Mpenzi msomaji, kumekuwa na tuhuma nyingi dhidi ya wakatoliki kwamba wanaabudu sanamu. Je, tuhuma hizo zina ukweli gani? Hilo ndilo swali tunalotaka kujibu leo.
Amri ya kukataza ibada kwa sanamu imewekwa wazi katika Biblia Takatifu, Kutoka 20:4-5, βUsijifanyie sanamu ya miungu wa uongo, au kinyago chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini chini ya dunia. Usiisujudie wala kuitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.β
Sheria hiyo inapatikana pia katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:8-9: βUsijifanyie sanamu za miungu za kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Isivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.β
Ni kutokana na vifungu hivyo vya Maandiko Matakatifu, Waamini wa Kikatoliki wamekuwa wakituhumiwa, kushtakiwa na kushambuliwa na baadhi ya waamini wa madhehebu mengine kwamba wanapingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu, yanayokataza ibada kwa sanamu. Tuhuma hizo zinakuwa nzito zaidi, hasa zinapohusishwa na Ibada inayofanywa na Waamini Wakatoliki siku ya Ijumaa Kuu kila mwaka.
KUNA TOFAUTI KATI YA KUABUDU NA KUHESHIMU
Mpenzi msomaji, kuna tofauti kubwa kati ya kuabudu na kuheshimu. Kamusi ya Kiswahili ya Maana na Matumizi, ya mwaka 1993, iliyoandikwa na SALIM K. BAKHRESSA, na kuchapishwa na OXFORD UNIVERSITY PRESS, DAR ES SALAAM, inaeleza kuwa neno βkuabuduβ maana yake ni βkuomba au kufanya ibadaβ; na neno βkuheshimuβ maana yake ni βkutukuza, kustahi au kuogopa.β
Katika maana yake ya ndani, anayeabudiwa na mwenye haki ya kuabudiwa ni Mungu peke yake. Hakuna mtu, kiumbe wala kitu chochote kinachopaswa kuabuduiwa na chenye haki ya kuabudiwa. Mtu, kiumbe au kitu hupewa heshima tu, tena ya kiwango maalum. Kwa mfano, Bikira Maria, kwa sababu ya nafasi yake katika kazi ya ukombozi, anapewa heshima ya juu kuliko watakatifu wengine. Watakatifu hao wengine hupewa heshima ya kadiri tu, chini ya heshima ile anayopewa Bikira Maria.
KWA NINI MUNGU PEKE YAKE ANASTAHILI KUABUDIWA?
Tumesema ni Mungu pekee yake, ndiye anayestahili kuabudiwa, kwa sababu ndiye MUUMBA wa vitu vyote, vinavyoonekana na visivyoonekana; ndiye anayevitawala na kuviongoza vitu vyote; ndiye mwenye uwezo juu yetu sisi wanadamu na viumbe vingine vyote; ndiye anayejua yote; ndiye aliye pote kwa ajili yetu; ndiye mwanzo na mwisho wa kila kitu; ndiye mkuu na Bwana wa wote.
Aidha, tunapomwabudu Mungu, tunakiri kwamba ndiye aliyetuumba na βndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu na tuko!β (Mdo.17:28). Kwa kufahamu hilo, Wakatoliki hawawezi kumwabudu mtu, kiumbe au kitu chochote, isipokuwa Mungu tu.
MAMBO MAKUU NA MUHIMU KATIKA IBADA YA SANAMU
Ili kufahamu vema kinachofanywa na Wakatoliki ni vema kufuatilia na kutafakari yale wanayoyafundisha na kuyasadiki wao wenyewe, badala ya kuwahukumu kadiri watu wengine wanavyofikiri na kusema. Ukweli ni kwamba hakuna Ibada yoyote ya sanamu katika Kanisa Katoliki. Hilo ni dhahiri kwa sababu ili ibada ya sanamu iwe kweli kuabudu sanamu lazima yawepo mambo makuu na muhimu mawili: Kwanza, NIA KAMILI YA KUABUDU SANAMU INAYOHUSIKA;
Pili, KUWEPO NA IBADA YA DHATI YA KUABUDU SANAMU. Ikitazamwa kwa makini, hayo mambo mawili yanakosekana katika Kanisa Katoliki linapokuja suala la picha na sanamu. Kwa hiyo, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala picha. Kama ni hivyo, wakatoliki wanafanya nini na hizo sanamu au picha? Wanaziheshimu tu! Tukumbuke kuwa anayemwabudu mtu, kiumbe au kitu, ni sharti akihesabu na kukisadiki kuwa ndicho kinachomwezesha kuishi, kujimudu na kuwa na uhai wake (Rej. Mdo.17:28).
JE, BINADAMU TUNAHITAJI SANAMU AU PICHA?
NDIYO. Binadamu tunahitaji sananmu au picha, tena ni jadi yetu! Kwa sababu gani tunahitaji picha maishani mwetu? Kwa sababu katika udhaifu wetu, mara nyingi tunaweza kufikiri vema kwa kutumia vielelezo au vichokoo vyenye kuonekana na kugusika. Kwa njia ya vielelezo hivyo, binadamu tunaweza kuyafikia kwa urahisi mambo magumu na mafumbo yaliyo juu ya fikra zetu za kawaida. Ndiyo maana tukiona picha au sanamu ya Yesu au Mama Maria au Watakatifu wengine, akili zetu zinaweza kutafakari mambo matakatifu na kupata picha ya kina cha msamaha wa dhambi na mapendo ya Mungu kwetu wanadamu.
KWA NINI WAKATOLIKI HAWAABUDU SANAMU AU PICHA?
Wakatolikihawaabudu sanamu kwa sababu wanajua kwamba Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa. Kwa hiyo, hawaziabudu sanamu au picha kwa sababu wanajua kwamba hivyo siyo Mungu. Zaidi hayo, wanajua kwamba Mungu mwenyewe amekataza kuziabudu sanamu na picha kwani hazina daraja la Muumba. Mungu amepiga marufuku kuzigeukia na kuzisujudia (Law.19:4). Aidha, wameaswa kuziepuka sanamu na Ibada kwa sanamu β βWatoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu!β (1Yoh.5:21). Pia wakatoliki wanajua kuwa sanamu na picha hazina uwezo wowote wa kimungu. βMungu wetu yuko mbinguni, hufanya yote anayotaka. Miungu yao ni fedha na dhahabu; imetengenezwa na mikono ya wanadamu. Ina vinywa lakini haisemi. Ina macho lakini haioni. Ina masikio lakini haisikii. Ina pua lakini hainusi. β¦ Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo, kadhalika na wote wanaoitumainia. Enyi wa nyumba ya Israeli mtumainieni Mwenyezi Mungu, yeye ndiye msaada wenu na ngao yenuβ (Zab.115:3-9). Pia kuziabudu sanamu ni jambo la kidunia, ambalo haliwezi kumpeleka mtu peponi (Rej. Isa.45:16; Isa.45:20; Gal.5:20). Kwa hiyo, Wakatoliki wanajua kuwa kuabudu sananmu na picha ni jambo haramu kabisa mbele ya Mungu, Mwumba wao (1Pet.4:3-4).
IBADA YA KWELI YA SANAMU INAKUWAJE?
Ibada ya kweli ya sanamu siyo rahisi hivyo, kama baadhi ya watu wanavyodhani! Ibada ya kweli ya sanamu siyo kitu cha mchezomchezo, kama baadhi ya watu wanavyofikiri na kusema. Ibada ya Sanamu ni suala la kuabudu, na kuabudu siyo suala la kuwa na kitu au kikiheshimu tu, bali ni kwenda mbali zaidi ya hapo! Hivyo kumiliki sanamu au picha, mathalani majumbani au kanisani, hakusemi lolote juu ya uwepo wa ibada ya sanamu kwa wale wanaohusika nazo. Kwa hiyo, ikiwa watu hawazipi sanamu au picha hizo mahali pa Mungu wa kweli, basi hawana hatia yoyote.
Jambo muhimu hapa ni kwamba wamiliki wa sanamu au picha hizo wanaziheshimu tu huku wakijua kuwa wenyewe wanaowakilishwa na sanamu au picha hizo hawapo pale kwa hali halisi. Katika maana hiyo, inakuwa sahihi kabisa kuziheshimu picha za marais, ndugu na marafiki wetu tunaowapenda, ambao hawapo karibu nasi. Picha zao hatuzikejeli wala hatuzibwagi chini na kuzikanyaga au kuzitia vumbi. Hatufanyi hivyo, siyo kwa sababu tunawaabudu watu hao au vitu hivyo, bali kwa sababu tunawapenda na kuwathamini wenyewe katika hali zao halisi.
Kwa mfano ikiwa tuna kitabu cha picha (Album) chumbani, chenye picha 100 za ndugu, rafiki na jamaa zetu, hatusemi tuna miungu 100 tunaowaabudu nyumbani mwetu! Vinginevyo, mambo yangetisha sana majumbani mwetu! Wenye picha hizo hatuwaabudu kamwe, ila tunawapa heshima tu kwa sababu tunawajali na kuwapenda. Kwa nini tusiwape heshima hiyo, ambayo ni kitu cha bure! Ukweli huo pia unahusu Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa, nk.
JE, MUNGU ANACHUKIA KILA SANAMU NA PICHA?
Mungu hachukii kila sanamu au picha. Hapa inafaa ieleweke vema kwamba Mungu alipopiga marufuku sanamu katika Kitabu cha Kut. 20:3-5 na Kumb. 5:7-10, hakupiga marufuku kila sanamu. Yeye mwenyewe anaonesha kwamba anazichukia sanamu zinazotengenezwa kusudi zichukue nafasi yake tu. Kama sanamu au picha hazihatarishi nafasi yake, hana maneno nazo! Ndiyo maana, basi, baada ya kumwagiza MUSA awaambie watu wasizitengeneze sanamu na kuziabudu kama miungu (Kut.20:4-5), alimwagiza MUSA huyo huyo azitengeneze sanamu zisizokuwa hatari, ambazo hazikupewa daraja la Mungu. Mungu alimwagiza MUSA kutengeneza sanamu katika nafasi mbili:
(i) Musa anaagizwa atengeneze sanamu mbili za Makerubi azibandike kwenye Sanduku la Agano wakifunike kiti chake cha rehema. βUtatengeneza pia mfano wa viumbe hai viwili kwa kufua dhahabu, uwaweke kwenye miisho miwili ya kiti hicho; kiumbe kimoja mwisho mmoja na kiumbe mwingine mwisho mwingine. Waweke viumbe hao kwenye miisho ya hicho kiti, lakini wawe kitu kimoja na hicho kiti. Viumbe hao wataelekeana, mabawa yao yamekunjuka kukifunika kiti cha rehema, nyuso zao zitakielekea kiti hichoβ (Kut.25:18-20; Rejea pia Ebr.9:5).
(ii) Mungu alimwagiza pia Musa atengeneze Nyoka wa Shaba kama dawa kwa wale ambao walingβatwa na nyoka wa moto kule Jangwani. Musa alielezwa wazi kwamba wale ambao wangemtazama huyo nyoka wa shaba kwa imani kwa Mungu wa Israeli wangepona. βNdipo naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: Tengeneza Nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona. Basi, Musa akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu aliyeumwa na nyoka alipomtazama huyo nyoka wa shaba, aliponaβ (Hes. 21:8-9; Rejea pia Yoh.3:14-15).
Basi, Musa alitekeleza maagizo hayo ya Mwenyezi Mungu, naye alifurahia. Kwa maagizo hayo mawili ni dhahiri kwamba Mungu hachukii kila sanamu au picha. Mungu anachukizwa na sanamu zile ambazo zimekusudiwa kuchukua daraja la umungu wake, maana ni yeye tu ndiye anayestahili kuabudiwa. Yule nyoka wa shaba alikuwa dawa kwa wale walioumwa na nyoka wa moto. Watu hao hawakumwabudu nyoka wa shaba, lakini walipona, siyo kwa sababu ya nguvu zake, ila kwa nguvu za mwokozi zilizokuwa nyuma yake. βKama mtu akiitazama alama hiyo aliponywa, lakini kilichomponya siyo hicho kitu alichokiona, bali wewe uliye Mwokozi wa watu woteβ (Hek.16:7).
Hapa ni vifungu vingine vya Maandiko Matakarifu, vinavyoonesha kuwa Mungu hachukii kila sanamu au picha.
1Fal. 7:29 βkulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe vyenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali zilikuwa, zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuriβ.
2Nyak.3:10 βAlitengeneza sanamu mbili za viumbe wenye mabawa kwa mbao, akazifunika kwa dhahabu na kuziweka mahali patakatifu sanaβ
Ezek.41:17-18 ββ¦ kwenye ukumbi palikuwepo na michoro iliyofanana na mitende na picha za viumbe vyenye mabawa. Kila baada ya mtende kulichorwa picha ya kiumbe chenye mabawa kukizunguka chumba choteβ.
Yoh. 3:14-15 βKama vile Musa alivyomwinua yule nyoka wa shaba kule Jangwani, naye Mwana wa mtu atainuiliwa juu vivyo hivyo, ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele.β
Ebr.9:5 βJuu ya hilo sanduku kulikuwa na viumbe wenye mabawa, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewaβ
UBAYA WA SANAMU AU PICHA UKO WAPI?
Ubaya wa sanamu au picha upo katika kuzipa sanamu au picha daraja la Mungu. Hatari na ubaya wa sanamu au picha vimo katika kitendo cha binadamu kuzipa sanamu au picha hizo daraja la Mwenyezi Mungu. Kama sanamu au picha hazipewi daraja la Mungu, haziwi hatari na wala hazina ubaya wowote mbele ya Mungu. Kwa sababu hiyo, basi, mtu anaweza kuwa na sanamu au picha ndani ya nyumba yake au kanisani, lakini bila kumkasirisha Mungu.
Zaidi ya hayo, Mungu mwenyewe anajua fika kuwa sanamu au picha fulani imepewa daraja lake au siyo. Kwa nini Mungu akasirike pale ambapo sanamu au picha haziingilii daraja na ukuu wake? Mungu mjinga wa aina hiyo hayupo! Mungu wa kweli hawezi kukasirikia picha na sanamu ambazo zinaheshimiwa tu, na wala haziabudiwi. Aidha, Mungu mwenye haki hawezi kumwadhibu na kumtupa Jehanamu mtu ambaye anamiliki picha au sanamu duniani lakini bila kuziabudu, yaani pasipo kuzipa daraja la Mungu.
BIBLIA INAWEZA KUTUSAIDIA KUIELEWA IBADA YA SANAMU?
Jibu ni ndiyo! Biblia inatoa maelezo ya kina na ufafanuzi mzuri juu ya ibada ya sanamu. Tumesema hapo juu kuwa ibada ya sanamu siyo jambo la mzaha au mchezo wa kitoto! Ni suala la kuabudu, na kuabudu siyo tu jambo la kuwa na sanamu au picha na kuiheshimu tu. Ni zaidi ya hapo! Kuna mambo muhimu ambayo lazima sanamu zitendewe, ndipo ihesabike kuwa ni ibada ya sanamu.
a) Tukitaka kujua kama kitendo fulani mbele ya sanamu ni kuabudu au sivyo, kwanza lazima iwepo nia thabiti ya mtu anayehusika katika kitendo hicho kinachofanyika. Ibada inakuwa ya kuabudu sanamu ikiwa mtu anayefanya kitendo hicho anaamini moyoni mwake kwamba hiyo sanamu au picha inayofanyiwa kitendo hicho inachukua daraja na nafasi ya Mwenyezi Mungu. Katika kitendo hicho, mtu anaamini kuwa sanamu au picha hiyo ndiyo inayomwezesha kwenda, kuishi, kujimudu na kuwa na uhai wake hapa duniani.
b) Jambo la pili ni kuangalia kama kitendo hicho kinachofanyika katika ibada hiyo ni Liturujia ya kueleweka/maalum. Baada ya kubaini nia thabiti ya mtendaji, tunaweza kuitambua ibada ya sanamu kwa kuangalia yale yanayofanyika mbele ya sanamu au picha kwa kufuatilia mambo ambayo waabudu sanamu huyafanya. Mambo hayo, ambayo waabudu sanamu wanayafanya tunaweza kuyakusanya kutoka katika Biblia yetu. Agano la Kale linaonesha kuwa Ibada ya Kuabudu Sanamu inajumuisha mambo makuu yafuatayo:
i. Kuzitolea sadaka: za kuteketezwa: Rej. Hos.4:13; nafaka na vyakula 2Fal.5:17.
ii. Kuzitolea ubani kwa heshima kamili: Rej. 1Fal.11:8; Isa. 57:6; Yer.7:18.
iii. Kuzimwagia matambiko: Rejea Isa. 57:6
iv. Kuzitolea zaka ya sehemu ya kumi ya mapato ya mwaka ya mazao ya mashambani: Rejea Hosea 2:8
v. Kuziandika meza mbele yao: Rejea Isa. 65:11
vi. Kuzibusu sanamu kwa kuzisujudia kama viumbe vyenye enzi.
Rejea 1Fal. 19:18; Hos.13:2; Ayu. 31:2.
vii. Kuziinulia sanamu mikono katika kuzisujudia: Rejea Isa.44:20
viii. Kuziangukia sanamu kifudifudi ama kuzipigia magoti kwa kuziabudu: Rejea 1Fal.18:26,28.
ix. Kuzichezea ngoma na wakati mwingine kujikatakata kwa visu kama kitendo cha ibada kwa sanamu: Rejea 1Fal.18:26,28.
Hayo yote yakichunguzwa kwa makini, tutaona wazi kuwa hakuna Ibada ya kuabudu sanamu katika Kanisa Katoliki. Kwa hiyo, shutuma kwamba Wakatoliki wanaabudu sanamu siyo za kweli, hazina msingi, na ni uchochezi wa bure wenye lengo la kuleta mafarakano na magomvi. Jambo hilo ni dhahiri kwa sababu Wakatoliki hawana nia thabiti ya kuabudu sanamu wanapotoa heshima kwa sanamu au picha mbalimbali. Pili, matendo ya kiliturujia yanayofanywa na wakatoliki katika kuheshimu sanamu hayalingani na matendo ya kiliturujia yanayofanywa na waabudu sanamu, kama ilivyoelezwa katika Biblia Takatifu, hususan Agano la Kale. Kifupi, wakatoliki hawana nia thabiti moyoni ya kuziabudu sanamu au picha, tena hawazifanyii liturujia yoyote sanamu au picha walizo nazo majumbani au makanisani.
Ni wapi ambapo Kanisa Katoliki linafanya au kuwafundisha rasmi na kuwahimiza wafuasi wake wafanye matendo hayo tisa ya kiliturujia kwa ajili ya kuabudu sanamu? Hakuna! Kwa hiyo, Wakatoliki hawana hatia yoyote ya kuabudu sanamu mbele ya Mungu. Kama mtu mmoja akifanya hivyo, hilo ni shauri lake binafsi, siyo shauri au utaratibu wa Kanisa lote. Aidha, afanyaye hivyo amepotoka peke yake, kwa sababu hajafundishwa na Kanisa Katoliki afanye hivyo. Hilo ni kweli kwa sababu mambo binafsi, siyo mambo rasmi ya Kanisa lote!
Kwa hiyo, tunaona wazi kwamba Wakatoliki hawaabudu sanamu kamwe, kama inavyodaiwa na baadhi ya waamini wa madhehebu mengine ya kikristo. Wanaotoa shutuma hizo inafaa wajiangalie kwanza wao wenyewe, maana imeandikwa: ββ¦ mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisiβ (Rom.14:14).
JE, IJUMAA KUU WAKATOLIKI WANAABUDU NINI?
Je, ni kweli kwamba Siku ya IJUMAA KUU Wakatoliki wanaabudu Sanamu au Mti wa Msalaba? HAPANA! WANAMWABUDU WOKOVU-YESU! Kiini cha utata hapa ni βNINI MAANA YA IBADA YA KUABUDU MSALABAβ inayoendeshwa siku ya Ijumaa Kuu? Madhehebu hayo yanayofanywa na Wakatoliki Siku ya IJUMAA KUU siyo Ibada ya Kuabudu Sanamu. Labda hapa ni tatizo la lugha au maneno yanayotumika, ndiyo yanayowachanganya watu! Hilo ni kweli kwa sababu jina la madhehebu yenyewe halisemi wazi kitu gani hasa kinanuiwa kufanywa katika ibada hiyo.
Wengi hawajui nini hasa kinanuiwa kufanyika siku ya Ijumaa Kuu katika βIbada ya Kuabudu Msalabaβ β jina ambalo nimesema halitoi picha halisi ya jambo linalokusudiwa kufanyika. Mtu mwenye akili timamu akijua kitu halisi kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu, hawezi kusema madhehebu hayo ni Ibada ya Sanamu au kuabudu mti. Tatizo hapo ni lugha tu inayotumika katika kuieleza ibada hiyo. Labda jina hilo lichunguzwe upya na wataalamu wetu katika Kanisa na ikiwezekana kulirekebisha ili kuondoa utata kwa baadhi ya watu wenye uelewa mdogo, wenye wanaokwazwa nalo!
NINI HASA KINAFANYIKA SIKU YA IJUMAA KUU?
Wanachofanya Wakatoliki Siku ya Ijumaa Kuu ni KUUHESHIMU MTI WA MSALABA na KUMWABUDU WOKOVU. WOKOVU ni nani? WOKOVU NI YESU KRSITO BWANA WETU. Basi, kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu ni kumwabudu WOKOVU yaani YESU KRISTO, ambaye alitundikwa msalabani. Hivyo ndivyo anavyotangaza Kiongozi wa Ibada hiyo ya Ijumaa Kuu, pale anapotoa mwaliko kwa waamini mara tatu, ili kila muumini ausikie na kuelewa vema: βHUU NDIO MTI WA MSALABA, AMBAO WOKOVU WA DUNIA UMETUNDIKWA JUU YAKE, NJOONI TUUABUDU.β Waamini wanaalikwa kiimani kuuabudu WOKOVU, na hilo ndilo linalofanyika, yaani kuuabudu WOKOVU β YESU KRISTO. Waamini wote wanaalikwa kujongea mbele kwa imani kwenda kumwabudu YESU. Watu wanamwabudu YESU kwa sababu WOKOVU maana yake ni YESU.
Jina YESU ambalo linatokana na Kiebrabia βYESHUAβ, maana yake βWOKOVUβ (Rej. Mt.1:21;1:25; Lk.1:31). Ikiwa wokovu ni YESU, basi Ijumaa Kuu Wakatoliki hawaabudu sanamu au mti, bali wanamwabudu YESU KRISTO. Kwa sababu hiyo, yote yanayofanyika Siku ya Ijumaa Kuu, yanafanyika kihalali na kwa haki kwa sababu YESU KRISTO, ambaye ni WOKOVU ni MUNGU, na MUNGU peke yake ndiye mwenye haki na anayepaswa kuabudiwa. Ikiwa mkristo hataki kumwabudu YESU KRISTO, aliye Mwana wa Mungu na Mungu kamili, na ambaye ameeleta wokovu, anafanya makosa makubwa!
Basi, nasisitiza kuwa Siku ya Ijumaa Kuu, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala mti. Wanamwabudu WOKOVU, yaani YESU KRISTO, Nafsi ya Pili ya MUNGU. Kutomwabudu YESU KRISTO ni sawa na kumkana Mungu, kukana wokovu ulioletwa naye. Basi, tujiepushe na ukanaji Mungu wa aina hiyo. Nawaalika wote Siku ya Ijumaa Kuu tufungue mioyo yetu kwa imani kubwa ili tumwone WOKOVU aliyetundikwa msalabani, apate kuukomboa ulimwengu. Kwa imani, wote tumsujudie YESU ili apate kutukumbuka katika Ufalme wake wa milele.
Hatimaye, niseme kwamba ingawa Mungu ametoa amri ya kukataza sanamu na picha (Kut. 20:4-5; Kumb. 5:6-10), lakini hachukizwi na kila sanamu au picha. Sanamu na picha ambazo hazipewi daraja la Mungu, Yeye hazichukii, kwa sababu hazichukui nafasi yake kama Muumba. Basi, Wakatoliki hawaendi kinyume na Biblia kwa kuziheshimu sanamu na picha zilizoko kwenye majumba yao na makanisani.
Read and Write Comments
Recent Comments