Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

Faida ya kuabudu Ekaristi Takatifu

1.Kila saa moja tunayotumia kuabudu, inafurahisha moyo wa Yesu na hivyo majina yetu huandikwa mbinguni kwa ajili ya uzima wa milele (Mama Thereza wa Calcuta)
2.Maisha ya kiroho ya familia zetu yanaimarishwa kwa njia ya saa ya kuabudu (John Paul II)
3. Saa takatifu ya kuabudu ni ya muhimu sana kiasi kwamba roho za waamini wengi huenda kwenye uzima (mbinguni) badala ya motoni (ufunuo wa Yesu kwa Dina Belanger)
4. Wakati pekee ambao Yesu aliwaomba kitu wanafunzi wake ni wakati anakaribia mateso na hakuomba chochote isipokua saa moja ya kukesha nae (Askofu Mkuu Fulton Sheen)
5.Saa moja takatifu ya kuabudu ni kushiriki katika harakati za ukombozi (Askofu mkuu Fulton Sheen)
6. Neema ya kuabudu Ekaristi iko juu ya watu wote (St Peter Julian Eymard)
7.Bwana wetu Yesu husikia maombi yetu yote na popote lakini amewafunulia watu wake kuwa wale watakaokwenda kukaa nae katika kuabudu Ekaristi wanapata neema zaidi (Mtakatifu Alphonsus Ligoria)
8.Kila saa unapokwenda kuabudu kumbuka kwamba Yesu amekusubiria wewe binafsi kwenda kumtembelea kwa karne ishirini (St Josemaria scavia)
9.Kuabudu kwa dhati kuna neema na manufaa makubwa ambayo huzidi kwa wale wanaoabudu, hupanuka na kugusa nyumba zao familia zao na mpaka katika parokia zao (Pope Paul VI)
10. Saa moja takatifu mbele ya Ekaristi ni muhimu kuliko miaka elfu moja ya utukufu wa mwanadamu (Mtakatifu Padre Pio)

Asili na matumizi ya Neno “AMINA” kama kiitikio muhimu katika Liturujia

Kiitikio hicho tunakifahamu sisi sote; tunaitikia mara nyingi lakini je, tunaelewa umuhimu wake? Binafsi nikichunguza wakati wa maadhimisho mbalimbali ya Liturujia hasa Adhimisho la Ekaristi, ni baadhi tu ya waamini wanaoitikiaAmina sehemu mbalimbali wakati wa Misa. Waamini wengine huitikia  kwa sauti  ya kuungama dhambi na wengine hawaitikii kabisa.

Asili yake 

Kwa asili Amina ni neno la kiebrania na maana yake ni: ni kweli kabisa.  Neno hilo lililotumika kukubali au kuthibitisha ukweli wa maneno au jambo lililokuwa limesemwa. Kwa hiyo mtu aliyesema Amina alitakiwa kusikia nini kilichosemwa na ndipo akubalie:    Amina.
Neno hilo limetumika katika Agano la Kale hasa katika Zaburi. Katika Agano Jipya Bwana Yesu alilitumia mara nyingi alipotaka kusisitiza siyo tu ukweli wa lile alilolisema bali pia uzito wake. Kwa namna hiyo Bwana Yesu alidhihirisha pia mamlaka yake katika lile alilosema.
Katika kitabu cha Ufunuo Yesu mwenyewe anaitwa Amina, kwani yeye ni mwaminifu kabisa katika maneno yake na kwamba yale anayosema kwa uhakika yatatimia. Tunasoma hivi: “Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina. Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli…” (Ufu 3:14). Yesu mwenyewe anajiita  “njia, na  ukweli na  uzima”(Yn 14:6).

Katika Liturujia

Katika Liturujia yetu Amina ni kiitikio muhimu sana. Tunapoanza Sala zetu na kuhitimisha tunafanya Ishara ya Msalaba na kuitikiaAmina.Tunaposema Amina tunasisitiza umuhimu wa kuanza Sala au Liturujia tunayoadhimisha kwa jina la Utatu Mtakatifu. Kwa Sala hiyo msingi tunautukuza Utatu Mtakatifu na kuomba utuongoze katika Liturujia yetu tunayoadhimisha au Sala yetu tunayoitoa. Kwa kupiga Ishara ya Msalaba tunajiweka mikononi mwa Utatu Mtakatifu tunapoanza Sala zetu au kuadhimisha Liturujia, na tunapomaliza tunapiga tena Ishara ya Msalaba na kusemaAmina. Katika Adhimisho la Liturujia kwa kawaida kuhani huhitimisha kwa Baraka ndipo waamini hujiandika Ishara ya Msalaba.
Hata hivi katika Adhimisho moja la Liturujia kuna Sala mbalimbali ambazo kuhani au atazitamka kwa sauti peke yake kama mwongoza Adhimisho ili waamini wasikie na hatimaye waitikie Amina lakini kuna Sala ambazo kuhani hutakiwa kusali pamoja na waamini na wote watazihitimisha kwa pamoja kwa kiitikio hichohicho Amina. Tufuatane kuangalia Aminakatika Adhimisho la Ekaristi, yaani Misa.

Mwanzo wa Misa  

Mwanzoni kuhani huanza: Kwa Jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Kama tulivyosema hapo juu hii ni Sala ya msingi ambayo inatuweka mikononi mwa Utatu Mtakatifu tunapoanza kuadhimisha Liturujia yetu. Kuhani akishasema vile Wakristo wote wanatakiwa kuitikia Amina. Wale wasioitikia wanafanya kosa kubwa la kutokukiri imani kwamba tunajiweka mikononi mwa Utatu Mtakatifu. Wanatakiwa kujiuliza wamefika kanisani kufanya nini?
Kuhani huwasalimu waamini na kisha hutualika kukiri dhambi zetu. Hapo kuna namna mbalimbali za kukiri dhambi, lakini zote huishia na Sala anayotamka kuhani: Mungu mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele. Waamini wote hutakiwa kuitikia  Amina. Kwa nini wengine basi hawaitikii?
Hata hivi tukumbuke tendo hilo ni la kukiri dhambi na kuomba msamaha wa jumla katika kujiweka tayari kuadhimisha mafumbo matakatifu kama mwaliko wa kuhani unavyosema. Hiyo siyo nafasi ya Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Mkristo mwenye dhambi kubwa lazima aende kuungama kwa kuhani yaani padri au Askofu.
Baada ya tendo la kukiri dhambi na kuomba msamaha hufuata Utenzi wa Utukufu ambao huimbwa au kusemwa siyo na kwaya peke yaobali na waamini wote pamoja na kuhani. Utenzi huishia na Amina. Waamini wote pamoja na kuhani hukiri kwamba walivyoimba au kusali ni ukweli kabisa.
Sehemu ya Mwanzo wa Misa huhitimishwa na Sala iitwayo Kolekta, kutokana na neno la kilatini lenye maana ya kukusanya. Kuhani akishasema: Tuombe, inampasa kunyamaa kitambo ili kila Mkristo na kuhani mwenyewe wasali kimya ndipo kuhani ahitimishe maombi yao kwa sala iliyomo katika kitabu cha Misa. Sala anayosali kuhani ni kama inakusanya na kuhitimisha maombi ya Wakristo wote wanaoshiriki Misa hiyo. Mwishoni mwa Kolekta hiyo wote hutakiwa kuitikia Amina. Asiyeitikia huwaza nini moyoni mwake?

Liturujia ya Neno

Wakati wa Liturujia ya Neno, kabla ya Injili, kuhani hujiandaa kwa Sala fupi  ili kutangaza Injili. Iwapo Misa huongozwa na Askofu, shemasi au padri iwapo shemasi hayuko huomba Baraka kwa Askofu. Anapopata Baraka hupiga ishara ya Msalaba na kutikia Amina.
Baada ya mahubiri, siku za Dominika na Sherehe hufuata Kanuni ya Imani ambayo, kama utenzi wa Utukufu kwa Mungu juu, huimbwa au husemwa na Wakristo wote, na mwishoni wote humaliza kwa Amina.
Tunapomaliza sehemu ya Liturujia ya Neno kuhani huwaalika waamini kusali: Salini ndugu, ili sadaka yangu na yenu ikubalike kwa Mungu Baba mwenyezi. Wakristo wakishasali hawasemiAmina kwa sababu kuhani huendelea mara na Sala iitwayo Sala juu ya Vipaji (oratio super oblata) ambayo ni ya kuombea dhabihu. Baada ya Sala hiyo ndipo Wakristo wote huitikia Amina.Tujibidishe kufanya vile.

Sala Kuu ya Ekaristi

Sala ya kuombea vipaji huhitimisha sehemu ya kuandaa vipaji. Hufuata Sala Kuu ya Ekaristi inayoanza na dayalojia: Bwana awe nanyi,… Inueni mioyo .. Mwishoni mwa Sala Kuu ya Ekaristi hufuata kiitikio cha Amina, ambayo huitwa Amina Kuu. Waamini wote hutakiwa kuitikia kwa nguvu Amina hiyo Kuu. Katika Sherehe  waamini wote siyo kwaya peke yao, waimbe Amina mara tatu. Wanamuziki wazingatie hilo wakitunga muziki.
Baada ya Amina kuu hufuata sehemu ya kujiandaa kwa Komunyo Takatifu, inayoanza na Sala ya Bwana: Baba yetu uliye mbinguni. Baada ya sala hiyo hatuitikii Amina kwa sababu kuhani huendelea`mara :Ee Bwana, tunakuomba utuopoe …hatimaye wote huitikia: Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu…
Hufuata mara Sala ya kuomba Amani ambayo kuhani husali na mwishoni wote huitikia Amina. Wakati wa kupokea Ekaristi kila Mkristo hutakiwa kuitikia Amina kabla ya kupokea Mwili wa Bwana. Ni tendo la kukiri imani kwamba unasadiki huo ni Mwili wa Kristo. Wote huitikiaAmina mwishoni mwa Sala baada ya Komunyo.

Hatima

Mwishoni mwa Misa wakati kuhani anapowabariki waamini ndipo wote wakiinamisha vichwa vyao, hupiga Ishara ya Msalaba na kuitikia Amina ya mwisho.Wito kwa Wakristo wote: Tuitikie AMINA wakati wa Liturujia, bila kusita.Kwa kufanya vile tunashiriki na kusali  na kuhani tena tunakiri imani yetu kwamba alivyotamka kuhani ninakubali, ni kweli kabisa na Sala hiyo huwa Sala yetu pia.

MATATIZO YANAYORUDISHA UIMBAJI WA KWAYA KATOLIKI NYUMA

1.Kuwaimbia binadamu.Yaani tupo kwa ajili ya kuimba ili tusifiwe na watu.
2.Kuimba bila tafakari.Mara nyingi tunaimba tu bila kuzingatia ujumbe Wa ule wimbo
3.Kuimba bila kusali!Yasemekana Kuimba ni kusali Mara mbili.Waimbaji wengi hukariri wimbo na nyimbo nyingi zimetungwa kwa njia ya sala lakini wanakwaya wengi huimba tu wala hali ya sala haimo ndani yao!
4.Walimu wenye hasira na ubinafsi.Mkufunzi Wa kwaya ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya uimbaji.Iwapo choirmaster ni mwenye vurugu, mchochezi na mpenda fitina, bila shaka itakuwa vigumu kwa kwaya kupiga hatua kiuimbaji!
5.Sheria Kali zisizoenda na maadili ya kanisa.Kila jamii INA sheria zake na sheria ni nzuri.lakini tukiwa na sheria zinazowakandamiza wengine, tutapoteza kondoo wengi badala ya kuwaleta kwa Mungu!
6.Utoaji Wa albamu au kurekodi nyimbo kwa nia ya kutafuta pesa au kigezo kwa kwaya.Kwaya nyingi zimeanguka pindi tu wanapotoa albamu ya kwanza!Maana tunakosa kufahamu kuwa sisi ni wainjilisiti na tunawasaidia mapadri wetu kuhubiri injili.
7.Kutotii viongozi Wa kanisa.Wanakwaya wanaokosa kufahamu kuwa wapo chini ya viongozi na kanisa husika Mara nyingi hujipata wakiwa kwa makosa bila kunuia!
8.Kutoishi kwa hali ya sakramenti!Kama kuna jambo kubwa ambalo ibilisi hufurahia, ni yule MTU anayeishi katika maisha ya ndoa isiyo halali mbele za Mungu.Yaani Maana yake unaishi na mke au Mme bila ndoa ya kanisa na huna kizuizi chochote kinachokufanya usipate sakramenti hiyo.
9.Kitubio.Wengi tunapokea sakramenti ya ekaristi katika hali ya dhambi na hatushughuliki kabisaa kwenda kitubio.Hii inachochea zaidi kuwepo kwa dhambi za mazoea katika maisha yetu!
10.Kutosali kila siku.Inakuwa rahisi kwetu sisi kujaribiwa tukiwa hatusali.Kuimba kwako kunawasha hasira za shetani kwa hivo usiposali, bila shaka atarudi kulipiza kisasi.

Nifunge nini Kwaresma? Mambo ya kufunga kipindi cha Kwaresima

NIFUNGE NINI?
Funga huzuni upate furaha,
Funga ulabu upate siha,
Funga majivuno upata utukufu,
Funga uzinzi upate wongofu,
Funga kisirani upate utakatifu,
Funga umbea upate fanaka,
Funga wivu upata baraka,
Funga unafiki upate uchaji,
Funga kinyongo upate faraja,
Funga kwaresima wakati ni huu
Funga kiburi ujazwe hekima,
Funga jeuri ujawe rehema,
Funga hofu ujazwe imani,
Funga kinywani ujazwe moyoni,
Funga kisirani ujazwe rohoni,
Funga dharau ujazwe heshima,
Funga majungu, ujazwe neema,
Funga usiri ujawe wafuasi,
Funga tamaa ujazwe kiasi,
Funga kwaresima wakati ni huu.

Maana kamili ya Kwaresma

Neno kwaresma ni neno la kilatini liitwalo Quadragesima maana yake ni arobaini(40). Mpenzi msomaji, katika maisha ya kikristo kuna kipindi cha siku 40.majira haya ya kwaresma huanza siku ya jumatano ya majivu na kuishia jumapili ya pasaka siku ambayo wakristo wanakumbuka kufufuka kwa yesu kristo kutoka katika wafu.
Kwaresma ni kipindi maalum ambacho wakristo wanakumbuka maisha ya Yesu kristo hapa duniani hususan mateso, kufa na kufufuka kwake.
Ni kipindi cha kutafakari maana na umuhimu wa dhabihu ya YESU kristo katika ukombozi wa dunia na kumrudia Mungu. Aidha ni kipindi ambacho wakristo wanakumbushwa kufanya toba na kumrudia Mungu kwa mujibu wa maandiko matakatifu.
Ingawa kipindi cha kwaresma ni kipindi cha mafungo kwa wakristo, watu wengi na hasa wa dini nyingine hushindwa kutambua funga inayofanywa na wakristo katika kipindi hiki na hasa kwa sababu wakristo wengi huonekana wakiendelea kula na kunywa wakati wa kwaresma. Wakristo walio wengi pamoja na kufuata kielelezo cha Yesu kristo ambae alifunga siku arobaini (usiku na mchana) huzingatia maagizo ya YESU mwenyewe na nabii Isaya ambao kwa kiasi kikubwa hufafanua aina ya funga ambayo wakristo wanapaswa kuizingatia.
Mwenyezi Mungu alitoa maagizo ya namna ya kufunga kupitia kwa nabii isaya akisema hivi
“Walakini wanitafuta kila siku, hupenda kujua njia zangu ; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao. Hutaka kwangu sheria za haki, humkaribia Mungu. Husema, mbona tumefunga lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu lakini huangalii? Fahamuni siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je, kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je, ni siku ya mtu kujitabisha nafsi yake? je ni kuinamisha kichwa kama unyasi na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? je utasema ni siku ya kufunga na ya kukubaliwa na BWANA? Je, saumu niliyoichagua sio ya namna hii? Kufunguo vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaachia huru walio onewa, na kwamba mvunje kila nira? Je, sio kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? umwonapo mtu aliye uchi umvike nguo, wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapo pambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia, utukufu wa BWANA (Mungu) utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita na BWANA ataitika, utalia nae atasema mimi hapa…” (Isaya 58: 2-9).
Mwenyezi Mungu alitoa maagizo haya baada ya kuona watu wengi wakipoteza muda mwingi na kujitabisha kuacha kula na kujitesa miili yao ili kumpendeza Mungu, huku wakisahau mambo muhimu zaidi ambayo Mungu anawataka wafanye ili kumpendeza. (Katika kipindi hicho wayahudi walikuwa wakifunga kwa kujitesa sana ikiwa ni pamoja na kuacha kula, kuvua nguo zao za thamani na kuvaa magunia, kujipaka majivu na wengine kujipiga na kujikata miili yao ili waone maumivu zaidi.
Aidha, watu walikuwa wakitumia kipindi cha kufunga kuuonesha umma jinsi walivyo wacha Mungu na hivyo kupewa heshima mtaani. Mtu asiyefunga alionekana mjinga, mtenda dhambi na asiyefaa katika jamii. Kufunga ilikuwa sehemu ya maisha na si suala la uhusiano binafsi kati ya mtu na Mungu).

Kwa vile Mwenyezi Mungu wetu ni wa upendo na huruma, alimtuma nabii isaya kuwaambia watu hao kuachana na funga hiyo isiyo na maana na badala yake kuelekeza nguvu zao katika mambo muhimu ambayo Mungu anaangalia katika kutathimini utu wa mtu. Mambo hayo ni upendo, huruma na kujitoa kama ilivyoelezwa hapo juu na kuachana uovu wa aina zote.. Kwa msingi huo, mtu mwenye upendo na anaejitoa kusaidia wengine ana thamani kubwa mbele za Mungu kuliko mtu anaeshinda njaa siku 300 za mwaka pasipo kuonesha upendo wa kweli kwa wengine.
Yesu kristo alipokuja ulimwenguni, alisisitiza maneno ya nabii Isaya kwa kutaka watu waache tabia ya funga za kujionesha kwa watu, na badala yake wajitahidi kumpendeza Mugu.
Yesu alisema “Tena mfungapo msiwe kama wanafiki wenye nyuso za kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amini nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na baba yako (Mungu) aliye sirini; na baba yako aonae sirini atakujazi” (Mathayo 6:16)
Kumbe tabia ya kujionesha mbele za watu kwamba tumefunga inamuudhi Mungu na kutufanya tukose thawabu. Mtu anaejionesha au kujisifu kwamba anafunga huambulia kusifiwa na watu wa kidunia ambao wanadhani mtu huyo ni mtakatifu sana, lakini kwa mujibu wa maandiko matakatifu mtu huyo anajisumbua na kupoteza muda wake bure kwani hakuna thawabu anayo pata kwa Mwenyezi Mungu.
Tumuombe Mungu sana atuongoze na kutusaidia katika kipindi hiki cha Kwaresma na baada ya hapo.Ni wajibu wetu kujitahidi kuachana na maovu yote, kufanya toba ya kweli na kumpokea Yesu katika mioyo yetu badala ya kumuabudu kwa midomo tu. Tunapaswa kukumbuka kuwa Mungu wetu ni yule yule kabla, wakati na baada ya kipindi cha Kwaresma na hivyo kipindi hiki kiwe kipindi cha kutukumbusha na kutuandaa kwa ajili ya wakati mrefu ujao baada ya Kwaresma.
Shopping Cart