Masomo ya Misa ya Kanisa Katoliki

MASOMO YA MISA, MACHI 29, 2022: JUMANNE: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

SOMO 1

Eze. 47:1-9, 12

Malaika alinileta mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume. Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini, akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpka viweko vya miguu.

Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno. Kisha akapima dhiraa elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika. Akaniambia, Mwanadamu, je! Umeona haya? Kisha akanichukua, akanirudisha mpaka ukingo wa mto.

Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu. Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari; maji yatokezwayo yataingia baharini, na maji yake yataponyeka. Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisonganamacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko; maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi popote utakapofikilia mto huo.

Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 46:1-2, 4-5, 7-8 (K) 7

(K) Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,

Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi,

Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. (K)

Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu,

Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.

Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa;

Mungu atausaidia asubuhi na mapema. (K)

Bwana wa majeshi yu pamoja nasi,

Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

Njoni myatazame matendo ya Bwana,

Jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi. (K)

SHANGILIO

Amo. 5:14

Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi, hivyo Bwana, atakuwa pamoja nanyi.

INJILI

Yn. 5:1-3, 5-16

Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akakwea kwenda Yerusalemu. Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Betzatha, nayo ina matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza.

Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda.

Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende. Basi wakamwuliza, Yule aliyekuambia, Jitwike uende, ni nani? Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maan aYesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale.

Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi. Yule akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya sabato.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MACHI 28, 2022: JUMATATU: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

SOMO 1

Isa. 65:17-21

 

Bwana asema: Tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni. Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.

Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza. Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa. Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 30:1, 3-5, 10-12 (K) 1

 

(K) Nitakutukuza, ee Bwana, kwa maana umeniinua.

 

Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,

Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.

Umeniinua nafsi yangu,

Ee Bwana, kutoka kuzimu.

Umenihuisha na kunitoa

Miongoni mwao washukao shimoni. (K)

 

Mwimbieni Bwana zaburi,

Enyi watauwa wake.

Na kufanya shukrani.

Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.

Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,

Katika radhi yake mna uhai.

Huenda kilio huja kukaa usiku,

Lakini asubuhi huwa furaha. (K)

 

Ee Bwana, usikie, unirehemu,

Bwana, uwe msaidizi wangu.

Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;

Ulinivua gunia, ukanivika furaha.

Ee Bwana, mungu wangu,

Nitakushukuru milele. (K)

 

SHANGILIO

Eze. 33:11

 

Sikufurahii kufa kwake mtu mwovu, asema Bwana, bali aiache njia yake mbaya, akaishi.

 

INJILI

Yn. 4:43-54

 

Baada ya siku mbili hizo Yesu aliondoka huko, akaenda Galilaya. Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi alipofika Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu.

Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa? Yule diwani akamwambia, Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu. Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia. Hata alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai. Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa hajambo; nao wakamwambia, jana, saa saba, homa ilimwacha. Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile alipoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake.

Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa ametoka Uyahudi kufika Galilaya.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, DOMINIKA YA 4 YA KWARESIMA, MARCHI 27, 2022

SOMO 1: Yos. 5:9a, 10-12

Bwana akamwambia Yoshua, Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu.

Basi wana wa Israeli wakapanga hema zao huko Gilgali; nao wakala sikukuu ya pasaka siku ya kumi ya nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandama hiyo sikukuu ya pasaka, mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku iyo hiyo.

Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala katika viliwa vya nchi ya Kanaani mwaka huo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 34:1-6 (K) 8

(K) Onjeni muone ya kuwa Bwana yu mwema.

Nitamhimidi Bwana kila wakati,

Sifa zake kinywani mwangu daima.

Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,

Wanyenyekevu wasikie wakafurahi. (K)

Mtukuzeni Bwana pamoja nami,

Na tuliadhimishe jina lake pamoja.

Nalimtafuta Bwana akanijibu,

Akaniponya na hofu zangu zote. (K)

Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,

Wala nyuso zao hazitaona haya.

Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,

Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

SOMO 2: 2 Kor. 5:17-21

Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya. Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.

SHANGILIO: Lk. 15:18

Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.

INJILI: Lk. 15:1-3, 11-32

Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao. Akawaambia mfano huu, akisema.

Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.

Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye.

Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteeni ndama yule aliyenona mkamchinje nje; nasi tule na kufurahi; kw akuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.

Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani.

Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema. Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wowote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.

Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami siku zote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.

Neno la Bwana…sifa kwako Ee Kristo

MASOMO YA MISA, MACHI 26, 2022: JUMAMOSI, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

SOMO 1

Hos. 5:15-6:6

Bwana asema: Katika taabu yao watanitafuta kwa bidii:

Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu. Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tuataishi mbele zake. Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyeshayo nchi.

Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema. Kwa sababu hiyo nimewakata-kata kwa vinya vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa change na hukumu yangu itatokea kama mwanga. Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 51:1-2, 16-19 (K) Hos. 6:6

(K) Ninavyotaka ni fadhili, si sadaka.

Ee Mungu, unirehemu,

Sawasawa na fadhili zako.

Kiasi cha wingi wa rehema zako,

Uyafute makosa yangu.

Unioshe kabisa na uovu wangu,

Unitakase dhambi zangu. (K)

Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,

Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.

Dhabihu za MUngu ni roho iliyovunjika;

Moyo uliovunjika na kupondeka,

Ee Mungu, hutaudharau. (K)

Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,

Uzijenge kuta za Yerusalemu.

Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki,

Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. (K)

SHANGILIO

Eze. 18:3

Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa yote, asema Bwana, jifanyieni moy mpya na roho mpya.

INJILI

Lk. 18:9-14

Yesu aliwaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mpato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MACHI 25, 2022: IJUMAA, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

MASOMO YA MISA, MACHI 25, 2022
IJUMAA, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

SHEREHE YA KUPASHWA HABARI YA KUZALIWA BWANA

 

SOMO 1

Isa. 7:10 – 14
Bwana alisema na Ahazi akinena, Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana. Naye akasema, Sikilizeni sana, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 40:6 – 10 (K) 7 , 8

(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya mapenzi yako.

Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)

Katika gombo la chuo nimeandikiwa
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)

Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)

Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
Katika kusanyiko kubwa. (K)

SOMO 2

Ebr. 10:4 – 10
Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) niyafanye mapenzi yako, Mungu.
Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.

Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO

Yn. 1:14

Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukaona utukufu wake.

INJILI

Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye ju, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Shopping Cart