Mafuta kwenye kondomu

Mafuta yanayowekwa kwenye pakiti ya kondomu ni mafuta maalum na yana kazi ya kuhifadhi kondomu mpaka siku yake ya kutumiwa. Bila mafuta haya kondomu isingekuwa imara, ingekauka na isingekuwa nyumbufu vya kutosha. Vilevile mafuta hayo yanalainisha mpira ili kurahisisha uvaaji na matumizi yake. Kwa watu wengi, mafuta haya hayawaletei matatizo yoyote. Watu wachache sana ambao ngozi yao ni nyepesi kuathirika wanapata matatizo ya kuwasha baada ya kutumia kondomu.

Muwasho huwa sio wa kudumu. Watu wa namna hii wanashauriwa kunawa na sabuni ya kawaida baada ya kujamiiana.
Kuna uvumi kwamba mafuta haya yaliyomo ndani ya pakiti ya kondomu yana virusi vya UKIMWI. Hii siyo kweli, mafuta hayo yanawekwa kwa ajili ya kuhakikisha uimara wa kondomu tu.

Je, mbegu za kiume zinaweza kupita kwenye kondomu?

Hapana, mbegu za kiume haziwezi kupita kwenye kondomu. Kondomu zimetengenezwa ili kuzuia mbegu za kiume kufikia ukeni wakati wa kujamiiana. Kwa sababu shahawa haziwezi kupita kwenye kondomu, kondomu ni njia nzuri ya kuzuia mimba pamoja na maambukizi ya magonjwa ya zinaa pamoja na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Watu wengine wanasema kwamba kuna mashimo madogo kwenye kondomu yanayorahisisha mbegu pamoja na vijidudu vya magonjwa ya zinaa kupita. Huu ni uongo. Ukitaka kuwa na uhakika kwamba kondomu mpya haina mashimo, chukua kondomu moja na ijaze maji ya kawaida. Utaona kwamba maji hayapiti kwenye kondomu kabisa. Baada ya kujaribisha itupe kondomu ndani ya choo cha shimo au ichome moto, lakini usiitumie wakati wa kujamiiana

Kupasuka kwa kondomu

Kupasuka kwa kondomu mara nyingi kunasababishwa na kondomu kutowekwa vizuri uumeni. Ni muhimu sana kutoa hewa ndani ya kondomu wakati wa kuvalisha uume. Kwa sababu ile hewa ndani ya kondomu inaweza ikasababisha kondomu kupasuka wakati wa kujamiiana.
Vilevile siyo vizuri kupaka mafuta kama vaselini juu ya kondomu ili kurahisisha kitendo cha kuingiliana. Mafuta kama vaseline yanadhoofisha uimara wa kondomu na yanarahisisha kondomu kupasuka. Mafuta haya yanayowekwa kwenye pakiti ya kondomu yanahifadhi uimara wa kondomu, na ni aina maalumu ya mafuta.
Ni muhimu kukumbuka kwamba mwanaume akivaa kondomu vizuri jinsi tulivyoeleza awali, uwezekano wa kondomu kupasuka ni mdogo sana.

Ukubwa wa kondomu

Kuna aina kondomu za ukubwa mbalimbali. Kwa wastani ukubwa wa kondomu unafaa kwa wanaume watu wazima karibu wote na vijana balehe waliokomaa. Mara chache sana, kondomu ni ndogo kwa wanaume fulani, lakini wakati mwingine wanaume wanaringa tu kuwa na uume mkubwa au wanatumia kisingizio tu kwa sababu hawataki kutumia kondomu.
Kwa upande wa vijana, balehe kondomu zinaweza kuwa ndogo ukilinganisha na ukubwa wa uume wao. Kwa vijana, ambao uume bado mdogo, ni vizuri zaidi wangeacha kujamiiana badala yake watumie njia nyingine za kumaliza hamu ya kutaka kujamiiana kama vile kukumbatiana na kubusu.

Jinsi ya kutumia kondomu ya kike

Kondomu ya kike inafahamika kwa jina la β€žcareβ€œ na β€œLady Peteta”. Hapa Tanzania hazipatikani sehemu zote na bei yake ni kubwa kidogo.
Kondomu ya kike huingizwa ukeni kabla ya kujamiiana. Kama unatumia kondomu ya kike, chana kwa uangalifu pembezoni mwa pakiti. Kondomu ina pete mbili za plastiki na uwazi upande wa juu. Pete moja imelegea ni ndogo na iko kwa ndani, upande usio na uwazi. Pete ya pili ni kubwa zaidi, imeshikiliwa na iko upande wa tundu. Shikilia kondomu upande uliozibwa na minya pete ya ndani kwa dole gumba na kidole cha pili na cha kati. Mara nyingine inaweza ikakuponyoka, (kuteleza) lakini endelea kujaribu hadi umeiminya vizuri. Tafuta mkao mzuri na ingiza kondomu ya kike. Huku bado unaminya kwa vidole vyako iongoze kondomu ndani ya uke wako. Ukiiachia pete ya ndani itashikilia kondomu ndani ya uke. Sasa ingiza kidole chako kwenye kondomu, sukuma pete mpaka inapogota kwenye mlango wa uzazi.
Kondomu ya kike inaweza kuvaliwa saa kadhaa kabla ya kufanya ngono na pia inaweza kuvuliwa baada ya muda wa kufanyika ngono kupita. Ili kuhakikisha kuwa uume umeingia sehemu husika, msaidie mwenzi wako kuongoza uume kuingia kwenye uke ili usipenye pembeni.
Baada ya kujamiiana, vua kondomu kwa uangalifu. Tupa kondomu iliyotumika kwenye choo cha shimo au uichome. Usitupe kondomu iliyotumika ovyo.
Kama ilivyo kwa kondomu ya kiume, kondomu ya kike itatumika kwa mafanikio zaidi pale ambapo wahusikia wanakuwa na makubaliano na maelewano juu ya matumizi yake.

Jinsi ya kutumia Kondomu

Wakati wa kutumia kondomu ya kiume ni muhimu kufuata hatua zifuatazo. Hakikisha kwamba pakiti inayoihifadhi haijapasuka na kwamba tarehe ya kuisha muda wake haijafika.
Uume ukishadinda, fungua pakiti kwa uangalifu. Minya sehemu ya juu kutoa hewa ndani ya kondomu wakati wa kuvalisha uume, ili kuzuia kupasuka kwa kondomu wakati wa kujamiiana. Visha uume kondomu taratibu mpaka uufunike wote. Ukiwa na uhakika kwamba kondomu imevishwa inavyotakiwa, unaweza kukutana kimwili na mwanamke.
Wakati wa kutoa uume kutoka ukeni, uwe mwangalifu kwamba kondomu bado ipo sehemu inayopaswa kuwa. Baada ya kutoa uume kutoka ukeni, vua kondomu kwa uangalifu uume ukiwa bado umedinda, ili kuepuka shahawa zisimwagikie ukeni. Tupa kondomu iliyotumika kwenye choo cha shimo au uichome. Usitupe kondomu iliyotumika ovyo. Pia usitupe kondomu iliyotumika kwenye vyoo vya kisasa yaani vya kuflashi na maji.
Ukinunua β€œsalama kondomuβ€œ ndani ya pakiti, kuna maelekezo kuhusu matumizi ya kondom. Unapotaka kutumia kondom wakati wa kujamiiana, ni vizuri ukajaribisha kwanza ukiwa peke yako ili kuzoea jinsi ya kuitumia.

Njia ya kuzuia mimba inayofaa kwa kijana anayeanza kujamiiana

Kila njia ya kuzuia mimba ina faida na hasara zake. Kwa mfano faida ya vidonge ni kwamba kama mwanamke atavimeza kila siku, hakuna haja ya kufanya chochote wakati wa kujamiiana. Matatizo ya vidonge ni kwamba mwanamke anahitaji kufikiria kuvinywa kila siku. Kondomu, kwa mfano ina faida kwamba pamoja na mimba inazuia magonjwa ya zinaa, lakini kasoro yake ni kwamba unahitaji kuivaa wakati wa kujamiiana.
Hakika, ushauri wa sasa ni kuwa kondomu ndiyo njia bora zaidi kwani ni njia pekee inayozuia kwa pamoja mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya magonjwa yatokananyo na kujamiiana.

Je, ni lazima kumeza vidonge vya kuzuia mimba siku zote, hata zile siku nisipojamiiana?

Ndiyo, vidonge vya kuzuia mimba ni lazima vimezwe kila siku hata kama hufanyi ngono siku hiyo. Kuna aina ya vidonge vya kuzuia mimba inayokuja katika pakiti yenye vidonge 21 na kuna inayokuja katika pakiti ya vidonge 28. Iwapo utapewa ile ya vidonge 21 utapumzika kunywa siku 7 katika mwezi. Iwapo utapewa ile ya vidonge 28, itabidi kumeza kidonge kimoja kila siku, hata siku za hedhi. Ili kuhakikisha vidonge vya kuzuia mimba vinafanya kazi sawasawa, mwulize yule aliyekushauri kutumia vidonge hivyo jinsi ya kuvimeza.
Kama mwanamke akisahau kunywa kidonge hata kama ni siku moja kuna uwezekano wa kupata mimba. Anaposahau kumeza vidonge, ni vizuri zaidi watumie kondom wakati wa kujamiiana kwa kuhakikisha kutopata mimba. Hii inahusika vilevile kama mwanamke ameharisha au ametapika katika kipindi cha saa 4 tangu ameze vidonge. Kama mwanamke anashindwa kukumbuka kunywa vidonge mara kwa mara, ni vizuri zaidi apate ushauri kutoka kwenye kliniki ya uzazi wa mpango kutumia njia nyingine ya kuzuia mimba.

Je, baada ya kutumia vidonge au sindano kwa muda mrefu, mwamamke akiacha kuzitumia hizo njia ataweza kupata mimba tena?

Vidonge na sindano zinazuia mimba kwa kuzuia yai lisipevuke. Akitumia njia hizi za kuzuia mimba, mwanamke anaona hedhi yake kama kawaida, lakini hakuna yai linalokuwa limepevuka kwa ajili ya kurutubishwa.
Mara mwanamke akiacha kutumia vidonge, mayai hupevuka tena ndani ya kokwa na mwanamke huweza kupata mimba. Mwanamke aliyetumia sindano, anaweza akachukua muda kiasi kurudia hali yake ya uzazi. Kwa wanawake wengine inachukua miezi 12.
Muhimu ni kukumbuka kwamba sindano na vidonge siyo njia za kudumu za kuzuia mimba, hata kama itachukua muda fulani kurudia hali ya kawaida ya uzazi

Vidonge vya kuzuia mimba vinasababisha vidonda vya tumbo?

Wanawake wengine wanapata vidonda vya tumbo, lakini haya hayana uhusiano na vidonge vya kuzuia mimba. Vyanzo vya vidonda vya tumbo mara nyingi ni maambukizi yatokanayo na msongo wa mawazo, kula vyakula vyenye mafuta mengi na viungo vingi, au kuwa na historia ya ugonjwa huu katika familia. Baadhi ya dawa huathiri tumbo kama vile asprini na ndiyo maana sio kila mtu anashauriwa kuzitumia. Vidonge vya kuzuia mimba havisababishi vidonda vya tumbo.

Umri wa kuanza kutumia njia za uzazi wa mpango

Muda unaofaa kutumia njia ya kupanga uzazi ni wakati unapojamiiana kwa mara ya kwanza. Huu ni wakati mzuri wa kutumia kondomu, kwa sababu kondomu inazuia kupata mimba isiyotarajiwa pamoja na magonjwa ya zinaa.
Huu pia ni muda mzuri wa kwenda kliniki ili kupata ufafanuzi kuhusu njia mbalimbali za kuzuia mimba. Daktari au muuguzi anaweza kuwasaidia mwanaume na mwanamke kuamua njia inayofaa kwa hali yao.
Mara nyingi, watu wanafikiri kwamba huduma ya uzazi wa mpango ni kwa wanawake ambao wameshaolewa, kwa mama wajawazito au wanawake waliozaa tu. Lakini si kweli. Hapa Tanzania, kisheria kila mtu aliyebalehe, iwe mvulana au msichana ana haki ya kupata huduma ya uzazi wa mpango.

Njia za Kuzuia Mimba

Njia za uzazi wa mpango zinatofautiana sana na zinaweza kugawanywa katika makundi mengi:

Vizuizi

(hizi huzuia mbegu kulifikia yai): Kuna mpira wa kiume (kondomu ya kiume), yaani mfuko wa mpira uliozibwa upande moja. Unavishwa kwenye uume uliosimama kabla ya kuingia ukeni. Pia kuna mpira wa kike (kondomu ya kike), yaani mpira unaoingizwa ukeni kabla ya kujamiiana.

Vidonge vya kuzuia mimba:

Lazima mwanamke anywe vidonge hivi kila siku hata kama hajamiiani.

Njia nyingine za kuzuia mimba kwa muda mrefu

. Njia hizi hazihitaji maandalizi maalum, ili kuzuia mimba, kabla ya kujamiiana na pia mwanamke hahitaji kukumbuka kufanya chochote kila siku. Kati ya njia hizi ni pamoja na sindano anazopewa mwanamke kila baada ya miezi mitatu. Pili, kuna vipandikizi, yaani vijiti vyembamba vya plastiki vinavyowekwa kwenye sehemu ya juu ya mkono wa mama kwa njia ya upasuaji mdogo. Vijiti vina kichocheo kinachozuia kupevuka kwa yai. Pia, kuna kitanzi ambacho ni kitu kidogo kilichotengenezwa kwa aina maalum ya plastiki. Kwa ufupi kinaitwa IUD. Huwekwa kwa utaalamu ndani ya mfuko wa uzazi. Sindano, vipandikizi na vitanzi lazima viwekwe na mtaalamu mwenye ujuzi kwenye kituo cha afya chenye vifaa vya kutosha. Kwa vile dawa za kuzuia mimba kwa muda mrefu zinaingiliana na mzunguko wa kawaida wa hedhi kwa kiasi, athari zake ni kubwa kuliko kutumia vidonge.

Kwa mwanaume na mwanamke kuna njia ya kudumu ya kufunga kizazi kwa njia ya upasuaji

. Kwa mwanaume mirija inayopitisha mbegu hukatwa na kufungwa, ili kuzuia mbegu zisitoke. Akijamiiana, anaweza kumwaga shahawa, lakini ndani ya shahawa hakuna mbegu. Kama mwanaume amefunga kizazi uume utadinda kama kawaida na kufikia mshindo atamwaga maji ya shahawa ambayo hayatakuwa na mbegu. Kwa mwanamke mirija ya kupitisha mayai hukatwa na kufungwa, ili kuzuia mayai kufika kwenye mfuko wa uzazi. Baada ya upasuaji huu, mama ataendelea na hedhi kama mwanzo, lakini yai halitaweza kukutana na mbegu za kiume tena.

Vilevile kuna njia nyingine mbalimbali ambazo hazina uhusiano na matumizi ya dawa au vizuizi vya mimba. Njia hizi hazina uhakika mkubwa wa kutopata mimba. Mara nyingine mama anatumia ishara mbalimbali, au tarehe kujua lini anaweza kupata mimba, ili kuepuka kujamiiana katika kipindi hicho. Kumwaga mbegu za kiume nje ya uke, au kutegemea kwamba mimba hazishiki wakati wa kunyonyesha ni njia nyingine za asili zinazotumiwa. Kumbuka kwamba njia hizi hutumika sana, lakini si njia salama sana za kuzuia mimba wala kuambukizwa na magonjwa ya zinaa.
Ni muhimu kukumbuka kwamba njia ya uzazi wa mpango inaweza kufaa kwa mtu huyu na isifae kwa mtu mwingine. Kwa hiyo, ni vizuri kila mtu aliyeamua kupanga uzazi apate ushauri kwenye kliniki kuhusu njia inayomfaa zaidi

Mapenzi salama ni yapi?

Mapenzi salama ni yale yanayofanyika bila wasiwasi wa kupata mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa pamoja na maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Mapenzi salama yanaweza kuwa ni vitendo vya kumaliza hamu bila uume kuingizwa ukeni. Ngono ya kuingiza uume ukeni inaweza kuwa ngono salama kama tahadhari husika zinatumika.
Vitendo vya kumaliza hamu bila kujamiiana ni kupiga busu, kukumbatia, kunyonyana ndimi, kushikana mikono na kupiga punyeto. Matendo haya yote ni salama kabisa kuhusiana na mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Ili kuhakikisha mnafanya mapenzi salama wakati mnahusisha mwingiliano kati ya uume na uke, lazima mchukue tahadhari. Tahadhari mojawapo ni uaminifu katika mapenzi, kwa maana wewe uwe mwaminifu na yeye awe mwaminifu. Lakini pia inabidi muwe na uhakika kwamba wote wawili hamjaambukizwa magonjwa wakati mnapojamiiana kwa mara ya kwanza. Tahadhari nyingine ni kutumia kondomu. Kondomu inazuia mimba pamoja na magonjwa ya zinaa. Kuwa mwaminifu pekee yake haitoshi kama mmoja wenu au wote wawili mliwahi kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi ambao haukuwa salama. Kama kweli mnataka kuwa upande wa uhakika wote ni vyema kwenda kupima Virusi vya Ukimwi kwa hiari.

Je, kama mwanamke na mwanaume wanapata watoto wa jinsia moja tu, ni kosa la nani?

Hakuna mwenye kosa, kwa sababu jinsia ya mtoto i inategemea na bahati na hamna uwezekano wa kupanga kuzaa aina fulani ya mtoto. Tulivyoona juu ni mwanaume ndiye aliye na aina mbili za mbegu. Aina moja husababisha kutokea mtoto wa kike na aina nyingine mtoto wa kiume. Mwanaume hana uwezo wa kuhakikisha achangie aina ya mbegu gani. Kwa hiyo, hata kama ni mwanaume anayeyakinisha jinsia ya mtoto, hana kosa, kwa sababu hana uwezo wa kuamua achangie mbegu ya aina gani.

Je, ni madhara gani atapata mama mjamzito endapo atajamiiana na mwenzi wake?

Kama kati ya mwanamke na mwanaume hakuna mwenye magonjwa ya zinaa, hakuna madhara yoyote kwa mwanamke mwenye mimba kujamii ana na mwenzi wake. Mfuko wa mimba hufunga kabisa na kifuko kinamzunguka mtoto vizuri, na hivyo hakuna uwezekano wowote wa mbegu za kiume kupenya na kumfikia mtoto.
Inashauriwa lakini wakati wa kujamii ana na mwanamke mjamzito tumbo lisigandamizwe sana. Wanawake wengine hawana hamu kubwa ya kujamii ana hasa mwishoni mwa ujauzito, na mwanaume anashauriwa kuheshimu hisia hizi za mwanamke.
Kama mwanaume atakuwa ameambukizwa magonjwa ya zinaa wakati wa kujamii ana, hii i ii inaweza kuwa hatari sana kwa mwanamke na pia kwa mtoto tumboni. Wakijamii ana mume na mke wakati wa ujauzito, lazima wawe na uhakika kwamba hamna mwenye magonjwa ya zinaa au watumie kondomu kwa ajili ya kinga. Iwapo watakuwa na wasiwasi wowote, wamwone daktari kwa uchunguzi.

Mama anayenyonyesha mtoto anaweza kupata mimba?

Katika miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua, mwanamke anayenyonyesha mtoto anapata kinga ya mimba kwa asilimia kubwa. Lakini i i inabidi mama anyonyeshe mtoto kwa kipindi kirefu (muda wote mtoto awe ananyonya maziwa ya mama tu na anyonye kila anapohitaji) na vilevile mama awe hajaanza kupata hedhi yake. Kama mama ameanza kupata hedhi yake au kama anampa mtoto chakula kingine, anaweza kupata mimba tena. Kwa hivyo, anashauriwa kutumia njia za kupanga uzazi i i ili kuzuia mimba za mfululizo.

Shopping Cart
0
    0
    Your Cart
    Your cart is emptyReturn to Shop
    🏠 Home πŸ“– Reading πŸ–ΌοΈ Gallery πŸ’¬ AI Chat πŸ“˜ About