Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Nini maana ya neno Albino?

Neno Albino linamaanisha
mtu mweupe, linatokana na
neno la lugha ya Kilatini –
albus-linamaanisha “eupe”.
Kuanzia karne ya 17 neno
Albino limekuwa likitumika
katika kueleza hali ya kundi
la viumbe hai (watu, wanyama
na hata mimea) ambao wana
upungufu au ukosefu wa rangi
katika ngozi, macho na nywele.
Kwa binadamu ni bora kutumia
maneno “Watu wanaoishi na
ualbino
kwani itamaanisha kuwa ni watu kama wengine ila wanaishi na
hali tofauti ya “ualbino”. Katika kitabu hiki maneno haya mawili
yatatumika.
Lugha inajenga dhana na kuunda hali ya ukweli / uhalisi. Kwa
sababu hiyo ni lazima tuache kutumia maneno kama “zeruzeru”.
Neno hili linamaanisha sifuri mara mbili au mtu asiye na
thamani. Utumiaji wa neno hili ni dharau ya utu na kulaumu
watu wanaoishi na ualbino kama kosa lao.

Ninawezaje kumsaidia mtu kuacha kuvuta sigara na kunywa pombe?

Jaribu kutafuta sababu zinazowafanya rafiki, ndugu na jamaa
zako kuwa na tabia ya kuvuta sigara na kunywa sana pombe.
Jaribu kuwa naye karibu na mshughulishe asipate muda wa
kuvuta na kunywa pombe. Kuwa naye kwa muda mrefu, fanya
naye kazi na mtambulishe kwa rafiki zako ambao hawatumii
sigara wala pombe. Mweleze umuhimu wa yeye kukaa mbali na
vishawishi. Mweleze kwa nini ni vigumu sana kushinda vishawishi
ukiwa katika hali ya ulevi, na unapotoa ushauri huo yakupasa
usiwe mlevi na mvutaji.
Inaweza ikatokea, jamaa unayemshauri kuhusu madhara ya
kunywa pombe na kuvuta sigara, akachukia au ukawa ndio mwisho
wa urafiki wenu. Usijilaumu, ujitahidi kumsaidia kadiri uwezavyo.
Wakati mwingine ni vyema ukavunja urafiki huo kwa usalama
wako na wa rafiki yako. Endapo kama itatokea akaanza kutambua
madhara na matokeo ya uvutaji sigara na unywaji pombe na
hatimaye kuchukua uamuzi wa kuelezea matatizo yake, itampasa
amtafute mtaalamu ili aweze kupata ushauri nasaha.

Kama watu wanataka kuacha kuvuta sigara au kunywa pombe wafanyeje?

Kwanza kabisa, watu ni kweli wawe wamedhamiria kuacha.
Hii inataka uamuzi wa wazi na nia imara kwa sababu si rahisi
kuacha.
Pili, mtu anatakiwa kufikiria ni katika mazingira gani huwa
anajisikia kuvuta sigara au kunywa pombe. Hii kwa kawaida ni
pamoja na kundi maalumu la marafiki, katika sherehe, baada ya
kazi ngumu, baada au wakati wa kula. Kwa hiyo, kama wanataka
kuacha kuvuta sigara au kunywa pombe, wanatakiwa kubadili
mtindo wa maisha na kuepuka vishawishi.
Hatua ya kwanza katika kuacha kuvuta sigara au kunywa
pombe, inaweza ikawa ni kujiwekea malengo; kwa mfano, kuacha
kuvuta sigara kwa wiki nzima. Jipongeze kuwa umetimiza lengo
lako. Kama umeshindwa anza tena. Ni watu wachache ambao
wameweza kuacha kabisa katika jaribio la kwanza. Watu
wengine wanapata ugumu kuacha kabisa pombe na sigara.

Nimwambie nini mtu anayejaribu kunishawishi nijihusishe na makundi ya watu wanaokunywa pombe na wavutaji sigara?

Kama umeamua kutovuta sigara wala kunywa pombe ni uamuzi
mzuri sana na wa kiafya. Ni haki yako binafsi kuchukua uamuzi
huu, kama vile watu wengine pia wanavyoruhusiwa kufanya
maamuzi kuhusu maisha yao wenyewe.

Mara nyingine ni vigumu sana, lakini kama umeamua hutaki
kujiunga na kundi la watu wavutao sigara au kunywa pombe ni
muhimu kusema hivyo. Jaribu kuwa wazi na kusema HAPANA.
Jaribu kueleza kwamba unataka kuishi maisha yenye afya bila
kutumia pombe na sigara na uwaeleze rafiki zako ni kwa nini.
Waambie kuwa unajua unachokifanya na kwamba umeridhika
kuwa uvutaji sigara na unywaji pombe unahatarisha afya yako,
unagharimu fedha nyingi na kukuzuia kufikia malengo yako.
Kama umeridhika na kuwathibitishia watu hao, hawatakusumbua
tena. Na kama unatafuta rafiki usisahau: Rafiki ni mtu anayejali,
kulinda na kuthamini maisha ya mwenzake! Kwa hivyo, ni kwa
vipi mtu ambaye anayekushawishi ufanye kitu cha kudhuru
afya yako kwa kusudi na haheshimu maamuzi yako awe rafiki
wa kweli?

Kwa nini pombe na sigara bado zinatangazwa wakati zina madhara?

Serikali inatakiwa iamue kuwepo kwa matangazo ya biashara
ya pombe na sigara au la? Serikali ina wakati mgumu katika
kuamua kati ya kulinda afya za watu na shinikizo litokalo
kwa wakulima pamoja na makampuni yanayotengeneza pombe
na sigara. Wenye viwanda na wauzaji wanataka bidhaa hizi
zitangazwe kibiashara kwa sababu wanapata pato kutokana na
kuzalishwa na kuuzwa kwa bidhaa hizi. Serikali yenyewe pia
inapata faida kutokana na kutangazwa kwa tumbaku na pombe
kwa sababu uuzaji wake unaipatia serikali ushuru kupitia kodi.
Nchini Tanzania serikali imeamua kuwa matangazo ya biashara
ya sigara yawe na onyo lisemalo,“Uvutaji wa sigara ni hatari kwa
afya yako”. Hii inawajulisha wavutaji wa sigara kuhusu hatari
za uvutaji wa sigara na kuacha kila mtu ajiamulie mwenyewe.

Shopping Cart