AMINI UNA AKILI YENYE UWEZO MKUBWA WA KUBUNI WAZO LA KUWEZA KUKUSAIDIA KUFANIKIWA KIMAISHA

AMINI UNA AKILI YENYE UWEZO MKUBWA WA KUBUNI WAZO LA KUWEZA KUKUSAIDIA KUFANIKIWA KIMAISHA.

Huwa nikikaa na kufikiri ni namna gani binadamu aliweza kubuni ndege, meli kubwa hasa za mizigo, gari na vitu vinginevyo na badae kuja kuwa msaada mkubwa katika dunia yetu ya siku leo hata kurahisisha maisha katika eneo fulani lililokuwa na ugumu kwetu, basi nauona uwezo wa Mungu aliouweka ndani ya binadamu huyu ingawa yeye binafsi kama binadamu wakati mwingine hatulitambui hilo na kama tunalitambua basi ni wachache na wakati mwingine hatujakaa vizuri kuitumia hii fursa ya uwezo huo tuliopewa. Hii inaonyesha ni jinsi gani binadamu alivyo na uwezo mkubwa wa kufanya ubunifu kwa kupitia akili aliyonayo na kuleta mageuzi na mshangao mkubwa katika ulimwengu tunaoishi.

Hebu tazama wengi wa wabunifu waliojitoa kwa kuumiza akili na kubuni vitu vipya katika ulimwengu huu tunaoishi leo hii, ndio tunaowaona matajiri katika dunia hii ya leo kuliko watu wengine waliokataa kutumia uwezo na akili zao walizopewa na Mwenyezi Mungu na zaidi sana kubakia kulalamikia watu wengine wanaofanikiwa. Nataka nikuambie unauwezo mkubwa sana ndani yako unaoweza kuutumia ili kubuni jambo kubwa litakaloleta matokeo chanya na kuwa msaada mkubwa katika jamii yako unayoishi na kwako pia.

Ndio. Una uwezo mkubwa sana tena sana unaoweza kuleta matokeo chanya na makubwa katika ulimwengu wako na ukasahau hata habari ya kuajiriwa na kuanza kujiajiri binafsi kupitia jambo ulilobuni. Tatizo ni kwamba hupendi kutumia akili yako kufikiri kwa upana na kwa kiwango cha juu kwa hofu ya kupoteza muda, kuumiza akili, kutokutaka matatizo (stress), nakadhalika. Kila siku umekuwa ni mtu wa kusema “mimi sitaki kuumiza akili yangu” mara unasema “mimi masuala yanayochosha akili yangu siyataki” unataka kufanya mambo marahisi marahisi ili utoke kimaisha, ni gumu sana kwa namna hiyo rafiki.

“If you do what is easy your life will be hard, but if you do what is hard your life will be easy.” – Les Brown

Nataka nikuambie akili yako inauwezo mkubwa sana, narudia “inauwezo mkubwa sana” tena sana wa kubuni biashara ya kukutoa kimaisha, kutatua matatizo yaliyo magumu kwa jamii iliyokuzunguka, kuleta mbinu na mikakati mipya kwenye kazi au ofisini ili kusaidia kampuni kusimama, nakadhalika. Tatizo unajitetea na kujenga hofu kubwa ndani yako ya kujitoa na kufikiri ili kuhakikisha unaleta matokeo mapya na makubwa mahali ulipo muda huu. Hebu fikiri kama binadamu huyu huyu unayemjua na aliye kama wewe alibuni balbu za umeme anaitwa Thomas Edison kutoka nchini Marekani; na zaidi sana binadamu huyu huyu kama wewe aliweza kugeuza historia ya muonekano wa magari na kuja na kitu kipya zaidi anaitwa Henry Ford, na binadamu huyu huyu aliweza kubuni biashara ya kuuza kuku walioandaliwa kama chakula na hatimaye kuwa na mgahawa mkubwa wa KFC uliosambaa karibu nchi 123 duniani kote anaitwa Harland Sanders. Na wengine wengi sana ambao sitaweza kuwamaliza kwa kuwataja wote mahali hapa siku ya leo.

Naamini wapo watu wanaoweza kujitetea na kusema kwa kuwa hao ni watu weupe yaani wazungu na sijaona mtu mweusi hata mmoja hapo. Hebu fikiri ni watu wangapi wanabiashara ambayo leo hii inawaingizia mabilioni ya pesa na wakati mwingine biashara wanazozifanya ni za kawaida na zilizokuwa zikidharaulika na watu kwenye jamii zao na wapo hapa afrika. Angalia mtu kama Aliko Dangote kwa sasa zaidi ya kujishughulisha na uzalishaji wa cement na bidhaa nyingine za ujenzi na hata biashara zake kubwa nyingine kwa sasa ameenza kuzalisha nyanya na kuuza kwenye nchi yake huko nchini Nigeria. Ulitegemea mtu kama huyu ambaye ni tajiri wa kwanza afrika kuwaza kufanya biashara kama hiyo ya nyaya kwa sasa? Yawezekana wewe ulipoambiwa kuuza nyanya uliona ni biashara kichaa na haina maana ya kuifanya. Ukweli ni kuwa usipende kuanzia pakubwa bali anza na madogo ili kukupeleka kwenye kilele chako cha mafanikio na kutimiliza ndoto yako uliyonayo.

Hivyo hivyo kwa Bakhresa, Mengi, Dewji, Sheria Ngowi na wengine wengi tunaowaona nchini mwetu Tanzania wamefanikiwa kiuchumi, hii yote ni kutokana na kuamua kubuni kitu kipya kilichoweza kuwa msaada mkubwa kwenye jamii yao na kuweza kuwaletea wao mafanikio makubwa katika maisha yao. Sheria Ngowi pamoja na kusomea masuala ya Sheria nchini India lakini alijua bado ana kitu cha ziada ndani yake kinachoweza kumlipa na kumfanya awe na uhuru wa kifedha na maisha mazuri sawa na anavyotaka. Leo hii ni mbunifu wa mavazi Africa nzima inamjua na kumtazama. Jiulize kama asingetumia akili yake kwa kufikiri zaidi na kufuata ndoto yake aliyokuwanayo leo hii ingekuwaje kwake na kwenye jamii yake iliyohitaji mchango wake?

Nataka nikuambie huwezi kutoka kwa siku moja ni lazima uumize kichwa na akili yako leo hii na kujua ni nini cha kufanya kinachoweza kukupa uhuru unaoutaka kesho. Na suala la kuumiza kichwa chako na akili ni sasa na si kesho, narudia tena suala la kuumiza akili yako kwa ajili ya kubuni wazo la kukutoa kimaisha “ni sasa na si kesho” kama unavyofikiri. Usiridhike na maisha yako unayoishi leo, usiridhike na kipato unachokipata huku sema ukweli ndani ya moyo wako na kwa uhalisia hakikutoshelezi kabisa kufikia kwenye kilele cha mafanikio makubwa unayoyataka. Usikubali kuwa mvivu wa kuumiza kichwa na kutumia akili yako kwa ajili ya kuja na kitu kipya kinachoweza kuleta manufaa kwako na kwa jamii yako iliyokuzunguka, anza kuwa mbunifu ili uweze kufikia ndoto yako ya maisha.

Umiza kichwa kuanzia sasa na amini katika wazo (idea) utakayoipata ndani ya moyo na akili yako ili kukusaidia na wewe kuwa miongoni mwa watatuzi wa matatizo katika ulimwengu huu. Unaweza kutumia matatizo yaliyopo kwenye jamii yako kama sehemu ya kukupatia wazo jipya na baada ya hapo kubuni njia na mkakati wa kulitatua tatizo ili kuleta matokeo chanya katikati ya watu waliokuzunguka na kwako pia. Mwombe Mungu akupe mwongozo wa kukusaidia kulitimiza na kulifanya hilo wazo (idea) kuwa wazi katika ulimwengu wa nje ili usibaki na wazo lililo kwenye akili na kichwa tu pasipo kuleta matokeo na mchango wowote makubwa kwa watu wako.

Nakusihi usisubiri kesho. Usione una siku nyingi za kuwaza au kuleta matokeo (ku_implement) ya hilo wazo lako (idea) uliyonayo au ndoto ya siku nyingi unayotembea nayo kila kukicha pasipo kuweka vitendo vya kuifanya izae faida na matunda kwako. Anza leo kuhidhilishia dunia kuwa nawe unauwezo mkubwa aliouweka Mungu ndani yako. Usijikatae wala usiogope kukataliwa na wengine pale utakapofanya uamuzi wa kuja na kitu chako kipya kwenye jamii yako, kumbuka kukataliwa ni sehemu ya kukupeleka katika mafanikio. Kadri unavyoongeza kukataliwa ndio unavyoongeza kufanikiwa.

Kama unahitaji kuwa mbunifu wa mavazi kama sheria ngowi anza kubuni leo hii au ikibidi mtafute na uwe chini yake na afanyike kuwa msaada na mshauri wako (mentor) wa hicho kitu unachotaka kukifanya. Amini inawezekana kwani watu waliofanikiwa si wachoyo unapojishusha na kuonesha uhitaji wa kujifunza kutoka kwao. Kama unataka kuwa mfanyabiashara mkubwa kama Dangote lakini bado huna wazo la biashara. Basi elewa una uwezo mkubwa wa kuumiza kichwa na akili kuanzia sasa na ukapata wazo linaloweza kuishangaza dunia yote hapo badae.

Lakini kumbuka si lazima ukaja na kitu kipya kabisa kwani tambua unauwezo pia wa “kuboresha wazo” au kitu fulani kinachofanyika na watu wengine ila wewe ukaleta ubunifu mpya kwenye hicho kitu na kuleta utofauti mkubwa kwenye eneo (industries) hiyo. Na hii ndio njia inayofanyika kwenye makampuni ya simu, magari, televisheni, nakadhalika. Leo hii samsung akileta simu yenye kamera yenye uwezo wa mega pixel 16 kesho yake utasikia Iphone ametoa simu yake mpya yenye kamera yenye uwezo wa mega pixel 20. Huu ni ubunifu tu ili kuzidi kutawala soko na kuteka wateja wa soko la simu ulimwenguni kote. Nataka nikuambie nawe unauwezo wa kufanya ubunifu mkubwa kwenye jambo lolote lile ili kukuletea mafanikio makubwa na hatimaye ukafanikiwa kufikia katika ndoto yako.

Nataka nikuambie una mawazo milioni na zaidi ndani yako ambayo hadi sasa dunia inayasubiri ili yaweze kuwa msaada kwa watu wengi na kufanyika kuwa faraja kubwa hata kwa watu waliokata tamaa. Ndio. usishangae wala sijakosea kusema ni mawazo “milioni na zaidi” uliyonayo ndani yako. Ni wewe tu umejidharau, ni wewe unajiona huwezi kuwaza na kutoka na kitu kipya au kilichojaa ubunifu, ni wewe tu unajaa hofu ya kukataliwa kisa unaona utaonekana unaiga, huigi kwani hata waandishi wanaoandika kama mimi wanaandika kutokana na walichokipitia kwenye maisha na kujifunza kwa wengine, ni wewe tu unajiona huna lolote na si chochote katika ulimwengu huu hivyo huwezi kufanya mambo makubwa. Unajikosea heshima kwa kujiwiza mawazo hayo ya chini na kumkosea Mwenyezi Mungu yeye aliyekuumba na kukupa akili zote timamu ili uzitumie kwa ajili ya kuwaza na kubuni mambo mapya yanayoweza kuwa msaada mkubwa kwako na kwa jamii yako iliyokuzunguka. Anza kuwaza na kuumiza akili na kichwa chako leo hii, na amini kesho utafanikiwa.

JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.

Melkisedeck Leon Shine

Editor: Melkisedeck Leon Shine. About Me | Contact Me | LinkedIn | TikTok | WhatsApp

Read and Write Comments

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Shopping Cart