Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu. Zab 95:7-8
Tunaalikwa kutubu na kumrudia Mungu kwa Mioyo yetu yote na kwa nia dhabiti. Mungu ni mwaminifu, atatusamehe dhambi zetu na kutufanya kuwa wapya.
Dawa ya dhambi ni kutubu na kusamehewa.
Kutubu sio kusema tuu “Ninatubu” au “Ninaomba msamaha”. Kutubu ni kuona uchungu kweli rohoni kwa dhambi tulizotenda, tukizikataa na kunuia kutokuzitenda tena.
12“Lakini hata sasa,”
nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
“Nirudieni kwa moyo wote,
kwa kufunga, kulia na kuomboleza.
13Msirarue mavazi yenu kuonesha huzuni
bali nirudieni kwa moyo wa toba.”
Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu;
yeye amejaa neema na huruma;
hakasiriki upesi, ni mwingi wa fadhili;
daima yu tayari kuacha kuadhibu.
14Huenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atabadili nia
na kuwapeni baraka ya mazao,
mkamtolea sadaka za nafaka na kinywaji.
15Pigeni tarumbeta huko Siyoni!
Toeni amri watu wafunge;
itisheni mkutano wa kidini.
16Wakusanyeni watu wote,
wawekeni watu wakfu.
Waleteni wazee,
wakusanyeni watoto,
hata watoto wanyonyao.
Bwana arusi na bibi arusi
na watoke vyumbani mwao.
17Kati ya madhabahu na lango la hekalu,
makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu,
walie na kuomba wakisema:
“Wahurumie watu wako, ee Mwenyezi-Mungu.
Usiyaache mataifa mengine yatudharau
na kutudhihaki yakisema,
‘Yuko wapi basi Mungu wao?’” Yoeli 2:12-17
Uzuri wa Mungu ni kwamba anasamehe na kusahau, tunapotubu dhambi zetu Mungu anatufutia makosa yetu, anaponya majeraha au madhara yaliyoletwa na dhambi hiyo na kisha antubariki kwa Neema na Vipawa vya kusonga Mbele.
Maana nitawasamehe makosa yao, wala sitazikumbuka tena dhambi zao.” Yeremia 31:34
Mungu anatambua kwamba Binadamu ni dhaifu na anaweza kuanguka dhambini ndio maana anatupa nafasi ya Kutubu na Kumrudia yeye.
13Afichaye makosa yake hatafanikiwa;
lakini anayeungama na kuyaacha atapata rehema. Methali 28:13
Mungu anazifahamu juhudi zetu katika kutafuta kutenda mema ndio maana anakubali toba ya kweli na anatupa matumaini ya kusonga mbele.
“Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”. Isaya 1:18
Biblia inatuambia kuwa anaheri yule atubuye na kusamehewa kosa lake kwa sababu hana hatia mbele ya Mungu.
1 Heri yake mtu aliyesamehewa kosa lake,
mtu ambaye dhambi yake imeondolewa kabisa.
2Heri mtu ambaye Mwenyezi-Mungu hamwekei hatia,
mtu ambaye hana hila moyoni mwake. Zaburi 32:1-2
Tunapaswa kukumbuka kuwa toba ya kweli ya kutupa msamamaha inaambatana na kuwasamehe wengine na kuondoa kinyongo kwa wengine waliotukosea. Yesu anatufundisha kuwa inatupasa tusamehe ili na sisi tusamehewe.
14“Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia. 15Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu. Mathayo 6:14-15
Tena, Mungu anatusamehe Makosa Yetu bila kujali tunakosea Mara nagpi na tunarudi kwake mara ngapi. Ndio maana Yesu alitufundisha kuwa tunapokosewa na wenzetu ni lazima tuwasamehe haijalishi wametukosea mara ngapi.
3Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, muonye; akitubu, msamehe. 4Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema, ‘Nimetubu,’ lazima umsamehe.” Luka 17:3-4
Unapotubu na kuomba msamaha ni sharti uwasamehe pia wale waliokukosea ili na wewe usamehewe. Kusameheana na wenzetu ndio tabia ya Kimungu ambayo yatupasa kujifunza na kuiishi ili na sisi tuwe watoto wema wa Mungu.
12Nyinyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe nyinyi. Wakolosai 3:12-13
Tumuombe Mungu atujalie Moyo wa toba na kujirudi kwake Kila tunapokosea. Na tumuombe pia atupe nguvu na uwezo wa kuwasamehe wale wanaotukosea.
KUMBUKA: Unapotubu dhambi zako na kusamehewa ndipo inapokuwa rahisi kwa sala zako kujibiwa. Mungu ni rafiki ya waliosafi Moyoni, na ndio anaowasikiliza na kuwaonyesha nguvu na uwezo wake.
Nakualika kwa Sala ya Toba, uweze kurudi kwa Mungu. Sali kutoka moyoni, kwa kujua kuwa unapendwa na Mungu, Kwa Imani na Matumaini Kwake.
Sala ya Toba
Mungu wangu, Baba wa mbinguni, nakuja mbele zako nikiwa na moyo uliovunjika na toba ya kweli. Nakiri kuwa mimi ni mwenye dhambi, na nimekosa mbele zako kwa njia nyingi. Nimefanya mambo ambayo hayakupendeza, na nimeshindwa kutenda yale uliyoniagiza. Kwa kuwa Neno lako linasema, “Kwa maana wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23).
Ee Bwana, naomba unisamehe dhambi zangu zote. Nimetenda dhambi kwa mawazo, kwa maneno, na kwa matendo. Ninatubu kwa dhati na kwa kweli kutoka moyoni mwangu. Naomba unioshe kwa damu ya Yesu Kristo, Mwanao mpendwa, ambaye alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu. Kama unavyosema katika Neno lako, “Lakini ikiwa tutatembea katika nuru kama Yeye alivyo katika nuru, tu ushirika sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote” (1 Yohana 1:7).
Ninakiri kuwa mimi ni mnyonge bila wewe, na siwezi kufanya lolote bila msaada wako. Naomba unijaze na Roho Mtakatifu, aniongoze na kunipa nguvu ya kushinda majaribu na dhambi. Ee Mungu, niongoze katika njia zako za haki, na unisaidie kuishi maisha yanayokupendeza. Kwa kuwa Neno lako linasema, “Basi kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu” (Wakolosai 3:1).
Ninakuja mbele zako nikiwa na unyenyekevu na moyo wa toba. Naomba unirehemu na unifanye kuwa kiumbe kipya ndani ya Kristo. Kama unavyosema katika Neno lako, “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama! yamekuwa mapya” (2 Wakorintho 5:17). Asante kwa upendo wako usio na kikomo, na kwa neema yako inayotosha kila siku. Naomba haya yote kwa jina la Yesu Kristo, aliye Mwokozi wangu.
Bwana, naomba unifundishe kuwa mtiifu na kuwa na moyo wa shukrani kwa kila jambo. Acha neno lako likae kwa wingi ndani yangu, na linibadilishe kutoka ndani hadi nje. Nisaidie kuacha njia zote za dhambi, na kuwa mwaminifu kwako katika kila hali. Kwa kuwa Neno lako linasema, “Neno lako nimeliweka moyoni mwangu, nisije nikakutenda dhambi” (Zaburi 119:11).
Ninakubali kuwa mimi ni mnyonge na ninahitaji msaada wako kila siku. Nakiri dhambi zangu na naomba unisamehe. Naomba unipatie moyo safi, na kunifufua kiroho. Kama unavyosema katika Neno lako, “Ee Mungu, uniumbie moyo safi, unirejeshee roho iliyotulia ndani yangu” (Zaburi 51:10). Naomba unifanye kuwa mwanga na chumvi duniani, ili niweze kuonyesha upendo wako kwa wengine. Kwa kuwa Neno lako linasema, “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima” (Mathayo 5:14).
Asante, Bwana, kwa kusikia sala yangu. Naamini kuwa umesikia na kujibu ombi langu. Ninatangaza kuwa mimi ni wa Kristo, na ninakubaliana na mapenzi yako maishani mwangu. Kama unavyosema katika Neno lako, “Ninaweza kufanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” (Wafilipi 4:13). Kwa jina la Yesu, Amina.
Recent Comments