Dondoo za Urembo na Mitindo

Namna nzuri ya kuhudumia nywele zako za asili kirahisi

Kwa wale ambao tuna nywele asilia (natural hair), tayari tunafahamu changamoto kadhaa tunazokumbana nazo. Kwa wale mnaofikiria kuanza kuwa na nywele asilia, karibuni sana tuendelee kujuzana namna ya kutunza nywele zetu kama tulivyopewa na Mungu.

Katika mada ya leo, nitakwenda kuzungumzia vitu vya kuzingatia ili kuikuza nywele yako asilia kwa haraka zaidi. Je,unazifahamu nywele zako vizuri?Una nywele za aina gani? Zina tabia gani? Zinataka nini?

Zifuatazo ndizo njia ya kuzihudumia nywele zako;

1. Kuzikubali kama zilivyo na kuzipenda.

Utasikia ..hiki kipilipili changu ni steelwire ya kimataifa, ..hakitikisiki hata upepo wa dunia yote ungevumia pande hizi. Mwingine oh..nywele zangu kama miti ya mibuyu kichwani…hazishikiki.T atizo ni kwamba hamjafahamiana vizuri yani wewe na nywele zako. Hata mimi niligombana nazo sana huko nyuma kabla ya kuzielewa vizuri. Jenga mahusiano mazuri tu na nywele zako,zielewe,ukifikia hapo utaanza kuzipatia hata hazitakusumbua.

2. Usafi wa ngozi ya nywele na nywele zenyewe.

Nywele zenye afya huanzia kwenye ngozi safi ya nywele.Nafahamu unataka nywele zako zisidumae kwa hiyo zioshe vizuri.Wakati uliopita nilizungumzia kuziosha kwa product zilizo rafiki( ‘friendly’) .Ngozi safi ya nywele itasababisha nywele kupata njia ya kujitokeza nje kwa urahisi.Unapoziacha chafu,ule uchafu unaziba matundu ya nywele zako na kuzuia njia,kama ambavyo matundu ya uso yakiziba unapata machunusi maana uchafu unajaa basi kwa nywele hazitakua vizuri.

3. Linda unyevu wa nywele zako

Kila mtu akisikia kiu hunywa maji.Nywele zako zinahitaji kulindwa zisisikie kiu.Unapoziosha,yale mafuta asilia ya kuzilinda huondoka na uchafu.Nywele inabaki ikiwa na udhaifu fulani maana haiwezi hata kushikilia hayo maji yaliyopo vizuri,na zikikauka zinakua kavu sana.Ni vizuri kabla hazijakauka vizuri,ukazi-’condition’.Kwa nywele ambazo ni nyepesi na chache,pia kuna product za kuzisaidia ziweze kutunza vizuri unyevu na hivyo kuwa na afya nzuri.

4. Zifahamu nywele zako

Yani hapa ndo shule ilipolalia kabisaa maana ukizijua tu basi utazihudumia kwa usahihi. Unatakiwa kuangalia namna gani nywele zako zinanyonya unyevu .Unajuaje?

Chukua kikombe,kijaze maji safi.Ukipata glass itakuwa vizuri zaidi.

Chomoa unywele mmoja kichwani,hakikisha unatoka na kale kamzizi kake keupe keupe hivi.

Tumbukiza unywele wako kwenye glass yako ya maji hakikisha imeingia yote.Kama ikizama hapo hapo na hainyanyuki tena,basi nywele zako zinanyonya unyevu kwa haraka kabisa.Kama inachukua muda kuzama,au haizami kabisa,nywele zako zinanyonya unyevu taratibu au zinanyonya kwa shida.

(Wala usihofu,zipo namna ya kuzifanya zinyonye unyevu kwa haraka,tutajuzana.)Ni kwamba ‘cuticle’ zake zimefunga haswa,ndio maana unyevu au maji haviingii kwa haraka.

Kwa hiyo ukifanya ‘deep conditioner’ kwa kutumia joto kama la drier lakini uwe moto mdogo sana au ufanye ‘hot oil treatment’ itakusaidia ‘cuticle’kufunguka na unyevu kupita.

Mbadala,unaweza baada ya kuosha suuza na maji ya vuguvugu halafu weka mafuta ya kimiminika.Inasaidia sana.

Mimi nina aina gani?..Nina nywele zinazonyonya unyevu haraka.

5. Mafuta ya Kupaka kichwani.

Ni ya muhimu mnoo!.Nimefanya utafiti wa kina nimeona mafuta ya nazi yanaweka afya nzuri kwa nywele aina nyingi hivyo na mimi nikaanza kuyatumia. Kwangu mimi,mafuta ya nazi ya kutengeneza mwenyewe yamenikubali sana. Japo huwa nanunua pia mafuta kama ya olive(extra virgin) na ya tea tree.

6. Kuzichambua vizuri kabla ya kuchana.

Uwe mkarimu na mwenye subira kwa nywele zako. Mimi zikijifunga huwa nazichambua kwa mikono taratibu wakati mwingine nazilowesha na maji kwa mbali halafu nachana kwa chanuo lenye mapana sio ambalo reli zake zimebanana. sio kitana. Chanuo kubwa(wide toothed comb).

7. Usizisumbue mara kwa mara na usuke mitindo ya kuzitunza zikue.

Kama unataka zikue haraka, usizisumbue sana. Unaweza ukasuka mitindo mizuri tu ukakaa nazo wiki nzima au kadri zitakavyodumu. Au upunguze kuzichana mara kwa mara lakini utafute siku kama wikiendi ukae uzichambue taratibu na vidole kuondoa mafundo. Kuchana mara kwa mara zinapukutika,zinaanguka. Zitakua lakini sio kwa kasi ya kama ukizisuka ukaziacha kwa muda.

8. Punguza matumizi ya vitu vya moto kwenye nywele zako kama pasi ya nywele na vingine vya hivyo.

Mimi dryer la nywele situmii zaidi ya mara mbili kwa mwezi. Mara nyingi naziacha zikauke na hewa hata kama nimezifunga rollers natoa kesho baada ya masaa 24

Mavazi ya Ofisini kwa Wadada

Wengi wetu tunashindwa kutofautisha mavazi ya sehemu husika mfano Ofisini, michezoni, na yale ya usiku na sehemu nyinginezo leo nitagusia vazi la ofisini kwa akina dada.

Unapotaka kuvaa vazi ,lazima uangalie vazi unalolivaa mda gani na mahala unapokwenda,siyo vazi la kutokea usiku au la kimichezo unalivaa ofisini,utakuwa kichekesho mbele za watu hata kwa wafanyakazi wenzio.

Mavazi ya kiofisi yanaeleweka lakini hasa kwa mwanamke basi vaa sketi fupi au ndefu na blauzi ya heshima iliyofunika kitovu chako, au suti ya heshima na koti na hata suruali ambayo haijakubana sana inafaa sana kwa ofisi.

Kama utapendelea kuvaa gauni basi angalia mkao wa hilo gauni ukoje maana mara nyingi gauni huwa halipendezi kuwa vazi la ofisini bali vazi la jioni.

Jinsi ya kuondoa weusi kwenye magoti na viwiko vya mikono

Ngozi nyeusi katika magoti na nyuma ya mikono hutokana na mkusanyiko wa cells zilizokufa, na hata unavyoweka pressure kwenye magoti na vipepsi vya mikono yako. Kama ukiwa unaweka mikono kwenye meza ukiwa kazini, ule msuguano unafanya ngozi iwe nyeusi.

Kama una magoti myeusi na nyuma ya mikono pia ni peiusi, tumia hizi njia asili kuweza kuondoa weusi huo:

Tumia Aloe Vera Juice.

Juice ya Aloe Vera inasaidia kuondoa weusi, all you have to do ni kupaka juice hiyo kwenye sehemu yenye weusi na uache kwa nusu saa kisha nawa na upake moisturizer. Rudia kufanya hivi mara mbili kila siku.

Tumia Binzari Manjano, Asali na Maziwa.

Changanya vyote hivi utapata mchanganiko mzito, paka kwenye magoti na kwenye mikono yako palipo na weusi. Kaa nayo kwa dakika 30, nawa na paka moisturizer. Rudia hii kila siku kwa wiki 3-4, utapata matokeo mazuri.

Tumia Ndimu.

Chukua pamba na uitumie kupaka juice ya ndimu katika sehemu zenye weusi. Au unaweza kuikata tu ndimu na kuipaka directly kwenye sehemu zenye weusi. Kaa nayo kwa lisaa 1 kisha nawa. Rudia hivi kila siku hadi weusi utakapopotea.

Tumia Olive Oil na Sukari.

Changanya vizuri, hii itakuwa kama exfoliation/scrub kwa ajili ya magoti na mikono. Paka katika hizo sehemu zenye weusi kisha kuwa kama una-massage polepole. nawa kwa maji ya uvuguvugu kisha paka moisturizer.

Dawa za nywele zinazosababisha uvimbe kwenye Kizazi kwa wanawake

Dawa za kulainisha nywele (relaxer) zimekuwa zinapendwa na wanawake wengi wa Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele na kumfanya apendeze na awe wa kuvutia.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo zinasababisha uvimbe kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa hizo ambazo huingia mwilini kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupaka.

Daktari wa Manispaa ya Ilala, Laurent Chipata alifanya utafiti na kubaini kuwa dawa za nywele na vipodozi zina kemikali ambazo husababisha uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi kikubwa na kusababisha uvimbe kwenye kizazi uitwao fibroids au leimyoma.

“Kemikali hizi hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine hata kwa harufu tu, husababisha kuzalishwa kwa wingi wa vichocheo aina ya estrogen ambavyo huchangia kuota kwa uvimbe wa fibroids,” anasema.

Dk Chipata anasema kukua kwa uvimbe kwenye kizazi hutokea katika kipindi ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma hedhi.

Utafiti wa Dk Chipata ulifanywa nchini na kujumuisha wanawake wa kada tofauti tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia na ukubwa wa tatizo hili ulibainika.

“Zipo kemikali tofauti tofauti zinazosababisha uvinbe kwenye kizazi, zipo za kwenye dawa za kilimo kama DDT na za kwenye mafuta ya ngozi kama vile mercury na hydroquionone,” anasema.

Dk Chipata anasema madhara yanayopatikana katika kemikali za vipodozi ni makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha saratani au kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya zebaki (mercury).

“Dawa za nywele zina madhara si lazima zipenye kwenye ngozi baada ya mtu kupata jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya zenyewe kwenye ngozi kutokana na mfumo wa ngozi,” anasema.

Anashauri kuwa ni vyema watu wakasoma kipodozi kimetengenezwa kwa nini kabla ya kukitumia na kuongeza kuwa ni salama zaidi kubaki na ngozi au nywele halisi badala ya kujibadilisha.

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza vipodozi vyenye kemikali kama biothionol, hexachlorophene, mercury, vinyl chloride, zirconium na bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform.

Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dk Lauren Wise na wenzake nchini Marekani na kuchapishwa kwenye jarida la afya la nchini Marekani ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya estrogen ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au vivimbe hivi hujulikana kama fibroids au myoma.

Dk Wise anasema aliwafanyia uchunguzi wanawake wanaotumia dawa za kulainisha nywele na kuangali umri walioanza kutumia dawa hizo, mara ngapi, waliungua kiasi gani na walikaa na dawa hizo kichwani kwa kipindi gani.

Aliwafuatilia wanawake 23,580 wanaotumia dawa za kulainisha nywele na baada ya kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146 waligundulika kuwa na uvimbe kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi na wengine kufanyiwa upasuaji.

Kwa nini relaxer ni hatari kwa wanawake?
Dk Wise anasema mchanganyiko ulio kenye dawa za nywele hasa zilizoandikwa “Lye Relaxer” ni sodium hydroxide wakati makopo ya dawa yaliyoandikwa “No Lye Relaxer” yana calcium hydroxide na guanidine carbonate.

Bidhaa za kulainishwa nywele zilizoandikwa ‘no lye relaxer’ zinadaiwa kusababisha majeraha kwa kiasi kidogo ukilinganisha na zile zilizoandikwa “Lye Relaxer”.

Jinsi ya kufanya ili uwe na umbo dogo la kuvutia

Unaweza kujiuliza, hivi inawezekanaje kuwa na umbo dogo la aina hii? Ukweli ni kwamba inawezekana, lakini inahitaji kazi ya ziada kufikia kwenye lengo hilo.

Unalifahamu umbile la sifuri au saizi zero?

Kwa wale wanaojali maumbo ya kupendeza saizi zero linatafsiriwa ni kuwa na kiuno kisichozidi inchi 23, nyonga 32 na kifua 31. Kikubwa unachotakiwa kuzingatia ni mazoezi na ulaji wako, kwa kuwa mwangalifu katika kiasi cha kalori unachoingiza mwilini kila siku.

Unatakiwa kuwa mwadilifu katika uchaguaji wako wa chakula, haimaanishi ukae na njaa. Inawezekana ikawa ni vigumu kuelewa makala haya.

Kinachosisitizwa katika mpango huu, ni kuwa waangalifu katika upangiliaji wa vyakula. Aina hii ya mpangilio wa ulaji inafahamika zaidi kitaalamu kama ‘crash diet’ Kula kiasi cha kalori 400- 500 kwa siku. Lakini unatakiwa kufanya mazoezi angalau kwa saa mbili kwa siku, ili kupunguza mara mbili ya kiasi cha mafuta uliyokula katika siku hiyo.

Kunywa maji kwa wingi:

Kwa kunywa kiasi kikubwa cha maji itakusaidia kurahisisha umeng’enyaji wa chakula mwilini. Ni vyema mwili wako ukawa na maji ya kutosha ikiwa umeingia kwenye mpango huu wa ulaji Kula mboga za kijani: Zina Vitamini, protini na virutubisho vingine kwa wingi ambavyo ni muhimu kwa afya. Kama ilivyoainisha awali, utaratibu huu hauhamasishi kukaa na njaa, bali kula vyakula vilivyo bora kiafya.

Kula vyakula visivyokobolewa.

Mara nyingi vyakula vya aina hii, huwa na virutubisho muhimu na vinavyohitajika katika ustawi wa mwili.

Punguza wanga katika mlo wako.

Badala yake unaweza kula protini na kuingiza vyakula kama mayai na samaki kwenye mlo wako.

Epuka kula vyakula vya mtaani.

Vyakula kama chips, mihogo ya kukaanga na jamii yake vinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzito wa mwili na pia hulifanya zoezi la umeng’enywaji wa chakula tumboni kuwa gumu.

Kula supu za mbogamboga;

Supu kama ya kabichi licha ya kujaza tumbo, husaidia katika kurahisisha mfumo wa umeng’enyaji chakula tumboni.

Kula saladi na matunda kwa wingi.

Hii itasaidia kukuweka sawa kiafya.

Jizuie kula vyakula vyenye sukari nyingi na hata vile vya mtaani unavyohisi vinaweza kukwamisha mpango wako wa kupungua.

Lakini pamoja na yote jipe mazoezi ya kutosha kama kukimbia, kuruka kamba au mazoezi ya kupunguza tumbo na maziwa

Madhara ya Kujichubua

Katika baadhi ya sehemu duniani watu wanaamini kuwa ngozi angavu huashiria uzuri, utajiri na uwezo(kifedha) alionao mtu.Katika baadhi ya sehemu watu wenye ngozi nyeusi huchukuliwa kuwa wapo chini ya kiwango, hii hupelekea watu hawa kutumia ving´arisha ngozi kama krimu, vidonge au nyenzo zingine kubadilisha ngozi zao.

Tafiti zinaonyesha kwamba wavulana na wasichana hupendelea kutumia bidhaa zinazong´arisha ngozi ili waweze kupata hadhi nzuri katika kundi la familia zao, na jamii. Kwa kweli,hata matangazo yanayoonyeshwa kwenye televisheni mbalimbali huonyesha kitu hiki. Mambo hayo yote huwa na athari kubwa juu ya mawazo ya vijana wa kiume na wakike ambayo hupelekea kuwafanya wachague chochote wanachomudu kati ya krimu au vidonge.

Madhara ya kujichubua ni yapi?
Mtu anaeyejichubua anaweza kupata kansa ya ngozi, chunusi, uvimbe katika ngozi, ngozi kuwa nyembamba,Kuongezeka kwa hamu ya kula na uzito,kutokwa na mabaka, pumu, kupata watoto wenye kasoro, kupata matatizo ya akili, kuharibika kwa ini, kuharibika kwa mishipa ya fahamu pamoja na figo kutokana na kiwango kikubwa cha zebaki(mercury) kilichomo katika krimu,Osteoporosis(kupungua kwa uzito wa mifupa ambapo huongeza hatari ya kuvunjika kwa mifupa)

Baadhi ya madhara haya huonekaa mara moja na mengine hujitokeza kadri mtu anavyotumia ving´arisha ngozi.

Jinsi ya Kujaza nywele kwa njia za Asili

Zingatia mambo haya yafuatayo;

  1. Chukua parachichi kubwa moja, asali vijiko vitatu na kiini cha yai.
  2. Osha nywele zako kwa shampoo na uzikaushe.
  3. Ponda ponda parachichi mpaka lilainike kabisa. Chukua vijiko vitatu vya asali na kiini cha yai kisha changanya yote kwa pamoja.
  4. Paka mchanganyiko huo kaa nao kwa muda wa dakika 15 kisha osha.
  5. Fanya hivyo kwa muda wa wiki moja hadi mbili na utaweza kuona matokeo mazuri katika nywele yako

Tiba mbadala ya chunusi na vipele usoni

Kuna idadi kubwa ya watu wanao kabiliwa na tatizo la vipele vya usoni ( Chunusi ). Kuwa na chunusi ni jambo lenye karaha sana, kwani linakufanya upoteze mvuto wako wa asili na hivyo kukukosesha raha.

Zipo njia mbalimbali za asili zinazo weza kutumika kutibu tatizo la chunusi na vipele vya usoni.

Ifuatayo ni miongoni mwa njia bora kabisa na ya uhakika itakayo kusaidia kuondokana na tatizo la Chunusi au vipele kwenye uso.

Komamanga: Maganda Ya Mkomamanga yaliyosagwa, yakichanganywa na habbat sodah ya unga, hutengeneza dawa nzuri ya asili ya kuondoa tatizo la vipele vya usoni ( chunusi )

Habbat Soda: Hii ni Habbat Sodah Ya Mbegumbegu. Habbat Sodah iliyosagwa ndio inayo hitajika katika kutengeneza dawa ya asili ya kuondoa tatizo la vipele vya usoni ama chunusi.

MAHITAJI:

Habbat Sawdah ya Unga iliyo sagwa.
Nusu kikombe ya maganda ya komamanga yaliyo sagwa.
Nusu kikombe ya siki ya tofaha(apple )

MATAYARISHO NA MATUMIZI

Changanya na pasha moto kwa dakika mbili kikombe kimoja cha Habbat-Sawdaa iliyosagwa, ½ (nusu)
kikombe cha maganda ya komamanga yaliyosagwa, na ½ (nusu) kikombe cha siki ambayo inatokana na juisi ya tofaha (apple).

Paka katika sehemu inayotakiwa kabla ya kwenda kulala kila siku usiku mpaka vipele (chunusi) vitakapoondoka. Mchanganyiko unaweza kukaa mpaka wiki tatu na ni lazima uwekwe katika hali ya ubarid.

Mambo ya Msingi kujua kuhusu uvaaji wa Tai

Kuna mambo mengi ya kufanya ili tuwe watu wa kuvutia kila wakati.Mpangilio wa mavazi hufanya mtu kuonekana maridadi.

Kama wewe ni mvaaji wa tai unapovaa unazingatia mambo yapi? Na je unafunga tai yako kwa namna inayokubalika?

Wengine huwa hawafahamu jinsi ya kufunga tai na hivyo kuleta mushkeri wakati wa kuvaa tai na kusababisha tai kukaa upande. Unapoamua kuvaa tai na shati ambalo halijanyooshwa ambalo linakuwa kwenye mikunjo au kuvaa tai na ndala unakuwa umeua maananzima na kulivunjia heshima vazi hili.

Tai ni vazi lawatu walio maridadi kama huwezi kuwa maridadi basi vazi hili halikufai kabisa.
Unapovaa taa unatakiwa kuzingatia aina ya umbo lako kama wewe ni mnene vaa tai inayoendana na mtu mnene na kama wewe ni mwembamba basi vaa tai inayoendana na mtu mwembamba.

Kuna wengine huvaa tai zinazofika magotini na kuwa kichekesho anapopita mtaani
Tai ni vazi ambalo huongeza heshima na hadhi ya mvaaji cha muhimu ni jinsi gani unavaa tai yako na ikiwezekana jaribu kumechisha tai na suruali kwa vile ili tai upendeze ni laima iendane na nguo unayovaa.

Ni vyema ukahakikisha kuwa unakuwa na tai zenye rangi tofauti ambazo zitaendana na nguo unazovaa.

Jinsi ya kung’arisha sura yako kwa kutumia Asali, Sukari, Maziwa, na Limao

Usafi wa uso ni moja ya mambo muhimu sana kwa mwanamke au mwanaume yeyote yule ambaye anapenda kuwa nadhifu na mwenye mvuto. Kumbuka “reception ndio kila kitu “. Unapokutana na mtu sura yako na mwonekano wa sura yako ndio kitu cha kwanza kinachomtambulisha kwamba wewe ni nani na upo kwenye hali gani.

Kuna njia nyingi za kuufanya uso wako uvutie na kupendeza. Leo tutaongelea zaidi jinsi ya kusafisha uso kwa njia ya asili. Mie hupenda kutumia njia ya asili sababu ni rahisi kupata vifaa na ni nafuu . Pia mtu anaweza kufanya kwa mazingira yoyote yale. Na matumizi ya vitu vya asili kwenye mwili husaidia kupunguza sumu mwilini kwani kutumia vipodozi vyenye kemikali husababisha miili yetu kujaaa sumu.

Njia ya asili ya kusafisha na kupendezesha mwili ninayokueleza leo inahitaji vitu vikuu vinne : asali, sukari, maziwa, na limao.

Haijalishi aina gani ya ngozi unayo , njia hii ya asili inaweza kutumika kwa aina yoyote ile ya ngozi iwe ngozi yenye mafuta au ngozi kavu.

Kiasi cha mahitaji yanayohitajika:

  • Kijiko kimoja cha asali
  • Kijiko kimoja cha sukari
  • Kijiko kimoja cha maziwa
  • Kijiko kimoja cha limao

Utaratibu wa kusafisha uso

Weka mahitaji hapo juu kwenye chombo kilicho kisafi, changanya vitu vyako mpaka vilainike, viache kwa muda wa dakika 10 ili viweze kuchanganyikana vizuri na na sukari iweze kuyayuka vizuri.

Baada ya mchanganyiko wako kuwa tayari chukua kipande cha pamba kilicho kisafi tumia kupakia mchanganyiko wako usoni . Na kumbuka ni vizuri uso ukiwa mchafu na upaswi kuosha uso alafu ufanye zoezi hili. Baada ya kupaka mchanganyiko wako usoni kaa kwa dk 15 .

Baada ya hapo chukua maji ya uvuguvugu, kitaulo kisafi na sabuni ya kipande “vizuri kutumia sabuni ya kipande maana haina kemikali nyingi” tumia kitambaa kuoshea uso wako pamoja na sabuni.

Basi baada ya hapo umekuwa umemaliza zoezi lako la usafi wa ngozi yako
Kumbuka njia hii aina madhara yoyote na haibadilishi rangi au muonekano wa ngozi yako na unashauliwa kufanya mara kwa mara ili kukupa mvuto zaidi.

Mambo ya kuzingatia kama una ngozi yenye Mafuta

Ngozi yenye mafuta kwa kawaida huwa inang’ara, nene na yenye rangi iliyotitia. Mara nyingi ngozi yenye mafuta mengi sana huwa na chunusi nyingi na vipelepele na mara nyingine huwa na chunusi zenye vichwa vyeusi. Katika aina hizi za ngozi mafuta hutokana na tezi za sebaceous na kuzalisha mafuta zaidi ya kiwango kinachotakiwa. Mafuta hayo husambaa katika ngozi na kuifanya iwe na mafuta mafuta.

Mafuta katika mwili yanatengenezwa na ‘sebaceous glands’,kwa hiyo kuna baadhi ya watu wana sebaceous glands ambazo zinatengeneza mafuta kwa wingi sana na hivyo kufanya ngozi zao kung’aa kwa sababu ya hayo mafuta mengi.

Sebaceous gland zipo kwa wingi usoni(face) shingoni(neck), kifuani, kichwani na mgongoni, ndiyo maana hayo maeneo yanakuwa na mafuta kwa wingi.

Sababu zinazosababisha ngozi kuwa na mafuta:

  1. Kurithi.
  2. Lishe.
  3. Kiwango cha homoni mbalimbali mwilini.
  4. Ujauzito.
  5. Vidonge vya kuzuia mimba.
  6. Baadhi ya vipodozi.
  7. Hali ya hewa ya joto.

Namna ya kutunza ngozi zenye mafuta

Faida kubwa ya kuwa na ngozi yenye mafuta ni kuwa haizeeki kwa haraka ikilinganishwa na aina nyinginezo za ngozi. Miongoni mwa mambo yanayosaidia ili kuitunza ngozi yenye mafuta na kuiepusha na chunusi na hali isiyopendeza ni:-

Ngozi yenye mafuta inahitajia kusafishwa vyema kwa maji ya moto na sabuni ili kuzuia vinyweleo visizibwe na mafuta.

Epusha vifaa vigumu visikwaruze uso wako na kupelekea ngozi kubanduka, kwani suala hilo husababisha tezi za mafuta kufanya kazi zaidi ili kujaza sehemu iliyopotea ya mafuta.

Epuka kutumia vipodozi ambavyo huifanya ngozi yako ipoteze maji au kukauka. Kwani husababisha sehemu ya juu ya ngozi inyauke, na hivyo kusababisha mafuta kuziba vinyweleo na kupelekea kutokea vichwa vyeusi.

Jitahidi kuitunza vyema ngozi yako na kuisafisha vizuri. Jaribu kuosha uso mara mbili au tatu kwa siku. Usioshe mara nyingi kwani kufanya hivyo huufanya uso kutoa mafuta zaidi.

Chagua kile unachosafishia kwa makini, jiepushe kutumia cream nzito nzito au vifaa vugumu wakati wa kuosha uso wako. Ni bora utumie sabuni za kawaida zisizokuwa na madawa. Unaweza kutumia lotion ya kuua bacteria au sabuni zisizo na dawa nyingi (lightly medicated), au sabuni zenye madini mbalimbali. Ni bora usioshe au kutumia lotion au michanganyiko yenye alkoholi.

Tumia maji ya moto au ya vuguvugu wakati unaosha uso wako.

Wakati unapoosha uso wako, ukande kwa kutumia ncha za vidole, jiepushe kupaka sabuni moja kwa moja usoni, inaweza kuganda na kuzuia vinyweleo kuziba.

Kutumia mask za udongo (clay) na tope (mud) husaidia katika ngozi za aina hii. Ni bora utumie mask mara moja au mbili kwa wiki.

Jitahidi kutumia vipodozi vya uso ambavyo vimetengenezwa kwa ajili ya ngozi yenye mafuta.

Namna ndizi inavyotumika katika urembo

Mbali na kulika, ndizi zina manufaa mengine, hasa katika urembo wa ngozi.
Ndizi zina virutubisho muhimu vinavyoboresha ngozi. Ndizi pia zina aina tatu za sukari zinazojulikana kama ‘sucrose’, ‘fructose’ na ‘glucose’.

Hakikisha unanawa uso wako mara tatu kwa siku. Unapofanya hivyo unaondoa uchafu.

Ndizi pia husaidia kuzuia chunusi.

Hakikisha unanawa uso kwa sabuni ambayo inaendana na ngozi yako. Ikiwa ngozi yako ni ya mafuta, hakikisha unatumia sabuni ambayo itakuacha ukiwa mkavu na kama ngozi yako ina ukavu, jioshe na sabuni itakayokufanya uwe na unyevu.

Kulainisha ngozi

Changanya asali na ndizi moja iliyopondwa na upake kwenye uso na shingo. Nawa uso kwa maji ya fufutende baada ya muda wa nusu saa. Fanya hivi angalau mara moja kwa wiki.

Kung’arisha uso

Ndizi huwa na Vitamin C ambayo husaidia kuiweka ngozi kuonekana iking’aa. Kwenye ndizi iliyopondwa, ongeza vijiko viwili vidogo vya juisi ya limau na upake kwa uso na shingo. Osha kwa maji ya fufutende baada ya dakika 20. Ni vizuri kupaka mchanganyiko huu wakati unapoenda kulala.

Kuzuia mikunjo

Ponda parachichi na ndizi pamoja. Paka kwa uso na uoshe baada ya muda. Mchanganyiko huu hulainisha ngozi ya uso na kuwa laini lakini pia upunguza ukubwa wa matundu ya ngozi ya uso wako.

Kusugulia uso (Scrubing)

Changanya ndizi na sukari kijiko kimoja, kisha paka usoni na usugue taratibu. Ndizi hulainisha ngozi kavu na sukari huondoa seli zilizokufa kwenye ngozi.

Saga ndizi moja na Oats vijiko vitatu kisha changanya na asali na maziwa. Paka usoni kwa dakika 15 kisha sugua.

Chanzo, dalili na matibabu ya chunusi

Chunusi ni ugonjwa wa ngozi ambao hujit-okeza kama viuvimbe/vipele vidogo vidogo hasa sehemu za uso,kifuani na hata mgongoni.Vipele hivi hutokea wakati vishimo vya kupitisha jasho katika ngozi vinapozibwa kwa mafuta au seli za ngozi zilizokufa au wadudu yaani Bacteria.

Kwa lugha ya kidaktari chunusi huitwa Acne Vulgaris.Chunusi ndio ugonjwa wa ngozi ambao humwathiri binadamu kwa kiasi kikubwa kwa mfano nchini Marekani pekee huathiri watu zaidi ya milioni kumi na sa-ba..Chunusi huweza kujitokeza katika umri wowote lakini huathiri sana vijana hasa wa-kati wa balehe (adolescents) .

Karibu asilimia 85 ya vijana kati ya umri wa miaka 12 hadi 25 hupata chunusi na zaidi ya asilimia 20 ya wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka ishirini hupata chunusi wakati mwingine hata watoto wadogo pia huweza kupata chunusi hii ni tofauti na watu wengi wanavyofikiria kuwa chunusi ni dalili ya balehe.

Chunusi ni ugonjwa unaoathiri vifuko au glandi za ngozi.Katika ngozi ya binadamu kuna glandi ziitwazo Sebaceous ambazo zipo chini ya ngozi na kazi yake kubwa ni kutoa mafutamafuta yaitwayo Sebum ambayo hu-saidia kuiweka ngozi kuwa nyevu na yenye mvuto.

Wakati wa balehe mwili wa binadamu hutoa Sebum kwa wingi na kwa sababu wakati huu vikemikali vya mwili yaani sex hormones hutolewa kwa wingi hasa hormone ya kiume iitwayo androgen husababisha utoaji wa sebum kuwa mwingi zaidi kuliko kawaida. Sebum inapotolewa kwa wingi huungana na seli za ngozi zilizo-kufa na kutengeneza mchanganyiko mzito kama nta uitwao comedo ambao huziba vishimo vya kutolea joto.

Maambukizi zaidi hutokea pale ambapo vijidudu yaani baktaria vinaposhambulia vishimo vilivyoziba hapo kivimbe ambacho watu wengine huita Pimple hujitokeza pale ambapo Sebum, bacteria, seli za ngozi na seli nyeupe za damu zinapo-changanyika na kujikusanya katika vishimo vya jasho vilivyoziba na eneo husika hupata vivimbe au vipele ambavyo tunaviita chunusi.

Ukubwa wa kipele hutegemea ngozi ya mtu au kiasi cha mchanganyiko nilioeleza hapo juu katika eneo husika.Vipele vinaweza kuwa vidogo au vikubwa. Chunusi wakati mwingine husababisha mabaka katika ngozi hali hii hutokea pale ambapo seli za ngozi zilizoharibika huondolewa na seli mpya kutengenezwa.

Ngozi mpya hutengenezwa kirahisi tu mahali palipokuwa na chunusi hali hii husababisha mlingano usiosahihi wa ngozi na hutoa kidonda ambacho baadaye hubaki kama baka. Chunusi hutokea zaidi katika uso,kifua ,mabega na mgongoni kwa sababu maeneo hayo yana vifuko au glandi za Sebaceous nyingi.

CHANZO CHA CHUNUSI

Chanzo halisi cha chunusi hakijulikani.hata hivyo baadhi ya vitu vinavyoongeza uwezekanifu wa kupata chunusi ni;

UMRI – Kama nilivyosema hor-mone/vikemikali hutolewa kwa wingi sana mtu anapofikia umri wa kubale-he.Kemikali hizi huongeza utengenezaji wa nta (sebum) katika ngozi ambayo huchochea kutokea kwa chunusi
VIPODOZI –Baadhi ya vipodozi kama Make-up za kina dada na Sprays za ny-wele zina mafuta ambayo yanaweza kusababisha chunusi kuwa nyingi zaidi.
CHAKULA- Chunusi hazisababishwi na chakula bali baadhi ya vyakula hufan-ya chunusi kuwa nyingi zaidi.
DAWA-Chunusi zinaweza kujitokeza kutokana na kutumia dawa kadhaa kama vile antibiotics,Vidonge vya uzazi wa mpango,steroids na tranquilizers.Steroid ni dawa zenye homoni zilizotengenezwa kitaalamu ambazo wakati mwingine wanariadha huzitumia tofauti na ma-kusudio ili kuongeza unene wa misuli yao.
MAGONJWA- Magonjwa yatokanayo na matatizo katika vikemikali (hormonal disorders) huongeza matatizo ya chunusi hasa kwa wasichana.
MAZINGIRA- Chunusi huweza kuwa nyingi zaidi hasa unapoishi mazingira yenye mafuta,grisi au hewa chafu .Kutoa jasho sana hasa katika mazingira ya joto huongeza uwezekanifu wa kupata chunusi.
JINSIA-Wavulana hupata sana chunusi kuliko wasichana.
FAMILIA- Wakati mwingine chunusi hujitokeza sana kwa wanafamilia wa familia kadhaa kuliko nyingine.
HOMONI- Mabadiliko ya homoni za mwili hasa wakati mwanamke akiwa katika siku zake,ujauzito au mwanamke anapokuwa na umri mkuwa hupelekea kupata chunusi.
USAFI WA MWILI- Kutumia sabuni zenye kemikali,kujisugua sana na kuzitoboatoboa chunusi au vipele hu-sababisha chunusi kuongezeka zaidi.Kukaa muda mrefu na jasho mwi-lini au kutooga huongeza uwezekanifu wa kupata chunusi
MAWAZO AU STRESS-Mtu anapokuwa na mawazo mengi vimkemikali kadha hutolewa mwilini ambavyo huwe-za kuchangia au kusababisha chunusi

DALILI ZA CHUNUSI

Vipele au vivimbe vidogo vidogo ambavyo pengine husababisha mwasho au vinavyouma ni dalili ya chunusi.Wakati mwingine huweza kujitokeza kama baka dogo na wakati mwingine mtu anaweza utambuzi wa chunusi unaweza kuwa mgumu kutokana na watu walivyomakini au wanavyojenga wasiwasi kubwa katika mwonekano wao hasa usoni.Ikumbukwe kuwa kutokana mwonekano wa chunusi ni rahisi sana.

Daktari kuzigundua, japokuwa katika familia zetu ni mara chache sana mtu akaenda kumwona daktari au mtaalamu wa magonjwa ya ngozi kwa sababu ya chunusi.Pale inavyotokea hivyo basi hali inakuwa ni mbaya zaidi.Hata hivyo si vibaya kumwona daktari ambaye atakuuliza kuhusu chakula, ngozi, dawa unazotumia na vitu vingine vinavyowe-za.kuchangia mtu kupata chunusi

MATIBABU

Matibabu ya chunusi yanajumuisha kupunguza utoaji wa anta (sebamu ), kuondoa seli za ngozi zilizokufa na kuua wadudu yaani bacteria.

Matibabu huweza kutofautiana kutokana na wingia au ukubwa wa tatizo. Suala la kuzingatia ni kuepuka mambo yanayoweza kusababisha chunusi kama nilivyoeleza hapo juu.

DAWA ZA KUPAKA

Kuna dawa za kupaka ambazo hupaka katika eneo la ngozi lililoathirika kwa chunusi. Dawa hizi hupatikana kama cream,lotion,gel au pad.

Dawa hizi hutumika kutibu chunusi ambazo haziko katika hali mbaya hasa kama kuna vijipele vidogo vidogo tu. Mojawapo ya dawa hizi ni antibi-otic kama zenye mchanganyiko wa gentamyicin na betamethasone au dexame-thasone kama vile Gentrisone au Gentriderm cream, Erythromycin,B-Tex na kadhalika.Pia Persol forte Gel husaidia hasa ukianza na asilimia ndogo (2.5%) na kuen-delea kadri ngozi yako inavyohimili dawa. Gentamycin huua wadudu wanaosababisha chunusi wakati dawa nyingine huondoa mwasho.

Dawa nyingine ni zile zinzolainisha nta au Comedolytics na kufanya vishimo vya jasho kufunguka na dawa nyingine huongeza kasi ya utengenezwaji wa seli mpya za ngozi.

Dawa hizi za kupaka hushauriwa kupakwa angalau mara mbili au tatu kila siku hasa baada ya kusafisha kwa maji safi na sabuni ya kawaida na kukausha kwa taulo eneo lenye chunusi na matibabu yanaweza kuchukua wiki kadhaa.

DAWAZA KUMEZA

Wakati mwingine daktari anaweza kumshauri mgonjwa kutumia dawa za kumeza kulingana na wingi au ukubwa wa tatizo.

Dawa kama antibiotics huua wadudu na huzuia chunusi ,dawa hizo ni kama vile Erythromycin topical, Accutane (isotret-inoin), Benzamycin Cleocin T (clindamycin phosphate), Desquam-E (benzoyl peroxide) Minocin (minocycline hydrochloride) na ”Si vema kujinunulia mwenyewe tu na kuanza kutumia bila ushauri wa daktari au mtaal-amu wa magonjwa ya ngozi.”

Wanawake wenye chunusi zisizotibika wanaweza kupewa Anti-androgens kama vile baadhi ya vidonge wa uzazi wa mpango.Chunusi sugu hutibiwa kwa ciorticosteroids na anti-iflammatory drugs ambazo hutibu chunusi sugu ambazo huitwa Acne fulminans na hupatikana zaidi kwa vijana.

MATIBABU MENGINE

Kwa nchi zilizoendelea matibabu yanaweza kuwa hata upasuaji mdogo (skin grafting) au plastic surgery kama chunusi imesaba-bisha baka kubwa na kuna njia kama vile Chemical peel ambapo kemikali hupakwa kwenye ngozi na inapokauka kipande au gamba la juu la ngozi huondolewa na kuondoa baka.

MATIBABU MBADALA

Haya hujumuisha lishe bora na usafi wa mwili.Ni vema kuoga mara kwa mara na kujifuta maji kwa taulo safi na kuiweka ngozi katika hali ya ukavu nakuepuka upakaji wa mafuta mengi ya mgando hasa wakati wa joto.

Watu wenye chunusi wanashauriwa kulAa mlo kamili wenye vyakula vyenye madini ya zinki,nyuzinyuzi, matunda, mboga za ma-jani,vitamin B complex na Chromium. Ni vema kuepuka au kupunguza matumizi ya pombe,vyakula vya maziwa, tumbaku, sukari, vyakula vilivyoandaliwa viwandani na vyakula vyenye Iodine nyingi kama vile chumvi

MUHIMU

Chunusi haziwezi kutibika kabisa japokuwa iwapo matibabu Yatakuwa sahihi watu 60 kati ya 100 hupona na unapokuwa unatumia dawa usitarajie kupona haraka kwani inaweza kuchukua hata miezi miwili kupata nafuu na zinaweza kujitokeza unapoacha kutumia dawa.Chunusi pia huweza kupona kwa kuacha mabaka ambayo kwa hapa nchini hakuna utaalamu sahihi wa kuyaondoa bali huweza kuondoka kadri muda unavyoenda au kwa kemikali kali ambazo zinaweza kuwa na madhara katika ngozi.

MAMBO YA KUFANYA ILI USIPATE CHUNUSI

  1. Hakuna njia sahihi ya kujizuia ila unaweza kufanya yafuatayo;
  2. Osha taratibu sehemu unayodhani ina chunusi kwa maji safi na sabuni angalau mara mbili kila siku huku ukisugua taratibu ,usikwaruze kwa kucha au kitu choichote kigumu.
  3. Tumia make-up au vilainisha ngozi visivyo na mafuta mgando
  4. Osha nywele zako kila mara na epuka nywele kuziba uso (kwa wenye nywele ndefu)
  5. Kula mlo kamili na epuka vyakula vyenye mafuta mengi.
  6. Usibinye au kutoboa vipele kwa pini au kitu chenye ncha kali.
  7. Epuka kukaa sana juani,mwanga wa asubuhi ni mzuri ili kupata vitamin D
  8. Punguza mawazo

Jinsi ya kutumia maziwa ya mtindi kufanya ngozi yako kuwa laini na soft

Ulisha wahi kukaa ukajiuliza mbona kuna baadhi ya watu wana ngozi nzuri laini na soft? lakini kwako ni tofauti?

Ukawaza labda wanatumia vitu vya bei ghali ambavyo wewe huwezi ku – afford, au umesha hangaika na ma – cosmetics lakini bado ngozi yako haikubali kukaa vizuri?

Jaribu hii Home made Yogurt Cleansing, Tumia mtindi ambao hauna mafuta mengi au hauna kabisa (low fat),

Paka mtindi wako usoni fanya kama una sugua kwa muda mchache halafu uache kwa dakika 15, fanya hivi mara mbili kila siku na utapata matokeo kwa muda mchache.

Hii husaidia kuondoa cell za ngozi zilizo kufa (dead skin cells) na protein tighten the pore.

Jinsi ya Kutumia Papai na Asali kuondoa Madoa Usoni

KUMEKUWA na sababu mbalimbali zinazofanya watu kutokuwa na ngozi zisizokubalika.Mbali na hali ya hewa pia matumizi ya pombe na sigara hata matumizi ya cream kali ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu bila kujua madhara yake kumechangia kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.

Ngozi kwa kawaida inatakiwa ijitengeneze yenyewe na si kuitengeneza kwa vipodozi kama wengi wanavyodhani. Ulaji wa matunda na mboga za majani kwa wingi kunywa glasi nane za maji kwa siku ni njia nzuri kama unataka kuwa na ngozi nzuri isiyo na madoa wala ukavu ambao haupendezi.

Wengi wanaacha kula mbogamboga na matunda kwa wingi hata kutokunywa maji ya kutosha na badala yake wamekuwa akitegemea kuwa na ngozi nzuri jambo ambalo ni gumu.Mara kadhaa tumeshuhudia watu wanaopaka cream kali wakiwa kama wameungua usoni huku uso na mwili ukionekana kuwa makavu jambo ambalo linaashiria kuwa kupaka cream si suruhisho la kuwa na ngozi nzuri.

Kuna watu wamekuwa na ngozi za asili na hata unapowauliza baadhi yao hawajawahi kupaka cream hata siku moja na bado wana ngozi nzuri zinazovutia hao wamekuwa wakila kwa ajili ya kuhakikisha wanatengeneza ngozi zao kutoka ndani.

Pia wengi wanaharibu ngozi zao na kuwa na madoa kutokana na kutumia make up kwa muda mrefu na hata anapogundua kuwa ana tatizo la madoa amekuwa akijaribu kutumia cream nyingine kwa ajili ya kumaliza tatizo hilo jambo ambali linazidisha madhara kwenye ngozi.

Unaweza kutibu ngozi yenye madoa usoni pia mashavuni kwa kujitibu na juisi ya limao.

Namna ya kufanya

Chukua limao lioshe na kisha likamue na kuchuja mbegu zake. Weka juisi hiyo kwenye kikombe na kisha tafuta kitambaa laini kichovye kwenye juisi ya limao na dondoshea juisi ya limao kwenye sehemu zenye tatizo.

Kaa kama dakika tano kisha usha uso kwa maji safi.Pia unaweza kuchanganya na asali mbichi na maji ya limao husaidia pia kuondoa madoa usoni.

Limao lina sifa kubwa ya kuzuia harufu pia unaweza kulitumia katika kuondoa harufu kali ya jasho mwilini na husaidia kuondoa weusi kwenye kwapa, chini ya macho, mapajani pia.

Chukua kipande cha limao weka sukari kidogo, sugua.Unatakiwa kutumia kwenye kwapa ambalo ni safi, vizuri kutumia njia hii kabla na baada ya kuoga.

Mambo ya Kuzingatia Kama una ngozi Kavu na Kuepuka kuwa na ngozi kavu

Ngozi kavu inaweza kukufanya ukose raha kutokana na kuwasha mara kwa mara, lakini pia kupauka hii inaweza kusababisha mikunjo ya ngozi na hata kupatwa na vidonda katika ngozi. Ngozi kavu husababishwa na baridi lakini pia unaweza ukawa umezaliwa nayo tu upo hivyo. kama una ngozi ya aina hii basi haya ni mambo matatu ya kuyaepuka kufanya.

Kuoga maji ya moto kwa muda mrefu

Epuka kuoga maji ya moto mara kwa mara kunaweza kufanya yale mafuta natural yanayo moisturize mwili kukauka, ili kuepuka tatizo hili ni vyema ukatumia maji ya uvuguvugu au baridi katika kuoga au kunawa mwili wako.

kutumia vipodozi vyenye Alcohol Nyingi

Alcohol nyingi husababisha ngozi kuzidi kuwa kavu, wakati wa kwenda kununua vipodozi vyako hakikisha unasoma maelezo na kujua kiasi cha alcohol kilichopo kama ni nyingi usichukue chukua yenye kiasi kidogo.

Kuosha Ngozi Na Sabuni Mara Kwa Mara Na Kusugua Kwa Nguvu

Kuosha ngozi mara nyingi sana na sabuni ni njia ya mojawapo ya kupata ngozi kavu. Ngozi kavu iliyokasirika huathirika zaidi na maambukizi ya bakteria kwa sababu kuosha mara nyingi huondosha safu za kinga ya ngozi yako.

Mambo ya Kuzingatia ili uwe mrembo siku zote

Katika Jamii nyingi duniani, dhana ya urembo imekuwa na mitazamo tofauti kwa watu wengi. Kila mmoja anautafakari urembo kwa namna yake kulingana na malezi na tamaduni za mahali husika. Wako wanaoamini kuwa mrembo ni lazima awe na ngozi nyeupe, wengine hudhani kuwa ili kuonekana mrembo, lazima uwe na nywele ndefu, lakini pia wapo wanaodhani kwamba ili uwe mrembo ni lazima uwe na umbo namba nane na wapo wanaojua urembo ni kuwa mwembamba (kimbaumbau au Miss) au kuwa mrefu na wapo wanaoamini urembo ni kuwa mnene.

Hiyo yote ni mitazamo tu, lakini tafsiri halisi kutoka kwa wataalamu wa urembo ni kwamba; urembo ni hali ya kuwa na afya bora.

Je, Mpenzi msomaji ulikuwa unajua hili? Nakuomba Kabla hujafanya chochote kuhusu afya yako, unatakiwa kuamini kwamba wewe ni mrembo. Ikiwa utasimama katika hilo ni kweli utakuwa mrembo siku zote. Basi ili kubaki kuwa mrembo tujifunze haya machache leo ya kufanya:

1. SAFISHA NGOZI YAKO:

Hakikisha ngozi yako inakuwa safi muda wote. Unaweza kutumia njia mbalimbali kama vile kuondoa ngozi zilizokufa mara kwa mara. Kuondoa mafuta yaliyogandamana katika ngozi kwa kufanyia masaji ngozi yako ili kurahisisha mzunguko wa damu yako.
Ikiwa hili litafanyika kwa umakini ni wazi kuwa matatizo ya kuwa na chunusi au weusi katika ngozi yako havitakuwepo kwako.

2. SAFISHA NYWELE ZAKO:

Tumia bidhaa za nywele, ambazo zinaendana na nywele zako na hakikisha unazingatia mambo muhimu katika uboreshaji wa nywele zako.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kutokutumia vifaa vinavyounguza vywele.

Epuka kuosha nywele kwa maji ya moto, pia kuchana nywele zikiwa na maji, kwani unaweza kusababisha kukatika kwa nywele zako.

3. USIPAKE VIPODOZI MARA KWA MARA:

Tumia vipodozi pale inapobidi, usipendelee kutumia vipodozi mara kwa mara kwani wakati mwingine matumizi ya mara kwa mara ya vipodozi, husababisha madhara katika ngozi yako, hasa unapotumia bila kufuata maelekezo ya wataalamu.

4. PATA USINGIZI WA KUTOSHA:

Hakikisha unapata usingizi wa kutosha kila siku. Kwa mujibu wa wataalamu, unatakiwa kulala si chini ya saa nane kila siku. Ikiwa utapata usingizi wa kutosha ni wazi kuwa macho yako yataonekana yenye nuru siku zote. Pia utazidi kuonekana kuwa mrembo zaidi.

5. FANYA MAZOEZI YA VIUNGO:

Hakikisha mazoezi yanakuwa sehemu ya maisha yako, hii itasaidia kukufanya uonekane siyo tu mrembo, bali pia mwenye kujiamini.

6. SAFISHA MENO YAKO:

Usafi wa meno pia ni miongoni mwa mambo ya kuzingatia unapoamua kuboresha urembo wako. Hakikisha unapiga mswaki walau mara mbili kwa siku kila siku au kila baada ya kula.

Haya yameorodheshwa na wataalamu mbalimbali kuwa ni mambo yanayochangia urembo wa asili na mvuto wa ngozi na mwili.

Mavazi Mazuri kwa wanawake wanene

Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiangaika kupata aina ya nguo za kuvaa tena hasa wanawake wanene, kutokana na maumbo yao wanaona ni kazi sana kutafuta nguo, wengine hukosa hata uhuru wa kutoka out na watu wao wa karibu kwa sababu tu wanakosa nguo.Wengi ujikuta wakichagua nguo pana pana ili kuficha maumbo yao, lakini kumbe unaweza kuwa huru sana na mwili wako.

Zifuatazo ni badhi ya tips zinazoweza kukusaidi kuchagua nguo za kuvaa kwa mwanamke mnene.Inawezekana nguo hizi unazo ndani lakini unashindwa kuzipangilia;

1. Kabla ya kuchagua nguo ni lazima kujua mwili wako una unene wa aina gani,ikiwa wewe ni mnene na unatumbo kubwa basi ni bora kuvaa gauni maana gauni uweza kukuweka vizuri na pia ni mazuri hasa kwa watu wanene.

2. Lakini pia kama wewe ni mnene na umebahatika kuwa na maziwa makubwa, ni vizuri kupendelea kuvaa nguo zenye v-shape, siri ya nguo hizi ni kwamba huwa na tabia ya kuficha ukubwa wa maziwa na kufanya uwe maridadi zaidi ila zingatia kuchagua brazia nzuri kuikaa blauzi yako sawia.

3. Kwa mwanamke mwenye hipsi anashauriwa kuvaa nguo zinakazo mfanya hasionyeshe sana hipsi zake tofauti ya yule hasiekuwa na hipsi , maana yeye anatakiwa kuvaa nguo itakavyo onyesha hipsi zake , hata hivyo kwa wanawake wanene wenye hipsi hawana haja ya kujibana sana kwa sababu hipsi huweza kujitokeza zenyewe tu.

4. Lakini pia kuchagua rangi ya nguo nzuri pia husaidia kupunguza au kuongeza umbile la mtu, kuna rangi huweza kukufanya ukawa mnene sana au mwembamba sana,kwa mfano nguo zenye mistari ya kulala sio nzuri kwa watu wanene maana hutanua miili yao.Lakini pia rangi za giza hupunguza muonekano wa unene ilihali rangi za mwanga huangaza na kufanya mtu aonekane sana.

Zingaia:

-Ni bora zaidi katika kuchagua rangi nguo za rangi nyeusi na nyeupe iliyochanganywa ni nzuri zaidi inafanya muonekano wa mtu uonekane maridadi zaidi.

-Lakini pia jitahidi kuvaa viatu vinavyoendana na mwili wako ,sio lazima kuvaa kiatu kirefu wakati mwili wako hauimili mikikimikiki ya kiatu kirefu, flatshoes pia hupendeza zaidi kwa mtu mnene .

Madhara ya kuvaa miwani ya Urembo maarufu kama miwani ya Jua

Miwani za urembo maarufu kama miwani za jua zimetajwa kuwa na madhara kwa watumiaji wake kutokana na watu kutofahamu saizi za namba ambazo wanapaswa kuzivaa kabla ya kununua.

Akifafanua kwenye kipindi cha Supamix kinachorushwa East Africa Redio, Daktari Ningwa wa Upasuaji wa macho kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dk.Neema Daniel Kanyaro amesema watu wengi amekuwa wakivaa miwani pasipokjua kwamba zinaweza kuwasababishia matatizo ya kuona.

Dk. Kanyaro amesema kwamba watu wamekuwa wakivaa miwani za jua kama urembo pasipo kwenda kupima kujua ni aina gani ya miwani wanazotakiwa kuzitumia lakini pia bila kujua kama miwani hizo zina namba ambazo kila mtu ana namba kutokana na uono wake.

“Miwani ni dawa lakini usivae bila kupima kwani inaweza kukusababishia matatizo ikiwemo uoni hafifu. Unaweza kukuta unavaa miweani nyeusi lakini kumbe siyo namba yako. Kama hujijui unaweza kuta ukitazama unaona giza kumbe umeshaua macho kwa urembo” amesema.

Akizungumzia kuhsu presha ya macho Dk. Kanyaro amesema kwamba ugonjwa huo hauna dalili za moja kwa moja bali ni lazima kupima na huathiri watu wa rika zote.

Madhara ya Kuvaa viatu virefu

NI wazi kuwa viatu virefu huvutia sana vinapo kuwa vimevaliwa.Tulio wengi hasa mabinti au wanawake tunaokwenda na wakati hupenda kuvaa viatu virefu ilikuongeza muonekano wa umbile lako nikiwa na maana kuwa miguu huonekana yenye kuvutia zaidi unapo kuwa umevaa viatu virefu.

Kutokana na utafiti wa kitaalamu, mwanamke ana uwezo wa kutembea wastani wa hatua 10,000 kwa siku.Visigino virefu hufanya nguvu inayotumika kutembea hatua moja kuwa kubwa kuliko kawaida, huku vikikunyima raha ya kutembea kwa uhuru kiasi kwamba wengine hufikia hatua ya kuvua na kutembea peku.

Leo hii napenda kukujuza madhara ya uvaaji wa wa viatu virefu.Kwa kawaida, miguu ya binadamu hasa visigino, vimeumbwa ili kuuzuia uzito wa mwili juu ya ardhi.Uvaaji wa viatu virefu hufanya uzito wa mwili kubebwa na kisigino, hivyo uzito wa mwili kushindwa kuhimili uzito wote.

Matokeo yake husababisha misuli na mishipa ya miguu, kiuno, mgongo na shingo kufanya kazi kubwa ya kujaribu kusawazisha uzito.Kazi ambayo kwa kawaida hufanywa na visigino.Tatizo hilo hupelekea kiuno,Miguu na mgongo kuwa katika hatari ya matatizo ya kiafya pamoja na kuteguka na kuvunjika miguu.

Visigino virefu hubadili muundo wa mifupa ya miguu, hivyo hupelekea magoti na misuli ya mapaja kufanya kazi ya ziada ili kuupa mwili usawa.Kwa kuwa misuli inafanya kazi kubwa, uwezekano wa kupatwa na maumivu makali ya miguu na kushindwa kutembea katika siku za baadae huwa mkubwa zaidi. Visigino virefu husababisha maumivu ya visigino, damu kuvilia ndani ya miguu, mpangilio wa mifupa ya vidole kuvurugika, mishipa na misuli ya mapaja kuuma, neva za fahamu kufungana na kushindwa kufanya kazi yake.

Tatizo huendelea kwa vifundo vya miguu, magoti, na mifupa ya kwenye mapaja kushindwa kujivuta na kulegea na hivyo kusuguana wakati wa kutembea.

Jambo la kuzingatia kwa wale wanaopenda kuvaa viatu virefu,ni vema kama unapenda kuvaa viatu virefu hakikisha hutembei umbali mrefu kama una usafiri sio mbaya ukivaa viatu virefu,na kwa wale wanao kwenda ofisini jitahidi kuwa na viatu flati ndani ya mkoba wako ili unapokuwa umechoka unavua na kuvaa viatu vyako pia ukiwa ofisini waweza kuvua viatu virefu.

Mpenzi msomaji kama huwezi kutembelea viatu virefu nivema ukipitwa na wakati kuliko kujiabisha barabarani na kuonekana rimbukeni ikiwa wewe ni mjamzito epuka uvaaji wa viatu virefu.Usikose kujumuika nami katika safu hii ya urembo na mitindo.

Shopping Cart
22
    22
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About