Usiyoyajua kuhusu pesa haya hapa

Habari za Leo Rafiki yangu wa Muhimu sana. Ni furaha yangu kujua unaendelea vyema sana na majukumu yako.

Ni wakati mwingine tena tunaenda kujifunza pamoja juu ya mambo mbalimbali ili tuweze kufikia mafanikio kila siku. Leo tunakwenda kujifunza kuhusu pesa na utajua mambo mengi sana juu ya pesa.

Ni siri gani ipo ndani ya fedha na wengi hawaijui?

Kwanini watu wengi wanakua matajiri halafu wanapoteza utajiri wao wote na kuwa maskini tena?

Ulishawahi kuona watu maarufu wamekua na pesa nyingi lakini baada ya muda wanapotea na pesa zao zinapotea na kurudi kuwa watu wa kawaida kabisa?

Hujawahi kuona watu wakiuza mashamba ya urithi kwa mamilioni ya pesa na wakabadilisha aina ya maisha wanayoishi lakini baada ya muda pesa zinapotea na wanarudia hali yao ya zamani?

Hujakutana na vijana waliochimba madini wakajikuta wamepata mawe wakawa milionea lakini ghafla baada ya muda Fulani wanarudi kule kule walipokua?

Wengi wakiona hayo utawasikia wanasema pesa za mashamba hazika! Pesa za madini zina mashetani! Ni siri gani ipo kwenye hii pesa?

Inawezekana umeshajiuliza sana maswali haya na hata kuogopa kuwa nayo. Ukaamua kuwa mtu wa kawaida tu kwasababu ya hofu hizi zinazokujia unapofikiri kuwa tajiri kisha uje upoteze pesa zako zote!

Watu wengi wamekuwa na fikra kwamba pesa ni mbaya, zinaharibu watu, zinawafanya watu kuwa wachoyo, zinawafanya watu kuwa na tamaa pamoja na mengine mengi unayoyafahamu.

Ukweli ni kwamba pesa haina tatizo lolote pesa haina shetani wala pepo lolote linaloifanya imharibu mtu anapokuwa nayo nyingi. Pesa sio kiumbe hai. Pesa tunaitumia kununua bidhaa mbalimbali au kulipia huduma tunazozihitaji katika maisha yetu ya kila siku.

Ukweli kuhusu pesa ni huu hapa. Kwanza pesa haimbadilishi mtu bali inamfanya awe Zaidi ya vile alivyokuwa mwanzo yaani kama mtu alikuwa ni mchoyo akipata pesa atakuwa mchoyo maradufu, kama alikua mlevi akipata pesa anazidisha kuwa mlevi Zaidi.

Na wengine wakiwa hawana pesa kuna tabia nyingi wanakuwa nazo ndani zimejificha hawazionyeshi wakishapata pesa zile tabia zinafunguka na kuwa wazi.

Kama mtu alikuwa Malaya akipata pesa ndio utaona anaanza kubadilisha wanawake. Pesa zinabaki kuwa pesa na tabia za mtu zinabakia kuwa tabia za mtu.

Kama mtu alikua mtoaji akipata pesa atakuwa mtoaji Zaidi.
Kama alikua mcha Mungu akipata pesa atakwenda kuabudu Zaidi.
Hivyo pesa sio tatizo watu ndio wenye matatizo ndani yetu.

“Having more money won’t change you as a person. It will, however, magnify
the person you already are.” – Bob Proctor

Huwa napenda kuutumia mfano wa chombo. Watu wengi wanaopata pesa nyingi ghafla na kuzipoteza zote ni kama maji yaliyojaa kwenye ndoo utake kuyaweka yote kwenye kikombe cha chai.

Ukweli ni kwamba kikombe kitajaa lakini yale yaliyobaki yatamwagika yote chini hivyo hivyo na pesa zinazopatikana ghafla ni sawa na kuziweka kwenye kikombe ambacho ni uwezo wa akili yako.

Kama Akili yako bado haijaweza kupangilia milioni ishirini hivyo hata ukipewa leo zote zitapotea na zitabaki kile kiwango ambacho akili yako inaweza kutawala na kuendesha. Hivyo njia sahihi ya wewe kuweza kumiliki mamilioni ya shilingi na kubakia nayo ni kuanza kubadili ufahamu wako. Kuza ufahamu wako kidogo kidogo ili uweze kuendesha utajiri mkubwa. Na hili halitokei ndani ya siku moja ni kadiri unavyojifunza kila siku. Kwa kusoma vitabu na kufanyia kazi yale unayojifunza.

Jambo moja na muhimu la kufanya ni kutokuweka akili yako yote kwenye pesa. Usiweke malengo yako kwenye pesa unapofanya biashara unafanya ili upate pesa lakini siku zote pesa hazikai huwa zinaisha hivyo badala ya wewe kuweka nguvu zako na mawazo yako kwenye pesa weka Zaidi katika kuwasaidia watu kama unauza nguo kazana Zaidi katika kuwafanya watu wafurahie huduma yako pesa zitakuja.

Kama unatoa huduma hakikisha unatoa huduma bora ili kuvutia wateja Zaidi kila siku. Pesa utaziona kwako na zitaongezeka kila wakati.

Wekeza pia muda wako kwenye kutengeneza mifumo mbalimbali ambayo itakuwa inakuingizia pesa bila kuwa na kikomo. Unapotegemea mfereji mmoja wa kipato lazima utabakia pale pale siku zote.

Jambo la muhimu la kufanya ili uweze kubakia juu kwenye mafanikio siku zote ni kujifunza na kujijengea misingi ambayo itakuwezesha wewe usiyumbe na ubakie na utajiri wako.

Kuwa mwaminifu, kua mtoaji, wapende wengine, kuwa muadilifu, usidhulumu mtu, kabla hujafanya lolote angalia lina manufaa gani kwako na kwa wengine.

Nikutakie wakati mwema Asante sana kwa kusoma Makala hii.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Shopping Cart