Sala za Katoliki: Sala Muhimu Kwa Mkristu Mkatoliki

ROSARI YA BIKIRA MARIA MAMA WA MSAADA WA DAIMA

Namna ya kusali Rozari kwa Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima

(Tumia rosari ya kawaida)

Mwanzo, kwenye Msalaba:

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

Kwenye chembe ndogo za awali:

K: Ee Mungu utuelekezee msaada W: Ee Bwana utusaidie hima
W: Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.

Maria ametusaidia,
Maria anataka kutusaidia,
Maria anaweza kutusaidia,
Maria atatusaidia.

KATIKA KILA FUNGU SALI SALA ZIFUATAZO:

Kwenye chembe kubwa:

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama mwanzo na sasa, na siku zote, na milele. Amina.

Maria ametusaidia,
Maria anataka kutusaidia,
Maria anaweza kutusaidia,
Maria atatusaidia.

Ee Maria Mama wa Msaada wa daima
Sikiliza maombi ya roho zetu
Unaweza kutusaidia katika mahitaji yetu
Ee Maria kwa matumaini twakuita wewe.

Kwenye chembe ndogo:

Kama unasali mwenyewe: β€œEe Maria, utusaidie! (mara kumi)
Kama mnasali zaidi ya mmoja kwa pamoja: K; Ee Maria, W: Utusaidie. (mara kumi)

MWISHO SALI SALA ZIFUATAZO:

Salamu Maria

Salamu Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu Mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa, na saa ya kufa kwetu. Amina. (mara tatu)

Tunaukimbilia

Tunaukimbilia ulinzi wako, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, usitunyime tukiomba katika shida zetu, utuokoe siku zote, kila tuingiapo hatarini, ee Bikira Mtukufu na mwenye baraka,. Amina.

Majitoleo ya Asubuhi

Ee Baba yetu Mungu Mkuu, Umenilinda usiku huu, Ninakushukuru kwa moyo, Ee Baba, Mwana na Roho, Nilinde tena siku hii, Niache dhambi nikutii, Naomba sana Baba wee, Baraka yako nipokee, Bikira safi ee Maria, Nisipotee unisimamie, Mlinzi Mkuu Malaika wee, Kwa Mungu wetu niombee, Nitake nitende mema tu, Na mwisho nije kwake juu, Amina.

SALA YA MAJITOLEO KWA MAMA WA HUZUNI

Mama Mtakatifu, Mama wa Mungu na Malkia wa Mashahidi, leo nakuchagua Wewe uwe mfano wangu, mkingaji na mteteaji wangu. Naweka roho fukara katika moyo wako uliotobolewa na panga nyingi za mateso. Unipokee mimi niwe mtumishi wako wa pekee na mshiriki wa mateso yako. Nijalie nguvu niwe daima karibu na msalaba ule alikosulibiwa Yesu. Nakutolea nafsi yangu na mali yangu yote. Pokea kila tendo langu jema ukalisindikize kwa Mwanao, Mama, nifanye nistahili kuitwa mtumishi wa Maria, Simama karibu yangu katika matendo yangu yote ili yafanwe kwa sifa ya Mungu. Ulivyosimama karibu kabisa ya Mwanao alipokufa msalabani uwe karibu nami saa ya kufa kwangu. Nijalie niweze kutaja jina lako na la Mwana wako nikisema: β€œYesu, Maria na Yosef mnisaidie saa ya kufa kwangu. Yesu, maria na Yosef, naomba nife kwa amani kati yenu!” . Amina.

Shopping Cart