Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Ugumba wa mwanamke unasababishwa na nini?

Ugumba wa mwanamke ni hali ya mwanamke kushindwa kupata mimba. Kama kwa wanaume kuna mambo mengi yanayoweza kusababisha ugumba wa wanawake.
Ili mwanamke aweze kupata mimba, vitu vingi lazima vitokee. Lazima yai lipevushwe, lazima yai lii ngie kwenye mrija wa kupitisha yai ambapo mimba hutungwa, tena lazima yai lililorutubishwa lifikie kwenye mfuko wa mimba na mwishoni lazima utando ndani ya mfuko wa uzazi uandaliwe. Endapo yoyote kati ya hali hizi hazitafikiwa kwa sababu fulani, mimba haiwezi kutunga. Sababu za kutopevuka yai mara nyingi ni mfadhaiko wa kiakili na kisaikologia na sababu za kuziba mrija wa kupitisha yai mara nyingi ni magonjwa ya zinaa. Wanawake wengine wamepata ugumba kutokana na kujaribu kutoa mimba, matokeo yake wameziharibu kabisa sehemu za ndani za viungo vya uzazi. Bahati mbaya, hali nyingi katika hizi haziwezi kurekebishwa na wanawake wanabaki wagumba wa kudumu.
Kuna mambo mengine yanayosababisha ugumba wa muda. Mambo hayo ni pamoja na ugonjwa, ulevi, matumizi ya dawa za kulevya, lishe duni, mshituko na majonzi. Vingi vya vyanzo hivi vinaweza kutibwa, kwa mfano, kutumia madawa ya kulevya. Mara vikitibiwa, mwanamke ataweza kupata mimba.

Ugumba wa mwanaume unasababishwa na nini?

Ugumba wa mwanaume ni hali ya mwanaume kushindwa kumpa mwanamke mimba. Kuna mambo mengi yanayoweza kusababisha ugumba.

Kati ya wanaume wagumba, wengi wanazaliwa na ugumba na hakuna marekebisho yoyote yanayoweza kufanywa. Katika hali hii , ugumba unasababishwa na kutokamilika kwa via vya uzazi vya mwanaume, mfano kutokuwa na sehemu ya kutengenezea mbegu za kiume au kuwa na shahawa duni. Kwa kuongezeka, kuharibika via vya uzazi kutokana na maradhi, kuziba kwa mirija ya kupitisha mbegu kutokana na magonjwa ya zinaa kama vile kaswende na kisonono. Sababu nyingine za ugumba ni kuwa na uume dhaifu. Hii i ii inaweza kusababishwa na magonjwa ya zinaa, au na mfadhaiko wa kiakili na kisaikologia. Hali nyingi katika hizi haziwezi kurekebishwa, na zinamsababishia mwanaume kuwa mgumba wa kudumu.

Hata hivyo, pia kuna mambo yanayosababisha ugumba wa muda. Mambo hayo ni pamoja na ugonjwa, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, lishe duni, mshituko na majonzi. Mara zikirekebishwa, mwanaume anarudia hali ya kuwa na uwezo wa kumpa mwanamke mimba.

Je, ni matatizo yapi yanayotokana na ujauzito katika umri mkubwa?

Kwa wanawake wenye miaka zaidi ya 35 uwezekano wa kupata matatizo ya kiafya wakati wa ujauzito au wakati wa kujifungua ni mkubwa zaidi kuliko wanawake kati ya miaka 20 na 35.
Matatizo ni mengi zaidi kama mama ameshakuwa na watoto wengi. Baada ya kuzaa mimba tano au zaidi, misuli ya mfuko wa uzazi hulegea. Hivyo hufanya mama kutokwa na damu nyingi, kuwa na uchungu wa muda mrefu na kuchanika kwa mji wa mimba. Matatizo mengine ni mtoto kukaa vibaya tumboni na kuwa na watoto wakubwa. Wanawake wa umri mkubwa ambao wamekuwa na i idadi kubwa ya mimba za karibukaribu (za kufululiza) wanakabiliwa na uwezekano mkubwa wa kufariki wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua.

Matatizo yanayotokana na ujauzito katika umri mdogo

Wataalamu wanashauri kwamba msichana anastahili kuanza kubeba mimba kuanzia umri wa miaka 18 hadi 20. Kabla ya umri huu, mwili wa msichana bado haujakomaa vizuri. Viungo vya uzazi bado ni vidogo na ngozi ni laini. Vilevile mfupa wa nyonga bado mwembamba kiasi cha kumwezesha mtoto kupitia wakati wa kuzaliwa.
Wasichana chini ya miaka 18 wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata matatizo, hasa wakati wa kujifungua. Matatizo hayo ni pamoja na mapigo ya moyo kuwa juu, kuumwa uchungu kwa muda mrefu, kukwama kwa mtoto, kujifungua kwa njia ya operesheni, kujifungua kabla ya wakati na watoto kuzaliwa na uzito mdogo. Mwili huwa na mahitaji makubwa wakati wa ujauzito na kujifungua na mwili wa wasichana wenye umri chini ya miaka 18 huwa haujakomaa vya kutosha kwa kazi ya kubeba mimba.
Mbali ya shida za kiafya, kuna matatizo mengine yatokanayo na kupata mimba mapema. Mara nyingi msichana na mwenzie wanakuwa bado wanasoma shule, msichana hufukuzwa shule na hata hutengwa katika jamii . Vijana mara nyingi hawana mapato ya kumlea na kumtunza mtoto, na mahali pa kuishi huwa hawana. Vilevile mvulana mara nyingi hayuko tayari kuchukua jukumu la kuwa baba. Kwa sababu hizi zote, ni vizuri zaidi mimba zitungwe baada ya msichana kufikia umri wa miaka 18.

Nikishatambua kwamba nina mimba, nifanye nini?

Ukishatambua kwamba una mimba kuna mambo mbalimbali tofauti ya kufanya. Kwanza kabisa mweleze mwenzi wako na mshauriane hatua zipi mchukue. Pia, kwa msichana mdogo lazima uwaeleze wazazi wako. Siyo rahisi kuwaambia wazazi, kwa sababu hawatafurahi kuhusu ujumbe huu. Lakini uhusiano mzuri na wazazi unaweza kuwasaidia sana katika kulea mimba na baadaye mtoto.
Kwa upande wa kiafya ni muhimu sana kuanza kuhudhuria kliniki au hospitali mapema, yaani kabla ya mimba kufikisha miezi mitatu. Hii huwawezesha wataalamu kukupima na kukupa ufafanuzi kuhusu afya yako na maendeleo ya mimba. Vilevile wanaweza kugundua matatizo kama yatakuwepo na kukutibu mapema. Kwa usalama wako na usalama wa mtoto hakikisha kuyafuata maelekezo ya wataalamu kila mara.
Wasichana au wanawake wengine wanafikiria kutoa mimba mara tu wanapokuta wamepata mimba bila ya kupangilia. Kutoa mimba ni jambo la hatari sana na linaweza kuleta madhara kiafya kwa mwanamke, na hasa utoaji mimba unaofanywa na mtu ambaye hakusomea na pia katika mazingira yasio safi.

Shopping Cart