Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

Ijue Ishara ya Msalaba

Ishara ya Msalaba ni tendo la mtu kugusa paji la uso, kifua na mabega kwa kutumia mkono wa kulia na kutamka ‘Kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina’.
Kugusa paji la uso tuna maana kukubali kwa akili, kugusa kifua maana yake ni kupokea na kuupenda msalaba moyoni na kugusa Mabega maana yake ni kuwa tayari kuubeba Msalaba kwa nguvu zetu zote.
Tunafanya njia ya Msalaba kwa nia ya kumkiri Mungu Mmoja katika Nafsi tatu. Pia Msalaba ni Ishara ya Ukombozi wetu.
Ishara ya Msalaba Juu ya Paji la uso, mdomo na kifua kabla ya injili:
Hii ina maana kwamba Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu Kwa Akili yangu,
Nitalitangaza kishujaa kwa midomo yangu, na Nitalipenda na kulishika kwa Moyo wangu Wote.

Maana ya siku ya Jumatano ya Majivu

Utangulizi

Wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili, (Mk 1:15), haya ndiyo maneno ya kwanza ya Yesu ambayo kadri ya Mwinjili Marko yanafungua kazi ya hadhara ya Yesu, kwa maana hiyo kazi ya Yesu inaanza kwa kuwaandaa watu katika toba ili hatimaye, wapate kuukaribia au kuingia katika ufalme wa Mungu.
Na wakati ndiyo sasa. Wakati ni sasa, Yesu anatuhubiria na Kwaresima imewadia, na ndiyo maana siku ya Jumatano ya majivu, kwa kuitikia mwito wa maneno ya Yesu kanisa linatualika kuingia katika kipindi cha Kwaresma, ambacho ni kipindi cha kujikusanya, kujitayarisha, kijitengeneza na kujikarabati hasa kwa toba, kufunga, kusali na kujitoa sadaka zaidi mambo yanayorutubishwa kwa tafakari ya kina ya Neno la Mungu.

Nini maana ya Jumatano ya majivu?

Jumatano ya majivu ni mwanzo wa kipindi cha kwaresima katika kanisa, Ni mwanzo wa siku arobaini za kutafakari kwa undani fumbo kuu la upendo wa Mungu linalofunuliwa kwa kujitoa kwake na kufa msalabani, kifo cha aibu cha Msalaba ili kuichukua aibu yetu au dhambi zetu.

Kwaresma ni nini?

Kwaresma ni kipindi cha siku 40 cha kujiandaa kuadhimisha Sherehe kuu ya PASAKA yaani kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunajiandaa kwa Kufunga Kusali, Kutubu, na Matendo mema.
Mama kanisa anatupatia kipindi hiki ili tuweze kutafakari njia na mienendo yetu na kubadilika kama haimpendezi Mungu
Tunapofunga tunatakiwa kuzuia vilema vyetu na kuviacha kabisa, tunaomba kujaliwa moyo wa toba, tunainua mioyo yetu na tunaomba Mungu atujalie nguvu na tuzo. Haitoshi tu kukiri makosa yetu bali tunahimizwa kuungama na kutubu hayo makosa na kuwa tayari kuanza upya. Kipindi cha Kwaresima huanza tangu Jumatano ya majivu. Mwanzoni mwa kazi yake ya kuhubiri Habari njema Yesu anaanza kwa kusema tubuni na kuiamini Injili – Mk 1,15. Maneno haya haya tunayasikia/tumeyasikia kila tunapopakwa majivu. Mwaliko huu wa Yesu unatuingiza katika kipindi cha toba – tubuni na kuiamini Injili. Huu ni mwaliko wa uzima. Ni mwaliko ili tuongoke, tuanze maisha mapya, maisha ya sala, kufunga na kutoa sadaka.

Kwa nini ikaitwa Jumatano ya majivu?

Jina linatokana na desturi ya kumpaka mtu majivu kichwani pamoja na kumtamkia maneno ya kumhimiza afanye toba inavyotakiwa na kipindi hicho cha liturujia kinachoandaa Pasaka.
Kwa kawaida siku ya Jumatano ya majivu unaanza mfungo unaofuata kielelezo cha Yesu kufunga chakula siku arubaini jangwani baada ya kubatizwa na Yohane Mbatizaji na kabla ya kuanza utume wake mwenyewe.

Nini maana ya majivu tunayopaka?

Majivu ni ishara ya majuto, nayo hufanywa visakramenti kwa kubarikiwa na kanisa. Tunapopakwa majivu katika paji la uso hutusaidia kutafakari na kutukumbusha kuwa wanadamu sisi tu mavumbi na mavumbini tutarudi. Hutukumbusha zaidi kuwa maisha ya hapa duniani tunapita na safari yetu itakamilika pale tutakapoungana na Bwana na mwokozi wetu katika ufalme wako.
Angalia; Isaya 61:3, Ester 4:1-3, Yeremia 6:26, Ezekieli 27:30, Mathayo 11:21 na Luka 10:13.

Kwa nini majivu yanapakwa kwenye paji la uso na si vinginevyo?

Ishara yoyote iwekwayo katika paji la uso huonesha umiliki (soma Ufunuo 7:3, Ufunuo 9:4, Ufunuo 14:1, Ezekieli 9:4-6, ). Tunapochorwa ishara ya msalaba katika paji la uso ni ishara kwamba sisi tupo chini yake yeye aliyekufa msalabani kwa ajili yetu.
Hali kadhalika hutukumbusha ishara ya msalaba tuliyochorwa na mafuta matakatifu siku ya ubatizo wetu, hutukumbusha ahadi tuliyoiweka siku hiyo ya ubatizo na kutuita tuishi maisha ya utakatifu

Padri hutamka maneno gani wakati anapaka majivu?

Tunapopakwa majivu Padre husema; Mwanadamu kumbuka u mavumbi na mavumbini utarudi AU Tubuni na kuiamini Injili.

Maneno anayosema padre yana maana gani?

Maneno haya kwa upande mmoja hutukumbusha tunapoelekea, tusisikitike kwamba siku moja tutarudi mavumbini bali tuwe na furaha kwani wakati miili yetu unarudi mavumbini roho zetu zitakwenda kuungana na Mungu Baba mbinguni.
Hivyo maandalizi tunayoalikwa kuyafanaya si maandalizi ya kuelekea mavumbini bali maandalizi ya kuelekeza roho zetu mbinguni. Ndio maana pia twaambiwa tubuni na kuiamini Injili.

Majivu tunayopakwa yanatoka wapi?

Majivu tunayopakwa hutoka katika matawi yaliyotumika katika jumapili ya matawi ya mwaka jana. Majivu haya hubarikiwa na kuwa visakramenti. Hivyo majivu yanapoashiria toba na majuto pia hutukumbusha wema wa Mungu na utayari wake wa kutusamehe.

Kwa nini unatumia matawi ya Jumapili ya Matawi?

Matawi haya yalimkaribisha Yesu Yerusalemu akiwa tayari kufa kwa ajili ya dhambi zetu, yalimpokea mfalme kwa furaha na shangwe kuu. Matawi haya yanapochomwa na sisi kupakwa majivu yetu yanatukumbusha kuwa ni kwa ajili ya dhambi zetu Mungu alimtoa mwanae wa pekee kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu sisi wanaadamu. Hivyo hututafakarisha kuacha dhambi.

Kanisa limekataza nini siku ya Jumatano ya majivu?

Tumekatazwa kula chakula siku ya Jumatano ya Majivu na kula nyama siku ya Ijumaa Kuu katika Amri ya Pili ya Kanisa.

Nani analazima kufunga siku ya Jumatano ya majivu na Kwaresma?

Kila Mkristo aliyetimiza miaka 14 na zaidi anapaswa kufunga kula nyama (Ijumaa kuu) na mwenye miaka zaidi ya 21 kufunga chakula Jumatano ya Majivu

Tunaposema kujinyima wakati wa Kwaresma tunamaana gani?

Kujinyima ni kujikatalia kitu ukipendacho mfano nyama, pombe, sigara, muziki, safari, maongezi n.k.

Mwisho

Wakati wa Kwaresma Waamini wanapaswa kujitakasa zaidi kwa kusali, kufunga, toba na matendo mema
Kipindi cha Kwaresima ni fursa makini ya kumkimbilia Mwenyezi Mungu, kwani kwa njia ya dhambi wamejikuta wakiwa mbali na Uso wa huruma ya Mungu, kiasi hata cha kupoteza imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kumpenda Mungu na jirani badala ya kukumbatia malimwengu yanayoendelea kuwatumbukiza katika utupu wa maisha ya kiroho. Kwaresima ni kipindi cha waamini kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu inayoganga na kuponya dhambi. Ni wakati wa sala, upendo na kufunga.

Mambo ya kufahamu katika kipindi cha kwaresima

Nini maana ya Kwaresima?

Kwa Kilatini na Kiitaliano neno Kwaresima lilimaanisha “40” yaani siku 40 za kufunga za wiki kati ya Jumatano ya Majivu hadi Jumamosi Kuu. Kwa Kijerumani Kwaresima maana yake “Kipindi cha kufunga.”

Kwaresima ilianzaje?

Kabla ya kuona Kwaresima jinsi ilivyoanza, ni vizuri kuongea kidogo kuhusu Sikukuu ya Pasaka ili tuweze kupata mwanga wa kuelewa mwanzo wa kipindi hiki muhimu cha Kwaresima.
Habari Njema yatuambia kwamba YESU KRISTO alifufuka “Siku ya kwanza ya juma.” “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.” (Mt.28:1) Hii ni kwasababu Wakristo walianza kukutana pamoja kwa sikukuu ya ufufuko wa BWANA kila wiki sio Jumamosi kama Wayahudi, bali siku iliyo fuata. “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza -`maneno yake hata usiku wa manane.” (Mdo.20:7). “Siku ya Kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake: ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja.” (1Kor.16:2), siku ambayo Warumi waliita “Siku ya Jua”. Mara moja jina hilo lilibadilika na kuwa “Siku ya BWANA”
Kanisa la mwanzoni halikusherehekea sikukuu kama vile Noel, Sikukuu kwa heshima ya Mama Bikira Maria au sikukuu yeyote ile. Kulikuwepo na adhimisho la ufufuko wa BWANA kila wiki na hakuna zaidi.
Miaka mingi ikapita kanisa likiwa katika hali hii. Baadaye kulikuwepo na hitaji la kusherehekea tukio la kiini cha imani yetu kwa namna ya pekee. Wakristo waliona umuhimu wa kuwa na muda kwa sikukuu ya kwanza kati ya sikukuu zao yaani “Jumapili ya Pasaka”, ambayo ilifikiriwa kama “Mama wa Jumapili zote”, “Mama wa skikukuu zote”. Waliiona sikukuu hiyo kama “Malkia wa sikukuu zote, wa Jumapili zote, na kiujumla kama Malkia wa siku zote za mwaka. Tangu mwanzoni mwa karne ya pili, Jumuiya zote za Kikristo walikuwa wanasherehekea sikukuu hii ya Pasaka. Sherehe zilikuwa zinahitimishwa na kusanyiko la sala lililofanyika usiku na kumalizikia na Ekaristi. Ushiriki wa kwenye ibada hiyo, ulichukuliwa kama ni kitu muhimu sana kwa mkristo.

Kuanza kwa Kwaresma

Wote tunafahamu kwamba, ufanisi au mafanikio yoyote ya sikukuu au ya jambo lolote yanategemea sana maandalizi yake. Miaka miambili hivi baada ya KRISTO, Wakristo walitaka kuvuna matunda ya kiroho ya Paska kwa wingi. Ili kufanikisha hili, walianzisha utamaduni wa kuwa na siku tatu kabla ya Pasaka kwa sala, tafakari na kufunga kwa nia ya kuonyesha masikitiko yao juu ya kifo cha YESU KRISTO. Kutokana na ukubwa na umuhimu wa sikukuu hii, mbali ya kuona umuhimu wa maandalizi, walitafuta njia za kuongeza muda wa furaha na utajiri wa kiroho utokanao na Pasaka. Hivyo walianzisha “Wiki Saba,” yaani siku 50 za Pentekoste ambapo walisherehekea na kuzipitisha siku hizo kwa hali ya furaha. Askofu Mt. Ireneus alisema kuwa muda huo wa siku 50 ni kama Sikukuu ya Siku moja yenye umuhimu sawa na Jumapili. Katika kipindi cha siku za Pentekoste, sala zilikuwa zinasaliwa hali wamesimama, kufunga kulikatazwa na sakramenti ya ubatizo ilikuwa ikiadhimishwa. Ni kama vile sikukuu ya Pasaka ilidumu kwa kipindi chote cha siku 50. Miaka 150 ilipita na mwishoni mwa mwaka 350 B.K., Wakristo waliona kama siku tatu hazikutosha kwa maandalizi ya sikukuu kama hii. Hivyo waliongeza hadi kufikia siku 40. Hivi ndivyo Kwaresima ilivyoanza.

Kwa nini siku 40?

Tunaposema kuku wanne au kilo saba za mchele tuna maana kama ilivyo yaani kuku wanne na kilo saba za mchele. Si zaidi au pungufu.
Namba au tarakimu mbalimbali tunazokutana nazo katika Biblia zinaashiria lugha za picha na siyo kuchukulia katika thamani ya kuhesabu. Hivyio basi, tunapokutana na namba kama 40 huenda isimaanishe 40 kama tunavyo hesabu fedha. Kati ya maana nyingi zilizotolewa kwa namba 40, kuna moja yenye maana ya pekee, inamaana ya kipindi cha maandalizi cha kutosha kisichokuwa na muda maalum, kwa tukio kubwa. Kwa mfano , Gharika ilidumu kwa siku 40 usiku na mchana…na ilikuwa ni maandalizi ya ubinadamu mpya; Waisraeli walitumia muda wa miaka 40 jangwani…maandalizi ya kuingia nchi ya ahadi; watu wa Ninawi walifunga na kufanya kitubio siku 40…maandalizi ya kupokea msamaha wa MUNGU; Elia alitembea kwa siku 40 mchana na usiku…kama maandalizi ya kufika mlima wa MUNGU; Musa na YESU walifunga kwa siku 40 mchana na usiku… kama maandalizi kabla ya kuanza utume wao. “Kisha ROHO alimwongoza YESU mpaka jangwani ili ajaribiwe na ibilisi. Akafunga siku arobaini usiku na mchana, na mwishoe akaona njaa” (Mt.4: 1-4)
Natumaini hadi hapo tumeelewa nini maana ya namba 40. Je, ni siku ngapi ambazo zinahitajika kwa ajili ya maandalizi ya sikukuu kubwa kuliko zote za kikristo? Bila shaka ni 40. (Kuanzia Jumatano ya majivu hadi Jumamosi Kuu ukiondoa Jumapili zote) Siku 40 ni muda wa kutosha wa kufanikisha kitu fulani chema, kizuri na chenye thamani.

Lengo la Kwaresima ni nini?

Lengo kuu la Kwaresima ni kufanya upya maisha yetu ya kiroho na kutufanya kuwa watu ambao MUNGU anataka tuwe yaani ni kipindi chenye kutupatia utakatifu, tukikumbuka kuwa sote tumeitwa kuwa watakatifu kama BABA yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu (Mt. 5:48). Ni kipindi cha kuuvua utu wetu wa kale na kuvaa utu mpya. Kwani tunasoma:- “Mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unao haribika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho na nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa na MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli. Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake…Mwibaji asiibe tena…Neno lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema na kufaa…tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.” (Efe.4:22-32.)
Kwaresima kwa hakika ni kipindi pia cha kuachana na matendo ya mwili. “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo;” (Gal.5:19 – 20).
Kwa ufupi Kwaresima ni kipindi cha kuachana na maisha ya dhambi na kurudi kwa MUNGU kwa kuishi maisha yanayompendeza MUNGU kwa njia ya kufanya toba ya kweli isiyo ya mazoea, na malipizi yasiyo ya nje tu, bali hasa mapinduzi ya kiroho. Katika kipindi hiki tunalazima ya kubadili hali yetu ya ndani. Badala ya kujitafuta wenyewe na kufuata mapenzi yetu, inatupasa sisi kumwelekea MUNGU na kuyatimiza mapenzi yake katika mawazo, maneno na matendo yetu.

Nguzo tatu kuu za Kwaresima ni:

i. Sala.

“Wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani. Usali mbele ya BABA yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini atakujazi.” (Mt. 6:6)
Kupata muda wa sala pamoja na MUNGU. Sio tu kunena maneno ya sala fulani, lakini pia kumsikiliza MUNGU akizungumza mioyoni mwetu. Kumuomba MUNGU nguvu ya kubadilika, yaani uongofu wa kweli. Ndiyo maana tunaambiwa. “Tubuni na kuiamini Injili”. Hayo ndiyo MUNGU aombayo kwetu wakati wa Kwaresima. MUNGU anatuita kutoka kwa dhambi, na tuupokee ujumbe wake kwetu – Injili, na kuwa waamninfu kuishi kadiri ya Injili. Ni wakati pia wa kuhudhuria misa mara kwa mara kwa ibada na uchaji, kuhudhuria ibada mbalimbali, kama vile Baraka ya Sakramenti Kuu, Kuabudu Ekaristi Takatifu, kusoma Neno la MUNGU na kuliishi baada ya kuyatafakari maneno hayo ya MUNGU ambayo ndiyo sauti yake MUNGU na kutumia muda wetu kwa mambo ya ki-MUNGU yaliyo matakatifu.

ii. Kufunga.

“Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso wako ili usionekane na watu ukifunga, ila na BABA yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini atakutuza.” (Mt. 6:17-18). Kufunga sio tu kujinyima kutokunywa pombe, kutokula chakula, kutovuta sigara n.k. Kifupi ni kwamba kufunga kuondokana na ubinafsi wetu na kuwafikiria na kuwasaidia wenye shida. Uovu hauwezi kushindwa bila kujitoa nafsi na bila kutoa na kuwapa wahitaji vile tuvipendavyo. MUNGU hapendezwi na kufunga tu, bali upendo kwa wanaoteseka utusukume na kufunga tupendavyo kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji. Hivyo kuna mahusiano makubwa sana kati ya kufunga na ukarimu. Kufunga lazima kuendane na ukarimu. Kufunga bila ukarimu huo ni mfungo tasa.

iii. Kutoa Sadaka.

“Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu kusudi mtazamwe nao. Bali wewe utoapo sadaka hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wa kuume; na BABA yako aonaye kwa siri atakujazi.” (Mt. 6:1) Hayo yanamaanisha kwamba usidai shukurani wala malipo kwa wema wowote uwatendeao jirani zako kwa sadaka yako. Malipo utakayopata uyatazamie tu kutoka kwa BABA yako wa mbinguni. Kutoa tunachojinyima kwa kumsaidia KRISTO anayeteseka kwa wenzetu. Kushirikiana na wengine tulivyo navyo kama vile fedha, nguo, chakula, ama kuwakaribisha wahitaji nyumbani.
Hivyo basi, Mazoezi tunayofanya katika kipindi cha Kwaresima kama kusali zaidi, kusikiliza au kusoma Neno la MUNGU, kutenda matendo ya huruma kwa wahitaji, kufunga chakula na kujihinisha kinywaji pamoja na kuzuia tamaa potovu za mwili wetu, yawe na kusudi la kuibadili hali yetu, kutufanya kuwa na upendo zaidi na huruma kwa wenzetu na kutufanya tuweze kuunganika zaidi na KRISTO MFUFUKA. Tumvue mtu wa zamani katika nafsi zetu na tumvae mtu mpya, yaani KRISTO Mfufuka.

Nini makusudi ya kufunga?

YESU alifunga ili awape wanadamu mfano au kielelezo halisi na sahihi cha kuiga, na apate kuokoa roho zetu. Watu wawe na namna bora ya kufanya malipizi, kuuadibisha na kuutumikisha mwili na tamaa kwa kuwa anatenda dhambi.

Nani anapaswa kufunga?

Inatubidi tujiangalie sana kwani miili yetu ni midhaifu na myepesi kwa kutenda dhambi na kuipeleka roho motoni. Tusiiendekeze miili yetu, bali tuitawale kwa kufuata maadili ya kimungu na kuinyima madai yake, ambayo ni kishawishi kinachotupeleka upotevuni. Tunapoamua kufuata njia hii, hakika, KRISTO atatuimarisha na kutuongoza kwenye uzima wa milele; na kutupa neema ya kupambanua mema na dhambi, huku tukielekea uzimani. Mdomo unao nena dhambi, na mwili unaotenda dhambi, sherti vyote vitende pia mema, siyo dhambi.
Mtu asiyetenda dhambi hana haja ya kufunga. Lakini hakuna mtu anyefikia utu uzima ambaye hatendi dhambi machoni pa MUNGU hata Wacha MUNGU wana dosari. Kwa hiyo, kila mtu afunge kufidia dhambi zake. Tusipofunga kuna hatari kubwa ya kuungua moto. Ni vizuri waamini wote wafunge ili kulipia fidia ya dhambi zinazotendwa. Tumwabudu KRISTO kwa unyofu na unyenyekevu, ili kwa huruma yake kuu atusamehe dhambi zetu na adhabu tunazostahili.

Mafundisho na mapokeo Katika Kanisa Katoliki yanapopatikana kwenye Biblia

Wakatoliki wengi huyumbishwa kwa kuambiwa huamini mambo ambayo hayako au ni kinyume na Biblia. Aya zifuatazo zitakusaidia wewe mkatoliki kuelewa au kujua mistari ya Biblia inayofafanua imani katoliki.
1) KUOMBEA MAREHEMU:
2 Mak. 12:38-46
Hek. 3:1
Tob 4:17
2) MATUMIZI YA SANAMU NA VISAKRAMENTI
2Fal 3:20-21
Hes. 21:8-9
Kut. 25:17-22
Kol. 1:20, 2:14
Yn. 12:32
Mt. 19:11-12
3) USAHIHI WA MAPOKEO YA KANISA KATOLIKI KAMA CHANZO CHA IMANI
2 The 2:15
2 Kor. 10:10-11
Yn 21-25
2 Yoh. 1:12
3 Yoh. 1:13
4) KUABUDU JUMAPILI BADALA YA JUMAMOSI(SABATO)…. Hasa ni kwa sababu Yesu aliitukuza siku ya kwanza ya juma kwa ufufuko wake na kwa kuwatokea wanafunzi wake siku hiyo.
Ufu 1:10
Mdo 20:7
Mt 28:1-8
Lk. 24:1-7
Lk. 24:13ff
1 Kor. 16:1-2
Yn. 20:1-22
5) MAMLAKA YA PAPA KAMA MFUASI AU MRITHI WA MT. PETRO
Yn. 21:15-17
Mt 16:18-19
W 2:1-14
6) MAPADRI KUITWA BABA WAKATI BABA NI MMOJA ALIYEKO MBINGUNI
Mwa 17:4
Yer. 7:7
Hes. 12:14
Yn. 6:49
Mt 23:30
Lk. 1:73
7) JE BIBLIA INATAMBUA MUUNDO WA UONGOZI WA KANISA?
Efe. 4:11-13
1Tim 5:17-25
1Tim 3:1-7,8-18
8) JE BIBLIA INASEMAJE KUHUSU TOHARANI.
Isa 35:8, 52:1
Zek 13:1-2
1Kor 3:15
Lk 12:47-48, 58-59
Ufu 21:27
Ebr 12:22-23
Ayu 14:13-17
9) KUHUSU MATUMIZI YA UBANI
Kut 30:34-37
Hes 16:6-7
Law 16:12-13
Lk 1:10
Ufu 8:32
10) ROZARI IKO KATIKA BIBLIA?
Lk 1:28
Lk 1:42
11) JE KUTUMIA MAJI YA BARAKA NI MAPENZI YA MUNGU?
2Fal 2:19-22
Yn 5:1-18
Yn 7:37
Hes 19:1-22
12) KWANINI TUNAOMBA WATAKATIFU WATUOMBEE?
Mit 15:8, 15:29
Ayu 42:8
Yak 5:16
Mt 16:19
13)KWANINI TUNATUMIA MEDALI, MISALABA, SCAPURALI NA MIFUPA YA WATAKATIFU?
2Fal 13:20-21
14) KWANINI TUNAUNGAMA DHAMBI ZETU KWA PADRI
Mt 16:19,1-20
Yak 5:15-16
15) UBATIZO WA WATOTO WACHANGA UKO KATIKA BIBLIA
Mdo 16:15-33
Mdo 18:8
Mt 28:19
Mdo 10:47-48
16) KUSIMIKWA KWA UTUME
Kut 28:4-43
17) RANGI ZA KANISA
Kut 27:9-29
18) MATUMIZI YA MISHUMAA
Kut 25:31-40; 27:20-21
Hes 8:1-4
19) MPAKO WA MAFUTA YA KRISMA
Kut 30:22-32
20) MPAKO WA MAFUTA YA WAGONJWA
Yak 5:14-15

Usiyumbishwe na kila upepo wa mafundisho

FROM FR TITUS AMIGU
Siku moja, miaka kama 14 hivi iliyopita, nilimzingua mchungaji wa kikanisa fulani. Alinijia mbio na kuniambia, “Ati… Kadinali wenu amesema kuwa pombe sio dhambi! Kwanini usihame huko? Angalia sasa, hata kiongozi wenu wa juu wa Kanisa amekosea kwa kusema pombe sio dhambi.”
Basi mimi nikamjibu huyo mzee kama ifuatavyo;
Je kisu ni dhambi? Mzee akajibu, “hapana!” Je sumu ya panya? Mzee akajibu tena, “hapana”. Nikampa changamoto hii; Je, kama mtu akimdunga mwenzake kisu na kumuua, hapo dhambi ni kisu au kuua? Au mtu afanyaye kujiua kwa kumeza sumu ya panya, je basi ndio tuseme kuwa sumu ya panya ni dhambi? Mzee akajibu, hapana.
Nikamkumbusha maneno ya Yesu kuwa kitu kimuingiacho mtu hakiwezi kumtia unajisi.
Nikamwambia, “Kanisa lako ni kanisa la walevi.” Mzee akatumbua macho, “… hee… kijana wewe?…” Nikamweleza;
Wengi kama si wote, wa wafuasi katika kanisa lenu ni walevi. Wanatamani kunywa na kulewa, lakini wewe kama mchungaji umewazuia kwa sheria, tena sheria kali yenye vitisho na kuwatia hofu. Umeweka mikono yako machoni pao na kuwaambia kuna shimo mbele, hivyo umewafanya vipofu zaidi. Kila mwanamume amtazamaye mwanamke kwa tamaa amekwisha kuzini naye moyoni , na vivyo hivyo, kila atamaniye ulevi amekwisha kulewa moyoni ; hata kama asipoonja pombe, ni mlevi tu.
Nikazidi kumweleza kuwa mimi niliimarishwa (Kipaimara) kwa kuwekewa mikono na Askofu, nikaombewa ujazo wa Roho Mtakatifu. Kunywa ama kutokunywa nafanya si kwa amri, bali kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu. Sheria ya usionje, usiguse hainihusu, maana mimi ni mtu huru katika Roho. Kwa hiyo siwezi kujiunga na kanisa la walevi, ambao badala ya kumtii Mungu, wanaitii hofu iliyopandwa ndani yao.
Yule mzee akasema, hapo umenijibu vema kijana, lakini mbona ninyi Wakatoliki mnawaomba wafu, kama Bikira Maria? Nikamjibu,;
Sisi Wakatoliki ni Kanisa lililo katika ushirika wa Watakatifu. Yesu aliwaambia Masadukayo kuwa Bwana ni Mungu wa walio hai, Ibrahimu, Isaka, na Yakobo. Ndio maana pale mlimani Yesu alipogeuka sura aliongea na Musa na Eliya walio hai. Katika kikanisa chenu hakuna imani ya kuweza kuongea na Yesu ili muingie katika utukufu wake, na awawezeshe kuongea na Musa na Eliya, Bikira Maria au watakatifu wengine walio hai katika Bwana. Mkifa, mnakufa kama mbwa, na mnakufa kweli kweli. Basi siko tayari kujiunga na kanisa la wafu, tena wasio na imani ya kuona mambo ya rohoni. Japo mnajiita kanisa la kiroho, mambo ya rohoni hamyajui, maana ninyi ni kanisa la wafu.
Yule mzee akazua ghafla safari ya kwenda kunywa chai aliyodai ameitwa na mjukuu wake akanywe, naye faster akasepa.
Je, waijua misingi ya imani yako? Je, unaongozwa na Roho Mtakatifu au na sheria za kidini?
Usiyumbishwe na kila upepo wa mafundisho.
Shopping Cart