Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

Thamani ya Kazi ya Upadre

UPADRE NI KAZI YA PEKEE YA HEKIMA, UWEZO NA MAPENDO YA UMUNGU WA KRISTU. KAMWE USIMSHAMBULIE PADRE. “Yesu Maria na Yosefu nawapenda, ziokoeni Roho. KUMTETA PADRE [Haya ni maelezo ya Bwana wetu kwa Mutter Vogel.] ” Kamwe mtu asimshambulie Padre hata anapokuwa katika makosa badala yake umwombee na fanya toba ili niweze kumpa tena NEEMA.
Ni yeye peke yake anaye niwakilisha mimi hata awe haishi kulingana na mimi. Endapo Padre anaanguka tumnyoshee mkono wa msaada kwa njia ya SALA na sio KUMSHAMBULIA. Ni mimi pekee nitakuwa HAKIMU wake si mwingine ila mimi”. “Mtu yeyote anapotamka HUKUMU dhidi ya padre ananihukumu mimi”. 
Mwanangu kamwe usiruhusu padre ashambuliwe, jitahidi kuwa upande wake na umtetee”. Mwanangu kamwe usimhukumu mwungamishi wako bali umwombee sana na tolea KOMUNIO TAKATIFU kwa ajili yake, kila siku ya ALHAMISI kupitia MIKONO au MAMA YANGU MTUKUFU. 
Tena kamwe usikubali neno lolote la kumdhalilisha Padre na kusema neno baya dhidi yake (yao), HATA KAMA INGELIKUWA NI KWELI! Kila Padre ni WAKILI wangu na moyo wangu utahuzunika na kusikia uchungu kwa ajili hiyo. Usikiapo HUKUMU dhidi ya Padre, sali SALAMU MARIA. Umwonapo Padre anayeadhimisha MISA TAKATIFU akiwa katika halo isiyostahili, usiongee nae lolote kumhusu yeye bali nieleze mimi tu! Huyo huwa nasimama naye ALTERANI”. ” Oh waombeeni mapadre wangu ili watamani USAFI NA WEUPE WA ROHO kuliko jambo lolote ili waweze kutolea sadaka TAKATIFU kwa moyo na mikono iliyotakata. Ni ukweli kwamba Misa ni ile ile hata ikiadhimishwa na Padre mwenye hali isiyostahiki lakini NEEMA zinazowashukia watu sio zile zile. [MARIA, MALKIA WA MAPADRE UWAOMBEE.]

Nafasi ya Bikira Maria Katika Kanisa Katoliki

Kanisa katoliki linamthamini Bikira Maria kama Mama wa Mungu, Mama wa Kristu, Mama wa Mkombozi pia Mama wa uhai kuna maneno kadhaa hutumika pia kufafanua zaidi hiyo heshima mfano HYPERDULIA zaidi ya…. Bikira Maria tunamheshimu zaidi ya watakatifu, PROTODULIA ikiwa na maana ya heshima kwa Bikira Maria zaidi ya Mt. Yoseph na pia LATRIA likiwa na maana ya heshima kwa Mungu peke yake kwani ndani yake kuna kunakuabudu pia!!!
🌻Bikira Maria anatuelekeza kwa mwanae kama alivyo waelekeza waliokuwa harusini kana lolote atakalo waambieni fanyeni Yoh.2:5
🌻Bikira Maria ni Mama wa uhai, mlei, muuguzi wa kwanza/ muhudumu wa kwanza alienda kwa haraka kuanzisha kliniki ndogo nyumbani mwa Zakaria amhudumie Elizabeti Mama wa Yohane Mbatizaji aliyekuwa mjamzito
🌻Tunasema Bikira Maria ni mzazi bora wa kuiga kwani alitetea uhai, Mama huyo hakutoa mimba japo misuko suko ilikuwa mingi Mfano maneno ya pembeni ya watu kwa vile mimba haikuwa ya Yoseph mumewe, hali mbaya ya uchumi na ukiangalia hivyo Familia takatifu ya Maria na Yosefu haikuwa na hali nzuri kifedha Lk. 2:22-24 Bikira Maria alivumilia hali hiyo kwani angetoa angemuua Mkombozi wetu, na sababu hizo ndizo hata dunia ya leo zina wafanya watu watoe mimba Ikiwa kutoa ni kuua na hatimaye tunapoteza
-Mama wa watoto wa kesho
-Baba wa watoto wa kesho
-Padre wa kesho
-Mtawa wa kesho
-Raisi wa kesho n.k
🌻Bikira Maria alikombolewa kwaajili ya mastahili ya mwanae tena kwa namna ya pekee sana, aliangaliwa na…..
-Baba kama Binti yake Mpenzi
-Mwana, mama mheshimiwa
-Roho Mtakatifu, hekalu lake
SWALI: Sisi nasi kama tunaamini heshima anayopaswa kupewa Bikira Maria ni sawa na kwamba pia sisi tunaelewa kwamba tumekombolewa kupitia yeye?
Nafasi ya Bikira Maria Katika Biblia ya kanisa katoliki
🌻Sisi kama wanakatoliki tunasema Bikira Maria ni Mama wa Mungu kweli kwa kzingatia mambo makuu mawili ambayo ni kama ifuatavyo:
1. Kwanza lazima Bikira Maria awe mama halisi wa Yesu
2. Pili ni kuwa Yesu aliyemzaa Ni Mungu.
1. BIKIRA MARIA NI MAMA HALISI WA YESU
🌻Sote tunapaswa kufahamu kama kweli BiKira Maria ni Mama halisi wa Yesu kupitia vifungu vifuatavyo na hii ndio nguzo pekee ya kujinasua katika makundi yasiyo amini kama Bikira Maria anastahili heshima twende pamoja sasa:
-Lk. 1:30-31 neno linasema
Malaika akamwambia ‘ usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu, tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume na jina lake utamwita Yesu kwahiyo ni dhahiri kwamba huyu ni mama halisi wa Yesu ambae sisi tunamuimba kila leo.
-Mt. 1:18 neno linasema:
kuzaliwa kwake Yesu Kristu kulikuwa hivi: Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu huu ni ushahidi tosha kuwa Bikira Maria ni Mama halisi wa Yesu kwani ndiye aliye pewa hadhi zaidi ya wanawake wote kuzaa kitakatifu Mwana wa Mungu.
-Rom 1:3 neno linasema hivi
yaani habari za mwanawe, aliye zaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili ikikumbuka wakati tunasali nasadiki kama sehemu ya kuikiri imani yetu kuna maneno huwa tunatamka kwamba akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria, akawa mwanadamu hivyo ni connection nzurii sana kwetu kuendelea kumheshimu Mama yetu Maria kwa kutuunganisha na Mungu kwa ubinadamu wetu!
-Nabii Isaya 7: 14 anatabili:
kwahiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara, tazama , Bikira atachukua mimba , atazaa mtoto mwanamume naye atamwita jina lake Imanueli(yaani Mungu pamoja nasi tazama maneno haya yalitabiliwa na Nabii huyu juu ya mama huyu Mtakatifu atakavyo tuletea ukombozi kwann tusimheshimu na kumtetea mpaka tunapotoshwa?
– Mate 1:14 neno linasema
hawa wote walikuwa wakidumu kwa Moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake na mariamu mama yake Yesu na ndugu zake wanawake wengine walihesabiwa pamoja lakini mama Maria anasemwa kwa upeke yake ktokana na uzito wake kupita wanawake wengine kwani ndiye mama wa Yesu Kristu ni heshima kubwa!!!
2. Yesu ni Mungu na Bikira Maria ni Mama wa Mungu
🌻katika sehemu ya jambo letu la pili ni kwamba je alichozaa Mama Maria ni Mungu? Kama ni muhimu kujua hilo hebu tuone uthibitisho wa hili kupitia baadhi ya vifungo bdani ya Biblia zetu ambazo pia wenzetu wanaopinga Habari ya mama yetu Maria waone twende pamoja:
-Yoh. 1:1-2 neno linasema
hapo mwanzo kulikuwako Neno naye Neno alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu Huyo Mwanzo alikuwako kwa Mungu kwa maneno hayo na ukiendelea kusoma ukitafakari utaona anaezungumziwa na Yesu Kristu ambaye ndie nuru halisi ya ulimwengu ni ndie uzima wetu kwa Mungu na huyu Yesu basi alizaliwa na Bikira Maria hivyo alichozaa Maria ni Mungu kweli.
-Rom 9:6 neno linasema:
ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya Mwili, ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu mwenye kuhimidiwa milele. Amina hayo ni maneno yanayo tambulisha koo ya kibinadamu kwamba ndiko pamoja ubinadamu wetu amezaliwa Mungu soma injili ya mtakatifu Mathayo sura ya kwanza aya ya kwanza na kuendelea habari za ukoo wa Yesu naamini hapa Tmcs tunapasikia sana!!!
– Fil 1:6-7 neno linasema:
nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu nakuendelea……….. maneno hayo yanaonyesha kuwa Kristo ndie mambo yote katika kuupata uzima wa milele na huyu anae onekana ni mwisho wa yote amaezaliwa na Mwanamke Maria.
-Mitume nao walikiri kuwa Yesu ni Mungu mtu Yoh. 20:28
Tomaso akajibu, akamwambia Bwana wangu na Mungu wangu kutokana na matendo na kazi ya Yesu Kristu iliwafanya mitume waone kuwa ufalme wake sio wa dunia hii tu bali ni wa milele na kazi yake ni Takatifu na sio hapo tu kumbuka pia wale wanafunzi walio kuwa wanasema yatufaa sasa tujenge vibanda vitatu kimoja cha Musa na kingine cha Eliya mara sauti ikasikika ikisema huyu ni mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye na mara akageuka sura maneno hayo ilikuwa ni uthibitisho juu ya umungu wa Yesu Kristu ambaye huyu alizaliwa na Bikira Maria.
– Lk. 1:35 neno linasema
Malaika akajibu akamwambia “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako , na nguvu zake aliyejuu zitakufunika kama kivuli, kwasababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu mwana wa Mungu” haya maneno ni dhahiri yanatufundisha kwamba Bikira Maria alimzaa Mungu katika ubinadamu wake.
-Gal. 4:4 neno linasema:
huyu ni mwana wa Mungu, ni mwana wa mwanamke, huyo mwana wa Mungu, pia ni mwana wa Maria tuseme nn sasa tusiyumbishwe yumbishwe na maneno yasiyo na tija juu ya mama Maria kwani kupitia yeye tunakuwa salama katika Roho na Mwili
Maneno ya Busara
-Mt. Germanus alishwahi kusema *Maria mahali pa kuishi pa Mungu*
-Mt. Jerome alisema Maria Hekalu la mwili wa Bwna
-Martine Luther, hata baada ya kujiengua kutoka kanisa katoliki alikiri kuwa Bikira maria ni Mama wa Mungu akisema:
hakuna jambo kubwa zaidi ya hili kuwa Bikira Maria alipata kuwa Mama wa Mungu ambalo kwalo zinatoka zawadi(heri) kubwa na Nyingi ambazo amepewa inakuaje leo tusione umhimu wa heshima kwa mama huyu?
-Mt. Bernado alisema Maria alimpendeza Mungu kwa ubikira wake, na alichukua mimba kwa unyenyekevu wake
MWISHO: FUNDISHO MAISHANI
– Sote ambao tupo chini ya utawala wa Yesu Kristo tunawajibu wa kutetea uhai kwa nguvu zote tukipiga marufuku utoaji mimba kwa visingizio mbalimbali
– Eva alishindwa kumtii Mungu akaleta mauti lakini Bikira Maria alitii kubaki mwamnifu na kumtunza Kristu na hatimaye ameleta uhai na neema zote , akina dada na mama zetu igeni mfano wa Maria na Elizabeti katika malezi bora!!
-Sisi sote tuliowabatizwa tunapapaswa kuwa wanyenyekevu kama Maria na familia yao yote kwani unyenyekevu umejengwa juu ya upendo pia ni mama wa fadhila nyingi utii, uchaji, ibada, uvumilivu, kiasi, upole na amani.

Je, Bikira Maria ni Bikira Daima au alizaa watoto wengine?

Jibu fupi ni kwamba Bikira Maria hakuzaa watoto wengine na hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu
Hapo zamani hakuna mkristu au dehebu lolote lililokuwa linapinga kuwa Bikira Maria sio Bikira Daima hata Waprotestanti/walokole waliamini Bikira Maria ni Bikira Hata Baada ya Kumzaa Yesu. Kwenye Miaka ya 1400-1600 Watu wote wakwanza waliopinga Kanisa Katoliki walikubali kuwa Bikira Maria ni Bikira daima wakiwemo Martin Lutha aliyeanzisha kanisa la Lutheran, John Calvin aliyeanzisha Ulokole/Protestanti, Mchungaji Ulrich Zwingli, Heinrich Bullinger, and Thomas Cranmer. Kwa miaka zaidi ya 350 Waprotestant/walokole waliendelea kuamini kuwa Bikira Maria ni Bikira Daima.
Lakini baadae wakristo wengi walianza kupinga kuwa Bikira Maria ni Bikira Daima.

Tunaweza kuthibitisha kuwa Bikira Maria hakuzaa watoto wengine kwa kunukuu Biblia Kama ifuatavyo;

1. Bikira Maria Alikuwa Bikira Kabla ya kumzaa Yesu

Biblia inatuambia wazi kwamba Bikira Maria alikuwa Bikira Kabla ya kumzaa Yesu Kama tunavyosoma katika Luka 1:26-35
26 Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27 kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28 Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe.” 29 Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30 Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31 Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33 Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” 34 Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?” 35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. (Luka 1:26-35)

2. Biblia Haiwataji ndugu wa Yesu wakati Yosefu na Maria walipokimbilia Misri kumficha Yesu na wakati waliporudi

19 Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, 20 akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumwua mtoto huyo wamekwisha kufa.” 21 Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea katika nchi ya Israeli. 22 Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao mwanawe Herode alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda katika mkoa wa Galilaya, 23 akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: “Ataitwa Mnazare.” Matayo 2:19-23
Kama wangekuwepo wadogo zake Yesu Biblia ingetuambia kwamba walikuwa wapi wakati huo na walikuwa na Yesu au la.

3. Biblia haituambii kuwa Yesu alikua na wadogo zake alipokuwa na miaka 12

Wakati wa Maria, Yoseph na Yesu walipoenda Yerusalemu Yesu akiwa na miaka 12 Biblia haituambii kuwa Yesu alikuwa na wadogo zake na walikuwa wapi. Kumbuka walikuwa na Desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka kwa ajili ya Pasaka familia nzima kama familia. Je hao watoto wengine walikuwa wapi. Kwa nini walikuwa na Yesu Mwenyewe? Maana yake ni kwamba Yesu hakuwa na Wadogo zake.
41 Wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. 42 Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43 Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. 44 Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. 45 Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta. 46 Siku ya tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. 48 Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, “Mwanangu, kwa nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni.” 49 Yeye akawajibu, “Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” 50 Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia. 51 Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. 52 Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu. (Luka 2:41-52).
Kwa hiyo Biblia haionyeshi kuwa Yesu alikuwa na kaka na dada wakati akiwa na miaka 12. Kama wangekuwepo wangetajwa hapa kuwa walikuwa pamoja na Wazazi wao kama Yesu au walikuwa na Yesu wakati anapotea. Biblia haituambii chochote kwa hiyo wakati huo hapakuwa na wadogo zake Yesu.

4. Kukosekana kwa neneo “Binamu” kwenye lugha ya Yesu

Wakristu wa kwanza pamoja na Yesu aliongea Kiaramaiki au Kiebrania. Katika lugha zote hizo hakuna neno “Binamu” kwa hiyo mabinamu walijulikana kama dada na kaka wa mtu. Kwenye Agano jipya Neno kaka na Dada lilitumika pia kuwakilisha binamu.
Biblia inapotuambia kuwa Kaka na dada zake Yesu haimaanishi kaka wa kuzaliwa bali ndugu au Binamu
55 Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?” (Mathayo 13:55-56)
Kwa hiyo wanaotajwa hapa ni ndugu wa Yesu kwa maana maneno kama; ndugu, kaka au dada lilitumika badala ya Binamu yaani mtoto wa shangazi au mjomba. Hapa juu Yosefu ametajwa kama kaka yake Yesu lakini tunajua kuwa Yosefu ni Baba yake Yesu. Baba na mwana hawawezi kuwa na jina sawa.

5. Biblia haitumii neno Ndugu, kaka au dada ikimaanisha ndugu wa kuzaliwa mama mmoja na baba mmoja

Sio mara zote Biblia imetumia neno Ndugu kumaanisha ndugu (Dada na Kaka) wa kuzaliwa yaani kaka na dada kwa mfano
Kwa kuangalia lugha ya Kiswahili na Kiingereza 1 Wakorintho 15:6 tunaona tafsiri tofauti.
KISWAHILI 6 Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa.
ENGLISH 6 After that, he appeared to more than five hundred of the brothers and sisters at the same time, most of whom are still living, though some have fallen asleep.
Kwa hiyo hapa neno kaka dada na ndugu linaonekana wazi halikumaanisha ndugu au kaka wa damu.

6. Undugu wa Yakobo, Simoni, Yosefu na Yuda kwa Yesu Sio wa mtu na kaka zake

Wasemao kuwa Bikira maria alikuwa na wana zaidi ya Yesu wananukuu kifungu hiki;
55 Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?” (Mathayo 13:55-56)
Kumbuka kulikuwa na Yakobo wawili wakati wa Yesu, Vifungu vifuatavyo yunaweza kuona kuwa kulikuwa na yakobo wawili ambao walikuwa ndugu za Yesu lakini sio kaka wa kuzaliwa kwa mama.
35 Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.” (Marko 10:35)
55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. 56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. (Matayo 27:55-56)
Tunaweza kuona Undugu huu na Yesu kwa kusoma;
19 Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. (Wagalatia 1:19)
Lakini Yuda anasema;
1 Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, nawaandikia ninyi mlioitwa na Mungu na ambao mnaishi katika upendo wa Mungu Baba, na katika ulinzi wa Yesu Kristo. (Yuda 1:1)
Kwa hiyo Yakobo na Yohane walikuwa watoto wa Mama mwingine ambao baba yao ni Zebedayo. Na Yakobo na Yosefu walikuwa watoto wa Maria Mwingine. Kwa hiyo ni Yakobo wa wili wa Mama wengine Tofauti na Maria. Yuda alikuwa ni ndugu yake Yakobo. Yakobo vilevile alikuwa ndugu yake Yesu.
Kuthibitisha kuwa Hawa kina Mama ndio waliokuwa Mama zao kina Yakobo wote hao wawili na wengine tunaweza kusoma;
25 Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene. (Yohana 19:25)
Kwa hiyo kwenye (Yohana 19:25) tunaona Kuwa ni kwenye Msalaba wa Yesu alikuwepo Mama yake Yesu (Bikira Maria), Dada yake Bikira Maria, Mke wa Cleopa na Maria Magdalena. Na kwenye (Matayo 27:55-56) wamwtajwa ni Mama za kina nani kama inavyoonekana kwenye kifungu kifuatachi;.
55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. 56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. (Matayo 27:55-56).
Kwa hiyo hii ina maanisha kulikua na wanawake watatu wenye majina sawa ya Maria waliokuwa chini ya Msalaba. Yakobo na Yuda walikuwa watoto wa Maria Mke wa Cleofasi, na sio Mama wa Yesu, na hivyo sio kaka za Yesu.

7. Yesu alimwacha Mama yake kwa Yohane kwa kuwa hakuwa na Kaka na dada wakumwachia mamaye

26 Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.” 27 Halafu akamwambia yule mwanafunzi: “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.
Ndiyo maana Bikira Maria tangu siku ile alihamia kwa Yohani kwa kuwa hakuwa na watoto wengine.

Utaratibu wa Mkristo Mkatoliki Kanisani

Ninapoingia kanisani nachovya maji ya baraka na kusema;
“Unitakase Ee Bwana mimi na uovu wangu wote, ili nipate kustahili kushiriki ibada takatifu’ Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” Amina!
Ninapiga goti huku nikisema
“Mungu wangu na Bwana wangu”
🙋🏽Nikiinuka nasema
“Nitakusifu na kukuabudu katika Ekaristi takatifu”
🙋🏽Naenda mpaka kwenye bench, napiga magoti au nakaa nikiwa mimeinamisha kichwa (kama mabenchi yameisha nabaki nimejisimamia) huku nikitoa nia yangu ya kusali misa siku hiyo, mfano
“Ee Mungu, ninaungana nawe na jeshi lote la mbinguni, pamoja na Mama Bikira Maria, nikiwa na nia ya kumwombea mama yangu ambaye ni mgonjwa, jirani yangu ambaye mpaka sasa hatuelewani na pia familia yetu ambayo haina amani, Mungu kupitia misa hii rejesha hali ya mama yangu, rejesha uelewano na jirani yangu, na pia rejesha amani ya familia yetu pamoja na familia zote ambazo hazina amani”
🙋🏽Ninaendelea na misa na Kushiriki litrujia kikamilifu
🙋🏽Wakati wa komunyo nikikumbuka kuwa nina dhambi kubwa huwa nakominika kwa sala ya tamaa wala siendi mbele, huwa najikalia tu kwenye bench naangalia wenye moyo safi wanaenda mbele kumpokea Yesu (Kweli huwa najisikia wivu sana, itanibidi katikati ya wiki nifanye kitubio ili nisikae tena)”
🙋🏽Mwisho wakati wa kuondoka nachovya maji ya baraka nikisema
“Unilinde Ee Mwenyezi Mungu, nikapate kuwa mfano katika jamii yangu, na nikushuhudie katika matendo yangu”
(Hapo nachovya maji ya baraka na kufanya ishara ya msalaba) “Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, amina”
Usiku mwema wapendwa. Malaika awalinde

Maswali na Majibu kuhusu Mitume

Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume siku gani?

Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume siku ya Pentekoste, yaani siku ya hamsini toka Pasaka. (Mdo 2:1-4)


Roho Mtakatifu aliwafanyia nini Mitume?

Roho Mtakatifu aliwatia Mitume Mwanga wa nguvu ili waweze kuhubiri Injili na kueneza Kanisa kote duniani


Kanisa ni la Kitume maana yake ni nini?

Kanisa ni la Kitume maana yake wakubwa wake yaani Baba Mtakatifu na Maaskofu nimahalifa wa Mitume


Yesu amemweka nani kuwa mkubwa wa Kanisa?

Yesu amemweka Mtume Petro kuwa Mkubwa wa Kanisa zima. (Mt 16:18-19). Halifa wa Mtume Petro ni Baba Mtakatifu.


Mapokeo ya Mitume ndiyo nini?

Mapokeo ya Mitume ndiyo yale yote ambayo Yesu aliwakabidhi Mitume wake, na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu yatadumu hata mwisho wa dunia katika mafundisho, liturujia na maisha ya Kanisa.
“Nawasifu, kwa sababu mmenikumbuka katika mambo yote, nanyi mmeyashika yale mapokeo vilevile kama nilivyowatolea… Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe” (1Kor 11:2; 15:3).
“Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu… Mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine” (2Tim 1:14; 2:2).
Tukikata huo mnyororo wa mapokeo, hata kama ni kwa kisingizio cha kushikilia Biblia, tunaachana na asili ya Kanisa.
“Basi, ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa waraka wetu… Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu” (2Thes 2:15; 3:6).


Je, tukipata mafundisho ya Kanisa tunapaswa kuyasadiki?

Ndiyo, tukipata mafundisho ya Kanisa tunapaswa kuyasadiki kwa moyo mmoja tupate uzima wa milele, kwa kuwa Yesu aliwaambia Mitume,
“Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa” (Mk 16:16).


Kanisa kuwa la Mitume maana yake nini?

Kanisa kuwa la Mitume maana yake limejengwa juu ya Mitume 12 wa Yesu na kuongozwa na waandamizi wao.
“Ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo” (Ufu 21:14).
“Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Yesu Kristo mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho” (Ef 2:20-22).


Je, Yesu amejenga Kanisa lake imara juu ya mwamba?

Ndiyo, Yesu amejenga Kanisa lake imara juu ya Mtume Petro, alichunge lote kwa niaba yake. Papa kama Askofu wa Roma ndiye mwandamizi wa Petro na mkuu wa kundi zima la Maaskofu, waandamizi wa Mitume.
“Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda” (Math 16:18).
“Atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba” (Math 7:24-25).
Historia ya miaka elfu mbili sasa imedhihirisha ukweli wa maneno hayo.


Maaskofu wote wamerithi mamlaka gani?

Maaskofu wote wamerithi mamlaka ya Mitume kwa kufundisha, kutakasa na kuongoza Kanisa lote pamoja na Papa na chini yake.
Wale waliokabidhiwa jimbo fulani ni msingi wa umoja kwa waamini wao na kati yao na Kanisa lote duniani.
“Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe” (Mdo 20:28).


Pamoja na kuwekewa mikono na mwandamizi wa Mitume, mtu anapewa kipaimara vipi?

Pamoja na kuwekea mikono na mwandamizi wa Mitume, mtu anapewa kipaimara kwa kupakwa krisma kama mhuri wa kuwa mali ya Bwana. Ndiyo inayotufanya tuitwe Wakristo nyuma ya Yesu aliyeitwa Kristo.
“Kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu” (Yoh 6:27).
“Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu” (2Kor 1:21-22).


Je, wenye daraja wanaweza wakatenda dhambi?

Ndiyo, wenye daraja wanaweza wakatenda dhambi kwa sababu ni binadamu kama sisi sote. Yesu alionja ukosefu wa Mitume hasa wakati wa mateso.
“Je, mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani?” (Yoh 6:70).
“Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao, na kuniacha mimi peke yangu” (Yoh 16:32).
Paulo alionya mapadri, “Katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao” (Mdo 20:30).


Mwenye kuwaondolea watu dhambi ni nani?

Mwenyezi Mungu pekee yake aweza kuwaondolea watu dhambi. Ndiye aliyewapa Mitume, Maaskofu na Mapadri uwezo wa kuwaondolea watu dhambi (Yoh 20:21-23)


Kabla ya Kupaa mbinguni Yesu aliwaahidi nini Mitume?

Kabla ya kupaa mbinguni Yesu aliwaahidia Mitume kuwapelekea Roho Mtakatifu; ndiye nafsi ya Tatu ya Utatu Mtakatifu. (Yoh 16:7)


Biblia ni nini? Asili, Historia, waandishi na mipaka yake

Biblia ni mkusanyiko wa vitabu mbalimbali vinavyohusu kazi ya Mungu ya kuwakomboa mwanadamu kuanzia enzi za Mababu na manabii Wa Waisraeli, Enzi za Yesu na za Mitume wa Yesu.

Je, Biblia ilipatikanaje? Nini chanzo na asili ya Biblia.

Biblia iliundwa kwa kukusanya vitabu vya dini vya wakristo hapo awali na kuunda kitabu kimoja. Kwa maana hii, Biblia ni vitabu teule vya dini vilivyoonekana vinafaa kutumika kwa waumini Wakristo ili kusaidia Imani yao. Hivyo basi, kama Biblia ni vitabu teule tuu vipo vitabu vingine vya dini ambavyo havikuwekwa Kwenye Biblia.
Wakristo wa kwanza walichagua vitabu kadhaa na kuviweka pamoja na kisha kuvita Biblia. Biblia ni mkusanyiko wa vitabu muhimu tuu vya dini mpaka kufikia Enzi za Mitume.

Je, Biblia ndicho kitabu pekee cha neno la Mungu?

Hapana, Biblia sio kitabu pekee cha neno la Mungu isipokua Biblia ni kitabu kilichoidhinishwa rasmi kutumika Kama kitabu kikuu cha Wakristo. Hii ni kwa sababu Biblia imeundwa na vitabu muhimu tuu vilivyochaguliwa na wakristo wa kwanza vilivyoonekana vinafaa kwa kufundishia, Ibada na kukuza Imani. Kwa hiyo basi vipo vitabu vingine ambavyo haikuwekwa Kwenye Biblia ambavyo ni Maneno ya Mungu.
Hii ndiyo sababu kwa nini Wakatoliki wana vitabu vingi kuliko madhehebu Mengine. Yaani sababu ni kwamba madhehebu Mengine walivitoa vitabu vingine vilivyounda Biblia. Na Wakatoliki waliweka vitabu vingine vya dini Kwenye Biblia walivyoona vinafaa pia kutumika.

Je nje ya Biblia hakuna Neno la Mungu au Maandiko matakatifu?

Nje ya Biblia kuna Neno la Mungu na Maandiko Matakatifu. Hii Inamaanisha kuwa Biblia sio kitabu pekee cha neno la Mungu. Zipo nyaraka na Vipo vitabu vingine vingi ambavyo viliandikwa na Manabii na Mitume ambavyo havikuwekwa kwenye Biblia lakini ni mafundisho ya Mungu. Biblia ni mkusanyiko wa vitabu vikuu vya Mungu.
Kumbuka kuwa sio nyaraka zote za Mitume ziliandikwa Kwenye Biblia. Vile vile manabii walikuwa ni wengi kuliko waliowekwa Kwenye Biblia.

Je Biblia ndiyo mafundisho ya Mungu pekee?

Hapana, Biblia sio mafundisho pekee ya Mungu. Hii ni kwa sababu sio mambo yote aliyofanya na kusema Mungu yaliandikwa na vilevile Mitume hawakua watu wa Mwisho kupokea Roho mtakatifu na kupokea neno la Mungu.

Biblia inatuthibitishia yenyewe kuwa haijakamilika na Si mambo yote yameandikwa Kwenye Biblia

Biblia inatuthibitishia kuwa haijakamilika tunaposoma (Yohane 21:25)
Biblia inatuambia hivi…”Kuna mambo Mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo Kama yangeandikwa yote, moja baada ya jingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa.”…Kwa mstari huu Biblia inatuthibitishia kuwa haikuandikwa vitu vyote.

Je Biblia ni mwisho wa Maandiko ya Mungu?

Biblia sio mwisho wa Maandiko ya Kimungu.
Biblia ni sehemu ya maneno ya Mungu mpaka miaka ya Mitume
Hata sasa Mungu anafanya kazi na watu wake kupitia Roho Mtakatifu na kwa kwa sababu hii Biblia sio mwisho wa kazi ya Mungu ya kusema na watu wake.
Mungu yu hai na anafanya kazi na watu wake mpaka sasa kwa kutumia vinywa vya watu Kama aliyofanya hapo awali.
Hata maneno unayohubiriwa sasa yanaweza kuwa ni kutoka kwa Mungu kwa maana hata waandishi wa Biblia walitumiwa na Mungu Kama wahubiri wa sasa. Mungu ni yule yule, Roho Mtakatifu ni yuleyule na Neno ni lile lile.
Kwa hiyo Biblia ni maneno yaliyochaguliwa mpaka enzi za Mitume. Vitabu vilivyofwata Baada ya Mitume japokuwa viliandikwa kwa Roho Mtakatifu havikuwekwa Kwenye Biblia.

Sababu ya Kanisa katoliki kutumia mapokeo na Maandiko ya Watakatifu

Kanisa katoliki linatumia mapokeo na Makala za watakatifu kwa Imani kuwa Mungu yule yule aliyefanya kazi tangu zamani anafanya kazi na watu wake mpaka sasa na hivyo Maandiko ya watu wa Mungu yanafaa kutumika kama yalivyotumika ya watu wa kale.

Yesu alituambia nini kuhusu Neno la Mungu na Mwendelezo wa kazi ya Mungu ya kusema na watu?

Yesu alituambia hivi katika (Yohane 16:12-15)..”Ninayo mengi ya kuwaambieni Ila kwa sasa hamuwezi kuyastahimili. Lakini atakapokuja huyo Roho wa Ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote. Maana hatasema kwa Mamlaka yake mwenyewe bali atasema atakayoyasikia na kuwajulisheni yatakayokuja. Yeye atanitukuza Mimi kwa kuwa atawajulisheni Yale atakayoyapata kutoka kwangu “…
Sasa basi,kama Roho Mtakatifu ni yuleyule na kazi zake ni Zile Zile za tangu Mitume, kwa nini hatukubali kuwa Anafanya kazi mpaka sasa kupitia watu wa Mungu? Kwa nini tunakataa mafundisho yao? Kwa nini tunashindwa kuelewa kuwa Biblia haikuwa mwisho wa Neno la Mungu? Kwa nini tunakana Mapokeo ya Watakatifu? Kwa nini hatuwaamini watumishi wake wa sasa?


Nyaraka za Mitume katika Biblia ni zipi?

Nyaraka za Mitume ni;
1. Waroma
2. 1 Wakorinto
3. 2 Wakorinto
4. Wagalatia
5. Waefeso
6. Wafilipi
7. Wakolosai
8. 1 Wathesalonike
9. 2 Wathesalonike
10. 1 Timotheo
11. 2 Timotheo
12. Tito
13. Filemoni
14. Waebrania
15. Yakobo
16. 1 Petro
17. 2 Petro
18. 1 Yohane
19. 2 Yohane
20. 3 Yohane
21. Yuda


Mitume kumi na wawili wa Yesu Kristu ni wapi?

Mitume wa yesu ni;
1. Simoni/Petro
2. Yakobo
3. Yohane
4. Andrea
5. Filipo
6. Barttholomayo
7. Mathayo
8. Thomaso
9. Yakobo wa ALfayo
10. Thadayo (Yuda Thadey)
11. Simoni Mkanaani
13. Yuda Iskarioti – Aliyemsaliti


Baba Mtakatifu wa kwanza ni nani?

Baba Mtakatifu wa Kwanza ni Mt. Petro


Nani ni Mitume wa Mataifa?

Mitume wa mataifa ni Paulo na Barnaba

Maswali na Majibu kuhusu Ibada ya Misa

Ishara ndogo ya Msalaba juu ya panda la uso, mdomo, na kifua kabla ya Injili ina maana gani?

Maana yake ni kama Ahadi kuwa, Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu kwa akili yangu, Nitalitangaza kishujaa kwa Midomo yangu, Nitalipenda na kulishika kwa Moyo wangu wote.


Je ni dhambi kukosa Misa Jumapili?

NDIYO. Ni dhambi kubwa kukosa Misa kwa Makusudi siku ya Jumapili/Dominika na Sikukuu zilizoamriwa.


Sakramenti ya Ekaristi ni nini?

Sakramenti ya Ekaristi ni Sakramenti ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo, aliye kweli katika Maumbo ya Mkate na Divai. (Yoh 6:1-17, Mt 26:26-28)


Ni wakati gani katika Misa Mkate na Divai vinageuka Mwili na Damu yake Kristo?

Ni katikati ya Misa padri asemapo maneno Matakatifu aliyosema Yesu mwenyewe: “HUU NDIO MWILI WANGU; HII NDIO DAMU YANGU”
26 Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” 27 Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, “Kunyweni nyote; 28 maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi. 29 Nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”
30 Baada ya kuimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni. (Mat 26:26-30)


Je Sakramenti ya Ekaristi hujulikana kwa majina yapi?

Majina haya;
1. Ekaristi Takatifu
2. Karamu ya Bwana
3. Misa Takatifu
4. Sakramenti Takatifu ya Altare
5. Komunyo Takatifu
6. Sadaka Takatifu
7. Kumega Mkate


Baada ya Mitume kufa ni nani wanafanya Sakramenti ya Ekaristi

Badaa ya Mitume kufa Maaskofu na Mapadri wanaendelea kuadhimisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu


Ni lini Yesu Kristo aliwapa Maaskofu na Mapadri Uwezo wa kugeuza mkate na divai kuwa Mwili na Damu yake?

Yesu Kristo aliwapa Maaskofu na Mapadri Uwezo wa kugeuza mkate na divai kuwa Mwili na Damu yake alipowafanya Mitume kuwa Mapadri katika karamu ya mwisho aliposema “FANYENI HIVI KWA UKUMBUSHO WANGU” (Lk 22:14-20)


Misa ni nini?

Misa ni sadaka safi ya Wakristo kwa Mungu, ndiyo sadaka ya Agano Jipya ambayo
Kristo kwa njia ya Padri anamtolea Mungu Baba mwili na damu yake katika umbo la mkate na divai kama alivyojitolea mwenyewe juu ya msalaba.


Sadaka ya Msalaba ni nini?

Sadaka ya Msalaba ni tendo la mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristojuu ya Msalaba pale Kalvari


Ni kwa nini Sadaka ya Misa Takatifu ni Sadaka ile ile ya Msalaba?

Sadaka ya Misa Takatifu ni ile ile ya Msalaba kwa sababu ni sadaka moja tu, kuhani na kafara ni yule yule.
Tofauti ni namna tu yankuitoa hiyo sadaka. (1Kor 11:26, Ebr 9:14,25-28)
Pale msalabani damu ilimwagika lakini katika Ekaristi damu haimwagiki tena


Misa Takatifu hutolewa kwa nani?

Misa Takatifu hutolewa kwa Mungu Baba Mwenyezi (Ebr 5:1-10, Law 9:7).


Yesu aliweka sadaka ya Misa Takatifu kwa makusudi gani?

Yesu aliweka sadaka ya Misa Takatifu ili;
1. Amtolee Baba sadaka bora siku zote
2. Atujalie mastahili yake Msalabani
3. Azilishe roho kwa neema za sadaka hiyo. (Ebr 5:1-10, 7:27).


Sadaka ya Misa Takatifu yatolewa kwa nia gani?

Sadaka ya Misa Takatifu yatolewa kwa nia ya kumwabudu Mungu, kumshukuru, kujipatanisha nae na kumwomba. (Ebr 9:14)


Misa Takatifu hutolewa kwa ajili ya nani?

Misa Takatifu hutolewa kwa ajili ya kanisa nzima yaani kwa ajili ya watu wote wazima na wafu. (Ebr 9:14. Rum 1:9)


Kutolea Misa kwa Marehemu maana yake ni nini?

Kutolea Misa kwa Marehemu ni kutolea Misa kwa ajili ya roho zilizoko toharani ili ziweze kuingia mbinguni


Misa Takatifu ina sehemu kuu ngapi?

Misa Takatifu ina sehemu kuu mbili
1. Litrujia ya Neno
2. Liturujia ya Ekaristi


Litrujia ya Ekaristi ina sehemu kuu ngapi?

Litrujia ya Ekaristi ina sehemu kuu tatu
1. Matayarisho ya vipaji
2. Sala ya Ekaristi
3. Ibada ya Komunyo


Ni vitu gani vya msingi na vya lazima katika kuadhimisha Ekaristi Takatifu?

Vitu vya lazima katika kuadhimisha Ekaristi Takatifu ni
1. Mkate wa Ngano
2. Divai ya mzabibu


Kabla ya Kupokea Ekaristi Takatifu Tunasali sala gani?

Tunasali “Ee Bwana sistahili uingie kwangu lakini sema neno tu na roho yangu itapona”


Katika Ekaristi Takatifu Tunampokea nani?

Katika Ekaristi Takatifu Tunampokea Yesu Kristo Katika Maumbo ya Mkate na Divai na tunaungana naye (Yoh 6:57)


Mkristo awe katika hali gani kabla ya kupokea Ekaristi Takatifu?

1. Awe na Neema ya Utakaso yaani asiwe na dhambi ya mauti.
2. Awe na Imani, Ibada na Kumtamani Yesu.
3. Afunge chakula Muda wa saa Moja na Kileo zaidi ya masaa matatu.
4. Awe safi kimwili.
5. Awe na adabu na heshima.


Komunyo Takatifu Hutuletea neema gani?

1. Hulinda na kuongeza neema ya Utakaso iliyo uzima wa roho zetu.
2. Hutuondolea dhambi ndogo na kupunguza hatari ya kutenda dhambio kubwa.
3. Hututia bidii na nguvu ya kutenda mema kwa kutuongezea Imani, Matumaini na Mapendo.
4. Huleta Umoja katika Kanisa, sio sisi na Kristo tuu bali sisi kwa sisi.


Mkristo akipokea Ekaristi Takatifu akiwa na dhambi rohoni anatenda dhambi gani?

Mkristo akipokea Ekaristi Takatifu akiwa na dhambi anatenda dhambi kubwa yaani kufuru Sakramenti.
26 Maana kila mnapokula mkate huu na kukinywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja. 27 Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana. (1 Kor 11;26 – 27)
28Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho; 29 maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe. 30 Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa. 31 Kama tungejichunguza wenyewe vizuri hatungeadhibiwa hivyo. 32Lakini tunapohukumiwa na Bwana, tunafunzwa tuwe na nidhamu, ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu. (1 Kor 11;28 – 32)


Je, Kanisa linahimiza waamini wapokee Ekaristi wakati gani?

Kanisa linahimiza waamini wapokee Komunyo Takatifu kila siku wanaposhiriki Misa


Nani Mhudumu wa adhimisho la Ekaristi Takatifu?

Mhudumu wa adhimisho la Ekaristi Takatifu ni Askofu na Padre


Je, Mkristo akipokea kipande cha Hostia amempokea Yesu Mzima?

Ndiyo, Amempokea Yesu Mzima kabisa, Hata akipewa zaidi ya hostia moja amempokea Yesu Mzima


Sakramenti ya Ekaristi Takatifu Huifadhiwa wapi?

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu Huifadhiwa kwenye Tabernakulo


Tabernakulo ni nini?

Tabernakulo ni mahali Patakatifu anapokaa Yesu wa Ekaristi siku zote


Sakramenti ya Ekaristi Takatifu hukaa Tabernakulo kwa sababu gani

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu hukaa Tabernakulo kwa ajili ya watu wote hasa wagonjwa


Ishara wazi ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni nini?

Ishara wazi ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni maumbo ya mkate na divai, na maneneo ya mageuzo ya Yesu mwenyewe Padri akiyatamka.


Baada ya kumpokea Yesu wa Ekaristi tufanye nini?

Baada ya kumpokea Yesu wa Ekaristi: Tumwabudu,tumshukuru, tumwombe kwani yeye ni Mwenyezi. (Mt 2:11, Lk 17:11)
Shopping Cart