Maswali na majibu kuhusu Mpako wa wagonjwa au Mpako wa Mwisho

Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu gani?
Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu alijua udhaifu wa binadamu hauishi mara anapopokea uzima wa Mungu kwa sakramenti tatu za kuingizwa katika Ukristo. Hivyo alipanga kusaidia mpaka mwisho wa dunia waamini wake watakaopatwa na dhambi na ugonjwa, kama alivyowasaidia wengi aliokutana nao katika maisha yake.
β€œYesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, β€˜Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako’… β€˜Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi’ – amwambia yule mwenye kupooza – β€˜Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako’. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii” (Math 9:2,6-8).


Mpako wa Wagonjwa ulianzishwa na nani?
Mpako wa Wagonjwa ulianzishwa na Yesu, kama sakramenti zote. Maandiko yanasimulia huruma yake iliyomfanya awaponye wengi kwa namna mbalimbali na kuwapa Mitume uwezo wa kufanya vilevile kwa β€œkupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina” (Math 10:1). Nao
β€œwakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza” (Mk 6:13).
β€œMtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa, nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa” (Yak 5:14-15).


Mafuta ya mpako wa wagonjwa yanamaanisha nini?
Mafuta ya wagonjwa yanamaanisha lengo la kuwaponya na kuwarudishia nguvu na uzuri.
Kama kawaida, maneno yanaweka wazi zaidi kuwa lengo si kuponya mwili tu, bali hasa roho kwa kuitia msamaha na faraja katika mateso ambayo huenda yakaendelea. Kwa kuwa Mungu haponyi mwili kila mara, isipokuwa kwa faida na wokovu wa mgonjwa na wa wengine. Kama ndiyo mapenzi yake, kila mmoja ajifunze kufaidika vilevile na ugonjwa:
β€œMakusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, β€˜Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu’. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu” (2Kor 12:7-9).
β€œSasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu, tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake” (Kol 1:24).


Sakramenti ya Mpako wa wagonjwa ni nini?
Ni Sakramenti ambayo Padri humuombea neema ya Mungu na kumpaka Mafuta Matakatifu mgonjwa aliye katika hatari ya kifo kwa ajili ya neema ya roho na mwili. (Yak 5:14-15, Mk 6:13)
Sakramenti ya Mpako wa wagonjwa ilianza lini? Je, wakati wa Yesu kulikuwa na sakramenti hii?
Sakramenti ya mpako wa wagonjwa ilikuwepo tangu wakati Yesu akiwa hai. Tunaweza kuiona Kwenye Biblia tunaposoma Yesu alivyowatuma wanafunzi wake waliwapaka watu mafuta. “Waliwatoa pepo wengi Wabaya, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta wakawaponya. (Marko 6:13)


Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa inaadhimishwaje?
Inaadhimishwa kwa Padre kumuombea mgonjwa, kumuwekea mikono na kumpaka mafuta katika panda la uso na viganja vya mikono; kwa kutumia mafuta aliyobariki Askofu siku ya Alhamisi kuu.


Sakramenti ya Mpako Wa Wagonjwa inamanufaa gani rohoni mwa mtu?
Manufaa ya Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa ni
1. Nguvu ya kuvumilia mateso na kuyaunganisha na mateso ya Yesu Kristo
2. Maondoleo ya dhambi zote asizoweza kuziungama
3. Nafuu ya mwili, hata uzima ikifaa kwa wokovu wa roho yake
4. Neema ya kujiandaa kuaga dunia na kuingia katika uzima wa milele


Ni nani anayetoa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa?
Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa hutolewa na kuhani tuu yaani Askofu au Padri


Padri aitwe kwa mgonjwa lini?
Padri aitwe kwa mgonjwa mara inapoonekana Hatari ya Kifo na kamwe isisubiriwe mpaka mgonjwa apoteze fahamu.


Ni nani aweza kupokea Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa?
Ni kila Mkatoliki aliyefikia umri wa kufikiri na aliye katika hatari ya kufa kwa ugonjwa au uzee aweza kupokea Sakramenti hii.


Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa yaweza kupokelewa mara ngapi?
Sakramenti hii yaweza kupokelewa mara nyingi ugonjwa ukizidi au akipatwa na ugonjwa mwingine mkubwa


Alama wazi ya Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa ni nini?
Alama wazi ya Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa ni tendo la kupaka Mafuta Matakatifu wagonjwa na kutamka maneno
“Kwa mpako huu Mtakatifu na kwa pendo lake kuu, Bwana Akujaze na nguvu ya Roho Mtakatifu. Amina Akuondoe katika enzi ya dhambi, akuweke huru. Kwa wema wake akupe nafuu katika mateso yako na kukujalia neema. Amina”


Kama padri hatapatika na mgonjwa afanye nini?
Kama padri hatapatikana mgonjwa aweke nia ya kuungama na afanye majuto kamili


Komunyo pamba ndio nini?
Komunyo pamba ndio Ekaristi inayopokelewa na wale wanaokaribia kuaga maisha ya duniani na wanaojiandaa kuvukia uzima wa milele
Melkisedeck Leon Shine

Editor: Melkisedeck Leon Shine, Enjoyed? Drop your Comment Below. OR Chat Live here. Download My Books in PDF Format here. More: Legal Guidelines | About Me | Contact Me | LinkedIn | TikTok | WhatsApp

Read and Write Comments
Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments