Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Wali, samaki wa nazi na kisamvu

Mahitaji

Mchele
Kisamvu kilichotwangwa
Samaki
Mbaazi
Nyanya chungu
Vitunguu
Nyanya ya kopo
Tangawizi
Kitunguu swaum
Vegetable oil
Curry powder
Tui la nazi (kopo 2)
Chumvi
Pilipili
Limao

Matayarisho

Safisha samaki kisha wamarineti na kitunguu swaum, tangawizi, pilipili, chumvi na limao kwa muda wa masaa 3.Baada ya hapo wakaange na usiwakaushe sana na uwaweke pembeni kwa ajili ya kuungwa.Katakata vitunguu maji, saga tangawizi na kitunguu swaum. Baada ya hapo injika sufuria ya mchuzi jikoni na mafuta kiasi ya kupikia, mafuta yakisha pata moto, tia vitunguu maji na vikaange mpaka viwe vya rangi ya brown. kisha tia kitunguu swaum na tangawizi.kaanga kidogo kisha tia nyanya ya kopo moja na ufunike. acha mpaka nyanya ziive. Kisha tia chumvi na curry powder na uache ikaangike kwa muda wa dakika 2 kisha tia samaki na nyanya chungu nakisha kamulia nusu ya limao. Geuza mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri kisha tia tui la nazi kopo moja na uache ichemke mpaka mchuzi uive.

Baada ya hapo chemsha kisamvu pamoja na mbaazi Kikisha iva, kaanga kitu na nyanya pembeni mpaka ziive kisha tia kisamvu. geuza mchanganyiko mpaka uchanganyike vizuri kisha tia tui la nazi na chumvi na aacha ichemke mpaka tui liive kisha ipua.malizia kwa kupika wali ambapo utachemsha maji kisha tia mafuta,chumvi na mchele na uupike mpaka uive kisha sevu na mboga ulizopika na mlo wako utakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali, mchicha wa nazi na nyama ya kukaanga

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Mchicha uliokatwakatwa (spinach mafungu 2)
Nyama (beef 1/2 ya kilo)
Nyanya (tin tomato 1/2 ya tin)
Nyanya chungu ( garden egg 3)
Kitunguu swaum (garlic cloves 3)
Tangawizi (ginger)
Curry powder
Vitunguu (onion 2)
Limao (lemon 1)
Chumvi
Pilipili (scotch bonnet pepper )
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)

Matayarisho

Kaanga kitunguu kikishaiva tia nyanya na chumvi. kaanga mpaka nyanya ziive kisha tia nyanya chungu,curry powder na pilipili 1 nzima, baada ya hapo tia mchicha na uuchanganye vizuri kwa kuugeuzageuza. Mchicha ukishanywea tia tui la nazi na uache lichemke mpaka liive na hapo mchicha utakuwa tayari.
Safisha nyama kisha iweke kwenye sufuria na utie chumvi, tangawizi, limao na kitunguu swaum. Ichemshe mpaka itakapoiva na kuwa laini. Baada ya hapo weka sufuria jikoni na mafuta kidogo yakisha pata moto tia vitunguu na nyama na uvikaange pamoja, kisha tia curry powder na ukaange mpaka nyama na viunguu vya brown. na hapo nyama itakuwa imeiva. Malizia kwa kupika wali kwa kuchemsha maji kisha tia mafuta, chumvi na mchele na upike mpaka uive. Baada ya hapo chakula kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Madhara ya kula yai bichi

Yai bichi linaweza kuwa na vijidudu viitwavyo kwa kitaalamu โ€œSALMONELLAโ€ vinavyoweza kusababisha tumbo kuuma, kichefuchefu na pia kuharisha.
Vijidudu ya โ€œSalmonellaโ€ vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watoto, wazee na wale wenye hali dhaifu ya kimwili kama wagonjwa wa UKIMWI.

Pia yai bichi lililowazi linaweza kuwa zalio zuri la vimelea vya maradhi mbalimbali. Inashauriwa kupika yai mpaka liive kabisa, na kuhakikisha kwamba hakuna ute unaoteleza.

Kama ni yai la kuchemsha, lichemshwe kwa dakika kumi zaidi baada ya maji kuchemka. Pia ni muhimu kuhakikisha kwamba vyombo vilivyotumika k u k o rogea yai bichi vinaoshwa kwa maji na sabuni kabla ya kuvitumia tena kwa matumizi mengine ili kuepuka maradhi.

Mapishi ya Maini ya kuku

Mahitaji

Maini ya kuku 1/2 kilo
Vitunguu vikubwa 2
Hoho 1
Pilipil 1
Limao 1/2
Swaum/tangawizi 1 kijiko cha chai
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Safisha maini weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu,swaum na tangawizi pamoja (hakikisha vitunguu visiwe vya brown), kisha tia maini, curry powder, pilipili, chumvi ,hoho na limao kisha changanya vizuri na ufunike. Pika mpaka maini yaive na hakikisha yanakuwa na rojo kidogo. Baada ya hapo ipua na yatakuwa tayari kwa kuliwa na chochote upendacho kama vile chapati, chips, ugali, wali.

Jinsi ya kutengeneza Nangatai

MAHITAJI

Unga wa ngano – 2 – 2 ยผ Vikombe

Siagi – 1 ยฝ Kikombe

Sukari – 1 Kikombe

Yai – 1

Vanilla -Tone moja

Baking Powder -kijiko 1 cha chai

Chumvi – Kiasi kidogo (pinch)

Unga wa Kastadi – 2 Vijiko vya supu

MATAYARISHO

Changanya vitu vyote isipokuwa unga.
Tia unga kidogo kidogo mpaka mchanganyiko uwe sawa.
Kisha fanya duara ndogo ndogo uzipange kwenye treya na utie rangi katikati.
Halafu zichome katika moto wa 300ยฐF kwa muda wa dakika 20 – 25 na zisiwe browni .
Kisha panga kwenye sahani tayari kuliwa na chai.

Jinsi ya kupika Biriyani Ya Nyama Ng’ombe

Viambaupishi Vya Masala

Nyama vipande – 3 LB

Mtindi – ยฝ kopo

Kitunguu (thomu/galic) – 1ยฝ kijiko cha supu

Tangawizi – 1ยฝ kijiko cha supu

Nyanya – 2

Pilipili mbichi – kiasi

Nyanya kopo – 4 vijiko vya supu

Vidonge supu – 2

Pilipili nyekundu paprika – kiasi

Bizari zote saga – 2 vijiko vya supu

Viazi – 4

Mafuta – 2 mug

Samli – ยฝ kikombe

Vitungu – 6

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika masala

Kwenye sufuria tia nyama, saga nyanya na thomu, pilipili mbichi, tangawizi. Mimina kwenye nyama na mtindi, tia na nyanya kopo, bizari paprika, vidonge vya supu, chumvi kisha changanya vyote pamoja weka motoni.
Katika sufuria nyengine tia mafuta na samli kaanga vitungu mpaka viwe rangi ya hudhurungi toa weka pembeni.
Kanga viazi weka pembeni.
Chukua mafuta kidogo uliyokangia tia kwenye nyama acha katika moto wa kiasi mpaka nyama iwive na maji ya punguke.
Tia viazi na vitunguu vivunje vunje tia ndani ya nyama acha moto mdogo.

Vipimo Vya Wali

Mchele – 5 mug

Maji – kiasi

Chumvi – kiasi

Mafuta uliyokaanga vitungu – kiasi

Rangi ya biriani – ยผ kijiko cha chai

*Zafarani – ยฝ kijiko cha chai

*roweka rangi na zafarani

Namna Ya Kutarisha Na Kupika Wali

Osha mchele roweka muda wa saa.
Chemsha maji kama magi 10 hivi na chumvi tia mchele.
Uache uchemke ukishaiva kiini nusu, mwaga maji chuja.
Mimina juu ya nyama tia rangi na mafuta kwa juu funika.
Aacha kidogo katika oveni kwa muda wa dakika 20 hivi kisha epua ikiwa tayari.

Mapishi ya Wali Wa Kichina Wa Kuku Na Mboga Mchanganyiko

Vipimo

Mchele wa basmati/pishori – 4 vikombe vikubwa (mugs)

Kuku – 2

Vitnguu vya kijani (sprin onions) katakata – 5 miche

Maharage machanga (spring beans) katakata – kiasi kujaza mug moja

Pilipili boga la (capsicum) katakata – 1

Karoti katakata vipande virefu – 1

Kitunguu thomu (garlic) kuna (grate) – 1 kubwa

Tangawizi mbichi kuna (grate) – 1 kubwa

Sosi ya soya (soy sauce) – 2 vijiko vya supu

Kidonge cha supu – 1

Mafuta ya kupikia – ยผ kikombe cha chai

Chumvi – kiasi

Pilipili manga – 1 kijiko cha supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha kuku vizuri, katakata vipande, weka katika sufuria, tia chumvi, pilipili manga, mfunike, umkaushe motoni huku ukimgeuza geuza.

Roweka mchele kisha uchemshe uive nusu. Chuja maji, tia siagi kidogo ili usigandane.

Weka karai ya kupika mboga (wok) au sufuria kisha tia mafuta yashite moto.

Tia kitunguu thomu, tangawizi, kaanga kidogo.

Tia mboga zote, ulizokatakata.

kaanga kidogo, kisha tia sosi ya soya na kidonge cha supu. Usizipike sana mboga mpaka zikalainika mno. Sababu zitaiva katika mchele

Changanya kuku na mboga kisha changanya vyote katika mchele, urudishe katika moto.

Funika upike hadi uive kamilifu.

Pakua kwenye sahani.

Jinsi ya kutengeneza Fagi Ya Kumumunyuka Mdomoni

VIAMBAUPISHI

Maziwa mazito matamu (condensed milk) – 2 vibati

Sukari – 1 kikombe

Samli 1 ยฝ kikombe

Vanilla 2 kifuniko cha chupa yake

Hiliki ilosagwa – 2 vijiko vya chai

Sinia kubwa ya bati Paka samli

MAANDALIZI

Changanya maziwa, sukari na samli katika sufuria isiyogandisha chakula (non-stick) uweke katika moto.
Koroga huku ikipikika hadi ianze kugeuka rangi na kuanza kuachana. Usiache mkono kuroga isije kufanya madonge.
Tia hiliki na vanilla, endelea kuipika.
Itakapogeuka rangi vizuri mimina katika sinia na haraka uitandaze kwa mwiko huku ukiuchovya katika maji na kuendelea kuitandaza hadi ikae sawa kote.
Pitisha kisu kuikataka ili ikipoa iwe wepesi kuitoa vipande.

Kila inapozidi kupoa na kukaa ndipo fagi inakauka na kumumunyuka.

Mapishi ya Mchuzi wa kambale

Mahitaji

Kambale 2
Nazi kopo 1
Nyanya kopo 1
Vitunguu 2
Curry powder 1 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga 1/2 kijiko cha chai
Swaum/ tangawizi 1 kijiko cha chakula
Giligilani kiasi
Limao 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Loweka samaki katika maji ya moto kwa muda wa muda wa nusu saa.Baada ya hapo Saga pamoja nyanya, vitunguu, swaum na tangawizi kisha vibandike jikoni na uvipike mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta. Pika mpaka nyanya zitengane na mafuta kisha tia spice zote.Zipike kwa muda mdogo kisha tia tui la nazi, maji kiasi, samaki, pilipili nzima, chumvi na kamulia limao. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na samaki pia wawe wameiva na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo ipua kisha tia giligilani iliyokatwa na mchuzi utakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuulia kwa chochote kile upendacho. Mi hupendaga kuulia na ugali mlaiiini au na wali pia.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Kamba Wa Nazi, Kisamvu Na Kachumbari Ya Papa Mkavu

Vipimo – Ugali

Maji – 4 vikombe kiasi inategemea na unga wenyewe.

Unga wa sembe – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria, weka motoni, yakipata moto korogea unga wa sembe kiasi na ufanye uji mzito uache uchemke vizuri huku ukikoroga.
Chota kibakuli kimoja cha uji huo weka pembeni kisha mimina unga wote uliobaki upigepige uchanganyike vizuri kwenye uji huo mpaka ushikamane
Punguza moto anza kuusonga taratibu huku ukiongeza ule uji ulioweka pembeni kidogo kidogo mpaka uone sasa umeshikamana vizuri.
Endelea kusonga mpaka ulainike kisha mimina kwenye bakuli au sahani iliyolowanishwa na maji kisha upete pete huku ukiugeuza geuza mpaka ukae shepu nzuri ya duara.Weka tayari kwa kuliwa.

Vipimo – Mchuzi wa kamba wa nazi

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kamba waliomenywa – 1 Kilo

Pilipili mbichi iliyosagwa – ยฝ kijiko cha chai

Kitunguu saumu na tangawizi ilivyosagwa – 1 kijiko cha supu

Nazi nzito iliyochujwa – 1 kikombe

Bizari ya mchuzi – ยฝ kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Ndimu – Nusu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha na osha kamba vizuri kisha mtie katika sufuria. Katia kitunguu, nyanya, tia chumvi, pilipili mbichi ya kusaga, thomu na tangawizi, bizari ya mchuzi na ndimu. Tia maji kidogo kiasi acha ichemke.
Watakapoiva na karibu kukauka, mimina tui la nazi taratibu koroga kiasi
Punguza moto aacha ichemke kidogo ukiwa mchuzi tayari.

Vipimo – Kisamvu

Kisamvu – 2 vikombe

Kunde mbichi zilizochemshwa – 1 kikombe

Kitunguu – 1

Nazi nzito iliyochujwa – 1 vikombe

Chumvi – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka kisamvu katika sufuria, katia kitunguu, tia chumvi, maji kidogo acha kichemke.
Huku ikichemka mimina kunde mbichi zilizochemshwa acha zipikikie kidogo mpaka kisamvu kikaribie kukauka na kunde kuiva.
Mimina nazi nzito punguza moto acha ichemke kidogo, mimina kwenye bakuli tayari kwa kuliwa.

Vipimo – Kachumbari Ya Papa

Papa mkavu (au nguru) – kipande

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Muoshe papa vizuri atoke mchanga kisha mchome kwenye jiko la mkaa au unaweza kumtia kwenye treya kisha kwenye oven kwa moto wa 350 kwa dakika 15 mpaka 20.
Akikauka mchambue chambue weka kando.
Tengeneza kachumbari, kwa kukata kitunguu, nyanya na pilipili mbichi, tia ndimu na chumvi.
Changanya na papa mkavu uliyemchambu ikiwa tayari.

Jinsi ya kupika Wali Wa Kichina wa mboga mboga Na Mayai

Viambaupishi

  1. Mchele (Basmati) – 3 vikombe
  2. Mbogamboga za barafu (karot, njegere, spring beans na mahindi) – 1 kikombe
  3. Kuku Kidari – 1 LB (ratili)
  4. Mayai – 2 mayai
  5. Vitunguu (vikubwa) – 2 au 3 vidogo
  6. Pili pili manga – 1 kijiko cha chai
  7. Paprika – 1 kijiko cha chai
  8. Chumvi – Kiasi
  9. Mafuta – 1/3 kikombe cha chai
  10. Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha supu
  11. Tangawizi – 1 kijiko cha chai
  12. Kidonge cha supu – 1
  13. Soy sauce – 2 vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Kuku

Kata kidari cha kuku vipande vidogo vidogo vya kiasi.

Tia mafuta kidogo katika wok (karai ya kichina)

Kisha mtie kuku, thomu, tangawizi, soy sauce, pilipilimanga, paprika chumvi.

Tia mboga za barafu, kidonge cha supu, kaanga kuku na mboga viwive yitu vyote na mchanganyiko ukauke.

Namna Ya Kutayarisha Na kupika Wali

Roweka mchele wa basmati kwa muda wa saa au zaidi.

Halafu chemsha mchele pamoja na chumvi

Wacha uchemke asilimia 70%

Chuja maji na weka kando

Katika sufuria, tia mafuta kidogo tu

Kisha tia mayai mawili ukaange haraka haraka (crumbled egg)

Changanya mchanganyiko wa kuku na mboga

Kisha tia wali changanye vizuri

Rudisha katika moto, funika upikike kidogo hadi uive

Kisha pakua katika sahani na tolea na mayai ya kuchemsha ukipenda.

Mapishi ya Pilau Ya Nafaka Na Nyama Ya Kusaga

VIAMBAUPISHI

Mchele – 3 vikombe

Nyama ya kusaga – 1 LB

Mchanganyiko wa Nafaka upendazo; maharagwe, njegere, mbaazi n.k 1 mug

Vitunguu maji kata vipande vipande – 3 vya kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi – 2 vijiko vya supu

Mafuta – ยฝ Kikombe

Mchanganyiko wa bizari (Garam Masala) – 2 vijiko vya chai

Vipande vya supu (Maggi cubes) – 3

Maji (inategemea mchele) – 5

Chumvi – Kiasi

MAPISHI

Osha mchele na roweka.
Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitunguu mpaka viwe brown.
Tia Thomu na tangawizi, kaanga kidogo.
Weka nyama ya kusaga, chumvi na garam masala, endelea kukaanga mpaka nyama iwive.
Mwaga maji yaliomo katika kopo la nafaka na utie nafaka pekee humo.
Tia maji na vipande vya supu (Maggi cubes) huku unavivuruga, koroga kidogo.
Tia mchele, koroga kidogo.
Funika na pika kwa moto mdogo mpaka karibu na kukauka ukikorogoka kidogo. (kama unavyopika pilau ya kawaida)
*Epua uipike katika moto wa oven 350-400 Deg kwa muda wa dakika 15.
*Kama sufuria uliyotumia sio ya kupikia katika oven, mimina katika chombo chochote kinachotumika kwa oven kama bakuli la pyrex au treya za foil.
Pakua katika sahani na iko tayari kuliwa.

Jinsi ya kupika Mgagani

Viamba upishi

Mgagani mkono 1
Mafuta vijiko vikubwa 4
Karanga zilizosagwa kikombe ยฝ
Maji kikombe 1
Kitunguu 1
Karoti 2
Maziwa kikombe 1
Chumvi kiasi

Hatua

โ€ข Chambua mgagani, oshana katakata.
โ€ข Chemsha maji, weka chumvi kisha ongeza mgagani, funika zichemmke kwa
โ€ข dakika 5-10.
โ€ข Menye osha na katakata kitunguu.
โ€ข Osha, menya na kwaruza karoti.
โ€ข Kaanga karanga, ondoa maganda na saga.
โ€ข Kaanga vitunguu na karoti mpaka zilainike ukikoroga.
โ€ข Weka mgagani uliochemshwa koroga sawasa na funika kwa dakika 5 zilainike.
โ€ข Changanya maziwa na karanga ongeza kwenye mgagani ukikoroga kasha punguza moto kwa dakika 5 ziive.
โ€ข Onja chumvi na pakua kama kitoweo.

Jinsi ya kutengeneza Pilau Ya Kuku

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 vikombe

Kuku – ยฝ

Viazi – 4

Vitunguu – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Binzari ya pilau nzima – 1 Kijiko cha chakula

Binzari ya pilau – ยฝ kijiko cha chai

Pilipili manga nzima – ยฝ kijiko cha chai

Karafuu nzima – 8

Iliki nzima – 6

Mdalasini nzima – 5 vijiti

Pilipili mbichi iliyosagwa – 2

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kupikia – ยผ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika:

Osha mchele na roweka kwa muda kutegemea na aina ya mchele.
Kata kuku vipande upendavyo, safisha kisha mchemshe kwa chumvi, pilipili iliyosagwa, thomu na tangawizi.
Akiwiva kuku, mtoe weka kando, bakisha supu katika sufuria.
Katika sufuria, kaanga vitunguu hadi vigeuke rangu ya hudhurungi.
Tia thomu na tangawizi na binzari zote kaanga kidogo
Kisha tia viazi kanga kidogo kisha tia kisha tia vipande vyako vya kuku na supu acha ichemke kidogo kisha tia maji ukisie kutokana na mchele unaotumia.
Mwisho tia mchele koroga uchanganye na vitu vyote acha ichemke kiasi kisha funika na punguza moto mpaka uive (huku ukiugeuzageuza)
Ukishakuwa tayari pakua kwenye sahani tayari kwa kula na salad na pilipili.

UNYONYESHAJI BORA WA MAZIWA YA MAMA

โ€ข Maziwa ya mama pekee ndio chakula na kinywaji cha mtoto bora zaidi kwa watoto kwa miezi sita ya kwanza.
โ€ข Ni jambo la muhimu sana kunyonyesha watoto wachanga kwa muda wa miezi minne na uendelee kunyonyesha hadi mtoto atakapofikisha mwaka mmoja na kuendelea.

โ€ข Mtoto akifikisha miezi sita ndio wakati muafaka wa kumpa vyakula vya nyongeza vilivyotayarishwakatika hali ya usafi.

โ€ข Onana na mnasihi akushauri kuhusu muda na jinsi ya kumuanzishia mtoto wako vyakula vya nyongeza

โ€ข Vyakula vya ngogeza viwe ni vya mchanganyiko wa makundi yafuatayo ya chakula:- vyakula vya nafaka, venye asili ya nyama, mbogamboga na matunda, mafuta na sukari (kiasi). Lisha kila chakula kwa siku kadhaa kwa kufuatanisha kabla hujaaza chakula chengine kipya.

โ€ข Usimuachilie mtoto alale kama chupa ya maziwa ingali mdomoni, ili kuepukana na kuoza kwa meno na madhara ya.

โ€ข Watoto wanaopewa maziwa ya mama pekee hawaugui mara kwa mara, na wakiugua, makali ya ugonjwa hupungua na hupona mapema kwa sababu yale maziwa ya mwanzo ya njano yenye viini vingi vya kumkinga dhidi ya magonjwa.

Mapishi ya Biriani Ya Kuku Wa Kuchoma (Grilled)

Mahitaji

Mchele wa Basmati /Pishori – 4 vikombe

Kuku

Vitunguu – 3

Nyanya/Tungule – 2

Tangawizi mbichi ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi nzima – 3

Ndimu – 2

Garama Masala/bizari mchanganyiko – 1 kijiko cha supu

Haldi/tumeric/bizari manjano – 1 kijiko cha chai

Pilipilu ya unga nyekundu – 1 kijiko cha chai

Mtindi /yoghurt – 3 vijiko vya supu

Mafuta ยฝ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele, roweka.
Safisha kuku vizuri, mkate vipande vya saizi ya kiasi weka katika bakuli.
Katika kibakuli kidogo, changanya tangawizi mbichi, thomu, bizari zote, pilipili nyekundu ya unga, chumvi, mtindi, kamulia ndimu.
Punguza mchanganyiko kidogo weka kando.
Mchanganyiko uliobakia, tia katika bakuli la kuku uchanganye vizuri arowanike (marinate) kwa dakika chache hata nusu saa au zaidi.
Weka kuku katika treya ya kuoka au kuchoma katika oveni kisha mchome (grill) uwe unageuzageuza hadi aive.
Epua, weka kando.
Katakata vitunguu, nyanya/tungule, pilipili boga weka kando.
Katika sufuria ya kupikia biriani, tia mafuta, kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi ya hudhurungi (brown).
Tia nyanya na pilipili mbichi, pilipili boga na mchanganyiko uliopunguza awali.
Tia kuku uchaganye vizuri.
Wakati unakaanga vitunguu ili uokoe muda, huku chemsha mchele uive nusu kiini, mwaga maji, chuja.
Punguza masala nusu yake weka kando.
Mimina wali kiasi juu ya masala, kisha mimina masala yaliyobakia kisha juu yake tena mimina wali.
Funika upike katika oveni hadi uive.
Changanya unapopakua katika sahani.

Jinsi ya kutengeneza biskuti za Matunda Makavu Na Cornflakes

VIAMBAUPISHI

Unga – 4 Vikombe

Sukari – 1 Kikombe

Baking powder 1 kijiko cha chai mfuto

Siagi – 454 gms

Mayai – 2

Matunda makavu (tende, zabibu, lozi) – 1 Kikombe

Vanilla – 2 Vijiko vya chai

Cornflakes – ยฝ kikombe

JINSI YA KUANDAA

Changanya sukari na siagi katika mashine ya keki (cake mixer) mpaka iwe laini (creamy)
Tia yai moja moja huku unachanganya mpaka iwe laini kama sufi. (fluffy)
Tia unga, baking powder, matunda makavu, changanya na mwiko.
Chota mchanganyiko wa biskuti kwa mkono kama (kiasi cha kijiko kimoja cha supu) fanya duara na uchovye katika cornflakes iliyopondwa kwa mkono (crushed)
Zipange katika treya ya kupikia na zipike (bake) katika moto wa 375ยฐF kwa muda wa kiasi dakika 15 huku unazitazama tazama.

Mapishi ya Sponge keki

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) 100g
Sukari (sugar) 100g
Siagi isiyokuwa na chumvi (unsalted butter) 100g
Mayai (eggs) 2
Vanila 1 kijiko cha chai
Chumvi pinch
Warm water 3 vijiko vya chakula

Matayarisho

Kwanza washa oven moto wa 200ย C. Baada ya hapo saga butter na sukari mpaka viwe laini kisha tia mayai na uendelee kusaga mpaka vichanganyike vizuri kisha tia unga, vanila, chumvi na na maji na usage mpaka upate uji usiokuwa mzito sana au mwepesi sana. Baada ya hapo utie kwenye baking tin na u bake kwa muda wa dakika 25 na mpaka cake yako iive yani juu na chini iwe ya brown na ukidumbukiza kijiti katikati kinatoka kikiwa clean. Baada ya hapo itoe kwenye tin na uiache ipoe. Ikisha poa itakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Samaki Na Rojo La Bilingani Na Viazi/Mbatata

Wali Wa Nazi

Mpunga – 4 vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha
Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.
Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi Wa Samaki Nguru

Samaki – 4

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 2 viijiko vya supu

Kitunguu maji kilokatwakawa – 2 slice ndogo

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Pilipili mbichi – 2

Kotmiri ilokatwakatwa – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ยผ kikombe

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata samaki mkaange kwa kumtia viungo.
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi thomu na tangawizi mbichi, nyanya, nyanya kopo, kitunguu na bizari ya mchuzi endelea kukaanga.
Tia maji kiasi na ndimu, pilipili mbichi ilosagwa kisha tia kotmiri.
Mwisho tia nusu ya samaki alokaangwa ukiwa tayari

Bilingani Za Kukaanga Na Viazi

Bilingani – 4 madogodogo

Viazi/mbatata – 3

Nyanya – 3

Majani ya mchuzi/mvuje/curry leaves – kiasi 6-7

Nnyanya kopo – 2 vijiko vya supu

Methi/uwatu ulosagwa – 1 kijiko cha chia

Rai/mustard seeds – 1 kijiko cha supu

Bizari ya manjano/haldi/turmeric – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

1. Weka mafuta ya kukaangia katika karai

2. Katakakata bilingani vipande vipande vya mraba (cubes) kaanga katika mafuta ya moto hadi yageuke rangi. Eupa weka kando.

3. Katakataka viazi/mbatata vipande vidogodogo vya mraba (cubes) Kaanga hadi viive epua weka kando.

4. Ondosha mafuta yote katika karai bakisha kidogo tu kiasi ya vijiko 2 vya supu.

5. Kaanga rai kisha majani ya mchuzi, na methi/uwatu kisha kaanga nyanya.

6. Tia nyanya ya kopo kisha changanya pamoja bilingani na viazi ikiwa tayari.

Mapishi ya Pilau ya nyama ya ng’ombe na kachumbari

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 3)
Nyama ya ng’ombe (beef 1/2 kilo)
Viazi mbatata (potato 3)
Vitunguu maji (onions 3)
Kitunguu swaum (garlic cloves 4)
Tangawizi iliyosagwa (ginger kiasi)
Hiliki nzima (cardamon 4)
Karafuu (clove 4)
Pilipili mtama (blackpepper 4)
Amdalasini (cirnamon stick 1)
Binzari nyembamba nzima(cumin seeds 1/2 ya kijiko cha chai)
Binzari nyembamba ya kusaga (ground cumin 1 kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Nyanya (fresh tomato 3)
Limao (lemon 1)
Pilipili (chilli 1)
Hoho (green pepper)

Matayarisho

Chemsha nyama na chumvi na nusu ya limao mpaka iive kisha weka pembeni. Baada ya hapo andaa vitu vya pilau kwa kuloweka mchele kwenye maji kwa muda wa dakika 10.Menya na kukatakata vitunguu na viazi kisha weka pembeni na pia chemsha maji ya moto na uweke pembeni. Baada ya hapo weka sufuri jikoni na tia mafuta kiasi . Yakisha pata moto tia vitunguu na uvikaange mpaka viwe vya rangi ya kahawia na kisha uitie nyama na ikaange mpaka ipate rangi ya bown pia. Baada ya hapo tia kitunguu swaum na tangawizi na uikoroge vizuri kisha iache ikaangike kwa muda wa dakika 2 kisha tia spice ambazo ni Binzari nyembamba ya unga, hiliki,karafuu, amdalasini na pilipili mtama na viazi. Baada ya hapo unatakiwa ugeuze geuze mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri kisha tia mchele na ugeuzege mpaka uchanganyike na viungo. Baada ya hapo tia chumvi na maji ya kutosha na ukoroge vizuri kisha funika na uache uchemke katika moto wa wastani. Maji yakikaribia kukauka tia binzari nyembamba nzima na ufunike uache mpaka maji yakauke kabisa. maji yakisha kauka ugeuze na ufunike tena na uuache mpaka uive.
Baada ya hapo andaa kachumbali kwa kukatakata vitunguu katika bakuli na kisha tia chumvi kwa ajili ya kuondoa ukali wa vitunguu. Baada ya hapo vioshe mpaka chumvi yote iishe. osha nyanya, Pilipili, hoho na kisha katakata slice nyembamba na uchanganye na vitunguu. Baada ya hapo tia chumvi, kamulia limao na uchanganye zote pamoja. Baada ya hapo chakula kitakuwa tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
๐Ÿ  Home ๐Ÿ“– Reading ๐Ÿ–ผ๏ธ Gallery ๐Ÿ’ฌ AI Chat ๐Ÿ“˜ About