Masomo ya Misa ya Kanisa Katoliki

MASOMO YA MISA, JUMAPILI JULAI 25 2021: DOMINIKA YA 17 YA MWAKA B WA KANISA

SOMO 1

2 Wafalme:4.42

Alikuja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale. Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandikie hiki watu mia? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa Bwana asema hivi, Watakula na kusaza. Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.

WIMBO WA KATIKATI

1. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako. (K)

Waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.

2. Macho ya watu yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake. (K)

3. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu.

SOMO 2

Waefeso:4.1 – 6

Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.

SHANGILIO

Yohana:14.6

Aleluya Aleluya!

Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, asema Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Aleluya

INJILI

Yn. 6:1-15

Yesu alikwenda zake ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.

Neno la Bwana….. Sifa Kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JULAI 24, 2021: JUMAMOSI, JUMA LA 16 LA MWAKA

SOMO 1

Kut. 24:3-8

Musa aliwambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 50:1-2, 5-6, 14-15 (K) 14 (K)

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru. Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi, Toka maawio ya jua hata machweo yake. Tokea Sayuni,, ukamilifu wa uzuri, Mungu amemulika. (K)

Nikusanyieni wacha Mungu wangu, Waliofanya agano nami kwa dhabihu. Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu. (K)

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru; Mtimizie Aliye juu nadhiri zako. Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza. (K)

SHANGILIO

Zab. 8:15

Aleluya, aleluya,

Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika.

Aleluya.

INJILI

Mt. 13:24 – 30

Yesu aliwatolea makutano mfano akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala akaja adui yake akapanda magugu katikati ya agano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Shopping Cart