Ukishatambua kwamba una mimba kuna mambo mbalimbali tofauti ya kufanya. Kwanza kabisa mweleze mwenzi wako na mshauriane hatua zipi mchukue. Pia, kwa msichana mdogo lazima uwaeleze wazazi wako. Siyo rahisi kuwaambia wazazi, kwa sababu hawatafurahi kuhusu ujumbe huu. Lakini uhusiano mzuri na wazazi unaweza kuwasaidia sana katika kulea mimba na baadaye mtoto.
Kwa upande wa kiafya ni muhimu sana kuanza kuhudhuria kliniki au hospitali mapema, yaani kabla ya mimba kufikisha miezi mitatu. Hii huwawezesha wataalamu kukupima na kukupa ufafanuzi kuhusu afya yako na maendeleo ya mimba. Vilevile wanaweza kugundua matatizo kama yatakuwepo na kukutibu mapema. Kwa usalama wako na usalama wa mtoto hakikisha kuyafuata maelekezo ya wataalamu kila mara.
Wasichana au wanawake wengine wanafikiria kutoa mimba mara tu wanapokuta wamepata mimba bila ya kupangilia. Kutoa mimba ni jambo la hatari sana na linaweza kuleta madhara kiafya kwa mwanamke, na hasa utoaji mimba unaofanywa na mtu ambaye hakusomea na pia katika mazingira yasio safi.
Recent Comments