MITAGUSO MIKUU
Yesu Kristo aliwakabidhi mitume kumi na wawili uongozi wa Kanisa wakiwa kundi moja lenye mkuu wake, yaani Petro. Vilevile waandamizi wao, yaani maaskofu wote, ni kundi moja na Papa wa Roma ndiye mkuu wao. Huyo peke yake, na kundi la maaskofu likiwa pamoja naye na chini yake, ndio wenye mamlaka ya juu katika Kanisa lote. Mamlaka hiyo inatumika kwa namna ya pekee unapofanyika mtaguso mkuu, yaani mkutano maalumu wa maaskofu uliokubaliwa na Papa kuwa unawakilisha kundi hilo lote. Hakuna uamuzi wa kudumu kuhusu ipi ni mikuu kati ya mitaguso yote iliyofanyika katika historia ya Kanisa. Tangu karne XVI Wakatoliki wataalamu wa sheria za Kanisa wanatoa orodha yao, ambayo kwa sasa ni kama ifuatavyo.
ORODHA YA MITAGUSO MIKUU
• Katika milenia ya kwanza ilifanyika mashariki (Uturuki wa leo):
1. Nisea I (mwaka 325)
2. Kostantinopoli I (381)
3. Efeso (431)
4. Kalsedonia (451)
5. Kostantinopoli II (553)
6. Kostantinopoli III (680-681)
7. Nisea II (787)
8. Kostantinopoli IV (869-870)
• Katika milenia ya pili ilifanyika magharibi (Italia, Ufaransa, Ujerumani, Uswisi na Vatikano ya leo):
9. Laterano I (1123)
10. Laterano II (1139)
11. Laterano III (1179)
12. Laterano IV (1215)
13. Lyon I (1245)
14. Lyon II (1274)
15. Vienne (1311-1312)
16. Konstanz (1414-1418)
17. Firenze (1431-1445)
18. Laterano V (1512-1517)
19. Trento (1545-1563)
20. Vatikano I (1869-1870)
21. Vatikano II (1962-1965)
HISTORIA YA MITAGUSO MIKUU
Mitaguso mikuu ya kwanza ilifanyika hasa ili kubainisha katika mafundisho yaliyogongana yapi yanalingana na imani sahihi. Mwisho wake ulikuwa kutangaza dogma fulani na kutenga na Kanisa watakaokataa kuiamini na watakaofundisha tofauti.
Mitaguso iliyofanyika baada ya farakano la mwaka 1054 kati ya Kanisa la mashariki na la magharibi, pamoja na kulenga umoja uliovunjika na kufundisha dogma mpya, ilishughulikia zaidi urekebisho wa Kanisa katika ngazi na nyanja zote. Kwa namna ya pekee Mtaguso II wa Vatikano tangu uitishwe ulijulikana kuwa wa kichungaji, yaani usio na lengo la kufundisha dogma mpya wala kulaani mafundisho mengine.
Mtaguso I wa Nisea (325)
Mtaguso I wa Nisea ndio mtaguso wa kwanza kuitwa (tangu mwaka 338) mtaguso wa kiekumeni, yaani mtaguso wa dunia yote au mtaguso mkuu. Ndiyo sababu inashika nafasi ya pekee kati ya mitaguso yote.
Uliitishwa na kusimamiwa na kaisari Konstantino Mkuu, aliyehofia mabishano kati ya raia wake Wakristo kuhusu Yesu Kristo, ambayo yalihatarisha umoja na usalama wa Dola la Roma lililoanza kuelekea kusambaratika. Yeye aliwaalika maaskofu wote wa dola, waliokuwa kama 1000 mashariki na kama 800 magharibi. Washiriki walitokea hata nje ya dola hilo, kama vile Persia na Armenia. 2
Katika hali hiyo mtaguso ulianza tarehe 20 Mei 325; washiriki walikuwa kama 318, wengi wao wakitokea upande wa mashariki wa dola hilo. Upande wa magharibi uliwakilishwa na watu 4 kutoka Ulaya na 1 kutoka Afrika. Papa Silvesta I (314-335) aliwakilishwa na mapadri wawili.
Asili ya mabishano ilitokea katika Kanisa la Aleksandria (Misri), ambapo kasisi Arios alikuwa amekanusha umungu wa Yesu, na hivyo alihukumiwa na Sinodi ya Aleksandria ya mwaka 321, iliyoitishwa na askofu Aleksanda wa Aleksandria. Hata hivyo Arios hakuacha mafundisho yake, akakimbilia Palestina kwa rafiki yake Eusebio wa Nikomedia.
Basi, mtaguso ulikiri karibu kwa kauli moja kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu kwa maana ana ousìa (yaani dhati) ileile ya Kimungu aliyonayo Baba. Ndiyo kiini cha Kanuni ya imani ya Nisea iliyopitishwa na mtaguso.
Uamuzi mwingine wa mtaguso ulikuwa kupanga siku ya Pasaka, sherehe kuu ya Kanisa, iwe Jumapili inayofuata mbalamwezi ya kwanza ya majira ya Springi, tofauti na kalenda ya Kiyahudi. Pia zilitungwa kanuni 20 kuratibu mambo mbalimbali.
Mtaguso ulipomalizika tarehe 25 Julai 325, Konstantino alifikiri uamuzi juu ya dogma utamaliza mabishano, lakini haikuwa hivyo, kwa sababu Wagiriki wengi, ingawa hawakukubaliana na Arios, hawakuridhika na msamiati uliotumika kuelezea uhusiano wa Baba na Mwana.
Mtaguso I wa Konstantinopoli (381)
Mtaguso I wa Konstantinopoli ndio wa pili kati ya mitaguso ya kiekumene yaliyofanyika wakati wa mababu wa Kanisa. Uliitishwa na kaisari Theodosius I ukafanyika Konstantinopoli mwaka 381.
Maaskofu 150 waliohudhuria walilaani aina mbalimbali za uzushi, hasa ule wa Masedoni wa Konstantinopoli aliyekanusha umungu wa Roho Mtakatifu, wakathibitisha maamuzi ya mtaguso mkuu wa kwanza (Mtaguso I wa Nisea), uliofanyika mwaka 325.
Hivyo walikiri kwamba Roho Mtakatifu pia, kama vile Yesu Mwana wa Mungu, anachanga dhati ileile ya Baba.
Pamoja na hayo, walikamilisha kanuni ya imani ya Nisea ambayo kwa sababu hiyo inaitwa sasa kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli na ambayo inatumika sana hata leo katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo, hasa katika liturujia.
Mtaguso wa Efeso (431)
Mtaguso wa Efeso unahesabiwa na Wakristo walio wengi kama mtaguso mkuu wa tatu. Ulifanyika Efeso katika mkoa wa Asia Ndogo, kwa amri ya kaisari Theodosi II; Papa Selestini I (422-432) alimteua Sirili wa Aleksandria kuuendesha; washiriki walikuwa zaidi ya 150 na kujadili vikali hasa uzushi wa Nestori wa Konstantinopoli.
Patriarki huyo alikuwa anasisitiza ubinadamu wa Yesu Kristo kuliko umungu wake, akisema Bikira Maria alimzaa mtu Yesu, si Mungu, wala si Neno wa Mungu aliyehifadhiwa ndani ya nafsi ya Kristo kama hekaluni. Kwa hiyo Kristo alikuwa Theophoros, yaani “mbeba Mungu”, na Maria Christotokos, “Mama wa Kristo” si Theotokos, “Mama wa Mungu”.
Mtaguso huo ulilaani haraka mafundisho hayo ukikiri kwamba nafsi ya Yesu Kristo ni moja tu, ile ya milele ya Mwana wa Mungu, na kwamba nafsi hiyo ilitwaa ubinadamu kamili wenye mwili na roho. Hivyo Maria ni Theotokos kwa kuwa alimzaa Mungu kama binadamu.
Wajumbe wa Papa walipofika walithibitisha uamuzi huo, lakini maaskofu kutoka Antiokia hawakuridhika, na uzushi huo uliendelea Mesopotamia na kuenea hata Asia mashariki.
Mtaguso ulitangaza kuwa Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli ni kamili ukakataza isibadilishwe kwa namna yoyote. Pia ulilaani Upelaji, uzushi kutoka Ulaya magharibi kuhusu uwezo wa binadamu kutenda mema bila kusaidiwa na neema ya Mungu.
Mtaguso wa Kalsedonia (451)
Mtaguso wa Kalsedonia (leo katika nchi ya Uturuki) unahesabiwa na Wakristo wengi kuwa wa nne kati ya mitaguso ya kiekumeni iliyofanyika katika historia ya Kanisa.
Mtaguso huo uliitishwa na kaisari Marcianus wa Dola la Roma Mashariki pamoja na mke wake Pulkeria wa Bizanti miaka 20 baada ya Mtaguso wa Efeso.
Hao waliona haja ya kudumisha umoja wa Wakristo, uliokuwa msingi wa uimara wa dola hilo, hasa wakati huo ambapo makabila yasiyo na ustaarabu kutoka Asia yalikuwa yanajaribu kuteka Ulaya.
Umoja huo uliingia hatari ya kuvunjika kutokana na uamuzi wa mtaguso mkuu wa Efeso kuhusu imani sahihi juu ya Yesu Kristo kutoeleweka kwa namna moja.
Hasa baadhi ya walioshinda mtaguso huo walionekana kusisitiza mno umungu wake hata kutia shaka kama wanaamini sawasawa ubinadamu wake.
Vikao vilianza tarehe 8 Oktoba 451 vikiwa na washiriki zaidi ya 350: mara nyingi inatajwa idadi ya 600 hivi. Hatimaye mafundisho ya Eutike na Dioskoro wa Aleksandria yalilaaniwa.
Ufanisi wa mtaguso ulichangiwa na msimamo wa kaisari Valentiniano III wa Dola la Roma Magharibi, binamu wa Pulkeria. Kaisari huyo alimuunga mkono Papa Leo I (440-461) aliyekuwa ametoa msimamo wake na wa Kanisa la Roma tangu mwaka 449 katika Tomus ad Flavianum, yaani Waraka kwa Flaviano, Patriarki wa Konstantinopoli aliyeuawa na wafuasi wa Eutike. 3
Ingawa msimamo huo wa kati ulikubaliwa na wengi, wengine waliuona ni kinyume cha uamuzi wa Efeso, hivyo walishikilia sana mtazamo hao hata walipodhulumiwa na serikali. Ndiyo asili ya farakano la Misri, Syria, Armenia n.k. linalodumu hata leo.
Mtaguso huo ulitunga pia kanuni mbalimbali, kama vile kwa kumpatia Patriarki wa Konstantinopoli nafasi ya pili kati ya maaskofu wote.
Mtaguso II wa Konstantinopoli (553)
Mtaguso II wa Konstantinopoli uliitishwa na kaisari Justiniani I mwaka 553 kwa lengo la kupatanisha tena na Kanisa Katoliki Wakristo wote wa Misri, Syria n.k. waliojitenga miaka 100 iliyopita kufuatana na Mtaguso wa Kalsedonia.
Kwa ajili hiyo kaisari huyo alifanya yalaaniwe maandishi ya Wanestori watatu (Teodoro wa Mopsuestia, Teodoreto wa Kiro na Iba wa Edesa) yaliyochukiwa sana na Wamisri.
Pia mtaguso mkuu huo ulilaani baadhi ya mafundisho wa Origene.
Walihudhuria maaskofu 168; kati yao 11 walitokea magharibi. Kumbe Papa Vigili (537-555) na maaskofu wengine 12 wa magharibi walikataa kuhudhuria ingawa walikuwepo Konstantinopoli, ila mwaka uliofuata alikubali maamuzi ya mtaguso.
Hatimaye Papa Gregori I (590-604) aliutambua kama mtaguso mkuu kwa sababu haukuharibu kitu. Hivyo Wakristo wengi wanauhesabu kuwa wa tano kati ya mitaguso ya kiekumeni, ingawa lengo halikufikiwa, kwa kuwa Wamisri waliendelea kukataa Mtaguso wa Kalsedonia.
Mtaguso III wa Konstantinopoli (680-681)
Mtaguso III wa Konstantinopoli unahesabiwa na Wakristo wengi kuwa wa sita kati ya Mitaguso ya kiekumeni.
Kaisari Konstantino IV wa Konstantinopoli ndiye aliyeuitisha na kuuendesha kuanzia tarehe 7 Novemba 680 hadi tarehe 16 Septemba 681.
Suala kuu lililosumbua Wakristo wa karne VII lilimhusu Yesu Kristo upande wa utashi. Ulikuwa unaenea mtazamo wa kwamba hakuwa na utashi wa kibinadamu, bali ule wa Kimungu tu.
Lakini wamonaki Sofronio wa Yerusalemu na Maksimo Muungamadini walipinga vikali jaribio hilo la kuleta upatanisho wa Waorthodoksi wa Mashariki (Wamisri n.k.) kwa kumpunguza Yesu katika ubinadamu wake kamili uliosisitizwa na Mtaguso wa Kalsedonia (451).
Vilevile Papa Martin I (649-655), katika mtaguso uliofanyika Laterani, alilaani mtazamo huo, kinyume cha Kaisari na Patriarki wa Konstantinopoli.
Konstantino IV alikubaliana na Papa Agatoni (678-681), na hivyo Mtaguso III wa Konstantinopoli ulilaani rasmi mtazamo wa kwamba Yesu hakuwa na utashi wa kibinadamu.
Mtaguso II wa Nisea (787)
Mtaguso II wa Nisea uliitishwa na malkia Irene wa Bizanti mwaka 787 ili kujadili matumizi ya sanamu katika Ukristo, kutokana na ombi la Papa Adrian I (772-795).
Wakristo wengi wanauhesabu kuwa wa saba kati ya Mitaguso ya kiekumeni. Ni wa mwisho kufanyika wakati wa mababu wa Kanisa.
Mtaguso mkuu huo ulihitajika ili kumaliza mabishano makali kuhusu sanamu za Kikristo yaliyochukua zaidi ya miaka 100 hasa katika Dola la Roma Mashariki yakimalizika mwaka 843 tu.
Chanzo ni uamuzi wa kaisari Leo III wa Konstantinopoli (717-741) wa kuteketeza sanamu zote ili kujilinganisha na Waislamu waliotishia utawala wake.
Patriarki wa Konstantinopoli alilazimika kujiuzulu, lakini uamuzi wa kaisari ulizidi kupingwa hasa na wamonaki na mwanateolojia Yohane wa Damasko. Mapapa wa Roma pia walipinga uamuzi huo.
Sera ya dola ilibadilika aliposhika uongozi Irene kwa niaba ya mtoto wake mdogo Konstantino VI.
Mtaguso ulianza Konstantinopoli mwaka 786, lakini ulipoingiliwa na jeshi waliowaunga mkono maaskofu wengi waliopinga sanamu, Irene aliuhamishia Nisea ambapo vilifanyika vikao 7 kuanzia tarehe 28 Septemba 787. Cha mwisho kilifanyika katika ikulu tarehe 23 Oktoba 787.
Pamoja na maaskofu 300 hivi wa dola hilo, walihudhuria wamonaki wengi. Papa alituma mabalozi wake wawili na barua moja.
Mtaguso ulitofautisha heshima inayokubalika kwa sanamu na ibada isiyovumilika. Hoja kuu ni kwamba sanamu si kitu, ila inamwakilisha yule aliyechorwa ndani yake. Kimsingi sanamu zinakubalika kutokana na umwilisho wa Mwana wa Mungu uliomfanya atwae sura na kuonekana.
Mtaguso ulichukua pia maamuzi mbalimbali ili kurekebisha Kanisa.
Mtaguso IV wa Konstantinopoli (869-870)
Mtaguso IV wa Konstantinopoli ni jina linalotumiwa na Wakristo kwa namna tofauti, kadiri wanavyokubali au kukataa uhalali na uekumeni wa mitaguso fulanifulani.
Kanisa Katoliki linahesabu kuwa Mtaguso Mkuu IV wa Konstantinopoli ule uliofanyika tangu tarehe 5 Oktoba 869 hadi 28 Februari 870.
Uliitishwa na Kaisari Basili I wa Konstantinopoli na Papa Adrian II (867-872), kwa sababu mwisho wa ikonoklastia katika sinodi ya mwaka 843 ulikuwa umeacha athari kubwa katika Kanisa la Mashariki. 4
Patriarki Metodi wa Konstantinopoli (843-847) alijitahidi kutuliza pande zote, lakini hakufaulu.
Alipofariki, malkia Teodora, akitawala kwa niaba ya mtoto Mikaeli III, alilazimisha nafasi yake ishikwe na Ignas I, mmonaki mwenye msimamo mkali, ambaye hatimaye aliondoshwa.
Badala yake alichaguliwa mlei msomi Fosyo ambaye kwa siku chache alipewa daraja na kutawazwa, lakini kufikia Februari 859 lililotea farakano kati ya waliomkubali yeye na waliomkubali Ignas I.
Ndipo Fosyo alipojitahidi kuungwa mkono na Papa Nikolaus I (858-867), ambaye kwanza alimkubali pamoja na pendekezo la Kaisari Mikaeli III la kuitisha mtaguso uliofanyika Konstantinopoli kati ya Aprili na Agosti 861 wakihudhuria maaskofu zaidi ya 300.
Papa hakupendezwa na maamuzi ya mtaguso huo, akashindana na Kaisari kimaandishi kwa sababu za kiutamaduni na za kisiasa pia.
Hapo Fosyo alipata nguvu dhidi ya Papa akaitisha mtaguso uliovunja umoja kati ya Makanisa ya Mashariki na yale ya Magharibi mwaka 867, akithubutu kwa mara ya kwanza kumhukumu Papa kama mzushi na kutaka kumuondoa madarakani.
Kumbe Kaisari mpya alimrudisha Ignas I kuwa Patriarki na pamoja naye akamuomba Papa atume mabalozi kwa mtaguso mwingine wa kufanyika Konstantinopoli.
Mtaguso ulipoanza tarehe 5 Oktoba 869 walikuwepo tu maaskofu wakuu 5 na maaskofu wengine 7, lakini walikuwepo mabalozi wa Mapatriarki wa Antiokia na Yerusalemu (wale wa Aleksandria walifika baadaye).
Waliokuwa upande wa Fosyo walikubaliwa kuhudhuria kuanzia tarehe 7 Oktoba wakamtetea sana dhidi ya msimamo wa Papa, lakini wakashindwa na kutengwa (29 Oktoba).
Baada ya miezi mitatu mtaguso uliendelea tarehe 12 Februari 870, wakiwepo maaskofu 67 walioongezeka tena hadi kufikia 103 siku ya mwisho (28 Februari), lilipotolewa tamko la imani pamoja na kanuni 26 kuhusu teolojia na sheria, bila kutoa mafundisho mapya. Pamoja na idadi yenyewe kutokuwa kubwa sana, ni muhimu kwamba walikuwepo maaskofu wakuu 37 kati ya 40.
Kwa kuwa mtaguso huu haukukubaliwa sana huko Konstantinopoli (hasa baada ya Fosyo kurudia Upatriarki mwaka 877), na pande mbili zilishindwa zaidi na zaidi kuelewana, uliitishwa mtaguso mwingine, ambapo wafuasi wa Fosyo walikuwa ndio wengi.
Baadhi ya Waorthodoksi wanahesabu mtaguso huo mpya (879-880), uliofuta maamuzi dhidi ya Fosyo, kuwa wa kiekumeni na kuukataa ule wa miaka 10 ya nyuma. Lakini wengine hawakubali kuwa wa kiekumeni kwa sababu haukutoa mafundisho ya imani.
Ingawa wajumbe wa Papa Yohane VIII (872-882) walikubali kwanza maamuzi wa mtaguso huo ili kudumisha amani, na labda hata yeye mwenyewe, waandamizi wake waliukataa, na Fosyo mwenyewe aliondoshwa tena mwaka 886.
Mtaguso I wa Laterano (1123)
Mtaguso I wa Laterano unahesabiwa na Kanisa Katoliki mtaguso mkuu wa tisa katika historia yake, wa kwanza kufanyika Magharibi. Ulianza tarehe 18 Machi ukamalizika tarehe 11 Aprili 1123.
Mahali pake ni kwenye Kanisa Kuu la Roma (Italia) katika mtaa wa Laterano, alipokuwa anaishi askofu wake. Hukohuko baadaye ilifanyika mitaguso mingine minne ya Karne za Kati, halafu umuhimu wake ukapungua Papa alipohamia Vatikano.
Mtaguso uliitishwa na Papa Kalisti II (1119-1124) mnamo Desemba 1122, mara baada ya Mapatano ya Worms, ya kwanza kufanyika kati ya Papa na Dola Takatifu la Kirumi, iliyofurahisha sana wanakanisa, hata mwaka huo ulitajwa kuwa mwanzo wa kipindi kipya.
Mapatano hayo yalikomesha desturi ya walei kuteua viongozi wa Kanisa na wa utawa, yakitenganisha shughuli za kiserikali na zile za kidini, na kukubali kwamba mamlaka ya kiroho inatokana na daraja takatifu.
Ili kuthibitisha mapatano hayo, Papa alialika Roma maaskofu wote wa Magharibi. Waliohudhuria kweli walikuwa zaidi ya 900 kati ya maaskofu zaidi ya 300 na maabati 600 hivi). Papa mwenyewe aliendesha vikao.
Hakuna hati za mtaguso, ila matunda yake. Tunachojua ni kwamba Mapatano hayo yalisomwa yakapitishwa rasmi, pamoja na kanuni 22 au 25, ambazo nyingi zilikuwa zimeshapitishwa zamani.
Mtaguso II wa Laterano (1139)
Mtaguso II wa Laterano, uliofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 11 Aprili 1139 chini ya Papa Inosenti II (1130-1143), unahesabiwa na Kanisa Katoliki kuwa mtaguso mkuu wa kumi. Ni wa pili kufanyika Magharibi, kwenye Kanisa kuu la Roma (Italia).
Mtaguso ulihitajika kutokana na farakano lililotokea mwaka 1130 alipofariki Papa Honori II (1124-1130): hapo makardinali waligawanyika kuhusu Mapatano ya Worms, ambayo mwaka 1122 yalikuwa yamekomesha mashindano kuhusu uteuzi wa maaskofu.
Isitoshe, kulikuwa na ushindani kati ya koo mbili za Roma, yaani Frangipane na Pierleoni.
Tarehe 14 Februari 1130, makardinali 16 waliosimama upande wa familia ya Frangipane walimchagua Gregorio Papareschi, aliyejiita Papa Inosenti II. Saa chache baadaye, Pietro Pierleoni alichaguliwa na makardinali wengine na kujiita Anakleti II.
Hatimaye, kwa msaada wa Bernardo wa Clairvaux, Inosenti II alishinda na kukubaliwa na wengi, ingawa hakuweza kuhamia Roma mpaka baada ya mpinzani wake kufa (1138). 5
Mtaguso ulipaswa kurekebisha matokeo ya farakano hilo. Basi, Inosenti II alifungua kikao na kuondoa madarakani maaskofu waliomfuata mpinzani wake.
Halafu papa alikusudia kuendeleza juhudi za urekebisho za Mtaguso I wa Laterano. Hivyo zikapitishwa kanuni 30, ambazo nyingi kati yake zilikuwa za kurudia zile za zamani kuhusu usimoni, mapadri wenye wake n.k.
Mtaguso III wa Laterano (1179)
Mtaguso III wa Laterano uliitishwa na Papa Aleksanda III (1159-1181) ufanyike huko Roma mwaka 1179, kutokana na Amani ya Venezia kati ya Kaisari Federiko I wa Ujerumani na Lega Lombarda ya Italia kaskazini.
Unahesabiwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa kumi na moja. Ulijadili masuala mbalimbali na kuyatungia kanuni. Kati ya maamuzi muhimu zaidi, mmojawapo ulihusu uchaguzi wa Papa, ukidai thuluthi mbili za kura za makardinali wote, bila kutofautisha haki za makundi yao matatu.
Mtaguso IV wa Laterano (1215)
Mtaguso IV wa Laterano unahesabiwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa kumi na mbili.
Uliitishwa na Papa Inosenti III (1198-1216) kama kilele cha kazi yake.
Ulihudhuriwa na maaskofu zaidi ya 400 (wakiwemo mapatriarki wa Kilatini wa Konstantinopoli na Yerusalemu na wawakilishi wa wale wa Antiokia na Aleksandria), na wakuu wa watawa zaidi ya 800, mbali na mabalozi wa watawala wa nchi mbalimbali.
Mada kuu zilikuwa Vita vya msalaba, Mashindano kuhusu uteuzi wa viongozi wa Kanisa, mamlaka ya Papa, mwenendo wa makleri, mashirika ya kitawa, imani (kuhusu ekaristi n.k.) na wajibu wa Wakristo wote kupokea sakramenti ya kitubio walau mara moja kwa mwaka.
Kutokana na wingi na umuhimu wa mafundisho na maamuzi yaliyotolewa, mtaguso huo unahesabiwa kuwa kati ya ile iliyoathiri zaidi Kanisa hadi leo.
Mtaguso I wa Lyon (1245)
Mtaguso I wa Lyon uliitishwa na Papa Inosenti IV (1243-1254) tarehe 24 Juni 1245 akiwa huko Lyon (Ufaransa), alipokimbilia usalama. Waliushiriki karibu viongozi 150 wa Kanisa Katoliki, ambalo linauhesabu kuwa mtaguso mkuu wa kumi na tatu.
Baada ya mashindano makali kati ya mamlaka ya kiroho ya Papa na ile ya kisiasa ya kaisari huko Ulaya, mtaguso huo uliitishwa ili kumhukumu moja kwa moja kaisari Federiko II kuwa Mpinga Kristo.
Mtaguso ulianza tarehe 28 Juni 1245 wakiwepo maaskofu 144, halafu ukawa na vikao viwili vingine tena tarehe 5 Julai na 17 Julai. Hatimaye maaskofu walikuwa 225.
Mwanzoni papa alitangaza matatizo 5 yanayotesa Kanisa:
• kuharibika kwa imani na maadili;
• kushindwa kuikomboa Nchi takatifu (Yerusalemu ulitekwa tena na Waturuki mwaka 1244);
• kudumu kwa farakano la Waorthodoksi;
• kujitokeza hatari ya kuvamiwa na Watartari;
• kupambana na Federiko II.
Maamuzi yalitangazwa tarehe 25 Agosti tu, baada ya papa na wasaidizi wake kurekebisha miswada, yakapokewa na kufafanuliwa na vyuo vikuu. Lakini uamuzi wa kumuondoa madarakani kaisari haukuweza kutekelezwa hata kwa vita.
Mtaguso II wa Lyon (1274)
Mtaguso II wa Lyon unahesabiwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa kumi na nne. Ulikusudiwa hasa kurudisha umoja kamili kati ya Wakatoliki na Waorthodoksi, uliotafutwa katika karne XIII yote.
Mnamo Februari 1274, katika ikulu ya Konstantinopoli, kaisari Mikaeli VIII ilifaulu kufanya maaskofu wengi wakiri ungamo la imani lililodaiwa na Papa Klementi IV (1265-1268).
Ndipo Papa Gregori X (1271-1276) alipoitisha mtaguso huko Lyon, ambao uhudhuriwe na wawakilishi wa Waorthodoksi ili kukamilisha umoja.
Papa Gregori X alifungua mtaguso tarehe 7 Mei 1274 akitangaza tena malengo yake matatu:
• kusaidia Wakristo wa Nchi takatifu,
• kuungana tena na Waorthodoksi,
• kurekebisha maadili ndani ya Kanisa.
Vilifuata vikao viwili tarehe 18 Mei na 4 Juni. Halafu tarehe 24 Juni ulifika na kupokewa kwa shangwe ujumbe kutoka Ugiriki, ukiundwa na maaskofu 2 na katibu wa kaisari.
Tarehe 6 Julai kilifanyika kikao cha nne kwa ajili ya muungano na hatimaye tarehe 16 Julai kile cha mwisho kilichopitisha hati mbalimbali za urekebisho. Kesho yake mtaguso ulifungwa.
Muungano haukuweza kudumu, kwa sababu, alivyoandika Papa Paulo VI (1963-1978) tarehe 19 Oktoba 1974, ulifanyika «bila kulipatia Kanisa la Kigiriki nafasi ya kutokeza kwa hiari mtazamo wake kuhusu jambo hilo. Wakristo wa Kilatini ndio waliotunga hati na matamko kufuatana na mafundisho juu ya Kanisa yaliyofafanuliwa na kupangwa magharibi». 6
Mikaeli VIII alijaribu kulazimisha raia zake wapokee mambo wasiyoyakubali kwa moyo, hata akatumia nguvu kuwadhulumu waliokataa; akilaumiwa na watu wa Roma kwa kushindwa kufanikisha muungano, akaja kutengwa na Kanisa. Alipokufa (1282), mwanae Androniko II aliyemrithi, alifuta maamuzi ya baba yake kwa ajili ya muungano.
Vilevile mipango kwa ajili ya vita vya msalaba haikutekelezwa, na hatimaye (1291) Waturuki waliteka Akri, mji wa mwisho kubaki mikononi mwa Wakristo huko Mashariki ya Kati.
Maamuzi mengine yalihusu utaratibu mpya wa kumchagua Papa kwa lengo la kuzuia uchelewaji uliojitokeza hapo nyuma, na katazo la mashirika mapya ya kitawa.
Mtaguso wa Vienne (1311-1312)
Mtaguso wa Vienne unahesabiwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa kumi na tano.
Mtaguso huu ulifanyika Vienne (Ufaransa) baada ya mashindano kati ya Papa Bonifas VIII (1294-1303) na mfalme wa Ufaransa Filipo IV.
Hatimaye mwaka 1309 mwandamizi wake, Papa Klementi V (1305-1314) alikubali kubaki Avignon (leo nchini Ufaransa), karibu na himaya ya mfalme huyo.
Mapapa walibaki huko hadi mwaka 1377, waliporudi Roma.
Kwa shinikizo la mfalme, Papa alitoa hati Regnans in excelsis (12 Agosti 1308) ili kuitisha mtaguso mkuu huko Vienne tarehe 1 Novemba 1310, kwa lengo la kujadili mada 4:
• suala la Wahekalu;
• vita vya msalaba;
• hali ya imani na Kanisa kwa jumla;
• urekebisho wa Kanisa.
Mtaguso ulichelewa kuanza hadi tarehe 16 Oktoba 1311, walipokuwepo washiriki 170 hivi, ambao kati yao Wafaransa walikuwa zaidi ya thuluthi moja. Wengine walizuiwa na mfalme wa Ufaransa.
Vikao rasmi vikawa vitatu hadi Machi 1312.
Kuhusu Wahekalu, mtaguso uliamua kufuta shirika lao kama alivyopenda mfalme, bila kulifanyia utafiti wala kulitolea hukumu.
Kuhusu Vita vya Msalaba, uliamua kuvianza upya na kwa ajili hiyo kutoza zaka kwa miaka sita, lakini mfalme alijitwalia hizo pesa bila kutekeleza ahadi yake ya kuongoza vita hivyo.
Kuhusu imani, ulijadili baadhi ya mafundisho hasa ya makundi kadhaa ya watawa, lakini uamuzi ulichukuliwa baadaye tu.
Kuhusu urekebisho, ulidai haki za Kanisa ziheshimiwe na serikali za nchi. Pia ulijadili kirefu mahusiano ya ndani, hasa kati ya maaskofu, maparoko na watawa.
Mtaguso wa Konstanz (1414-1418)
Mtaguso wa Konstanz (Ujerumani) unahesabiwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa kumi na sita. Uliitishwa na antipapa Yohane XXIII kwa ombi la kaisari Sigismund wa Ujerumani ukathibitishwa na Papa Gregori XII (1406-1415).
Lengo kuu lilikuwa kumaliza Farakano la Magharibi lililofikia hatua ya kuona maaskofu watatu kujidai Papa kwa wakati mmoja. Malengo mengine yalikuwa kung’oa uzushi na kurekebisha Kanisa “katika kichwa na viungo vyake”.
Hatimaye Papa Gregori XII alikubali kujiuzulu, wapinzani wake wawili waliondolewa, na Papa Martin V akachaguliwa.
Ulikuwa mtaguso muhimu kwa wingi wa waliohudhuria (makardinali 29, maaskofu 186, maabati zaidi ya 100 na wataalamu 300 hivi), muda (vikao 55) na mafanikio, ingawa majaribio yake ya mapinduzi yalishindikana, hasa ulipodai kuwa na mamlaka ya juu kuliko Papa.
Kati ya maamuzi mengine kuna hukumu dhidi ya John Wyclif na Jan Hus kama wazushi.
Mtaguso wa Firenze (1431-1445)
Mtaguso wa Firenze uliitishwa na Papa Martin V (1417-1431) mwaka wa mwisho wa uongozi wake ili kutekeleza shingo upande agizo la Mtaguso wa Konstanz la kwamba mtaguso ufanyike mara kwa mara.
Mtaguso ulianza Basel (Uswisi) chini ya Papa Eugenio IV (1431-1447), ukiwa na maaskofu wachache kulingana na mapadri na walei wenye haki ya kupiga kura.
Ingawa mtaguso ulifaulu kupatanisha wafuasi wa Hus na Kanisa, na kutoa sheria kadhaa za urekebisho kwa kibali cha Papa, baadaye ulianza kumshambulia yeye pamoja na makardinali, ukionyesha wazi wengi waliuona una mamlaka ya juu kuliko Papa, kinyume cha mapokeo.
Hapo Eugenio IV aliuvunja halafu akauhamishia Ferrara (Italia), ulipokutanika tarehe 8-1-1438, bila kujali upinzani wa wale ambao walibaki Basel na kumchagua antipapa wa mwisho, Felix V.
Huko Italia ulifika ujumbe mkubwa kutoka Konstantinopoli kwa ajili ya kurudisha umoja kati ya Kanisa Katoliki na Waorthodoksi. Kati ya wajumbe 700 kulikuwa na kaisari na patriarki wa Konstantinopoli, walioogopa Waturuki watateka mji wao (kama ilivyotokea kweli tarehe 29 Mei 1453); hivyo walihitaji msaada wa Wakristo wenzao wa magharibi.
Ferrara iliachwa kutokana na uhaba wa majengo na hofu ya tauni. 7
Mwaka 1439 mtaguso ulihamia Firenze ukafikia makubaliano ya kurudisha umoja (6-7-1439), ingawa uamuzi ukashindwa kutekelezwa kwa kiasi kikubwa kutokana na upinzani wa waumini wa Konstantinopoli.
Vilevile tarehe 22-11-1439 yalifikiwa makubaliano na Waarmenia na tarehe 4-2-1440 yale na Wamisri.
Hatimaye tarehe 24-9-1443 mtaguso ulihamia Roma kwenye Laterano. Huko yalifikiwa makubaliano ya kurudisha umoja na Wasiria kadhaa (30-4-1444) na Wakaldayo na Wamaroni wa Kupro (7-8-1445).
Hakuna hati kuhusu mwisho wa mtaguso. Lakini waliobaki Basel na kujitenga na Papa, kufikia tarehe 19-4-1449 walimkubali Nikolaus V na siku sita baadaye walifunga mkutano wao.
Mtaguso huo ulichochea Wakristo wa magharibi kutamani mawasiliano na wenzao wa Ethiopia na India, jambo lililowafanya waanze zile safari za mbali kupitia baharini zilizowafikisha Afrika Kusini na Mashariki, China na Amerika.
Mtaguso V wa Laterano (1512-1517)
Mtaguso V wa Laterano ulifanyika kuanzia mwaka 1512 hadi 1517 huko Roma. Kanisa Katoliki linauhesabu kama mtaguso mkuu wa kumi na nane.
Uliitishwa na Papa Julius II (1503-1513) ambaye alianza kuusimamia tarehe 3 Mei 1512. Baada ya kifo chake, uliendelezwa na Papa Leo X (1513-1521) hadi kikao cha 12 na cha mwisho kilichofanyika tarehe 16 Machi 1517.
Ulihudhuriwa na maaskofu 100 hivi, wengi wao wakitokea Italia. Kutofika kwa wajumbe kutoka nchi nyingine, pamoja na wengi kukosa nia ya kujirekebisha, kulichangia kufanya utekelezaji wa maamuzi ya mtaguso ushindikane.
Maamuzi hayo yalitolewa kwa hati za Papa. Mengine yanahusu mafundisho ya imani, mengine maagizo ya urekebisho wa Kanisa.
Kabla yake kilifanyika “Kitaguso” cha Pisa: kwa kuwa Papa Julius II alikuwa hatekelezi kiapo chake cha kuitisha mtaguso kwa ajili ya urekebisho, baadhi ya makardinali, wakihimizwa na watawala wa Ujerumani na Ufaransa, waliuitisha huko Pisa (Italia) kuanzia tarehe 1 Septemba 1511. Walikusanyika wachache tarehe 1 Oktoba, halafu katika kikao cha nane walimsimamisha Papa wakahamia Lyon (Ufaransa).
Papa aliitikia “kitaguso” hicho kwa hati ya tarehe 18 Julai 1511, ambayo pamoja na kukipinga na kujitetea aliitisha mtaguso mkuu ukusanyike tarehe 19 Aprili 1512 huko Laterano.
Vita vilichelewesha mwanzo wa mtaguso wenyewe hadi tarehe 3 Mei 1512, walipokusanyika katika basilika la Laterano makardinali 15, mapatriarki 2, maaskofu wakuu 10, maaskofu 56, maabati na wakuu wa mashirika ya kitawa wachache pamoja na mabalozi wa nchi 3. Mwisho walikuwepo makardinali 23 na maaskofu 122.
Upande wa matokeo, utekelezaji wa maagizo ya mtaguso ulikuwa mdogo sana, la sivyo pengine Matengenezo ya Kiprotestanti yasingetokea. Ukweli ni kwamba Martin Luther aliyaanzisha miezi sita tu baada ya mtaguso kwisha.
Mtaguso wa Trento (1545-1563)
Mtaguso wa Trento (uliofanyika kwa kwikwi kuanzia mwaka 1545 hadi 1563), unahesabiwa na Kanisa Katoliki kuwa mtaguso mkuu wa kumi na tisa.
Mtaguso huo, uliochukua muda mrefu kuliko yote ya historia, ulieneza urekebisho wa Kanisa na kuchukua msimamo kuhusu mafundisho ya Waprotestanti waliojitokeza katika hiyo karne XVI.
Mtu wa kwanza kulilia mtaguso ambao uamue kati yake na papa alikuwa Martin Luther (1517): huko Ujerumani ombi lake liliungwa mkono na wengi, pamoja na kaisari Karolo V aliyeuona kuwa njia ya kurekebisha Kanisa lakini pia ya kujiimarisha kimamlaka. Ndiyo sababu kuu iliyomfanya Papa Klementi VII (1523-1534), aliyesimama upande wa Ufaransa, kukataa kabisa kuuitisha.
Wazo hilo lilipata nguvu tena chini ya mwandamizi wake, Papa Paulo III (1534-1549), ambaye mwaka 1536 aliitia kwanza Mantova halafu Vicenza maaskofu na maabati wote, pamoja na wafalme wadogo wengi wa Dola takatifu la Kijerumani.
Baada ya juhudi mbalimbali kushindikana, mwaka 1542 uamuzi ulifikiwa wa kuitisha mtaguso huko Trento kwa sababu ni mji wa Italia lakini ulikuwa ndani ya mipaka ya dola hilo. Hatimaye (Novemba 1544) papa aliweza kutoa hati ya kuitisha mtaguso inayoitwa Laetare Jerusalem.
Mtaguso ulifunguliwa rasmi tarehe 13 Desemba 1545 katika kanisa kuu la Mt. Vigilio.
Mwanzoni mtaguso ulikuwa na maaskofu wachache, karibu wote kutoka Italia, ukatawaliwa na wajumbe wa papa. Kati ya makardinali wapya (Contarini, Sadoleto, Carafa, Fisher na huyo Pole) wengi walipenda urekebisho.
Zilijadiliwa na kupitishwa hasa dogma dhidi ya mafundisho ya Waprotestanti, kama vile kuhusu utakaso na wokovu. Pamoja na kupitisha tafsiri rasmi ya Biblia katika Kilatini iliyo maarufu kwa jina la Vulgata, kati ya maamuzi muhimu zaidi upo ule wa kudai maaskofu waishi katika majimbo yao ili kufanya uchungaji uliowapasa.
Baada ya mtaguso kuhamishiwa Bologna, Papa Paulo III aliusimamisha mnamo Septemba 1549.
Papa Julius III (1550-1555) aliuitisha tena kuanzia tarehe 1 Mei 1551 na zikatolewa hati juu ya sakramenti za Ekaristi, Kitubio na Mpako wa wagonjwa. Polepole waliohudhuria waliongozeka, 8
wakiwemo Waprotestanti wengi pia, wakidai wanateolojia wao wawe na haki ya kupiga kura na hati zilizokwishatolewa zifutwe. Ndipo ilipoonekana wazi kwamba tofauti katika imani ni kubwa mno.
Majeshi ya Kiprotestanti yalipokaribia Trento, Papa alikubali kusimamisha tena mtaguso tarehe 28 Aprili 1552.
Sehemu ya mwisho ya mtaguso baada ya kuitishwa ilichelewa kuanza hadi tarehe 18 Januari 1562, tena ilikabili matatizo mengi, lakini iliokolewa na kutawaliwa na askofu wa Milano Karolo Borromeo, mpwa wa Papa Pius IV (1559-1565) aliyemalizia haraka mtaguso wakiwemo wajumbe 255.
Katika sehemu hiyo yalitolewa mafundisho rasmi kuhusu Misa, Daraja takatifu na Ndoa, Toharani, sala kwa watakatifu, heshima kwa masalia na rehema. Pia Kanisa la Roma lilikubaliwa kama mama na mwalimu wa makanisa yote. Maaskofu wote walitakiwa kuahidia utiifu kwa Papa, ambaye peke yake ana haki ya kuitisha mtaguso mkuu. Kwa msingi huo, mtaguso ulimuachia Papa kuthibitisha maamuzi yote, naye alifanya hivyo bila kujali upinzani wa maofisa wake huko Roma.
Isitoshe, mwishoni, maamuzi mbalimbali yaliachwa mikononi mwa Papa na ofisi zake, yakachukuliwa miaka iliyofuata; kati yake, urekebisho wa Breviari na Misale, kwa kusawazisha liturujia za majimbo ya magharibi (isipokuwa chache, kama ya Milano na Lyon) kulingana na mapokeo ya Roma. Halafu ikatolewa Katekisimu ya Trento na Orodha ya vitabu vilivyokatazwa (Index librorum prohibitorum).
Mtaguso I wa Vatikano (1869-1870)
Mtaguso I wa Vatikano unatazamwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa ishirini katika historia yake.
Uliitishwa rasmi na Papa Pius IX (1846-1878) mnamo 29 Juni 1867 na vikao vyake viliendelea katika Basilika la Mt. Petro huko Vatikano mjini Roma kuanzia tarehe 8 Desemba 1869 hadi vilipokatika mnamo 1870, kutokana na jeshi la Italia kuteka Roma tarehe 20 Septemba.
Walishiriki maaskofu na mapadri 774 (kati ya 1050 wenye haki ya kuhudhuria), ambao kwa mara ya kwanza walitokea mabara yote. Pia ilikuwa mara ya kwanza ya kutokuwepo wawakilishi wa serikali. Kumbe wajumbe wa Waorthodoksi na wa Waprotestanti walialikwa pia, lakini hawakufika.
Tarehe 24 Aprili 1870, baada ya majadiliano mengi, ilipitishwa hati Dei Filius juu ya Mungu, ufunuo, imani, na uhusiano kati ya imani na akili.
Ingawa lengo halikuwa hilo, tokeo kuu la kazi ya mtaguso huo ni tangazo la dogma ya Papa kuwa na karama ya kutokosea katika mafundisho ya imani na maadili anayoyatoa ili yadumu moja kwa moja pale anapotimiza masharti fulani (kwa kifupi: akisema “ex cathedra”, yaani “kutoka ukulu).
Dogma hiyo iliimarisha mamlaka ya Papa na umoja wa Kanisa dhidi ya maelekeo ya kitaifa ambayo yalitawala karne zilizotangulia yakisababisha matatizo mengi.
Mtaguso II wa Vatikano (1962-1965)
Malengo ya Mtaguso II wa Vatikano
Muda mfupi baada ya kuchaguliwa Papa, mwenye heri Yohane XXIII alitangaza uamuzi wake wa kuitisha mtaguso mkuu akiamini kwamba utaweza kuandaa na kusababisha ustawi mpya wa maisha ya Kanisa. Lengo kuu la mtaguso lilikuwa kuliamsha Kanisa likumbuke wito wake na kwa kujifanya upya kwa ndani lipate msukumo mpya wa kimisionari ili kuwatangazia watu wote ujumbe wa milele wa wokovu, amani na umoja.
Tangazo hilo lilitolewa tarehe 25-1-1959. Baada ya maandalizi, Mtaguso II wa Vatikano ulifunguliwa tarehe 11-10-1962. Vikao vinne vikafanyika mpaka ulipofungwa tarehe 8-12-1965. Kila kikao kilianza Oktoba na kumalizika Desemba ya miaka hiyo.
Kwa kuwa Yohane XXIII alifariki tarehe 2-6-1963, vikao vitatu vya mwisho viliongozwa na mwandamizi wake, Paulo VI, na hati zote kumi na sita zikatolewa chini yake pia kwa kupigiwa kura ya ndiyo karibu kwa kauli moja. Maaskofu na wakuu wa mashirika kadhaa wenye haki ya kupiga kura walikuwa kama elfu tatu, wakiwakilisha karibu Kanisa lote duniani, isipokuwa nchi zile zenye kuwadhulumu Wakristo.
Read and Write Comments
Recent Comments