Mafundisho makubwa ya Yesu Kristo

Heri

Basi Yesu alipoona makutano, alipanda
mlimani akaketi chini, nao wanafunzi
wake wakamjia. 2Ndipo akaanza kuwafundisha,
akisema:
3 “Wana heri walio masikini wa roho,
maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao.
4Wana heri wale wanaohuzunika,
maana hao watafarijiwa.
5Wana heri walio wapole,
maana hao watairithi nchi.
6Wana heri wenye njaa na kiu ya haki,
maana hao watatoshelezwa.
7Wana heri wenye huruma,
maana hao watapata rehema.
8Wana heri walio na moyo safi,
maana hao watamwona Mungu.
9Wana heri walio wapatanishi,
maana hao wataitwa wana wa Mungu.
10Wana heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,
maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao.
11Mna heri ninyi watu watakapowashutumu
na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya
aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. 12Furahini
na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni
kuu.

Chumvi na Nuru

13‘‘Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini
chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje
kurudishiwa ladha yake tena ? Haifai tena kwa
kitu cho chote, ila kutupwa nje ikanyagwe na
watu.
14‘‘Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji
uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15Wala
watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli.
Badala yake, huiweka kwenye kinara chake,
nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani
ya ile nyumba. 16Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze
mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu
mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

Kutimiza Sheria

17“Msidhani kwamba nimekuja kuondoa
Torati au Manabii, sikuja kuondoa bali kutimiza.
18Kwa maana,amin, nawaambia, mpaka mbingu
na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja
ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yo
yote kutoka kwenye Torati mpaka kila kitu kiwe
kimetimia. 19Kwa hiyo, ye yote atakayevunja
mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri
hizi, naye akawafundisha wengine kufanya
hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa
Mbinguni, lakini ye yote azitendaye na
kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika
Ufalme ya Mbinguni. 20Kwa maana nawaambia,
haki yenu isipozidi haki ya waandishi wa sheria
na Mafarisayo, kamwe hamtaingia katika
Ufalme wa Mbinguni.

Mafundisho ya Yesu Kuhusu Hasira

21“Mmesikia walivyoambiwa watu wa
zamani kwamba, ‘Usiue, ye yote atakayeua
atapasiwa hukumu.’ 22Lakini mimi nawaambia
kwamba, ye yote atakayemkasirikia ndugu yake
wa kiume au wa kike, atapasiwa hukumu. Tena,
ye yote atakayemwambia ndugu yake wa kiume
au wa kike, ‘Raca’a, yaani kumdharau na
kumdhihaki, atapasiwa kufanyiwa baraza. Lakini
ye yote atakayesema ‘We mpumbavu ulaaniwe!’
Atapasiwa hukumu ya moto wa jehanam.
23“Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako
madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako
ana kitu dhidi yako, 24iache sadaka yako hapo
hapo, mbele ya madhabahu, uende kwanza
ukapatane na ndugu yako wa kiume au wa kike,
kisha urudi na ukatoe sadaka yako.
25“Patana na mshtaki wako upesi wakati
uwapo njiani pamoja naye kwenda
mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia
mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia
mikononi mwa walinzi, nawe ukatupwa
gerezani. 26Amin, nakuambia, hutatoka humo
mpaka umelipa hadi senti ya mwisho”

Mafundisho ya Yesu Kuhusu Uzinzi

27“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini’.
28Lakini mimi nawaambia: kwamba ye yote
amtazamaye mwanamke kwa kumtamani,
amekwisha kuzini naye moyoni mwake. 29Jicho
lako la kuume likikufanya utende dhambi, ling’oe
ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza
kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako
mzima utupwe jehanam. 30Kama mkono wako
wa kuume ukikufanya utende dhambi, ukate
uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza
kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako
mzima utupwe jehanam.

Mafundisho ya Yesu Kuhusu Talaka

31‘‘Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu ye yote
amwachaye mkewe na ampe hati ya talaka.’
32Lakini mimi nawaambia, ye yote amwachaye
mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati,
amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na ye yote
amwoaye yule mwanamke aliyeachwa azini.’’

Mafundisho ya Yesu Kuhusu Kuapa

33“Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa
zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali
timizeni, nadhiri zile ulizofanya kwa Bwana’
34Lakini mimi nawaambia,’’Msiape kabisa, ama
kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha
Mungu, 35au kwa nchi, kwa kuwa ndipo mahali
pake pa kuwekea miguu, au kwa Yerusalemu,
kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu. 36Nanyi
msiape kwa vichwa vyenu kwa kuwa hamwezi
kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe
au mweusi. 37‘Ndiyo,’ yenu iwe ‘Ndiyo’ na
‘Hapana’, yenu iwe ‘Hapana.’ Lo lote zaidi ya hili
latoka kwa yule mwovu.’’

Mafundisho ya Yesu Kuhusu Kulipiza Kisasi

38“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa
jicho na jino kwa jino.’ 39Lakini mimi nawaambia,
msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu
akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na
la pili pia, 40Kama mtu akitaka kukushtaki na
kuchukua shati lako, mwachie achukue na koti
pia. 41Kama mtu akikulazimisha kwenda
kilometa moja, nenda naye kilometa mbili.
42Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie
kisogo yeye atakaye kukukopa.’’

Mafundisho ya Yesu kuhusu Upendo Kwa Adui

43‘‘Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende
jirani yako na umchukie adui yako.’ 44Lakini
mimi ninawaambia : Wapendeni adui zenu na
waombeeni wanaowatesa ninyi, 45ili mpate
kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa
maana Yeye huwaangazia jua lake watu waovu
na watu wema, naye huwanyeshea mvua
wenye haki na wasio haki. 46Kama mkiwapenda
wale wanaowapenda tu, mtapata thawabu gani?
Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo?
47Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je,
mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu
wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? 48Kwa hiyo
iweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni
alivyo mkamilifu.’’

Mafundisho ya Yesu kuhusu Kuwapa Wahitaji

‘‘Angalieni msitende wema wenu mbele ya
watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya
hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu
aliye mbinguni.
2‘‘Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige
panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki
katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na
watu. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha
kupokea thawabu yao. 3Lakini ninyi mtoapo
sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa
kushoto usijue mkono wako wa kuume
unachofanya, 4ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo
Baba yako wa mbinguni, Yeye aonaye sirini
atakupa thawabu kwa wazi.

Mafundisho ya Yesu Kuhusu kusali

5“Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki,
maana wao hupenda kusali wakiwa
wamesimama katika masinagogi na kando ya
barabara ili waonekane na watu. Amin, amin
nawaambieni, wao wamekwisha kupata
thawabu yao. 6Lakini wewe unaposali, ingia
chumbani mwako, funga mlango na umwombe
Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye
sirini atakupa thawabu yako. 7“Nanyi mnaposali
msiseme maneno kama wafanyavyo watu
wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani
kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa
maneno yao. 8Msiwe kama wao, kwa sababu
Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla
hamjamwomba.’’
9‘‘Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba :
“Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako litukuzwe.
10Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike hapa duniani
kama huko mbinguni.
11Utupatie leo riziki zetu za kila siku.
12Utusamehe deni zetu,
kama sisi nasi tulivyokwisha
kuwasamehe wadeni wetu.
13 Usitutie majaribuni,
bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu,
kwa kuwa Ufalme ni Wako na nguvu
na utukufu hata milele. Amen.”
14Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine
wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni
atawasamehe pia na ninyi. 15Lakini
msipowasamehe watu wengine makosa yao,
wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa
yenu.

Mafundisho ya Yesu Kuhusu Kufunga

16“Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama
wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja
nyuso zao ili kuwaonyesha wengine kwamba
wamefunga. Amin, amin nawaambia wao
wamekwisha kupata thawabu yao kamilifu.
17Lakini mnapofunga, jipakeni mafuta kichwani
na kunawa nyuso zenu 18ili kufunga kwenu
kusionekane na watu wengine ila Baba yenu
aliye sirini, naye Baba yenu aonaye sirini
atawapa thawabu yenu kwa wazi.”

Akiba Ya Mbinguni

19“Msijiwekee hazina duniani, mahali
ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi
huvunja na kuiba. 20Lakini jiwekeeni hazina
mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu
haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba.
21Kwa sababu mahali akiba yako ilipo, hapo
ndipo pia moyo wako utakapokuwa.’’

Jicho Ni Taa Ya Mwili

22‘‘Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni
nyofu, mwili wako wote utakuwa na nuru.
23Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote
utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru
iliyomo ndani yako ikiwa giza, hilo ni giza kuu
namna gani ! ”

Mungu Na Mali

24‘‘Hakuna mtu ye yote awezaye
kuwatumikia mabwana wawili, kwa kuwa ama
atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine,
au atashikamana sana na huyu na kumdharau
huyu mwingine. Ninyi hamwezi kumtumikia
Mungu na malia.’’

Msiwe Na Wasiwasi

25‘‘Kwa hiyo nawaambia, msiwe na
wasiwasi kuhusu maisha yenu: mtakula nini au
mtakunywa nini, au kuhusu miili yenu, mtavaa
nini. Je, maisha si zaidi ya chakula na mwili
zaidi ya mavazi? 26Waangalieni ndege wa
angani, wao hawapandi wala hawavuni au
kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni
huwalisha hao. Je, ninyi si wa thamani zaidi
kuliko hao ndege? 27Ni nani miongoni mwenu
ambaye kwa kujitaabisha kwake aweza
kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha
yake au kuongeza dhiraa mojab kwenye kimo
chake ?
28‘‘Nanyi kwa nini kujitaabisha kwa ajili ya
mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo.
Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29Lakini
nawaambia, hata mfalme Solomoni katika fahari
yake yote hakuvikwa kama mojawapo ya hayo
maua. 30Lakini ikiwa Mungu anayavika hivi
majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho
yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri
zaidi, enyi wa imani haba? 31Kwa hiyo msiwe na
wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ Au
‘Tutakunywa nini?’ Au ‘Tutavaa nini?’ 32Kwa
maana watu wasiomjua Mungu ndio
wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa
mbinguni anafahamu kwamba mnahitaji hayo
yote. 33Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa
Mungu na haki yake na haya yote
mtaongezewa. 34Kwa hiyo msiwe na wasi wasi
kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia
yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.’’

Mafundisho ya Yesu kuhusu Kuwahukumu Wengine

“Usihukumu ili usije ukahukumiwa. 2Kwa
maana kwa jinsi ile unavyowahukumu
wengine, ndivyo utakavyohukumiwa na kwa
kipimo kile utakachotoa ndicho utakachopokea.
3‘‘Kwa nini unatazama kibanzi kidogo
kilichomo kwenye jicho la ndugu yako na wala
huoni boriti iliyoko kwenye jicho lako? 4Au
unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe
kibanzi kwenye jicho lako wakati kuna boriti
kwenye jicho lako mwenyewe ?’ 5Ewe mnafiki,
toa kwanza boriti kwenye jicho lako mwenyewe,
nawe ndipo utakapoona wazi ili kuondoa kibanzi
kilichoko kwenye jicho la ndugu yako.
6‘‘Msiwape mbwa vitu vilivyo vitakatifu, wala
msitupie nguruwe lulu zenu. Kama mkifanya
hivyo, watazikanyaga kanyaga na kisha
watawageukia na kuwararua vipande vipande. ”

Omba, Tafuta, Bisha

7“Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi
mtapata, bisheni nanyi mtafunguliwa mlango.
8Kwa maana kila aombaye hupewa, naye
atafutaye huona, naye abishaye hufunguliwa
mlango.
9‘‘Au ni nani miongoni mwenu ambaye
mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe?
10Au mwanawe akimwomba samaki atampa
nyoka? 11Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua
jinsi ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi
sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu
vizuri wale wamwombao ? 12Kwa hiyo cho chote
ambacho mngetaka mtendewe na watu, ninyi
nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii
ndiyo Torati na Manabii.’’

Njia Nyembamba Na Njia Pana

13‘‘Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba,
kwa maana lango ni pana na njia ni pana
ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa
kupitia lango hilo. 14Lakini mlango ni
mwembamba na njia ni finyo ielekayo kwenye
uzima, nao ni wachache tu waionao.’’

Mti na Tunda lake

15“Jihadharini na manabii wa uongo,
wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya
kondoo, lakini ndani wao ni mbwa mwitu
wakali.16Mtawatambua kwa matunda yao. Je,
watu huchuma zabibu kwenye miiba au tini
kwenye michongoma? 17Vivyo hivyo, mti
mwema huzaa matunda mazuri na mti mbaya
huzaa matunda mabaya. 18Mti mwema hauwezi
kuzaa matunda mabaya wala mti mbaya
hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19Kila mti
usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa
motoni. 20Hivyo, kwa matunda yao,
mtawatambua.’

Mwanafunzi Wa Kweli

21“Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’
atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni bali ni
yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye
mbinguni. 22Wengi wataniambia siku ile,
‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako
na kwa jina lako kutoa pepo na kufanya miujiza
mingi? 23Ndipo nitakapowaambia wazi,
`’Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi
watenda maovu!’

Msikiaji Na Mtendaji

24‘‘Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya
maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu
mwenye busara aliyejenga nyumba yake
kwenye mwamba. 25Mvua ikanyesha, mafuriko
yakaja na upepo ukavuma ukaipiga hiyo
nyumba, lakini haikuanguka kwa sababu msingi
wake ulikuwa kwenye mwamba. 26Naye kila
anayesikia haya maneno yangu wala
asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga
nyumba yake kwenye mchanga. 27Mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo
ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo
ikaanguka kwa kishindo kikubwa.’’
28Yesu alipomaliza kusema maneno haya,
makutano ya watu wakashangazwa sana na
mafundisho yake, 29kwa sababu alifundisha
kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama
walimu wao wa sheria.