Katoliki: Ibada

Mungu anapenda kutenda jambo baada ya mtu kumuomba/kusali ili mtu aelewe Ukuu wa Mungu na ili Mungu atukuzwe.
Mungu anapenda kutenda jambo baada ya mtu kumuomba/kusali ili mtu aelewe Ukuu wa Mungu na ili Mungu atukuzwe.

Maswali yanayoulizwa sana kuhusu Ibada ya Kanisa Katoliki

Masifu ni nini?

Masifu ni sala au wimbo unaomsifu na kumtambua Mungu kuwa Mungu


Ishara ndogo ya Msalaba juu ya panda la uso, mdomo, na kifua kabla ya Injili ina maana gani?

Maana yake ni kama Ahadi kuwa, Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu kwa akili yangu, Nitalitangaza kishujaa kwa Midomo yangu, Nitalipenda na kulishika kwa Moyo wangu wote.


Kwa nini wakatoliki wanaweka sanamu Kanisani?

Tunaweka sanamu Kanisani kwa sababu tunaheshimu anayewakilishwa na sanamu hiyo kwa mfano Yesu Kristo, Mama Bikira Maria, Malaika na Watakatifu; na kamwe hatuziabudu. (Kutoka 25:18-22)
Hata Waisraeli kwenye hekalu lao walikua na sanamu kama tunavyosoma hapa;
“18 Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. 19 Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku.20 Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. 21 Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. 22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli. (Kutoka 25 :18-22.)
Kwa hiyo kama Mungu mwenyewe aliagiza Sanamu za Malaika zichongwe na kusema atakua hapo na kuongea na watu wake. Je sio vyema zaidi kuwa na sanamu na Picha ya Mwanae wa Pekee Yesu Kristo na kuongea na Mungu mbele yake kama alitaka ya malaika ambao sio Mungu?
Mfano mwingine ni pale Mungu alivyomwabia Musa achonge Sanamu ya Nyoka wa shaba.
“BWANA akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti, ye yote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.’’ 9Kwa hiyo Mose akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu ye yote alipoumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.” (Hesabu 21:8-9).
Kwa Mfano huu Je tunaweza kusema kuwa sanamu ya nyoka ina nguvu ya uponyaji kuliko ya Yesu aliye Mungu? Kumbuka hapa watu walioona sanamu hii ya nyoka hawakukoponywa na nguvu ya sanamu ya shaba bali kwa nguvu ya neema ya Mungu kupitia Imani kwa Mungu. Kwa hiyo unaposali mbele ya picha au sanamu hautegemei nguvu ya sanamu bali unategemea neema ya Mungu kwa njia ya Imani yako kwa Mungu.
Kama vile Sanamu hii ya nyoka aliyoagiza Mungu iwekwe ilivyowekwa kwa nia ya uponyaji kwa yule aitazamaye vivyo hivyo Sanamu na Picha za Kanisani zinawekwa kwa nia maalumu na kwa neema maalumu. Ndiyo maana hazifanani. Na zinabarikiwa kwa kuombewa Baraka Ili zizae neema kwa wanaozitumia.

Sanamu au picha sio haramu bali maana ya hiyo sanamu au picha ndio inaiharamisha.

Kuna tofauti kati ya kuabudu na kuheshimu. Wakatoliki wanaweka sanamu kwa heshima na sio kwa kuabudu, ndio maana unaposali mbele ya picha ya Yesu hausali ee sanamu nisaidie bali unasema ee Yesu nisaidie.
Je tuseme tunamwabudu Raisi kwa kuheshimu picha yake kwa kuiinamia? Je tunaabudu bendera kwa kuheshimu na kupigia saluti? Je taratibu zabunge za kutoa heshima na taratibu za mahakama ni kuabudu?. Je kuapa mbele ya picha ya Raisi ni kumuabudu Raisi? Je kuapa na Biblia ni kuabudu Biblia? Je tunapobusu Biblia na kuitunza kwa heshima tunaiabudu? Tofauti ya Biblia na sanamu ni nini? Je, kwenye Biblia kinachoheshimiwa ni karatasi au maana ya yale maneno kwenye karatasi. Pengine usingeheshimu kama hujajua kuyasoma.
Kuna tofauti gani kati ya biblia yenye Maandishi na msalaba wa kuchonga wenye kuonyesha kile kinachosemwa na biblia? kama unaweza kuheshimu biblia yenye karatasi tena pale unapoweza kuzisoma na pengine ungeizarau kama ni ya lugha tofauti na hujui kilichoandikwa? Je Msalaba uliobeba maana ya kile kilichoandikwa kwenye Biblia unaona si kitu? Kama Kinachoheshimiwa kwenye Biblia sio karatasi bali maana maneno yaliyoandikwa vivyo hivyo kinachoheshimiwa kwenye picha au sanamu sio chuma yake au mti ukiochongwa bali ni maana ya hiyo sanamu.
Hii ndio maana nasema kuna tofauti ya kuabudu na kuheshimu.
Kumbuka kuwa picha au sanamu yoyote ya Kikatoliki lazima ibarikiwe kwanza ndio uweze Kusali mbele yake. Inapobarikiwa inaombewa uwepo wa yule anayewakilishwa na picha/sanamu hiyo uwe pale sanamu ilipo na anayesali pale sala yake Ifike kwa mlengwa anayeonekana kwa ishara ya sanamu/picha. Kwa Mfano askofu au padri anapobariki sanamu ya Yesu anaomba kuwa “Yesu awepo pale kwenye sanamu na Neema zake”, kwa hiyo yeyote anayesali mbele ya sanamu hiyo anaamini kuwa Yesu yuko pale na anasali Mbele yake. Kwa hiyo kinachopewa heshima sio ile sanamu bali ni yule anayeonekana kwa ishara ya ile sanamu au picha.

Tofauti ya Sanamu za Kikatoliki na za kipagani ni Kwamba,

Sanamu za Kipagani: Sanamu hizi huchukuliwa kama Mungu na huabudiwa na kutolewa Sadaka kama Mungu Mwenyewe.

Sanamu za Kikatoliki: Sanamu hizi huchukuliwa kama ishara ya kile inachokiwakilisha, haiabudiwi kamwe bali inaheshimiwa tuu.

Daima Tumia Sanamu na Picha zilizobarikiwa kwani zimenuiwa uwepo wa yule inayemuwakilisha na utaongea naye hapo. Sisi tunaamini kwamba kwenye Sanamu ya Yesu kuna uwepo wa Yesu. Kama vile Mungu anavyowaambia Waisraeli katika (Kutoka 25 :22) baada ya kuwaagiza wachonge sanamu za Makerubi (Malaika) 22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli. (Kutoka 25 :22)Sanamu au picha ni ishara wazi ya uwepo wa kile kisichoonekana.

Jifunze kupitia Sanduku la Agano na Msalaba wa Yesu

Kwenye Agano la kale: Ndani ya hekalu la Waisraeli walikua na Sanduku la agano, sanduku hilo lilikua na vibao vya Amri za Mungu ambavyo ni Ishara ya Agano lao na Mungu na ndani ya sanduku kulikuwepo pia Mfano wa Kiti ambacho kimezugukwa na sanamu za viumbe kama malaika nyuso zao zikielekea kiti hicho Kutoka 25:10-22. Waisraeli walikua wanasali kuelekea sanduku la Agano wanapokuwa Hekaluni na hata wakiwa majumbani mwao walisali kuelekea upande lilipo Hekalu. Waisraeli walisali kuelekea Sanduku la Agano wakiamini kwamba Mungu yupo kati ya sanduku lile. Lakini sanduku lile halikuwa Mungu. Waisraeli waliona fahari juu ya Sanduku lile na walilithamini na kuliheshimu kwa kuwa lilionyesha uwepo wa Mungu na popote lilipokuwa waliamini Mungu yupo.
Kwenye Agano jipya: Wakristu wanasali Mbele ya Msalaba wa Yesu ambao unaonyesha kazi ya wokovu alioufanya Yesu kwa wanadamu ya Kuwakomboa watu kwa kifo chake Msalabani. Na Msalaba huo ni Ishara ya Ukombozi wa Agano jipya na la Milele. Kama ilivyokuwa kwa Sanduku la Agano, Wakristu wanaheshimu msalaba ambao ni ishara ya wokovu wao na wanaamini kuwa Mungu yupo kati ya Msalaba huo lakini Msalaba huo sio Mungu. Wakristu wanaona fahari juu ya msalaba wa Yesu kwa kuwa ndio ishara ya wokovu wao.
FUNZO:Kupitia Mfano wa Sanduku la Agano na Msalaba tunajifunza kuwa Vyote havikuwa Mungu ila vinaheshimiwa kwa Imani kuwa Mungu yupo pale. Vilevile, vyote ni ishara ya wazi ya Agano la Mungu na Wanadamu.

Kwa nini tunasali mbele ya Picha/Sanamu na Hasa kufanya Ishara ya msalaba?

Tunasali mbela ya sanamu kwa sababu tunaamini sanamu inaakisi uwepo wa mhusika aliyechorwa au kuchongwa kwenye hiyo sanamu/picha. Ndio maana wakatoliki wanasali kwenye picha au sanamu iliyobarikiwa tuu kwa sababu Sanamu inapobarikiwa inaombewa uwepo wayule anayewakilishwa pale.
Tunafanya ishara ya msalaba kwenye sanamu kama sala ya utangulizi ambayo inathibitisha kuwa hatuabudu kile kilichoko pale bali kile tunachokifanya tunakifanya huku tukikiri Umungu na Heshima ya Utatu Mtakatifu (Mungu; Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.). Vile vile tunamtukuza Mungu katika Utatu Mtakatifu kwa sababu ya yule anayewakilishwa na picha au sanamu.

Kwa nini watu wanabusu picha na sanamu?

Hii ni ishara ya Upendo kwa yule anayewakilishwa kwenye picha au sanamu husika. Hata katika maisha ya kawaida watu hubusu picha za wazazi na wapendwa wao. Maana ni ile ile.


Tumuadhimishe nani?

Tumuadhimishe Mungu pekee siku zote za maisha yetu kwa tumaini la kumuadhimisha milele.
“Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, nitalihimidi jina lako milele na milele. Kila siku nitakuhimidi, nitalisifu jina lako milele na milele” (Zab 145:1-2).
“Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina” (Rom 11:36).


Je, tumuadhimishe Mungu katika Nafsi zake tatu pia?

Ndiyo, tumuadhimishe Mungu katika Nafsi zake tatu pia: Baba kama asili ya umungu na ya uhai wote, Mwana kama Neno wake aliyejifanya mtu atukomboe, tena Roho Mtakatifu kama Upendo wao ambao unawaunganisha na kututakasa.
Pamoja na viumbe vyote tuwaimbie usiku na mchana, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja!” (Ufu 4:8).
“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yoh 4:24).


Tumuadhimishe Mungu kwa jinsi alivyo au kwa maajabu anayotutendea?

Tumuadhimishe Mungu kwa jinsi alivyo, halafu kwa maajabu anayotutendea tangu awali, ambayo anatujulisha kidogo jinsi alivyo.
“Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele” (Zab 136:1).


Tumuadhimishe Mungu hasa kwa maajabu gani?

Tumuadhimishe Mungu hasa kwa maajabu aliyoyatenda katika Yesu, lakini pia katika Maria na wengine ambao wamefanana naye na kutuonyesha uwezo wa neema yake kwetu.
“Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa” (Ef 1:5-6).
Yeye atakuja “ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki” (2Th 1:10).


Tumuadhimishe Mungu kwanza kwa njia gani?

Tumuadhimishe Mungu kwanza kwa kumsikiliza kwa makini na kumuitikia kwa imani.
“Masikio ya watu wote yalikisikiliza kitabu cha torati… watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati” (Ne 8:3,9).
Kunyamaza ni sehemu ya ibada yoyote: tunahitaji kimya ili tuelewe tunachoambiwa na tunachosema.
“Nisikieni nyote na kufahamu” (Mk 7:14).
“Hamjui mnaloliomba” (Mk 10:38).


Je, ibada zetu ziishie katika kusadiki?

Hapana, ibada zetu zisiishie katika kusadiki, kwa kuwa tangu Agano la Kale Mungu aliagiza matendo mbalimbali ya ibada yanayolisha imani.
“Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako: Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa… Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu” (Mwa 17:10,12).
“Mwanakondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja… Kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni… Ni Pasaka ya Bwana… Siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana” (Kut 12:5,6,11,14).
Kwetu sisi Wakristo ni yale tuliyoagizwa na Yesu ili yatuletee wokovu.
“Aaminiye na kubatizwa ataokoka” (Mk 16:16).


Kanisa linaitaje ibada hizo tulizoagizwa na Yesu?

Kanisa linaita ibada hizo tulizoagizwa na Yesu sakramenti, yaani mafumbo. Ziko saba: Ubatizo, Kipaimara, Ekaristi, Kitubio, Mpako wa Wagonjwa, Daraja na Ndoa. Ndiyo “mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono” (Eb 6:2) tuliyoyapata kupitia Mitume.
Tujihadhari na madhehebu yaliyopunguza sakramenti hizo saba tulizoachiwa na wema wa Yesu kwa kuwa alijua tunavyozihitaji.


Je, tuishie katika kusadiki na kuadhimisha mafumbo?

Hapana, tusiishie katika kusadiki na kuadhimisha mafumbo, kwa kuwa imani na sakramenti zinadai kutekelezwa maishani.
“Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?… Itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana” (Rom 6:2-3; 12:1).
“Nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Math 5:16).


Matendo yetu yasipomtukuza Mungu, maana yake nini?

Matendo yetu yasipomtukuza Mungu, maana yake mafumbo hayakuadhimishwa vizuri.
“Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa” (Yak 2:26).


Mungu ametuagiza matendo maalumu ya ibada kwa sababu gani?

Mungu ametuagiza matendo maalumu ya ibada kwa kuzingatia umbile letu, kwamba binadamu ni umoja wa roho na mwili, hivyo anahitaji mwili na hisi zake ili kuingiza chochote rohoni na kutokeza yaliyomo katika roho yake isiyoonekana.
Ndiyo sababu Yesu alipoletewa kiziwi mwenye utasi “akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, ‘Efatha’, maana yake, ‘Funguka!’” (Mk 7:33-34).
Hizo zote ni ishara wazi kwa milango yetu ya fahamu.


Je, hisi zetu zote zinaweza kutumika kuadhimishia mafumbo?

Ndiyo, hisi zetu zote zinaweza kutumika kuadhimishia mafumbo, kila moja kadiri ya uwezo wake: macho kwa kuona, pua kwa kunusa, kinywa kwa kuonja na kusema, mwili mzima kwa kugusa na kutenda, lakini hasa masikio kwa kupokea maneno yaletayo uzima wa Kimungu.
“Maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima” (Yoh 6:63).
“Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia… Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Rom 10:13-14,17).


Kwa nini maneno ndiyo muhimu zaidi kuadhimishia mafumbo?

Maneno ndiyo muhimu zaidi kuadhimishia mafumbo kwa sababu yanafafanua ishara nyingine na kuzitia nguvu ya kututakasa.
“Kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno” (Ef 5:25-26).
Pasipo maneno hapana sakramenti yoyote.


Ishara za mafumbo zimetokana na nini?

Ishara za mafumbo zimetokana na viumbe (maji, mafuta, mkate, divai n.k.) na maisha ya jamii (kuosha, kupaka, kula na kunywa pamoja n.k.) na historia ya wokovu (kunyunyiza na kuzamisha, kuwekea mikono, kula Pasaka, n.k.),
lakini ni kwa kuagizwa na Yesu kwamba zinabeba kazi yake ya kuokoa na kutakasa.
“Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Lk 22:19).


Maneno na ishara kwenye ibada vinaweza kubadilishwa na nani?

Maneno na ishara vinaweza kubadilishwa na waandamizi wa Mitume, waliokabidhiwa na Yesu mamlaka ya kuendeleza kazi yake katika mazingira mbalimbali hata mwisho wa dunia.
“Amin, nawaambieni: Yoyote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni, na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni” (Math 18:18).
Hao Maaskofu wanakiri hawawezi kamwe kuyabadilisha yale ambayo Yesu aliyaweka kuwa ya lazima kama yalivyo mafumbo yenyewe.
“Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi” (1Kor 11:23).
Mengine yote wanaweza kuyapanga na kuyarekebisha kadiri ya mazingira, kuanzia lugha, wakilenga daima wokovu wa watu.


Faida ya kupanga taratibu za ibada ni ipi?

Faida ya kupanga taratibu za ibada ni hasa kuhakikisha yote yafuate usahihi wa imani na maadili, yakidumisha umoja na upendo, badala ya kumuachia kiongozi au mwingine yeyote aseme na kufanya anavyotaka. Mitume wenyewe walianza kazi hiyo, wakidhibiti hata karama.
“Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga. Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri. Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu. Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue. Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze… Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana. Lakini mtu akiwa mjinga, na awe mjinga… Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu” (1Kor 14:26-30,37-38,40).
Polepole taratibu ziliongezeka na ibada zikapata mtiririko rasmi wa kueleweka: ndizo liturujia za mashariki na za magharibi ambazo zinaweza kuwa mbalimbali mradi zisipishane upande wa imani.


Mhusika mkuu wa mafumbo hayo ni nani?

Mhusika mkuu wa mafumbo hayo ni Mungu ambaye kwa njia hiyo anazidi kutufanyia maajabu alivyoyafanya Yesu alipokuwa duniani. Kama tunda la kutukomboa kwa kifo na ufufuko wake, Baba anatujaza humo Roho Mtakatifu kama advansi ya uzima wa milele.
“Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi yake aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake” (Ef 1:13-14).


Sisi tunahusika na mafumbo hayo kama nani?

Sisi tunahusika na mafumbo hayo kama walengwa ambao tuyatumie vema ili yazae matunda yote yaliyokusudiwa na Mungu.
Ndiyo kiini cha ukuhani wetu ambao tunashiriki ule wa Kristo tangu tubatizwe.
“Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo” (1Pet 2:4-5).


Tunapoadhimisha mafumbo hayo, Mungu anatukuzwa vipi?

Tunapoadhimisha mafumbo hayo, Mungu anatukuzwa kwa kuwa ndivyo anavyotufanya “tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo… tupate kuwa sifa ya utukufu wake” (Ef 1:4,12).
Tukipokea neema hiyo tunampatia ibada, sifa na shukrani na tunazidi kumuomba atujaze Roho Mtakatifu kwa njia ya Mwanae.
“Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina” (Ef 3:20-21).


Je, mafumbo yote saba yanazaa matunda yaleyale?

Hapana, mafumbo yote saba hayazai matunda yaleyale, bali Yesu aliweka kila moja kwa lengo maalumu, litupatie Roho Mtakatifu kadiri ya nafasi na haja fulani ya maisha yetu.
Ubatizo, kipaimara na ekaristi vinatuingiza katika fumbo la Pasaka tuweze kuishi upya kama wana wa Mungu.
Kitubio na mpako wa wagonjwa vinatuponya roho na hata mwili. Daraja na ndoa zinatufanya wahudumu wa Kanisa na wa familia.
Ni muhimu tujue tunachohitaji na tukipate vipi.
“Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa” (1Kor 11:29-31).


Tushiriki mafumbo hayo mara ngapi?

Tushiriki mafumbo hayo kadiri ya umbile la kila mojawapo. Kuna “ubatizo mmoja” (Ef 4:5) kwa sababu ni kuzaliwa upya “kwa maji na kwa Roho” (Yoh 3:5), jambo lisiloweza kurudiwa.
Vilevile katika kipaimara na daraja, karama inayopatikana kwa kuwekewa mikono na mwandamizi wa Mitume haifutiki, inadai kuchochewa tu.
“Nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu” (1Tim 1:6).
Kumbe tunahitaji ekaristi mara nyingi, kwa sababu ni chakula cha roho.
“Bwana, sikuzote utupe chakula hiki” (Yoh 6:34).
“Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo” (1Kor 11:26).


Je, mafumbo yote yanaweza kuadhimishwa na yeyote?

Hapana, si mafumbo yote yanaweza kuadhimishwa na yeyote, bali mengine yanahitaji mhudumu wake awe amepewa daraja inayoshirikisha uwezo ambao Yesu aliwapa Mitume wake.
“Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume” (Lk 6:12-13).
“Yesu aliwaambia tena, ‘Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi’. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, ‘Pokeeni Roho Mtakatifu’” (Yoh 20:21-22).
Kwa kuwa Waprotestanti hawana sakramenti ya daraja, kati yao zinapatikana sakramenti zile mbili tu zisizohitaji padri, yaani ubatizo na ndoa.


Je, tunapoadhimisha mafumbo hayo tuko peke yetu?

Hapana, tunapoadhimisha mafumbo hayo hatuko peke yetu, bali tunashiriki ibada ambayo Yesu anamtolea Baba milele.
“Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao” (Math 18:20).
Kwa kuungana na Kristo Kichwa, tunaungana na viungo vyote vya Mwili wake, vya duniani, toharani na mbinguni.
“Ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu wa kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili” (Eb 12:22-24).


Je, kuna nyakati za kufaa zaidi kumuadhimishia Mungu?

Ndiyo, kuna nyakati za kufaa zaidi kumuadhimishia Mungu. Yesu aliyesema, “Sikuja kutangua, bali kutimiliza” (Math 5:17), alifuata kalenda ya dini ya Kiyahudi, halafu kwa kufa na kufufuka amekuwa kiini cha ibada zetu zote. Hivyo Mitume waliadhimisha siku aliyofufuka kama “siku ya Bwana” (Ufu 1:10) ambapo wakutane “ili kumega mkate” (Mdo 20:7) wa ekaristi.
Vilevile kwenye Pasaka hawakuadhimisha tu kazi ya Musa, bali ukumbusho wa Yesu.
“Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo” (1Kor 5:7).
Fumbo hilo ndio moyo wa mwaka wa liturujia, yaani wa mpangilio wa maadhimisho katika mzunguko wa mwaka.
“Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo” (Kol 2:16).


Je, kuna mahali pa lazima pa kumuadhimishia Mungu?

La! Hakuna mahali pa lazima pa kumuadhimishia Mungu, kwa kuwa yeye hafungwi na mahali.
“Mungu je, atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga!” (1Fal 8:27).
“Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono” (Mdo 17:24).
Hata hivyo sisi watu tunahitaji mahali maalumu kwa matendo yetu mbalimbali, na kumwekea Mungu mahali patakatifu.
“Mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu asema: Ki wapi chumba changu cha wageni, niile Pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu?’ Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni” (Mk 14:14-15).


Hekalu ndiyo nini?

Hekalu ndipo tunapomuendea Mungu kwa ibada. Vilevile sisi wenyewe ni Mahekalu.
Yesu aliheshimu na kutakasa hekalu pekee la taifa lake kama “nyumba ya Baba” yake (Yoh 2:16), lakini alitabiri kuwa litabomolewa moja kwa moja, na kuwa watu watapaswa kuabudu ndani yake aliye hekalu hai. “Wayahudi walisema, ‘Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?’ Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake” (Yoh 2:20-21).
“Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho” (Ef 2:22).
“Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi” (1Kor 3:16-17).


Je, sanaa zinafaa kumuadhimishia Mungu?

Ndiyo, sanaa zinafaa kumuadhimishia Mungu kwa sababu tunapaswa kutumia kwa utukufu wake vipawa alivyotujalia, kama vile vya kujenga, kupamba, kuchonga, kuchora na kucheza. Kwa njia hizo tutokeze na kukoleza imani yetu na ya wenzetu.
Mungu “amewajaza watu hao akili za moyoni, ili watumike katika kazi za kila aina, ya mwenye kuchora mawe, na kazi ya werevu, na ya mwenye kutia taraza, katika nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na ya mwenye kufuma nguo; ya hao wafanyao kazi yoyote, na ya wenye kuvumbua kazi za werevu. Basi, Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye Bwana amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote Bwana aliyoyaagiza” (Kut 35:35-36:1).
“Maskani zako zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi!” (Zab 84:1).


Kati ya sanaa kwenye ibada/kumuadhimisha Mungu, muhimu zaidi ni ipi?

Kati ya sanaa, muhimu zaidi ni uimbaji, kwa kuwa unahusiana zaidi na Neno la Mungu, ukilitia maanani kwa uzuri wa muziki. Katika Agano la Kale, kitabu cha Zaburi ni nyimbo tupu za kutumia katika ibada.
“Msifuni kwa mvumo wa baragumu; msifuni kwa kinanda na kinubi! Msifuni kwa matari na kucheza; msifuni kwa zeze na filimbi! Msifuni kwa matoazi yaliayo; msifuni kwa matoazi yavumayo sana!” (Zab 150:3-5).
Agano Jipya pia linatuletea nyimbo nyingi.
“Mjazwe Roho, mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu” (Ef 5:18-19).
Mbinguni washindi wana “vinubi vya Mungu. Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwanakondoo” (Ufu 15:2-3).


Kuimba wakati wa ibada ni kazi ya nani?

Kuimba ni kazi ya kusanyiko lote, yaani ya kila mwamini. Kwaya ziimbishe watu wamwadhimishe Mungu, zisiwaimbie tu na kuwanyima nafasi ya kuimba.
“Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote, mtumikieni Bwana kwa furaha, njoni mbele zake kwa kuimba” (Zab 100:1-2).
“Kila kiumbe kilichopo mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi na juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, ‘Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwanakondoo, hata milele na milele’” (Ufu 5:13).


Katika kutumia sanaa kwa ibada tuzingatie nini?

Katika kutumia sanaa kwa ibada tuzingatie utakatifu na ukweli, si uzuri tu. Zisiigeuze kamwe kuwa igizo wala tamasha, kwa kuwa lengo si kuchangamsha watu bali kumtukuza Mungu.
Ziinue mioyo kwake, zitokeze na kuchangia maisha safi, zilete ujumbe sahihi kadiri ya imani na maadili, kama ilivyo lazima kwa mahubiri na mafundisho.
“Watu hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu” (Math 15:8-9).


Je, ni halali kuheshimu sanamu?

Ndiyo, ni halali kuheshimu sanamu kama viwakilishi vya Yesu, Mama yake na watakatifu wake, ambao zinaleta sura zao.
Kwa msingi huo walimsihi Yesu “waguse hata pindo la vazi lake tu. Na wote waliogusa wakaponywa kabisa” (Math 14:36).
“Mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote il msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo” (Gal 6:14).


Wakati wa ibada tuvae vipi?

Wakati wa ibada tuvae namna inayodhihirisha malengo ya moyo wetu, hasa usafi na heshima, unyenyekevu na udugu.
“Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki, kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote” (Math 23:27).
“Akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri, kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, ‘Keti wewe hapa mahali pazuri’, na kumwambia yule maskini, ‘Simama wewe pale’, au ‘Keti miguuni pangu’, je, hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?” (Yak 2:2-4).
“Wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani, bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu” (1Tim 2:9-10).
Kanisa si mahali pa mashindano: hatuendi kupendeza watu, ila Mungu.
“Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu?” (1Kor 11:22).


Mbali ya sakramenti, Kanisa linamuadhimisha Mungu vipi?

Mbali ya sakramenti, Kanisa linamuadhimisha Mungu hasa kwa Liturujia ya Vipindi, yaani kwa sala rasmi zinazotolewa mara kadhaa kwa siku, kufuatana na ratiba ya binadamu ya usiku na mchana. Hivyo linajitahidi kutimiza agizo la kusali daima.
“Imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa” (Lk 18:1).
“Kesheni ninyi kila wakati, mkiomba” (Lk 21:36).
“Ombeni bila kukoma, shukuruni kwa kila jambo” (1Thes 5:17).
“Kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote” (Ef 6:18).
“Huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku” (1Tim 5:5).


Kanisa linamuadhimishaje Mungu tena?

Kanisa linamuadhimisha Mungu tena kwa visakramenti ambavyo kwa mamlaka ya Kristo linawatia watu neema zake katika nafasi yoyote ya maisha. Kati yake muhimu zaidi ni baraka na mazinguo, ambavyo vipo tangu zamani, hata nje ya taifa la Israeli.
Melkisedek alisema, “Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako” (Mwa 14:19-20).
Farao aliomba, “Mkanibariki mimi pia” (Kut 12:32).
Balaam alisifiwa, “Najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa” (Hes 22:6).
“Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha” (1Sam 16:23).
“Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je, wana wenu huwatoa kwa nani?” (Math 12:27).


Maana ya baraka ni ipi?

Maana ya baraka ni kumsifu Mungu kwa yale aliyokwishatujalia na kumuomba azidi kutujalia kadiri ya mahitaji ya wahusika. Mara nyingi inatolewa na mtu mwenye daraja au mamlaka fulani.
Yesu aliletewa “watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea” (Math 19:13).
Siku ya kupaa mbinguni “aliinua mikono yake akawabariki” (Lk 24:50).
“Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao” (Mdo 13:3).
Pengine vinabarikiwa vitu vinavyotumiwa na watu, au mahali wanapoishi.
“Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie mkutano” (Lk 9:16).


Mazinguo ndiyo nini?

Mazinguo ni sala za kupungia mashetani ili kuepusha watu na balaa au madhara, hasa kama wamepagawa nao.
“Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu” (Mk 5:8).
“Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena!” (Mk 9:25).
Yesu ameliachia Kanisa mamlaka yake juu yao.
“Aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu” (Mk 6:7).
“Paulo alisikitika, akageuka akamwambia yule pepo, ‘Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu’. Akamtoka saa ileile” (Mdo 16:18).


Je, ni halali kwa Wakristo kujitungia ibada nyingine?

Ndiyo, ni halali kwa Wakristo kujitungia ibada nyingine, mradi wakubali zipimwe na Maaskofu kama zinalingana na imani, maadili na taratibu za Kanisa.
“Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure… Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu” (Kol 2:18,23).
“Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao” (2Tim 3:14).


Ni halali kujitungia ibada kwa sababu gani?

Ni halali kujitungia ibada kwa sababu sala ni hasa maongezi ya Mungu na mtu.
Adamu na Eva “walisikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga” (Mwa 3:8).
Yeye hachoki kumvuta kila mmojawetu kwake na kumtia hamu ya kumhimidi na kumuabudu, kumuomba kwa ajili yake na ya wengine, kumshukuru na kumsifu.
“Ee Bwana, uisikie sala yangu, uzisikilize dua zangu, kwa uaminifu wako unijibu kwa haki yako” (Zab 143:1).
Hata tukisali pamoja, uhusiano wa kila mmojawetu na Mungu ni wa pekee. Tusiposali kwa moyo, ibada ni ya bure.
“Watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami” (Isa 29:13).


Ikiwa sala ni maongezi ya Mungu na mtu, kwanza tufanye nini?

Ikiwa sala ni maongezi ya Mungu na mtu, kwanza tumsikilize kwa makini na kutafakari alichosema ili tukifanyie kazi. Tukisema peke yetu si sala, kwa kuwa ukisema upande mmoja tu si maongezi.
“Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia” (1Sam 3:10).
“Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku” (Zab 63:6).
“Sheria yako naipenda mno ajabu, ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa” (Zab 119:97).
“Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu” (Yer 15:16).


Kielelezo cha sala yetu ni nani?

Kielelezo cha sala yetu ni Yesu Kristo.
“Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, ‘Bwana, tufundishe sisi kusali” (Lk 11:1).
Yeye kama binadamu alichota humo uaminifu kwa wito wake wa pekee.
“Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe” (Yoh 17:1).
“Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe” (Mk 14:36).


Kama binadamu Yesu alijifunza kusali kwa nani?

Kama binadamu Yesu alijifunza kusali kwa Mama yake na kwa mapokeo yote ya Israeli, yaliyojitokeza hasa katika Zaburi.
“Wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu” (Lk 2:41-42).
“Saa tisa Yesu alipaza sauti yake kwa nguvu, ‘Eloi, Eloi, lama sabakthani?’” (Mk 15:34).
“Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu” (Lk 23:46).
Read and Write Comments

Maswali na Majibu kuhusu Kuabudu kwa Wakatoliki

Wakatoliki tunamwabudu Mungu kwa namna gani?

Tunamwabudu Mungu kwa sala , sadaka na matendo mema


Je, tuna ruhusa ya kuwaabudu Watakatifu?

Hatuna ruhusa ya kuwaabudu Watakatifu tunawaheshimu tu.


Je sanamu zimekatazwa?

Sanamu hazijakatazwa, ila tunaziheshimu kwa sababu zinatukumbusha Mungu na Watakatifu. (Kut 25:18-22).
18 Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. 19 Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. 20 Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. 21 Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. 22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli. Kutoka 25 :18-22.
Vile vile Mungu alishawahi kuwaagiza Waisraeli Wachonge sanamu ya nyoka na yeyote atakayeumwa na nyoka akiiangalia atapona.


Mfano wa sanamu takatifu ni zipi?

Sanamu ya Bikira Maria, Mtoto Yesu, Mt. Yosefu, Moyo wa Yesu na za Watakatifu.


Ni nanai ana kosa kumuabudu Mungu?

Anayekosa kumuabudu Mungu ni yule;
1. Anayeacha kusali au anayesali hovyo
2. Anayemkufuru Mungu
3. Anayeamini na kushika mambo ya kipagani


Ni nini maana ya kuabudu sanamu?

Kuabudu sanamu ni kukipa kiumbe chochote heshima au upendo anaostahili Mungu peke yake.


Kutokumuabudu Mungu ni kwa namna gani?

Ni kuruhusu kitu chochote kimtawale mtu badala ya Mungu, mfano cheo, pombe, mali, shetani, tuisheni, kazi, na kutoadhimisha Jumapili au kutoshiriki.


Mkatoliki anaabuduje?

Mkatoliki anaabudu kwa kupiga goti au magoti mawili na ni mbele ya sakramenti ya Ekaristi Takatifu tuu hasa wakati wa kuingia na kutoka kanisani


Je magoti yanayopigwa wakati mwingine tofauti na wakati wa kuabudu yana maana gani?

Magoti yanayopigwa wakati wa sala mfano kanisani, nyumbani, mbele ya sanamu, jumuiyani, shuleni yanaitwa Mkao wa sala


Kwa nini wakatoliki wanaweka sanamu Kanisani?

Tunaweka sanamu Kanisani kwa sababu tunaheshimu anayewakilishwa na sanamu hiyo kwa mfano Yesu Kristo, Mama Bikira Maria, Malaika na Watakatifu; na kamwe hatuziabudu. (Kutoka 25:18-22)
Hata Waisraeli kwenye hekalu lao walikua na sanamu kama tunavyosoma hapa;
“18 Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. 19 Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku.20 Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. 21 Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. 22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli. (Kutoka 25 :18-22.)
Kwa hiyo kama Mungu mwenyewe aliagiza Sanamu za Malaika zichongwe na kusema atakua hapo na kuongea na watu wake. Je sio vyema zaidi kuwa na sanamu na Picha ya Mwanae wa Pekee Yesu Kristo na kuongea na Mungu mbele yake kama alitaka ya malaika ambao sio Mungu?
Mfano mwingine ni pale Mungu alivyomwabia Musa achonge Sanamu ya Nyoka wa shaba.
“BWANA akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti, ye yote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.’’ 9Kwa hiyo Mose akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu ye yote alipoumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.” (Hesabu 21:8-9).
Kwa Mfano huu Je tunaweza kusema kuwa sanamu ya nyoka ina nguvu ya uponyaji kuliko ya Yesu aliye Mungu? Kumbuka hapa watu walioona sanamu hii ya nyoka hawakukoponywa na nguvu ya sanamu ya shaba bali kwa nguvu ya neema ya Mungu kupitia Imani kwa Mungu. Kwa hiyo unaposali mbele ya picha au sanamu hautegemei nguvu ya sanamu bali unategemea neema ya Mungu kwa njia ya Imani yako kwa Mungu.
Kama vile Sanamu hii ya nyoka aliyoagiza Mungu iwekwe ilivyowekwa kwa nia ya uponyaji kwa yule aitazamaye vivyo hivyo Sanamu na Picha za Kanisani zinawekwa kwa nia maalumu na kwa neema maalumu. Ndiyo maana hazifanani. Na zinabarikiwa kwa kuombewa Baraka Ili zizae neema kwa wanaozitumia.

Sanamu au picha sio haramu bali maana ya hiyo sanamu au picha ndio inaiharamisha.

Kuna tofauti kati ya kuabudu na kuheshimu. Wakatoliki wanaweka sanamu kwa heshima na sio kwa kuabudu, ndio maana unaposali mbele ya picha ya Yesu hausali ee sanamu nisaidie bali unasema ee Yesu nisaidie.
Je tuseme tunamwabudu Raisi kwa kuheshimu picha yake kwa kuiinamia? Je tunaabudu bendera kwa kuheshimu na kupigia saluti? Je taratibu zabunge za kutoa heshima na taratibu za mahakama ni kuabudu?. Je kuapa mbele ya picha ya Raisi ni kumuabudu Raisi? Je kuapa na Biblia ni kuabudu Biblia? Je tunapobusu Biblia na kuitunza kwa heshima tunaiabudu? Tofauti ya Biblia na sanamu ni nini? Je, kwenye Biblia kinachoheshimiwa ni karatasi au maana ya yale maneno kwenye karatasi. Pengine usingeheshimu kama hujajua kuyasoma.
Kuna tofauti gani kati ya biblia yenye Maandishi na msalaba wa kuchonga wenye kuonyesha kile kinachosemwa na biblia? kama unaweza kuheshimu biblia yenye karatasi tena pale unapoweza kuzisoma na pengine ungeizarau kama ni ya lugha tofauti na hujui kilichoandikwa? Je Msalaba uliobeba maana ya kile kilichoandikwa kwenye Biblia unaona si kitu? Kama Kinachoheshimiwa kwenye Biblia sio karatasi bali maana maneno yaliyoandikwa vivyo hivyo kinachoheshimiwa kwenye picha au sanamu sio chuma yake au mti ukiochongwa bali ni maana ya hiyo sanamu.
Hii ndio maana nasema kuna tofauti ya kuabudu na kuheshimu.
Kumbuka kuwa picha au sanamu yoyote ya Kikatoliki lazima ibarikiwe kwanza ndio uweze Kusali mbele yake. Inapobarikiwa inaombewa uwepo wa yule anayewakilishwa na picha/sanamu hiyo uwe pale sanamu ilipo na anayesali pale sala yake Ifike kwa mlengwa anayeonekana kwa ishara ya sanamu/picha. Kwa Mfano askofu au padri anapobariki sanamu ya Yesu anaomba kuwa “Yesu awepo pale kwenye sanamu na Neema zake”, kwa hiyo yeyote anayesali mbele ya sanamu hiyo anaamini kuwa Yesu yuko pale na anasali Mbele yake. Kwa hiyo kinachopewa heshima sio ile sanamu bali ni yule anayeonekana kwa ishara ya ile sanamu au picha.

Tofauti ya Sanamu za Kikatoliki na za kipagani ni Kwamba,

Sanamu za Kipagani: Sanamu hizi huchukuliwa kama Mungu na huabudiwa na kutolewa Sadaka kama Mungu Mwenyewe.

Sanamu za Kikatoliki: Sanamu hizi huchukuliwa kama ishara ya kile inachokiwakilisha, haiabudiwi kamwe bali inaheshimiwa tuu.

Daima Tumia Sanamu na Picha zilizobarikiwa kwani zimenuiwa uwepo wa yule inayemuwakilisha na utaongea naye hapo. Sisi tunaamini kwamba kwenye Sanamu ya Yesu kuna uwepo wa Yesu. Kama vile Mungu anavyowaambia Waisraeli katika (Kutoka 25 :22) baada ya kuwaagiza wachonge sanamu za Makerubi (Malaika) 22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli. (Kutoka 25 :22)Sanamu au picha ni ishara wazi ya uwepo wa kile kisichoonekana.

Jifunze kupitia Sanduku la Agano na Msalaba wa Yesu

Kwenye Agano la kale: Ndani ya hekalu la Waisraeli walikua na Sanduku la agano, sanduku hilo lilikua na vibao vya Amri za Mungu ambavyo ni Ishara ya Agano lao na Mungu na ndani ya sanduku kulikuwepo pia Mfano wa Kiti ambacho kimezugukwa na sanamu za viumbe kama malaika nyuso zao zikielekea kiti hicho Kutoka 25:10-22. Waisraeli walikua wanasali kuelekea sanduku la Agano wanapokuwa Hekaluni na hata wakiwa majumbani mwao walisali kuelekea upande lilipo Hekalu. Waisraeli walisali kuelekea Sanduku la Agano wakiamini kwamba Mungu yupo kati ya sanduku lile. Lakini sanduku lile halikuwa Mungu. Waisraeli waliona fahari juu ya Sanduku lile na walilithamini na kuliheshimu kwa kuwa lilionyesha uwepo wa Mungu na popote lilipokuwa waliamini Mungu yupo.
Kwenye Agano jipya: Wakristu wanasali Mbele ya Msalaba wa Yesu ambao unaonyesha kazi ya wokovu alioufanya Yesu kwa wanadamu ya Kuwakomboa watu kwa kifo chake Msalabani. Na Msalaba huo ni Ishara ya Ukombozi wa Agano jipya na la Milele. Kama ilivyokuwa kwa Sanduku la Agano, Wakristu wanaheshimu msalaba ambao ni ishara ya wokovu wao na wanaamini kuwa Mungu yupo kati ya Msalaba huo lakini Msalaba huo sio Mungu. Wakristu wanaona fahari juu ya msalaba wa Yesu kwa kuwa ndio ishara ya wokovu wao.
FUNZO:Kupitia Mfano wa Sanduku la Agano na Msalaba tunajifunza kuwa Vyote havikuwa Mungu ila vinaheshimiwa kwa Imani kuwa Mungu yupo pale. Vilevile, vyote ni ishara ya wazi ya Agano la Mungu na Wanadamu.

Kwa nini tunasali mbele ya Picha/Sanamu na Hasa kufanya Ishara ya msalaba?

Tunasali mbela ya sanamu kwa sababu tunaamini sanamu inaakisi uwepo wa mhusika aliyechorwa au kuchongwa kwenye hiyo sanamu/picha. Ndio maana wakatoliki wanasali kwenye picha au sanamu iliyobarikiwa tuu kwa sababu Sanamu inapobarikiwa inaombewa uwepo wayule anayewakilishwa pale.
Tunafanya ishara ya msalaba kwenye sanamu kama sala ya utangulizi ambayo inathibitisha kuwa hatuabudu kile kilichoko pale bali kile tunachokifanya tunakifanya huku tukikiri Umungu na Heshima ya Utatu Mtakatifu (Mungu; Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.). Vile vile tunamtukuza Mungu katika Utatu Mtakatifu kwa sababu ya yule anayewakilishwa na picha au sanamu.

Kwa nini watu wanabusu picha na sanamu?

Hii ni ishara ya Upendo kwa yule anayewakilishwa kwenye picha au sanamu husika. Hata katika maisha ya kawaida watu hubusu picha za wazazi na wapendwa wao. Maana ni ile ile.


Mungu akiwa Roho, viungo ambavyo pengine anapewa vina maana gani?

Mungu akiwa Roho, viungo ambavyo pengine anapewa vinamaanisha tu sifa fulani: k.mf. macho ujuzi wake, mikono uwezo wake, mabawa ulinzi wake, n.k. “Roho haina mwili na mifupa” (Lk 24:39).


Je, ni halali kuheshimu sanamu?

Ndiyo, ni halali kuheshimu sanamu kama viwakilishi vya Yesu, Mama yake na watakatifu wake, ambao zinaleta sura zao.
Kwa msingi huo walimsihi Yesu “waguse hata pindo la vazi lake tu. Na wote waliogusa wakaponywa kabisa” (Math 14:36).
“Mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote il msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo” (Gal 6:14).
Read and Write Comments

Utaratibu wa Mkristo Mkatoliki Kanisani

Ninapoingia kanisani nachovya maji ya baraka na kusema;
“Unitakase Ee Bwana mimi na uovu wangu wote, ili nipate kustahili kushiriki ibada takatifu’ Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” Amina!
Ninapiga goti huku nikisema
“Mungu wangu na Bwana wangu”
🙋🏽Nikiinuka nasema
“Nitakusifu na kukuabudu katika Ekaristi takatifu”
🙋🏽Naenda mpaka kwenye bench, napiga magoti au nakaa nikiwa mimeinamisha kichwa (kama mabenchi yameisha nabaki nimejisimamia) huku nikitoa nia yangu ya kusali misa siku hiyo, mfano
“Ee Mungu, ninaungana nawe na jeshi lote la mbinguni, pamoja na Mama Bikira Maria, nikiwa na nia ya kumwombea mama yangu ambaye ni mgonjwa, jirani yangu ambaye mpaka sasa hatuelewani na pia familia yetu ambayo haina amani, Mungu kupitia misa hii rejesha hali ya mama yangu, rejesha uelewano na jirani yangu, na pia rejesha amani ya familia yetu pamoja na familia zote ambazo hazina amani”
🙋🏽Ninaendelea na misa na Kushiriki litrujia kikamilifu
🙋🏽Wakati wa komunyo nikikumbuka kuwa nina dhambi kubwa huwa nakominika kwa sala ya tamaa wala siendi mbele, huwa najikalia tu kwenye bench naangalia wenye moyo safi wanaenda mbele kumpokea Yesu (Kweli huwa najisikia wivu sana, itanibidi katikati ya wiki nifanye kitubio ili nisikae tena)”
🙋🏽Mwisho wakati wa kuondoka nachovya maji ya baraka nikisema
“Unilinde Ee Mwenyezi Mungu, nikapate kuwa mfano katika jamii yangu, na nikushuhudie katika matendo yangu”
(Hapo nachovya maji ya baraka na kufanya ishara ya msalaba) “Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, amina”
Usiku mwema wapendwa. Malaika awalinde
Read and Write Comments

JE, WAKATOLIKI WANABUDU SANAMU?

Mpenzi msomaji, kumekuwa na tuhuma nyingi dhidi ya wakatoliki kwamba wanaabudu sanamu. Je, tuhuma hizo zina ukweli gani? Hilo ndilo swali tunalotaka kujibu leo.
Amri ya kukataza ibada kwa sanamu imewekwa wazi katika Biblia Takatifu, Kutoka 20:4-5, “Usijifanyie sanamu ya miungu wa uongo, au kinyago chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini chini ya dunia. Usiisujudie wala kuitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.”
Sheria hiyo inapatikana pia katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:8-9: “Usijifanyie sanamu za miungu za kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Isivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.”
Ni kutokana na vifungu hivyo vya Maandiko Matakatifu, Waamini wa Kikatoliki wamekuwa wakituhumiwa, kushtakiwa na kushambuliwa na baadhi ya waamini wa madhehebu mengine kwamba wanapingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu, yanayokataza ibada kwa sanamu. Tuhuma hizo zinakuwa nzito zaidi, hasa zinapohusishwa na Ibada inayofanywa na Waamini Wakatoliki siku ya Ijumaa Kuu kila mwaka.

KUNA TOFAUTI KATI YA KUABUDU NA KUHESHIMU

Mpenzi msomaji, kuna tofauti kubwa kati ya kuabudu na kuheshimu. Kamusi ya Kiswahili ya Maana na Matumizi, ya mwaka 1993, iliyoandikwa na SALIM K. BAKHRESSA, na kuchapishwa na OXFORD UNIVERSITY PRESS, DAR ES SALAAM, inaeleza kuwa neno “kuabudu” maana yake ni “kuomba au kufanya ibada”; na neno “kuheshimu” maana yake ni “kutukuza, kustahi au kuogopa.”
Katika maana yake ya ndani, anayeabudiwa na mwenye haki ya kuabudiwa ni Mungu peke yake. Hakuna mtu, kiumbe wala kitu chochote kinachopaswa kuabuduiwa na chenye haki ya kuabudiwa. Mtu, kiumbe au kitu hupewa heshima tu, tena ya kiwango maalum. Kwa mfano, Bikira Maria, kwa sababu ya nafasi yake katika kazi ya ukombozi, anapewa heshima ya juu kuliko watakatifu wengine. Watakatifu hao wengine hupewa heshima ya kadiri tu, chini ya heshima ile anayopewa Bikira Maria.

KWA NINI MUNGU PEKE YAKE ANASTAHILI KUABUDIWA?

Tumesema ni Mungu pekee yake, ndiye anayestahili kuabudiwa, kwa sababu ndiye MUUMBA wa vitu vyote, vinavyoonekana na visivyoonekana; ndiye anayevitawala na kuviongoza vitu vyote; ndiye mwenye uwezo juu yetu sisi wanadamu na viumbe vingine vyote; ndiye anayejua yote; ndiye aliye pote kwa ajili yetu; ndiye mwanzo na mwisho wa kila kitu; ndiye mkuu na Bwana wa wote.
Aidha, tunapomwabudu Mungu, tunakiri kwamba ndiye aliyetuumba na “ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu na tuko!” (Mdo.17:28). Kwa kufahamu hilo, Wakatoliki hawawezi kumwabudu mtu, kiumbe au kitu chochote, isipokuwa Mungu tu.

MAMBO MAKUU NA MUHIMU KATIKA IBADA YA SANAMU

Ili kufahamu vema kinachofanywa na Wakatoliki ni vema kufuatilia na kutafakari yale wanayoyafundisha na kuyasadiki wao wenyewe, badala ya kuwahukumu kadiri watu wengine wanavyofikiri na kusema. Ukweli ni kwamba hakuna Ibada yoyote ya sanamu katika Kanisa Katoliki. Hilo ni dhahiri kwa sababu ili ibada ya sanamu iwe kweli kuabudu sanamu lazima yawepo mambo makuu na muhimu mawili: Kwanza, NIA KAMILI YA KUABUDU SANAMU INAYOHUSIKA;
Pili, KUWEPO NA IBADA YA DHATI YA KUABUDU SANAMU. Ikitazamwa kwa makini, hayo mambo mawili yanakosekana katika Kanisa Katoliki linapokuja suala la picha na sanamu. Kwa hiyo, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala picha. Kama ni hivyo, wakatoliki wanafanya nini na hizo sanamu au picha? Wanaziheshimu tu! Tukumbuke kuwa anayemwabudu mtu, kiumbe au kitu, ni sharti akihesabu na kukisadiki kuwa ndicho kinachomwezesha kuishi, kujimudu na kuwa na uhai wake (Rej. Mdo.17:28).

JE, BINADAMU TUNAHITAJI SANAMU AU PICHA?

NDIYO. Binadamu tunahitaji sananmu au picha, tena ni jadi yetu! Kwa sababu gani tunahitaji picha maishani mwetu? Kwa sababu katika udhaifu wetu, mara nyingi tunaweza kufikiri vema kwa kutumia vielelezo au vichokoo vyenye kuonekana na kugusika. Kwa njia ya vielelezo hivyo, binadamu tunaweza kuyafikia kwa urahisi mambo magumu na mafumbo yaliyo juu ya fikra zetu za kawaida. Ndiyo maana tukiona picha au sanamu ya Yesu au Mama Maria au Watakatifu wengine, akili zetu zinaweza kutafakari mambo matakatifu na kupata picha ya kina cha msamaha wa dhambi na mapendo ya Mungu kwetu wanadamu.

KWA NINI WAKATOLIKI HAWAABUDU SANAMU AU PICHA?

Wakatolikihawaabudu sanamu kwa sababu wanajua kwamba Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa. Kwa hiyo, hawaziabudu sanamu au picha kwa sababu wanajua kwamba hivyo siyo Mungu. Zaidi hayo, wanajua kwamba Mungu mwenyewe amekataza kuziabudu sanamu na picha kwani hazina daraja la Muumba. Mungu amepiga marufuku kuzigeukia na kuzisujudia (Law.19:4). Aidha, wameaswa kuziepuka sanamu na Ibada kwa sanamu – “Watoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu!” (1Yoh.5:21). Pia wakatoliki wanajua kuwa sanamu na picha hazina uwezo wowote wa kimungu. “Mungu wetu yuko mbinguni, hufanya yote anayotaka. Miungu yao ni fedha na dhahabu; imetengenezwa na mikono ya wanadamu. Ina vinywa lakini haisemi. Ina macho lakini haioni. Ina masikio lakini haisikii. Ina pua lakini hainusi. … Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo, kadhalika na wote wanaoitumainia. Enyi wa nyumba ya Israeli mtumainieni Mwenyezi Mungu, yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu” (Zab.115:3-9). Pia kuziabudu sanamu ni jambo la kidunia, ambalo haliwezi kumpeleka mtu peponi (Rej. Isa.45:16; Isa.45:20; Gal.5:20). Kwa hiyo, Wakatoliki wanajua kuwa kuabudu sananmu na picha ni jambo haramu kabisa mbele ya Mungu, Mwumba wao (1Pet.4:3-4).

IBADA YA KWELI YA SANAMU INAKUWAJE?

Ibada ya kweli ya sanamu siyo rahisi hivyo, kama baadhi ya watu wanavyodhani! Ibada ya kweli ya sanamu siyo kitu cha mchezomchezo, kama baadhi ya watu wanavyofikiri na kusema. Ibada ya Sanamu ni suala la kuabudu, na kuabudu siyo suala la kuwa na kitu au kikiheshimu tu, bali ni kwenda mbali zaidi ya hapo! Hivyo kumiliki sanamu au picha, mathalani majumbani au kanisani, hakusemi lolote juu ya uwepo wa ibada ya sanamu kwa wale wanaohusika nazo. Kwa hiyo, ikiwa watu hawazipi sanamu au picha hizo mahali pa Mungu wa kweli, basi hawana hatia yoyote.
Jambo muhimu hapa ni kwamba wamiliki wa sanamu au picha hizo wanaziheshimu tu huku wakijua kuwa wenyewe wanaowakilishwa na sanamu au picha hizo hawapo pale kwa hali halisi. Katika maana hiyo, inakuwa sahihi kabisa kuziheshimu picha za marais, ndugu na marafiki wetu tunaowapenda, ambao hawapo karibu nasi. Picha zao hatuzikejeli wala hatuzibwagi chini na kuzikanyaga au kuzitia vumbi. Hatufanyi hivyo, siyo kwa sababu tunawaabudu watu hao au vitu hivyo, bali kwa sababu tunawapenda na kuwathamini wenyewe katika hali zao halisi.
Kwa mfano ikiwa tuna kitabu cha picha (Album) chumbani, chenye picha 100 za ndugu, rafiki na jamaa zetu, hatusemi tuna miungu 100 tunaowaabudu nyumbani mwetu! Vinginevyo, mambo yangetisha sana majumbani mwetu! Wenye picha hizo hatuwaabudu kamwe, ila tunawapa heshima tu kwa sababu tunawajali na kuwapenda. Kwa nini tusiwape heshima hiyo, ambayo ni kitu cha bure! Ukweli huo pia unahusu Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa, nk.

JE, MUNGU ANACHUKIA KILA SANAMU NA PICHA?

Mungu hachukii kila sanamu au picha. Hapa inafaa ieleweke vema kwamba Mungu alipopiga marufuku sanamu katika Kitabu cha Kut. 20:3-5 na Kumb. 5:7-10, hakupiga marufuku kila sanamu. Yeye mwenyewe anaonesha kwamba anazichukia sanamu zinazotengenezwa kusudi zichukue nafasi yake tu. Kama sanamu au picha hazihatarishi nafasi yake, hana maneno nazo! Ndiyo maana, basi, baada ya kumwagiza MUSA awaambie watu wasizitengeneze sanamu na kuziabudu kama miungu (Kut.20:4-5), alimwagiza MUSA huyo huyo azitengeneze sanamu zisizokuwa hatari, ambazo hazikupewa daraja la Mungu. Mungu alimwagiza MUSA kutengeneza sanamu katika nafasi mbili:
(i) Musa anaagizwa atengeneze sanamu mbili za Makerubi azibandike kwenye Sanduku la Agano wakifunike kiti chake cha rehema. “Utatengeneza pia mfano wa viumbe hai viwili kwa kufua dhahabu, uwaweke kwenye miisho miwili ya kiti hicho; kiumbe kimoja mwisho mmoja na kiumbe mwingine mwisho mwingine. Waweke viumbe hao kwenye miisho ya hicho kiti, lakini wawe kitu kimoja na hicho kiti. Viumbe hao wataelekeana, mabawa yao yamekunjuka kukifunika kiti cha rehema, nyuso zao zitakielekea kiti hicho” (Kut.25:18-20; Rejea pia Ebr.9:5).
(ii) Mungu alimwagiza pia Musa atengeneze Nyoka wa Shaba kama dawa kwa wale ambao waling’atwa na nyoka wa moto kule Jangwani. Musa alielezwa wazi kwamba wale ambao wangemtazama huyo nyoka wa shaba kwa imani kwa Mungu wa Israeli wangepona. “Ndipo naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: Tengeneza Nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona. Basi, Musa akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu aliyeumwa na nyoka alipomtazama huyo nyoka wa shaba, alipona” (Hes. 21:8-9; Rejea pia Yoh.3:14-15).
Basi, Musa alitekeleza maagizo hayo ya Mwenyezi Mungu, naye alifurahia. Kwa maagizo hayo mawili ni dhahiri kwamba Mungu hachukii kila sanamu au picha. Mungu anachukizwa na sanamu zile ambazo zimekusudiwa kuchukua daraja la umungu wake, maana ni yeye tu ndiye anayestahili kuabudiwa. Yule nyoka wa shaba alikuwa dawa kwa wale walioumwa na nyoka wa moto. Watu hao hawakumwabudu nyoka wa shaba, lakini walipona, siyo kwa sababu ya nguvu zake, ila kwa nguvu za mwokozi zilizokuwa nyuma yake. “Kama mtu akiitazama alama hiyo aliponywa, lakini kilichomponya siyo hicho kitu alichokiona, bali wewe uliye Mwokozi wa watu wote” (Hek.16:7).
Hapa ni vifungu vingine vya Maandiko Matakarifu, vinavyoonesha kuwa Mungu hachukii kila sanamu au picha.
1Fal. 7:29 “kulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe vyenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali zilikuwa, zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuri”.
2Nyak.3:10 “Alitengeneza sanamu mbili za viumbe wenye mabawa kwa mbao, akazifunika kwa dhahabu na kuziweka mahali patakatifu sana”
Ezek.41:17-18 “… kwenye ukumbi palikuwepo na michoro iliyofanana na mitende na picha za viumbe vyenye mabawa. Kila baada ya mtende kulichorwa picha ya kiumbe chenye mabawa kukizunguka chumba chote”.
Yoh. 3:14-15 “Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka wa shaba kule Jangwani, naye Mwana wa mtu atainuiliwa juu vivyo hivyo, ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele.”
Ebr.9:5 “Juu ya hilo sanduku kulikuwa na viumbe wenye mabawa, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewa”

UBAYA WA SANAMU AU PICHA UKO WAPI?

Ubaya wa sanamu au picha upo katika kuzipa sanamu au picha daraja la Mungu. Hatari na ubaya wa sanamu au picha vimo katika kitendo cha binadamu kuzipa sanamu au picha hizo daraja la Mwenyezi Mungu. Kama sanamu au picha hazipewi daraja la Mungu, haziwi hatari na wala hazina ubaya wowote mbele ya Mungu. Kwa sababu hiyo, basi, mtu anaweza kuwa na sanamu au picha ndani ya nyumba yake au kanisani, lakini bila kumkasirisha Mungu.
Zaidi ya hayo, Mungu mwenyewe anajua fika kuwa sanamu au picha fulani imepewa daraja lake au siyo. Kwa nini Mungu akasirike pale ambapo sanamu au picha haziingilii daraja na ukuu wake? Mungu mjinga wa aina hiyo hayupo! Mungu wa kweli hawezi kukasirikia picha na sanamu ambazo zinaheshimiwa tu, na wala haziabudiwi. Aidha, Mungu mwenye haki hawezi kumwadhibu na kumtupa Jehanamu mtu ambaye anamiliki picha au sanamu duniani lakini bila kuziabudu, yaani pasipo kuzipa daraja la Mungu.

BIBLIA INAWEZA KUTUSAIDIA KUIELEWA IBADA YA SANAMU?

Jibu ni ndiyo! Biblia inatoa maelezo ya kina na ufafanuzi mzuri juu ya ibada ya sanamu. Tumesema hapo juu kuwa ibada ya sanamu siyo jambo la mzaha au mchezo wa kitoto! Ni suala la kuabudu, na kuabudu siyo tu jambo la kuwa na sanamu au picha na kuiheshimu tu. Ni zaidi ya hapo! Kuna mambo muhimu ambayo lazima sanamu zitendewe, ndipo ihesabike kuwa ni ibada ya sanamu.
a) Tukitaka kujua kama kitendo fulani mbele ya sanamu ni kuabudu au sivyo, kwanza lazima iwepo nia thabiti ya mtu anayehusika katika kitendo hicho kinachofanyika. Ibada inakuwa ya kuabudu sanamu ikiwa mtu anayefanya kitendo hicho anaamini moyoni mwake kwamba hiyo sanamu au picha inayofanyiwa kitendo hicho inachukua daraja na nafasi ya Mwenyezi Mungu. Katika kitendo hicho, mtu anaamini kuwa sanamu au picha hiyo ndiyo inayomwezesha kwenda, kuishi, kujimudu na kuwa na uhai wake hapa duniani.
b) Jambo la pili ni kuangalia kama kitendo hicho kinachofanyika katika ibada hiyo ni Liturujia ya kueleweka/maalum. Baada ya kubaini nia thabiti ya mtendaji, tunaweza kuitambua ibada ya sanamu kwa kuangalia yale yanayofanyika mbele ya sanamu au picha kwa kufuatilia mambo ambayo waabudu sanamu huyafanya. Mambo hayo, ambayo waabudu sanamu wanayafanya tunaweza kuyakusanya kutoka katika Biblia yetu. Agano la Kale linaonesha kuwa Ibada ya Kuabudu Sanamu inajumuisha mambo makuu yafuatayo:
i. Kuzitolea sadaka: za kuteketezwa: Rej. Hos.4:13; nafaka na vyakula 2Fal.5:17.
ii. Kuzitolea ubani kwa heshima kamili: Rej. 1Fal.11:8; Isa. 57:6; Yer.7:18.
iii. Kuzimwagia matambiko: Rejea Isa. 57:6
iv. Kuzitolea zaka ya sehemu ya kumi ya mapato ya mwaka ya mazao ya mashambani: Rejea Hosea 2:8
v. Kuziandika meza mbele yao: Rejea Isa. 65:11
vi. Kuzibusu sanamu kwa kuzisujudia kama viumbe vyenye enzi.
Rejea 1Fal. 19:18; Hos.13:2; Ayu. 31:2.
vii. Kuziinulia sanamu mikono katika kuzisujudia: Rejea Isa.44:20
viii. Kuziangukia sanamu kifudifudi ama kuzipigia magoti kwa kuziabudu: Rejea 1Fal.18:26,28.
ix. Kuzichezea ngoma na wakati mwingine kujikatakata kwa visu kama kitendo cha ibada kwa sanamu: Rejea 1Fal.18:26,28.
Hayo yote yakichunguzwa kwa makini, tutaona wazi kuwa hakuna Ibada ya kuabudu sanamu katika Kanisa Katoliki. Kwa hiyo, shutuma kwamba Wakatoliki wanaabudu sanamu siyo za kweli, hazina msingi, na ni uchochezi wa bure wenye lengo la kuleta mafarakano na magomvi. Jambo hilo ni dhahiri kwa sababu Wakatoliki hawana nia thabiti ya kuabudu sanamu wanapotoa heshima kwa sanamu au picha mbalimbali. Pili, matendo ya kiliturujia yanayofanywa na wakatoliki katika kuheshimu sanamu hayalingani na matendo ya kiliturujia yanayofanywa na waabudu sanamu, kama ilivyoelezwa katika Biblia Takatifu, hususan Agano la Kale. Kifupi, wakatoliki hawana nia thabiti moyoni ya kuziabudu sanamu au picha, tena hawazifanyii liturujia yoyote sanamu au picha walizo nazo majumbani au makanisani.
Ni wapi ambapo Kanisa Katoliki linafanya au kuwafundisha rasmi na kuwahimiza wafuasi wake wafanye matendo hayo tisa ya kiliturujia kwa ajili ya kuabudu sanamu? Hakuna! Kwa hiyo, Wakatoliki hawana hatia yoyote ya kuabudu sanamu mbele ya Mungu. Kama mtu mmoja akifanya hivyo, hilo ni shauri lake binafsi, siyo shauri au utaratibu wa Kanisa lote. Aidha, afanyaye hivyo amepotoka peke yake, kwa sababu hajafundishwa na Kanisa Katoliki afanye hivyo. Hilo ni kweli kwa sababu mambo binafsi, siyo mambo rasmi ya Kanisa lote!
Kwa hiyo, tunaona wazi kwamba Wakatoliki hawaabudu sanamu kamwe, kama inavyodaiwa na baadhi ya waamini wa madhehebu mengine ya kikristo. Wanaotoa shutuma hizo inafaa wajiangalie kwanza wao wenyewe, maana imeandikwa: “… mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi” (Rom.14:14).

JE, IJUMAA KUU WAKATOLIKI WANAABUDU NINI?

Je, ni kweli kwamba Siku ya IJUMAA KUU Wakatoliki wanaabudu Sanamu au Mti wa Msalaba? HAPANA! WANAMWABUDU WOKOVU-YESU! Kiini cha utata hapa ni “NINI MAANA YA IBADA YA KUABUDU MSALABA” inayoendeshwa siku ya Ijumaa Kuu? Madhehebu hayo yanayofanywa na Wakatoliki Siku ya IJUMAA KUU siyo Ibada ya Kuabudu Sanamu. Labda hapa ni tatizo la lugha au maneno yanayotumika, ndiyo yanayowachanganya watu! Hilo ni kweli kwa sababu jina la madhehebu yenyewe halisemi wazi kitu gani hasa kinanuiwa kufanywa katika ibada hiyo.
Wengi hawajui nini hasa kinanuiwa kufanyika siku ya Ijumaa Kuu katika “Ibada ya Kuabudu Msalaba” – jina ambalo nimesema halitoi picha halisi ya jambo linalokusudiwa kufanyika. Mtu mwenye akili timamu akijua kitu halisi kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu, hawezi kusema madhehebu hayo ni Ibada ya Sanamu au kuabudu mti. Tatizo hapo ni lugha tu inayotumika katika kuieleza ibada hiyo. Labda jina hilo lichunguzwe upya na wataalamu wetu katika Kanisa na ikiwezekana kulirekebisha ili kuondoa utata kwa baadhi ya watu wenye uelewa mdogo, wenye wanaokwazwa nalo!

NINI HASA KINAFANYIKA SIKU YA IJUMAA KUU?

Wanachofanya Wakatoliki Siku ya Ijumaa Kuu ni KUUHESHIMU MTI WA MSALABA na KUMWABUDU WOKOVU. WOKOVU ni nani? WOKOVU NI YESU KRSITO BWANA WETU. Basi, kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu ni kumwabudu WOKOVU yaani YESU KRISTO, ambaye alitundikwa msalabani. Hivyo ndivyo anavyotangaza Kiongozi wa Ibada hiyo ya Ijumaa Kuu, pale anapotoa mwaliko kwa waamini mara tatu, ili kila muumini ausikie na kuelewa vema: “HUU NDIO MTI WA MSALABA, AMBAO WOKOVU WA DUNIA UMETUNDIKWA JUU YAKE, NJOONI TUUABUDU.” Waamini wanaalikwa kiimani kuuabudu WOKOVU, na hilo ndilo linalofanyika, yaani kuuabudu WOKOVU – YESU KRISTO. Waamini wote wanaalikwa kujongea mbele kwa imani kwenda kumwabudu YESU. Watu wanamwabudu YESU kwa sababu WOKOVU maana yake ni YESU.
Jina YESU ambalo linatokana na Kiebrabia “YESHUA”, maana yake “WOKOVU” (Rej. Mt.1:21;1:25; Lk.1:31). Ikiwa wokovu ni YESU, basi Ijumaa Kuu Wakatoliki hawaabudu sanamu au mti, bali wanamwabudu YESU KRISTO. Kwa sababu hiyo, yote yanayofanyika Siku ya Ijumaa Kuu, yanafanyika kihalali na kwa haki kwa sababu YESU KRISTO, ambaye ni WOKOVU ni MUNGU, na MUNGU peke yake ndiye mwenye haki na anayepaswa kuabudiwa. Ikiwa mkristo hataki kumwabudu YESU KRISTO, aliye Mwana wa Mungu na Mungu kamili, na ambaye ameeleta wokovu, anafanya makosa makubwa!
Basi, nasisitiza kuwa Siku ya Ijumaa Kuu, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala mti. Wanamwabudu WOKOVU, yaani YESU KRISTO, Nafsi ya Pili ya MUNGU. Kutomwabudu YESU KRISTO ni sawa na kumkana Mungu, kukana wokovu ulioletwa naye. Basi, tujiepushe na ukanaji Mungu wa aina hiyo. Nawaalika wote Siku ya Ijumaa Kuu tufungue mioyo yetu kwa imani kubwa ili tumwone WOKOVU aliyetundikwa msalabani, apate kuukomboa ulimwengu. Kwa imani, wote tumsujudie YESU ili apate kutukumbuka katika Ufalme wake wa milele.
Hatimaye, niseme kwamba ingawa Mungu ametoa amri ya kukataza sanamu na picha (Kut. 20:4-5; Kumb. 5:6-10), lakini hachukizwi na kila sanamu au picha. Sanamu na picha ambazo hazipewi daraja la Mungu, Yeye hazichukii, kwa sababu hazichukui nafasi yake kama Muumba. Basi, Wakatoliki hawaendi kinyume na Biblia kwa kuziheshimu sanamu na picha zilizoko kwenye majumba yao na makanisani.
Read and Write Comments

Mambo ya Muhimu kufahamu kuhusu Ishara ya Msalaba

Ishara ya msalaba ni nini?
Ishara ya Msalaba ni tendo la mtu kugusa panda la uso, kifua na mabega kwa kutumia mkono wa kulia na kutamka “Kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina”


Kwa kugusa paji la uso tuna maana gani?
Kwa kugusa paji la uso tuna maana ya kukubali kwa akili


Kwa kugusa kifua tuna maana gani?
Kwa kugusa kifua maana yake ni kuupokea na kuukubali msalaba moyoni.


Kwa kugusa mabega tuna maana gani?
Kwa kugusa mabega maana yake ni kuwa tayari kuubeba msalaba kwa nguvu zetu zote


Kwa nini tunafanya Ishara ya Msalaba?
Tunafanya Ishara ya Msalaba kwa nia ya kumkiri Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Pia msalaba ni Ishara ya Ukombozi wetu


Ishara ndogo ya Msalaba juu ya panda la uso, mdomo, na kifua kabla ya Injili ina maana gani?
Maana yake ni kama Ahadi kuwa, Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu kwa akili yangu, Nitalitangaza kishujaa kwa Midomo yangu, Nitalipenda na kulishika kwa Moyo wangu wote.
Read and Write Comments
Shopping Cart