Mafundisho ya Katekisimu

Je, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha Ndoa kama sakramenti ya agano la upendo na uaminifu?

Je, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha Ndoa kama sakramenti ya agano la upendo na uaminifu?

Ndio, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha Ndoa kama sakramenti ya agano la upendo na uaminifu. Kwa mujibu wa kanuni za Kanisa Katoliki, ndoa ni sakramenti ambayo inawezeshwa na Mungu kwa ajili ya wawili wanaokubali kwenda pamoja kwa maisha yao yote. Ndoa ina maana kubwa sana kwetu sote, kwani ni wakati ambapo tunaahidi kuwa na mtu mwingine maisha yetu yote.

Kama vile Kristo alivyohusisha sakramenti yake ya mwili na damu yake na Wakristo wake, vivyo hivyo ndoa inahusisha sakramenti ya upendo na uaminifu kati ya wawili wanaotaka kuwa pamoja maisha yao yote. Ndoa ina lengo la kuleta furaha, amani, na upendo kwa wawili hao, na kuunda familia ambayo inaishi kwa upendo na amani.

Ndoa ina thamani kubwa sana kwa Mungu, na ndio maana inahusishwa na agano la upendo na uaminifu. Katika agano hili, wawili wanakubali kuwa pamoja maisha yao yote, na kuahidi kuwa waaminifu kwa kila mmoja, kushirikiana katika matatizo na furaha, na kujenga familia ambayo inaishi kwa upendo na amani.

Katika Biblia, tunaona jinsi ndoa inavyopewa umuhimu mkubwa. Kwa mfano, katika Mwanzo 2:24, tunasoma "Kwa hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja." Hii inaonyesha jinsi Mungu alivyokusudia ndoa iwe kitu cha maana sana katika maisha yetu.

Kwa mujibu wa Catechism ya Kanisa Katoliki, ndoa ina maana kubwa sana kwetu sote. Inasema kuwa ndoa ni "umoja wa maisha ya wanaume na wanawake, ambao unawekwa na Mungu mwenyewe, na ambao unapatikana kwa njia ya kujitolea kwa kila mmoja na kwa ajili ya ajili ya watoto." (Catechism ya Kanisa Katoliki, 1601).

Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha Ndoa kama sakramenti ya agano la upendo na uaminifu kwa sababu inajua jinsi muhimu ndoa ni katika maisha yetu. Ndoa inatuletea furaha, amani, na upendo, na inatufanya tuishi kwa amani na upendo na wale tunaowapenda. Tunapofuata kanuni za Kanisa Katoliki, tunaweza kuishi kwa amani na upendo na wale tunaowapenda, na kusaidia kujenga familia ambayo inaishi kwa upendo na amani.

Amri ya Sita ya Mungu: Kutunza usafi wa moyo na kuwa waaminifu

Katika Amri ya Sita na Tisa Mungu ametuamuru nini?

Mungu ametuamuru kutunza usafi wa moyo na kuwa waaminifu katika ndoa.


Usafi wa Moyo ndio nini?

Usafi wa Moyo ni fadhila ya kiutu, zawadi ya Mungu, neema na tunda la Roho Mtakatifu.


Kwa sababu gani yatupasa kuwa na usafi wa moyo?

Yatupasa kuwa na usafi wa moyo kwa sababu:

1. Mungu awapenda hasa wenye usafi wa moyo. (Mt 5:8)
2. Sisi Wakristo ni Hekalu la Roho Mtakatifu. (1Kor 3:16-17)


Tumekatazwa nini ili tulinde usafi wa moyo?

Tumekatazwa haya;

1. Kutazama mwili kwa Tamaa mbaya na kuvaa vibaya
2. Kusema na kuimba, ngoma zisizo na adabu.
3. Kusikiliza machafu, kucheza michezo mixhafu.
4. Kutenda machafu peke yetu au pamoja na wenzetu. (Efe 5:3)
5. Kusoma vitabu na magazeti machafu na kuangalia picha chafu.


Katika Amri ya Tisa ya Mungu tumekatazwa nini?

Tumekatazwa haya;

1. Kutomtamani mke au mume wa mwingine
2. Kutamani mambo ya zinaa


Dhambi za uchafu huleta hasara gani?

Huleta hasara hizi;

1. Kuharibu usafi wa Moyo na Hekalu la Mungu
2. Huleta Magonjwa duniani na hasara ya baadae. mf UKIMWI. (Efe 5:5)
3. Huvunja amani ya familia
4. Kujijengea mazoea ya uchafu


Tulinde usafi wa Moyo namna gani?

1. Kusali mara dhidi ya kishawishi.
2. Kupokea sakramenti hasa Kitubio na Ekaristi mara nyingi
3. Kuepuka uvivu, ulevi na madawa ya kulevya.
4. Kukimbia nafasi dha dhambi.
5. Kutunza haya au soni
6. Kuwa na mazoea ya kufunga na kujinyima.

Maswali na Majibu kuhusu Ufufuko wa wafu

Ufufuko wa wafu maana yake nini?

Ufufuko wa wafu maana yake mwisho wa dunia watu wote watafufuka na miili yao na kwenda nayo katika furaha ya milele au moto wa milele. (Ayu 19:25-26, Mt 22:30-32, Yh 28-29)


Mbinguni ni mahali pa namna gani?

Mbinguni ni makao mema ya heri na furaha (2Kor 5:1, Ufu, 2:17).
Waendao mbinguni ni wale wanaokufa katika hali ya neema ya utakaso na urafiki na Mungu na waliotakaswa kikamilifu


Motoni ni nini?

Motoni ni makao mabaya kwa Shetani walaaniwa wakaapo mbali na Mungu wakiteswa milele. (Mt 25:41, Mik 9:42-43, 1Yoh 14:15)


Uzima wa milele ni nini?

Uzima wa milele ni maisha ya kukaa mbinguni na Mungu yasiyokua na mwisho.


Toharani ni mahali gani?

Toharani ni mahali pa mateso zinakosafishwa roho ambazo hazikutimiza kitubio vizuri baada ya kuungama dhambi. (1Kor 3:15, 1Pet 1:7).


Je, hatuwezi kupunguza mateso ya roho za marehemu waliokwenda toharani?

Ndiyo: twaweza kupunguza hata kuyamaliza kwa kuwasalia na kuwapatia rehema na hasa kwa kuadhimisha Misa kwa ajili yao. (2Mik 12:38-46)


Mambo makuu manne ya mwisho ni yapi?

Mambo hayo ni;
1. Kifo
2. Hukumu
3. Jehanamu (Motoni)
4. Paradiso. (Toharani/Mbinguni)


Je, ufufuko wa Yesu ni muhimu kwetu pia?

Ndiyo, ufufuko wa Yesu ni muhimu kwetu pia, kwa sababu kwa njia yake tu tunatiwa uzima: sasa rohoni kwa kuondolewa dhambi, na siku ya mwisho mwilini pia kwa kufufuliwa.
Mwenyewe alisema, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele” (Yoh 11:25- 26).
“Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu” (1Kor 15:20-21).
“Alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuka ili tupate kuhesabiwa haki” (Rom 4:25).


Je, ni muhimu tujiandae kufa?

Ndiyo, ni muhimu tujiandae kufa wakati wowote na namna yoyote kwa kuishi kitakatifu sasa na kwa kujiombea neema tutakazohitaji saa ya kufa kwetu, tukijua tumewekewa “kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu” (Eb 9:27).
“Katika mambo yako yote uukumbuke mwisho wako, hivyo hutakosa kamwe hata hatima” (YbS 7:36).
“Hamjui yatakayokuwako kesho! Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka” (Yak 4:14).
“Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni” (Math 26:41).


Je, ina thamani machoni pa Bwana mauti ya mtu aliyemcha?

Ndiyo, “ina thamani machoni pa Bwana mauti ya wacha Mungu wake” (Zab 116:15).
Hasa utiifu wa Yesu msalabani umegeuza laana ya kifo iwe baraka kwa waamini wake.
“Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao” (Ufu 14:13).


Je, sisi wanyonge tunaweza kushiriki uzima wa milele wa Mungu?

Ndiyo, sisi wanyonge tunaweza kushiriki uzima wa milele wa Mungu: hapa duniani katika mwanga hafifu wa imani, na kisha kufa katika uangavu wa utukufu usiofifia kamwe. Kwa kuwa lengo la Baba ni kwamba tuungane na Yesu Mwanae kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ili tuwe na utukufu wake.
“Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yoh 17:3).
“Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa” (2Pet 1:3-4).
Sisi tuliobatizwa tunaitwa “wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo!” (1Yoh. 3:1).
Kwa sababu tumesadiki kwamba “Mungu ni upendo” (1Yoh 4:8) na kwamba “hakuna lisilowezekana kwa Bwana” (Lk 1:37).
“Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’ Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu” (Gal 4:6-7).


Aliyezungumzia moto wa milele ni nani?

Aliyezungumzia moto wa milele ni hasa Yesu: akitufunulia ukuu wa upendo wa Mungu, aliye heri yetu pekee, alituangalisha juu ya hatari ya kutengana naye milele kwa dhambi. Mwenyewe atatoa hukumu hiyo:
“Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake” (Math 25:41).
“Humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki” (Mk 9:48).
“Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku” (Ufu 14:11).


Toharani maana yake nini?

Toharani maana yake kuna hali ya muda ambayo huruma ya Mungu inawatakasa marehemu waliofariki dunia katika urafiki naye lakini bila ya usafi kamili unaotakiwa kwa kuingia mbinguni. Sisi tunaweza kuharakisha utakaso wao kwa kumtolea Mungu sala na sadaka, hasa ekaristi. Yuda Mmakabayo “alichanga fedha kwa kila mtu jumla drakma elfu mbili, akazipeleka Yerusalemu kutoa sadaka ya dhambi.
Kwa kufanya hivi alitenda vema na kwa haki, kwa kuwa aliukumbuka ufufuo wa wafu. Maana kama asingalitumaini ya kuwa wale waliokufa watafufuka, ingalikuwa kazi bure isiyo na maana kuwaombea wafu. Lakini kwa kuwa aliufikiri utukufu wa thawabu waliowekewa wale wafao katika utauwa, wazo lake lilikuwa takatifu na la kicho. Ndiyo sababu alifanya upatanisho kwa wafu ili wafunguliwe dhambi zao” (2Mak 12:43-46). Imani hiyohiyo iliongoza Wakristo wa kwanza kuwafanyia marehemu ibada ambayo haieleweki vizuri, lakini hailaumiwi na Mtume Paulo: “Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?” (1Kor 15:29).


Je, mwili utakaofufuliwa ni huuhuu tulionao sasa?

Ndiyo, mwili utakaofufuliwa ni huuhuu tulionao sasa, lakini katika hali tofauti: > “hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika” (1Kor 15:42).
Siku ya ufufuo “ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi” (Lk 21:27).
“Saa yaja ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuko wa uzima, na waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu” (Yoh 5:28-29).
“Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele” (Math 25:46).


Siku ya ufufuo Kristo mfalme atatuhukumu vipi?

Siku ya ufufuo Kristo mfalme atatuhukumu kwa kudhihirisha misimamo ya watu wote ambao, kwa kupokea au kukataa upendo wa Mungu moyoni mwao, wametenda mema au la.
“Imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyopenda, kwamba ni mema au mabaya” (2Kor 5:10).
“Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu” (1Kor 4:5).
“Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake. Na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, ‘Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia… Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi’” (Math 25:31-36,40).
“Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema” (Math 5:7).


Baada ya hukumu ya mwisho itakuwaje?

Baada ya hukumu ya mwisho, waadilifu watatukuzwa mwili na roho pamoja na Yesu, na ulimwengu pia utageuzwa.
“Kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake” (2Pet 3:13).
“Na Roho na Bibi arusi wasema, ‘Njoo!’ naye asikiaye na aseme, ‘Njoo!’… Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, ‘Naam, naja upesi’. Amina. Na uje, Bwana Yesu! Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina” (Ufu 22:17,20-21).

Kuhusu Ubatizo, Haya ndiyo mambo ya Msingi unayotakiwa kufahamu

Kwa nini ubatizo unafanyika kwa maji?

Ubatizo unafanyika kwa maji kwa kuwa ndiyo ishara ya usafi na ya uhai unaotupatia kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
“Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu” (Ez 36:26-27).
“Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwanakondoo” (Ufu 22:1).


Ubatizo unatolewa pia kwa maji machache tangu lini?

Ubatizo unatolewa pia kwa maji machache tangu mwanzo. Kutokana na umuhimu wa sakramenti hiyo Yesu ametuagiza twende kubatiza watu duniani kote.
Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaonyesha waamini walivyotekeleza agizo hilo katika mazingira mbalimbali, sio tu yalipopatikana maji mengi. Hivyo Paulo alipokuwa ndani ya nyumba “akasimama akabatizwa” (Mdo 9:18).
Kumbe Yohane Mbatizaji hakusogea mbali na mto Yordani, akisubiri watu wamuendee kutoka maeneo yote ya nchi ile kame.
“Alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele” (Yoh 3:23).


Je, ubatizo uliotolewa na Yohane Mbatizaji ulikuwa sakramenti?

Hapana, ubatizo uliotolewa na Yohan Mbatizaji haukuwa sakramenti, kwa sababu yeye alikuwa mtangulizi tu wa Yesu, mwanzilishi wa sakramenti zote.
“Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” (Math 3:11).
Paulo aliuliza watu, “‘Mlibatizwa kwa ubatizo gani?’ Wakasema, ‘Kwa ubatizo wa Yohane’. Paulo akasema, ‘Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu’. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu” (Mdo 19:3-5).


Tofauti kubwa kati ya ubatizo wa Yohane na ule wa Yesu ni zipi?

Tofauti kubwa kati ya ubatizo wa Yohane na ule wa Yesu ni kwamba sakramenti inategemea imani kwa Kristo na kutushirikisha kifo na ufufuko wake.
“Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo” (Gal 3:27).
Ndivyo inavyoondolea dhambi zote na kuingiza katika uzima wa Utatu Mtakatifu. Kwa sababu hiyo Yesu aliagiza tubatize “kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” (Math 28:19).
Maneno hayo ndiyo muhimu zaidi katika sakramenti hiyo. Maji peke yake, hasa yakiwa mengi, yanaweza kuosha mwili, lakini si roho. Kumbe ubatizo unaotuokoa
“siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu” (1Pet 3:21).


Je, watoto wachanga wanaweza kubatizwa?

Ndiyo, watoto wachanga wanaweza kubatizwa kwa sababu hawakatai neema ya Mungu. Wanafunzi wa Yesu walipotaka kuwazuia wasiletwe kwake “alichukizwa sana, akawaambia, ‘Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni: Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa” (Mk 10:14-15).
Yeremia aliambiwa,
“Kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yer 1:5).
Yohane Mbatizaji alitabiriwa “atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye” (Lk 1:15).
Mitume walipokea katika Kanisa familia nzima, si wazazi tu.
Walibatizwa “yeye na nyumba yake”, “yeye na watu wake wote” (Mdo 16:15,33);
“watu wa nyumbani mwa Stefana” (1Kor 1:16).
Kwa hiyo tunaona kuwa tangu wakati wa Mitume sio watu wazima tuu waliokua wakibatizwa bali na watoto pia.


Mbona watoto wachanga hawawezi kuelewa kinachofanyika wakati wa ubatizo halafu wanabatizwa?

Ingawa watoto wachanga hawawezi kuelewa kinachofanyika, Mungu anaweza kuwamiminia rohoni mwanga wa imani.
“Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao umeiweka misingi ya nguvu” (Zab 8:2).
“Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake… kwa shangwe” (Lk 1:41,44).
“Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako” (Math 11:25-26).


Je, watu wazima wanaweza kuelewa sakramenti kwa dhati?

Hapana, watu wazima hawawezi kuelewa sakramenti kwa dhati, kwa kuwa zote ni mafumbo yanayotuzidi. Basi, kama Petro alipooshwa miguu, tumuachie Bwana atufanyie kazi anavyojua yeye.
“Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye” (Yoh 13:7).
Kisha kuoshwa tuzidi kuchimba mafumbo hayo kwa mwanga wa Neno na wa Roho Mtakatifu.
“Je, mmeelewa na hayo niliyowatendea?… Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yoh 13:12,15).


Je, imani ya watu wazima inaweza kufaidisha watoto?

Ndiyo, imani ya watu wazima inaweza kufaidisha watoto kama wengine pia.
Walimletea Yesu “mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne… Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, ‘Mwanangu, umesamehewa dhambi zako” (Mk 2:5).
Yesu aliiona imani yao akamponya. Imani ya watu wengine ndio ilivyopelekea kuponywa kwa huyu mtu. Vivyo hivyo Imani ya Mzazi inaweza kumsaidia mtoto.
Kwa ubatizo watoto wanaunganishwa naye na kuanza kuponywa madonda ya dhambi ya asili.
“Tazama, mimi naliumbwa kati hali ya uovu, mama yangu alinichukua mimba hatiani” (Zab 51:5).
“Ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo” (Rom 5:19).


Ubatizo wa watoto wachanga unafanyika tangu lini?

Ubatizo wa watoto wachanga unafanyika tangu mwanzo, usipingwe na yeyote kwa miaka elfu na zaidi. Ni kwamba Wayahudi walipokea watoto katika dini yao kwa kuwatahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa.
“Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu” (Lk 2:21).
Watu wa mataifa walipoongokea dini hiyo, walioshwa na kutahiriwa pamoja na watoto wao. Mitume pia walipokea katika Kanisa familia nzima, si wazazi tu. Walibatizwa “yeye na nyumba yake”, “yeye na watu wake wote” (Mdo 16:15,33); “watu wa nyumbani mwa Stefana” (1Kor 1:16).
Kwa hiyo tunaona kuwa tangu wakati wa Mitume sio watu wazima tuu waliokua wakibatizwa bali na watoto pia.
Kwa Kanisa Katoliki, ubatizo sio ukamilifu wa kuwa Mkristo. Ubatizo ni Sakramenti ya kwanza ambayo inakamilishwa na Sakramenti ya Kipaimara ambayo humfanya Mkristo kuwa mkamilifu kwa kukiri na kuahidi mwenyewe kuwa Mfuasi wa Yesu Kristu kwa kumkataa Shetani na Mambo yake yote. Kwa maana hiyo, watoto wanapobatizwa wazazi wanamtoa au wanamwalika mtoto katika Imani ya Kikristu wakiahidi kumtumza na kumwelekeza katika njia ya Imani kwa Yesu Kristu mpaka atakapokua mkubwa na kuwa na ufahamu na Elimu ya kutosha kuhusu Imani yake ndipo na yeye atakiri na kuahidi mwenyewe wakati wa Sakramenti ya Kipaimara.


Je, ubatizo tuu unatosha?

Hapana, ubatizo hautoshi, bali unahitaji kukamilishwa na kipaimara na ekaristi, kama vile baada ya kuzaliwa tunahitaji kukomaa na kudumisha uhai wetu kwa chakula.
Sakramenti hizo tatu kwa pamoja ni msingi wa maisha ya Wakristo wote, kumbe nyingine zinahitajika tu katika hali na nafasi maalumu. Mitume waliwaendea Wasamaria
“wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu” (Mdo 8:15-16).
“Amin, amin, nawaambieni: Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndaniyenu” (Yoh 6:53).


Sakramenti inayohusiana zaidi na ubatizo ni ipi?

Sakramenti inayohusiana zaidi na ubatizo ni kipaimara, kinachoendeleza kazi yake.
“Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao” (Mdo 19:5-6).
Sakramenti hizo ni kama pande mbili za pesa moja. Zinahusiana kama Pasaka na Pentekoste, ambayo ni utimilifu wake, kwa kuwa siku alipofufuka Yesu aliwapulizia Mitume Roho Mtakatifu, ambaye siku hamsini baadaye akawajia kama
“upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote” (Mdo 2:2).


Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ipi?

Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ekaristi, iliyo kuu kuliko sakramenti zote kwa sababu ndiyo Yesu mzima, Mungu-mtu, katika maumbo ya mkate na divai.
Sisi ambao tulishiriki kifumbo kifo na ufufuko wake tukapokea kwake paji la Roho Mtakatifu, tunaalikwa kukaribia mara kwa mara meza anapotulisha na kutunywesha Mwili na Damu yake ili tushiriki uhai wake kwa dhati zaidi na zaidi.
“Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yoh 6:56-57).
Ubatizo na kipaimara havirudiwi, vinadumu ndani mwetu kama mifupa ambayo ekaristi ya mara kwa mara inazidi kuitia mwili na damu.


Sakramenti ya ubatizo ni nini?

Sakramenti ya Ubatizo ni Sakramenti yenye kuondoa dhambi ya asili pamoja na dhambi nyingine zote tulizotenda, kufufua roho zetu kwa kututia uzima wa Mungu, Kutuandika Wakristu Watoto wateule wa Mungu na wa Kanisa.


Ubatizo ni nini?

Ubatizo ni Sakramenti inayotuwezesha kuzaliwa mara ya pili kwa Maji na Roho Mtakatifu, ni mlango (Kiingilio) kwa Sakramenti nyingine zote na ni ufunguo wa uzima wa milele. (Yoh 3:3, Mt28:19)


Sakramenti ya Ubatizo yatuletea nini?

Sakramenti ya Ubatizo yatuletea;
1. Maondoleo ya dhambi ya asili
2. Maondoleo ya dhambi zote za binafsi na adhabu zake
3. Neema ya Utakaso kwa mara ya kwanza
4. Yatutia alama isiyofutika (1Kor 6:11, 12:13)


Kuna Ubatizo wa namna ngapi?

Kuna Ubatizo wa namna tatu;
1. Ubatizo wa maji – Ubatizo wa kawaida
2. Ubatizo wa tamaa – Mfano mtu akifa akiwa na nia ya kubatizwa au akitamani kubatizwa
3. Ubatizo wa Damu – Mtu akiifia Imani japo hajabatizwa


Nani aweza kubatiza?

Mwenye mamlaka ya kubatiza kwa kawaida ni yule mwenye dataja takatifu katika Kanisa, lakini katika hatari ya kufa kila mtu anaweza kubatiza.


Kwa nini Kanisa linabatiza watoto wadogo?

Kwa sababu wanazaliwa na dhambi ya asili hivyo wanahitaji kuwekwa huru kutoka mamlaka ya yule mwovu na kuingizwa katika ufalme wa uhuru wa wana wa Mungu


Je, Ubatizo ni lazima kwa wokovu?

Ndiyo, nilazima kwa wokovu kwa wale ambao wametangaziwa injili na wanasifa ya kuomba Sakramenti hiyo


Anayebatizwa yampasa nini?

Yampasa kuungama imani yake ama mwenyewe akiwa mtu mzima ama kupitia wazazi kama akiwa mtoto mdogo


Alama wazi ya Sakramenti ya Ubatizo ni nini?

Alama wazi ya Sakramenti ya Ubatizo ni kumwagia maji katika panda la uso na kutamka maneno “Fulani (jina lake linatajwa) nakubatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” (Mt 28:19)


Msimamizi wa ubatizo ana wajibu gani?

Msimamizi wa ubatizo ana wajibu hizi;
1. Kutoa mfano mzuri wa maisha ya Kikristo
2. Kumuongoza mbatizwa katika maisha ya Ukristo
3. Kumuombea mbatizwa
4. Kushirikiana na wazazi katika malezi
Shopping Cart