Jiunge na Kampeni ya Wafanye Watabasamu Uongeze Furaha Katika Maisha Yako na ya Wengine
Kampeni Ya Wafanye Watabasamu | Let Them Smile Campaign
Utangulizi
Let Them Smile Campaign au Kampeni ya Wafanye nao Watabasamu ni kampeni endelevu ya kuhamasisha ushirikiano, umoja na kusaidiana katika jamii kwa watu wa matabaka yote.
Kampeni hii ina lengo la kuamsha na kueneza furaha itokanayo na umoja na mshikamano kwenye jamii kwa njia ya kusaidiana na kushirikiana kimawazo, kwa matendo na kifedha. Ni kweli kwamba furaha ya kweli haiji kwa kujifurahisha mwenyewe bali kwa kufurahishwa.
Vile vile kuwa tajiri haimaanishi kuwa ndio una furaha na amani katika maisha ndio maana wapo matajiri wanaojiua kwa kutoona thamani ya maisha yao.
Na kuwa maskini haimaanishi ndio unakosa furaha na amani.
Lengo la Kampeni hii ni kuongeza furaha kwa kusaidiana na kuelewesha kuwa misaada sio lazima iwe fedha tuu bali hata maneno na matendo ya kufariji. Vile vile wale wanaohitaji msaada sio masikini tuu na wasiojiweza bali hata matajiri na wenye uwezo. Masikini mara nyingi anahitaji msaada wa kiuchumi wakati tajiri anaweza akahitaji msaada wa maneno, mawazo au faraja kwa matendo. Kwa hiyo makundi yote mawili yanahitaji msaada na tunawaita wahitaji.
Kampeni hii imeanzishwa na Melkisedeck Leon Shine Disemba 2015 kama kampeni binafsi na kushirikishwa rasmi kwa uma Julai 2017.
“Natamani watu wakumbuke kuwa vile unavyojisikia unapokuwa na shida au changamoto ndivyo vivyo hivyo mtu mwenye mahitaji/maskini anavyojisikia…Mfano unavyosikia njaa na kujisikia vibaya fikiri ni jinsi gani mtu anavyojisikia anapokaa na njaa siku zote ambaye yeye ni binadamu kama wewe…Vile unavyotamani kuwa na furaha katika Maisha ndivyo na Wengine wanavyotamani….Vile vile watu wajue kuwa sio maskini tuu wenye shida bali hata matajiri wanashida na wanahitaji msaada japo sio wa kifedha.” — Melkisedeck Shine
Kampeni ya Wafanye nao Watabasamu inawahamasisha watu wawe chanzo cha furaha kwa Wengine hasa wahitaji na wasiojiweza pia wanaojiweza na wenye navyo.
Nia au Malengo ya Kampeni Hii
- Kuelimisha jamii kuwa furaha katika maisha haiji kwa kuwa na kipato kizuri cha kiuchumi tuu.
- Kuelimisha jamii kuwa umasikini sio kukosa fedha tuu bali hata kukosa mawazo, kukosa malengo, kukosa faraja n.k. Ndio maana hata matajiri ni wahitaji na hata maskini wa fedha anaweza akawa tajiri kwenye nyanja nyingine.
- Kuleta furaha na matumaini ya kuishi kwa watu hasa wenye mahitaji na wasiojiweza kwa kuwasaidia moja kwa moja au kuwaongoza kukabiliana na changamoto zao. Mfano kwa Fedha, maneno ya faraja na uwepo wakati wa changamoto.
- Kuleta amani katika jamii kwa kudumisha ushirikiano na upendo baina ya wenye nacho na wasiokuwa nacho.
- Kudumisha ushirikiano na umoja kwa kujumuika pamoja katika shida na raha.
- Kuleta maendeleo ya kizazi hiki na kijacho kwa kujenga msingi mzuri wa maisha.
Walengwa wa Kampeni
Watu wote ni walengwa wa kampeni hii kwa maana kila mtu anaishi na wahitaji kando yake katika maisha ya kawaida ya kila siku. Uhitaji sio lazima wa kifedha, hata wa mawazo.
Kila mtu kwa nafasi yake anaalikwa kutoa Misaada ya hali na mali pamoja na Kujumuika katika shida na raha kwa maneno na matendo. Awe tajiri au Masikini ana nafasi yake kwa mwenzake.
Unachoweza kukifanya kwa Sasa kuitikia kampeni hii
Kampeni kwa sasa inahamasisha watu kwa njia ya mtandao kujiunga nayo kwa kufanya vile vilivyotajwa hapo juu kama nia kampeni hii.
Unaweza ukajiunga au ukaitikia wito wa kampeni hii kwa kufanya haya yafuatayo unapoweza;
- Kutowapa kisogo wahitaji pale unapoweza.
- Kumsaidia mhitaji kwa mawazo, matendo au fedha.
- Kusaidia watoto yatima au wale wanaoishi katika mazingira magumu. Unaweza kusaidia mahitaji ya shule au chakula. Mfano unaweza ukampa mtoto chakula cha mchana pale unapomkuta na sio lazima kila siku.
- Kujumuika na kuwasaidia wahitaji wanapokuwa katika changamoto za maisha kama Magonjwa, misiba nakadhalika.
Recent Comments