Wosia mzuri wa baba kwa mwanae

Mwanangu, mimi baba yako nimeishi miaka mingi kuliko wewe ndio maana unaniita baba. Ni kweli sijasoma kama wewe ulivyosoma Ila mambo niliyokutana nayo tangu nimezaliwa ni elimu tosha ambayo wewe huna. Sasa nataka nikupe Elimu hiyo ili ukijumlisha na elimu yako ya darasani ujue namna nzuri ya kuishi katika dunia hii iliyojaa mishangazo mingi.

Maisha ni jumla ya mambo yote unayoyatenda kila siku. Namaanisha kila unalolifanya Leo linaathiri maisha yako ya kesho kwa hali chanya au hali hasi. Na kama ni hali hasi ni kwa ukubwa gani halikadharika kama ni hali chanya ni kwa kiwango gani. Mwanangu kila jambo unalolifanya Leo huamua ni mlango gani Unaweza ingia Kesho lakini pia mlango upi huwezi ingia Kesho. Ndio maana ni muhimu kuijua Kesho yako ukiwa Leo.

Mwanangu ili ufanikiwe ni lazima ujue kuishi na watu vizuri. Na mimi sikushauri kabisa kwamba uwe na marafiki wengi. Kuwa na marafiki wengi ni moja ya eneo unaweza jitengenezea mtego mbaya wa kukuangamiza kesho yako. Mwenye hekima mmoja aliwahi kusema ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe. Mwanangu kwa kusema hivyo simaanishi uwe na maadui,hapana. Ila marafiki zako watakusaidia mlango unaotaka kuingia Kesho uingie kwa urahisi au kwa ugumu au usiingie kabisa na wakati mwingine Unaweza kuingia na wakahusika kukutoa kwa aibu kubwa. Ndio maana ni muhimu Kuwa na marafiki ila Kuwa nao wachache chagua kwa makini mno. Sio lazima kila akufaaye kwa dhiki ndiye awe rafiki. Kuna watu wanakufaa kwa dhiki Leo ila Kesho wakutumikishe Kuwa makini sana.

Mwanangu, kuwa makini sana na mahusiano yako ya kimapenzi maana yanagusa hisia zako na mtu unayehusiana naye moja kwa moja. Hivyo basi kuwa makini maana mahusiano hayo yanaweza kukufanya Kesho ukamkosesha raha utakayekuwa naye kama sio huyo uliyenaye leo ndie ukajaaliwa Kuwa naye Kesho. Mwanangu, Unaweza kuniona mshamba sababu ulimwengu wenu unaonekana kama haujali sana haya mambo ila tafadhari zingatia utakapofika Kesho utaelewa sana hiki ninachokuambia.

Mwanangu, jichunge sana na mambo unayoyafanya Leo na uwe muungwana na kupenda haki. Tamaa isikupeleke ukafanya mambo mabaya ambayo yatakulazimisha kutunza siri moyoni mwako hata kama utafika ile Kesho yako. Jiepushe kabisa na mambo mabaya ya siri ya nafsi. Hakuna utumwa mbaya kama utumwa ndani ya nafsi yako mwenyewe maana kila ukikumbuka nafsi itakusuta na kukukosesha raha ya kweli. Hivyo kubali na kuridhika na ulivyo kama huwezi kujiongeza kwa njia halali na za haki. Ni heri uwe masikini mwenye uhuru ndani kuliko uwe tajiri na maarufu mwenye siri mbaya ndani ya Moyo wako. Mwanangu tafadhari uwe makini sana.

Mwanangu, siwezi sahau kukwambia kuhusu Mungu. Maisha ya uchaji wa Mungu yatakuepusha na mengi. Hapa naomba unielewe kwamba usijifanye unamcha Mungu bali mche Mungu. Sio kwasababu unashida ya kufanikiwa ndio umche Mungu, hapana! Bali umche Mungu sababu ni Mungu na yeye ndiye anaijua Kesho yako vizuri kuliko wewe mwenyewe. Ukimshirikisha mambo yako na ukawa mwaminifu kwake hakika hatakuacha kamwe.

Mwanangu, usiku umeenda nenda kalale sasa ila usije ukapenda na kutamani waovu kwa uovu wao na wakakushawishi ujiunge nao. Tafadhari usikubali.

#Kizazi Ganzi#

JIFUNZE KUJIFUNZA

Mwl Makwaya
Kuwa Ni Kufanya.

I would like to hear from you, write your comment!.

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Shopping Cart
Explore
Books
0
Comments
Account