Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

Malkia wa Mbingu

Malkia wa mbingu, furahi, aleluya. Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya. Amefufuka alivyosema, Aleluya. Utuombee kwa Mungu, Aleluya. Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya. Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya. Tuombe. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.

Novena ya Noeli

Novena ya Noeli (maarufu kama novena ya Mt. Andrea)

Husaliwa kuanzia tar 30 Nov hadi usiku wa Noeli, tar 24 Disemba. Inajulikana kama novena ya Mt. Andrea kwa sababu novena hii huanza kusaliwa katika siku ya kumbukumbu ya Mt. Andrea Mtume.

“IHESHIMIWE, NA IBARIKIWE, SAA ILE NA WAKATI ULE, AMBAO MWANA WA MUNGU, ALIZALIWA NA BIKIRA MBARIKIWA SANA, USIKU WA MANANE, KULE BETHLEHEM, WAKATI WA BARIDI KALI.
WAKATI HUO, UPENDE E MUNGU WANGU, KUSIKIA MAOMBI YANGU, NA KUNIJALIA YALE NINAYOYAOMBA KWAKO, KWA NJIA YA MASTAHILI YA MWOKOZI WETU YESU KRISTO, NA YA MAMA YAKE MBARIKIWA. AMINA. (Sali mara 15 kwa siku).

Inasadikika kuwa chochote uombacho kwa imani kwa sala hii utakipata mradi kipatane na mapenzi ya Mungu. Sali na watoto/ familia kuwatafakarisha na kuwaongezea matazamio juu ya sikukuu ya Noeli.

Isambaze sala hii kwa wengine.

Sala ya Asubuhi ya kila siku

Kwa jina la Baba…..

Ee Baba yetu Mungu mkuu,umenilinda usiku huu.
Nakushukuru kwa moyo, ee Baba,Mwana na Roho.
Nilinde tena siku hii,niache dhambi nikutii.Naomba sana Baba wee, baraka yako nipokee.
Bikira safi, Ee Maria nisipotee nisimamie.
Mlinzi mkuu malaika wee kwa Mungu wetu niombee,nitake nitende mema tu na mwisho nije kwako juu.Amina.

NIA NJEMA.

Kumueshimu Mungu wangu,namtolea roho yangu.
Nifanye kazi nipumzike ,amri zake tu nishike.
Wazo,neno,tendo lote namtolea Mungu pote Roho,Mwili chote changu.
Pendo na uzima wangu.
Mungu wangu nitampenda wala dhambi sitatenda.
Jina lako nasifia,utakalo hutimia kwa utii navumili.
Teso na matata pia,nipe Bwana neema zako, niongeze sifa yako.Amina.

SALA YA MATOLEO.

Ee Yesu kwa mikono ya Bikira Maria,na kwa maungano na sadaka yako kuu.
Ninakutolea sala,matendo,masumbuko na furaha zangu zote za leo.
Ee Yesu ufalme wako utufikie.Amina.

BABA YETU.

Baba yetu uliye mbinguni,jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku.Utusamehe makosa yetu,kama tunavyo wasamehe na sisi waliyo tukosea.
Usitutie katika kishawishi,lakini utuopoe maovuni.Amina.

SALAMU MARIA.

Salamu Maria,umejaa neema Bwana yu nawe,umebarikiwa kuliko wanawake wote,na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa.
Maria mtakatifu Mama wa Mungu,utuombee sisi wakosefu sasa na saa ya kufa kwetu.Amina.

KANUNI YA IMANI.

Nasadiki kwa Mungu,Baba Mwenyezi,muumba mbingu na dunia.
Na kwa Yesu Kristu Mwanaye wa pekee,Bwana wetu aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu,akazaliwa na Bikira Maria,akateswa kwa mamlaka ya ponsyo Pilato,akasulibiwa, akafa,akazikwa,akashukia kuzimu siku ya tatu akafufuka katika wafu, akapaa mbinguni amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi,toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu.
Nasadiki kwa Roho Mtakatifu,kanisa takatifu katoliki ushirika wa Watakatifu,maondoleo ya dhambi,ufufuko wa miili na uzima wa milele.Amina.

AMRI ZA MUNGU.

1.Ndimi Bwana Mungu wako,usiabudu miungu wengine.
2.Usilitaje bure jina la Mungu wako.
3.Shika kitakatifu siku ya Mungu.
4.Waheshimu Baba na Mama upate miaka mingi na heri duniani.
5.Usiue.
6.Usizini.
7.Usiibe.
8.Usiseme uwongo.
9.Usitamani mwanamke asiye mke wako.
10.Usitamani mali ya mtu mwingine.

AMRI ZA KANISA.

1.Hudhuria misa takatifu domonica na sikukuu zilizo amuliwa.
2.Funga siku ya jumatano ya majivu,usile nyama siku ya Ijumaa kuuu.
3.Ungama dhambi zako walau mara moja kwa mwaka.
4.Pokea Ekarist takatifu hasa wakati wa Pasaka
5.Saidia kanisa katoliki kwa zaka.
6.Shika sheria katoliki za ndoa.

SALA YA IMANI.

Mungu wangu,nasadiki maneno yote linayo sadiki na kufundisha kanisa katoliki la Roma kwani ndiwe uliye fumbuliwa hayo,wala hudanganyiki na wala hudanganyi.Amina.

SALA YA MATUMAINI.

Mungu wangu,natumaini kwako nitapewa kwa njia ya Yesu Kristu,neema zako duniani na utukufu mbinguni.Kwani ndiwe uliyeagana hayo nasi nawe mwamini.Amina.

SALA YA MAPENDO.

Mungu wangu,nakupenda zaidi ya chochote, kwani ndiwe mwema ndiwe mwenye kupendeza.
Nampenda na jirani yangu kama nafisi yangu kwa ajiri yako.Amina.

SALA YA KUTUBU.

Mungu wangu,nimetubu sana dhambi zangu kwani ndiwe mwema,ndiwe mwenye kupendeza wachukizwa na dhambi.
Basi sitaki kukosa tena nitafanya kitubio,naomba neema yako nipate kurudi.Amina.

SALA KWA MALAIKA MLINZI.

Malaika mlinzi wangu,unilinde katika hatari zote za Roho na za Mwili.Amina.

MALAIKA WA BWANA.

K.Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria.
W.Naye akapata mimba kwa Roho mtakatifu.

Salamu Maria…..

K.Ndimi mtumishi wa Bwana.
W.Nitendewe ulivyo nena.

Salamu Maria…..

K. Neno la Mungu akatwaa Mwili.
W. Akakaa kwetu.

Salamu Maria….

K. Utuombee Mzazi Mtakatifu wa Mungu.
W. Tujaliwe ahadi za Kristu.

Tuombe.

Tunakuomba Ee Bwana utie neema yako mioyoni mwetu ili sisi tuliyojuwa kwa maelezo ya malaika kwamba, Kristu mwanao amejifanya mtu kwa mateso na msalaba wake.
Tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu.Amina.

ATUKUZWE BABA.

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,kama mwanzo na sasa na siku zote na milele.Amina.

K. Moyo Mtakatifu wa Yesu
W.Utuhurumie.

K. Moyo safi wa Bikira Maria.
W. Utuombee.

K. Mtakatifu Yosefu.
W. Utuombee.

K. Watakatifu somo wa majina yetu.
W. Mtuombee.

K.Watakatifu wote wa Mungu.
W.Mtuombee.

Kwa jina la Baba…..

Sala ya Usiku kabla ya kulala

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

SALA YA KUSHUKURU

Tunakushukuru, ee Mungu, kwa mapaji uliyotujalia leo. Amina.

Baba yetu …

Salamu Maria …

SALA YA IMANI

Mungu wangu, nasadiki maneno yote. Linayosadiki na linayofundisha Kanisa Katoliki la Roma. Kwani ndiwe uliyetufumbulia hayo. Wala hudanganyiki, wala hudanganyi. Amina.

SALA YA MATUMAINI

Mungu wangu, natumaini kwako, nitapewa kwa njia ya Yesu Kristo. Neema zako hapa duniani, na utukufu mbinguni. Kwani ndiwe uliye agana hayo nasi, nawe mwamini. Amina.

SALA YA MAPENDO

Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote. Kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu, kama nafsi yangu, kwa ajili yako. Amina.

KUTUBU DHAMBI

Tuwaze katika moyo wetu makosa ya leo tuliyomkosea Mungu kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu. (Husubiri kidogo ).

Nakuungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno, kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo, na kwa kutotimiza wajibu.
Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana nakuomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.
Mungu Mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele. Amina.

SALA YA KUWAOMBEA WATU

Ee Mungu, nawaombea watu wa nchi hii, wapate kusikia maneno yako na kukupenda wewe Bwana Mungu wetu.

SALA KWA MALAIKA MLINZI

Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote za roho na za mwili. Amina.

MALAIKA WA BWANA

(kipindi kisicho cha Pasaka)
Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria.
Naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Salamu, Maria,…..
Ndimi mtumishi wa Bwana.
Nitendewe ulivyonena.
Salamu, Maria….
Neno la Mungu akatwaa mwili.
Akakaa kwetu.
Salamu, Maria….
Utuombee, Mzazi mtakatifu wa Mungu.
Tujaliwe ahadi za Kristu.
Tuombe:
Tunakuomba, Ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba Mwanao amejifanya Mtu kwa mateso na msalaba wake tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. AMINA.

AU;

MALKIA WA MBINGU (kipindi cha Pasaka)

Malkia wa mbingu, furahi, aleluya.
Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.
Amefufuka alivyosema, Aleluya.
Utuombee kwa Mungu, Aleluya.
Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya.
Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.
Tuombe.
Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao, fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.

ATUKUZWE (mara tatu)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.

KUJIKABIDHI

Enyi Yesu, Maria na Yosefu nawatolea moyo na roho na uzima wangu!
Enyi Yesu, Maria na Yosefu mnijilie saa ya kufa kwangu!
Enyi Yesu, Maria na Yosefu mnijalie nife mikononi mwenu!

(Rehema ya siku 300).

WIMBO:

Kwa heri Yesu mpenzi mwema,
Naenda usiudhike mno.
Nakushukuru, nakupenda,
Kwa hizo nyimbo za mwisho.
Asubuhi nitarudi.
Yesu kwa heri.

Kwa heri Mama mtakatifu,
Sasa napita pumzika.
Asante kwa moyo na nguvu,
Leo umeniombea.
Asubuhi nitarudi.
Mama kwa heri.

Kwa heri Yosefu mnyenyekevu,
Kazi zatimilizika.
Kama mchana, leo usiku,
Nisimamie salama.
Asubuhi nitarudi.
Yosefu kwa heri.

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

KUOMBA ULINZI WA USIKU

Mungu wangu naenda kulala naomba malaika 14, waende nami, wawili juu, wawili chini, wawili upande wa kuume, wawili upande wa kushoto, wawili wanifunike, wawili waniamshe, wawili wanipeleke juu mbinguni. Mimi mtoto mdogo, roho yangu ni ndogo, haina nafasi kwa mtu yoyote ila kwa Yesu pekee. Amina.

Shopping Cart