Neno Bwana lina maana gani katika Biblia?
Neno Bwana Katika Biblia linamaanisha “Mungu Mtawala”
Mapokeo ya Mitume ndiyo nini?
Mapokeo ya Mitume ndiyo yale yote ambayo Yesu aliwakabidhi Mitume wake, na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu yatadumu hata mwisho wa dunia katika mafundisho, liturujia na maisha ya Kanisa.
“Nawasifu, kwa sababu mmenikumbuka katika mambo yote, nanyi mmeyashika yale mapokeo vilevile kama nilivyowatolea… Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe” (1Kor 11:2; 15:3).
“Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu… Mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine” (2Tim 1:14; 2:2).
Tukikata huo mnyororo wa mapokeo, hata kama ni kwa kisingizio cha kushikilia Biblia, tunaachana na asili ya Kanisa.
“Basi, ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa waraka wetu… Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu” (2Thes 2:15; 3:6).
Maandiko Matakatifu ndiyo nini?
Maandiko Matakatifu ndiyo vitabu vyote 73 ambavyo viliandikwa na watu kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu vikakusanywa na Kanisa kwa jina la “Biblia”, yaani “Vitabu”.
Hao “wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu” (2Pet 1:21).
Je, Biblia zote ni sawa?
Hapana, Biblia zote si sawa. Tujihadhari na matoleo mapungufu ambamo vimenyofolewa vitabu 7 vizima na sehemu kadhaa za vitabu vingine vilivyotumiwa na Wakristo wa kwanza.
“Amin, nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie” (Math 5:18). “Na mtu yeyote akiondoa lolote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki” (Ufu 22:19).
Je wakristo Wakatoliki wanasoma Biblia kwenye Ibada ya Misa? Biblia inanukuliwa mara ngapi Kwenye Ibada ya misa ya Wakatoliki?
Ndiyo, Wakatoliki wanasoma Biblia kila siku wanapoadhimisha Ibada ya Misa wakati wa Liturujia ya Neno.
Wakatoliki wananukuu Biblia mara Tano kwenye Ibada ya Misa. Wananukuu wanaposoma somo la Kwanzaa, Somo la pili, wimbo wa katikati, Shangilio na Injili.
Tunatambuaje Maandiko Matakatifu kati ya maandishi yote ya binadamu?
Tunatambua Maandiko Matakatifu kati ya maandishi yote ya binadamu kwa njia ya Mapokeo, yaani kwa sababu yametumiwa na Kanisa tangu mwanzo kwa kulisha kwa hakika imani yake.
Tunahitaji Mapokeo kwa kuwa Maandiko yenyewe hayataji orodha ya vitabu vyake vyote, Sanasana Yesu alividokeza baadhi akisema yanamzungumzia na kutimia ndani yake,
“Ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi” (Lk 24:44).
Halafu Barua ya Pili ya Mtume Petro ikalinganisha “na Maandiko mengine” nyaraka zote ambazo Paulo aliziandika “kwa hekima aliyopewa” (2Pet 3:15-16).
Sababu nyingine za Biblia kutojitosheleza ni zipi?
Sababu nyingine za Biblia kutojitosheleza ni kwamba mambo mengi muhimu hayakuandikwa,
“Kuna mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu, ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa” (Yoh 21:25).
Tena barua ni nusu tu ya kuonana; hivyo Yesu hakuandika lolote, nao Mitume hawakupenda kuandika yote.
“Kwa kuwa ninayo mambo mengi, sitaki kuyaandika kwa karatasi na wino; lakini nataraji kuja kwenu, na kusema nanyi mdomo kwa mdomo, ili furaha yetu iwe imetimizwa” (2Yoh 12).
“Nalikuwa na mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kukuandikia kwa wino na kalamu. Lakini nataraji kukuona karibu, nasi tutasema mdomo kwa mdomo” (3Yoh 13-14).
Hasa ibada haziwezi kufanyika kwa barua; k.mf. kuwekea mikono ili kumshirikisha Roho Mtakatifu. Paji la namna hiyo halipitii Maandiko, bali Mapokeo tu. Hatimaye Biblia ikipotoshwa haipingi, kwa kuwa si mtu hai anayeweza kujitetea.
Biblia iliandikwa kwa kusudi gani?
Biblia iliandikwa kusudi tupate “kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini” tuwe “na uzima wa milele” (Yoh 20:31).
“Tangu utoto umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila Andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki” (2Tim 3:15-16).
Si lengo lake kutufundisha historia, jiografia wala sayansi: kuhusu elimu hizo na kuhusu ufasaha wa lugha Biblia ilitegemea ujuzi na vipawa vya watu walioiandika.
Je, vitabu vya Biblia vinatofautiana?
Ndiyo, vitabu vya Biblia vinatofautiana kwa kuwa Mungu alijifunua hatua kwa hatua; hivyo vitabu 46 vilivyoandikwa kabla ya Yesu vinaitwa Agano la Kale na 27 vilivyomfuata vinaitwa Agano Jipya.
“Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka” (Eb 8:13).
Mungu “ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha” (2Kor 3:6).
Je, vitabu vyote vya Biblia vinahusiana?
Ndiyo, vitabu vyote vya Biblia vinahusiana kwa kuwa vinaangaziana na kuunda kitabu kimoja ambacho ni Neno la Mungu yuleyule, ingawa katika hatua tofauti: Agano la Kale ndiyo maandalizi na Agano Jipya ndio utimilifu wake.
Yesu alisema, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza” (Math 5:17).
Tunahitaji Agano la Kale ili tuelewe vizuri Agano Jipya katika maandalizi yake, na tunahitaji Agano Jipya ili tuelewe Agano la Kale lilivyotimilizwa na Yesu.
Je, inafaa tushike neno lolote la Agano la Kale kama Wayahudi?
Hapana, haifai tushike neno lolote la Agano la Kale kama Wayahudi wasiozingatia jinsi Yesu alivyolitimiliza kwa maneno na matendo hata wakamshutumu kutenda kinyume:
“Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato” (Yoh 9:16).
Alipofafanua amri 10 za Mungu alikariri:
“Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa… lakini mimi nawaambieni…” (Math 5:21,27,31,33,38,43).
Alipouliziwa unajisi wa vyakula kadhaa, alisisitiza,
“’Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni?’ Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote” (Mk 7:18- 19).
“Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo” (Kol 2:16-17).
Hakika, mwili ni mzito kuliko kivuli chake.
Vile vile katika Warumi 4:16. Tunasoma “Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi hiyo ni kwa ajili ya wote:si kwa wale tu wanaoishika sheria, bali kwa wale waishio kwa Imani kama Abrahamu. Yeye ni Baba yetu sote.”
Wakristo wengine wanachanganywa na wale wasioyajua maandiko na kuwataka washike sheria na Torati,basi tukisema ni lazima kushika sheria tutakua tunakataa kua Abrahamu hakuwa mtu wa Mungu maana kwa Abrahamu hatukuwa na Sheria wala Torati na alipata kibali machoni Pa Mungu tuu kwa Imani. Kumbuka pia Abrahamu alitahiriwa baada ya Kuwa tayari mtu wa Mungu kwa Imani yake na sio kwamba Kutahiriwa ndio kulifanya mtu wa Mungu.
Tumekombolewa kwa Imani na sio kwa Sheria. Wagalatia 5:18 “Lakini Mkiongozwa na Roho hampo chini ya sheria”
Hatumtumikii Mungu ili tuwe watu wa Mungu bali tukishakua watu wa Mungu ndio tunamtumikia Mungu.
Yesu alitimiliza Agano la Kale kwa namna isiyotarajiwa hasa lini?
Yesu alitimiliza Agano la Kale kwa namna isiyotarajiwa hasa aliposulubiwa, akionekana na Wayahudi wenzake kama kwamba amelaaniwa:
“Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa: ‘Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti’; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani” (Gal 3:13-14).
Kati ya vitabu vya Biblia, vilivyo bora ni vipi?
Kati ya vitabu vya Biblia, vilivyo bora ni Injili 4 zilizoandikwa na Mathayo, Marko, Luka na Yohane.
Ndio moyo wa Maandiko Matakatifu yote, kwa kuwa ndizo shuhuda kuu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu.
Yeye “amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora. Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili” (Eb 8:6-7).
Tueleweje Maandiko Matakatifu?
Tuelewe Maandiko Matakatifu kwa kuzingatia hasa Mungu alitaka kusema nini kuhusu wokovu wetu kupitia waandishi wengi aliowaongoza kuyatunga kwa lugha na mitindo mbalimbali.
Lakini ebu, “Yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na Maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe” (2Pet 3:16).
Utitiri wa madhehebu yanayoshindana yakidai kushikilia Biblia tu unathibitisha uwekezano mkubwa wa kuipotosha kwa namna moja au nyingine.
“Utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia walimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo” (2Tim 4:3-4).
Njia pekee ya kukwepa fujo hiyo ni kuelewa Maandiko ndani ya Kanisa, kadiri ya Mapokeo yake hai.
“Lakini mtu yeyote akitaka kuleta fitina, sisi hatuna desturi kama hiyo, wala makanisa ya Mungu” (1Kor 11:16).
Biblia nje ya Kanisa ni kama samaki nje ya maji.
Tupokeeje ufunuo wa Mungu?
Tupokee ufunuo wa Mungu kwa kusadiki mafundisho ya Kanisa lake, ili tuzidi kumjua na kuambatana naye bila ya kudanganyika. Yesu aliwaambia Mitume wake,
“Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma” (Lk 10:16).
“Sisi nasi twamsukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kwelikweli, litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini” (1Thes 2:13).
Neno “BIBLIA” maana yake ni nini?
Neno “BIBLIA” ni neno linalotokana na neno la Kigiriki “Biblion” lenye maana ya vitabu.
Biblia ni Mkusanyiko wa vitabu mbalimbali vya dini vilivyochaguliwa na kuidhinishwa kua vyafaa kutumika.
Biblia ni nini? Asili, Historia, waandishi na mipaka yake
Biblia ni mkusanyiko wa vitabu mbalimbali vinavyohusu kazi ya Mungu ya kuwakomboa mwanadamu kuanzia enzi za Mababu na manabii Wa Waisraeli, Enzi za Yesu na za Mitume wa Yesu.
Je, Biblia ilipatikanaje? Nini chanzo na asili ya Biblia.
Biblia iliundwa kwa kukusanya vitabu vya dini vya wakristo hapo awali na kuunda kitabu kimoja. Kwa maana hii, Biblia ni vitabu teule vya dini vilivyoonekana vinafaa kutumika kwa waumini Wakristo ili kusaidia Imani yao. Hivyo basi, kama Biblia ni vitabu teule tuu vipo vitabu vingine vya dini ambavyo havikuwekwa Kwenye Biblia.
Wakristo wa kwanza walichagua vitabu kadhaa na kuviweka pamoja na kisha kuvita Biblia. Biblia ni mkusanyiko wa vitabu muhimu tuu vya dini mpaka kufikia Enzi za Mitume.
Je, Biblia ndicho kitabu pekee cha neno la Mungu?
Hapana, Biblia sio kitabu pekee cha neno la Mungu isipokua Biblia ni kitabu kilichoidhinishwa rasmi kutumika Kama kitabu kikuu cha Wakristo. Hii ni kwa sababu Biblia imeundwa na vitabu muhimu tuu vilivyochaguliwa na wakristo wa kwanza vilivyoonekana vinafaa kwa kufundishia, Ibada na kukuza Imani. Kwa hiyo basi vipo vitabu vingine ambavyo haikuwekwa Kwenye Biblia ambavyo ni Maneno ya Mungu.
Hii ndiyo sababu kwa nini Wakatoliki wana vitabu vingi kuliko madhehebu Mengine. Yaani sababu ni kwamba madhehebu Mengine walivitoa vitabu vingine vilivyounda Biblia. Na Wakatoliki waliweka vitabu vingine vya dini Kwenye Biblia walivyoona vinafaa pia kutumika.
Je nje ya Biblia hakuna Neno la Mungu au Maandiko matakatifu?
Nje ya Biblia kuna Neno la Mungu na Maandiko Matakatifu. Hii Inamaanisha kuwa Biblia sio kitabu pekee cha neno la Mungu. Zipo nyaraka na Vipo vitabu vingine vingi ambavyo viliandikwa na Manabii na Mitume ambavyo havikuwekwa kwenye Biblia lakini ni mafundisho ya Mungu. Biblia ni mkusanyiko wa vitabu vikuu vya Mungu.
Kumbuka kuwa sio nyaraka zote za Mitume ziliandikwa Kwenye Biblia. Vile vile manabii walikuwa ni wengi kuliko waliowekwa Kwenye Biblia.
Je Biblia ndiyo mafundisho ya Mungu pekee?
Hapana, Biblia sio mafundisho pekee ya Mungu. Hii ni kwa sababu sio mambo yote aliyofanya na kusema Mungu yaliandikwa na vilevile Mitume hawakua watu wa Mwisho kupokea Roho mtakatifu na kupokea neno la Mungu.
Biblia inatuthibitishia yenyewe kuwa haijakamilika na Si mambo yote yameandikwa Kwenye Biblia
Biblia inatuthibitishia kuwa haijakamilika tunaposoma (Yohane 21:25)
Biblia inatuambia hivi…”Kuna mambo Mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo Kama yangeandikwa yote, moja baada ya jingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa.”…Kwa mstari huu Biblia inatuthibitishia kuwa haikuandikwa vitu vyote.
Je Biblia ni mwisho wa Maandiko ya Mungu?
Biblia sio mwisho wa Maandiko ya Kimungu.
Biblia ni sehemu ya maneno ya Mungu mpaka miaka ya Mitume
Hata sasa Mungu anafanya kazi na watu wake kupitia Roho Mtakatifu na kwa kwa sababu hii Biblia sio mwisho wa kazi ya Mungu ya kusema na watu wake.
Mungu yu hai na anafanya kazi na watu wake mpaka sasa kwa kutumia vinywa vya watu Kama aliyofanya hapo awali.
Hata maneno unayohubiriwa sasa yanaweza kuwa ni kutoka kwa Mungu kwa maana hata waandishi wa Biblia walitumiwa na Mungu Kama wahubiri wa sasa. Mungu ni yule yule, Roho Mtakatifu ni yuleyule na Neno ni lile lile.
Kwa hiyo Biblia ni maneno yaliyochaguliwa mpaka enzi za Mitume. Vitabu vilivyofwata Baada ya Mitume japokuwa viliandikwa kwa Roho Mtakatifu havikuwekwa Kwenye Biblia.
Sababu ya Kanisa katoliki kutumia mapokeo na Maandiko ya Watakatifu
Kanisa katoliki linatumia mapokeo na Makala za watakatifu kwa Imani kuwa Mungu yule yule aliyefanya kazi tangu zamani anafanya kazi na watu wake mpaka sasa na hivyo Maandiko ya watu wa Mungu yanafaa kutumika kama yalivyotumika ya watu wa kale.
Yesu alituambia nini kuhusu Neno la Mungu na Mwendelezo wa kazi ya Mungu ya kusema na watu?
Yesu alituambia hivi katika (Yohane 16:12-15)..”Ninayo mengi ya kuwaambieni Ila kwa sasa hamuwezi kuyastahimili. Lakini atakapokuja huyo Roho wa Ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote. Maana hatasema kwa Mamlaka yake mwenyewe bali atasema atakayoyasikia na kuwajulisheni yatakayokuja. Yeye atanitukuza Mimi kwa kuwa atawajulisheni Yale atakayoyapata kutoka kwangu “…
Sasa basi,kama Roho Mtakatifu ni yuleyule na kazi zake ni Zile Zile za tangu Mitume, kwa nini hatukubali kuwa Anafanya kazi mpaka sasa kupitia watu wa Mungu? Kwa nini tunakataa mafundisho yao? Kwa nini tunashindwa kuelewa kuwa Biblia haikuwa mwisho wa Neno la Mungu? Kwa nini tunakana Mapokeo ya Watakatifu? Kwa nini hatuwaamini watumishi wake wa sasa?
Biblia ina sehemu kuu ngapi?
Biblia ina sehemu kuu 2 (mbili) ambazo ni
1. Agano la Kale (A.K)
2. Agano Jipya (A.J)
Agano la Kale lina vitabu vingapi?
Agano la Kale lina vitabu 46
Agano Jipya lina vitabu vingapi?
Agano Jipya lina vitabu 27
Biblia nzima ina vitabu vingapi?
Biblia nzima ina vitabu 73
Vitabu vya Agano la Kale vimegawanywa katika sehemu ngapi?
Vitabu vya Agano la Kale vimegawanywa katika sehemu 4 nazo ni
1. Vitabu vya Musa (5)
2. Vitabu vya Historia (16)
3. Vitabu vya Hekima (7)
4. Vitabu vya Manabii (18)
Vitabu vya Agano Jipya Vimegawanywa katika sehemu ngapi?
Vitabu vya Agano Jipya Vimegawanywa katika sehemu 4 nazo ni
1. Injili (4)
2. Kitabu cha Matendo ya Mitume
3. Nyaraka mbalimbali (21)
4. Kitabu cha Ufunuo
Vitabu vya Musa ni vipi?
Vitabu vya Musa ni
1. Mwanzo
2. Kutoka
3. Walawi
4. Hesabu
5. Kumbukumbu la Torati
Wainjili wanne Katika Agano Jipya ni wakina nani?
Wainjili wanne Katika Agano Jipya ni
1. Mathayo
2. Marko
3. Luka
4. Yohane
Kitabu cha kwanza na cha mwisho katika Agano la Kale ni vipi?
Kitabu cha kwanza na cha mwisho katika Agano la Kale ni
1. Cha kwanza ni Kitabu cha Mwanzo
2. Cha mwisho ni Kitabu cha Malaki
Kitabu cha kwanza na cha mwisho katika Agano Jipya ni vipi?
Kitabu cha kwanza na cha mwisho katika Agano Jipya ni
1. Kitabu cha kwanza ni Injili ya Mathayo
2. Kitabu cha mwisho ni Kitabu cha Ufunuo
Injili ni nini?
Injili ni Habari njema ya wokovu iliyoletwa na Yesu Kristo
Watoto wawili wa Adamu na Eva walkikuwa wepi?
Walikuwa ni Kaini na Abeli
Watoto wa Nuhu ni wepi?
Watoto wa Nuhu ni Shemu, Hamu na Nefteli
Mababu watatu wa Imani Katika Biblia ni wakina nani?
Mababu wa Imani ni Ibrahimu, Isaka na Yakobo
Watoto wa Yakobo ni Wepi?
Watoto wa Yakobo ni
1. Reubeni
2. Simeoni
3. Lawi
4.Yuda
5. Dani
6. Naftali
7. Gadi
8. Asheri
9. Isakari
10. Zabuloni
11. Yosefu
12. Benjamini
Nani aliwatoa Waisraeli MIsri na Kuwaongoza Katika nchi ya Ahadi?
Musa ndiye aliwatoa Waisraeli MIsri na Kuwaongoza Katika nchi ya Ahadi
Mungu alimpa Musa Amri Kumi wapi?
Mungu alimpa Musa Amri Kumi katika mlima wa Sinai
Vitabu vya Historia katika Biblia ni vipi?
Vitabu vya Historia katika Biblia ni
1. Yoshua
2. Waamuzi
3. Ruthu
4. 1 Samweli
5. 2 Samweli
6. 1 Wafalme
7. 2 Wafalme
8. 1 Mambo ya Nyakati
9. 2 Mambo ya Nyakati
10. Nehemia
11. Ezra
12. Tobiti
13. Yudith
14. Esta
15. 1 Wamakabayo
16. 2 Wamakabayo
Vitabu vya manabii katika Biblia ni vipi?
Vitabu vya Manabii ni
1. Isaya
2. Yeremia
3. Maombolezo
4. Baruku
5. Eekieli
6. Danieli
7. Hosea
8. Yoeli
9. Amosi
10. Obadia
11. Yona
12. Mika
13. Nahumu
14. Habakuki
15. Sefania
16. Hagai
17. Zekaria
18. Malaki
Vitabu vya Hekima Katika Biblia ni Vipi?
Vitabu vya Hekima ni
1. Yobu
2. Zaburi
3. Mithali
4. Mhubiri
5. Wimbo ulio Bora
6. Hekima ya Solomoni
7. Yoshua Bin Sira
Nyaraka za Mitume katika Biblia ni zipi?
Nyaraka za Mitume ni;
1. Waroma
2. 1 Wakorinto
3. 2 Wakorinto
4. Wagalatia
5. Waefeso
6. Wafilipi
7. Wakolosai
8. 1 Wathesalonike
9. 2 Wathesalonike
10. 1 Timotheo
11. 2 Timotheo
12. Tito
13. Filemoni
14. Waebrania
15. Yakobo
16. 1 Petro
17. 2 Petro
18. 1 Yohane
19. 2 Yohane
20. 3 Yohane
21. Yuda
Je, Bikira Maria alikua na watoto wengine Mbali na Yesu?
Je, Bikira Maria ni Bikira Daima au alizaa watoto wengine?
Jibu fupi ni kwamba Bikira Maria hakuzaa watoto wengine na hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu
Hapo zamani hakuna mkristu au dehebu lolote lililokuwa linapinga kuwa Bikira Maria sio Bikira Daima hata Waprotestanti/walokole waliamini Bikira Maria ni Bikira Hata Baada ya Kumzaa Yesu. Kwenye Miaka ya 1400-1600 Watu wote wakwanza waliopinga Kanisa Katoliki walikubali kuwa Bikira Maria ni Bikira daima wakiwemo Martin Lutha aliyeanzisha kanisa la Lutheran, John Calvin aliyeanzisha Ulokole/Protestanti, Mchungaji Ulrich Zwingli, Heinrich Bullinger, and Thomas Cranmer. Kwa miaka zaidi ya 350 Waprotestant/walokole waliendelea kuamini kuwa Bikira Maria ni Bikira Daima.
Lakini baadae wakristo wengi walianza kupinga kuwa Bikira Maria ni Bikira Daima.
Tunaweza kuthibitisha kuwa Bikira Maria hakuzaa watoto wengine kwa kunukuu Biblia Kama ifuatavyo;
1. Bikira Maria Alikuwa Bikira Kabla ya kumzaa Yesu
Biblia inatuambia wazi kwamba Bikira Maria alikuwa Bikira Kabla ya kumzaa Yesu Kama tunavyosoma katika Luka 1:26-35
26 Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27 kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28 Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe.” 29 Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30 Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31 Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33 Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” 34 Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?” 35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. (Luka 1:26-35)
2. Biblia Haiwataji ndugu wa Yesu wakati Yosefu na Maria walipokimbilia Misri kumficha Yesu na wakati waliporudi
19 Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, 20 akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumwua mtoto huyo wamekwisha kufa.” 21 Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea katika nchi ya Israeli. 22 Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao mwanawe Herode alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda katika mkoa wa Galilaya, 23 akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: “Ataitwa Mnazare.” Matayo 2:19-23
Kama wangekuwepo wadogo zake Yesu Biblia ingetuambia kwamba walikuwa wapi wakati huo na walikuwa na Yesu au la.
3. Biblia haituambii kuwa Yesu alikua na wadogo zake alipokuwa na miaka 12
Wakati wa Maria, Yoseph na Yesu walipoenda Yerusalemu Yesu akiwa na miaka 12 Biblia haituambii kuwa Yesu alikuwa na wadogo zake na walikuwa wapi. Kumbuka walikuwa na Desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka kwa ajili ya Pasaka familia nzima kama familia. Je hao watoto wengine walikuwa wapi. Kwa nini walikuwa na Yesu Mwenyewe? Maana yake ni kwamba Yesu hakuwa na Wadogo zake.
41 Wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. 42 Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43 Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. 44 Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. 45 Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta. 46 Siku ya tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. 48 Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, “Mwanangu, kwa nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni.” 49 Yeye akawajibu, “Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” 50 Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia. 51 Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. 52 Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu. (Luka 2:41-52).
Kwa hiyo Biblia haionyeshi kuwa Yesu alikuwa na kaka na dada wakati akiwa na miaka 12. Kama wangekuwepo wangetajwa hapa kuwa walikuwa pamoja na Wazazi wao kama Yesu au walikuwa na Yesu wakati anapotea. Biblia haituambii chochote kwa hiyo wakati huo hapakuwa na wadogo zake Yesu.
4. Kukosekana kwa neneo “Binamu” kwenye lugha ya Yesu
Wakristu wa kwanza pamoja na Yesu aliongea Kiaramaiki au Kiebrania. Katika lugha zote hizo hakuna neno “Binamu” kwa hiyo mabinamu walijulikana kama dada na kaka wa mtu. Kwenye Agano jipya Neno kaka na Dada lilitumika pia kuwakilisha binamu.
Biblia inapotuambia kuwa Kaka na dada zake Yesu haimaanishi kaka wa kuzaliwa bali ndugu au Binamu
55 Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?” (Mathayo 13:55-56)
Kwa hiyo wanaotajwa hapa ni ndugu wa Yesu kwa maana maneno kama; ndugu, kaka au dada lilitumika badala ya Binamu yaani mtoto wa shangazi au mjomba. Hapa juu Yosefu ametajwa kama kaka yake Yesu lakini tunajua kuwa Yosefu ni Baba yake Yesu. Baba na mwana hawawezi kuwa na jina sawa.
5. Biblia haitumii neno Ndugu, kaka au dada ikimaanisha ndugu wa kuzaliwa mama mmoja na baba mmoja
Sio mara zote Biblia imetumia neno Ndugu kumaanisha ndugu (Dada na Kaka) wa kuzaliwa yaani kaka na dada kwa mfano
Kwa kuangalia lugha ya Kiswahili na Kiingereza 1 Wakorintho 15:6 tunaona tafsiri tofauti.
KISWAHILI 6 Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa.
ENGLISH 6 After that, he appeared to more than five hundred of the brothers and sisters at the same time, most of whom are still living, though some have fallen asleep.
Kwa hiyo hapa neno kaka dada na ndugu linaonekana wazi halikumaanisha ndugu au kaka wa damu.
6. Undugu wa Yakobo, Simoni, Yosefu na Yuda kwa Yesu Sio wa mtu na kaka zake
Wasemao kuwa Bikira maria alikuwa na wana zaidi ya Yesu wananukuu kifungu hiki;
55 Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?” (Mathayo 13:55-56)
Kumbuka kulikuwa na Yakobo wawili wakati wa Yesu, Vifungu vifuatavyo yunaweza kuona kuwa kulikuwa na yakobo wawili ambao walikuwa ndugu za Yesu lakini sio kaka wa kuzaliwa kwa mama.
35 Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.” (Marko 10:35)
55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. 56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. (Matayo 27:55-56)
Tunaweza kuona Undugu huu na Yesu kwa kusoma;
19 Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. (Wagalatia 1:19)
Lakini Yuda anasema;
1 Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, nawaandikia ninyi mlioitwa na Mungu na ambao mnaishi katika upendo wa Mungu Baba, na katika ulinzi wa Yesu Kristo. (Yuda 1:1)
Kwa hiyo Yakobo na Yohane walikuwa watoto wa Mama mwingine ambao baba yao ni Zebedayo. Na Yakobo na Yosefu walikuwa watoto wa Maria Mwingine. Kwa hiyo ni Yakobo wa wili wa Mama wengine Tofauti na Maria. Yuda alikuwa ni ndugu yake Yakobo. Yakobo vilevile alikuwa ndugu yake Yesu.
Kuthibitisha kuwa Hawa kina Mama ndio waliokuwa Mama zao kina Yakobo wote hao wawili na wengine tunaweza kusoma;
25 Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene. (Yohana 19:25)
Kwa hiyo kwenye (Yohana 19:25) tunaona Kuwa ni kwenye Msalaba wa Yesu alikuwepo Mama yake Yesu (Bikira Maria), Dada yake Bikira Maria, Mke wa Cleopa na Maria Magdalena. Na kwenye (Matayo 27:55-56) wamwtajwa ni Mama za kina nani kama inavyoonekana kwenye kifungu kifuatachi;.
55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. 56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. (Matayo 27:55-56).
Kwa hiyo hii ina maanisha kulikua na wanawake watatu wenye majina sawa ya Maria waliokuwa chini ya Msalaba. Yakobo na Yuda walikuwa watoto wa Maria Mke wa Cleofasi, na sio Mama wa Yesu, na hivyo sio kaka za Yesu.
7. Yesu alimwacha Mama yake kwa Yohane kwa kuwa hakuwa na Kaka na dada wakumwachia mamaye
26 Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.” 27 Halafu akamwambia yule mwanafunzi: “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.
Ndiyo maana Bikira Maria tangu siku ile alihamia kwa Yohani kwa kuwa hakuwa na watoto wengine.
Baba wa Yesu Kristo ni nani?
Baba wa Yesu Kristo ni Mungu Mwenyewe
Baba Mlishi wa Yesu Kristu ni nani?
Baba mlishi wa Yesu Kristo ni Yosefu Mtakatifu (Mt 1:18-20)
Yesu Kristu alizaliwa wapi?
Yesu Kristu alizaliwa Bethlehemu pangoni (Lk 2:4-7)
Nini maana ya Jina Bethlehemu?
Bethlehemu maana yake ni
Nyumba ya mkate
Yesu Kristu aliishi wapi kabala ya kuanza kazi yake?
Yesu Kristu Aliishi Nazareti kabla ya kuanza kazi yake
Mtangulizi wa Yesu Kristu ni nan?
Mtangulizi wa Yesu Kristu ni Yohani Mbatizaji
Wazazi wa Yohani Mbatizaji ni nani?
Wazazi wa Yohani Mbatizaji ni Zakaria na Eizabeti
Wazazi wa Bikira Maria ni nani?
Wazazi wa Bikira Maria ni Yoakimu na Anna
Mitume kumi na wawili wa Yesu Kristu ni wapi?
Mitume wa yesu ni;
1. Simoni/Petro
2. Yakobo
3. Yohane
4. Andrea
5. Filipo
6. Barttholomayo
7. Mathayo
8. Thomaso
9. Yakobo wa ALfayo
10. Thadayo (Yuda Thadey)
11. Simoni Mkanaani
13. Yuda Iskarioti – Aliyemsaliti
Baba Mtakatifu wa kwanza ni nani?
Baba Mtakatifu wa Kwanza ni Mt. Petro
Nani ni Mitume wa Mataifa?
Mitume wa mataifa ni Paulo na Barnaba
Nani ni shahidi wa kwanza katika Agano Jipya?
Shahidi wa Kwanza ni Mt Stefano
Yesu Alianza kuhubiri injili kwa maneno gani?
“Wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili” (Mk 1:15)
Yesu alitukomboa kwa hatua zipi?
Yesu alitukomboa kwa Hatua Mbili (2) ambazo ni;
1. Mafundisho yake
2. Mateso, Kifo na Ufufuko wake
Sentesi saba za Yesu msalabani ni zipi?
Sentesi saba za Yesu Msalabani ni;
1. Baba uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya (Lk 23:34)
2. Nakuambia Hakika leo utakuwa pamojanami Mbinguni (Lk 23:43)
3. Mama huyu ndiye mwanao (Yoh 19:26)
4. Tazama huyu ndiye Mama yako (Yoh 19:27)
5. Eloi, Eloi, lema Sabakthani (Mk. 15:34) Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha?
6. Naona kiu (Yoh 19:28)
7. Yametimia (Yoh 19:30)
Read and Write CommentsReferences:
Google ScholarResearchGateSemantic ScholarAckySHINE