Mungu Anatuita Na Kutupa Nafasi Ya Kutubu Na Kumrudia Yeye Ili Atusamehe na Kutubariki

Tunaalikwa kutubu na kumrudia Mungu kwa Mioyo yetu yote na kwa nia dhabiti. Mungu ni mwaminifu, atatusamehe dhambi zetu na kutufanya kuwa wapya.

Dawa ya dhambi ni kutubu na kusamehewa.

Kutubu sio kusema tuu “Ninatubu” au “Ninaomba msamaha”. Kutubu ni kuona uchungu kweli rohoni kwa dhambi tulizotenda, tukizikataa na kunuia kutokuzitenda tena.

12“Lakini hata sasa,”
nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
“Nirudieni kwa moyo wote,
kwa kufunga, kulia na kuomboleza.
13Msirarue mavazi yenu kuonesha huzuni
bali nirudieni kwa moyo wa toba.”
Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu;
yeye amejaa neema na huruma;
hakasiriki upesi, ni mwingi wa fadhili;
daima yu tayari kuacha kuadhibu.
14Huenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atabadili nia
na kuwapeni baraka ya mazao,
mkamtolea sadaka za nafaka na kinywaji.
15Pigeni tarumbeta huko Siyoni!
Toeni amri watu wafunge;
itisheni mkutano wa kidini.
16Wakusanyeni watu wote,
wawekeni watu wakfu.
Waleteni wazee,
wakusanyeni watoto,
hata watoto wanyonyao.
Bwana arusi na bibi arusi
na watoke vyumbani mwao.
17Kati ya madhabahu na lango la hekalu,
makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu,
walie na kuomba wakisema:
“Wahurumie watu wako, ee Mwenyezi-Mungu.
Usiyaache mataifa mengine yatudharau
na kutudhihaki yakisema,
‘Yuko wapi basi Mungu wao?’” Yoeli 2:12-17

Uzuri wa Mungu ni kwamba anasamehe na kusahau, tunapotubu dhambi zetu Mungu anatufutia makosa yetu, anaponya majeraha au madhara yaliyoletwa na dhambi hiyo na kisha antubariki kwa Neema na Vipawa vya kusonga Mbele.

Maana nitawasamehe makosa yao, wala sitazikumbuka tena dhambi zao.” Yeremia 31:34

Mungu anatambua kwamba Binadamu ni dhaifu na anaweza kuanguka dhambini ndio maana anatupa nafasi ya Kutubu na Kumrudia yeye.

13Afichaye makosa yake hatafanikiwa;
lakini anayeungama na kuyaacha atapata rehema. Methali 28:13

Mungu anazifahamu juhudi zetu katika kutafuta kutenda mema ndio maana anakubali toba ya kweli na anatupa matumaini ya kusonga mbele.

“Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”. Isaya 1:18

Biblia inatuambia kuwa anaheri yule atubuye na kusamehewa kosa lake kwa sababu hana hatia mbele ya Mungu.

1 Heri yake mtu aliyesamehewa kosa lake,
mtu ambaye dhambi yake imeondolewa kabisa.
2Heri mtu ambaye Mwenyezi-Mungu hamwekei hatia,
mtu ambaye hana hila moyoni mwake. Zaburi 32:1-2

Tunapaswa kukumbuka kuwa toba ya kweli ya kutupa msamamaha inaambatana na kuwasamehe wengine na kuondoa kinyongo kwa wengine waliotukosea. Yesu anatufundisha kuwa inatupasa tusamehe ili na sisi tusamehewe.

14“Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia. 15Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu. Mathayo 6:14-15

Tena, Mungu anatusamehe Makosa Yetu bila kujali tunakosea Mara nagpi na tunarudi kwake mara ngapi. Ndio maana Yesu alitufundisha kuwa tunapokosewa na wenzetu ni lazima tuwasamehe haijalishi wametukosea mara ngapi.

3Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, muonye; akitubu, msamehe. 4Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema, ‘Nimetubu,’ lazima umsamehe.” Luka 17:3-4

Unapotubu na kuomba msamaha ni sharti uwasamehe pia wale waliokukosea ili na wewe usamehewe. Kusameheana na wenzetu ndio tabia ya Kimungu ambayo yatupasa kujifunza na kuiishi ili na sisi tuwe watoto wema wa Mungu.

12Nyinyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe nyinyi. Wakolosai 3:12-13

Tumuombe Mungu atujalie Moyo wa toba na kujirudi kwake Kila tunapokosea. Na tumuombe pia atupe nguvu na uwezo wa kuwasamehe wale wanaotukosea.

KUMBUKA: Unapotubu dhambi zako na kusamehewa ndipo inapokuwa rahisi kwa sala zako kujibiwa. Mungu ni rafiki ya waliosafi Moyoni, na ndio anaowasikiliza na kuwaonyesha nguvu na uwezo wake.

Melkisedeck Leon Shine

Editor: Melkisedeck Leon Shine. About Me | Contact Me | LinkedIn | TikTok | WhatsApp

Read and Write Comments

Views: 0

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Shopping Cart