwombea padre aliyenibatiza na wale walioniondolea dhambi zangu, wakinipatanisha na Wewe na Kanisa lako.
Ninawaombea mapadre ambao nimeshiriki Misa walizoadhimisha, na walionipa Mwili wako kama chakula. Ninawaombea mapadre walionishirikisha Neno lako, na wale walionisaidia na kuniongoza kwako. Amina.

SALA YA KUANGUKA MIGUUNI PA BWANA YESU KATIKA EKARISTI

Ee Yesu Mfungwa wa Upendo wa Mungu,/ ninapofikiri Upendo wako na jinsi ulivyojitolea kwa ajili yangu,/ nashindwa kuelewa./ Unaficha Ukuu wako usiofahamika/ na kujidhihirisha kwa ajili yangu mimi mnyonge./ Ee Mfalme wa utukufu,/ unaficha uzuri wako,/ lakini jicho la moyo wangu/ linapenya pazia na kuona Majeshi ya Malaika/ wakikuimbia kwa heshima bila kukoma/ na nguvu zote mbinguni zikikusifu bila mwisho zikisema:/ “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu..”/

Ni nani awezaye kufahamu Upendo wako/ na huruma yako isiyo na kipimo kwa ajili yetu!/ Ee Mfungwa wa Upendo,/ nafungia moyo wangu masikini/ kwenye Tabarnakulo hii/ ili niweze kukuabudu usiku na mchana bila mwisho./ Najua hakuna kizuizi/ na hata kama naonekana kukaa mbali,/ lakini moyo wangu u pamoja nawe/ katika ibada hii./ Hakuna kinachoweza kuzuia upendo wangu kwako./ Kwangu hakuna kizuizi chochote./

Ee Utatu Mtakatifu,/ Mungu Mmoja usiyegawanyika,/ utukuzwe kwa zawadi yako hii kuu/ na agano hili la huruma!/

Nakuabudu,/ Bwana na Muumba uliyefichika katika Sakramenti Takatifu!/ Ee Bwana,/ nakuabudu kwa kazi zote za mikono yako/ zinazonifunulia Hekima yako kuu,/ Wema wako na Huruma yako kuu./ Uzuri uliousambaza hapa/ Uzuri ulio nao Wewe mwenyewe/ ambaye U Uzuri usioelezeka;/ na ingawaje umejificha na kusitiri uzuri wako,/ jicho langu,/ kwa mwanga wa imani linafika kwako,/ na roho yangu inapata kumtambua Muumba wake/ aliye Uzuri usiopimika,/ ulio juu ya kila uzuri,/ na moyo wangu unazama kabisa katika sala ya kukuabudu./

Bwana wangu na Muumba wangu,/ wema wako wanitia moyo wa kuongea nawe,/ Huruma yako huondoa kiambaza/ kitenganishacho Muumba na kiumbe./ Furaha ya moyo wangu,/ ee Mungu, ni kuongea na Wewe./ Yote ambayo moyo wangu unayatamni nayapata kwako./ Hapa ndipo mwanga wako unaponiangaza akili yangu/ na kuiwezesha kukujua Wewe zaidi na zaidi/ – ndipo mikondo ya neema inapoutiririkia moyo wangu,/ ndipo roho yangu inapochota uzima wa milele./ Ee Bwana na Muumba wangu,/ licha ya mapaji yote haya,/ unajitoa mwenyewe kwangu,/ ili uweze kujiunganisha na kiumbe dhaifu na maskini./

Ee Kristu,/ nafurahi sana nionapo kwamba unapendwa/ na kwamba sifa na utukufu wako vinaongezwa/ hasa ya Huruma yako./ Ee Kristu,/ sitaacha kamwe kuutukuza wema wako na huruma yako,/ hadi dakika ya mwisho ya maisha yangu./ Kwa kila tone la damu yangu/ na kwa kila pigo la moyo wangu/ naitukuza Huruma yako./ Natamani kugeuzwa kabisa/ na kuwa utenzi wa utukufu wako./ Naomba siku ya kufa kwangu/ popote nitakapokuwa nimelala,/ pigo la mwisho la moyo wangu/ liwe utenzi mpendevu/ usifuo Huruma yako isiyo na kipimo./ Amina

(Na Mt. Faustina Kowalska).

SALA YA KUUABUDU MOYO MTAKATIFU WA YESU KATIKA EKARISTI TAKATIFU

Kwa nguvu zangu zote za moyo wangu/ ninakuabudu ee Moyo Mtakatifu/ na Mwabudiwa sana,/ Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristu/ ambao ninataka kumpenda/ na kukusalimu kwa usikivu unaoendelea./ Kamwe nisikuudhi tena/ kwa sababu Wewe ni Mwema sana;/ Ee Mwema sana./ Ee Moyo Mtakatifu sana/ ninakupenda/ na ninataka kukupenda zaidi ya vitu vyote,/ kwa nguvu zangu zote/ na kwa uwezo wangu wote,/ ninatamani kuwa mali yako/ Wewe uliyejitoa Msalabani kwa ajili yangu/ kwa mateso makali./ Unionee huruma na udhaifu wangu/ na usiniruhusu kupotea./

Ninajitoa kabisa kwako/ ee moyo wa mapendo,/ kwa makusudi kuwa utu wangu,/ maisha na mateso yangu/ yalipie kukupenda,/ kukuheshimu/ na kukutukuza Wewe sasa na milele./ Ninakupenda ee Moyo Mwabudiwa wa Mwokozi wangu,/ ninakuomba kwako/ uamuru moyo wangu na kila kitu ndani yangu/ kikutukuze sasa na milele./ Amina.

(Na Mt Margareta Maria Alakoki)

Kanuni ya imani

Nasadiki kwa Mungu, Baba Mwenyezi,/ mwumba mbingu na dunia./ Na kwa Yesu Kristu, Mwanaye wa pekee, Bwana wetu;/ aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu,/ akazaliwa na Bikira Maria,/ akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato,/ akasulubiwa, akafa, akazikwa,/ akashukia kuzimu;/ siku ya tatu akafufuka katika wafu;/ akapaa mbinguni;/ amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi;/ toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu,/ Kanisa takatifu katoliki,/ ushirika wa Watakatifu,/ maondoleo ya dhambi,/ ufufuko wa miili,/ uzima wa milele. Amina.

SALA MBELE YA KITI CHA ENZI CHA MUNGU

Sali Atukuzwe 7 kwa heshima ya Malaika 7 wateule ujipatie neema ya kuepa dhambi mbaya saba na kutujaza mapaji saba ya Roho Mtakatifu.

TUOMBE
Ee Mungu Mwenyezi wa milele, kwa wema na huruma yako ya ajabu, umetaka watu wako waokoke, ukamweka Malaika Mkuu Mikaeli kuwa Mkuu wa Kanisa lako, Utukinge na adui zetu, wasitusmbue saa ya kufa kwetu, bali tuongozwe naye kwenye utukufu wako Mkuu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana Wetu Yesu Kristo. Amina.

Utuombee Ee Mtukufu Mtakatifu Mikaeli Mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo, tujaliwe ahadi za Kristo. Amina.

Sala za kuheshimu Damu Takatifu ya Yesu

Tusali kila siku sala hizi, angalau kwa mwezi wa saba (Julai) kila mwaka, mwezi wa kuheshimu Damu Takatifu ya Mkombozi wetu.

Yesu alimwahidi Mt. Brigita wa Sweden kwamba wale watakaosali Baba Yetu 7 na Salamu Maria 7 kwa miaka 12 kwa kuheshimu damu yake takatifu na kutafakari juu ya Kutahiriwa kwake, jasho lake la damu, kupigwa kwake mijeledi, kuvikwa taji la miiba, kuchukua kwake Msalaba, kusuliwa kwake na kuchomwa ubavuni; watapata neema 5 zifuatazo: (1) Hawataingia toharani, (2) Yesu atawapa cheo cha mashahidi waliomwaga damu yao kwa ajili ya imani, (3) Yesu atawadumisha jamaa zake watatu katika hali ya neema, (4) Roho za jamaa zake zitakingwa na Jehanam mpaka kizazi cha nne, (5) Mwezi kabla ya kufa, Yesu atawajulisha. Wakifa kabla ya kutimiza miaka ile, watahesabiwa wamemaliza.

Ee Yesu, sasa ninataka kusali Baba yetu mara saba nikiungana na ule upendo ambao kwao uliitakasa sala hii katika Moyo wako. Uichukue kutoka mdomoni mwangu hadi moyoni mwako. Uiboreshe na kuikamilisha hivyo kwamba iupatie heshima na furaha kwa Utatu Mtakatifu kama vile Wewe ulivyoupatia kupitia sala hii wakati ulipokuwa bado hapa duniani. Utukuzwe ee Yesu, itukuzwe Damu Yako Takatifu sana uliyoimwaga kutoka katika Majeraha Yako Matakatifu.

1. Yesu anatahiriwa.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea Majeraha ya kwanza, maumivu ya kwanza na Damu ya kwanza aliyomwaga Mwanao mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu na dhambi za dunia nzima, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi ya kwanza ya mauti, hasa kati ya ndugu zangu.

2. Yesu anatokwa Jasho la Damu bustanini Gethsemane.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea mateso na mahangaiko makali sana ya moyoni, ya Bwana wetu Yesu Kristu katika mlima wa mizeituni na kila tone la jasho lake la damu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za kimoyomoyo, na dhambi za namna hiyo zinazotendwa na dunia nzima, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za moyoni na kwa ajili ya kueneza upendo wa kiMungu na wa kindugu.

3. Yesu anapigwa mijeledi.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea majeraha elfu elfu aliyopata, maumivu makali sana na Damu Takatifu sana aliyomwaga, alipopigwa mijeledi, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za tamaa ya mwili, kwa malipizi ya dhambi za tamaa ya mwili za wanadamu wote, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za tamaa ya mwili, na kwa kulinda usafi wa moyo, hasa kati ya ndugu zangu.

4. Yesu anavikwa taji la miiba.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea majeraha, maumivu na Damu Takatifu kutoka katika Kichwa Kitakatifu cha Yesu wakati alipovikwa taji la miiba, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za rohoni, kwa malipizi ya dhambi za rohoni za wanadamu wote, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za rohoni, na kwa ajili ya kueneza Ufalme wa Kristu hapa duniani.

5. Yesu anachukua Msalaba.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea mateso ya njia ya Msalaba, hasa donda lake la begani na Damu Takatifu iliyomwagika, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za ukaidi dhidi ya msalaba, na dhambi za ukaidi dhidi ya msalaba za wanadamu wote, malalamiko yote dhidi ya mipango yako mitakatifu na dhambi zote za ulimi, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za ulimi na kwa ajili ya upendo wa kweli kwa Msalaba.

6. Yesu anasulibiwa.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea Mwanao Msalabani, kupigwa kwake misumari na kuinuliwa kwake, madonda yake mikononi na miguuni na mifereji mitatu ya Damu yake Takatifu iliyomwagika kutoka katika majeraha haya, mateso yake makali sana ya mwili na roho, kifo chake kitakatifu, ukumbusho usio wa kumwaga wa damu wa kifo hiki katika Misa zote Takatifu ulimwenguni, kwa ajili ya majeraha yote yanayosababishwa na ukaidi wa nadhiri na kanuni katika madaraja matakatifu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu zote na za ulimwenguni mzima, kwa ajili ya wagonjwa na wanaokufa, kwa ajili ya mapadre watakatifu na walei, kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu za kukarabati familia za kikristu, kwa ajili ya kuimarika kwa imani ya kikristu ulimwenguni, kwa ajili ya nchi yetu na muungano kati ya mataifa ndani ya Kristu na Kanisa lake, na kwa ajili ya wokovu wa dunia nzima.

7. Yesu anachomwa kwa mkuki moyoni.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, ukubali kupokea, kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa Takatifu na kwa ajili ya malipizi ya dhambi za wanadamu wote, Damu na Maji Takatifu vilivyomwagika kutoka jeraha la Moyo Mtakatifu wa Yesu. Utuhurumie. Damu Takatifu ya Yesu, tone lile la mwisho lililomwagika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu, unioshe mimi na wengine wote dhambi zetu zote! Ee Maji kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, unioshe na adhabu zote za dhambi zangu na uizime miale ya moto wa toharani kwa ajili yangu na kwa ajili ya roho zote zilizomo toharani. Amina.

Katika mwaka wa Kanisa wa kiliturjia, mwezi Julai ni wa kuiheshimu Damu Takatifu ya Yesu.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About