Katoliki: Ushauri kuhusu mambo mbalimbali Katika Maisha

Ufanyialo wengine ndilo utakalofanyiwa

Siku niliposoma hili andiko kwa mara ya kwanza nakumbuka, kwanza nilipata mshtuko flani baada ya kulisoma, halafu nikajikuta nikitafakari vitu vingi sana.

Hebu kwanza tusome pamoja andiko hili

ZABURI 109

17 Naye alipenda kulaani, nako kukampata.Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye

▶Huu mstari wa 17 umenishangaza sana, halafu ukanifungua na kunifundisha vitu vya msingi sana katika haya maisha tunayoishi

Ngoja tuuchambue kidogo hapa ili tuelewane vizuri

_Alipenda kulaani?………………………….Nako (laana/kulaaniwa) kukampata_

_Hakupendezwa na kubariki……………………(Kubarikiwa) kukawa mbali nae_

NET BIBLE inasema hivii

“He loved to curse others, so those curses have come upon him, He had no desire to bless anyone, so he has experienced no blessings” Kumbe the more ninakuwa na shauku ya kuona wengine wakibarikiwa, the more baraka zinanijia mimi and vice versa

Hapa nikajifunza kwamba kumbe yale mabaya tunayowafanyia au kuwawazia watu kuna uwezekano mkubwa sana yakatupata sisi wenyewe

Na tunapotamani kubarikiwa na kuinuliwa wakati hatufurahii kuona wengine wakiinuliwa, kuinuliwa kutakuwa mbali nasi

Huu mstari unaniongezea maarifa na kunifundisha namna ya kuishi katika ulimwengu huu

Nimewaza pia inawezekana wakati mwingine kuna vitu hatupati ni kwasababu tuu hatufurahii wala hatuombi wengine wapate hivyo

Kumbe kubarikiwa kwangu kunategemea na namna ambavyo ninakuwa baraka kwa wengine na kutamani kuona wengine wakibarikiwa

Shauku yangu ya kutamani wengine wabarikiwe na kuinuliwa ndio nyenzo ya kuinuliwa kwangu na moyo mbovu wa kufurahi kuona wengine wakikwama ndio sababu ya kukwama kwangu?

_”Hii ni kanuni ya ajabu”
Ndugu yangu, unajua hapa najifunza kwamba kumbe kuna uwezekano mkubwa kwamba mikwamo mingine tumekuwa tukijikwamisha sisi wenyewe

Ni kweli ninataka kubarikiwa, lakini ni mara ngapi nimefurahi au kuombea wengine ili wabarikiwe?

Unatamani kupandishwa cheo sawa, lakini wengine wakipandishwa vyeo unanuna? Au ukiona ofisini ndio anapewa safari nyingi za nje unakasirika?

Unatamani kuoa/kuolewa halafu wengine wakioa na kuolewa unaona uchungu juu yao, unawanunia, unapunguza ukaribu?

Unatamani kupata gari zuri lakini wengine wakipata unakasirika?

Nikiwa mtoto mdogo nakumbuka mwalimu mmoja aliwahi fundisha kwamba nisipende sana kujiombea mwenyewe, na akasema kama unahitaji kitu, waombee wengine wasionacho wapate, nawe utajibiwa pia, andiko hili limenifanya nielewe kwanini mwalimu yule alifundisha vile

Na wakati mzaburi anaongea maneno haya hapa chini sikumuelewaga, nilijua ni kawaida tuu, nilisoma kikawaida tuu, lakini sasa ndio nimefunguka ufahamu zaidi

*ZABURI 35*

13 Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu

Bila kujali watu walikuwa wakimuwazia na kumfanyia nini, alipowaombea tuu, maombi yale yalirejea, yalifanya kazi na katika maisha yake. Kumbe kuomba kwaajili ya wengine wafanikiwe, wainuliwe, wabarikiwe na wapandishwe kunarejesha matunda kwetu pia

Ubaya unaomfanyia mwingine si ajabu ukakupata

Kuanguka unakomuombea mwingine kutakujia wewe

Kanuni hii inanifundisha pia kuwa YESU aliposisitiza tupendane alikuwa na maana kuu

Alijua kwamba ukiwa na chuki kwa mwingine chuki ile itakuathiri wewe

Ukiwa na moyo wa kufurahi wengine wanaposhindwa, kushindwa kutakupata wewe

Kwanini sasa tusichague kubariki wengine ili baraka zile zitupate na sisi pia?

Kwanini tusiwaombee mema wengine ili maombi yale ya mema yatutendee mema sisi?
Ni vyema sasa tukachagua kuwa na moyo wa upendo, moyo utakaowawazia na kuwatendea mema wengine kwasababu mema yale tuwafanyiayo wengine yatatuletea mema maishani mwetu pia

Jipime, jiangalie, jichunguze

Waza mema kwaajili ya wengine, mema yaje kwaajili yako

MITHALI 17

13 Yeye arudishaye mabaya badala ya mema,Mabaya hayataondoka nyumbani mwake

If you love to curse others, those curses will come upon you

If you have NO desire to bless others, then you will experience NO blessings

CHOOSE TO BLESS OTHERS,BLESSING WILL FOLLOW YOU

Read and Write Comments

Mambo 7 ya kubadili katika maisha ili ubadilike

1. Huwezi kubadili namna watu walivyokutendea mpaka ubadili namna unavyowatendea.​

Matayo 7:12;
“Basi yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo Torati na Manabii.”

​2. Huwezi kubadili tabia mpaka ubadili marafiki.​

1Wakorintho 15:33
“Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.”

​3. Huwezi kubadili ulichovuna mpaka ubadili ulichokipanda.​

Wagalatia 6:7;
“Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.”

​4. Huwezi kubadili mwelekeo wa maisha yako mpaka ubadili dereva.​

Kutoka 23:1-3;
“Msivumishe habari za uongo; usishirikiane na mwovu kwa kuwa shahidi wa uongo. Usiwafuate walio wengi katika kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lolote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotosha hukumu; wala usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake”.

Maisha yako yaweza ongozwa na mkumbo wa watu au ​MSIMAMO​ wako ​BINAFSI​ kwa ​UNACHOKIAMINI.​

​5. Huwezi kubadili hali yako ya kifedha mpaka ubadili tabia yako ya kifedha.​

Mithali 21:17;
Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; yeyote apendaye mvinyo, kula na manukato hatakuwa tajiri.”

​Mtindo wa maisha ya ufukara ndiyo busara kwa wengi.​

​6. Huwezi kunibadili mpaka ujibadili mwenyewe.​

Matayo 7:3-5.
“Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huioni? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”

​7. Huwezi kubadili mtazamo wako wa kifikra mpaka ubadilipo usikiacho.​

Mithali 23:7;
“Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.
Akuambia haya kula, kunywa; lakini moyo wake hauwi pamoja nawe.”

​(Waache wenye Hekima wasikilize na kuongeza ufahamu wao.)​

Huyo anayesikiliza, huashiria na kuamua kile anachojifunza.

Kile unachojifunza, huashiria uelewa ulio nao kichwani mwako.

Uelewa ulionao kichwani mwako, huashiria maamuzi yako.

Na maamuzi yako, huashiria ​mwelekeo wa maisha yako.​

Read and Write Comments

Uzinzi na Uasherati ndio mtego wa kizazi hiki

Uzinzi na uasherati wakati huu umekuwa ndio sumaku kuu ya kuwanasa watu ili waende jehanamu.

Sumaki hii imewanasa hata ambao hawakutegemewa wala kutarajiwa.

Uzinzi uzinzi uzinzi umekuwa kama perfume ya kujipulizia kila Mara mtu akipenda.

Uasherati umekuwa kama heshima ya kibinadamu kwa vijana wengi.

Mbingu zimenyamaza kwa sababu iko jehanamu inawangoja wazinzi na waasherati.

Dhambi hii imekuwa sumaku kubwa ya shetani ya kukamata wanadamu ili waende jehanamu.

Wanadamu wa Leo ukimwambia kwamba aache uzinifu maana wazinzi na waasherati hawataenda uzima wa milele, mtu huyo anakuambia unamhukumu.

Ni Neno la MUNGU ndile limesema katika maandiko mengi tu kwamba wazinzi na waasherati sehemu yako itakuwa katika ziwa la moto.

Hata makanisani baadhi ya watu wamenasa kwenye sumaku hii.

Dada mmoja ambaye kila wiki anasimama na kushika mic kanisani kwao siku moja aliniambia kwamba hawezi kumaliza wiki bila kufanya ngono, na hajaolewa. Niliumia sana rohoni nikamwambia aache kutumika madhabahuni, yeye akasema itakuaje maana yeye ndiye tegemeo.

Mama mmoja alisema yeye ana mume mema sana na mume wake ni mwaminifu sana katika ndoa yao lakini yeye huyo mama ndio hutoka nje ya ndoa Mara kwa Mara, ni hatari inayohitaji neema ya MUNGU tu ili kutubu na kuacha.

Mama mmoja yeye ana watoto zaidi ya wawili na yuko katika ndoa lakini hana uhakika kama watoto wale ni wa mume wake wa ndoa, ni hatari sana.

Baba mmoja akiwa ndani ya ndoa amezaa watoto zaidi ya watatu nje ya ndoa tena wanawake zaidi ya wanne(4) tofauti tofauti.

Mwanaume moja ambaye husimama madhabahuni yeye kila Mara humdanganya mkewe kwamba anaenda safari kumbe ana mahawara karibia kila mkoa, ni hatari sana.

Watu wengi sasa wanaona uzinzi na uasherati ndio fashion nzuri ya wakati kuu.

Kila kijana ana girlfriend kwa lengo la ngono tu na sio vinginevyo.

Kila binti ana boyfriend kwa ajili ya uasherati.

Ukitaka watu wakuchukie basi kemea uzinzi na uasherati.

Watu wengi wamekuwa vipofu wa kiroho kwa sababu ya uzinzi na uasherati.

Lakini upo mwisho mmoja kwa watenda dhambi wote ambayo ni jehanamu.

Ndugu unahitaji kutubu Leo na kuacha dhambi.

Ndugu mmoja akasema yeye anaishi maisha matakatifu ila dhambi moja tu yaani uzinifu ndio imemshinda, hiyo ni hatari.

Leo hata ndoa takatifu zimeadimika maana wahusika huanza kwanza uzinzi na uasherati ndio baadae ndoa, ndugu mnahitaji kutubu.

Ndugu yangu unayenisikiliza kwa njia ya ujumbe huu nakuomba tubu na acha dhambi hiyo.

Amua kuiacha.

Mwisho wa uzinzi na uasherati ni kifo(Mauti) na baada ya kifo ni hukumu(Waebrania 10:27)

Nimekuonya wewe Leo ili ukishupasa shingo usije ukalaumu siku ile ukiwa katikati ya bahari ya moto huku kifo kimezuiliwa ili uteseke milele.

Mimi naamini utatengeneza ndugu baada ya kuusoma ujumbe huu.

Mimi naamini utaachana na mahawara na kuanza kuiheshimu ndoa yako.

Mimi naamini hutamsaliti tena mkeo/Mumeo.

Mimi naamini utaachana na huyo girlfriend/Boyfriend, wengine wanao zaidi ya mmoja, nakuomba ndugu achana nao.

Kijana au binti kaa tulia hadi wakati wako wa ndoa.

Uliyenisikia na utatubu na kuacha dhambi hiyo, MUNGU akubariki sana.“`

ALIYE NA AKILI AWEKE MOYONI MANENO HAYA. AMINA

Read and Write Comments

Ushauri wangu kwa leo, ni Heri kuchagua kunyamaza

MITHALI 11:12 Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.

MITHALI 17:28 Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.

Changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba tunataka kuongea kila wakati, tunataka kujibu kila tunachokisikia, kila tunachokiona tunataka kukisemea kitu.

Kuna wakati tunasikia na kukutana na mambo ambayo kiuhalisia moyo unagoma kabisa kunyamaza, unatamani ujibu, unatamani uwaambie watu yale umefanyiwa, unatamani uelezee vile umeumizwa lakini kumbe si kila jambo linatakiwa kuongelewa.

Si kila ukionacho unatakiwa kukisemea kitu. Si kila usikiacho/uambiwacho ni lazima ujibu.

Si kila ufanyiwacho ni lazima umwambie kila mtu.

MUHUBIRI 3:1 Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.

7 Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;

Ipo nguvu katika kunyamaza

Yapo mambo ambayo tunapaswa kuongea, kusema, lakini yapo mambo ambayo tunapaswa kunyamaza kwa ajili ya usalama wa Roho zetu.

Ni kweli kuna wakati unasemwa sana vibaya, unasingiziwa, unatukanwa nk nk, lakini ni lazima ukumbuke kwamba kuna mazingira ambayo hupaswi kujibizana hata kama umeumia kiasi gani.

Unajua ni kwanini?

Ukisemwa vibaya, ukitukanwa, ukidharauliwa lazima moyo utaghafilika, moyo ukighafilika lazima utakuwa na hasira na ghadhabu.

Ukiwa na hasira katu usitegemee kuwa utajadiliana na mtu kwa hekima.

Ukiongea utaongea katika uwepo wa hasira, ukijibu utajibu kulingana na kiwango cha hasira ulichonacho.

Sasa jiulize majibu yanayotoka kutokana na msukumo wa hasira huwa yanakuwaje?

Mazuri? Ya upole? Ya hekima? Ya unyenyekevu? I am sure jibu ni hapana.

Kama jibu ni hapana that means utaongea vitu vibaya ambavyo ni chukizo kwa MUNGU kwa sababu amesema maneno yetu na yakolee munyu (chumvi).

Sasa badala ya kuongea upumbavu na ukamkosea MUNGU kwanini usichague kunyamaza?

AMOSI 5:3 Kwa ajili ya hayo mwenye busara atanyamaza kimya wakati kama huo; kwa kuwa ni wakati mbaya.

Nimekuwa inspired sana na mwanamke Abigaili, ni kweli mumewe alikuwa na makosa, ni kweli alikuwa mlevi, lakini mwanamke huyu alijua ni wakati gani, na mazingira gani alipaswa kuongea na mumewe na alijua aongee nini. Alipomkuta mumewe yupo katika hali ya ulevi, ALINYAMAZA, alijua kuwa huu sio wakati wa kusema jambo lolote.

1 SAMWELI 25:1

Ni vyema sisi pia tukajifunza kusoma mazingira na nyakati na hali za watu zilivyo ili tujue ni wakati gani tujibu, tuongee nini na ni wakati gani tunyamaze

Kilinde kinywa, hakikisha haukiachi kinene mabaya – ZABURI 50:19.

Usipoteze marafiki na kuharibu mahusiano kwa ajili ya kinywa kibovu – MITHALI 11:9.

Ni vyema tukajifunza kujua ni neno gani tukitamka kwa wakati/hali/mazingira gani litakubaliwa –MITHALI 10:32.

ZABURI 19:14 – Bwana na akafanye maneno yetu yakapate kibali mbele zake MUNGU na mbele za wanadamu pia.

1SAMWELI 25:36

Umeumizwa, umekwazwa, umetukanwa, umedharauliwa, KATIKA MAZINGIRA YA HASIRA NA GHADHABU JITAHIDI KUNYAMAZA.

Ni kweli moyo na akili na hisia vinakusukuma kujibu, kubisha nk nk, lakini elewa impact za kujibizana ukiwa na hasira na hizo ni bora ukae kimya.

*”AKUSHINDAE KUONGEA, MSHINDE KUNYAMAZA
“Uwe na siku njema!

Read and Write Comments

Mbinu 4 anazotumia Shetani kuteka na kurubuni Watu

1. Kutushawishi tuache kusali maaana njia kuu ya mawasiliano kati yetu na MUNGU.Hivyo akifanikiwa hapo kwisha habari yako

2. Kufanya umwogope shetani na nguvu zake kuliko unavyompenda MUNGU. Wakristo wengi leo hii husali na kuomba kwa nguvu mno siyo sababu wanampenda MUNGU mno hapana ni sababu wanamwogopa shetani na majeshi yake na muda mwingine hata watumishi wa MUNGU wanamsaidia kwa kuhubiri mno na muda mwingine kuongeza jumvi juu ya nguvu za giza kuna wahubiri huambatanisha kila kitu na vifungo vya nguvu za giza na kusahau kuhubiri uzuri na wema wa MUNGU kwetu.

3.Kutufanya tusahau uwepo wake au kuupuzia. pale tunapokuwa hatupay attention existance ya shetani yeye ndio hupata wakati mzuri wa kutupiga ,sababu ni rahisi mno kutouutambua ubaya wa dhambi kama hatutaamini uwepo wa shetani ktk uovu…hii hutupelekea kutenda dhambi na kuziona siyo dhambi mfano kwa wasomi wengi hupuuzia baadhi ya mambo kama kujilinda na zinaa wakiamini ni kupitwa na wkt kama utakuwa hauna mahusiano ya kingono mpaka umefika chuo kikuu tena huchukulia wasiokuwa hivyo ni wagonjwa.hapo ni kuwa wengi wameignore uwepo wa shetani “no devil no evil” hivyo watu ndio hupotea.

4.KUTUTIA MOYO WAKATI WA KUTENDA DHAMBI NA KUTUKATISHA TAMAA YA KUSAMEHEWA. nitatoa mfano huu mtu ambaaye anataka kufanya uzinzi shetani humtia moyo kuwa MUNGU anajua kuwa sisi ni binadamu dhaifu na yeye husamehe dhambi zetu daima lakini ifikiapo wakati ukataka kutubu hafanya kila njia kukukatisha tamaa ya kusamehewa na hututia aibu hata kutsmka kwa padri kuwa nimedhini maana huanza kufikiria padre atanionaje mimi.

BASI NDUGU TUSISINZIE BALI TUWE MACHO DAIMA MSHITAKI WETU YU MACHO KUTUJARIBU.

Read and Write Comments

Biblia inatuambia nini kuhusu pombe?

Angalizo; Tunapoongelea kuhusu pombe sio kwamba tunahamasisha kutumia pombe bali tuelewe kile tunachofanya kwa mapenzi ya Mungu!
pombe haikukataliwa ila itumike kwa kiasi.

Mhubiri 9:7
Wewe enenda zako, ule chakula chako kwa furaha, unywe mvinyo yako kwa moyo wa kuchangamka; kwa kuwa Mungu amekwisha kuzikubali kazi zako.

Tito 2:3
Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema;

1Timotheo 5:21,23
“21 Nakuamuru mbele ya Mungu, mbele ya Kristo Yesu na mbele ya malaika watakatifu, uyazingatie maagizo haya bila kuacha hata moja, wala kumpendelea mtu yeyote katika kila unachotenda.

23 Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara.

Yoshua Bin Sira 31:25-29
“25 Usijionyeshe kuwa hodari wa kunywa pombe, maana imewaangamiza wengi.
26 Tanuru hupima ugumu wa chuma, na pombe hupima mioyo katika shindano la wenye kiburi.
27 Pombe ni kama uhai kwa mtu akinywa kwa kiasi, Maisha yafaa nini bila pombe?
Imeumbwa iwafurahishe watu.
28 Kunywa pombe kwa wakati wake na kwa kiasi, kwaleta shangwe moyoni na furaha rohoni.
29 Lakini kunywa pombe kupita kiasi, kunaleta kuumwa kichwa, uchungu na fedheha.”

Wakolosai 2:16-18a

“kwa hiyo basi, msikubali kupewa masharti na mtu yeyote kuhusu VYAKULA au VINYWAJI, siku za sherehe, sikukuu ya mwezi mpya au sabato.

17 mambo ya namna hiyo ni kivuli cha yale yatakayokuja; ukweli wenyewe ndiye kristo.

18 msikubali kuhukumiwa na mtu anayejitakia kuwa wa maana kwa sababu ya maono ya pekee….”

Luka 7:31-35
“31 Yesu akaendelea kusema, “Basi, nitawafananisha watu wa kizazi hiki na kitu gani? Ni watu wa namna gani?

32 Ni kama vijana waliokuwa wamekaa sokoni na kuambiana, kikundi kimoja na kingine:
‘Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza!
Tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkulia!’

33 Kwa maana Yohane alikuja, akawa anafunga na hakunywa divai, nanyi mkasema: ‘Amepagawa na pepo!’

34 Naye mwana wa Mtu amekuja anakula na kunywa, nanyi mkasema:
‘Mwangalieni mlafi huyu na mlevi; rafiki ya watoza ushuru na wenye dhambi!’

35 Hata hivyo, hekima ya Mungu imethibitishwa kuwa njema na wote wale wanaoikubali.”

#Note; mvyinyo itumike kwa kiasi, kama huwezi kutumia kwa kiasi, ni afadhali kuacha kabisa.

Read and Write Comments

Siri ya kamba nyekundu

Miaka zaidi ya 3000 iliyopita katika mji wa Yeriko alikuwepo mwanamke mmoja kahaba, jina lake Rahabu. Huyu mwanamke aliwaokoa wapelelezi wa Israel waliotumwa kwenda kufanya uchunguzi ktk nchi yao.

Wakati wana wa Israel wanatoka Misri kuelekea nchi ya Kaanani, Mungu aliwaahidi kuwapa mji wa Yeriko. Kwahiyo walipofika ng’ambo ya mto Yordani, Yoshua akatuma wapelezi wawili kwenda kuipeleleza Yeriko kabla wana wa Israel kuivamia na kuitwaa. Wale wapelelezi walipofika mji wa Yeriko mfalme akapelekewa taarifa kuwa kuna watu wawili wameingia kuipeleleza nchi.

Kwahiyo mfalme akaagiza wakamatwe na wauawe. Wale wapelelezi wakaingia ktk nyumba ya mwanamke kahaba aitwaye Rahabu akawaficha darini. Akawafunika kwa mabua ya kitani. Wale askari walipofika na kumuuliza Rahabu kwamba wako wapi waisrael wawili walioingia humu ndani, Rahabu akajibu kuwa wameondoka.

Akasema ni kweli waliingia ktk nyumba yangu lakini walitoka kabla lango la mji halijafungwa. Akawaambia wafuateni haraka kabla hawajafika mbali. Wale askari wakatoka kuwafuata wale wapelelezi hadi katika vilima vya nje ya mji lakini wasiwaone. Ilipofika usiku Rahabu akawashusha darini wale wapelelezi na kuwaelekeza namna ya kutoroka mji wa Yeriko. Akawaelekeza wapite njia nyingine tofauti na ile waliyoiendea wale askari. Akawashusha kupitia dirishani ili watu wa mji ule wasiwaone.

Kwa ukarimu aliowatendea wale wapelelezi wakaweka agano nae kwamba siku wana wa Israel wakija kuiangamiza Yeriko, BWANA ataiponya nyumba ya Rahabu na ndugu zake wote. Ili kutimiza agano hilo wale wapelezi wakamwambia Rahabu weka kamba nyekundu katika dirisha lako kama alama, ili jeshi la Israel liltakapouteketeza mji nyumba yako isiangamizwe.

Yoshua 2:17 &18 “Wale wapelelezi wakamwambia Rahabu, Sisi tunataka tusiwe na hatia kwa ajili ya kiapo hiki ulichotuapisha. Angalia, tutakapoingia katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu katika dirisha hili ulilotuteremshia; nawe uwakusanye nyumbani mwako, baba yako, mama yako, na ndugu zako, na watu wote wa nyumba ya baba yako.”

Rahabu akafanya hivyo, na siku Jeshi la Israel lilipovamia Mji wa Yeriko ili kuuteketeza, Rahabu na ndugu zake walipona.

Yoshua 6:23 &24 “Basi wale vijana wapelelezi wakaingia, wakamtoa Rahabu, na baba yake, na mama yake, na ndugu zake, na vitu vyote walivyokuwa navyo, wakawatoa na jamaa zake wote pia; wakawaweka nje ya matuo ya Israeli. Kisha wakauteketeza mji kwa moto, na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake…”

MORAL OF THE STORY.!
Habari hii ina mengi ya kutufundisha lakini leo nataka nikufundishe kuhusiana na siri ya kamba nyekundu ambayo Rahabu aliiweka katika dirisha lake na jinsi ilivyomuokoa.

Rahabu hakua mtakatifu, hakuwa mteule wa Mungu wala hakuwa kizazi cha Israel. Alikua mwanamke wa mataifa, tena kahaba. Hakuwa mwema sana machoni pa Mungu. Lakini aliokoka kwa sababu ya “kamba nyekundu” dirishani mwake. Pengine wapo maaskofu, wachungaji, mitume au manabii walioangamizwa, lakini kahaba Rahabu akaokolewa yeye na ndugu zake licha ya kwamba alikua kahaba. Siri ni “kamba nyekundu” dirishani mwake.

Jiulize je wewe unayo kamba nyekundu? Kuna watu katika maisha wanaonekana wenye dhambi, wachafu, dhaifu au wasiofaa, lakini Mungu huwanyanyua na kuwabariki na kuwaacha wale tunaodhani ni watakatifu au wenye haki. Mungu anaangalia “kamba nyekundu”. Unaweza kuwa mtakatifu lakini huna “kamba nyekundu” itakayomfanya Mungu akurehemu.

Unaweza kuwa umemaliza masomo yako na umefaulu vizuri, lakini kila unapoomba kazi huitwi hata kwenye usaili, na ukiitwa hupati kazi, miaka inazidi kwenda. Unaamua kwenda kwenye maombi. Kila siku unafanya maombi lakini bado hufanikiwi. Unajiuliza tatizo liko wapi. Unaji-asses na kuona hakuna tatizo mahali. Kumbe huna “kamba nyekundu”

Au unaweza kuwa una biashara yako lakini haifanikiwi. Hupati wateja. Umehitahidi kwa kila hali lakini bado huoni faida. Unadhani tatizo labda Mungu amekuacha. Unaamua kuwa mtu wa maombi. Unazunguka makanisa mbalimbali kuonbewa lakini bado haufanikiwi. Kumbe huna “kamba nyekundu”.

“Kamba nyekundu” imekuwa siri ya mafanikio ya watu wengi bila kujalisha mahusiano yao kiroho na Mungu. Bila kujalisha kama ni wakristo au si wakristo. Kamba nyekundu imewasaidia hata wenye dhambi kubarikiwa. Rahabu alikua kahaba lakini yeye na ndugu zake waliokolewa kwa sababu ya “kamba nyekundu”.

Je kamba nyekundu ni nini? Kamba nyekundu ni mfumo wako wa maisha; jinsi unavyoishi na unayowatendea watu wengine, hasa “wateule” wa Mungu.

Kuna wakati Mungu huamua kukubariki si kwa sababu wewe ni mwema sana, bali kwa sababu kuna watu wema wanaoomba kwa ajili yako. Inawezekana tangu uanze kuomba, maombi yako hayajawahi kufika kwa Mungu lakini unabarikiwa, kwa sababu ya kamba nyekundu.

Kuna watu ambao ni “wateule” wa Mungu, kwahiyo kadri unavyowatendea mema hao watu baraka zinakuja kwako “automatically” hata kama wewe si mkristo. Rahabu aliwatendendea mema wapelelezi wa Israel baraka zikaenda kwake “automatically” bila kujalisha kwamba alikua kahaba.

Yatima, wajane, maskini, wazee, wagonjwa na wengine wenye uhitaji ni wateule wa Mungu. Kwahiyo ukiwatendea mema watu hawa baraka zinakuja kwako hata kama wewe ni mwenye dhambi.

Kwa mfano kama kuna watoto yatima unawasomesha, au kuna wajane unawasaidia mahitaji yao, au wagonjwa unawasaidia matibabu, si rahisi Mungu kuondoa mkono wake wa baraka kwako hata kama wewe ni mwenye dhambi. Mungu akiondoa baraka kwako watu wake watateseka.

Wale yatima, wajane, wagonjwa ambao wewe ni msaada kwao kila wakiomba Mungu huongeza baraka kwako ili uzidi kuwahudumia. Inawezekana maombi yako hayafikagi kwa Mungu lakini unabarikiwa kwa sababu ya maombi ya hao unawaosaidia.

Kuna wakati Mungu anaweza kuamua kuzipiga dhoruba biashara za wenzako, lakini ya kwako ikasimama imara. Si kwa sababu wewe ni mwema sana, bali kwa sababu kuna watu wanamlilia Mungu kwa ajili yako. Kuna wanategemea ada za shule kwenye hiyo biashara yako. Kuna watu wanategemea pesa za matibabu kwenye biashara yako. Kwa hiyo Mungu akiyumbisha biashara yako atakua anawaumiza watu hao. So ili asiwaumize anaamua kukuaacha. Hiyo ni kamba nyekundu.!

Kuna wakati wenzio wakifanya makosa madogo kazini wanafukuzwa kazi, lakini unajishangaa wewe umefanya makosa makubwa na hufukuzwi. Si kwa sababu una bahati sana. Ni kamba nyekundu. Kuna watu walioko nyuma yako ambao ni wateule wa Mungu. Kuna yatima wanategemea kulipiwa ada kwa mshahara wako, kuna wagonjwa wanategemea kusaidiwa hela za matibabu kwenye mshahara wako, kuna wajane wanategemea hela ya kuishi kutoka kwako. Kwahiyo Mungu akikuadhibu anakua amewaadhibu na wao. Kwahiyo ili wapone inabidi akulinde hata kama umefanya kosa kazini. Unashangaa tu kesi imeisha hata kwa namna ambayo hujui. Hiyo ni kamba nyekundu.!

Kuna mtu ambaye ni maskini wa kutupwa hana hata uwezo wa kununua sukari. Lakini anamuomba Mungu kwa imani kuwa ampe sukari aweze kunywa chai kila siku. Kwa kuwa huyo maskini huwa anapata sukari kutoka kwako, Mungu atazidi kukubariki ili uendelee kumhudumia huyo maskini. Hiyo ni Kamba nyekundu.!

Kamba nyekundu ilimuokoa Rahabu na ndugu zake licha ya kwamba alikua kahaba. Jiulize wewe una kamba nyekundu? Je kuna watu wako nyuma yako ambao Mungu akiwaangalia anakubariki, anakuokoa hata kama upo kwenye hatari?

Kama unamsomesha mwanao shule ya “mamilioni” kwa mwaka wakati mtoto wa jirani yako hana hata uniform za kuendea shule, au unatumia “mamilioni” kwa pombe na starehe wakati kuna wagonjwa wanaokufa kwa kukosa panadol, siku Mungu akitaka kukuadhibu hajiulizi mara mbili maana huna “kamba nyekundu” nyuma yako.

Lakini yule anayesaidia wenye uhitaji, kama yatima, wagonjwa, wazee, wajane,walemavu, au maskini atazidi kubarikiwa tu hata kama ni mwenye dhambi, maana anayo kamba nyekundu.

Hii ni kwa sababu Mungu akitaka kumuadhibu, kabla hajamtizama yeye anatizama kwanza yatima walioko nyuma yake anaowasaidia, anatizama wagonjwa wanaomtegemea kwa matibabu, anatizama wajane. Anaona akimuadhibu, atakuwa ameadhibu na hao wanaomtegemea. Kwa hiyo anaamua kumuacha.

Hii ina maana kuwa baraka na utakatifu ni vitu viwili tofauti. Unaweza usiwe mtakatifu lakini Mungu akakubariki na akakulinda. Unaweza kubarikiwa si kwa sababu unastahili, bali kwa sababu kuna “wanaostahili” wapo nyuma yako wakikupigania kwa baba yao (Yehova). Ndio maana kuna watu wengi wasio Wakristo wanabarikiwa kila siku hata kama hawamjui Mungu. Ni kwa sababu wana “kamba nyekundu”.

Malisa G.J

Read and Write Comments

Ishi kama Penseli ili uwe mtu bora

Muumbaji wa penseli alipomaliza kuiumba penseli yake aliiambia mambo muhimu ya kuzingatia ili iweze kuwa penseli bora kabla hajaituma kuingia kazini kwa matumizi.

“Kuna vitu sita unatakiwa uvitambue, “ Aliiambia penseli,

“Kabla sijakutuma kwenda kutumika, unatakiwa uviweke akilini vitu hivyo na usivisahau kamwe. Vitakusaidia siku zote na utakuwa penseli bora maisha yako yote.”

Alisema muumbaji wa penseli.

“Moja,” alianza kuvitaja,”utakuwa na uwezo wa kufanya vitu vingi, lakini kama utakubali na utaruhusu kuongozwa na mkono wa mtumiaji wako”

“Mbili” aliendelea kutoa nasaha, “utapata maumivu makali kutokana na kuchongwa mara kwa mara. Lakini vumilia kwani itakusaidia kuwa penseli bora na kuandika vizuri.”

“Tatu, utakuwa na uwezo wa kusahihisha makosa utakayo yafanya.”

“Nne, kitu pekee cha muhimu katika maisha yako ni kile kilicho ndani yako kwa sababu ndicho chenye uwezo wa kuandika.”

“Tano” alisisitiza mtengenezaji penseli, “kwenye kila sehemu utakayotumika, utaacha alama yako. Hata ikiwa ni kwenye sehemu ngumu au mbaya kiasi gani, ni lazima alama yako ibaki.

“Na sita”, alimalizia muumbaji yule wa penseli, “ipo siku utaisha na kupotea. Hivyo usiwe na hofu wala woga wala hudhuni uikaribiapo siku hiyo na ukaogopa kutimiza wajibu wako kwa kuhofia kuisha. Ukiogopa kuisha hautotumika na umuhimu wako hautonekana kwani hautatimiza wajibu uliombiwa kuufanya”

Penseli ilielewa na kuahidi kukumbuka na ikaingia sokoni ikiwa na dhamira yake moyoni.

Sasa tutumie mfano huo wa penseli katika maisha yetu halisi. Ukivikumbuka vitu hivyo sita ilivyopewa penseli, utaweza kuwa mtu bora kabisa kwenye maisha yako yote.

Moja, una uwezo wa kufanya mambo mengi na makubwa, kama utajiweka kwenye mikono ya Mungu.

Mbili, utakutana na magumu mengi ya kuumiza, lakini hayo ndiyo yatakufanya uwe mtu imara na bora, usiyakimbie.

Tatu, una uwezo wa kurekebisha makosa yote uliyoyafanya. Usijilaumu.

Nne, sehemu yako ya muhimu ni ile iliyo ndani yako kwani ndiyo inayoandika maisha yako. Ilinde.

Tano, kila sehemu utakayopita, acha alama yako kwa kufanya mazuri yatakayokufanya ukumbukwe daima, bila kujali mazingira. Timiza wajibu wako kwa kiwango cha juu.

Sita, tambua kuwa ipo siku utakufa. Usiwe na hofu yoyote juu ya kifo kwani ukiogopa kifo hutafanya lolote hapa duniani.

Tumia mfano huu wa penseli upate ujasiri wa kutambua kuwa wewe ni mtu muhimu hapa duniani na umeumbwa kwa madhumuni maalumu na umepewa uwezo mkubwa sana na Muumba wako! Ni wewe pekee mwenye uwezo wa kutimiza dhamira uliyotumwa na Muumba.

UBARIKIWE SANA.

Read and Write Comments

Maana halisi ya kuolewa au ya kuwa mke

NDOA sio kichaka cha kujificha kukimbia matatizo. NDOA sio mahali pa kutolea mkosi. Wala sio mahali pa kupunguzia shida. Ndoa sio mbadala wa elimu na michakato ya kimaisha. Huolewi ili kupunguza adha za maisha. NDOA ni jukumu zito kuliko hata kusoma masters degree ya Neuro-surgeon. Wengi hamjaweza kumudu maisha yenu binafsi na bado mnalilia Mungu kuwaongezea jukumu la kumeneji maisha ya mtu mwingine.

Kama huwezi hata kujitafutia hela ya kusuka nywele zako utawezaje kuendesha maisha ya familia. Maana unaweza kuolewa na mwanaume mwenye pesa lakini akapitia mithihani pesa zikatoweka utafanyaje kama huna akili ya kujiongeza? Ndio maana wengi mnawakataa watu wenye Ndoto lakini hawanapesa kwa sasa kwa sababu ya akili ya utegemezi. Unataka mwanaume mwenye kila kitu, sababu kubwa ni uvivu na uzembe. Hutaki kujitafutia vya kwako.
Ukisoma MITHALI 31 inaeleza habari za MKE MWEMA.

Hapo ndio pa kujipima je unakidhi hivyo viwango? Mke mwema sio tegemezi ila ni mwanamke mwenye uhuru wa kifedha (Financial Freedom). JIULIZE TU KAMA IKITOKEA HUJAOLEWA MIAKA MITANO IJAYO UTAKUWAJE? MAISHA YAKO YATAKUWAJE? UTAKUWA NA HALI GANI? Maswali kama haya yatakusaidia kujiongeza. Tafuta kitu cha kufanya hata kama Ndoa isipotokea leo isiwe mwisho wa maisha, Ndoto na maono yako. Siku hizi wanaume hawaulizi ukoo wanauliza UNAFANYA NINI?

Mtu anapiga hesabu akikuoa mkaunganisha nguvu mtafanya nini kwenye maisha. Sasa wewe kalia kubandika kope na kuchora kucha kutwa nzima huna shughuli ya kufanya huku ukingoja kuombewa upate Mume. Watu hawaoi mapambo wanataka Wake watakao tengeneza nao hatma zao. Pambo ni kwaajili ya Starehe lakini MKE ni kwaajili ya maisha. Sikupondi wala sio nia yangu kukuvunja moyo, nataka utoke hapo ulipo ujiongeze ili hata ukiingia kwenye Ndoa isijae visa na kuonewa. Pesa itakupa heshima, pesa inakupa sauti, hata Wakwe zako hawawezi kukunyanyasa ukiwa na pesa kwani wanajua watakosa vitenge.

Nataka nikwambie kweli, ukiwa na hela utachagua mwanaume wa kukuoa kwani wapo wengi ila kama umefulia, tegemezi kweli utaona wanaume ni wachache. Pata kitu cha kufanya, tengeneza milango ya kipato. Badala ya kukesha unaomba Mungu akupe Mume anza kuomba Mungu akupe uhuru wa kifedha, kama itakubidi kurudi shule rudi tu. Jiongeze usibaki hapo ulipo. Ni Yesu peke yake asiyebadilika (Hebrania 13) Lakini wanadamu wote lazima tubadilike kila kukicha tukihama hatua moja kwenda nyingine.

Mungu akufungue macho kuona kiini cha ujumbe huu na lengoF lake na wala usichukuliwe na upepo wa adui upindishao maana katika jumbe zenye kubadilisha maisha kama hii.

Kuolewa sio mwisho wa maisha, Mungu kwanza achukue nafasi kwenye maisha yako na akupe utoshelevu katika moyo wako kiasi kwamba uone hata bila Mume unaweza kuishi.

Read and Write Comments

Ufalme wa simu wa sasa

➡ Asubuhi saa 12 : 00 mtu anaamka, kabla hata HAJAMUSHUKURU MUNGU, kabla hata hajatoka kitandani, kabla hata hajajifunua shuka,

👉ATARIPOTI KWA SIMU KWANZA KABLA YA KURIPOTI KWA YEYOTE, NDIO HAPO UNAONA MTU AKIAMKA KABLA HATA HAJASALI KWA MUNGU ANAAMKIA SIMU KWANZA KUIKAGUA,
– Nani alinitafuta?
-Nani alini-text?
-WhatsApp nani kanitumia msg?
– kwenye magroup kuna mpya gani?
– Fb kuna post gani kali?
– nani kaweka picha kali leo?
Nk.
Akimaliza KURIPOTI KWA Simu, faster faster, anapiga kaombi ka kidesturi, sekunde 20 basi.
Biblia ipo hapo kando tu ya kitanda, lkn anaona hana muda wa kuisoma.
✴BADALA YA KUANZA SIKU NA BWANA, MTU ANAANZA SIKU NA SIMU.
Pamoja na kazi za kuutwa, za mtu huyo, lkn atafanyq juu chini, apate muda wa KURIPOTI kwa SIMU.
Lakini mtu huyo huyo, hawez kbsa kupata muda wa kujitenga angalau kwa dk 3 tu, kw kutwa nzima ARIPOTI KWA MUNGU KWA NJIA YA MAOMBI.
Ana muda wa kusoma status kwenye social media kutwa nzima,
Lkn hana muda kbsa wa kupitia angalau sura moja tu, ya Biblia kwa siku.
Ana bundle la dk, sms, WhatsApp kila siku, lkn hana sadaka ya kumtolea Mungu.
Umeme ukikatika kutwa moja tu, akakosa kuwa na simu sababu ya chaji, anajisikia mpwekee, siku anaiona ndefuu, anajiona amepungukiwa saana!
Lakini huyo huyo, siku nzima inaisha, na ya pili, ya tatu , hajawahi kuwa na muda na Mungu wake hata kidogo, na anaona ni sawa tu.
Hata ktk siku ya ibada, yale masaa machache tu ya ibada, ambapo inatakiwa iwe ni mtu na Mungu wake tu, bila kuingiliwa na chochote, 👉mtu bado hawezi kukaa bila KURIPOTI kwa simu, ibada inaendelea huku mtu kawasha data, na anasoma na kujibu msg zake km kawaida.
👉 au kama ana kaustaraabu kidogo, atatoka nje, huko anaenda kukagua msg, kuangalia updates nk.
SIMU UNAYO KUTWA, KUCHWA, KIIILA SIKU, YANI HUKUWEZA KUVUMILIA KUIWEKA PEMBENI KWA MASAA TU?
➡ Swali nauliza, Mtu wa aina hiyo Mungu wake ni nani?
” Usiwe na miungu mingine ila mimi”.
KUTOKA 20 : 3
Kumuabudu Mungu peke yake, ni kumfanya Mungu awe wa KWANZA MOYONI NA MAWAZONI MWAKO.
Kumfanya awe kipaumbele kwenye kiila ulitendalo.
➡WENGI WAMEZIFANYA SIMU ZAO, ZICHUKUE NAFASI YA MUNGU KATIKA MIOYO, FIKRA NA MAISHA YAO KWA UJUMLA.
➡Wamekuwa tayari kupoteza karibu kiila kitu kwa ajili ya simu
– kupoteza marafiki > hawana muda na marafiki zao, wanajifungia ndani, wakichati.
– hawana muda na wazazi wao, hata kama wanaishi nyumba moja. > kijana akifika nyumbani, anapitiliza chumbani, ni yeye na simu, ataonekana muda wa kula tu, tena sometimes hata mezani anakuwa na simu, pale mezani wako wazazi wake kbsa, ndugu zake nk, lkn hajali uwepo wao, anaendelea na simu tu.
– Hawana muda na Mungu > Anahakikisha vyovyote itakavyokuwa, muda wa kuwa na simu unapatikana, HATA KAMA HILO LITAMAANISHA KUUPORA MUDA WA MUNGU (muda wa ibada).
Atakosa fedha za kusaidia wahitaji, fedha za zaka na sadaka, lkn fedha ya SIMU, (bundles) , lzm inakuwepo.
➡Mtu wa aina hiyo, anaiabudu simu bila kujua.
➡KITU CHOCHOTE KINACHOUVUTA MOYO KUTOKA KWA MUNGU, KUKIELEKEA CHENYEWE, KITU HICHO KINAJARIBU KUCHUKUA NAFASI YA MUNGU MOYONI.
NB: Sio lengo langu kupinga matumizi ya simu, lkn nilitaka tuwe na kiasi.

Read and Write Comments

Usipite bila kusoma kisa hiki cha kusisimua

Siku moja jioni katika mji flani, kulikuwa na basi likisafiri kutoka mji huo kuelekea mji mwingine. Lilikuwa ni basi kubwa na limejaa abiria. Wakati wakiendelea na safari, ghafla, mvua kubwa iliyoambatana na radi ikaanza kunyesha. Dereva hakuogopa, wala abiria, wakaendelea na safari. Mara wakati wanaenda, radi ikaanza kufuatilia gari. Kila wakienda, radi inapiga karibu na basi kana kwamba inalifuata basi. Likisimama, radi inapiga pembezoni mwa basi.

Dereva kuona hivyo, akasimamisha gari mita 5 kutoka kwenye mti… Akawaambia abiria, “Humu ndani ya basi, kuna mtu ambaye leo ni siku yake ya kufa, tena kufa kwa radi. Ili tusife wote, nataka kila abiria ashuke akaguse mti ili anayepigwa na radi, apigwe wengine wasife kwa ajili yake. “Abiria wakitetemeka, wakaanza kushuka mmoja mmoja. Unaenda unagusa mti , kisha unarudi kwenye basi. Abiria wote pamoja na dereva mmoja mmoja, wakaenda, wakagusa mti na kurudi bila dhara lolote! Akawa kabaki abiria mmoja tu, ambaye alikuwa hajagusa mti. Abiria wote kwa macho ya hasira wakamwambia akaguse mti. Akawa anaogopa kufa. Akagoma. Wakamlazimisha kwa nguvu sana na kumtoa nje……. …….. Yule abiria akiwa amefumba macho, akaenda akagusa mti. Hamadi bin Vuu! Radi kali sana ikalipiga basi, abiria na wote waliokuwamo, wakafa palepale. Kumbe uwepo wake ndio ulikuwa unazuia abiria wengine wasidhurike na radi.

MAFUNZO

1. Unapofanikiwa, huwezi jua uwepo wa nani umefanikisha mafanikio yako, usichukue sifa zote peke yako. Wapatie na wengine bila kumsahau MUNGU.
2. Unaweza kujiona huna thamani sehemu ulipo, iwe kwenye kundi la WhatsApp, darasani, kazini, kwenye basi, barabarani bila kujua kama uwepo wako ni wa muhimu sana kwa ustawi wa wengine.
3. Usimtenge wala kumnyanyasa mtu au jirani yako, huwezi jua uwepo wake ni kwa ajili gani.

Read and Write Comments
Shopping Cart
0
    0
    Your Cart
    Your cart is emptyReturn to Shop