Baini Siri za Kuwa na Afya Bora na Utimamu

Jinsi ya kupika Pilau Ya Nyama Ya Ng’ombe Na Nyanya

Viambaupishi

Mchele (Basmati) 3 vikombe

Nyama ya ngo’mbe 1 kg

Pilipili boga 1 kubwa

Nyanya 2 kubwa

Vitunguu maji 2 vikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa 1 kijiko cha supu

Tangawizi 1 kijiko cha chai

Ndimu 1

Mafuta ya kupikia ½ kikombe

Mdalasini ½ kijiko cha chai

Binzari nyembamba 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ½ Kijiko cha chai

Hiliki ½ Kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

Loweka mchele wako katika chombo

Chukuwa nyama na ioshe vizuri na itie thomu, tangawizi, ndimu, pilipili manga na chumvi kiasi

Iweke jikoni hadi ikauke maji na kuwa imewiva huku ukiikaanga kaanga kwa hayo hayo mafuta yake hadi kuwa rangi ya hudhurungi

katakata Vitunguu na nyanya weka pembeni

Chukua pilipili boga, thomu, tangawizi na visage katika mashine ya kusagia

Weka sufuria pembeni na utie mafuta, subiri yapate moto

Kisha tia vitunguu na vikaange hadi kuwa hudhurungi na tia nyanya

Kisha mimina mchanganyiko wako ulio usaga wa pilipili boga, thomu na tangawizi

Koroga kwa dakika kadhaa Kisha mininia nyama uliyokuwa tayari, maji kiasi na chumvi wastani na subiri maji hayo yachemke

Weka mchele humo na koroga kiasi na onja chumvi kama ipo sawa au kama ndogo unaweza kuongeza

Funika na punguza moto na uache uive taratibu

Baada ya kukauka maji kabisa basi ugeuze na subiri tena kwa dakika kama mbili na tayari kuliwa.

Jinsi ya kuongeza kiasi cha utokaji wa maziwa kwa kina mama wanaonyonyesha na kwa afya ya mtoto

Maziwa ni chakula kikuu cha mtoto punde anapozaliwa. Mama anahitaji kuwa na Maziwa ya kutosha ili mtoto aweze kuwa na afya. Zipo sababu mbalimbali zinazopelekea wakina mama wengi kushindwa kuzalisha maziwa mengi kwa ajili ya kuwanyonyesha watoto zao. Hata hivyo kama wewe ni mama na una tatizo hilo basi unatakiwa kufanya yafuatayio ili utengeneze maziwa kwa wingi;

1. Nyonyesha mara kwa mara.

Nyonyesha angalau mara nane kwa siku. Kadri unavyonyonyesha, ndivyo utatengeneza maziwa zaidi.

2.Tumia vinywaji vya kutosha na kula zaidi.

Epuka kukosa mlo wowote wa siku.

3. Pumzika mara kwa mara.

Iwapo baba na wanafamilia wengine watasaidia na kazi zingine za nyumbani, mama atamhudumia mtoto vizuri zaidi.

4. Hakikisha maziwa yametoka yote wakati wa kunyonyesha au unapokamua.

Usiache maziwa yako kujaa kwa muda mrefu. Hata kama uko mbali na mtoto hakikisha unakamua maziwa.

5. Hakikisha mtoto amenyonya maziwa yote mara mbili kila unaponyonyesha
6. Kwa kina mama ambao hawana maziwa ya kutosha wanaweza kuongea na daktari akawaandikia dawa za kusaidia kuzalisha maziwa.

Mambo ya kuzingatia kuhusu ugonjwa wa Kaswende

Kaswende husababishwa na bakteria aitwaye Treponema pallidum , ambaye pia huitwa spirochetes kutokana na umbo lake la mzunguko. Viumbe hawa hujipenyeza kwenye ngozi laini inayotanda midomo au sehemu nyeti. Yafuatayo ni mambo Muhimu ambayo unapaswa kuyafahamu kuhusu Ugonjwa wa Kaswende.

Jinsi ugonjwa wa Kaswende unavyoonea

Ugonjwa huu huenezwa kwa kugusa moja kwa moja mchubuko wa kaswende (syphilitic sore) uliopo kwenye ngozi. Kaswende haiambukizi kwa kuchangia vyoo, vitasa vya milango, mabwawa ya kuogelea, kuchangia nguo au vyombo vya chakula.

Kwa njia ya Kujamiiana

Kaswende ni ugonjwa unaoambukiza haraka sana, mara nyingi huambikizwa kupitia ngono. Kwa sababu ugonjwa huu huenezwa kwa kugusa moja kwa moja mchubuko wa kaswende (syphilitic sore) uliopo kwenye ngozi, njia kuu ya kuenea ni kupitia ngono ya kawaida, ya kutumia midomo na ile ya kinyume na maumbile.

Kwa njia ya kugusana Miili

Mara chache ugonjwa huu huweza kuambukiza kwa kubusiana au kugusana miili. Pamoja na kuwa ugonjwa huambukiza kupitia michubuko, mara nyingi michubuko hatarishi haitambulikani. Mtu aliyeambukizwa huwa hajielewi na hivyo kumwambukiza mpenzi wake.

Kwa mtoto kipindi cha ujauzito

Mwanamke mwenye mimba na ugonjwa huu anaweza kumwambukiza mtoto aliye tumboni kupitia placenta au wakati wa kuzaliwa.

Aina hii ya kaswende huitwa congenital syphilis, na inaweza kusababisha kujifungua mtoto mfu au mtoto akafa muda mfupi baada ya kuzaliwa. Watoto wengi hawaonyeshi dalili wanapozaliwa. Baadaye watoto huota vijipele, hupata matatizo ya meno, na kubonyea kwa mfupa wa pua – hali inayoitwa saddle nose, kuwa viziwi, kuwa na watoto wa jicho na kifafa.

Hatua za Kaswende

Ugonjwa wa kaswende hugawanywa katika hatua na kila hatua ikiwa na dalili tofauti, lakini wakati mwingine hakuna dalili zitakazojitokeza kwa miaka mingi.

Uambukizaji unatokea kwenye hatua ya kwanza, ya pili na mara chache mwanzoni mwa hatua ya latent phase.

Hatua Ya kwanza Ya Kaswende – Primary Syphilis

Kaswende huanza kama mchubuko mmoja (au zaidi ya mmoja) mgumu usio na maumivu unaojulikana kama chancre kwenye sehemu za siri, kwenye mdomo, au kwenye ngoz,i siku 10-90 (wastani wa miezi 3) baada ya maambukizi.

Mchubuko huu unaweza kubaki hapo bila kuleta usumbufu kwa kipindi kirefu na hata maiaka mingi. Mchubuko huu wa mviringo hutokea kwenye eneo la maambuikizi. Hata bila ya tiba yo yote, mchubuko huu unaweza ukapona wenyewe bila kuacha kovu katika wiki sita.

Hatua Ya Pili Ya Kaswende – Secondary Syphilis

Hatua ya pili inaweza ikadumu kwa mwezi mmoja hadi miezi sita ikianza kama wiki sita hadi miezi sita baada ya maambukizi.
Dalili
Katika hatua ya pili, vijipele huota mara nyingi vikianzia mgongoni na kuenea mwili mzima, pamoja na kwenye viganja vya mikono na kwenye nyayo. Vijipele hivi huwa vya mviringo vyenye rangi nyekundu au vyenye wekundu wa kahawia.
Michubuko inayofanana na chunjua hutokea kwenye sehemu za midomo na mkundu. Vile kutatokea maumivu ya misuli, homa, kukauka koo, kuvimba tezi, kupunyuka nywele, kukonda na uchovu wa mwili.

Latent Syphilis
Kama tiba ya kaswende ya hatua ya pili haitatolewa, ugonjwa utaendelea kwenye hatua iitwayo latent stage. Katika hatua hii inayoweza kudumu kwa miaka kadhaa, mwili utautunza ugonjwa bila kuonyesha dalili zo zote. Pamoja na kuwa hakuna dalili zo zote zitakazoonekana, ugonjwa huu unaweza kuendelea kwenye hatua ya mwisho.

Hatua Ya Tatu Ya Kaswende – Tertiary syphilis

Asilimia 15 ya watu ambao hawakupata tiba kwenye hatua ya pili ya kaswende watapata kaswende ya hatua ya tatu – tertiary syphilis. Hatua hii inatokea miaka 10 hadi 30 baada ya dalili za mwanzo za kaswende.
Dalili
Dalili za kaswende za hatua hii ni pamoja na kushindwa kumudu matumizi ya viungo vya mwili, ganzi, upofu, ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu, madhara kwenye moyo na mishipa ya damu, madhara kwenye ini, mifupa na maungio ya mifupa. Kifo huweza kutokea kutokana na uharibifu wa viungo vya mwili.

Matibabu ya ugonjwa wa Kaswende

Ugonjwa wa kaswende unatibika. Kuwahi kumpa tiba mgonjwa wa kaswende ni muhimu kwani kuchelewa kunaweza kumletea madhara makubwa ya mwili au kifo. Kama ugonjwa haujazidi mwaka mmoja, mara nyingi dozi moja ya ya penicillin hutosha.

Kaswende iliyoendelea kwenye hatua nyingine, dozi nyingine zitahitajika.

Madhara ya Kuvaa viatu virefu wakati wa Ujauzito

Wakati wa ujauzito ni kipindi cha kubadili mambo mengi katika mfumo wa maisha wa mjamzito. Mjamzito anapaswa kubadili mambo mbalimbali ili kuhakikisha anakua na afya nzuri katika kipindi chote cha ujauzito na ili kuhakikisha kwamba atajifungua mtoto mwenye afya nzuri. Moja ya mambo makubwa ni pamoja na tabia ya kuvaa viatu vyenye visigino virefu. Mjamzito hashauriwi kuvaa viatu vyenye visigino virefu kutokana na athari zinazoweza kutokana na aina hizi za viatu.

Zifuatazo ni athari za kuvaa viatu vyenye visigino virefu wakati wa ujauzito:

Mimba kutoka.

Mjamzito akivaa viatu vyenye visigino virefu anakua katika hatari kubwa ya kuanguka. Hii huweza kusababisha majeraha makubwa kwa mtoto aliyeko tumboni hali inayoweza kusababisha mimba kutoka.

Maumivu ya misuli ya mapaja.

Wadada hupenda kuvaa “high heels” husababisha misuli ya mapaja kukaza na kuwa na muonekano mzuri. Katika ujauzito, mabadiliko ya homoni huweza kupelekea misuli hii kuwa na maumivu tofauti na ilivyokua kabla ya ujauzito.

Hatari ya kuanguka.

Ni wazi kuwa uzito huongezeka wakati wa ujauzito na mabadiliko ya vichocheo vya mwili huweza kupelekea kizunguzungu cha hapa na pale. Hii huongeza hatari ya kuanguka iwapo utavaa “high heels” na kupelekea majeraha kwako na kwa mtoto aliyeko tumboni.
Uvimbe miguuni.
Ni jambo la kawaida miguu kuvimba wakati wa ujauzito. Kuvaa viatu vyenye visigino virefu na vyenye kubana huweza kuongeza tatizo hilo na kupelekea maumivu.

Maumivu ya mgongo.

Wakati wa ujauzito, uzito mkubwa huhamia mbele na misuli ya nyonga hulegea. Mabadiliko haya ya kimsawazo huweza kusababisha maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo na kiuno.

Mambo ya Kuzingatia kama ni lazima kuvaa

Iwapo kuna ulazima sana wa kuvaa viatu hivyo, unapaswa kuzingatia yafuatayo:

  1. Epuka visigino vyembamba sana.
  2. Usivae siku nzima. Vitoe mara kwa mara kupumzisha miguu.
  3. Epuka kutembea au kusimama muda mrefu ukiwa umevivaa.
  4. Ukihisi maumivu kwenye misuli ya mapaja jaribu kufanya mazoezi ya kujinyoosha na kujikanda.
  5. Ni salama kuvaa viatu hivi katika muhula wa kwanza wa ujauzito (Miezi mitatu ya mwanzo).
  6. Viatu visiwe virefu sana na visigino viwe imara.
  7. Vaa viatu visivyo na bugdha na usivikaze sana.

Faida za kula Tende kiafya

Zifutazo ni faida zitokanazo na ulaji wa tende;

1. Tende huongeza nguvu kutokana na kuwa na sukari ya asili, unaweza kuchanganya na maziwa na kupata mchanganyiko bora.

2. Tendehuzuia meno kuoza, na ni tiba nzuri kwa wagonjwa wa anemia kutokana na kuwa na madini mengi ya chuma.

3. Hupunguza uwezekano wa kupata Kiharusi (stroke) kwani hazina cholesterol kabisa! Pia zina vitamini na madini kwa wingi.

4. Hupunguza madhara ya pombe mwilini na kurudisha afya ya mtu.

5. Zina kiasi kikubwa cha kamba kamba ambazo hufanya mtu apate choo kirahisi na laini.

6. Licha ya kuwa tamu, tende haziongezi kiwango cha sukari mwilini, hivyo zinaweza kutumika kama mbadala wa sukari.

7. Huimarisha Mifupa na kuondoa maumivu ya mara kwa mara ya mifupa kutokana na kuwa na madini ya chuma, na potassium kwa wingi.

8. Tende ina msaada mkubwa kwa mama mjamzito, humuongeza nguvu, na hazina madhara kiafya kwa mtoto. Pia husaidia kupata uzazi salama.

9. Ulaji wa tende kwa wingi husaidia kuongeza mwili kwa wale waliokonda kupita kiasi. Hivyo hushauriwa kula tende kupita kiasi kama huhitaji kuongeza mwili

Shopping Cart