Sala za Katoliki: Sala Muhimu Kwa Mkristu Mkatoliki

SALA YA NOVENA KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Ee Moyo Mtakatifu sana wa Yesu, chemchemi ya kila baraka, ninakuabudu, ninakupenda, na kwa majuto halisi ya dhambi zangu, nakutolea moyo wangu dhaifu. Nifanye mnyenyekevu, mvumilivu na safi, nikikubali na kuyatii kabisa mapenzi yako. Ee Yesu mwema, unijalie niishi nawe na kwa ajili yako. Unilinde niwapo katikati ya hatari, unifariji katika mateso, unipe afya ya mwili na msaada katika mahitaji ya mwili, Baraka yako juu ya kila nilifanyalo, na neema ya kifo chema. Amina.

Ee Yesu uliyesema “Kweli nawaambieni, ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, gongeni nanyi mtafunguliwa”, tazama ninagonga, ninatafuta na kuomba …….. (Taja ombi lako)
Baba Yetu….., Salamu Maria …….., Atukuzwe Baba……..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!

Ee Yesu uliyesema “Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu mtapewa”, tazama kwa jina lako ninaomba ……. (Taja ombi lako)
Baba Yetu….., Salamu Maria …….., Atukuzwe Baba……..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!

Ee Yesu uliyesema “Kweli nawaambieni, mbingu na dunia zitapita lakini maneno yangu hayatapita kamwe”, tazama, nikitiwa nguvu na maneno yako ya kweli ninaomba …….. (Taja ombi lako)
Baba Yetu….., Salamu Maria …….., Atukuzwe Baba……..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!

Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambaye kwako ni kitu kimoja tu kisichowezekana, ambacho ni kutoacha kutowaonea huruma wenye huzuni, utuhurumie sisi wakosefu maskini na utujalie neema tukuombayo kwa njia ya Moyo Imakulata wa Maria, Mama yetu mpole.

Sali ‘Salamu Malkia’ na kuongezea, ‘Mtakatifu Yosefu Baba Mlishi wa Yesu, utuombee’.

P.S. – Sala hii ya Novena ilisaliwa kila siku na PADRE PIO kwa ajili ya kuwaombea wale wote waliomwomba msaada wa sala zake. Unaweza kuisali kwa namna tofauti tofauti. Mfano, kama Novena ya siku tisa, ambapo unasali sala hii mara moja au zaidi kila siku kwa siku tisa, au unaweza kuifanya kama Novena ya masaa, ambapo unasali sala hii kila baada ya saa moja kwa masaa tisa kwa siku hiyo hiyo, hasa kama kitu unachokiomba ni cha haraka au umesongwa moyoni. Vilevile unaweza kuifanya sala hii kama sehemu ya sala zako za kila siku katika mwezi Juni ambao ni mwezi uliotengwa na Kanisa kwa ajili ya kuuheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu, na hapo utaitumia kuwaombea watu waliokuomba msaada wa sala zako kama alivyofanya Mtakatifu Padre Pio. Pia unaweza kuitumia kama sala yako ya siku zote au ya mara kwa mara kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.

Kanuni ya imani

Nasadiki kwa Mungu, Baba Mwenyezi,/ mwumba mbingu na dunia./ Na kwa Yesu Kristu, Mwanaye wa pekee, Bwana wetu;/ aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu,/ akazaliwa na Bikira Maria,/ akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato,/ akasulubiwa, akafa, akazikwa,/ akashukia kuzimu;/ siku ya tatu akafufuka katika wafu;/ akapaa mbinguni;/ amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi;/ toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu,/ Kanisa takatifu katoliki,/ ushirika wa Watakatifu,/ maondoleo ya dhambi,/ ufufuko wa miili,/ uzima wa milele. Amina.

Sala fupi ya Asubuhi

Tuusifu Utatu Mtakatifu wa Mungu Mwenyezi, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, milele na milele, Amina.

Ee Utatu Mtakatifu wa Mwenyezi Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, nasadiki kuwa upo hapa na mahali pote. Ee Mungu wangu, umeniumba, umenikomboa, umenifanya mkristo, umenizidishia neema zako hapa duniani, umenitayarishia makao yangu mbinguni, umenijalia na siku hii nikutumikie. Ee Mungu wangu! Nakuabudu, nakushukuru, nakuomba toba, nakupenda! Ee Mungu wangu, nakutolea roho yangu, na mawazo, na maneno, na kazi, na furaha, na mateso yangu: uyapokee unipe neema yako nisikutende leo dhambi!

SALA KWA MT. YOSEFU KUOMBA KUFAHAMU WITO WAKO

Ee uliye Mkuu, Mt. Yosefu, uliyatii kabisa maongozi ya Roho Mt. Unijalie neema ya kufahamu aina ya maisha ambayo Mungu anapenda mimi niishi. Usiniache nidanganyike katika jambo muhimu kama hili, ambalo furaha yangu hapa duniani inalitegemea, na hata pia wokovu wa roho yangu.

Unijalie, nikiangazwa na matakwa matakatifu na nikiwa mwaminifu katika kuyatimiza, nikumbatie aina ya maisha ambayo Mungu ameniandalia na yatakayoniongoza kwenye furaha ya milele.
Amina.

Shopping Cart