Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

SALA KWA BIKIRA MARIA KATIKA UKIWA WAKE

Nakusikitikia sana Mama Mtakatifu Maria kwa sababu ya ukiwa wako mkuu. Uchungu wako ulikuwa mkubwa sana ulipotazama mateso na kifo cha Mwana wako mpenzi. Muda ule uliweza kutuliz kidogo kwa sababu ya kumwona angali hai. Lakini je, baada ya kufa na kumzika? Sasa wewe ni mkiwa mkubwa mno! Uh, ukiwa wa pekee, uniombee mimi ninayempoteza mara nyingi kwa dhambi zangu. Unijalie nisimpoteze tena Yesu wangu kwa ubaya wa uvivu wangu, bali nimtumikie kiaminifu duniani hapa ili nimwone na kumfurahia milele mbinguni. Amina.

ROZARI YA MATESO SABA YA BIKIRA MARIA

Tumia Rozari ya Mateso Saba ya Bikira Maria iliyo na mafungu 7 yaani mateso 7 yenye Salamu Maria saba kwa kila teso.

TESO LA KWANZA

Mzee Simeoni aliagua kuwa Moyo wa Mama Maria utachomwa kwa upanga.
Tuombe neema ya kuvumilia mateso.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA PILI

Maria na Yosefu walikimbilia Misri usiku ili kumficha Mtoto Yesu asiuawe na Herodi.
Tuombe neema ili miili yetu iwe kimbilio lake Yesu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA TATU

Mama Maria aliona uchungu sana Mtoto Yesu alipopotea kwa siku tatu.
Tuombe neema ya kudumu na Yesu mioyoni mwetu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA NNE

Mama Maria aliona uchungu sana alipokutana na Mwanae Yesu katika njia ya Msalaba.
Tuombe neema ya kudumu na Yesu siku zote.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA TANO

Mama Maria aliona uchungu sana alipomwona Mwanae Yesu akisulibiwa Msalabani.
Tuombe neema ya kufa mikononi mwa Yesu na Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA SITA

Mama Maria aliona uchungu sana alipopakata maiti ya Mwanae Yesu baada ya kushushwa Msalabani.
Tuombe neema ya kutotenda dhambi.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA SABA

Mama Maria aliona uchungu sana aliporudi nyumbani baada ya kumzika Mwanae Yesu
Tuombe neema ya kitulizo kwa Mama Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

SALA YA MAOMBI KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakukimbilia, ninakuja kwako katika mikono yako yenye huruma. Ndiwe tegemeo langu na tumaini langu dhabiti. Ndiwe mwenye dawa ya maovu yangu yote, malipizi ya makosa yangu yote. Waweza kunipatia haja zangu na neema ninazoziomba mimi na wengine. Wewe uko ili kutusaidia sote, ndiwe mwanga mkuu usiozimika, ndiwe chanzo cha nguvu, uvumilivu, amani na faraja. Nina hakika kuwa maombi yangu hayatakuchosha, nawe hutaacha kunisaidia, kunilinda, kunipenda, kwani, ee Moyo Mtakatifu , upendo wako hauna mwisho. Ee Moyo Mtakatifu, unihurumie, kwa ajili ya maombi yangu, kadiri ya huruma yako. Nawe katika sisi, na kwa ajili yetu, ufanye lolote unalolihitaji, kwani tunajitoa kwako kwa imani na uhakika thabiti kwamba kamwe hautatuacha, kwa milele. Amina.

LITANIA YA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie
Kristo utuhurumie Kristo utuhurumie
Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie
Kristo utusikie Kristo utusikilize
Baba wa mbinguni Mungu Utuhurumie
Mwana, Mkombozi wa dunia Mungu Utuhurumie
Roho Mtakatifu Mungu Utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu mmoja Utuhurumie
Moyo wa Yesu Mwana wa Baba wa Milele Utuhurumie
Moyo wa Yesu uliotungwa na Roho Mtakatifu mwilini mwa Mama Bikira Maria Utuhurumie
Moyo wa Yesu ulioungana na Neno wa Mungu Utuhurumie
Moyo wa Yesu ulio na utukufu pasipo mfano Utuhurumie
Moyo wa Yesu, hekalu takatifu la Mungu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, hema la Yule aliye juu Utuhurumie
Moyo wa Yesu tanuru lenye kuwaka mapendo Utuhurumie
Moyo wa Yesu, nyumba ya Mungu na mlango wa Mbingu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, tanuru yenye kuwaka mapendo Utuhurumie
Moyo wa Yesu, chombo cha haki na upendo Utuhurumie
Moyo wa Yesu, unaojaa upendo na wema Utuhurumie
Moyo wa Yesu, kilindi cha fadhila zote Utuhurumie
Moyo wa Yesu, unaostahili sifa zote Utuhurumie
Moyo wa Yesu, unaotawala mioyo yote Utuhurumie
Moyo wa Yesu, zinamokaa hazina za hekima na elimu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uliopendelewa na Mungu Baba Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uliotuenezea maziada yake Utuhurumie
Moyo wa Yesu, mtamaniwa wa vilima vya milele Utuhurumie
Moyo wa Yesu, wenye uvumilivu na huruma nyingi Utuhurumie
Moyo wa Yesu, tajiri kwa wote wenye kukuomba Utuhurumie
Moyo wa Yesu, chemchemi ya uzima na utakatifu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, malipo kwa dhambi zetu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, ulioshibishwa matusi Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uliovunjika kwa sababu ya ubaya wetu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uliotii mpaka kufa Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uliochomwa kwa mkuki Utuhurumie
Moyo wa Yesu, chemchemi ya faraja zote Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uzima na ufufuo wetu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, amani na upatanisho wetu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, sadaka ya wakosefu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, unamokaa wokovu wao wenye kukutumaini Utuhurumie
Moyo wa Yesu, matumaini yao wenye kuzimia kwako Utuhurumie
Moyo wa Yesu, sababu ya furaha ya watakatifu wote Utuhurumie
Mwanakondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za dunia Utusamehe Bwana
Mwanakondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za dunia Utusikilize Bwana
Mwanakondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za dunia Utuhurumie

Kiongozi: Yesu mwenye Moyo mpole na mnyenyekevu,
Wote: Ufanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako

TUOMBE: (W) Ee Mungu Mwenyezi milele, uuangalie Moyo wa mwanao mpendelevu, pia na heshima na malipo aliyokutolea kwa ajili ya wenye dhambi, uridhike, uwaondolee wenye kuomba toba kwako kwa njia ya huyo Mwanao Yesu Kristo anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu milele. Amina.

Mungu Anakuita Na Kukupa Nafasi Ya Kutubu Na Kumrudia Yeye Ili Akusamehe na Kukubariki

Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu. Zab 95:7-8

Tunaalikwa kutubu na kumrudia Mungu kwa Mioyo yetu yote na kwa nia dhabiti. Mungu ni mwaminifu, atatusamehe dhambi zetu na kutufanya kuwa wapya.

Dawa ya dhambi ni kutubu na kusamehewa.

Kutubu sio kusema tuu “Ninatubu” au “Ninaomba msamaha”. Kutubu ni kuona uchungu kweli rohoni kwa dhambi tulizotenda, tukizikataa na kunuia kutokuzitenda tena.

12“Lakini hata sasa,”
nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
“Nirudieni kwa moyo wote,
kwa kufunga, kulia na kuomboleza.
13Msirarue mavazi yenu kuonesha huzuni
bali nirudieni kwa moyo wa toba.”
Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu;
yeye amejaa neema na huruma;
hakasiriki upesi, ni mwingi wa fadhili;
daima yu tayari kuacha kuadhibu.
14Huenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atabadili nia
na kuwapeni baraka ya mazao,
mkamtolea sadaka za nafaka na kinywaji.
15Pigeni tarumbeta huko Siyoni!
Toeni amri watu wafunge;
itisheni mkutano wa kidini.
16Wakusanyeni watu wote,
wawekeni watu wakfu.
Waleteni wazee,
wakusanyeni watoto,
hata watoto wanyonyao.
Bwana arusi na bibi arusi
na watoke vyumbani mwao.
17Kati ya madhabahu na lango la hekalu,
makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu,
walie na kuomba wakisema:
“Wahurumie watu wako, ee Mwenyezi-Mungu.
Usiyaache mataifa mengine yatudharau
na kutudhihaki yakisema,
‘Yuko wapi basi Mungu wao?’” Yoeli 2:12-17

Uzuri wa Mungu ni kwamba anasamehe na kusahau, tunapotubu dhambi zetu Mungu anatufutia makosa yetu, anaponya majeraha au madhara yaliyoletwa na dhambi hiyo na kisha antubariki kwa Neema na Vipawa vya kusonga Mbele.

Maana nitawasamehe makosa yao, wala sitazikumbuka tena dhambi zao.” Yeremia 31:34

Mungu anatambua kwamba Binadamu ni dhaifu na anaweza kuanguka dhambini ndio maana anatupa nafasi ya Kutubu na Kumrudia yeye.

13Afichaye makosa yake hatafanikiwa;
lakini anayeungama na kuyaacha atapata rehema. Methali 28:13

Mungu anazifahamu juhudi zetu katika kutafuta kutenda mema ndio maana anakubali toba ya kweli na anatupa matumaini ya kusonga mbele.

“Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”. Isaya 1:18

Biblia inatuambia kuwa anaheri yule atubuye na kusamehewa kosa lake kwa sababu hana hatia mbele ya Mungu.

1 Heri yake mtu aliyesamehewa kosa lake,
mtu ambaye dhambi yake imeondolewa kabisa.
2Heri mtu ambaye Mwenyezi-Mungu hamwekei hatia,
mtu ambaye hana hila moyoni mwake. Zaburi 32:1-2

Tunapaswa kukumbuka kuwa toba ya kweli ya kutupa msamamaha inaambatana na kuwasamehe wengine na kuondoa kinyongo kwa wengine waliotukosea. Yesu anatufundisha kuwa inatupasa tusamehe ili na sisi tusamehewe.

14“Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia. 15Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu. Mathayo 6:14-15

Tena, Mungu anatusamehe Makosa Yetu bila kujali tunakosea Mara nagpi na tunarudi kwake mara ngapi. Ndio maana Yesu alitufundisha kuwa tunapokosewa na wenzetu ni lazima tuwasamehe haijalishi wametukosea mara ngapi.

3Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, muonye; akitubu, msamehe. 4Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema, ‘Nimetubu,’ lazima umsamehe.” Luka 17:3-4

Unapotubu na kuomba msamaha ni sharti uwasamehe pia wale waliokukosea ili na wewe usamehewe. Kusameheana na wenzetu ndio tabia ya Kimungu ambayo yatupasa kujifunza na kuiishi ili na sisi tuwe watoto wema wa Mungu.

12Nyinyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe nyinyi. Wakolosai 3:12-13

Tumuombe Mungu atujalie Moyo wa toba na kujirudi kwake Kila tunapokosea. Na tumuombe pia atupe nguvu na uwezo wa kuwasamehe wale wanaotukosea.

KUMBUKA: Unapotubu dhambi zako na kusamehewa ndipo inapokuwa rahisi kwa sala zako kujibiwa. Mungu ni rafiki ya waliosafi Moyoni, na ndio anaowasikiliza na kuwaonyesha nguvu na uwezo wake.

Nakualika kwa Sala ya Toba, uweze kurudi kwa Mungu. Sali kutoka moyoni, kwa kujua kuwa unapendwa na Mungu, Kwa Imani na Matumaini Kwake.

Sala ya Toba

Mungu wangu, Baba wa mbinguni, nakuja mbele zako nikiwa na moyo uliovunjika na toba ya kweli. Nakiri kuwa mimi ni mwenye dhambi, na nimekosa mbele zako kwa njia nyingi. Nimefanya mambo ambayo hayakupendeza, na nimeshindwa kutenda yale uliyoniagiza. Kwa kuwa Neno lako linasema, “Kwa maana wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23).

Ee Bwana, naomba unisamehe dhambi zangu zote. Nimetenda dhambi kwa mawazo, kwa maneno, na kwa matendo. Ninatubu kwa dhati na kwa kweli kutoka moyoni mwangu. Naomba unioshe kwa damu ya Yesu Kristo, Mwanao mpendwa, ambaye alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu. Kama unavyosema katika Neno lako, “Lakini ikiwa tutatembea katika nuru kama Yeye alivyo katika nuru, tu ushirika sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote” (1 Yohana 1:7).

Ninakiri kuwa mimi ni mnyonge bila wewe, na siwezi kufanya lolote bila msaada wako. Naomba unijaze na Roho Mtakatifu, aniongoze na kunipa nguvu ya kushinda majaribu na dhambi. Ee Mungu, niongoze katika njia zako za haki, na unisaidie kuishi maisha yanayokupendeza. Kwa kuwa Neno lako linasema, “Basi kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu” (Wakolosai 3:1).

Ninakuja mbele zako nikiwa na unyenyekevu na moyo wa toba. Naomba unirehemu na unifanye kuwa kiumbe kipya ndani ya Kristo. Kama unavyosema katika Neno lako, “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama! yamekuwa mapya” (2 Wakorintho 5:17). Asante kwa upendo wako usio na kikomo, na kwa neema yako inayotosha kila siku. Naomba haya yote kwa jina la Yesu Kristo, aliye Mwokozi wangu.

Bwana, naomba unifundishe kuwa mtiifu na kuwa na moyo wa shukrani kwa kila jambo. Acha neno lako likae kwa wingi ndani yangu, na linibadilishe kutoka ndani hadi nje. Nisaidie kuacha njia zote za dhambi, na kuwa mwaminifu kwako katika kila hali. Kwa kuwa Neno lako linasema, “Neno lako nimeliweka moyoni mwangu, nisije nikakutenda dhambi” (Zaburi 119:11).

Ninakubali kuwa mimi ni mnyonge na ninahitaji msaada wako kila siku. Nakiri dhambi zangu na naomba unisamehe. Naomba unipatie moyo safi, na kunifufua kiroho. Kama unavyosema katika Neno lako, “Ee Mungu, uniumbie moyo safi, unirejeshee roho iliyotulia ndani yangu” (Zaburi 51:10). Naomba unifanye kuwa mwanga na chumvi duniani, ili niweze kuonyesha upendo wako kwa wengine. Kwa kuwa Neno lako linasema, “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima” (Mathayo 5:14).

Asante, Bwana, kwa kusikia sala yangu. Naamini kuwa umesikia na kujibu ombi langu. Ninatangaza kuwa mimi ni wa Kristo, na ninakubaliana na mapenzi yako maishani mwangu. Kama unavyosema katika Neno lako, “Ninaweza kufanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” (Wafilipi 4:13). Kwa jina la Yesu, Amina.

Shopping Cart