Ishara ndogo ya Msalaba juu ya panda la uso, mdomo, na kifua kabla ya Injili ina maana gani?
Maana yake ni kama Ahadi kuwa, Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu kwa akili yangu, Nitalitangaza kishujaa kwa Midomo yangu, Nitalipenda na kulishika kwa Moyo wangu wote.
Je ni dhambi kukosa Misa Jumapili?
NDIYO. Ni dhambi kubwa kukosa Misa kwa Makusudi siku ya Jumapili/Dominika na Sikukuu zilizoamriwa.
Sakramenti ya Ekaristi ni nini?
Sakramenti ya Ekaristi ni Sakramenti ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo, aliye kweli katika Maumbo ya Mkate na Divai. (Yoh 6:1-17, Mt 26:26-28)
Ni wakati gani katika Misa Mkate na Divai vinageuka Mwili na Damu yake Kristo?
Ni katikati ya Misa padri asemapo maneno Matakatifu aliyosema Yesu mwenyewe: “HUU NDIO MWILI WANGU; HII NDIO DAMU YANGU”
26 Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” 27 Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, “Kunyweni nyote; 28 maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi. 29 Nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”
30 Baada ya kuimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni. (Mat 26:26-30)
Je Sakramenti ya Ekaristi hujulikana kwa majina yapi?
Majina haya;
1. Ekaristi Takatifu
2. Karamu ya Bwana
3. Misa Takatifu
4. Sakramenti Takatifu ya Altare
5. Komunyo Takatifu
6. Sadaka Takatifu
7. Kumega Mkate
Baada ya Mitume kufa ni nani wanafanya Sakramenti ya Ekaristi
Badaa ya Mitume kufa Maaskofu na Mapadri wanaendelea kuadhimisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu
Ni lini Yesu Kristo aliwapa Maaskofu na Mapadri Uwezo wa kugeuza mkate na divai kuwa Mwili na Damu yake?
Yesu Kristo aliwapa Maaskofu na Mapadri Uwezo wa kugeuza mkate na divai kuwa Mwili na Damu yake alipowafanya Mitume kuwa Mapadri katika karamu ya mwisho aliposema “FANYENI HIVI KWA UKUMBUSHO WANGU” (Lk 22:14-20)
Misa ni nini?
Misa ni sadaka safi ya Wakristo kwa Mungu, ndiyo sadaka ya Agano Jipya ambayo
Kristo kwa njia ya Padri anamtolea Mungu Baba mwili na damu yake katika umbo la mkate na divai kama alivyojitolea mwenyewe juu ya msalaba.
Sadaka ya Msalaba ni nini?
Sadaka ya Msalaba ni tendo la mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristojuu ya Msalaba pale Kalvari
Ni kwa nini Sadaka ya Misa Takatifu ni Sadaka ile ile ya Msalaba?
Sadaka ya Misa Takatifu ni ile ile ya Msalaba kwa sababu ni sadaka moja tu, kuhani na kafara ni yule yule.
Tofauti ni namna tu yankuitoa hiyo sadaka. (1Kor 11:26, Ebr 9:14,25-28)
Pale msalabani damu ilimwagika lakini katika Ekaristi damu haimwagiki tena
Misa Takatifu hutolewa kwa nani?
Misa Takatifu hutolewa kwa Mungu Baba Mwenyezi (Ebr 5:1-10, Law 9:7).
Yesu aliweka sadaka ya Misa Takatifu kwa makusudi gani?
Yesu aliweka sadaka ya Misa Takatifu ili;
1. Amtolee Baba sadaka bora siku zote
2. Atujalie mastahili yake Msalabani
3. Azilishe roho kwa neema za sadaka hiyo. (Ebr 5:1-10, 7:27).
Sadaka ya Misa Takatifu yatolewa kwa nia gani?
Sadaka ya Misa Takatifu yatolewa kwa nia ya kumwabudu Mungu, kumshukuru, kujipatanisha nae na kumwomba. (Ebr 9:14)
Misa Takatifu hutolewa kwa ajili ya nani?
Misa Takatifu hutolewa kwa ajili ya kanisa nzima yaani kwa ajili ya watu wote wazima na wafu. (Ebr 9:14. Rum 1:9)
Kutolea Misa kwa Marehemu maana yake ni nini?
Kutolea Misa kwa Marehemu ni kutolea Misa kwa ajili ya roho zilizoko toharani ili ziweze kuingia mbinguni
Misa Takatifu ina sehemu kuu ngapi?
Misa Takatifu ina sehemu kuu mbili
1. Litrujia ya Neno
2. Liturujia ya Ekaristi
Litrujia ya Ekaristi ina sehemu kuu ngapi?
Litrujia ya Ekaristi ina sehemu kuu tatu
1. Matayarisho ya vipaji
2. Sala ya Ekaristi
3. Ibada ya Komunyo
Ni vitu gani vya msingi na vya lazima katika kuadhimisha Ekaristi Takatifu?
Vitu vya lazima katika kuadhimisha Ekaristi Takatifu ni
1. Mkate wa Ngano
2. Divai ya mzabibu
Kabla ya Kupokea Ekaristi Takatifu Tunasali sala gani?
Tunasali “Ee Bwana sistahili uingie kwangu lakini sema neno tu na roho yangu itapona”
Katika Ekaristi Takatifu Tunampokea nani?
Katika Ekaristi Takatifu Tunampokea Yesu Kristo Katika Maumbo ya Mkate na Divai na tunaungana naye (Yoh 6:57)
Mkristo awe katika hali gani kabla ya kupokea Ekaristi Takatifu?
1. Awe na Neema ya Utakaso yaani asiwe na dhambi ya mauti.
2. Awe na Imani, Ibada na Kumtamani Yesu.
3. Afunge chakula Muda wa saa Moja na Kileo zaidi ya masaa matatu.
4. Awe safi kimwili.
5. Awe na adabu na heshima.
Komunyo Takatifu Hutuletea neema gani?
1. Hulinda na kuongeza neema ya Utakaso iliyo uzima wa roho zetu.
2. Hutuondolea dhambi ndogo na kupunguza hatari ya kutenda dhambio kubwa.
3. Hututia bidii na nguvu ya kutenda mema kwa kutuongezea Imani, Matumaini na Mapendo.
4. Huleta Umoja katika Kanisa, sio sisi na Kristo tuu bali sisi kwa sisi.
Mkristo akipokea Ekaristi Takatifu akiwa na dhambi rohoni anatenda dhambi gani?
Mkristo akipokea Ekaristi Takatifu akiwa na dhambi anatenda dhambi kubwa yaani kufuru Sakramenti.
26 Maana kila mnapokula mkate huu na kukinywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja. 27 Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana. (1 Kor 11;26 – 27)
28Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho; 29 maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe. 30 Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa. 31 Kama tungejichunguza wenyewe vizuri hatungeadhibiwa hivyo. 32Lakini tunapohukumiwa na Bwana, tunafunzwa tuwe na nidhamu, ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu. (1 Kor 11;28 – 32)
Je, Kanisa linahimiza waamini wapokee Ekaristi wakati gani?
Kanisa linahimiza waamini wapokee Komunyo Takatifu kila siku wanaposhiriki Misa
Nani Mhudumu wa adhimisho la Ekaristi Takatifu?
Mhudumu wa adhimisho la Ekaristi Takatifu ni Askofu na Padre
Je, Mkristo akipokea kipande cha Hostia amempokea Yesu Mzima?
Ndiyo, Amempokea Yesu Mzima kabisa, Hata akipewa zaidi ya hostia moja amempokea Yesu Mzima
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu Huifadhiwa wapi?
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu Huifadhiwa kwenye Tabernakulo
Tabernakulo ni nini?
Tabernakulo ni mahali Patakatifu anapokaa Yesu wa Ekaristi siku zote
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu hukaa Tabernakulo kwa sababu gani
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu hukaa Tabernakulo kwa ajili ya watu wote hasa wagonjwa
Ishara wazi ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni nini?
Ishara wazi ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni maumbo ya mkate na divai, na maneneo ya mageuzo ya Yesu mwenyewe Padri akiyatamka.
Baada ya kumpokea Yesu wa Ekaristi tufanye nini?
Baada ya kumpokea Yesu wa Ekaristi: Tumwabudu,tumshukuru, tumwombe kwani yeye ni Mwenyezi. (Mt 2:11, Lk 17:11)
Read and Write Comments