Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha mama mjamzito mimba yake kuharibika. Sababu kuu huwa ni magonjwa kama vile ugonjwa hatari wa malaria, ugonjwa unaotokana na zinaa kama vile kaswende na kisonono na U.T.I, dawa fulani fulani mfano Albendazole, Misoprostol, Metronidazole na kadhalika.
Lakini pia mjamzito akifanya kazi za kutumia nguvu nyingi anaweza kusababisha mimba yake kuharibika. Lakini kuna sababu nyingi ambazo zinasababisha mimba kutoka huweza kuzuilika kwa kwenda kliniki mapema yaani pale tu unapohisi una mimba hata kama ni wiki mbili na kufuata ushauri wa wataalamu.
Ukweli ni kwamba kuna wanawake wengi mimba zao huharibika na wao hushindwa kugundua mapema na matokeo yake anakaa na mtoto mfu hata miezi kadhaa bila kujua.
Zipo dalili ambazo husababisha mimba kuharibika kama tutakavyoona leo hapa. Dalili hizo ni hizi zifuatazo:
1. Kuwa na maumivu makali tumboni.
Ikiwa mjamzito atakuwa ana maumivu makali ya tumbo wakati ni mjamzito hiyo pia ni dalili mbaya. Kwa kawaida maumivu makali ya tumbo hasa kwa mimba kubwa ya miezi zaidi ya mitano au mimba ndogo kama mwezi mmoja, basi kuna uwezekano mkubwa kondo imeanza kujiondoa kwenye kizazi kwa mimba kubwa au mimba ndogo imeshindwa kuendelea kukua na moja kwa moja hiyo inaweza kuwa dalili ya kuwa mimba imeharibika.
2. Mimba kutokukua
Ikiwa mimba itaacha kuongezeka au kukua ni dalili nyingine ya mimba kuharibika. Kila mtu aliye mjamzito anategemea mimba iwe inakua kila siku na iwe kubwa kulingana na umri unavyozidi kwenda mbele, ikiwa mimba iko vilevile kwa miezi kadhaa, yaani haikui au ukubwa wa tumbo haubadiliki ujue kwamba mimba hiyo imeharibika, ili kupata uhakika wahi hospitali kupimwa.
3. Mtoto kuacha kucheza tumboni.
Ikiwa mtoto ataacha kucheza tumboni ni tatizo kubwa kwani kwa kawaida mtoto huanza kucheza akiwa na wiki ya 18 mpaka 20 kwa wanawake ambao hawajawahi kubeba mimba na wiki ya 16 mpaka 20 kwa wanawake ambao wameshawahi kuzaa. Ikitokea mtoto aliye tumboni ameshawahi kucheza lakini ghafla akawa hachezi au muda huo umepitiliza na bado kimya kuna uwezekano mkubwa ikawa mtoto huyo amefia tumboni, hivyo haraka sana wahi hospitali kumuona daktari.
4. Kutokwa na damu nyingi sehemu za siri.
Mjamzito akitokwa na damu nyingi sehemu za siri ni dalili kwamba mimba imeanza kuachia na mlango wa uzazi umeanza kufunguka, na hiyo inaashiria kwamba kuna mambo mawili yameshatokea kwanza inawezekana mtoto ameshafia tumboni au bado hajafa, lakini kama damu imetoka kwa wingi inaashiria kuwa mtoto huyo aliye tumboni atakufa tu.
5. Kutoka na vipande vya vyama sehemu za siri.
Ikiwa mama mjamzito atakuwa akitokwa na vipande vya nyama sehemu za siri ni dalili mbaya sana. Kutokwa na vipande vya nyama sirini ni kuashiria kwamba kuna mtoto ameharibika tumboni. Hali hiyo ya hatari ikitokea mjamzito anatakiwa asafishwe kuondoa masalio yaliyobaki.
6. Kupotea kwa dalili za ujauzito.
Kupotea kwa dalili za ujauzito ni tatizo lingine baya kwa mama mjamzito. Mara kwa mara mwanamke akiwa na ujauzito anakuwa na dalili nyingi kama vile kuwa na kichefuchefu, kukosa hamu ya kula baadhi ya vyakula, kutapika, kulamba vitu vichachu kama vile limao, ndimu, wengine hula udogo na wengi hubadilika sana tabia, hivyo basi dalili zote hizo za mimba zikisimama ghafla basi ujue mimba imeharibika.
Read and Write Comments