Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Bokoboko La Kuku

Mahitaji

Ngano nzima (shayiri) – 3 Vikombe

Kuku – Β½ (3 LB takriban)

Thomu na tangawizi iliyosagwa – 1 kijko cha supu

Pilipili manga ya unga – Β½ kijiko cha chai

Jiyrah (cumin/bizari ya pilau) – Β½ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Kidonge cha supu – 1

Samli ya moto – Β½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Roweka ngano (shayiri) tokea usiku au muda wa masaa.
Katakata kuku mtie katika sufuria, tia maji kiasi viungo vyote. Mchemeshe awive na ibakie supu yake.
Toa kuku, toa mifupa na umchambue chambue vipande vidogo vidogo.
Chemisha ngano (shayiri) kwa kufunika sufuria hadi iwive na kukauka maji.
Tia supu ya kuku katika ngano (shayiri), na kuku uliyemechambua. Tia kidonge cha supu.
Tia samli nusu (bakisha nusu) kisha songa mchanganyiko uchanganye hadi ivurugike kuku na ngano (shayiri) vizuri.
Mimina katika sahani, mwagia samli imoto ilyobakia likiwa tayari.

Mapishi ya wali mtamu Wa Nazi Kwa Maharage Na Samaki Nguru Wa Kukaanga

Vipimo

Wali:

Mchele mpunga – 4 Vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele weka kando.
Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.
Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Maharage Ya Nazi

Maharage – 3 vikombe

Tui la nazi zito – 1 kikombe

Tui la nazi jepesi – 1 kikombe

Kitunguu maji – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa -1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chemsha maharage mpaka yaive.
Katiakatia kitunguu maji na tia thomu, tia na tui jepesi kikombe kimoja.
Tia tui zito endelea kuweka katika moto mdogomdogo hadi yakaribie kukauka yakiwa tayari.

Samaki Nguru Wa Kukaanga

Samaki Wa Nguru – 4 vipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) & tangawizi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi – 4

Ndimu – 2 kamua

Bizari ya samaki -1 kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Mwoshe samaki kisha mtie kitunguu thomu, tangawizi ilosagwa, chumvi, pilipilimbichi ilosagwa, ndimu na bizari ya samaki.
Mwache akolee viungo kwa muda kidogo.
Makaange katika mafuta hadi aive akiwa tayari.

Jinsi ya kutengeneza Keki Ya Mbegu Za Mchicha

Viamba upishi

Unga ngano vikombc 3
Unga mbegu za mchicha kikombe 1
Baking powder vijiko vidogo
Maziwa kikombe 1
Sukari kikombe 1
Blue band kikombe Β½
Mayai 10-12

Hatua

β€’ Chagua, osha, kausha mbegu za mchicha mweupe, kisha saga zilainike.
β€’ Chekecha unga wa ngano, unga wa mbegu za mchicha na baking powder Kwenye bakuli kubwa.
β€’ Ongeza sukari na changanya.
β€’ Ongeza mayai kidogo, kidogo ukikoroga na mwiko kwenda njia moja mpaka ilainike.
β€’ Kama rojo ni zito ongeza mayai, au maziwa ili iwe laini, ongeza vanilla na koroga.
β€’ Paka mafuta kwenye chombo cha kuoka au sufuria na chekechea unga kidogo.
β€’ Mimina rojo ya keki na oka kwenye oveni au kama ni sufuria funika, weka moto mwingi juu, chini weka moto kidogo.
β€’ Ukinusia harufu nzuri ya vanilla, funua, choma kisu katikati ya keki, kama ni kavu epua, pozesha na pakua kama kitafunio.

UNYONYESHAJI BORA WA MAZIWA YA MAMA

β€’ Maziwa ya mama pekee ndio chakula na kinywaji cha mtoto bora zaidi kwa watoto kwa miezi sita ya kwanza.
β€’ Ni jambo la muhimu sana kunyonyesha watoto wachanga kwa muda wa miezi minne na uendelee kunyonyesha hadi mtoto atakapofikisha mwaka mmoja na kuendelea.

β€’ Mtoto akifikisha miezi sita ndio wakati muafaka wa kumpa vyakula vya nyongeza vilivyotayarishwakatika hali ya usafi.

β€’ Onana na mnasihi akushauri kuhusu muda na jinsi ya kumuanzishia mtoto wako vyakula vya nyongeza

β€’ Vyakula vya ngogeza viwe ni vya mchanganyiko wa makundi yafuatayo ya chakula:- vyakula vya nafaka, venye asili ya nyama, mbogamboga na matunda, mafuta na sukari (kiasi). Lisha kila chakula kwa siku kadhaa kwa kufuatanisha kabla hujaaza chakula chengine kipya.

β€’ Usimuachilie mtoto alale kama chupa ya maziwa ingali mdomoni, ili kuepukana na kuoza kwa meno na madhara ya.

β€’ Watoto wanaopewa maziwa ya mama pekee hawaugui mara kwa mara, na wakiugua, makali ya ugonjwa hupungua na hupona mapema kwa sababu yale maziwa ya mwanzo ya njano yenye viini vingi vya kumkinga dhidi ya magonjwa.

Mapishi ya Mseto wa choroko

Mahitaji

Mchele 2 vikombe vya chai
Choroko kikombe 1 na 1/2
Nazi kopo 1
Swaum 1 kijiko cha chakula
Kitunguu 1 kikubwa
Binzari nyembamba 1 kijiko cha chai
Chumvi
Mafuta

Matayarisho

Loweka choroko usiku mzima, pindi ukianza kupika loweka mchele nusu saa kisha katika sufuria kubwa, kaanga vitunguu vikianza kuwa vya brown tia swaum na binzari nyembamba kisha tia choroko, mchele, chumvi,nazi na maji mengi kiasi yakuivisha choroko pamoja na mchele. Pika mpaka vitu vyote viive na viwe vilaini kisha upondeponde kiasi.Baada ya mseto wako kuiva utakuwa unaonekana kama uji wa mchele vile. Na Baada ya hapo mseto wako utakuwa tayari kwa kuliwa na mboga yoyote uipendayo.Inapendeza zaidi kuliwa vile tu ukishamalizwa kupikwa

Mapishi ya bagia na chatney ya machicha ya nazi

Mahitaji

Kunde (Ila mimi nilitumia Nigerian brown beans 1/2 kilo)
Vitunguu maji (onion 2)
Pilipili (scotch bonnet pepper 2)
Vitunguu swaum (garlic 4 cloves)
Chumvi (salt)
Barking powder (1/2 kijiko cha chai)
Machicha ya nazi (grated coconut 1 kikombe cha chai)
Limao (lemon 1)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka kunde usiku mzima kisha ziondoe maganda na uzitie kwenye blender pamoja na vitunguu maji, vitunguu swaum, pilipili, chumvi,barking powder na maji kiasi. Visage vitu vyote mpaka viwe laini na kisha uutoe na kuweka kwenye chujio ili uchuje maji. baada ya hapo zikaange katika mafuta mpaka ziwe za brown na uzitoe na kuziweka kwenye kitchen towel ili zichuje mafuta.Baada ya hapo saga machicha ya nazi,limao, pilipili chumvi pamoja na maji kidogo na hapo chatney yako itakuwa tayari kwa kuseviwa na bagia.

Jinsi ya kutengeneza Mkate wa mayai

Mahitaji

Slice za mkate 6
Mayai 3
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Vunja mayai yote katika sahani kisha tia chumvi kidogo sana na uyapige mpaka chumvi ichanganyike. Kisha chukua frying pan na utie vimafuta kidogo na uweke jikoni. Mafuta yakishapata moto kiasi,chovya slice za mkate katika hayo mayai na uzipike pande zote zikishaiva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili kukausha mafuta.Na baada ya hapo mikate yako itakuwa tayari kwa kuliwa na chai.

Jinsi ya kupika Biskuti Za Kuchoveya Chokoleti

Viambaupishi

Unga 300gm

Siagi 225gm

Icing Sugar 60gm

Chokoleti iliyokoza (Dark Chocolate) 225gm

Vanilla 2 kijiko cha chai

Yai 1

Baking Powder Β½ kijiko cha chai

Njugu za vipande Β½ kikombe cha chai

Njugu zilizosagwa ΒΌ kikombe cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Piga sukari na siagi katika mashine ya keki mpaka iwe laini

2. Kisha mimina yai na vanilla koroga vizuri

3. Mwisho mimina unga na baking powder polepole mpaka ichanganyike.

4. Kata kata umbo (shape) lolote unavyopenda (kama nyota, pembetatu,duara, kopa n.k)

5. Panga kwenye treya na choma kwa moto wa 350Β°C , vikibadilika rangi kidogo tu vitoe

6. Yayusha chokoleti tia kwenye bakuli ndogo.

7. kisha paka kwa kijiko au chovyea upande mmoja mmoja wa biskuti kisha nyunyizia njugu za kipande na njugu ya unga.

8. Panga kwenye sahani tiyari kunywewa na chai ya maziwa au kahawa.

Jinsi ya kupika Visheti

Viamba upishi

Unga 2 Vikombe

Samli au shortening ya mboga 2 Vijiko vya supu

Maziwa ΒΎ Kikombe

Iliki Kiasi

Mafuta ya kukarangia Kiasi

Shira

Sukari 1 Kikombe

Maji ΒΎ Kikombe

Vanila Β½ Kijiko cha chai

Zafarani (ukipenda) Kiasi

Jinsi ya kupika na kuandaa

Katika kisufuria pasha moto maziwa na wakati huo huo chemsha Samli katika kisufuria kengine.
Tia unga katika bakuli na iliki, kisha mimina samli iliyochemka na huku unachanganya, kisha tia maziwa na uwendele kuchanganya vizuri isiwe na madonge, ikiwa maziwa haitoshi ongeza maji kidogo.
Kisha uwache unga ukae mahali pa joto kwa muda wa dakika 10 hivi.
Halafu fanya viduara vidogo vidogo, kisha finyiza kwenye greta yenye vishimo vidogo ili upate umbo kama kwenye picha.
Kisha karanga kwenye mafuta yaliyopata moto hadi vibadilike rangi ya dhahabu, kisha viepue vichuje mafuta.
Chemsha shira, ikiwa tayari mimina visheti na upepete na kuzichanganya zipate shira kote.
Weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa na kahawa.

Mapishi ya Pilau Ya Nyama ya Kusaga, Adesi Za Brauni Na Zabibu

Mahitaji

Mchele wa Par boiled au basmati – 5 vikombe

Nyama kondoo/mbuzi ya kusaga – 1 kikombe

Kitunguu – 2

Kitunguu saumu (thomu/galic) – 7 chembe

Adesi za brauni (brown lentils) – 1 kikombe

Zabibu – 1 kikombe

Baharaat/bizari mchanganyiko – 1 kijiko cha supu

Chumvi – kiasi

Pilipilii manga – Β½ kijiko

Jiyra/bizari pilau/cummin – 1 kijiko cha chai

Supu ya nyama ng’ombe – Kiasi cha kufunikia mchele

Mafuta – Β½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha

Osha, roweka masaa 2 au zaidi.

Katakata (chopped)

Menya, saga, chuna

Osha, roweka, kisha chemsha ziive nusu kiini.

Osha, chuja maji

Namna Ya Kupika:

Tia mafuta katika sufuria, kaanga vitunguu hadi vianze kugeuka vyekundu.
Tia kitunguu thomu, kaanga, tia baharati/bizari zote kaanga.
Tia nyama uchanganye vizuri, ukaange iwive..
Tia mchele ukaange kidogo kisha tia supu, koroga kidogo, funika uivie mchele.
Karibu na kuiva, tia adesi, zabibu, changanya, funika uendelee kuiva kama unavyopika pilau.
Epua pakua katika chombo, ongezea zabibu kupambia ukipenda

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Chumvi

VIAMBAUPISHI

Unga – 3 Vikombe vya chai

Siagi – 250 gms

Baking powder – 3 Vijiko vya chai

Mayai – 2

Chumvi – 1 kijiko cha chai

Maziwa – 1/2 Kikombe

Pilipili manga ya unga 1 Kijiko cha chai

MAANDALIZI

Katika bakuli la kusagia (blender) au mashine ya keki, tia siagi, chumvi na mayai, piga mpaka iwe kama malai (cream).
Tia Unga, baking powder, pilipili manga.
Tia maziwa.
Kata usanifu (design) unayotaka na sokota au kunja kwa usanifu unaopenda.
Pika (bake) katika moto wa 350ΒΊ C – usiviache vikawa rangu ya udongo (brown) sana.

Mapishi ya wali kuku wa Kisomali

Mahitaji ya wali

Mchele – 3 vikombe

Vitunguu (viliokatwa vidogo vidogo) – 2

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha chai

Bizari ya pilau – 1 kijiko cha supu

Mdalasini – 1 kijiti

Hiliki – 3 chembe

Pilipili manga nzima – chembe chache

Siagi – Vijiko 2 vya supu

Chumvi – kiasi

Mahitaji kwa kuku

Kuku kidari (Breast) kata vipande vipande – 2 LB

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Kotmiri iliyokatwa ndogo ndogo – kiasi

Bizari ya pilau (cummin au jiyrah) – 1 kijiko cha chai

Pilipili kubwa tamu la kijani – 1

Pilipili kubwa tamu nyekundu – 1

(zikate vipande vipande)

Karoti iliyokunwa – 1 – 2

Chumvi – Kiasi

Mapishi ya Wali:

Roweka mchele kwa muda fulani kutegemea mchele
Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi vibadilike rangi kidogo.
Tia thomu iliyosagwa, mdalasini, bizari ya pilau, hiliki, pilipili manga na chumvi, kaanga kidogo.
Tia mchele kaanga kidogo, kisha tia maji ya moto kiasi kutegemea na aina ya mchele kama kawaida ya kupika wali kama pilau.
Tia sigai, funika upikike wali hadi uwive.

Mapishi ya Kuku:

Mchanganye kuku pamoja na thomu/tangawizi iliyosagwa, chumvi, pilipili mbichi.
Katika karai tia mafuta yapate moto vizuri.
Mtie kuku, bizari ya pilau (jiyrah) na ukaange, karibu na kuiva tia vitunguu.
Tia mapilipili makubwa, kotmiri, na kaanga kwa dakika moja tu uzime moto na epua weka kando.

Mapishi ya Biskuti Za Kastadi

VIAMBAUPISHI

Unga 6 Vikombe

Sukari ya kusaga 2 vikombe

Siagi 500 gm

Baking powder 1 Kijiko cha chai

Kastadi Β½kikombe

MAPISHI

Koroga siagi na sukari katika mashine ya keki (cake mixer) mpaka iwe laini (creamy).
Mimina mchanganyiko uliopiga kwa mashine kwenye bakuli.
Tia unga na baking powder na Kastadi.
Kata usanifu (design) unaopenda halafu panga kwenye sahani ya kupikia (baking tray).
Pika (bake) katika oven moto wa 350Β° F kama muda wa dakika 15 hivi huku unazitazama tazama.

Namna ya kutengeneza Visheti Vya Nazi Na Njugu (Sudani)

VIAMBAUPISHI

Unga – 3 mug za chai

Samli – Β½ mug ya chai

Maziwa – 1ΒΌ mug ya chai

Baking powder – 2 vijiko vya chai

VIAMBAUPISHI VYA MJAZO

Njugu zilizomenywa vipande vipande – 2 vikombe cha chai

Sukari – Β½ kikombe cha chai

Iliki – 1 kijiko cha chai

Nazi iliyokunwa – 2 vikombe vya chai

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 vikombe vya chai

Maji – 1 kikombe cha chai

Ndimu – 1

JINSI YA KUVIANDAA

1-Changanya unga na samli kisha tia baking powder na maziwa. Ukande ulainike kisha

uwache kama dakika 5 uumuke.

2-Kwenye bakuli nyingine changanya njugu, sukari na iliki.

3-Kata madonge madogo dogo sukuma kila donge duara jembamba, kisha tia kijiko cha mchanganyiko wa njugu juu yake ifunikie juu yake na ibane pembeni.

4-Panga kwenye treya isiyoganda (non stick) kisha choma kwenye oven kwa moto wa chini

(bake) 350Β° C kwa dakika kama 15-20.

5-Chemsha maji na sukari katika sufuria ndogo kisha tia ndimu acha ichemke mpaka inatenate unapoigusa.

6-Kwenye sahani ya chali mimina nazi iliyokunwa.

7-Vibiskuti vikiwa tayari vya motomoto chovea kwenye shira kisha zungushia katika nazi iliyokunwa,

panga kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

LISHE BORA KWA WATU WENYE AFYA NZURI

β€’ Kula chakula bora kunamaanisha kula vyakula aina tofauti ya vyakula kila siku kama vile matunda, mboga, maziwa na aina ya vyakula vyenye asili ya nyama wa kufuga kama kuku, mbuzi, ngombe, samaki na na vyakula vya nafaka.

β€’ Lishe bora linamaanisha pia kula chakula ambacho hakina mafuta mengi, sukari au chumvi nyingi

β€’ Zingatia angalau vyakula vya nafaka kama vile mtama, mahindi, mchele, ngano, wimbi, ndegu, njegere. n.k

β€’ Ni bora kula matunda mengi kama β€˜maembe, ndizimbivu, papai, pera, chungwa, ubuyu, nanasi, pesheni, zambarau” na mbogamboga kama vile β€œmchicha, majani ya mboga, karoti, nyanya chungu, nyanya, mkunde, biringanya” mara tano kwa siku.

β€’ Kama mboga na matunda hazipatikani ni bora kununua zile ambazo zimehifadhiwa tayari kwenye mikebe au zile ziko kwenye jokofu (friji).

β€’ Punguza kula vyakula ambavyo vinapikwa kwa mafuta mengi na chumvi nyingi

β€’ Lishe bora hukusaidia wewe na jamii yako kuishi vyema, kuwa na afya bora, kufanya kazi vizuri na kwa bidii, shuleni na hata kucheza.

Tofauti kati ya yai la kuku wa kienyeji na la kuku wa kisasa

Kilishe mayai yote ni sawa. Virutubishi vinavyopatikana kwenye yai la kuku wa kienyeji kama protini, vitamini A, madini ya chuma na virutubishi vya aina nyingine, ndivyo hivyo vinavyopatikana pia kwenye yai la kuku wa kisasa.

Tatizo linaweza kutokea pale ambapo wafugaji wa kuku wa kisasa hawafuati taratibu za ufugaji na pengine hawawapi kuku vyakula muhimu wanavyohitaji au wanawapa dawa na vyakula visivyo bora kiafya, hivyo wakati mwingine kiini cha yai la kuku wa kisasa huonekana kupungua rangi ya njano kuliko kiini cha yai la kuku wa kienyeji.

Mtu anashauriwa kula yai bila kujali ni la kuku gani, kwa kutegemea ni yai lipi linapatikana kwa urahisi. Lakini nivizuri kula mayai ambayo yapo salama.

Mapishi ya Wali na kuku wa kienyeji

Mahitaji

Kuku wa kienyeji (boiler chicken 1)
Mchele (rice 1/2 kilo)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1)
Vitunguu (onion 2)
Vitunguu swaum (garlic cloves 6)
Tangawizi (ginger)
Carry powder
Binzari ya njano (Turmaric 1/2)
Njegere(peas 1/2kikombe)
Carrot iliyokwanguliwa 1
Limao (lemon 1)
Bilinganya (aubergine 1)
Chumvi
Pilipili (scotch bonnet pepper)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka mchele kwa muda wa dakika 10 na uchuje maji yote kisha chemsha maji ya moto na uweke pembeni. Kisha tia mafuta kiasi katika sufuria na ukaange vitunguu, carrot na njegere pamoja. kwa muda wa dakika 5 baada ya hapo tia turmaric na chumvi. pika kwa muda wa dakika 5 na utie mchele na maji ya moto kiasi funika na upike mpaka uive.
Chemsha kuku pamoja na limao, chumvi, kitunguu swaum na tangawizi mpaka aive kisha mweke pembeni. Saga pamoja kitunguu,kitunguu swaum, tangawizi na nyanya. Kisha bandika jikoni na uache uchemke bila mafuta mpaka maji ya kauke.Baada ya hapo tia chumvi, mafuta ,curry powder, bilinganya na kuku. Kaanga pamoja kwa muda kisha tia maji au supu ya kuku kwa kukadiria mchuzi uutakao. Acha uchemke mpaka mabilinganya yaive na hapo mchuzi utakuwa tayari kuseviwa na wali.

Jinsi ya kupika Wali Wa Samaki Na Mboga

VIPIMO VYA SAMAKI

Samaki wa sea bass vipande – 1Β 1/2 LB (Ratili)
Kitunguu saumu(thomu/galic) -1 Kijiko cha supu
pilipili mbichi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chai
Bizari ya manjano au ya pilau – 1/2 Kijiko cha chai
Paprika ya unga au pilipili ya unga – 1 kijiko cha chai
Chumvi – Kiasi
Ndimu
Mafuta – 3 Vijiko vya supu

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Roweka samaki kwa viungo hivyo vyote kwa muda wa robo saa hivi.

Washa oven moto wa 400F.
Kisha weka samaki katika trea na choma kwa muda wa dakika 15 na weka moto wa juu dakika za mwisho ili ipate rangi nzuri.
Ikishaiva epua na itakuwa tayari kuliwa.

VIPIMO VYA MBOGA

Gwaru (green beans) – 1 LB
Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha supu
Karoti – 4-5
Chumvi – Kiasi
Bizari ya manjano – 1/2 Kijiko cha chai
Pilipili manga – 1/4 kijiko cha chai
Mafuta ya zaituni – Kiasi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Kata kata karoti na toa sehemu ya mwisho za binzi.
Weka mafuta katika sufuria kisha kaanga karoti na gwaru
Kisha weka moto mdogo na funika ili ziwive na sio kuvurujika.
Karibu na kuiiva tia thomu kaanga kidogo,tia bizari ,chumvi na pilipili manga.
Ikisha changanyikana vizuri epua na tayari kuliwa na wali na samaki.

Mapishi ya Samaki wa kupaka

Mahitaji

Samaki (Tilapia 2)
Nyanya ya kopo (Tomato tin 1)
Kitunguu (Onion 1)
Tangawizi (ginger kiasi)
Kitunguu swaum (garlic clove )
Mafuta (Vegetable oil)
Pilipili (scotch bonnet pepper 1)
Tui la nazi zito (coconut milk 2 vikombe vya chai)
Curry powder 1/2 cha kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga (ground cumin 1/2 kijiko cha chai
Binzari manjano (turmaric 1/2 kijiko cha chai
Chumvi (salt)
Limao (lemon 1)
Giligilani (fresh coriander)

Matayarisho

Marinate samaki na chumvi, limao, kitunguu swaum, tangawizi kwa muda wa masaa 6 au zaidi. Baada ya hapo wakaange au waoke katika oven mpaka waive ila usiwakaushe sana. Baada ya hapo saga pamoja nyanya ya kopo, kitunguu maji, kitunguu swaum na tangawizi. Kisha bandika huo mchanganyiko jikoni na upike mpaka ukauke maji kisha tia mafuta, binzari zote, curry powder, chumvi na pilipili na upike kwa muda wa dakika 5. Baada ya hapo tia maji kidogo (kama 1/2 kikombe) pamoja na tui la nazi. Acha uchemke mpaka tui liive na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo waweke samaki kwenye sufuria ya kuokea na kisha umwagie huo mchuzi juu ya hao samaki na owaoke (bake) kwa muda wa dakika 20. Ukisha toa kwenye oven katakata giligilani na utie kwenye hao samaki na hapo watakuwa tayari kwa kuliwa. unaweza kuwala na wali, ugali au chapati

Shopping Cart
🏠 Home πŸ“– Reading πŸ–ΌοΈ Gallery πŸ’¬ AI Chat πŸ“˜ About