Baini Siri za Kuwa na Afya Bora na Utimamu

Mapishi ya Pilau Ya Sosi Ya Soya Na Mboga

Viambaupishi

Kuku (mkate mkate vipande) 1

Mchele wa Basmati (rowanisha) 3 magi

Mdalasini 1 mchi mmoja

Vitunguu maji (vilivyokatwa vyembamba) 6

Mchanganyiko wa mboga za barafu 1 magi

(karoti, mahindi, njegere)

Kabichi (iliyokatwa katwa nyembamba) 1 magi

Pilipili mbichi (iliyosagwa) 3

Pilipili boga iliyokatwa vipande vidogo vidogo 1

Pilipili manga 1 kijiko cha chakula

Chumvi 1 kijiko cha chakula

Sosi ya soya (soy sauce) 5 vijiko vya chakula

Kotmiri iliyokatwa katwa 1 magi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa 2 vijiko vya chakula

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Tia mafuta ndani ya karai. Yakipata moto kiasi, mimina vitunguu maji na mdalasini 1 mzima kaanga. Itachukua muda kidogo. Kaanga mpaka viwe rangi ya hudhurungi (brown). Viepue na uweke kando.

2. Ndani ya sufuria kubwa, mimina kuku, chumvi, thomu na tangawizi, sosi ya soya, pilipili manga, pilipili mbichi, chemsha mpaka kuku awive na maji yakauke.

3. Changanya vitunguu ulivyokaanga, kabichi, pilipili, mboga, kotmiri, mchanganyiko wa mboga za barafu na weka kwa muda wa dakika tano au kumi. Tia na mafuta kidogo uliyokaangia vitunguu .

4. Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja. Ukishauchuja umwagie katika masala ya kuku.

5. Nyunyizia mafuta kidogo uliokaangia vitunguu.

6. Weka moto mdogo mpaka wali ukishawiva. Uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa.

KIDOKEZO:

Unaweza kuupika wali huo ndani ya jiko, yaani badala ya kutia masala kwenye sufuria ukayatia katika bakuli au treya ya jiko (oven), kisha ukamwagia wali uliouchuja humo na kuupika kaitka moto wa 400-450 Deg kwa muda wa dakika 15-20.

Jinsi ya kupika Vileja

VIPIMO

Unga wa mchele 500g

Samli 250g

Sukari 250g

Hiliki iliyosagwa 1/2 kijiko cha chai

Arki (rose flavour) 1/2 kijiko cha chai

Baking powder 1 kijiko cha chai

Mayai 4

Maji ya baridi 1/2 kikombe cha chai

NAMNA YA KUTAYRISHA NA KUPIKA

1. Saga sukari iwe laini kiasi, changanya unga wa mchele, baking powder, hiliki na sukari.

2. Pasha moto samli mpaka iwe nyepesi kama maji mimina kwenye ule mchanganyiko wa unga wa mchele, kisha uchanganye pamoja na arki.

3. Ongeza mayai yaliopigwa endelea kuchanganya mpaka unga umeanza kuchanganyika vizuri.

4. Ongeza maji ya baridi sana kama nusu kikombe tu ili uchanganyike vizuri.

5. Kata kwa design unayotaka viwe vinene visiwe kama cookies za kawaida kama ilivyo kwenye picha na ukipenda utaweka kidoto kwa kutumia zaafarani katikati ya kileja kama inavyoonesha hapo juu.

6. Choma kwa moto wa baina ya 300F na 350F kwa dakika 15 mpaka 20 visiwe vyekundu toa na tayari kwa kuliwa

Ifahamu Saratani ya Tezi Dume, chanzo, Dalili, Uchunguzi na Tiba

Tezi Dume ni nini?

Tezi dume (prostate), ni tezi iliyo kwenye kizazi cha mwanaume inayozalisha maji maji yanayobeba manii/shahawa. Inaizunguka urethra, mrija unaotoa mkojo kwenye kibofu kwenda nje. Tezi dume ya kila mwanaume huongezeka ukubwa kadri umri unavyoongezeka. Kadri tezi inapokua na kuongezeka ukubwa,inaweza kukandamiza urethra na kusababisha matatizo ya kibofu na matatizo ya kukojoa. Tezi dume inapoongezeka ukubwa huitwa ”benign prostatic hyperplasia” kwa kifupi ”BPH”. Hii sio saratani, na haiongezi hatari ya kupata saratani ya tezi dume.

Saratani ya tezi dume inashika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo vinavyotokana na kansa kwa wanaume duniani. Pia ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wenye umri wa miaka 70 na kuendelea. Hata hivyo, satarani ya tezi dume kwa sasa inawapata sana wanaume kuanzia miaka 25. Lakini kabla ya kuendelea mbele hebu kwanza tujue tezi dume ni zipi.

Kama tulivyosema neno saratani ni jina la gonjwa ambalo hutokea wakati chembe chembe za uhai au seli katika sehemu fulani ya mwili zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili na kutengeneza vijiuvimbe vidogo vidogo. Kwa kawaida seli huwa zinajigawa, kupevuka na baadaye kufa kwa kufuata taratibu za mfumo wa mwili. Lakini seli za saratani hazifuati mfumo huo. Badala ya kufa, zenyewe huishi muda mrefu kuliko chembe chembe za kawaida na wakati huo huo huendelea kutengeneza seli nyingine na kuwa uvimbe wa saratani au tumour.
Tezi dume linapatikana katika mwili wa mamalia dume tu na pale seli katika kiungo hicho zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili hapo ndipo mtu hupata saratani ya tezi dume. Ugonjwa huu pia hujulikana kama saratani ya kibofu cha mkojo. Saratani ya tezi dume huwapata wanaume tu na hasa wenye umri wa takribani miaka 50 na kuendelea. Kutokana na tafiti mbali mbali, saratani hii imethibitika kushika nafasi ya pili, ukiachia mbali saratani ya mapafu kwa kusababisha vifo vya wanaume wenye umri wa takribani miaka 50 na kuendelea.
Tafiti za Chama cha Saratani cha Marekani (ACS) na cha Afrika Kusini (CANSA) zimebaini kuwa, mwanaume mmoja kati ya sita hupata saratani ya tezi dume katika uhai wake. Kutokana na takwimu za mwaka 2010 za dunia nzima, malaria iliua watu laki tano, kifua kikuu watu milioni 2.1, Ukimwi watu milioni 1.8 na saratani watu milioni 9.9. Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa saratani ni kubwa ikilinganishwa na ya magonjwa mengine. Dk Emmanuel Kandusi ambaye ni miongoni mwa waathirika wa saratani hiyo, na mwanzilishi wa kampeni ya kuangamiza saratani ya tezi dume nchini Tanzania ya ’50 Plus Campaign’ anasema kuwa, ugonjwa huu ukitambuliwa mapema huweza kutibika kwa urahisi. Ameongeza kuwa, kutokana na ugonjwa huo kuwa hatari nchini, ifikapo mwaka 2020 unatarajiwa kuua watu milioni 20.

VIHATARISHI VYA TEZI DUME

Kuna vihatarishi vingi vinavyochangia mwanamume kupata saratani ya tezi dume. Vifuatavyo ni baadhi yake:-

👉🏿Kwanza kabisa ni umri. Nafasi ya kupata saratani ya tezi dume huongezeka sana hasa ukifikia umri wa karibu miaka 50 na kuendelea.

👉🏿Nasaba ni kihatarishi kingine ambapo wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu huwa katika hatarini ya kupata kansa hiyo kutokana na kurithi jeni za ugonjwa huo.

👉🏿Suala jingine ni lishe ambapo wanaume wanaopenda kula nyama au (red meat) na walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume.

Vilevile wataalamu wanatumbia kuwa, wanaume wasiopenda kufanya mazoezi, wanene na wenye upungufu wa virutubisho vya Vitamin E pia wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya kibofu cha mkojo.
Wanaume wengine walio katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume ni pamoja na wale wenye asili ya Afrika (Weusi) ikilinganishwa na wazungu, wakulima wanaotumia aina fulani ya mbolea za kemikali, wanaofanya kazi katika viwanda vya kutengeneza matairi na wachimbaji madini, hususan aina ya cadmium.

DALILI ZA TEZI DUME

Hayo yote yakiwa ni tisa, kumi ni je, dalili za saratani ya tezi dume ni zipi?Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani na zile za kuvimba kwa tezi dume au BPH.
Dalili hizo ni pamoja na,

1) Kupata shida wakati wa kuanza kukojoa.

2) Kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa.

3) Kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu.

4) Kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku.

5) Kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote

6) kutoa mkojo uliochanganyika na damu.
Pamoja na kueleza dalili hizo watu wanapashwa kutambua kuwa, mwanaume anapoanza kuona na kuhisi baadhi ya dalili hizo, anapaswa kujua kuwa, seli za saratani katika tezi dume lake huwa zina umri wa takribani miaka saba na kuendelea.
Iwapo saratani imesambaa mwilini kiasi cha kuhusisha sehemu nyigine za mwili, mgonjwa anaweza kuwa na maumivu makali ya mifupa katika maeneo ya nyonga, mapajani na kiunoni.
Aidha mgonjwa huwa na dalili nyingine zinazoweza kumpata mgonjwa mwingine yeyote wa saratani kama vile kupungua uzito, kuhisi kichefuchefu, uchovu, kizunguzungu na kadhalika.

UCHUNGUZI WA TEZI DUME

Wanaume wanashauriwa kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya kibofu cha mkojo au prostate cancer kwa kuwa imegundulika kuwa wanaume wengi wakiziona na kuzihisi dalili hizo huona soni kwenda kumwona daktari na kufanyiwa uchunguzi.
Baadhi ya watu huzihusisha na magonjwa ya zinaa au na dhana potofu za kishirikina. Wapo wanaokwenda mbali zaidi hata kuuita ugonjwa huo kuwa ni wa walawiti huku wengine wakiurahisisha kwa kuuita kuwa ni ugonjwa wa utu uzima kana kwamba saratani ya tezi dume ni jambo la kawaida kwa watu wazee.
Mambo kama hayo hupelekea wanaume wengi kujinyanyapaa wenyewe na hata wengine kujitibu kwa uficho au kwa kutumia waganga wababaishaji mpaka pale mambo yanapokuwa yamewazidi ndipo hupelekwa mahospitalini na mara nyingine huwa wamechelewa na kupoteza maisha yao bure kwa ugonjwa ambao ungeweza kutibiwa mapema.
Kwa ajili hiyo tunatoa wito kwa wanaume kutoona soni na kuwa na tabia ya kufanyiwa uchunguzi wa afya kwa ujumla, na hasa tezi dume angalau mara moja kwa mwaka.
Kuna vipimo viwili ambavyo daktari anaweza kumpima mwanaume ikiwa ni hatua ya kwanza ya kugundua ugonjwa huo. Vipimo hivyo vya kwanza ni “Digital Rectal Exam (DRE)” na cha pili ni “Prostate Specific Antigen (PSA)”. DRE pamoja na PSA huonesha uwepo wa tatizo kwenye tezi dume, lakini vipimo hivi havina uwezo wa kutofautisha iwapo tatizo hilo linamaanisha saratani au uvimbe katika tezi dume. Hivyo basi, ili kuweza kutofautisha kati ya magonjwa hayo mawili, kipimo kiitwacho Prostate biopsy hufanywa. Baada ya vipimo hivyo kama vitaashiria saratani ya tezi dume basi daktari anaweza kuamuru vipimo vingine ili kuthibitisha uwepo wa ugonjwa huo kama vile transrectal ultrasound au prostate needle biopsy.

MATIBABU YA TEZI DUME

Kuna njia kadhaa za matibabu ya saratani ya tezi dume. Hata hivyo uamuzi wa njia gani itumike unategemea ushauri na maoni ya daktari kulingana na hatua ya ugonjwa ulipofikia na umri wa mgonjwa husika. Katika hatua za awali za ugonjwa, daktari anaweza kushauri mgonjwa atibiwe kwa kufanyiwa upasuaji na tiba ya mionzi.
Hii ni katika hali ambayo kwa wagonjwa wazee, daktari anaweza kushauri mgonjwa kuwa chini ya uangalizi tu bila kufanyiwa upasuaji au bila kupatiwa tiba ya mionzi.

Matumizi ya dawa

Alpha 1-blockers kama vile doxazosin, prazosin, tamsulosin, terazosin, na alfuzosin ni dawa zilizo kwenye kundi la dawa zinazotumika kutibu shinikizo la juu la damu. Dawa hizi hulegeza misuli ya shingo ya kibofu na tezi dume. Hii huruhusu mkojo kutoka kwa urahisi. Watu wengi wanatumia dawa ya Alpha 1-blockers, na husaidia sana kupunguza dalili zao.

Finasteride na dutasteride  ni dawa zinazopunguza kiwango cha homoni zinazotengenezwa na tezi dume,hupunguza ukubwa wa  tezi dume, huongeza kiwango cha mtiririko wa mkojo, na kupunguza dalili zinazotokana na ukubwa wa tezi dume kuongezeka. Inaweza kuchukua miezi 3 hadi 6 kabla ya kuona mabadiliko makubwa katika dalili zako. Kutumia finasteride na dutasteride kunaweza kuwa na athari kama vile, kupungua kwa nguvu za kiume na hata kuwa hanithi.

Daktari anaweza kuagiza upewe dawa za antibiotiki ili kutibu kuvimba kwa tezi dume (prostatitis), mara nyingi prostatitis huambatana na kuongezeka kwa ukubwa wa tezi dume.

Upasuaji

Upasuaji wa tezi dume unaweza kupendekezwa  iwapo :

  • Unajikojolea/ unashindwa kuzuia mkojo
  • Unakojoa mkojo wenye damu mara kwa mara
  • Unashindwa kukojoa mkojo wote,(Mkojo unabaki kwenye kibofu hata baada ya kukojoa)
  • Maambukizi ya mara kwa mara kwenye njia ya mkojo
  • Kushindwa kwa figo kufanya kazi
  • Mawe kwenye kibofu

Uchaguzi wa aina maalum ya upasuaji, mara nyingi hutegemea ukali wa dalili ,ukubwa na umbo la tezi dume.

  • Transurethral resection of the prostate (TURP): Hii ni aina ya upasuaji inayopendelewa zaidi kutibu ugonjwa wa tezi dume. TURP hufanyika kwa kuingiza kifaa chenye kamera kupitia kwenye uume na kisha kukata na kuondoa tezi dume kipande baada ya kipande.
  • Transurethral incision of the prostate (TUIP): Upasuaji huu unafanana kidogo na TURP, na hufanyika kwa wanaume walio na tezi dume isiyo kubwa sana. Kwa kawaida upasuaji hufanyika na kisha mgonjwa huruhusiwa kwenda nyumbani (hakuna kulazwa). Kama ilivyo kwa TURP, kifaa chenye kamera huungizwa kupitia kwenye uume mpaka kuifikia tezi dume. Kisha, badala ya  kukatakata na kuiondoa, daktari hufanya mkato mdogo kupanua urethra ili kuruhusu mkojo kupita.
  • Simple Prostatectomy : Mgonjwa hupewa dawa ya nusu kaputi na kisha daktari hupasua tumbo (chini ya kitovu) ili kuifikia tezi dume. Sehemu ya ndani ya tezi dume huondolewa . sehemu ya nje huachwa . Huu ni utaratibu unaochukua muda mrefu, mgonjwa huhitajika kulazwa hospitalini kwa siku 5 hadi 10.


Iwapo saratani imesambaa na kuathiri sehemu nyingine za mwili, matibabu yake yanaweza kujumuisha upasuaji wa kuondoa korodani, matumizi ya dawa za kupunguza kiwango cha homoni ya testosterone katika damu au hormonal therapy, au matumizi ya kemikali za kuua seli za saratani (chemotherapy).

Tukumbuke kuwa, saratani ya tezi dume ni ugonjwa wa kawaida kama yalivyo magonjwa mengine na uchunguzi na matibabu ya mapema huweza kuokoa maisha ya waathirika wengi wa ugonjwa huo.

Jinsi ya kupika Wali Wa Sosi Ya Tuna

Viambaupishi

Sosi Ya tuna

Tuna (samaki/jodari) 2 Vikopo

Vitunguu (kata kata) 4

Nyanya zilizosagwa 5

Nyanya kopo 3 Vijiko vya supu

Viazi (vilivyokatwa vipande vidogo – cubes) 4

Dengu (chick peas) 1 kikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic)&Tangawizi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu

Hiliki 1/4 kijiko cha chai

Mchanganyiko wa bizari 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Pilipili manga 1 Kijiko cha chai

Vipande cha Maggi (Cube) 2

Wali

Mchele 3 Vikombe vikubwa (Mugs)

Mdalasini 2 Vijiti

Karafuu chembe 5

Zaafarani kiasi

*Jirsh (Komamanga kavu au zabibu kavu -raisins) 1/2 Kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Kosha Mchele na roweka.

2. Kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi (brown) chuja mafuta uweke kando.

3. Kaanga viazi, epua

4. Punguza mafuta, kaanga nyanya.

5. Tia thomu/tangawizi, bizari zote, vipande vya Maggi, nyanya kopo, chumvi.

6. Mwaga maji ya tuna iwe kavu, changanyisha kwenye sosi.

7. Tia zaafarani kidogo katika sosi na bakisha ya wali.

8. Chemsha mchele pamoja na mdalasini na karafuu.

9. Karibu na kuwiva, chuja maji utie katika chombo cha kupikia katika jiko (oven)

10. Nyunyizia zaafarani, mwagia vitunguu, viazi, na dengu juu ya wali.

11. Mwagia sosi ya tuna na pambia jirshi (au zabibu).

12. Funika wali na upike katika jiko moto wa 450º kwa muda wa kupikika wali.

* Jirsh (komamanga) kavu zioshwe vizuri kutoa vumbi au tumia zabibu kavu (raisins)

Mambo 8 ya kushangaza yanayofanywa na mwili wako kukulinda pasipo wewe kujua

Mwili wa binadamu unafanya mambo
mengi ya kibaiolojia ambayo mara
nyingi ni vigumu kuyaelewa. Mwili una mifumo mbalimbali ya ulinzi ambayo inatulinda na hatari zinazoweza kutudhuru. Mifumo hiyo
inatulinda masaa 24 ya siku, Siku zote 7 za wiki, katika mambo yote
yanayoweza kuhatarisha maisha yetu.
Yafuatayo ni mambo yanayofanywa
na mwili ambayo ni kati ya hiyo
mifumo ya ulinzi wa mwili wa
binadamu.

1. KUPIGA MIAYO (YAWNING)
Lengo kubwa la kupiga muayo ni
kuupoza ubongo baada ya joto kuzidi
kwenye ubongo au baada ya ubongo
kuchoka kufanya kazi.
Vile vile kama ukiwa umechoka au una
njaa husabababisha oxygen
kupungua kwenye damu na kwenye
mapafu, hii hupelekea tatizo la
kupumua, hivyo kupiga miayo
husaidia kuingiza oxygen ya ziada
mwilini ili irudishe mwili katika hali
yake ya kawaida.

2. KUPIGA CHAFYA (SNEEZING)
Mara nyingi tunapiga chafya pale pua
zetu zinapokua zimejaa bakteria wa
magonjwa ambao hawahitajiki
mwilini, Vumbi pamoja na takataka
mbali mbali zilizoingia kupitia pua.
Hivyo kupiga chafya ni kitenda cha
mwili kujisafisha kwa kuyatoa hayo
matakataka nje yaliyoingia mwilini.

3. KUJINYOOSHA (STRETCHING)
Kuninyoosha mwili ni kitendo kisicho
cha hiari ambacho lengo lake ni
kuuandaa mwili kwa ajili ya kazi
mbalimbali za kutumia nguvu
utakazokabiliana nazo kwa siku nzima.
Lakini pia kujinyoosha kunaipa misuli
ya mwili mazoezi na kuiweka sawa
vilevile kunarudisha mzunguko wa
damu katika hali yake ya kawaida na
kumtoa mtu katika uchovu.

4. KWIKWI (HICCUPING)
Najua umewahi kupata kwikwi, na
mara nyingi mara baada ya kumaliza
kula chakula. Je umeshawahi kujiuliza
ile sauti ya ajabu ya kwikwi
inasababishwa na nini au kwa
sabababu gani watu hushikwa na
kwikwi?
Hiyo yote husababishwa na
DIAPHRAGM (tamka DAYA – FRAM)
kiungo kinachopatikana ndani ya
mwili wa binadamu chini kabisa ya
kifua baada ya mapafu(lungs). Kazi
kubwa ya diaphragm ni kusaidia katika
upumuaji, (inhale) na (exhale). Pale
unapoingiza hewa ndani (inhale)
diaphragm hushuka chini ili kusaidia
kuivuta hewa ifike kwenye mapafu. Na
unapotoa hewa nje (exhale)
diaphragm hutulia kwa kubakia
sehem yake ili kuwezesha hewa chafu
kutoka nje kupitia pua na mdomo.
Sasa basi, kuna wakati diaphragm
kubugudhiwa na kuisababisha
kushuka chini kwa kasi sana jambo
linalosababisha wewe kuvuta hewa
(inhale) kwa kasi isiyo ya kawaida
kupitia koromeo la sauti, hewa ikifika
kwenye box la sauti (larynx), sehem
hiyo hujifunga kwa haraka sana ili
kuzuia hewa isipite huko na ndipo
KWIKWI hutokea.
Mambo mengine yanayoweza
kuibugudhi diaphragm na
kuisababisha kufanya kazi vibaya
mpaka kupelekea kwikwi ni kitendo
cha kula haraka haraka au
kuvimbewa.

5. KUJIKUNJA KWA NGOZI YA VIDOLE
VYA MIKONO BAADA YA KULOWA AU
KUKAA MUDA MREFU KWENYE MAJI.
Je umewahi shuhudia jinsi ngozi ya
vidole vyako inavyojikunja baada ya
kufua nguo muda mrefu au kushika
maji muda mrefu? Unajua ni kwa
sababu gani ngozi hujikunja kama ya
mtu aliyezeeka angali yu kijana mara
baada ya kukaa sana kwenye maji?
Watu wengi kabla walizani kwamba
kujikunja kwa ngozi hiyo hutokana na
maji kuingia kwenye ngozi na hivyo
ngozi hujikunja baada ya kulowa.
Lakini wanasayansi baada ya kufanya
utafiti kwa muda merefu juu ya nini
hasa hupelekea ngozi kujikunja?
Walisema HAPANA si kwa sababu ya
ngozi kulowana. Na walikuja na
majibu haya.
Mwili unapokutana na majimaji mara
moja hupeleka taarifa na kutafsiri
kwamba mazingira hayo yana UTELEZI
(Slippery) hivyo kutasababisha mikono
kushindwa kushika (Grip) au kukamata
vitu kwa urahisi kutokana na utelezi
huo. Hapo mwili huchukua hatua ya
haraka kuikunja ngozi ya mikono yako
ili kurahisisha ushikaji wa vitu
vinavyoteleza ndani ya maji pamoja na
kutembea kwenye utelezi.

6. VIPELE VIPELE VYA BARIDI KWENYE
NGOZI (GOOSEBUMPS)
Kazi kubwa ya vipele hivi ni kupunguza
kiasi cha joto la mwili linalopotea
kupitia matundu ya ngozi. Hivyo kwa
kufanya hivi humfanya binadamu
kutunza joto la mwili hata katika
mazingira ambayo hali yake ya hewa
si rafiki kwa mwili wa mwanadamu au
ni yenye baridi sana.

7. MACHOZI (TEARS)
Zaidi ya kuwa majimaji (MUCOUS
MEMBRANE ) yanayopatikana kwenye
Macho ambayo kazi zake ni kulilinda
jicho dhidi ya kitu chochote kigeni
kinachoingia jichoni (mfano
unapokata vitunguu au mdudu
anapoingia jichoni huwa unatoa
machozi mengi eeeh!! Pia dhidi ya
upepo na moshi) na pia hutumika
kama kilainishi cha jicho pale
linapokuwa linazunguka zunguka
(blink).
Vilevile machozi yana kazi ya
kupunguza HISIA ZA HUDHUNI
zinazozalishwa mwilini. Wanasayansi
wanaamini kuwa mtu anapokua
mwenye msongo wa mawazo (stress)
mwili hutengeneza kitu kipya ili
kwenda kubugudhi na kuharibu
maumivu yote ambayo mtu anajisikia.
Hivyo machozi yanayozalishwa hapa
huwa na kemikali na yanafahamika
kama NATURAL PAINKILLER. Machozi
haya ni tofauti na machozi ya kawaida,
lengo lake hasa la kuzalishwa ni kwa
ajili ya kuondoa kabisa maumivu
yaliyozalishwa mwilini
Hivyo mpaka hapa tumeona kua kuna
machozi ya aina tatu ambayo ni
i. Basal tears (vilainishi)
ii. Reflex tears (mlinzi)
iii. Emotion tears (mtuliza maumivu)

8. KUSHTUKA USINGIZINI
(MYOCLONIC JERKS or HYPNIC JERK).
Je! Ushawahi kutokewa na hali hii?
umelala halafu ghafla unashtuka
usingizini kwa mguvu nyingi kama
umepigwa na shoti ya umeme na akili
inakurudi ghafla huku mapigo ya
moyo yakikuenda mbio? Na hali hii
ikakutokea pasipo hata kuota ndoto
yoyote?
Basi usiogope au kuwasingizia watu
uchawi, hii ni hali ya sayansi ya
mwili.na ni njia moja wapo katika ile
mifumo ya mwili kujilinda.
Je hutokeaje?
Hii ni hali ya ajabu sana isiyofanywa
kwa hiari ambayo huwatokea watu
mara tu wamejinyoosha kitandani na
kupitiwa na usingizi, mwili
hutetemeshwa na kusukumwa kwa
nguvu na mtu hushtuka katika hali
kama vile kapigwa na shoti ya umeme.
Hali hii inaweza kupelekea mtu hata
kuanguka kitandani na humwamsha
mara moja kutoka usingizini.
Wanasayansi wanatuambia kua, pale
tu unapopata usingizi kiwango cha
upumuaji kinashuka ghafla, mapigo ya
moyo nayo taratibu yanapungua,
misuli inatulia kwa ku-relax, Kitu cha
AJABU hapa ubongo unatafsiri hali hii
kama ni DALILI ZA KIFO (brain’s
misinterpretation of muscle
relaxation), hivyo huchukua hatua za
haraka za kuushtua mwili kwa
kuutetemesha au kuuskuma kwa
nguvu, hali ambayo humfanya mtu
kuamka kutoka usingizini kwa KURUKA
kitu ambacho ni hali isiyo ya kawaida.
Hali hii ikimtokea mtu huambatana na
kuongezeka kwa mapigo ya moyo
(rapid heartbeat), kuhema haraka
haraka, na wakati mwingine mtu
hutokwa na jasho jingi.
Wakati mwingine mtu huamka ametoa
macho na kama ukimwangalia, nae
huishia hukuangalia tu huku akikosa
la kukujibu endapo utamuuliza vipi
kuna tatizo gani?
MWILI WAKO NI ZAIDI YA
UNAVYOUJUA. JAMBO LA MSINGI NI
KUONDOA HOFU KWANI MWILI WAKO
UNAJUA NINI UFANYE NA WAKATI
GANI ILI KUKULINDA USIKU NA
MCHANA KATIKA SIKU ZOTE ZA
MAISHA YAKO.

Shopping Cart