Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

Sala ya Kuombea Hali njema ya hewa na mvua

Ee Mungu Mwenyezi wa milele, mpaji wa mema yote, unayetusamehe na kutulinda. Utujalie sisi tunaokusihi, tufurahie hali njema ya hewa na mvua tunayoitamani na kuhitaji. Tutumie daima vipawa vya wema wako kwa ajili ya utukufu wa jina lako, na kwa ajili ya wokovu watu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana watu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele. Amina. `

`Baba Yetu………………. Salama Maria………… Atukuzwe Baba……….. `

K: `Bikra Maria mama wa msaada wa daima…. W: Utuombee na Utusaidie`

AMRI ZA MUNGU

1. NDIMI BWANA MUNGU WAKO, USIABUDU MIUNGU WENGINE.
2. USILITAJE BURE JINA LA MUNGU WAKO.
3. SHIKA KITAKATIFU SIKU YA MUNGU.
4. WAHESHIMU BABA NA MAMA, UPATE MIAKA MINGI NA HERI DUNIANI.
5. USIUE
6. USIZINI
7. USIIBE
8. USISEME UONGO
9. USITAMANI MWANAMKE ASIYE MKE WAKO
10. USITAMANI MALI YA MTU MWINGINE

SALA YA KUOMBEA FAMILIA

Ewe Mungu Mwenyezi, sisi kama familia tunakushukuru kwa zawadi ya Mama Kanisa Katoliki ambaye siku zote hutupatia malezi bora kwa ajili ya wokovu wetu. Kanisa halichoki kutuhimiza tutafakari na kuishi utakatifu wa familia ya Nazareti ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia hii iliishi upendo uliojengwa kwa fadhila za imani, uaminifu, utii, uvumilivu na upole hata wakawa watakatifu. Tunapoadhimisha mwaka wa Familia, tunaiweka mbele yetu familia ya Nazareti iwe dira, baraka na mfano kwa familia zetu.

Tunakushukuru Baba kwa ajili ya familia zote zinazojitahidi kuishi fadhila hizo za Familia takatifu na tunakuomba uzidi kuwaimarisha wanandoa ili tupate kwao mifano mingi na bora ya kuigwa. Ee Bwana, tunaomba Roho Mtakatifu atuangazie tuweze: kutambua familia kuwa Kanisa la nyumbani na shule ya imani na upendo; kuimarisha familia kwa sala, sakramenti na tunu za kiinjili na kushirikiana kwa heshima katika familia kwa usitawi wa roho na wa mwili kwa wanafamilia wote.

Tunaziombea familia zetu na Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ziwe bustani bora na salama za kuchipusha na kulea miito mitakatifu ya Ndoa, Utawa na Upadre. Tunawaombea vijana na watoto wetu Uchaji wa Mungu ili wawe na bidii ya kujitunza kwa kushika amri za Mungu na kuishi fadhila za kiinjili, wawe na roho ya kimisionari yaani walipende Kanisa na kuwa na moyo wa kueneza ufalme wako kwa matendo ya imani. Baba wa huruma, tunakukabidhi familia zenye misukosuko ya mafarakano, ulevi, ubinafsi, uregevu-dini, uvivu, ushirikina, hofu, magonjwa sugu na mengineyo yenye kuleta huzuni; kwa hisani yako uwape neema, mwanga na nguvu za kuanza maisha mapya yenye amani, waweze kufurahia upatanisho na uponyi wa pendo lako la kibaba kati yao.

Tunaomba toba na msamaha kwa ukatili, manyanyaso na hata mauaji katika familia zetu na uwaponye wote waliojeruhiwa kwa maneno, matendo na makwazo ya aina yeyote. Aidha tunakuomba uwe kitulizo na faraja kwa wagonjwa na wazee, pia tegemeo la yatima na wajane. Wenye matatizo ya kiafya au ya kijamii wasikate tamaa bali waunganishe hali zao na msalaba wa Mwanao na kukutumaini wewe Mweza yote. Jamii iwajibike nao kwa kuzijali haki zao na kuwapa misaada wanayohitaji.

Tunakuomba ubariki miradi na kazi zetu ili familia zipate usitawi na maendeleo; na utujalie hekima ya kukushukuru kwa maisha ya haki, amani na ukarimu na mwisho tukaimbe sifa zako pamoja na familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefuna jeshi lote la mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

Baba yetu… …..Salamu Maria….…Atukuzwe Baba………

Sala ya Malaika wa Bwana

Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria, naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Salamu Maria,….

Ndimi Mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena. Salamu Maria, ……
Neno wa Bwana akatwaa Mwili, akakaa kwetu. Salamu Maria, …..

Utuombee, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, tujaliwe ahadi za Kristo.

Tuombe:

Tunakuomba ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika, kwamba, Kristo Mwanao amejifanya mtu: kwa mateso na Msalaba wake, utufikishe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu, Amina.

Kuweka nia njema

Kumheshimu Mungu wangu, Namtolea roho yangu, Nifanye kazi nipumzike, Amri zake tu nishike, Wazo neno tendo lote, Namtolea Mungu pote, Roho, mwili chote changu, pendo na uzima wangu, Mungu wangu nitampenda, Wala dhambi sitatenda, Jina lako nasifia, Utakalo hutimia, Kwa utii navumilia, Teso na matata pia, Nipe Bwana neema zako, Niongezee sifa yako, Amina.

Shopping Cart