Mrija wa mkojo (urethra) ni kiungo muhimu kinachotoa mkojo nje ya mwili kutoka kwenye kibofu. Mrija huu unaposinyaa au kuziba hufanya utokaji wa mkojo kuwa wa
mashaka na maumivu makubwa. Kusinyaa/ Kuziba kwa mrija wa mkojo huitwa pia
urethral stricture.
Visababishi na vihatarishi vya tatizo hili
Kusinyaa kwa mrija wa mkojo husababishwa na kovu linalotokea katika sehemu ya
mrija baada ya mtu kuumia, kufanyiwa upasuaji au kupona magonjwa ya zinaa.
Inaweza pia kusababishwa na uvimbe karibu na eneo la kinena unaokandamiza mrija.
Vihatarishi vya tatizo hili ni pamoja na
Kuwa na historia ya kuugua magonjwa ya zinaa
kuwahi kuwekewa mipira ya mkojo au vifaa vya namna hiyo (catheter au
cystoscope)
- Kuvimba tezi dume (BPH) kwa wanaume
- Kuwa na historia ya kuumia au kupata majeraha maeneo ya kinena. Hii hutokea
sana kwa wale wanaopata ajali wakiendesha baiskeli
- Kupata maambukizi ya mara kwa mara ya mrija wa mkojo (urethritis)
- Ni nadra sana kwa tatizo hili kutokea kwa wanawake. Aidha ni nadra pia kwa
mtoto kuzaliwa akiwa na tatizo hili (congenital urethral stricture).
Dalili za tatizo hilo.
Mtu mwenye tatizo hili anaweza kuwa na dalili zifuatazo,
- Kutoa shahawa zilizochanganyika na damu.
- Kukojoa mkojo mweusi au uliochanganyika na damu.
- Kupungua kwa kiasi cha mkojo kinachotolewa.
- Kukojoa kwa shida.
- kutoa uchafu katika mrija wa mkojo.
- kukojoa mara kwa mara.
- Kushindwa kumaliza mkojo wote.
- Kushindwa kuhimili kutoka kwa mkojo (mkojo kujitokea wenyewe/kujikojolea).
- Maumivu wakati wa kukojoa.
- Maumivu chini ya tumbo.
- Maumivu ya kinena
- Mtiririko dhaifu wa mkojo (hutokea taratibu au ghafla)
- Mkojo kutawanyika ovyo wakati wa kukojoa
- Kuvimba uume
Uchunguzi
Daktari atakufanyia uchunguzi wa mwili na namna unavyokojoa. Uchunguzi wa mwili
unaweza kuonesha:
- Kupungua kwa mkondo wa mkojo
- Uchafu kutoka katika mrija wa mkojo
- Kibofu kilichojaa/kuvimba
- Kuvimba kwa mitoki ya maeneo ya kinena
- Tezi dume iliyovimba au yenye maumivu
- Kuhisi kitu kigumu chini ya uume
- Uume kuvimba au kuwa mwekundu
- Hata hivyo, wakati mwingine uchunguzi unaweza usioneshe tatizo lolote lile.
Vipimo
Vipimo ni pamoja na
- Kipimo cha kuchunguza mrija pamoja na kibofu cha mkojo (cystoscopy)
- Kuangalia kiasi cha mkojo kinachobaki katika kibofu baada ya kukojo (Post-void
residual (PVR) volume)
- X-ray ya mrija wa mkojo (Retrograde urethrogram)
- Vipimo vya magonjwa ya zinaa
Matibabu
Mrija unaweza kutanuliwa wakati wa kipimo cha cystoscopy na hiyo ikawa ndiyo
mojawapo ya tiba. Iwapo njia ya kutanua mrija haioneshi mafanikio sana, upasuaji
unaweza kuhitajika. Upasuaji unategemea eneo lilipo tatizo na ukubwa wa tatizo.
Kama tatizo ni dogo/fupi na lipo mbali na bawabu inayotenganisha mrija na kibofu cha mkojo,
linaweza kutatuliwa kwa kukata kasehemu kalikoziba wakati wa kufanya cystoscopy au
kwa kuweka kifaa maalum cha kuzibua na kutanua mrija.
Kama tatizo ni kubwa zaidi, upasuaji wa wazi wa eneo husika unaweza kufanyika.
Upasuaji huu unajumisha kukata sehemu iliyoziba na kisha kukarabati sehemu hiyo.
Kwa mgonjwa ambaye amepata shida ya ghafla ya kushindwa kutoa mkojo (acute
retention of urine), matibabu ya dharura ya kumuwekea catheter kupitia juu ya kinena
(suprapubic catherization) hufanyika. Hii husaidia kibofu kutoa mkojo nje kupitia kwenye
bomba lililowekwa chini ya tumbo.
Ifahamike kuwa mpaka sasa hakuna dawa ya tatizo hili zaidi ya njia za upasuaji na
nyingine zilizoelezwa hapo juu.
Matarajio
Mara nyingi matibabu huleta matokeo mazuri na mgonjwa anaweza kuishi maisha yake
kama kawaida. Hata hivyo wakati mwingine, mgonjwa anaweza kuhitaji matibabu ya
mara kwa mara ili kuondoa sehemu ya kovu iliyopo katika mrija wa mkojo.
Madhara ya tatizo hili
Tatizo hili halina budi kutibiwa haraka maana kama likiachwa linaweza kusababisha
kuziba kabisa kwa njia ya mkojo na kusababisha mkojo kujaa katika kibofu, hali
ambayo, pamoja na kuleta maumivu makali kwa mgonjwa inaweza pia kusababisha figo
kushindwa kufanya kazi (ARF).
Kinga
Ni muhimu kujikinga dhidi ya magonjwa ya zinaa kwa kufanya ngono salama au kuacha
kabisa kufanya ngono. Aidha kuwa makini na kazi au mambo ambayo yanaweza
kukusababishia kuumia maeneo ya kinena.
References:
Google ScholarResearchGate
Semantic Scholar
AckySHINE